Wednesday, October 18

UNIVERSAL AUCTION CENTRE: MNADA MKUBWA WA MALI ZA UBALOZI WA MAREKANI OKTOBA 21, 2017

 Kwa idhini waliyopewa na Ubalozi wa Marekani  watauza kwa mnada wa hadhara  Funicha za nyumbani na ofisini,Vifaa vya tehama, Gari, Generator na Digital Voltage Stablizer  tarehe 21 October, 2017 Jumamosi saa 4:00 asubuhi. Mnada utafanyika Golden Resort Sinza,  Lion Street.

Fenicha nyumbani na ofisini pamoja pamoja na vifaa vya tehama zitaanza kuuzwa kuanzia saa 4:00 asubuhi: Sofa set, Recliner, Wing chairs, Chest drawer, Dressers,  China base, Hutch, Credenza, Entertainment Centre, Coffee table, Meza za chakula /Viti, Meza za ofisi/Viti, Book case, Garden table/ Chairs,  Carpet, Vitanda ,Magodoro, Fridge, Freezer, Washer, Dryer, Majiko ya umeme, A/c split units, Maturubahi, Computer set, Pressure washer,  Air compressor na vingine vingi.

Generator, Gari na AVR vitaanza kuuzwa kuanzia saa 6:00 mchana: 

MASHARTI YA MNADA:
Mnunuzi  wa Fanicha na Voltage Stabilizer atatakiwa kulipa malipo yote kwa keshia (cashier). Na mnunuzi wa Gari na Generator  atatakiwa kulipa 25% pale pale na salio lilipwe ndani ya siku 4 za kazi  mwisho wa kulipa tarehe 26 October 2017, saa 10:00 jioni Ubalozi wa Marekani. ukishindwa kulipa kwa muda huo Gari/ Generator litauzwa  kwa mshindi mwingine aliyefata  na dhamana haitarudishwa.

Mali zote zitauzwa kama zilivyo bila dhamana. Malipo ni pesa taslimu (hundi na miamala haipokelewi). Mnunuzi atawajibika kulipa ushuru na kodi zingine zote.(TRA watakuwepo mnadani). Mali yote iliyouzwa itatakiwa kuondolewa baada ya kulipa malipo yote pamoja na kidi

Kila mtu atatakiwa kuwa na bid namba itakayo patikana getini.

Kwa maelezo zaidi waone:
UNIVERSAL AUCTION CENTRE 
PLOT NO: 5 “E” LION STREET SINZA                       DAR ES SALAAM
CELL NO:  0754 284 926, 0757 284 926               E-mail: universalauction@hotmail.com


