Sunday, March 11

Wasomi: Uhuru, Raila darasa tosha


Wagombanao ndiyo wapatanao. Msemo huu ndiyo unavyoweza kutumika kuelezea tukio la Ijumaa Machi 9 nchini Kenya baada ya mahasimu wakuu wa kisiasa nchini humo kukutana na kufanya mazungumzo.
Mahasimu hao wa kisiasa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa muungano wa National Super Alliance (Nasa), Raila Odinga wamekutana baada ya takribani miezi minne ya taharuki ya kisiasa iliyotokea nchini mwao.
Katika kipindi hicho Wakenya wameshuhudia matukio mbalimbali ikiwamo maandamano ya mara kwa mara ya kupinga uongozi wa Rais Kenyatta na pia tukio la kiongozi huyo wa upinzani kujiapisha kama rais wa wananchi wa nchi hiyo jambo ambalo lilielezwa ni kinyume cha sheria za nchi hiyo.
Tukio hilo la kukutana kwa mahasimu hao licha ya kuwashtua Wakenya, liliibua mjadala kote Afrika Mashariki na Afrika nzima, kwa jinsi mahasimu hao walivyokutana na kutoka kauli moja ya kujenga Kenya mpya.
Wanasiasa hao waliamua kukutana juzi mchana katika ofisi ya Rais iliyopo katika jengo la Harambee lililopo jijini Nairobi nchini Kenya na pamoja na mambo mengi waliweza kujadili mustakabali wa nchi hiyo huku Raila akitoa ya moyoni kwamba ulikuwa ni wakati wa kujitathimini kama nchi.
Baada ya mazungumzo hayo, Raila alivieleza vyombo vya habari kuwa wamekubaliana na ‘ndugu yake Kenyatta kwamba Kenya iwe taifa moja ili kuzima migawanyiko iliyopo.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema hiyo ni hatua nzuri katika kufuta tofauti zao zilizodumu kwa muda mrefu na hatimaye kujenga Kenya mpya kwa mustakabali wa nchi yao.
Ni wazi kuwa sasa Kenya imefungua ukurasa mpya katika demokrasia ya nchi hiyo baada ya kugundua kuwa anayeweza kujenga au kuibomoa nchi yao ni wao wenyewe.
Wachambuzi wazungumza
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amewapongeza viongozi hao kwa kuonyesha alichokiita ukomavu wa hali ya juu kwa kubaini ukweli kwamba katika siasa mnaweza kupingana kwa hoja bila kupigana.
“Wote ni mashahidi muda si mrefu Raila alitangaza maandamano makubwa lakini pamoja na kuandamana Rais Kenyatta alionyesha uvumilivu wa kiwango cha juu na Serikali iliwahakikishia ulinzi lakini mwisho wa siku walifikisha ujumbe wao kwa amani.”
“Hawakuishia hapo, siku chache baadaye kiongozi huyo wa upinzani aliamua kujiapisha; Rais Kenyatta alikuwa na uwezo wa kufanya chochote. Yeye ni kama headmaster (mkuu wa shule) kila mtu anamtii, pengine leo tusingekuwa na Raila lakini alionyesha uvumilivu wa kiwango cha juu na kwamba si kila kitu anakijua ila kuna wengine waweza kujua zaidi yake na matokeo yake leo tunashuhudia haya maridhiano,” anasisitiza.
Dk Mashinji anasema kitendo hicho ni somo kubwa kwa nchi za Afrika na kimesababisha wananchi wa Kenya sasa kujiona ni wamoja na kwamba hawana sababu ya kupingana kama ilivyokuwa awali.
Dk Mashinji anasema somo hilo liwafikie viongozi wa nchi nyingine, ikiwamo Tanzania, kwamba kunapotokea migogoro njia sahihi ni kufanya mazungumzo.
“Kuna msemo unasema kuwa, “Ukitaka kwenda haraka nenda peke yako, lakini ukitaka kwenda mbali nenda na wenzako”. Huu usemi una maana sana bila kushirikiana kamwe hatuwezi kufika mbali,” anasisitiza na kuongeza kuwa Wakenya wanazizidi nchi nyingi kwa uvumilivu wa kisiasa.
Akizungumzia kitendo cha Raila kujiapisha, Dk Mashinji anasema kiongozi huyo alikuwa akijua wazi kwamba hawezi kuwa Rais, lakini alitaka kuvuta hisia za watu na kufikisha ujumbe kwa Serikali kwamba haiwatendei haki.
“Unajua Raila sasa ni mzee, kitendo kile kweli ni cha kichekesho lakini kilikuwa na umuhimu mkubwa kwa kipindi kile kwa kuwa alihakikisha ujumbe wake umefika na cha muhimu zaidi ni Serikali ilikuwa sikivu na ilielewa nini dhamira yake na mwisho wa siku wameweza kukaa pamoja kwa mustakabari wa watu wa Kenya,” anasema.
Vilevile Dk Mashinji anasema kitendo hicho kitoe funzo kwa viongozi wengine, hata hapa Tanzania ambao anasema wamejifungia ndani, wananchi hawaongei jambo linalosababisha kutopata mrejesho wa jambo wanalokifikiria.
“Serikali ingeruhusu watu watoe wanachokifikiria, wangepata ukweli wanakubalika kwa asilimia ngapi na kugundua wanapokosea badala ya kuacha hofu ikitawala huku wakiamini wanakubalika kwa asilimia 100.
“Hata Rais wa Marekani John Kennedy aliwahi kunukuliwa akisema kuwa kiongozi ukiona unakubalika kwa asilimia zaidi ya asilimia 75, ujue kuna shida kwani ukweli ni kwamba kuna 25 ya watu wanaweza kukuchukia bila sababu za msingi, anasema Mashinji.”
Anasema Kenya imetoa funzo kubwa, kwanza kwa kuwa na Katiba imara inayoweza kuruhusu matokeo ya uchaguzi kupingwa mahakamani, kuruhusu wananchi waseme wanachofikiria lakini pia watawala wameonyesha kuwa kuna uwezekano wa kuwa na tume ya maridhiano ambayo ikitumika vyema nchi itapita katika demokrasia ya kweli.
“Upinzani si uadui na mara zote wanasiasa watambue kuwa bila Yanga imara huwezi kuwa na Simba na bila ya kuwa na upinzani imara huwezi kuwa na CCM.”
