Saturday, November 18

Jeshi la Polisi lasaidiwa vifaa tiba


Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limepokea vifaa tiba kutoka shirika la Project Cure la nchini Marekani vyenye thamani ya Sh2 bilioni.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Siro akizungumza alipopokea vifaa hivyo katika Hospitali Kuu ya Polisi Kilwa Road leo Ijumaa Novemba 17,2017, amesema vitasambazwa katika vituo vya tiba vya polisi 20.
IGP Siro amesema wanalenga kuhakikisha askari wanapata huduma bora na kuwafanya wawe imara katika kutekeleza majukumu yao.
“Tutajitahidi kuwasomesha wataalamu wetu wa afya ili waweze kufanya kazi kwa weledi. Hospitali kuu ya polisi ipo vizuri, hivyo tunawakaribisha kwa yeyote atakayehitaji kutibiwa hapa kwa kuwa ina vifaa bora,” amesema IGP Siro.
Pia, amezindua majengo matatu katika hospitali hiyo ambayo ni kwa ajili ya  wagonjwa mahututi, stoo kuu ya dawa na jengo la kuhifadhia maiti.
Kamanda wa Afya, Paul Kasabago amesema wanakabiliwa na changamoto ya vifaa tiba katika wodi ya wagonjwa mahututi itakayofunguliwa.
Kasabago amesema wanahitaji mashine za CT- scan na MRI ili kuendelea kuboresha hospitali hiyo iweze kutimiza vigezo vya kuwa hospitali ya rufaa.
Ameishukuru Serikali ya watu wa Marekani kupitia shirika la misaada la USAID kwa kufadhili juhudi za Serikali ya Tanzania katika kupambana na Ukimwi kupitia shirika lisilo la kiserikali la JSI na AIDSfree Tanzania linalofanya kazi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika majeshi ya Polisi na Magereza.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la JSI, Peter Maro amesema mradi wa AIDSFree umetoa mafunzo kwa watumishi wa afya katika nyanja mbalimbali za utoaji wa huduma za Ukimwi na Kifua Kikuu.

Mgombea udiwani kizimbani kwa kujeruhi


Mwanza. Mgombea udiwani kata ya  Mhandu (Chadema), Godfrey Misana na kampeni meneja wake, Charles Chinjibela, wamepandishwa kizimbani kujibu shtaka la kujeruhi.
Misana (46) na Chinjibela (37) wanadaiwa kumjeruhi meneja wa kampeni za CCM katika kata hiyo, Thomas Warioba.
Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, mbele ya hakimu Ainawe Moshi wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 14,2017.
Akisoma mashtaka katika shauri hilo namba 540/2017, mwendesha mashtaka wa Jamhuri, Elizaberth Barabara amedai leo Ijumaa Novemba 17,2017 kuwa washtakiwa walitumia visu na mawe kumjeruhi Warioba.
Kabla ya kuhamia CCM, Warioba alikuwa mwanachama wa Chadema.
Upande wa Jamhuri umeiomba Mahakama kuzuia dhamana ya washtakiwa kwa kile ilichoeleza ni kwa usalama wao.
Ombi hilo la Jamhuri limepingwa na wakili wa utetezi, Gasper Mwanaliela.
Wakili Mwanaliela amesema dhamana ni haki ya wateja wake na kwamba, kuwanyima kutawazuia kushiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani unaotarajiwa kufanyika Novemba 26,2017.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Moshi amesema Mahakama itatoa uamuzi kuhusu dhamana Novemba 21,2017.
Washtakiwa wamepelekwa mahabusu hadi siku huyo.