MISS TANZANIA JULITHA KABETE ATAMBA KUFANYA VYEMA MISS WORLD 2017

MISS World Tanzania, Julitha Kabete (21) ametamba kufanya vyema katika mashindano ya 67 ya kumsaka mrembo ya Dunia yaliyopangwa kufanyika mjini Sanya, nchini China mwezi ujao.
Julitha ambaye anaondoka leo, amesema kuwa amejiandaa vyema ili kuiletea sifa Tanzania katika mashindano hayo yaliyopangwa kufanyika Novemba 18 kwenye ukumbi wa Sanya City Arena in Sanya, China PR.
 Stephanie na kushirikisha jumla ya warembo 120. Julitha anaondoka leo kwenda China chini ya udhamini wa Turkish Airline. Mrembo huyo aliagwa na kukabidhiwa bendera na  Mwakilishi kutoka wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Habiby Msammy katika hafla iliyofanyika kwenye Hotel ya Hyatt jijini Dar es Salaam.
"Nimejiandaa vizuri katika mashindano haya, nina uzoefu mkubwa kwani nilishinda mashindano ya Miss Dar City Center, Miss Ilala na kwenye fainali za miss Tanzania 2016 ambako niliingia tano bora. Pia nilishiriki mashindano ya Afrika na kufanya vyema,” alisema Julitha.
Mkurugenzi wa Lino International Agency ambao ndiyo waandaaji wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga alisema Julitha ni mrembo wa 23 kuiwakilisha nchi kwenye Miss World.
"Mwaka huu shindano la Miss Tanzania limechelewa kufanyika, hivyo tukaamua kumtea Julitha akatuwakilishe kwenye Miss World, uteuzi wake umezingatia vigezo vyote na hakuna shaka atafanya vizuri katika fainali hizo ambazo tumekuwa na rekodi ya kutwaa taji la Miss World Afrika na mataji mengine," alisema Lundenga.
Mrembo huyo aliondoka nchini jana usiku kuelekea katika kambi ya Miss World nchini China ambapo atachuana na warembo wengine kutoka mataifa zaidi ya 120 kusaka mshindi katika fainali itakayofanyika baadae Novemba nchini humo.
 Mwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya kumsaka mrembo wa Dunia, Miss World 2017, Julitha Kabete (katikati) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye hotel ya Hyatt . Kulia Mkurugenzi wa Lino International Agency ambao ndiyo waandaaji wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga na kushoto ni  Mwakilishi kutoka wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Habiby Msammy katika hafla iliyofanyika kwenye Hotel ya Hyatt jijini Dar es Salaam.
 Mwakilishi kutoka wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Habiby Msammy  (kushoto) akimkabidhi bendera Mwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya kumsaka mrembo wa Dunia, Miss World 2017, Julitha Kabete (katikati)  katika hafla ya kumuaga iliyofanyika jana kwenye hotel ya Hyatt . Kulia Mkurugenzi wa Lino International Agency ambao ndiyo waandaaji wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga.
 Mwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya kumsaka mrembo wa Dunia, Miss World 2017, Julitha Kabete akiwa katika pozi mara baada ya kukabidhiwa bendera kwenye halfa fupi iliyofanyika kwenye hotel ya Hyatt.

MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA SULUHU HASSAN AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA WAZIRI WA IRELAND

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi katika Idara ya Mambo ya Nje na Biashara mwenye Jukumu Maalum kwa ajli ya Diaspora na Maendeleo ya Kimataifa wa Ireland Mhe. Ciaran Cannon aliyeambatana na Balozi wa Ireland nchini Tanzania.

Katika mazungumzo yao walitilia mkazo katika masuala ya Biashara na uwekezaji hasa ikizingatiwa kwamba nchi zote mbili mazingira yake yanaruhusu .

Makamu wa Rais alimuambia Waziri huyo Tanzania ni nchi nzuri na rafiki kwa kuwekeza hivyo wanakaribishwa kuwekeza hasa katika viwanda na teknolojia, Waziri huyo alieleza kuridhishwa kwake  na jitihada za Tanzania katika kusimamia uchumi wake kwa ujumla.

Mheshimiwa Makamu wa Rais alielezea vifo vya wakina mama kabla na wakati wa kujifungua na watoto wachanga na kuiomba Serikali ya Ireland kupitia Waziri huyo kuisaidia Tanzania kukabiliana na tatizo hilo, ambapo waziri huyo alioneshwa kuguswa sana hasa pale Makamu wa Rais alipoelezea uzoefu wake mwenyewe aliowahi kukutana nao wakati anajifungua mtoto wake wa tatu.

Makamu wa Rais na Waziri huyo kutoka Ireland kwa pamoja walikubaliana katika suala zima la kuboresha elimu, mafunzo  na kubadilishana ujuzi hasa katika masuala ya Afya, Teknolojia na Anga.Mwisho Makamu wa Rais alisema Ushirikiano wa nchi mbili hizi ni wakudumu na kuiomba Serikali ya Ireland kuendelea kushirikiana na kusaidia Tanzania.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waziri wa Nchi katika Idara ya Mambo ya Nje na Biashara mwenye Jukumu Maalum kwa ajili ya Diaspora na Maendeleo Kimataifa wa Ireland Mhe. Ciaran Cannon aliyefika ofisini kwa Makamu wa Rais Ikulu jijini Dar es Salaam akiongozana na Balozi wa Ireland nchini Mhe. Paul Sherlock pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Misaada la Irish Ndugu Ruairi De Burca's. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais) 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Waziri wa Nchi katika Idara ya Mambo ya Nje na Biashara mwenye Jukumu Maalum kwa ajili ya Diaspora na Maendeleo Kimataifa wa Ireland Mhe. Ciaran Cannon mara baada ya kumaliza mazungumzo ,Ikulu jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)