Dk Mashinji anaungwa mkono na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Mkulilo anayesema kuwa licha ya nchi hiyo kuwa na mgawanyiko mkubwa wa ukabila na rasilimali ya ardhi, imeweza kuonyesha ukomavu katika siasa.
Dk Makulilo ambaye ni msomi wa sayansi ya siasa anasema ingawa kitendo hicho si cha kwanza kutokea katika nchi za Afrika, lakini viongozi hao wameweza kuweka mazingira ya kufuta tofauti zao ukizingatia kwamba walikuwa katika kipindi kigumu baada ya kumaliza uchaguzi mkuu mwaka jana.
“Ni tukio jema, hata Zanzibar mwaka 2010 viongozi wa chama tawala na upinzani waliwahi kukutana na kufanya maridhiano. Hii inaonyesha siasa siyo ugomvi bali ni kuongoza wananchi ili kufikia malengo kama nchi,” anasisitiza Dk Makulilo.
Kwa mtazamo wake Dk Shoo Innocent, mtaalamu wa Diplomasia na Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia anasema sababu kubwa ya viongozi hao kuamua kukutana ni baada ya nchi hiyo kuanza kuyumba kiuchumi.
“Unajua Kenya ndiyo ina uchumi mkubwa kwa nchi za Afrika Mashariki lakini kutokana na hali ya kisiasa ilivyo, sasa nchini humo takwimu zake za uchumi kwa mujibu wa Benki Kuu ya Kenya zinaonyesha uchumi kuporomoka kwani ilitarajiwa kupanda kutoka asilimia 5.5 lakini sasa umekuwa kwa asilimia 4.5 pekee,” anasema.
Anasema hali hiyo imewatisha sana viongozi hao kwani nchi inayofuata kwa karibu ni Tanzania ambayo inaonekana ina hali nzuri, rushwa imepungua kwa kushika nafasi ya pili ikiongozwa na Rwanda, lakini pia biashara ya utalii inaongezeka kwa kasi hivyo wakaona si vyema kuendelea kulumbana kwani wataendelea kuwapoteza wawekezaji.
“Unaweza kusema kilichofanyika Kenya ni Politica Game (mchezo wa kisiasa) wameona uchumi wao haukui kama walivyotarajia. Kenya wana ofisi nyingi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa (UN), UNDP, UN Habitat, Tata na Volkswagen hivyo kuendelea kulumbana kutasababisha kuongoa huduma zao kwani hawawezi kukaa katika nchi ambayo haina utulivu na amani,” anasema.
Dk Innocent anasema kuwa nchi nyingi za Africa zinakosea kwa kushindwa kutoa kipaumbele kwa sekta binafsi na badala yake kufikiri Serikali pekee inaweza kufanya hivyo hata kunapokuwa na mgogoro wa siasa nchi inaamini inaweza kuweka mambo sawa.
“Ukiheshimu sekta binafsi huwezi kuacha hali yako ya kisiasa iende mrama. Haiwezekani Serikali ikafanya kila kitu, ni lazima iweke mazingira mazuri kwa kila mwekezaji wa ndani na nje kuwe na utulivu lakini pia kuwapo na sera ambazo zitasababisha uchumi ukue, hivyo wanasiasa wana nafasi kubwa katika kupingania hilo. Huwezi kuwa na migogoro kila siku ukategemea maendeleo,” anaonya.
Akijadilia hatua hiyo, Wakili wa Kujitegemea, Peter Mshikilwa anasema kuwa nchi hiyo imeonyesha ukomavu wa kidemokrasia na kwamba imetambua kuwa ili ukue ni lazima uwe na taasisi imara.
“Kenya imeonyesha mfano kwa kuwa na Katiba imara na kuweka maslahi ya wananchi mbele kuliko viongozi, mfano wameweza kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi wakati sisi Katiba yetu inasema matokeo yakishatangazwa hakuna chombo chochote chenye mamlaka ya kuhoji wala kubatilisha matokeo hayo.”
“Huo kwao ni mwanzo mzuri, ndiyo maana unaona demokrasia ya kweli inatamalaki, lakini pia kitendo cha kuwa na Tume ya maridhiano nayo ni hatua nyingine.”
Anawataka viongozi wa Afrika kuhakikisha wanapinga vikali siasa za uhasama kwani hazina nafasi badala yake wanatakiwa kutofautiana kimtazamo na mwisho wa siku wote wanakuwa kitu kimoja kama nchi.
“Hapa kwetu hali ni tofauti ukishakuwa mpinzani basi wewe unaonekana ni adui. Dhana hii haitatufikisha katika kutengeneza demokrasia ya kweli, lazima tubadilike,” anasisitiza Mshikilwa.
Vilevile Mhadhiri wa (UDSM), Dk Francis Michael anasema huwezi kupata maendeleo kama nchi haina amani na utulivu, hivyo viongozi hao wa Kenya wameliona hilo na kuamua kulifanyia kazi.
“Siasa zipo kwa ajili ya wananchi wote siyo kikundi fulani cha wananchi au viongozi wachache wanaojihusisha na mlengo mmoja, hivyo Raila na Rais Kenyatta wameona si busara kuendeleza migogoro ambayo haina tija kwa taifa lao.”
“Kenya ilishagawanyika na bado ina amani, hivyo kama tunataka kuwa na demokrasia ya kweli jambo la msingi kwa viongozi wahakikishe wanaangalia mustakabali wa wananchi wote badala ya maslahi ya makundi na viongozi binafsi,” anasisitiza.
Dk Michael ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uongozi anaongeza kuwa viongozi Afrika lazima watambue kwamba wapo madarakani kwa ajili ya watu wote na hata wapinzani ambao kwa wakati huo hawapo madarakani wana haki sawa na wananchi wengine.
“Suala kubwa ni ushirikiano kwa pande zote, tumejifunza kutoka Kenya, sasa kuna amani baada ya viongozi wake bila kujali kwamba wanatoka chama tawala au upinzani wameamua kukaa pamoja na kujadili mustakabali wa nchi yao kwa manufaa ya Wakenya wote.   

