Wednesday, September 13

Bunge la Ndugai ‘limeuza’ mamlaka yake Ikulu


Hivi karibuni niliandika makala nikijadili utendaji wa Spika wa Bunge, Job Ndugai. Nilisema katika makala hayo na naendelea kusisitiza kuwa Spika huyu ama ameshindwa kuyatambua mamlaka ya Bunge analoliongoza au anaogopa kuyatumia na kuishia kuiachia Serikali anayotakiwa kuisimamia.
Madaraka ya Bunge yanaelezwa katika ibara ya 63(2), ikisema:  “Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri  ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa
majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.”

Leo nitaangazia madaraka hayo ya Bunge katika uundwaji wa kamati teule. Kanuni za Bunge ibara ya 120 fasili ya 1 na 2 zinasema, “Kamati Teule inaweza kuundwa na Bunge kwa madhumuni maalumu kwa hoja mahsusi itakayotolewa na kuafikiwa. Baada ya kujadili hoja yoyote, Bunge linaweza kuunda Kamati Teule
kwa madhumuni ya kushughulikia jambo lolote lililotokana na hoja.”
Julai 5, Spika Ndugai aliunda kamati maalum ya Bunge kwa ajili ya kutathimini uchimbaji, usimamizi, umiliki na umiliki na udhibiti wa madini ya almasi nchini, kisha kuandaa mapendekezo mahsusi kwa ajili ya kuishauri Serikali juu ya uendeshaji wa biashara ya madini hayo.

Hadidu za rejea kwa kamati hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu zilikuwa pamoja na kuchunguza hadidu za rejea za kamati zilizoundwa awali zilizochunguza uchimbaji na udhibiti na kuona kama zinaweza kuhuishwa kwa matumizi ya sasa.

Nyingine ni kuchunguza mfumo wa usimamizi wa biashara ya almasi nchini na kuanisha manufaa na hasara ambayo Serikali kutegemea na uwekezaji uliopo.

Ya tatu ni kupendekeza mfumo bora unaoweza kutumika katika kusimamia uchimbaji na uwekezaji na kushughulikia jambo lolote linalohusiana na biashara ya almasi.
Kamati hiyo iliyopewa siku 30 kutekeleza majukumu yake iliwasilisha matokeo yake Septemba 7 bungeni Dodoma.
Tatizo sasa linapokuja na ndiyo hoja yangu kwa leo ni kitendo cha Spika mara tu baada ya kuipopokea, kumkabidhi makabrasha ya ripoti ya kamati hiyo pamoja na kamati ya kuchunguza madini ya Tanzanite Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye naye alizipeleka Ikulu kwa Rais John Magufuli.
Kanuni za Kudumu za Bunge ibara ya 122 na fasili za 2 na 3 zinasema, “Taarifa ya Kamati Teule itawasilishwa Bungeni na Mwenyekiti. Iwapo baada ya hoja kutolewa, Bunge litaamua kujadili taarifa hiyo, hoja itakayotolewa Bungeni itakuwa ni kwa madhumuni ya kuliomba Bunge likubali mapendekezo yaliyomo katika taarifa hiyo.”

Katika mchakato mzima hatukuona Spika akiwauliza wabunge kama kuna haja ya kujadili ripoti zile. Badala yake sherehe zilifanyika nje ya ukumbi wa Bunge aqmbapo ripoti zilikabidhiwa kutoka kwenye kamati husika kwenda kwa Spika ambaye naye alizikabidhi kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Sina uhakika, kama Spika Ndugai mwenyewe alipata muda wa kuzisoma ripoti zenyewe au alikwenda kusikia zikisomwa mbele ya Rais Ikulu ya Dar es Salaam.

Najiuliza tu, Spika Ndugai alikuwa na haraka gani ya kupeleka ripoti hizo Ikulu? Je, alilazimishwa? Alitishwa?