Vurugu, mabomu vyatawala mapokezi ya Raila


Nairobi, Kenya. Vurugu, mabomu ya machozi, na mapambano ya kukimbizana ni baadhi ya matukio yaliyogubika mapokezi ya kiongozi wa muungano wa Nasa Raila Odinga katikati ya jiji la Nairobi aliporejea jana akitokea Marekani alikofanya ziara ya siku 10.
Polisi walitumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya wafuasi wa Nasa ambao walijitokeza kwa mamia kumpokea Raila. Kuna madai kwamba risasi zilitumika na pia inadaiwa watu wawili walikufa katika makabiliano huo
Kioo cha mbele cha gari alilopanda Raila kiliharibiwa wakati polisi wakifukuzana na wafuasi wa kiongozi huyo. Hata hivyo, haikuweza kufahamika mara moja ikiwa kiliharibiwa kwa risasi au jiwe.
Kioo hicho kiliharibiwa katika Barabara ya Jogoo. Raila hakudhuriwa na msafara wake uliongoza moja kwa moja hadi Kibra ambako alihutubia mkutano mkubwa wa wafuasi wake.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani Mwenda Njoka alitupilia mbali madai ya kuwepo jaribio la kutoa uhai wa Raila. "Madai kwamba lilikuwepo jaribio la kutoa uhai wa Raila ambayo yanasambazwa kwenye mitandao ya kijamii ni ya uongo na hayana msingi,” alimsema katika ujumbe wa Twitter.
Njoka alisema madai hayo yanayosambazwa kupitia akunti iliyothibitika kuwa ni ya muungano wa Nasa ina lengo la kuomba huruma. “Madai hayo yapuuzwe na yadharauliwe,” alisema.
 Msafara wa Raila
Raila aliondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) katika msafara wa makumi ya magari yaliyoongozana nay a viongozi wa Nasa pamoja na mamia ya wafuasi wao.
Wafuasi wake walijimwaga mitaani tangu alipotua. Baadhi walilazimisha kufika na kuingia kwenye uwanja wa ndege ambako walizuiwa na polisi walikuwa wamejihami kwa silaha, mabomu ya kutoa machozi, magari ya kurusha maji ya kuwasha na helikopta.
Baadaye hali ilibadilika kuwa ya vurugu na mapambano kati ya polisi na wafuasi wa Nasa ambao walikuwa wakichoma matairi barabarani, wakiweka vizuizi, wakiwakejeli polisi na kuwarushia mawe, vijinga vya moto huku wakiimba.
Vurugu zilianza baada ya msafara wa Raila kuondoka JKIA lakini ukaingia kimakosa katika barabara ya Mombasa. Hii ni kwa sababu barabara hiyo ilikuwa na msafara mrefu umbali wa kilomita kadhaa kutokana na mapambano ya polisi na wafuasi wa Raila.
Wafuasi wa Nasa walitaka kulazimisha kuingia kwenye uwanja wa ndege lakini polisi waliwarushia mabomu ya kutoa machozi eneo la City Cabanas na maeneo mengine ili kuwazuia.
Baadaye msafara huyo uliacha barabara ya Mombasa na kuingia Barabara ya Jogoo lakini vurugu ziliufuata msafara wa Raila na wafuasi wake baada ya polisi kupambana na vijana walikuwa wakirusha mawe.
Lengo lao lilikuwa kutembea kwa miguu katika Barabara ya Jogoo kisha Haile Sellasie halafu waende viwanja vya Uhuru Park, lakini ilishindikana kutokana na mkabiliano wa ghasia.
 Hasara
Mapambano kati ya polisi na wafuasi wa Nasa yalisababisha biashara kusimama katika barabara hiyo ya kibiashara upande wa mashariki mwa jiji.
Mzunguko katika Uwanja wa Jiji ulitulia baada ya polisi kuziba barabara katika juhudi za kuzuia vurugu kuenea katika maeneo mengine ya jiji. Kwa kipindi kirefu magari yalitulia huku vibanda vya biashara vikifungwa na wauzaji wakikimbia kwa usalama wao.
Basi dogo linalomikiwa na kampuni ya Forward Travellers sacco, lori la polisi na mikokoteni miwili vyote vilichomwa moto nje ya soko la Burma. Barabarani kulikuwa na moshi wa matairi yaliyochomwa moto uliochanganyika na hewa ya machozi iliyopigwa kwa mabomu ya polisi.

Spika aunda kamati mbili kuchunguza sekta ya uvuvi, gesi


Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai ameunda kamati mbili zitakazoshughulikia sekta ya uvuvi wa bahari kuu na gesi akisema lazima wajue ni kwa nini hazichangii pato la Taifa.
Ndugai ameunda kamati hizo baada ya zingine mbili za kutathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya Tanzanite na almasi kuwasilisha taarifa kwa Rais John Magufuli Septemba,2017 na kusababisha baadhi ya mawaziri kujiuzulu.
Akitangaza kamati za sekta ya uvuvi na gesi bungeni mjini Dodoma leo Ijumaa Novemba 17,2017, Spika Ndugai amemrejesha Dotto Biteko aliyeongoza kamati iliyochunguza Tanzanite kuwa mwenyekiti wa kamati itakayochunguza sekta ya gesi.
Mussa Zungu alikuwa mwenyekiti wa kamati iliyochunguza almasi na sasa ni mjumbe katika kamati ya uvuvi.
Ndugai akitangaza kamati hizo amesema anatumia kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Bunge toleo la 2016 ambayo inampa madaraka ya kuziunda kwa kadri atakavyoona inafaa.
Amesema kumekuwa na hali ya kusuasua kwa sekta hizo, ukiwemo uvuvi wa bahari kuu. Amesema sekta hiyo inachangia pato la Taifa kwa asilimia 1.4 ambayo ni sawa na Sh3.2 bilioni wakati kuna zaidi ya Sh400 bilioni ambazo zinapotea bure.
Spika Ndugai amewataja wajumbe wa kamati ya sekta ya uvuvi itakayoongozwa na Anastazia Wambura kuwa ni Zungu, Salum Mwinyi Rehani, Masoud Salim Abdalla, Tauhida Nyimbo, Mbaraka Dau, Dk Immaculate Semesi, Dk Christina Ishengoma, Stanslaus Mabula, Mussa Mbarouk na Cosato Chumi.
Kamati ya sekta ya gesi itaundwa na Innocent Bashungwa, Dastan Kitandula, Dk Seleman Yusufu, Wanu Hafidhi Ameir, Oscar Mukasa, Ruth Mollel, Richard Mbogo, Omari Kigua, Abdallah Mtolea na Sebastian Kapufi.
Spika Ndugai amemwagiza Katibu wa Bunge kuwawezesha wabunge hao ili waanze kazi na kamati zimetakiwa kufanya kazi ndani ya siku 30 tangu siku watakayokabidhiwa majukumu yao.