Mtumishi Maliasili asimamishwa kazi kwa uchunguzi


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amemsimamisha kazi mkuu wa kanda Pori la Akiba Rukwa lililopo wilayani Mlele mkoani Katavi kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.
Taarifa ya Kaimu Katibu Mkuu, Dk Aloyce Nzuki iliyotolewa jana Machi 10,2018 inasema waziri amemsimamisha kazi Emmanuel Barabara ambaye pia ni mhifadhi wanyamapori mkuu.
Dk Kigwangalla amefikia uamuzi huo kutokana na taarifa za raia wema kuwa Barabara amekuwa akishirikiana na majangili kuhujumu rasilimali za misitu nchini.
Waziri Kigwangalla katika taarifa hiyo ameagiza iundwe kamati ya uchunguzi kubaini ukweli wa tuhuma hizo.
Amesema iwapo mtuhumiwa atatiwa hatia, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za utumishi wa umma ili iwe fundisho kwa wengine.
“Tunatoa onyo kali kwa watumishi wa wizara wanaojihusisha na vitendo vya uhujumu wa rasilimali za misitu, wanyamapori na mali kale. Tunawataka waache mara moja kwa kuwa hatutosita kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo hivyo, ikiwemo kufukuzwa kazi,” amesema.
Amewataka watumishi wa wizara kuzingatia sheria, kanuni, utaratibu na miongozo iliyowekwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ya uhifadhi wa rasilimali za nchi kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.  