Mbona uzoefu unaonyesha ripoti ya kamati teule za Bunge kusoma ripoti zake bungeni na zikajadiliwa na mapendekezo yalitolewa? Mfano mzuri ni kamati teul;e ya Bunge iliyochunguza mradi wa umeme tata wa Richmond mwaka 2007.
Kamati hiyo iliyoundwa na Spika Samuel Sitta iliongozwa na Waziri wa Habari wa sasa Dk Harrison Mwakyembe, ilileta taarifa yake bungeni, ikadiliwa na hatimaye aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa alijiuzulu.
Uzoefu pia umeonyesha ripoti za Serikali zimekuwa zikiletwa Bungeni na kujadiliwa kisha Bunge linaielekeza Serikali cha kufanya.

Tuliona kwa mfano, ripoti ya Operesheni tokomeza iliyotokana na tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete na kujadiliwa bungeni.
Tunaona pia ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) zikijadiliwa bungeni, licha ya kukabidhiwa kwa Rais.

Kinachofanyika sasa kwenye Bunge la Spika Ndugai ni kinyume, kamati anaiunda yeye mwenyewe, lakini matokeo yake yanakwenda kusomwa Ikulu.

Hata mpishi huonja kwanza chakula kabla hakijaenda mezani kwa walaji, kwa hiyo Ndugai naye kama mpishi wa ripoti hiyo alipaswa kuisoma na kuwaruhusu wabunge wachangie kabla ya kuipeleka Serikalini.

Tulitarajia kuona madudu yaliyomo kwenye ripoti hizo yakijadiliwa bungeni na wabunge watoe mapendekezo. Kwa mfano, katika ripoti hiyo kamati ilieleza kubaini, miaka ya nyuma kuna kiongozi mkubwa alipewa zawadi ya Almasi yenye thamani ya Dola za Marekani (USD) milioni 200 sawa na Sh400 bilioni za Tanzania.

Kiongozi huyo ni nani? Je, ni Rais mstaafu? Au ni mungu mtu? Haya yote yangebainika bungeni, lakini ni aibu kuona unge likizibwa mdomo na Spika anaridhia, madudu ya kamati hizo yanafunikwa kwa visingizio lukuki.

Pengine Rais Magufuli alikuwa na malengo yake ya kutaka ripoti hizo zikasomwe Ikulu moja kwa moja, lakini Spika Ndugai naye alipaswa kusimamia madaraka yake ya Bunge.

Lengo siyo ushindani bali ni kutekeleza madaraka yake kama mhimili mmojawapo wa Serikali. Kila mhimili una madaraka yake na haipaswi kuingiliana.

Ni kwa msingi huo tunaona jinsi Bunge linavyomong’onyolewa katika awamu hii ya tano. Walianza kukataza Bunge lisionyeshwe moja kwa moja katika televisheni, tumeona hata wabunge wakikatazwa kuwajadili marais wastaafu na sasa ripoti za Bunge zinakwenda kusomewa Ikulu.
Bunge kwa sasa limebakiza nini tena? Spika Ndugai na viongozi wenzake wamebakiza nini? Iko wapi dhana ya Bunge kuisimamia Serikali?

Dar yatoa msamaha wa ushuru wa mabango


Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam umetoa msamaha wa ushuru wa mabango ya matangazo ya vivutio vya utalii ikiwa ni sehemu ya mchango wa mkoa katika kukuza utalii.
Ofisa Misitu Mkoa wa Dar es Salaam, Mariam Kitula amesema hayo leo Jumatano katika warsha ya wadau wa utalii wa kanda ya pwani.
Warsha hiyo inalenga kukusanya maoni kuhusu marekebisho ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999.
Kitula amesema uamuzi huo ulifikiwa baada ya ofisi ya mkuu wa mkoa kufanya majadiliano na Bodi ya Utalii na kukubaliana kuruhusu mabango hayo bila kutozwa ushuru.
"Mkuu wa mkoa alitaka mabango ya utalii yawepo katika jiji lote, bodi wakasema hawawezi kutokana na gharama, tulirudi tukajadili tukaona ipo haja ya kufuta ushuru huo ili mtalii anapowasili uwanja wa ndege akute mabango yanayoonyesha vivutio vyetu," amesema.