Abiria mmoja anusurika ajali ya ndege iliyoua 11 Ngorongoro


Arusha. Mfanyakazi wa hoteli za kitalii za andBeyond Serengeti, Moses Muhina aliyetajwa kuwa ni miongoni mwa abiria waliofariki dunia katika ajali ya ndege ya shirika la Coastal Aviation, imebainika alibadili ndege muda mfupi kabla ya safari ili kuwahi kazini.
Muhina ambaye ni mwongozaji watalii katika hoteli hiyo, alikuwa aondoke na ndege ya Coastal Aviation saa nne asubuhi lakini viongozi wa hoteli walimbadilishia ndege, hivyo aliondoka na Air Exel iliyofika salama Serengeti.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Novemba 17,2017 Meneja Uendeshaji wa hoteli ya andBeyond Serengeti UnderCanvas, Mussa Matala amesema Muhina ambaye anasomeka kwenye orodha ya ndege kama Maina alikuwa apande ndege hiyo lakini waliamua kumbadilishia ili awahi kazini.
Amesema waliomba aondolewe kwenye orodha ya wasafiri wa ndege hiyo lakini kwa bahati mbaya hadi ndege ilipoondoka jina lake lilikuwepo.
Wakati huohuo, raia watano wa kigeni ambao walifariki dunia katika ajali ya ndege ya Coastal Aviation, akiwemo rubani, Dewald Raubenheimer raia wa Afrika Kusini, ambaye kwenye orodha ya awali ya waliofariki jina lake halikuwepo inatarajiwa kusafirishwa Jumapili Novemba 19,2017.
Mhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti  katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, Francis Costa amesema miili mitatu kati ya 11 imechukuliwa na ndugu.
Amesema miili iliyochukuliwa ni ya ndugu wawili waliokuwa wakurugenzi wa Masai Wondering, Nasibu na Shatri Mfinanga. Mwingine ni wa Joyce Mkama ambaye alikuwa mfanyakazi wa hoteli ya Serena.
"Uchunguzi wa miili ya wageni kutoka nje ya nchi unaendelea na ukikamilika itasafirishwa kwa mazishi katika nchi za Afrika Kusini, Ujerumani na Italia," amesema.
Ndege hiyo namba 5H-EGG aina ya Cessna Grand Caravan ilianguka baada ya kugonga kingo za creta ya Empakai, umbali wa mita 3,250 kutoka usawa wa bahari ikitoka Kilimanjaro kwenda Hifadhi ya Serengeti.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo amesema uchunguzi unaendelea kuhusu ajali hiyo.

Friday, November 17

USAID funded projects in Iringa voiced how keen their, in transforming people live

 The Chief of Party of the Sauti Project a Jhpiego’s lead program Dr. Albert Komba elaborating a point to the USAID Mission Director in Tanzanian Andy Karas when he visited projects interventions conducted to reduce HIV/Aids prevalence to the vulnerable groups in Iringa. The program is conducting Behavior Change Communication Sessions, Screening for Gender Based Violence and cancelling on usage of Alcohol and Drugs to the Vulnerable groups including young girls.
 Scholina Charles (22) a young girl from umoja groups in iringa giving her testimony to the USAID Mission Director in Tanzanian Andy Karas and his delegation on the risk she went through before joining the Sauti project to fight HIV/ AIDS. Looking center is the Sauti Project Chief of Party Dr. Albert Komba .
 The USAID Mission Director in Tanzanian Andy Karas,  Deputy Mission Director Helen Pataki (second right), Jhpiego Country Director (right) and Sauti Project Chief of Party Dr. Albert Komba (left) following a Behavior Change Communication Sessions conducted by Zera Mingo (23) to the young adolescences girls as part of HIV/ AIDS intervention to reduce HIV/Aids prevalence to the vulnerable groups in Iringa.
 The USAID Mission Director in Tanzanian Andy Karas and his Deputy Mission Director Helen Pataki looks at the clothes made by Mwanahamisi Mketo (23) during his field visit in Iringa to assess the implementation of USAID funded Project activities. Mwanahamisi Mketo she is a member of Behavior Change Communication group conducted by Jhpiego at kihesa ward in Iringa who are also economically empowered. 

The United State Agency for International Development (USAID) funded projects in iringa has demostrated how their bringing impacts to the lives of the people in Iringa. This expression was made by USAID funded NGO’s and local CSO’s to the newly USAID Mission Director in Tanzanian Andy Karas who conducted a field visit in Iringa to assess the implementation of USAID funded Project activities.

Andy who was accompanied by his deputy Mission Director Helen Pataki and other USAID staff expressed his appreciation to the regional administration and local authorities for the support their giving to all implementing partners funded by USAID in the region and thanks them for their work their doing for the people of Iringa.    