Tunawategemea wanawake kugundua kila kitu


Inaonekana kama tumewatawala hivi lakini uhalisia ni kwamba tunawategemea wanawake kufahamu asilimia kubwa ya mambo tunayotaka kuyafahamu.
Kwa mfano juzi ilikuwa ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake – tukiwa kwenye makutano yetu wanaume likaibuka swali, kwa nini hakuna siku ya wanaume duniani? Wengine wakasema eti ni kwa sababu matatizo tuliyonayo wanaume hayawezi kutengewa siku moja maalum yakazungumzwa yakaisha, labda kungekuwa na mwaka wa wanaume duniani na bado ingebidi tuchague baadhi ya mambo ya kuyapa kipaumbele.
Mwingine ndio akatuua kabisa, akasema kuna siku ya wanawake pekee duniani kwa sababu matatizo na shida zote zinazoitesa dunia zina siku zake maalum; kwa mfano kuna siku ya Malaria Duniani, siku ya Ukimwi duniani na siku ya Saratani duniani.
Lakini tamati ya kikao hicho tukaja kufahamu kwamba kumbe kuna Siku ya Wanaume duniani kama ilivyo ya wanawake, na yetu ni Novemba 9—tusingeifahamu kama kusingekuwa na siku ya wanawake.
Achilia hiyo, ukitaka kuamini zaidi kwamba wanawake ndiyo wanaotufanya tufahamu mambo lukuki fikiria umelelewa zaidi na nani, utagundua kuwa ni mama – kwa hiyo mengi unayoyafahamu yanaanzia kwake.
Pia wanawake ndiyo wanaotufanya tugundue baa mpya—fikiria ni mara ngapi umeamua kwenda baa ili kukwepa kelele za mkeo ndani ya nyumba, na ili kufurahia zaidi unajikuta unalazimika kwenda baa tofauti tofauti – ugunduzi huu pia ni kwa hisani ya mwanamke.
Na kama ni bachela, mara kadhaa umejikuta ukilazimika kutafuta kiwanja kwenda kutulia na mwanamke; na ili usionekane hujui viwanja? Hapa ni lazima uwe mgunduzi wa kutafuta viwanja vipya kila siku—ugunduzi huu unachochewa na wanawake.
Lakini wanawake pia wametusaidia kuelewa kuwa google ina majibu mengi lakini siyo majibu ya kila kitu. Ulishawahi kuzozana na mwanamke kuhusu chochote na akakosa cha kukujibu? Wana majibu ya kila kitu.
Na wanawake ndiyo wanaofanya tujue thamani halisi ya fedha; unaweza kuwa na visenti vyako. Ukaona una pesa nyingi lakini ukikutana na mwanamke mmoja tu anayejua kutumia ndiyo utagundua kuwa kumbe ulikuwa na vichenji sio pesa.
Na kubwa zaidi ndiyo wanaofanya wagunduzi wanaendelea kugundua bidhaa mpya kila siku kwa sababu asilimia sabini ya bidhaa zinazozalishwa duniani, watumiaji wake wakuu ni wanawake kama vile nguo, vipodozi na simu nzuri. Lakini pia hata kama si kwa vitu wanavyovitumia wao moja kwa moja, bado vinagunduliwa kwa msukumo wao. Kwa mfano magari, hata kama si wanawake wengi wanatumia lakini magari mengi mazuri yanagunduliwa ili kuwavutia wao – wenye magari wanaelewa kinachozungumziwa hapa.
Kwa hiyo kiuhalisia si sisi ambao tunatawala dunia, kwa namna moja au nyingine ni wao, kwa sababu karibu kila kitu kinafanyika kwa ajili yao. Ni vile tu wanawake hawajagundua nguvu walizonazo.

Rais aagiza ajirini wazawa 'walionipigia kura'

Rais John Magufuli (kushoto) na Waziri Charles Mwijage (kulia)
Serikali ya Tanzania imetoa agizo kwa wamiliki wa viwanda nchini kuajiri wazawa.
Rais John Magufuli siku ya Jumapili amemwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuhakikisha wamiliki wa viwanda vya ndani wanaajiri wazawa.
“Kama wewe ni waziri nimekuteua mimi, unaacha kuwaajiri wazawa walionipigia kura unaenda kuchukua watu wa nje hili halikubaliki,” amesema Rais.
Rais Magufuli amesema, “Nitoe wito kwa mawaziri wangu na wakurugenzi, hakikisheni viwanda mnavyovianzisha nchini mnaajiri Watanzania, hawa ndio walionipigia kura.”
Rais John Magufuli amesema wananchi wazawa ndio waliompigia kura, hivyo wanastahiki wapewe kipaumbele cha ajira.
Ametoa agizo hilo leo Jumapili Machi 11,2018 akizindua kiwanda cha kufua vyuma cha Kahama Oil Mill mjini Kahama, mkoa wa Shinyanga, limeripoti gazeti la Mwananchi.
Kadhalika amewataka wamiliki wa viwanda kuhakikisha wanatumia malighafi za ndani kutengeneza bidhaa badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.
“Mwaka huu pamba nyingi imelimwa, Kahama Oil Mill pia mnatengeneza mafuta, hakuna haja ya kuagiza pamba kutoka nje wakati tuna pamba ya kutosha hapa,” amesema.
Kuhusu kiwanda cha chuma amesema malighafi inapatikana nchini, hivyo iwapo mkurugenzi wa Kahama Oil Mill anahitaji yuko tayari kumpa bure badala ya kuagiza nje.
Kadhalika amewataka Watanzania kununua bidhaa zinazozalishwa nchini, huku akisisitiza wamiliki wa viwanda kutengeneza vitu vilivyo na ubora ili kukabiliana na ushindani.