Barclays imetenga Sh 157milion kwa ajili ya wanafunzi


Dar es Salaam. Kuongeza ufadhili, Benki ya Barclays Tanzania imetenga Sh157 milioni kwa ajili ya masomo ya wanafunzi 23 wenye mahitaji maalumu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika mwaka wa masomo unaoanza 2017.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo itakayowanufaisha wanafunzi 23 ambaye kila mmoja atapata Sh6.8 milioni, mwenyekiti wa bodi ya benki hiyo, Simon Mponji amesema fedha hizo zinahusisha ada, malazi na matumizi binafsi kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na chuo.
"Asilimia 50 itatoka wakiwa mwaka wa kwanza, asilimia 25 watakapokuwa mwaka wa pili na asilimia 25 inayobaki itatoka mwaka wa tatu. Asilimia 60 ya wanufaika ni wanawake," amesema Mponji.
"Taasisi nyingi zinahitaji watu wenye. Tuliowajengea uwezo tumewatafutia taasisi ambazo wanaweza kufanya kazi kwa kujitolea kwa muda," amesema Mponji.
Akitaja sifa za kupata ufadhili huo, mkurugenzi wa bodi ya wahitimu UDSM, Dk Lulu Kaaya alisema muombaji ni lazima awe anatoka familia duni au yatima ambaye amechaguliwa kujiunga na chuo hicho na akakosa mkopo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).
"Kozi zitakazopewa kipaumbele ni rasilimaliwatu, mawasiliano na uhusiano wa umma na usimamizi wa biashara," amesema Kaaya.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Taknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amezitaka kampuni nyingine kuiiga benki hiyo kuisaidia serikali kuendeleza wanafunzi wenye uhitaji.
"Serikali imeongeza fedha za mikopo ya wanafunzi hadi Sh487 bilioni lakini hazitoshi, uhitaji ni mkubwa," amesema Ndalichako.
Amesema ufadhili huo ni mkubwa na anaamini utazidi kuongezeka kila mwaka huku serikali ikiendelea kuzihamasisha taasisi na nchi rafiki kutoa ufadhili kwa wanafunzi.
"Tunaishukuru serikali ya Hungary kwa kutoa msaada kwa wanafunzi 30 kila mwaka hii inamaanisha kuwa ndani ya miaka 3 wanafunzi wetu 90 watakiwa wamenufaika na ufadhili huo," amesema Ndalichako

JARIDA LA WIZARA YA HABARI UTAMDUNI, SANAA NA MICHEZO

Polisi wakamata magruneti saba na SMG


Dar es Salaam. Watuhumiwa watano wa uhalifu wameuawa na polisi katika matukio mawili, huku jeshi hilo likisema limekamata mabomu saba ya kurusha kwa mkono (gruneti), SMG iliyofutwa namba, magazini yenye risasi 16, maganda 10 ya risasi za SMG na pikipiki.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema silaha hizo zimekamatwa na askari waliokuwa doria saa 4:30 usiku eneo la Msongola wilayani Ilala mkoani Dar es Salaam, Oktoba 16, 2017 wakiwafuatilia watuhumiwa wa mauaji wilayani Kibiti waliokuwa wamepanda pikipiki moja wakiwa watatu.
Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema hayo leo Jumatano Oktoba 18, 2017 alipozungumza na waandishi wa habari.
Amesema watuhumiwa hao watatu ambao hawajatambulika walipokuwa wakifuatiliwa na polisi waliongeza mwendo na kuingia barabara ya vumbi ambako walifyatua risasi.
Kamanda Mambosasa amesema askari waliwadhibiti watuhumiwa hao kwa kuwapiga risasi na kuanguka chini pamoja na pikipiki hiyo.
Amesema watuhumiwa hao wenye umri kati ya miaka 30 na 40 walipofikishwa katika Hospitali ya Temeke, daktari aliyekuwa zamu alithibitisha wamefariki dunia. Miili  imehifadhiwa hospitalini hapo.
Katika tukio lingine, amesema watuhumiwa wawili wa ujambazi wameuawa eneo la Kibonde, Mbagala Zakheim ambako walipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuwa walipanga kuvamia maduka ya Tigo-Pesa na M-Pesa.
Kamanda Mambosasa amesema watuhumiwa wakielekea eneo la tukio, wawili walipigwa risasi wakati wakiwashambulia askari na walipoteza maisha.
Amsema mtuhumiwa mmoja alitoroka na anaendelea kutafutwa na polisi.
Mambosasa amesema watuhumiwa walikutwa wakiwa na bastola ikiwa na magazine yenye risasi moja.
Pia, waliokota maganda matano ya risasi. Amesema bastola hiyo ilipakwa rangi nyeusi ili kuficha utambuzi.