Explaining on how they engage the local authorities and the entire community to fight the spread of the HIV/AIDS in Iringa, the Chief of Party with Sauti Project a Jhpiego’s lead program Dr. Albert Komba said despite the fact that the project works in 14 region countrywide, in Iringa Municipal they targets all Vulnerable groups including young girls by  linking them into services like Behavior Change Communication Sessions, Economic Empowerment groups, Screening for Gender Based Violence and cancelling on usage of Alcohol and Drugs.

“we are working to ensure we reduce the spread of HIV/AIDS because the groups we are targeting like these adolescence girls and female sex workers are more vulnerable and engaging them in the fight against HIV will lead to an HIV/AIDS free generation in Iringa” said Dr. Komba

As part of their interventions to reduce HIV/Aids prevalence, the project also has mobilized girls to form WORTH+ groups which is the voluntary money saving groups for income generating activities, and train them on economic empowerment, gender issues and how to protect themselves against high risk behaviors of which most girls from these groups have managed to change their lives by living a decent life.

Reaching a testimonie delivered by Scholina Charles (22) a young girls from umoja groups on the risk she went through before joining the sauti project, she said the situation was devastating and because of her economic status from her family she got engaged into sex business as part of income generating.

“The situation was bad, I remember men used to bribe me even for two hundred shilling to have sex with them and I had no option. But now that I have joined this group, I am empowered with self-awareness on the risk of HIV/AIDS, gender violence, and through this group I have also managed to raise money and now I am engaging into agricultural activities and employ men in my maize farm”. Said Scholina.

Earlier speaking with USAID delegation and other USAID funded implementing partners, the Iringa Regional Administration Secretary Wamoja Ayubu thanks the delegation for the support they are giving to the region level by complimenting government effort in the health sector agriculture sector and other sectors especially by emphasizing the inclusion and empowerment of youth and woman. 

“The government has policy and laws which advocates for the inclusion of gender especially youth and woman in all activities, I am happy that USAID is also advocating that and we promise to collaborate with all partners to empower them especially locals so that they bring up new ideas for development and at the regional level. In our side we will chip in to address all challenges that might be faced by our implementing partners” she insisted.

Sauti is implemented by Jhpiego in partnership with Pact, Engenderhealth and NIMR/ Mwanza with support from the American people through USAID under the United States President’s Emergency Plan for AIDS Relief (PEPFAR) and DREAMS Initiatives.

MICHORO YA WATOTO KUTOKA TANZANIA WAZAWADIWA FINLAND

Michoro mitatu iliyochorwa  na watoto kutoka Tanzania hivi karibuni ilitunukiwa tuzo ya heshima ya vyeti vya stashahada ya maonesho na Taasisi ya Sanaa za watoto na vijana ya Hyvinkää, Finland.

Bryton Manyewa(10), Neev  Mistry (9) wa shule ya Academic International Primary na Mandela Mtaya (5) wa shule ya chekechea ya Upendo Montessori ndiyo waliofanikiwa kupata tuzo hiyo kwa upande wa Tanzania baada ya  kushiriki shindano la michoro liloitwa 'Pamoja' lililotayarishwa na taasisi hiyo ya nchini Finland.

Zaidi ya michoro 6800 toka katika nchi 66 duniani zilishiriki shindano hilo ambapo majaji ambao walikuwa ni wachoraji magwiji a sanaa wa nchi hiyo walichagua michoro 670 kushiriki katika maonesho yaliyoanza Oktoba mwaka huu na yatamalizika 18 Januari 2018 kwenye ukumbi wa Taasisi hiyo inayojihusisha na elimu ya Sanaa kwa watoto na vijana ukuzaji wa muingiliano wa utamaduni wa nchi mbalimbali. 

Maonesho hayo yanaweza pia kutazamwa katika mfumo wa Kidijitali kupitia tovuti ya Taasisi hiyo www.artcentre.fi

Katika miaka ya nyuma, kwa ufadhili wa ubalozi wa Finland nchini, baadhi ya watoto kutoka Tanzania waliweza kuhudhuria mafunzo ya Sanaa yanayotolewa na taasisi hiyo
 

MUHIMBILI YAADHIMISHA SIKU YA MTOTO NJITI DUNIANI


  Kaimu Mkuurugenzi wa Kinga katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Janneth Mghamba akizungumza kwenye maadhimisho ya mtoto Njiti Duniani ambayo huadhimishwa Novemba 17 kila mwaka. Kushoto ni Mkurugenzi wa Tiba Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Hedwiga Swai.
  Mkurugenzi wa Tiba Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Hedwiga Swai akizungumza na kinamama pamoja na wataalamu wengine wa afya katika siku ya mtoto njiti duniani. Kulia ni Kaimu Mkuurugenzi wa Kinga katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Janneth Mghamba, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Afya ya Uzazi na Mtoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Felix Bundara na Kushoto ni Mkuu wa Idara ya Watoto, Dkt. Merry Charles.
 Baadhi ya kinamama wenye watoto njiti wakiwa kwenye maadhimisho hayo leo Muhimbili. 
 aktari Bingwa wa Watoto, Dkt Agustino Massawe akiweka saini kuthibitisha kuukoa maisha ya watoto njiti.