Chama cha UDP chadai maandamano ni uchochezi, uvunjifu wa amani

John Cheyo
Mwenyekiti wa chama cha upinzani UDP nchini Tanzania John Cheyo amesema Jumapili maandamano yaliyopangwa kufanyika April 26, 2018 ni uchochezi na uvunjifu wa amani na kwamba, mambo yanayolalamikiwa yangeweza kutatuliwa kupitia mabaraza ya vyama vya siasa.
Maandamano hayo kwa mujibu wa Cheyo yanaratibiwa kupitia mitandao ya jamiii, gazeti la Mwananchi limeripoti.
Rais John Magufuli
Rais John Magufuli
Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alivionya vyama vya siasa na wananchi ambao wamepanga kufanya maandamano.
Rais aliwataka waliojiandaa kutekeleza mpango waache mara mora vinginevyo watashughulikiwa.

“Nchi hii ni ya amani, ndiyo maana uvunjifu wa amani ulipoanza kutokea kule Kibiti tuliamua kuufuta mara moja. Kuna watu wanadhani tunafanya siasa kila wakati, kama wametumwa na baba zao kuandamana, watawasimulia vizuri.
Kwa mujibu wa maelezo ya Cheyo mabaraza ya vyama vya siasa yakitumika kikamilifu yanaweza kuondoa malalamiko ya wananchi na viongozi wa upinzani.
"Tusitake kufika hatua ya kuandamana barabarani ili kudai haki, Katiba mpya, Tume huru ya uchaguzi. Tukifikia huko amani iliyopo Tanzania tutashindwa kuipata tena na wananchi watakosa nchi nyingine yenye amani ya kukimbilia," amesema.
Gazeti la Mwananchi limeripoti kuwa Cheyo alisema kama tatizo ni fedha kwa ajili ya mabaraza hayo kukutana, Rais John Magufuli anapaswa kutoa fedha kuyawezesha kufanya vikao.
"Siungi mkono hoja za kudai kuwepo mikutano ya hadhara hata kama ni kwa ajili ya kuongeza wanachama kama wanavyodai wengine, naamini kwa sasa mitando ya kijamii ina nguvu kuliko kitu chochote nchini," amesema Cheyo.
Amesema kabla ya kudai haki ya kuandamana, zipo nyingine wananchi wapaswa kuzipa kipaumbele zikiwemo haki ya kuishi, kupata maji safi na salama, elimu na afya.
"Hatuwezi kufika mahali tuseme nchi hii imepotea na hakuna demokrasia kisa tumekosa haki ya kuandamana, haki ya kufanya mikutano ya hadhara. Kila mtu alishuhudia mikutano ya kampeni za uchaguzi wa ubunge wa marudio katika majimbo ya Kinondoni na Siha ilivyogeuka sehemu ya kutukanana," amesema Cheyo.
"Kama kitu mnachokidai kiliweza kusababisha watu kugombana na askari hadi mauaji yakatokea hicho kitu hakitusaidii kama nchi," amesema.
Cheyo ameongeza yanayodaiwa kwa nguvu hayana faida na manufaa ya kila siku kwa sababu watu wanahitaji kupata wakati wa kulima na kuvuna.
"Hiyo mikutano iliyoshupaliwa sasa na kuhitajika kwa nguvu zote si kweli kwamba kila siku watakuwa barabarani kuhutubia wananchi, fedha tutatafuta saa ngapi, tutalima saa ngapi, hivyo ni vyema tutambue kila kitu kinachofanyika kupitia mambo ya siasa kisiwe kisingizio cha kusema nchi haina amani, haina uhuru," amesema Cheyo.
Amesema viongozi wa dini wanapaswa kuwa kiunganishi cha wananchi na viongozi wa vyama vya siasa na si kufanya kinyume cha hilo.