Magufuli awasubiri wabunge watatu CCM


Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli anawasubiri wabunge watatu kujibu maswali kwa nini majina yao yamekuwa yakitajwa mara kwa mara katika ripoti zinazohusu ufisadi katika nyadhifa walizowahi kusimamia serikalini.
Hatua hiyo inawaweka wabunge hao kwenye wakati mgumu na kuna uwezekano wa kutopitishwa tena kwenye vikao vya juu ndani ya chama hicho katika mchakato wa uchaguzi mkuu 2020, licha ya kukubalika majimboni.
Wabunge hao ni Andrew Chenge (Bariadi), William Ngeleja (Sengerema) na Profesa Sospeter Muhongo (Musoma Vijijini).
Wabunge hao walitajwa katika sakata la Tegeta Escrow kwa tuhuma tofauti huku Chenge akionekana tena katika sakata la ununuzi wa rada alikolazimika kujiuzulu uwaziri wa Miundombinu katika serikali ya awamu ya nne iliyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Kwa upande wao, Ngeleja na Profesa Muhongo wametajwa pia katika sakata la makinikia ya madini kupitia nafasi zao kama mawaziri wa zamani wa Nishati na Madini. Hatua hiyo iko mbioni kuchukuliwa kama utekelezaji wa ahadi ya mwenyekiti huyo wa CCM.
Akizungumza wakati wa kukabidhi ripoti ya Tanzanite na almasi, Spika wa Bunge, Job Ndugai alionyesha kusikitishwa na wanasiasa hasa wabunge ambao wamekuwa wakitajwa katika ripoti nyingi za ufisadi, lakini bado wanarejea bungeni kwa kuchaguliwa.
Alisema pamoja na wabunge hao kutajwa kwenye matukio ya namna hiyo wakirudi majimboni wanachaguliwa na wananchi kwa kuwa wao hawajui tabia zao.
“Vyama vya siasa vinawapitisha, wanashinda ubunge na wakija mimi nitawaapisha na juzi Profesa Lipumba (Ibrahim) kaniletea wapya nimewaapisha,” alieleza Ndugai.
Baada ya kauli hiyo, Rais Magufuli alisema ni kweli kuna watu wametajwa kwenye ripoti nyingi na wakiwa bungeni wamekuwa wakichangia hoja kwa nguvu zote. Rais Magufuli alimuuliza Ndugai kama bungeni hawana utaratibu wa kuwashughulikia watu wa namna hiyo au hata kubadili kanuni ili waweze kushughulikiwa.
Hata hivyo, alisema kwa kuwa yeye ni mwenyekiti wa CCM anasubiri barua ya Spika na ikiwafikia watawashughulikia kwa mujibu wa miiko ya chama huku akiamini na vyama vingine navyo vitafanya hivyo.
Hoja ya kuwabana wanasiasa wenye tuhuma za ufisadi ziliibuka baada ya wanasiasa wengi hasa wabunge kutajwa kwenye ripoti mbalimbali zilizochunguza tuhuma za ufisadi. Wabunge wa CCM waliotajwa katika ripoti hizo na ambao hawana nafasi serikalini kwa sasa ni Ngeleja, Profesa Muhongo na Chenge. Wakati wa kashfa ya Escrow, Ngeleja, Chenge na Victor Mwambalaswa (Lupa-CCM) walilazimika kujiuzulu uenyekiti wa kamati mbalimbali za Bunge baada ya kutuhumiwa kupokea mgawo wa fedha za Escrow.
Ngeleja alidaiwa kupokea Sh40.4 milioni, Chenge Sh1.6 bilioni na Mwambalaswa alidaiwa kuwa na mgongano wa kimaslahi. Mbunge mwingine ni Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini) aliyedaiwa pia kupokea Sh1.6 bilioni katika mgawo wa Escrow na kulazimika kujiuzulu uwaziri wa Nyumba na Maendeleo na Makazi.
Kuhusu Chenge
Chenge alitajwa katika kashfa ya ununuzi wa rada ambayo ilimlazimu kuachia uwaziri. Rada hiyo ilinunuliwa kutoka kampuni ya BAE System ya Uingereza kwa Dola40 milioni mwaka 2001, kiwango kilicholishtua hadi Bunge la Uingereza.
Katika uchunguzi wa suala hilo kupitia Serious Fraud Office (SFO), ilibainika kuwa Chenge aliyekuwa mwanasheria mkuu wakati biashara hiyo ikifanyika alikuwa na akaunti kwenye kisiwa cha Jersey iliyokuwa na zaidi ya Dola1 milioni (sawa na zaidi ya Sh1.8 bilioni kwa kiwango cha sasa).
Katikati ya kashfa ya sakata hilo, Chenge aliyekuwa ziarani China akiwa na Rais Kikwete aliporejea aliwaambia waandishi waliomzonga kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuwa fedha hizo ni “vijisenti”. Hata hivyo, baadaye aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kujitetea kuwa ni mwadilifu, mtu safi na hakutenda kosa katika kashfa hiyo.
Pili, Chenge alitajwa kwenye sakata la Escrow akidaiwa kupokea Sh1.6 bilioni kutoka kwa wamiliki wa IPTL.
Akizungumzia kashfa hiyo, mbunge huyo aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti alisema kwa kilugha kuwa yeye ni ‘nyoka wa makengeza’.
Mbali ya kuwa waziri wa Miundombinu kati ya 2006-2008, pia aliongoza Wizara yaa Ushirikiano wa Afrika Mashariki mwaka 2006.
Pia Chenge aliwahi kupewa jukumu la kuongoza Kamati ya Maandishi ya Bunge Maalumu la Katiba iliyoandaa Katiba Inayopendekezwa.
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alijaribu kumtaja waziwazi kuwa anahusika katika mikataba yenye matatizo, lakini mwanasheria huyo wa zamani alimzima kwa kuomba mwongozo na kumtaka Spika amlazimishe awasilishe ushahidi wa anachokisema, la sivyo aache kuchafua watu.