Raila Odinga aitisha maandamano ya nchi nzima siku ya uchaguzi Kenya

Raila Odinga aitisha maandamano siku ya uchaguzi KenyaHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionRaila Odinga aitisha maandamano siku ya uchaguzi Kenya
Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya (Nasa), Raila Odinga, amesema kuwa upinzani utafanya maandamano ya nchi nzima tarehe 26 Okotoba.
Hii ndiyo siku ya kufanyika marudio ya uchaguzi wa urais.
Akihutubia wafuasi wake katika mtaa wa Kamukunji mjini Nairobi leo Jumatano, Bw. Odinga alisema kuwa ataendelea kushikiza Marekebisho katika tume ya uchaguzi ili kuweza kufanyinya uchaguzi ulio wa haki.
"Leo tunabadilisha kauli mbiu yetu kutoka "hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi" hadi "hakuna uchaguzi Oktoba," Bw. Odinga alisema huku akisisitiza kuwa amejiondoa kutoka kwa uchaguzi huo.
Bw. Odinga alitoa tangazo hilo hata baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuonya kuwa hatua kali zinachukuliwa dhidi ya yeyote ambaye atajaribu kuvuruga marudio ya uchaguzi.
Akizungumza eneo la Nanyuki, Rais Kenyatta alilaani visa ambapo maafisa wa IEBC walishambuliwa wakati wakifanya maandalizi kwa uchaguzi huo.
Haya yanajiri baada ya moja wa maafisa wakuu wa Tume ya Uchaguzi Kenya (IEBC) Dkt. Roselyn Akombe kutangaza kujiuzulu katika tume hiyo chini ya wiki moja kabla ya uchaguzi mpya wa urais kufanyika nchini humo.
Alitangaza kwamba anahofia usalama wake na hatarajii kurejea Kenya hivi karibuni.
Dkt Akombe alituma taarifa kutoka mjini New York anakoishi ambapo alikuwa akiufanyia kazi Umoja wa Mataifa kabla ya kujiunga na tume ya IEBC.
Katika taarifa, Dkt Akombe alisema kuwa merejeleo ya uchaguzi utakaofanyika hayaafikii matarajio ya uchaguzi ulio huru na wa haki.
Naye mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchi Kenya Wafula Chebukati amewashutumu wanasiasa nchini humo akisema wanatatiza maandalizi ya uchaguzi wa marudio Alhamisi wiki ijayo.
Bw Chebukati amesema maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vyema lakini katika mazingira ya sasa ni vigumu kuandaa uchaguzi huru na wa haki iwapo hakutakuwa na mabadiliko.

WAZIRI KAMWELWE AFURAHISHWA NA UTENDAJI WA MAMLAKA YA MAJI MOSHI

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Tenki la Maji la Njari.



Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mama Anna Mghwira wakifungua bomba kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Maji wa Mang’ana.
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe amkimtua ndoo kichwani mama kutoka Kijiji cha Mang’ana, akiashiria kutimiza lengo la Serikali ‘‘kumtua mama ndoo kichwani’’ baada ya uzinduzi wa Mradi wa Mang’ana.
Msafara wa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe ukielekea kwenye Chanzo cha Maji cha Mang’ana katika uzinduzi wa Mradi wa Mang’ana.



Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe ametoa pongezi nyingi kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Moshi (MUWSA) kwa kufanikiwa kutoa huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 100 kwa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Hayo aliyasema alipokuwa akizindua Mradi mkubwa wa Maji wa Manga’na, uliopo Kata ya Uru Kaskazini, utakaohudumia zaidi ya vijiji 11 katika Manispaa ya Moshi na Wilaya ya Moshi Vijijini baada ya kupokea taarifa ya hali ya huduma ya maji katika Mji wa Moshi.