Trump: Mazungumzo na Korea Kaskazini yatakuwa makubwa kwa dunia

President Donald J. Trump speaks to supporters at the Atlantic Aviation Hanger on March 10, 2018 in Moon Township, PennsylvaniaHaki miliki ya pichaJEFF SWENSEN/GETTY
Image captionTrump: Mazungumzo na Korea Kaskazini yatakuwa muhimu kwa dunia
Rais wa Marekani Donald Trump amesema mkutano ulipangawa na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un unaweza kufeli au ulete makubaliano makubwa zaidi kwa dunia.
Wakati wa mkutano wa kisiaza huko, Pennsylvania, Bw Trump aliwaamba wafuasi wake kuwa anaamini Korea Kaskazini inataka kuwe na amani.
Lakini amesema ataacha mazungumzo hayo kwa haraka ikiwa hayataangazia suala la kuharibu silaha za nyuklia.
Katika hotuba yake, Trump alionya kuhusu kodi kwa magari ya Ulaya na kuzindua kauli mbiu yake ya kuchaguliwa tena mwaka 2020.
Alisema ana matumaini kuwa makubaliano ya kupunguza misukosuko ya nyuklia yatafanyika kusaidia nchi kama Korea Kaskazini.
Pia alisema kuwa anaamini Korea Kaskazini wataheshimu ahadi za kutofanya majaribio zaidi ya makombora.
Mazungumzo kama haya yashawai kufanyika?
Hakuna rais wa Marekani ashawai kukutana na kiongozi wa korea Kaskazini lakini kumekuwa na majaribo kadha ya kuitaka Korea Kaskazini kuachana na mpango wa silaha za nyuklia.
Jitihada kubwa zaidi za mazungumzo ya pande sita yaliyovunjika mwaka 2008, kwa sababu Korea Kaskazini ilikataa kuruhusu wachunguzi kubaini ikiwa Korea Kaskazini ilikuwa imesitisha mipango yake ya nyuklia.
Majaribio kadhaa ya kufufua mazungumzo hayo yalishindikana, ikiwemo mwaka 2012 wakati Korea Kaskazini ilirusha kombora lingine, wiki mbili baada ya kutangaza makubaliano na Marekani.
Mazungumzo hayo yanaweza kufanyiwa wapi?
Kim Jong-un yuko chini ya vikiwazo kadhaa vya usafiri. Kwa hivyo kuna uwezoko kuwa anaweza kukutana na Trump nchini Korea Kaskazini.
Watakutana eneo lenye ulinzi mkali kwenye mpaka kati ya Korea Kaskazini na Kusini au labda huenda mkutano wao ukafanyika China.

Urusi yafanyia majaribio kombora lisiloweza kuzuiwa

missile with streak of light behind itHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionKombora la Kinzhal linaelezwa kuwa linaweza kusafiri mara kumi ya kasi ya sauti na linaweza kufika hadi kilomita 2,000
Urusi inasema kuwa imefanakiwa kulifanyia majaribio kombora lake lisiloweza kuzuiwa, moja ya makombora yaliyotangawa na Rais Vladimir Putin mapema mwezi huu.
Wizara wa ulinzi ya Urusi ilichapisha video ikionyesha kombora hilo likifyatuliwa kutoka kwa ndege ya vita na kuacha moshi nyuma.
Ilisema 'lengo' la kombora hilo liligongwa.
Tarehe mosi mwezi huu , Rai Putin alitangaza kuwa kombora la Kinzhal na la kiwango cha juu.
Kombora la Kinzhal linaelezewa kuwa linaweza kusafiri mara kumi ya kasi ya sauti na linaweza kufika hadi kilomita 2,000.
Wizara ya ulinzi ilisema kuwa kombora hilo lilifyatuliwa kutoka kwa ndege aina ya MiG-31 ambayo ilipaa kutoka uwanja ulio kusini magharibi mwa Urusi siku ya Jumamosi.
"Uzinduzi huo ulienda kulingana na mpango, kombora hilo liligonga lengo lake," wizara ilisema.
Putin anatarajiwa kuchaguliwa tena kama rais wa Urusi wiki moja inayokuja.
Kama sehemu ya hotuba yake kwa taifa ya tarehe mosi mwezi hu, alicheza kanda ya video ambayo ilionekana kuonyesha mvua wa makombora katika jimbo la Florida nchini Marekani.
Marekani ilijibu ikisema kwa hiyo haistahili kuwa taibia ya taifa kama Urusi.

Chama tawala China chaidhinisha "rais wa maisha"

Xi Jinping walking in front of delegates' tables and empty chairsHaki miliki ya pichaAFP
Image captionHatua hiyo sasa imemfanya Rais Xi Jinping, kusalia mamlakani hata baada ya muhula wake wa pili kumalizika mnamo mwaka 2023
Chama tawala cha National People's Congress nchini China, kimeidhinisha marekebisho ya kipengee cha katiba, ya kufutilia mbali uongozi wa mihula miwili kwa Rais wa nchi hiyo.
Hatua hiyo sasa imemfanya Rais Xi Jinping, kusalia mamlakani hata baada ya muhula wake wa pili kumalizika mnamo mwaka 2023 na kuendelea kuongoza kwa kipindi kisichojulikana.
Wakosoaji wameonya kuhusiana na hatari ya kuondoa muda wa mihula miwili ya uongozi wa Rais, ambayo ililetwa na Deng Xiaoping mwaka 1982.
Xi Jinping claps, looking slightly to the side of the frameHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionHatua hiyo sasa imemfanya Rais Xi Jinping, kusalia mamlakani hata baada ya muhula wake wa pili kumalizika mnamo mwaka 2023
Chama hicho kinasema kuwa, mabadiliko hayo yataupa nguvu na kuboresha mfumo wa uongozi nchini humo.
Yeyote anayepinga mabadiliko hayo, kwa hofu kuwa itampa nguvu zaidi mtu mmoja, amezimwa nchini humo.
Waandishi habari walinyimwa idhini ya kuingia Bungeni, kushuhudia zoezi hilo la kupiga kura likifanyika.