Serikali kuendelea kubana matumizi


Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuimarisha mifumo ya udhibiti katika taasisi zake.
Akizindua programu ya marekebisho ya usimamizi wa fedha za umma (PFMRP) jana Jumanne mjini hapa, Samia amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha inaboresha mfumo huo.
Samia amewahakikishia wadau wa maendeleo kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika kama zilivyokusudiwa.
Awali, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali katika awamu zilizotangulia zilionyesha mafanikio katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuongeza makusanyo ya kodi kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFDs).
“Programu hii ilisaidia kuboresha sheria, nidhamu katika matumizi ya fedha za umma, mipango na michakato ya bajeti na kuanzisha ofisi ya mkaguzi mkuu wa ndani,” amesema.
Amesema programu hiyo itatekelezwa kwa miaka mitano na itaanza kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha (2017/18) hadi
mwaka 2021/22.
Dk Mpango amesema programu hiyo itahusisha kuweka mifumo thabiti katika kukusanya, kutumia na kugawanya rasilimali ili kusimamia vyema fedha za umma.
Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID) nchini, Berth Arthy amesema usimamizi mzuri wa fedha za umma ndiyo utawezesha maendeleo kwa wananchi.
“Uingereza imekuwa ikishirikiana na Serikali ya Tanzania siku nyingi, usimamizi mzuri wa fedha za umma ni njia kuu ya kuleta
maendeleo kwa watu tunaowaongoza,” amesema.

Kelele zafikia kilele Zanzibar


Kwa jumla misemo ya Kiswahili imejaa hekima na busara. Misemo hii hutoa mafunzo hata kwa yule ambaye si kiziwi bali aliyeamua kuziba masikio au mtu ambaye si kipofu aliyeamua kuzuia macho yake yasione kwa kujifunga kitambaa cheusi usoni.
Hata hivyo ipo misemo ambayo ukiipa tafsiri ya neno kwa neno unajikuta unakwenda mchomo na kutoupata ujumbe uliokusudiwa.
Miongoni mwao ni ule msemo usemao kelele za mpangaji hazimzuii mwenye nyumba kulala.
Ukiuangalia msemo huu juujuu utaona haingii akilini hata dogo kwa kelele katika chumba cha pili cha nyumba moja kisababishe usumbufu wa kumzuia mtu, awe mwenye nyumba au wapangaji wenzake kupata usingizi wa raha mustarehe.