Serikali imesema imeweka mikakati endeleveu  ya kupunguza vifo vya watoto njiti kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Neema Rusibamayila katika Siku ya Kimataifa ya Watoto Njiti ambayo huadhimishwa kila mwaka Novemba 17.

“Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la vifo vya watoto wachanga chini ya mwezi mmoja hivyo kutokana na hali hii tunapaswa kudhibiti vifo kwa watoto wachanga,” alisema  Dkt. Rusibamayila.

Alisema takwimu zinaonyesha asilimia 13 hadi 17 ya watoto wote wanaozaliwa Tanzania ni njiti na kwamba kutokana na hali hiyo Serikali kupitia Wizara ya Afya, imekuwa ikiratibu progamu mbalimbali   za kupunguza  vifo vya watoto wachanga na wa chini ya miaka mitano.

Mkurugenzi huyo alisema moja ya program hizo ni kumsaidia mtoto kupumua baada ya kuzaliwa, kupanua huduma za watoto wachanga kwa kujenga wodi za watoto wachanga katika hospitali za manispaa na wilaya pamoja na kutoa mafunzo kwa wa hudumu wa afya jinsi ya ya kuhudumia watoto wachanga.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru alisema kuwa hospitali hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kutoa kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wauguzi na madaktari wa kitengo cha watoto wachanga ili kuongeza ufanisi wa kazi.
“Pia tumeongeza wodi mpya ya watoto wachanga na kukarabati wodi ya za zamani ili kutoa huduma bora kwa watoto wengi zaidi. Sambamba na kuongeza wodi nyingine, pia tunatarajia kuzindua wodi maalumu ya watoto wachanga mahututi (NICU) katika maadhimisho haya. Ili kutapunguza msongamano wodini,” alisema Profesa Museru.

Profesa Museru alisema hospitali imepiga hatua kubwa katika kuboresha huduma kwa watoto wachanga kama vile kuongeza vifaa tiba katika kitengo cha watoto wachanga zikiwamo mashine za kusaidia watoto kupumua, dawa ya kukomaza mapafu kwa watoto njiti.

“Katika kuadhimisha siku hii muhimu kwa watoto, Hospitali ya Taifa Muhimbili inajivunia kuwa na wodi maalumu yenye wauguzi waliobobea kwenye kutoa huduma na mafunzo kwa kina mama wenye watoto njiti wenye uzito wa kuanzia gramu 500 kwa njia ya Kangaroo mother care. Nina imani kuwa wamama wote wanaolazwa wodi ya Kangaroo ni walimu na mabalozi wazuri kwa wa mama wenzao,” alisema Profesa Museru.

Profesa Museru Muhimbili imefanikiwa kwa asilimia kubwa kupunguza vifo vya watoto wachanga kutoka asilimia 19.8 mwaka 2015/2016 hadi asilimia 7.4 mwaka 2016/17.

“Idadiya watoto waliolazwa kwenye wodi ya Kangaroo walikuwa kati ya gramu 500 na kilo 1.5 na idadi kubwa ya watoto waliotunzwa katika wodi ya Kangaroo waliofanikiwa kutoka wodini na uzito wa kilo 1.6 hadi 1.7 ambayo ni sawa na asilimia 99.5 ya watoto wote waliolazwa wodi ya kangaroo.

Alisema changamoto ni upungufu wa vifaa tiba, gharama kubwa ya kununua dawa za kukomaza mapafu na idadi ndogo ya watoa huduma.

Serikali Yawakaribisha wawekezaji kutoka China kuja kuwekeza kwenye miradi mbalimbali ya madini nchini

Waziri wa Madini, Angellah Kairuki ametoa wito huo Novemba 16, 2017 Jijini Dar es Salaam alipokutana na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Wang Ke na ujumbe alioambatana nao Wizarani hapo kutoka kwenye Ubalozi huo ili kujadiliana masuala mbalimbali ya madini ikiwemo fursa za uwekezaji.

Waziri Kairuki alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini na hivyo zipo fursa lukuki za uwekezaji ambazo zinaweza kutumiwa na kampuni za nchini China kwa manufaa ya pande zote mbili.

“Rasilimali za madini ni nyingi na hivyo zipo fursa mbalimbali ambazo zinaweza kutumiwa na kampuni za China na wakati huo huo kuchangia katika uchumi na pato la Taifa kwa ujumla,” alisema Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki vile vile alisema yapo maeneo ambayo wawekezaji wanaweza kushirikiana na Serikali ambapo alitaja baadhi yake kuwa ni uchimbaji wa madini kwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), tafiti za utambuzi wa maeneo yenye madini kwa kushirikiana na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Chuo cha Madini (MRI).

Aidha, aliongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha madini yanayochimbwa nchini yanaongezwa thamani kabla hayajasafirishwa ili kukuza uchumi wa Taifa na wakati huo huo, kuongeza mapato ya Serikali na kuzalisha ajira zaidi.