Radi yawaua watu wengi kanisani Rwanda

map showing Rwanda and Burundi with the former's capital Kigali marked out.
Image captionRadi yawaua watu wengi kanisani Rwanda
Radi imewaua takriban watu 16 na kuwajeruhiwa wengine kadhaa kwenye kanisa moja la KiAdiventista nchini Rwanda siku ya Jumamosi
Wengi wa waathiriwa walifariki papo hapo wakati radi ilipiga kwenye kanisa katika wilaya iliyo kusini mwa nchi ya Nyaruguru, kwa mujibu wa meya wa eneo hilo, Habitegeko Francois.
Watu wawili walifariki kutokana na majeraha, na watu 140 walikimbizwa hospitalini na vituo vya afya.
Radi pia ilimuua mwanafunzi eneo hilo siku ya Ijumaa kwa mujibu wa meya.
Ajali hiyo katika eneo lenye milima karibu na mpaka na Burundi, ilitokea saa za mchana wakati waumini walikuwa bado ndani ya kanisa.
Madaktari wanasema kuwa watu wangine watatu wako hali mahututi lakini wanapata nafuu, Bw Francois aliiambia AFP.
Alisema kuwa katika kisa cha siku ya Ijumaa, radi ilipiga kundi la wanafunzi 18 eneo hilo na kumuua mmoja.
Watatu kati ya wanafunzi hao wamebaki hospitalini huku wengine wakiruhisiwa kwenda nyumbani.

Saturday, March 10

WATOTO WASIORIPOTI MASHULENI WAZAZI WAO KUCHUKULIWA HATUA -SANGA


Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga imesema mpaka ifikapo machi 31 mwaka huu, itawachukulia hatua Kali za kisheria wazazi na walezi wote ambao watoto wao wamefaulu na hawajaripoti shuleni mpaka sasa kwa Sababu zisizo na msingi. 

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu Wa wilaya ya Mkuranga wakati akifungua kikao cha bajeti ya mwaka 2018/2019 cha baraza la madiwani kilicho fanyika wilayani humo,na kusema kuwa wanafunzi walioripoti ni 3,439 sawa na asilimia 46 na wanafunzi 217 hawajaripoti mpaka sasa ambao ni sawa na asilimia 5.46.

Aidha amesema mpaka ifikapo march 31 mwaka huu,wazazi na walezi ambao watakuwa hawajatoa taarifa zozote kuhusu sababu za watoto wao kutoripoti shuleni watachukuliwa hatua Kali za kisheria.

Aidha Sanga amewataka madiwani wote  wa wilaya hiyo kushirikiana nae kufuatilia kwa undani suala hilo ili kuhakikisha kuwa wanabaini changamoto zilizopelekea wanafunzi hao kutofika shuleni mpaka sasa."tunachotaka watoto wetu wasome,hatutaki kusukia mtu ameacha shule kwasababu ya kuolewa,wazazi watoe taarifa vinginevyo hatua zitachukuliwa dhidi yao".alisema Sanga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkuranga Juma Abeid amesema wamepitisha bajeti ya wilaya ya zaidi ya bilion 47 ya 2018/2019 ambayo imekidhi katika katika sekta zote na kipaumbele chao ni kwa mwaka huu ni elimu,afya na maji.

Abeid amesema elimu imepewa kipaumbele kwa sababu wananchi wengi wameitikia wito wa Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kupeleka watoto wao shule hivyo kusababisha utitiri aa wanafunzi hali inayopelekea uhaba Wa vyumba vya madarasa.

Naye Kaimu Mkurugenzi mtendaji Wa wilaya ya Mkuranga Peter Nambunga amesema wao wamelenga sana kwenye elimu na afya kwa sababu na jiografia ya wilaya hiyo pamoja na miundo kutokuwa rafiki hali inayosababisha Mwananchi kutembea umbali mrefu kufuata elimu na huduma ya afya.