Hata hivyo, si lengo langu hata kidogo kuzungumzia huo mkasa wa kelele za ndani ya nyumba za mpangaji ambazo tunaambiwa hazimzuii mwenye nyumba kulala, ninachokusudia kukieleza ni kukua kwa utamaduni mpya wa
kelele… kelele kelele kila pembe ya Zanzibar na wakati fulani hata ndani ya nyumba za ibada.

Kwa miaka mingi Zanzibar ilisifika kama visiwa shwari na watu wake kuwa wapole, makarimu na rahimu vyenye kiwango cha chini cha uhalifu.
Vitendo vya uhalifu vilivyofanyika Zanzibar hapo zamani ni kama vya kijana kuiba nguo zilizoanikwa kwenye kamba au watoto kulivuta kwa ndoana doriani lililopo kwenye meza ya duka.

Siku hizi hali ni tafauti kabisa. Unaposikiliza au kuangalia taarifa za habari katika radio  na runinga za Visiwani au kusoma gazeti la serikali la Zanzibar Leo unaona habari nyingi za vitendo vya uhalifu, mauaji, ubakaji, matumizi ya dawa za kulevya na kadhalika vimetawala.
Lakini kama lipo jambo ambalo linakera na kusikitisha, lakini
linaonekana kufumbiwa macho na kutiliwa pamba masikioni ni kelele.

Karibu kila kila pembe ya Zanzibar utasikia kelele, kama vile watu wa
visiwa vya Unguja na Pemba hawaoni na ni viziwi au labda ndio
wameipokea kwa tafsiri potofu ule msemo wa “ Kelele za mpangaji
hazimzuii mwenye nyumba kulala.”.


 Kwa mfano, katika soko kuu la mji wa Zanzibar kelele zimetia fora.
Hapa unakuta   wafanya biashara wanaouza kanda za muziki, miutano ya
vyama vya siasa na mawaidha ya dini , wanaouza sumu ya panya na kwenye
maduka ya simu wakitangaza bidhaa wanazouza  kwa kutumia vipaza sauti.
Ni kelele…kelele..kelele kla sehemu.

Gari za dala dala zimegeuzwa kumbi za muziki. Abiria hawawezi
kusikilizna na ukipigiwa simu bora usipokee kwa sababu hutaweza
kuwasiliana na aluyekupigia.
Vile vile matumizi ya ving’ora vya magari kwa misafara, hata ya magari
ya vikundi vya watalii yamekuwa mambo ya kawaida.

Lakini pia wapo abiria ambao  wamekuwa wakiongeza kasi za kelele kwa
kufungua mzuziki za simu zao za mkononi  kwa kelele kama vile
wamekodiwa kustarehesha abiriawaliopo safarini . Ni kawaida katika
dalala ukasikia  kwa wakati mmoja hata nyimbo nne, ya taarab, Bongo
Fleva, Kiarabu na Kihindi kwa  kwa wakai  mmoja.

Mtu hatakosea akielezea safari kama hiyo ni ya watu ambao labda akili
zao zina matatizo.

Kinachosikitisha zaidi ni kuona hakuna sheria , kama zipo zimefumbiwa
macho na kuhifadhiwa ndani ya kabati,  za kuidhibiti hali hii  mbaya
na  hakuna mtu anayekemea kama vile mambo haya ya kelele nyingi wakati
wote yanakubalika katika jamii ya kistaarabu.
.
Hu utamaduni wa kupenda kelele unaonekana hata katika maeneo ambayo
ukimya unahitajika sana, kama vile hospitali, misikitini na
makanisani.