“Madini yakiongezwa thamani hapa nchini, faida zitakazopatikana ni nyingi na ni kubwa ikiwemo ajira lakini pia mapato nayo yataongezeka kwa kuelewa thamani halisi ya madini husika,” alisema Waziri Kairuki.
Kwa upande wake Balozi Ke alipongeza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuwaletea wananchi wake maendeleo endelevu.

Alisema Serikali ya China itaendeleza ushirikiano wa karibu na wa dhati na Serikali ya Tanzania hususan kwenye Sekta ya Madini ili kuhakikisha sekta hiyo inaleta tija iliyokusudiwa kwa Taifa.

Alisema kampuni mahiri nyingi kutoka China tayari zimeonyesha nia ya kuwekeza kwenye Sekta ya Madini na ziko tayari kuja kuwekeza Nchini. 
 Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kulia) akizungumza na Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke na ujumbe alioambatana nao (hawapo pichani) walipomtembelea Ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (kulia) akimsikiliza Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke alipomtembelea Ofisini kwake jijini Dar es Salaam ili kujadili masuala mbalimbali.
 Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke (kulia) akiwa na ujumbe wake kutoka Ubalozi wa China nchini Tanzania walipomtembelea Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (hayupo pichani) ili kujadili masuala mbalimbali ya Sekta ya Madini.

 Waziri wa Madini, Angellah Kairuki (wa pili kutoka kulia) akijadiliana jambo na ujumbe kutoka Ubalozi wa China nchini ulioongozwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke (katikati).

SERIKALI YADHAMIRIA KUIMARISHA KAMPUNI YA TTCL

SERIKALI ya Tanzania chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, imedhamiria kuiimarisha Kampuni ya Simu nchini (TTCL) iIi iweze kuingia kwenye ushindani wa kibiashara dhidi ya makampuni mengine ya simu.
Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, Waziri Kindamba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam.
Kindamba alisema hayo kufuatia Novemba 14, mwaka huu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujadili na kupitisha miswada ya mapendekezo ya mabadiliko ya sheria yanayofuta sheria iliyounda Kampuni ya Simu ya TTCL (Tanzania Telecomunication Company, Incoporation Act 2002) na kutunga sheria inayounda Shirika la Mawasiliano Tanzania (Tanzania Telecommunication Corporation Act 2017).
Aliongeza kuwa, kujadiliwa na kupitishwa kwa muswada huu bungeni kunafuatia hatua za awali za miswada ya serikali ambapo maoni ya wananchi na wadau wa huduma za mawasiliano yalikusanywa na kuchambuliwa.
Aidha, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni zilichambua muswada huu na kuutolea mapendekezo yao, ambapo Kindamba alisema mambo muhimu yanayotajwa katika sheria hiyo mpya ni pamoja na; Kuweka utaratibu utakaowezesha TTCL kutekeleza majukumu yake kama shirika la Umma. Kuweka jukumu la ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa miundombinu ya kimsingi ya Taifa, Kuweka mazingira ya kinga ya mali (Asset) na miundombinu muhimu ya mawasiliano ya shirika na Kuanzishwa kwa shirika na kuainisha uongozi wa shirika.
Mambo mengine ni pamoja na Kuanisha vyanzo vya mapato na mtaji wa shirika, Kuanisha sheria zingine zitakazoguswa, Sheria kutumika pande zote za muungano na Kufuta kampuni ya simu Tanzania na kuanzisha shirika la mwasiliano Tanzania.
Kindamba aliongeza kuwa, katika mapendekezo ya sheria mpya yaliyoridhiwa na Bunge, Shirika la Mawasiliano Tanzania linapewa jukumu la msingi la kutoa huduma za mawasiliano kwa Taifa na kuhakikisha kuwa huduma hizo zinatolewa kwa viwango vya juu vya ubora.
Aidha, Kindamba alisema sheria mpya inataja jukumu jingine kuwa ni kusimamia na kuendeleza miundombinu ya Ki-Mkakati ya Mawasiliano kama vile Mkonga wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), Kituo Mahiri cha kutunzia kumbukumbu (National Data Centre) na miundombinu mingine itakayokuja siku za usoni.
Awali majukumu hayo yalikuwa yanafanywa na TTCL kwa niaba ya serikali bila kutajwa katika sheria. Amesema, miongoni mwa upungufu ulioonekana katika sheria ya awali ni kuwa, sheria hiyo ililenga kuwezesha mazingira ya ubia ndani ya TTCL, hitaji ambalo sasa halipo tena kutokana na TTCL kurejea mikononi mwa serikali kwa asilimia mia moja.
Kupitia utaratibu huo wa ubia, kwa kipindi cha miaka 15, TTCL ilimilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 65 na Kampuni ya Bharti Airtel ya India kwa asilimia 35.
Kaimu ofisa mtendaji huyo mkuu wa TTC L amesema, ubia huo ulifikia ukomo Juni 2016 baada ya Bharti Airtel ya India kulipwa jumla ya Tsh 14.7 Bilioni na kuondoka ndani ya TTCL.
Kindamba amesema hoja mahususi ni kwamba Shirika la Mwasiliano ni chombo muhimu katika ustawi wa nchi na kuongeza kuwa sheria mpya itaongeza ufanisi na tija katika shirika hilo ili liweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya Watanzania wote.
“TTCL ni taasisi yenye hazina kubwa ya watendaji wenye weledi na uzoefu mkubwa wa shughuli za mawasiliano hapa nchini,” alisema Kindamba na kuongeza; TTCL imeonesha weledi na uzoefu mkubwa katika kusimamia na kuendesha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye mtandao wa takriban kilomita elfu saba na mia nne nchi nzima.
Aidha, Kindamba amesema TTCL inasimamia na kuendesha kwa ufanisi mkubwa kituo mahiri cha kuhifadhi kumbukumbu (National Data Centre) kinachohudumia taasisi 28, taasisi 19 za serikali na taasisi 8 za sekta binafsi hadi sasa. “Makampuni yote ya mawasiliano na wadau mbalimbali wa biashara wanaotumia huduma zaTTCL wanaridhika sana na huduma inayotolewa,” alisema Kindamba na kuongeza;
“Kuhusu kuipa mtaji TTCL, serikali imeandaa mpango mkakati wa miaka mitano 2017/18-2021/2022 ambao pamoja na mambo mengine utaainisha mtaji unaohitajika na serikali ambapo serikali itatekeleza mpango huo.”
Aliongeza kuwa, kuhusu idadi ya wajumbe wa bodi kutoka Zanzibar, serikali imeridhia idadi hiyo kuongezeka kutoka mjumbe mmoja na kuwa wawili.