“Nawapongeza MUWSA kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya, kwa kuwa ndio lengo la Serikali, kuwa ifikapo mwaka 2020 maeneo ya vijijini huduma ya majisafi na salama ifikie asilimia 85 na mijini asilimia 95. Nyinyi leo hii mmeshavuka lengo hilo kwa Manispaa ya Moshi, kwa kweli nimefurahishwa sana na jambo hili na mnastahili pongezi nyingi’’, alisema Mhandisi Kamwelwe.

Waziri Kamwelwe aliendelea kusema kuwa kwa kufanikiwa lengo hilo, mamlaka hiyo sasa itaongezewa maeneo mengine zaidi, ili kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa wakazi wengine wa Moshi Vijijini ambao hawajafikiwa na huduma ya maji, na kuahidi kama Waziri mwenye dhamana ya maji atawatafutia fedha kwa ajili ya kufanikisha lengo hilo.

Katika hatua nyingine Mhandisi Kamwelwe ameagiza halmashauri zote nchini, kuwa usifanyike ujenzi wowote wa miradi kabla ya kupata chanzo cha maji cha uhakika, ili kuondokana na matumizi mabaya ya fedha za miradi ya maji nchini.

Waziri Kamwelwe alisema ni ufisadi kutengeneza miundombinu ya maji, bila kuwa na chanzo cha uhakika cha maji. Sitakubali miradi ikamilike halafu isitoe maji, wakati umefanyika uwekezaji mkubwa wa fedha za Serikali. Hivyo, ni marufuku mradi wowote kukamilika bila kutoa maji.

Naye Mkurugenzi wa MUWSA, Joyce Msiru alisema katika taarifa yake kuwa mradi huo ni moja ya miradi mikubwa iliyotekelezwa na mamlaka yake, ukiwa umegharimu zaidi ya Sh. bilioni 2 na utahudumia zaidi ya wananchi 34,000.

Mkurugenzi Msiru alitaja baadhi ya vijiji vitakavyohudumiwa na mradi huo kuwa ni Kariwa, Longuo, Njari, Rau, Okaseni na Msuni.

MAHAKAMA YATOA AMRI NG’OMBE WALIOTAIFISHWA KUPIGWA MNADA NA MWANDISHI MAALUM - MWANGA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina katikati, kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Mhe. Aaron Mbogho, kushoto kwake  katibu tawala wa wilaya ya Mwanga Bw. Yusuph  Kasuka wakiangalia ng'ombe waliotaifishwa  wakati wakinywa maji katika kijiji cha Mgagau wilayani Mwanga.
Waziri Mpina , Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Dkt. Maria Mashingo na Mkuu wa Wilaya ya Mwanga Bw. Aaron Mbogho wakijadili jambo baada ya kuongea na wanahabari kuhusu amri ya mahakama ya kupiga mnada ngombe walitaifishwa na Serikali.
Ng’ombe walioamriwa na mahakama kupigwa mnada, mnada utapigwa siku ya ijumaa. 

NG’OMBE waliotaifishwa na serikali katika wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, wamatarjiwa kupigwa mnada kufuatia uamuzi wa mahakama.
 Hayo yameelezwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, wakati alipokwenda kukagua lindo la ng’ombe hao, jana eneo la Mgagao, wilayani Mwanga, walikohifadhiwa.

“Kufuatia uamuzi wa mahakama, ng’ombe hawa watauzwa kwa njia ya mnada siku ya Ijumaa, Oktoba 20, mwaka huu, kutokana na hali za ng’ombe hawa kutokuwa nzuri”, alisema.

Aliongeza, “Tayari mahakama imeridhia ombi la serikali la kutoka kuuzwa kwa ng’mbe hawa na ishamteua dalali wa kufanya mnada huo ambaye ni Marepelanto ya mjini Moshi na kazi hii itafanywa haraka kutokana na ng’ombe wengine kuanza kufa, kama mlivyosikia tayari sita wameshakufa”.

Aidha alisema serikali itaanza operesheni maalum ya kuwakamata ng’ombe walioingizwa nchini kinyume cha sehria kuanzia Jumatatu ijayo.