Ni kawaida kuona wanaotembelea wagonjwa hospitali  wanafanya zogo kwa
kuzungumza na simu zao za mkononi  au wamevaa viatu vya visigino au
vile vyenye njumu na kusababisha kelele pale wanapopiga hatua katika
sakafu za wodi.

Hio miito mengine ya ya simu za mkononi kama ya Kuran na mengine ya
paka anayelia au mwana mama anayelilia mapenzi a nyimbo zenye ujumbe
ambao si mzuri kusikika hadhrani nayo inaongeza kelele  na bughdha za
aina yake kwa
wagonjwa na wale wanaokwenda kuwajulia hali jamaa zao.

Jamii ya Wazanzibari inaoonekana kuupokea kwa mikono miwilina tabasamu
 utamaduni huu wa kelele unaozusha fujo na kuathiri masikio na
kuhatarisha maisha ya watu.

Huko mitaani ndio mambo hayaelezeki. Kila mwenye radio au runinga
anaonekana kuwa na haki kufungua kwa sauti anayotaka radio au runinga
yake hata nyakai za usiku bila ya ujali huenda wapo watu waliola au
wagonjwa ambao wanahitaji hali ya utulivu.

Hata pale inapotokea kuwepo miba mtaani watu bado wanaona ni vizuri
kufurahia muziki wao bila ya kujali kwamba mila na tamaduni zinataka
uuone msiba wa jiani ni wako.

Katika baadhi ya vijiji, hasa vile katika fukwe wa pwani ambapo zipo
hoteli za kitalii na nyumba za agei na  starehe, wana vjiji wamekuwa
wakilalamikia kelele kutok katika nymba hizi.

Hata hivyo, katika baadhi ya maeneo kelele za wana vijiji za
kulalamikia kelele zimesikika na uchukuliwa hatua muwafaka, lakini
katika baadhi ya sehemu masikitiko yao hayazingatiwi kama vile
wanampigia gtaa mbuzi ambaye ni kiziwi.

Ni vizuri kwa viongozi wa serikali, jamii, mabaraza na halmashauri za
miji na wilaya kushirikiana na vyombo mbali mbali vya dola
kulitafakai suala hili kamakini na kulipatia ufumbuzi wa haraka
utakaoleta faraja.

Vyenginevyo, huu utamaduni wa kupenda na kuhabikia kelele ambao hivi
sasa umefikia kilele hapo baadaye utakuwa na athari mbaya zaidi kwa
watu wa Visiwani na kujkuta wanajjutia kwa kuvumilia kelele
zinazosikika hivi sasa..

Kama kelele za mpangaji hazimzuwii mwenye nyumba kulala ieleweke
kwamba kelele za vipaza sauti zinawakosesha watu usingizi na kuleta
bughudha yenye athari kwa mwili na akili za wana jamii.

Tujifunze kutoka nchi za wenzetu ambazo zimeweka sheria mbali mbali
zinazodhibti kelele za kipuuzi katika sehemu mbali mbali, ikiwa pamoja
na nyumba za starehe, kata vyombo vya usafiri na hata mitaani na
majumbani.

Tuachane na muhali na kuchukua hatua kuinusuru jamii na athari na
hatari zitokanazo na kelele.

Tusikubali wachache kuharibu sifa ya taifa letu


By Mussa Juma
Tanzania ni moja ya mataifa ya mfano duniani, kutokana na kustawi kwa amani na utulivu.
Viongozi wa mataifa mbalimbali wamekuwa wakija kujifunza, nini siri ya Tanzania kudumisha amani na utulivu tangu taifa kupata uhuru.
Tanzania kuna makabila zaidi ya 120 ambayo yanaishi pamoja bila vurugu kama zilivyo nchi nyingine.

Haijawahi kutokea ukabila ukawa sifa ya kuchaguliwa viongozi wa ngazi mbalimbali katika taifa hili.

Licha ya dosari kadhaa katika chaguzi zetu, umoja na mshikamano wetu vimedumishwa katika ngazi mbalimbali kwenye jamii zetu.