Kindamba amesema ieleweke kwamba mabadiliko haya ya sheria kutoka Kampuni ya Simu Tanzania kuwa Shirika la Mawasiliano Tanzania hayaathiri mikataba na makubaliano ya kibiashara yaliyofikiwa awali kati ya TTCL na wateja na wadau wa huduma zake.
Amesema madeni ambayo TTCL inadai wateja wake na ambayo TTCL inadaiwa na watoa huduma mbalimbali yapo palepale na yataendelea kufanyiwa kazi kwa mujibu wa makubaliano na mikataba ya kiabishara iliyofikiwa.

“TTCL ipo imara na thabiti zaidi kuliko ilivyokuwa awali kwa kuwa sasa inatarajia kupata mamlaka zaidi na uwezo zaidi wa kuhudumia umma,” alisema Kindamba.
Akielezea mustakabali wa ajira za wafanyakazi wa kampuni hiyo baada ya mabadiliko hayo, Kindamba amesema ajira zao ikiwa ni pamoja na mali na miuondombinu viko salama.

Kindamba amesema huduma zinazotolewa na TTCL yaani simu za mezani, simu za kiganjani, data na TTCL PESA zinaendelea kutolewa kwa ufanisi mkubwa na kuongeza kuwa huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo mahiri cha kutunzia kumbukumbu (National Data Centre) pia zinaendelea kutolewa kama kawaida na kwa weledi wa hali ya juu.
“Kilichobadilika ni sheria ya kampuni ya simu Tanzania ambayo sasa ni shirika la mawasiliano Tanzania ambapo mapendekezo haya yanasubiri idhini ya mheshimiwa rais ili kuwa sheria kamili,” amehitimisha Kindamba.

KESI YA JALADA LA VIGOGO WA SIMBA LAREJESHWA TAKUKURU.


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Novemba 17, imeambiwa jalada la kesi inayowakabili vigogo wa Klabu ya Simba Evans Aveva na Godfrey Nyange maarufu "Kaburu" limeisharudi kutoka kwa (DPP) na limerejeshwa TAKUKURU

Hayo yameelezwa na wakili wa Takukuru, Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa, wakati shauri hilo lilipokuja kwa kwa kutajwa.Wakili Swai alidai jalada hilo lilirudishwa juzi kutoka kwa DPP ambaye ametoa maelekezo ya kukamilisha zaidi upelelezi.

Upande wa jamhuri ulieleza hayo baada ya Wakili wa utetezi, Philemon Mutakyawa, kuhoji kuhusu jalada hilo la kesi ambalo lilielezwa kuwa kwa DPP, hivyo alitaka kujua lilipofikia.

Kesi hiyo imahirishwa hadi Novemba 30, mwaka huu,

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtak uhujumu uchumi ikiwa na mashitaka matano na ya utakatishaji wa fedha

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha wa Dola za Marekani (USD) 300,000.

WANAODURUFU KAZI ZA SANAA KUFIKISHWA MAHAKAMANI.



 Kampuni ya Udalali ya Msama Auction Mart imethibitisha kuwa Watuhumiwa wote waliokwamatwa kushiriki kufanya biashara ya kazi feki za sanaa watafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Msama Auction Mart, Alex Msama amesema kuwa Watuhumiwa hao watapelekwa Mahakamani kutokana na kuwa na kesi ya kujibu.

Ameendelea kusema ni kosa kuuza Kazi za Wasanii hao ambazo hazina Stika ya TRA, kwani zinawakosesha Mapato Wasanii hao na Serikali kwa ujumla.