“Baada ya operesheni ya hapa Kilimanjaro, nilitoa siku saba kwa Mikoa mingine kuiondoa mifugo iliyoingizwa nchini kinyume cha sheria kupitia Mikoa hiyo, muda huo umekwisha, Jumatatu tunaanza ingine itakayochukua siku 15 ili kuhakikisha mifugo hiyo inaondolewa yote”, alisema.

Akijibu maswali kutoka kwa baadhi ya viongozi wa eneo hilo, Bw. Mpina alisema kuwa iwapo kuna mifugo ya wenyeji ilikamatwa wakati wa operesheni hiyo wapeleke orodha ya wenye ng’ombe hao kwa kupitia ngazi husika ili waweze kurudishiwa.

“Wenyeji wenye ng’ombe waliokamatwa watumie taratibu kuzifuatilia kwa kuanzia kwa viongozi wa maeneo wanayotoka hadi ngazi ya kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ikidhibitishwa bila mashaka mifugo hiyo ni ya kwao zitatumika taratibu zinazohitajika kisheria kwa kuwa ng’ombe hizi sasa ni mali ya serikali”, alisema.

Aidha alitoa onyo kwa viongozi hao kuhakikisha wanafanya zoezi hilo kwa weledi na kwamba iwapo watafanya udanganyifu hatua kali za kisheria zitachuliwa dhidi yao bila kujali nyadhifa zao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Maria Mashingo, aliyeiongoza operesheni hiyo, alisema kuwa mwendelezo wa operesheni hiyo umepelekea serikali kukamata ng’ome wengine takribani 2,000.

“Tunawashukuru Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kutupatia ndege ambayo ilitusaidia sana katika zoezi hili tulilofanya kupitia vyombo vya ardhini na angani”, alisema.

Alisema kuwa amebaini ya kuwa wizara ya Mifugo na Uvuvi ina changamoto ya uhitaji wa vifaa kama ndege kwani operesheni hiyo imebainisha wazi uhitaji huo.

Awali akitoa rai yake kwa niaba ya wafugaji wenyeji ambao ng’ombe zao zimekamatwa kufuatia operesheni hiyo, Diwani wa Kata ya Kirya, Bw. Nyange Laizer aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa ng’ombe hizo kurudishiwa wenyewe.

“Unajua sisi malisho yetu tunafanya hapa hapa na ndiyo maana operesheni hii ikawakumba na watu wetu na hii ni kutokana na ukweli kuwa huwezi kutofautisha ng’ombe za hapa kwetu na zile zinazoingizwa kinyume cha sheria”, alisema.

Uamuzi huu wa mahakama unakuja baada ya ng’ombe hao kutaifishwa na serikali hivi karibuni baada ya kuingizwa hapa nchini kinyume cha sheria.

SERIKALI YALIPA MADENI YA NDANI BILIONI 190 KATIKA KIPINDI KIFUPI

Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akisalimiana na badhi ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera alipowasili katika Ofisi hiyo ili kuzungumza na watumishi wa Mamlaka hiyo.
Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera kuhusu masuala ya kiutendaji alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Mamlaka hiyo Mkoani humo.
Meneja Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoani Kagera, Bw. Adam Ntoga, akiwasilisha taarifa ya utendaji ya Mamlaka hiyo kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Mamlaka hiyo Mkoani Kagera.


Baadhi ya Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (hayupo pichani) alipokuwa akizungumzia kuhusu uadilifu katika kazi na utoaji wa elimu kwa mlipakodi baada ya Naibu Waziri huyo kufanya ziara ya kikazi katika Ofisi hiyo.


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati) akizungumza na viongozi pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoani Kagera, alipofanya ziara ya kikazi katika Mkoa huo ambapo amewaasa kuwa waadilifu katika kazi zao.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati -walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kagera na baadhi ya Maafisa Waandamizi katika Mkoa huo.
Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Kagera Bw. Seif Mkude (kulia) akielezea kuhusu utayari wa wafanyabiashara wa Mkoa huo kulipa kodi wakati wa Mkutano kati ya wafanyabiashara wa Mkoa huo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati).


Mfanyabiashara wa Mkoa wa Kagera Bw. Taimur Manyilizo, akieleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo wafanyabiashara Mkoani humo ikiwemo kile alichoeleza uwepo wa taasisi nyingi zinazodai kodi nyingi ikiwemo OSHA, TFDA, Zimamoto ambapo aliiomba Serikali iziangalie na kuzifanyia kazi.


Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kushoto) akizungumza kuhusu ushirikiano kati ya Serikali na Wafanyabiashara wa Mkoa wa Kagera katika kukuza Uchumi wa nchi baada ya Naibu Waziri huyo kufanyaziara ya kikazi Mkoani humo.


Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – WFM


Benny Mwaipaja, KAGERA

Serikali imelipa madeni ya wazabuni, wakandarasi na malimbikizo ya wafanyakazi yanayofikia kiasi cha shilingi bilioni 190 katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu baada ya kufanya uhakiki wa madeni halali inayodaiwa na wafanyakazi na watoa huduma mbalimbali.

Hayo yamesemwa Mjini Bukoba mkoani Kagera na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dokta Ashatu Kijaji (Mb), wakati akizungumza na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa mkoa huo akiwa katika ziara ya kikazi kukagua utendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).


Dokta Kijaji alisema kuwa wazabuni wamelipwa kiasi cha shilingi bilioni 67.2, wakandarasi wamelipwa shilingi bililioni 24.2, watoa huduma mbalimbali wamelipwa Shilingi bilioni 38, watumishi wa umma wamelipwa Shilingi bilioni 37, huku wadai wengine wakilipwa shilingi bilioni 24.


Alisema kuwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imetenga zaidi ya Shilingi trilioni 1 kwa ajili ya kulipa madeni mbalimbali na kwamba itaendelea kulipa madeni yote yaliyohakikiwa.

Dkt. Kijaji aliiambia Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Kagera kwamba Serikali inatambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa kutokana na kulipa kodi zinazochangia kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali za jamii.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara kutumia mashine za kielektroniki katika biashara zao, kutoa stakabadhi wanapouza bidhaa na huduma huku wananchi wakiaswa kudai stakabadhi wanapofanya manunuzi ya aina yoyote na kuhakikisha kuwa stakabadhi hizo zinaonesha kiasi halisi walicholipia huduma na bidhaa walizonunua.

Akizungumza kwaniaba ya Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Kagera, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Bw. Seif Mkude, alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna inavyohamasisha na kushikia bango masuala ya kodi kwa manufaa ya Taifa.

Alisema kuwa wafanyabiashara wameridhika na namna kodi wanazolipa zinavyosimamiwa kikamilifu na kutekeleza miradi dhahiri ya maendeleo na kuahidi kuwa wataendelea kulipa kodi hizo ili kujenga uchumi wa nchi.

Alitoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kuendelea kulipa kodi kwa hiari ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli huku akiishauri Serikali kuondoa kero ndogondogo zilizotolewa na wafanyabiashara wakati wa mkutano huo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Kagera, Mkuu wa wilaya ya Bukoba Bw. Deodatus Kinawiro, aliwashauri wafanyabiashara hao kupanua wigo wa biashara zao ili waweze kunufaika na uwepo wa soko huru katika nchi zaidi ya nne zinazopakana na mkoa huo ikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, DRC Kongo, Kenya na nchi nyingine.

SIDO WATOE MAFUNZO KWA WANAFUNZI WA VYUO ILI WAJIAJIRI: RC NCHIMBI.


 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akitoa hundi ya Mkopo uliotolewa na SIDO kwa mjasiriamali Sarah Isaya kutoka Singida katika hafla fupi ya kukabidhi mikopo kwa wajasiriamali mbalimbali mkoani hapa.
  Mkurugenzi Mtendaji SIDO Taifa Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji akitoa nasaha zake kwenye hafla ya utoaji wa hundi za mikopo kwa wajasiriamali mbalimbali mkoani Singida uliofanyika kwenye viwanja vya SIDO mjini hapa. Wa kwanza kushoto (aliyekaa) ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi.
  Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akitazama ubora wa mafuta ya alizeti  na kupata maelezo ya mafuta hayo yanayosindikwa katika viwanda vya Mkoa wa Singida kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya kuzalishaji  Mafuta ya alizeti  ya  Sunshiwe Oil Mill, Salum Khalifan.
 Meneja wa SIDO Mkoa wa Singida Shoma Kibende akitoa taarifa ya Viwanda Vidogo vidogo na ujasiriamali Mkoa wa Singida kwenye hafla ya utoaji wa hundi za mikopo kwa wajasiriamali mbalimbali. Wa kwanza kushoto (waliokaa) ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi na Mkurugenzi Mtendaji SIDO Taifa Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amelitaka shirika la Viwanda Vidogo vidogo (SIDO) kuandaa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa vyuo mbali mbali mkoani hapa ili wakihitimu waweze kujiajiri

Dkt. Nchimbi ametoa wito huo wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mikopo ya SIDO kwa wajasiriamali iliyofanyika kwenye viwanja vya SIDO ambapo amesema mafunzo hayo yatawajengea mazingira mazuri wahitimu kujiajiri.