Aidha Nambunga ameongeza kuwa katika harakati za kupunguza changamoto za huduma ya wanampango Wa kutafuta mobile clinic ili kuweza kuvifikia vijiji vya pembezoni kama koma na kwale.
Mwenyekiti Wa Halmashauri ya Mkuranga,Juma Abeid akizungumza na Madiwani wa Wilaya ya Mkuranga katika mkutano wa bajeti ya mwaka 2018/2019.Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya Jamii.
Diwani wa kata ya Mwanandege,Adroph Kowero akifafanua jambo katika mkutano huo.
Madiwani wakimsikiliza Mwenyekiti Wa Halmashauri ya Mkuranga,Juma Abeid.

MNEC SALIM ASAS BADO ANAUMIZWA NA USHINDI WA MBUNGE MSIGWA WA MWAKA 2015

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) MNEC Salim Asas bado anaumizwa na matokeo ya ubunge wa jimbo la Iringa mjini baada ya wapinzani kushinda kwa kishindo mwaka 2015 kwa ni jambo ambalo hakulitegemea.
Akizungumza wakati wa baraza la UWT manispaa  ya Iringa Asas alisema kuwa usaliti uliofanywa katika uchaguzi wa mwaka 2015 umekuwa ukimuumiza hadi sasa na kitendo anafikiri kitadumu moyoni mwake hata kwa miaka kumi kwakuwa bado anakumbuka mara kwa mara.

“Naombeni niongee ukweli kitendo kilichofanywa na wanaCCM wa manispaa ya Iringa katika uchaguzi wa mwaka 2015 kilikuwa kitendo ambacho ni usaliti mkubwa ambao unaumiza sana kichwa changu” alisema Asas

Asas alisema kuwa uchaguzi huo kulikuwa na wanaCCM wengi ambao mchana walikuwa CCM  na usikuwa walikuwa kwa wapinzani hivyo lazima tuondoe usaliti kwenye chama bila hivyo tutaendelea kushindwa kila siku.

“Unakuta rasilimali zilizokuwa zinatolewa na  CCM zote zinatumika kwa wapinzani kuhakikisha wanaiangusha,sasa hicho kitu ndio ambacho kinaniumiza sana kichwa hadi hii leo” alisema Asas.

Asas aliutaka umoja wa wanawake (UWT) manispaa ya Iringa kufanya kazi kwa umoja unatakiwa na kuhakikisha kuwa ccm inakuwa ila na isiyo na makundi ili kufika mwaka wa uchaguzi wanashinda kwa kishindo kwa kutumia umoja wao.
“Nawaombe muutunze umoja huu ambao sasa mnao hadi kipindi cha uchaguzi wowote ule ambao upo mbele yetu na kuhakikisha kuwa tunashinda kila chaguzi kwa kishindo kwa kuwa nyie akina mama ndio huwa mnakula ambazo haziamishiki” alisema Asas
Kwa upande wake mwenyekiti wa UWT manispaa ya Iringa Ashura jongo alimuhakikishia MNEC Salim Asas kuwa kosa lilofanyika mwaka 2015 halitajirudia tena katika chaguzi yoyote ambayo itakuwa inafanyika katika manispaa ya Iringa.
“Ndugu MNEC kwa kweli tumejifunza na tunajutia kitu kilichofanyika mwaka 2015 hivyo tunakuhadi kuwa kwenye umoja wetu wa wanawake Manispaa ya Iringa hakitaa tokea kama kilivyotokea,na tutashinda chaguzi zetu kwa kuwa kila mtu anaumia na kilichotokea mwaka 2015” alisema Jongoo.
“Mheshimiwa MNEC umoja ambao tunao hivi sasa tunatakiwa kuulinda na kuudumisha hadi kipindi cha chaguzi zote na kuhakikisha kuwa ccm inashinda kwa kushinda na kuendelea kuwa ngoja ya chama hicho kama ilivyokuwa hapo awali” alisema Jongoo
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) MNEC Salim Asas  akiwahutubia wajumbe wa baraza kuu la umoja wa wanawake manispaa ya Iringa na kusema kuwabado anaumizwa na matokeo ya ubunge wa jimbo la Iringa mjini baada ya wapinzani kushinda kwa kishindo mwaka 2015 kwa ni kitendo ambacho hakukitegemea.
Mwenyekiti wa umoja wa wanawake UWT manispaa ya Iringa Ashura jongo akimtoa hofu MNEC Salim Asas juu ya kukomba jimbo baada ya kulipoteza kwa kusalitia mwaka 2015 
 Baadhi ya wageni waliokuwa wamealikwa kwenye baraza hilo kwa ajili ya kujifunza na kutoa mapendekezo pale wanapopata nafasi
 Baadhi ya viongozi wa chama cha mapinduzi mkoani Iringa walipokuwa wakimsikiliza kwa umakinimjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) MNEC Salim Asas alipokuwa anatoa ya moyo kuhusu kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2015