Amesema wataendelea na zoezi hilo kwa kupita maeneo yote kuhakikisha wanadhibiti uuzwaji wa kazi hizo feki.Kwa jana zoezi letu liliendelea maeneo ya Mbande, Mbagala, Buza Tandika na Chanika", amesema Msama.

Amesisitiza kuwa kazi za nje na ndani lazima ziwe na Stika ya TRA, pia amesema ni marufuku kuweka nyimbo za Wasanii, Kuburn CD na kuweka kwenye Flash.
 Kampuni ya Udalali ya Msama Auction Mart inashirikiana na Jeshi la Polisi kwa ajili ya usalama, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuendelea na kuikamisha shughuli hiyo,ambayo pia inatarajiwa kufanyika katika mikoa mbalimbali.
  Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya Msama Auction Mart ya jijini Dar es salaam,Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari katika kituo kikuu cha Kanda Maalum Dar es salaam jana kabla ya kuanza kwa zoezi la kukamata wauzaji wa CD Feki katika maeneo mbalimbali ya ikiwemo eneo hatarishi kwa bishara hiyo la Kariakoo .
Baadhi ya watuhumiwa wakipandishwa kwenye gari na vifaa vyao.
 Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya Msama Auction Mart ya jijini Dar es salaam,Alex Msama akikagua baadhi ya CD kwenye moja ya duka.
Mmoja wa watuhumiwa akichukuliwa na na Askari baada ya kugundulika akiuza katika duka lake.
"Mfano huyu mmiliki wa duka hili, Leseni yake imeisha tangu 2014 mpaka leo na hajui taratibu zozote za kupata leseni mpya wala TIN number,bado anaendelea na biashara yake,kinyume cha sheria",alisema Alex Msama.

KWA MARA YA KWANZA UPASUAJI WA KUZIBUA MISHIPA YA MOYO KUPITIA MSHIPA WA DAMU WA MKONO (CATHETERIZATION) WAFANYIKA KATIKA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI)

16/11/2017 Jumla ya wagonjwa 20 wamefanyiwa upasuaji wa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa upasuaji wa aina hiyo kufanyika hapa nchini.

Akiongea na Waandishi wa Habari leo jijini Dar Salaam Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge alisema upasuaji huo unafanyika katika kambi ya matibabu ya Moyo inayofanywa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na madakatari kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini Saudi Arabia.

Dkt. Kisenge alisema kuwa kambi hiyo inaenda sambamba na utoaji wa elimu na kubadilishana ujuzi wa kazi kati ya wafanyakazi wa Taasisi hizo mbili ikiwemo aina mpya ya upasuaji wanaoufanya kitu ambacho kinawajengea uwezo zaidi. ”

“Faida ya upasuaji huu ni kumwezesha mgonjwa kutoka chumba cha upasuaji akiwa anatembea na baada ya masaa manne kama hali yake inaendelea vizuri anaweza kuruhusiwa.“Tofauti na upasuaji wa kutumia mshipa wa paja ambao tulikuwa tunaufanya, baada ya upasuaji mgonjwa ni lazima akae Hospitali kwa zaidi ya masaa 24 ili kuangalia maendeleo ya afya yake”, alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya IIRO Ali Al Masoud alisema kambi hiyo inaendelea vizuri kwani kwa siku wanatibu wagonjwa 10 na baada ya matibabu afya zao zinaimarika tofauti na ilivyokuwa kabla ya matibabu.Dkt. Masoud aliongeza kuwa wamekuja na utaalam mpya wa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono ambapo kabla ya hapo matibabu yaliyokuwa yanafanyika ni ya kutumia mshipa wa damu wa kwenye paja.

Alifafanua, “Hivi sasa tunafanya upasuaji wa Moyo wa bila kufungua kifua kitu ambacho wenzetu hawa walikuwa wanakifanya. Sisi tumewaongeza utaalam mpya wa kutumia mshipa ya mkononi badala ya mshipa wa paja.

Naye Bader Alanezi ambaye ni Mtaalamu wa magonjwa ya Moyo na mishipa ya damu kutoka IIRO alimalizia kwa kusema kuwa wamepata muda wa kujifunza vitu vingi na kupata uzoefu mpya wa baadhi ya magonjwa na mambo ya kiteknolojia ambayo katika nchi yao hakuna.

Jumla ya wagonjwa 40 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji katika kambi hiyo ya siku tano ambayo imeanza tarehe 14 hadi tarehe 18 mwezi huu.

Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini Saud Arabia wakimfanyia mgonjwa upasuaji wa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab katika kambi ya matibabu ya moyo inayoendelea kwenye Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa 40 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji katika kambi hiyo ya siku tano.


Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge na mwenzake wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini Saud Arabia Ali Al Masoud wakimfanyia mgonjwa upasuaji wa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab katika kambi ya matibabu ya moyo inayoendelea kwenye Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa 40 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji katika kambi hiyo ya siku tano.

Zoezi la kumfanyia mgonjwa upasuaji wa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab likiendelea. Picha na JKCI