Amesema Mkoa wa Singida una fursa nyingi za kujiajiri pamoja na kuwa na vijana wengi hasa walipo katika vyuo mbalimbali lakini hawawekezi katika fursa hizo kwa kutokujua au kukosa elimu ya kutosha juu ya ujasiriamali, na hata waliopo vyuoni wakihitimu wanasubiri kuajiriwa badala ya kujiajiri.

Dkt. Nchimbi amesema ili wananchi wakiwemo vijana waweze kuzitambua fursa hizo, SIDO Mkoa na wadau wengine wanapaswa kuongeza juhudi zaidi katika utoaji mafunzo ya ujasiriamali ambapo amewataka wajielekeze kwenye vyuo mbalimbali.

“Singida ina kila aina ya fursa ambazo zinaweza kumkomboa mwananchi kiuchumi. Kwa hiyo hakuna sababu vijana au watu wengine kuukimbia mkoa wao na kwenda kutafuta maisha katika mikoa mingine. Ni suala la kujipanga na kupata fursa ya mafunzo kutoka SIDO mkoa”, amefafanua.

Aidha ameziagiza halmashauri zote na manispaa Mkoani hapa kutangaza fursa, bidhaa, mazao, na huduma zinazopatikana katika maeneo yao ili kuwasaidia wajasiriamali kupata soko la uhakika.

“ Halmashauri zote tumieni fedha mnazopata kwenye vyanzo vya mapato ya ndani muwasaidie wajasiriamali wenu kutangaza kwenye vyombo vya habari, nina imani na uhakika kuwa mkitangaza bidhaa na mazao yao yatapata soko na nyinyi halmashauri mtapata mapato yenu”, amesema Dk.Nchimbi.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa SIDO Taifa Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji amesema SIDO imekuwa tegemeo kubwa kwa wajasiriamali hasa katika kutoa mafunzo na kusaidia teknolojia ya kuongeza thamani ya mazao na malighafi.

“Mikopo ya SIDO imeweza kuwasaidia wajasiriamali kuthubutu na kuanzisha miradi ya usindikaji mara tu baada ya kupata mafunzo. Kundi hili limekuwa na changamoto ya mitaji kwa kuwa halikidhi na halijaweza kuthubutu kuzifikia benki kutokana na woga na gharama za mikopo”, amesema.

Mhandisi Profesa Mpanduji amesema kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 SIDO imeweza kutoa mikopo 4,464 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 7.2. Mikopo hiyo imetengeneza ajira 11,861 kati ya ajira hizo asilimia 51 ni wanawake.

Kwa upande wake Meneja wa SIDO Mkoa wa Singida Shoma Kibende amesema kwa Mkoa wa Singida wametoa mikopo yenye jumla ya shilingi milioni 724.6 kwa wajasiriamali 693 na vikundi 47. Hali ya urejeshaji wa mikopo hiyo ni asilimia 98.

Kibende amesema SIDO wameweza kutoa mafunzo ya wajasiriamali mbalimbali 37 kwa wajasiriamali 996 ambao kati yao wanawake walikuwa 536 na wanaume 460.

Amesema baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu wa wafanyakazi na ukosefu wa fedha kwa ajili ya kutekeleza mipango waliyojiwekea ikiwemo kuendeleza na kuboresha mtaa wa viwanda.

Naye Mjasiriamali kutoka Kampuni ya Singida Super Quality Oil and Rice mills Simon Kitundu amezishauri halmashauri na manispaa kutenga maeneo maalum ya kufanyia biashara wajasiriamali waweze kuondokana na adha mbalimbali ikiwemo ya kuuza bidhaa zao kwenye madirisha ya mabasi.