Tofauti na mataifa mengine ambayo chaguzi husababisha machafuko makubwa, Tanzania tushukuru uchaguzi umekuwa ukipita na kutuacha salama.

Mazingira ya aina hii, hayakuja hivihivi bali tukubali kuna misingi bora iliyoachwa na waasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume.

Tanzania kwa miaka mingi, viongozi wamekuwa wakihubiri kuimarisha undugu bila kujali, dini, rangi, kabila wala mitazamo ya kisiasa.

Viongozi wetu wamekuwa wakieleza siasa za vyama ni majukwaa tu ya kuwasiliana na wananchi na si kitu ambacho kinaweza kufanya jamii moja kugombana na nyingine hadi kufikia kumwaga damu.

Lakini kadri siku zinavyoongezea kumeanza kuonekana nyufa katika jamii zetu, tofauti za kisiasa na mitazamo vimeanza kuonekana ni uadui na uasi.

Ufa huu unaongezeka kutokana na kauli za kutuhumiana hadharani na kuitana majina ambayo madhara yake ni makubwa katika siku za usoni.

Uelewa mdogo katika jamii, sasa umeanza kupokea vibaya kauli zetu na kuna Watanzania ambao wanaonekana kama maadui wa taifa.

Mazingira haya ya kutuhumiana ndiyo yamekuwa yakivuruga amani katika mataifa mengi barani Afrika.

Naamini mazingira ya aina hii, ndio ambayo yamemsukuma Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kutoa wito kwa vyama tawala barani Afrika kutowachukulia viongozi wa upinzani kuwa maadui.
Rais Kikwete alitoa tamko hilo wakati akichangia mada ya Utawala Bora na Utawala wa Sheria iliyowasilishwa na Profesa Barney Pityana, ambaye ni Makamu Mkuu Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini kwenye Kongamano la Uongozi barani Afrika.

Kauli hii imezua mjadala mkubwa hapa nchini, hadi kufikia hatua Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Humphrey Polepole kueleza kuwa kauli hiyo haikulenga Tanzania bali ililenga mataifa mengine kwani Tanzania ni  ni moja ya nchi vinara wa demokrasia Afrika.

Si vyema kuendelea mjadala huu kwa kutazama ulilenga wapi, lakini itoshe kumpongeza Kikwete kwa kutoa kauli hii, ambayo naamini mataifa mengi barani Afrika yataifanyia kazi.

Katika siku za karibuni, kumeanza kuonekana matukio ambayo yameanza kuwagawa Watanzania kwa misingi ya itikadi zao jambo ambalo ni hatari kwa mustakabali wa taifa letu.

Kukosekana uvumilivu wa kisiasa baina ya viongozi wetu, hali ambayo imesababisha kuongezeka kauli ambazo si nzuri baina ya viongozi wetu wa kisiasa na kamatakamata ya viongozi wa kisiasa wakiwamo wabunge.

Uhasama huu katika jamii, umefikia hatua ya kiongozi wa upinzani mbunge wa jimbo la Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika, Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 28 na baadhi ya watu kushabikia.

Nyufa hizi zimeanza kutumiwa vibaya na wale ambao hawataki, kuiona Tanzania inasonga mbele katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Ukifuatilia katika mitandao ya kijamii, utabaini tukio hili dhidi ya Lissu limeonyesha nyufa katika jamii na kuanza kujengeana uhasama ambao unaweza kuleta matatizo baadaye.

Tumuombe Mungu, wale ambao walijaribu kutaka kulivuruga taifa kupitia tukio la kumshambulia Lissu washindwe na walegee na vyombo vya dola viwakamate wote.

Lakini pia tukio hili linapaswa kutuunganisha Watanzania badala ya kutugawa, kwani isionekane kuna ambao wanafurahia kwani hawajui kesho nani atashambuliwa.

Kundi la watu hawa wachache, wakiachwa watatumia mwanya huo kuchonganisha Serikali na wananchi jambo ambalo si sahihi.

Hivyo itoshe kutoa wito kwa wanasiasa wote, vyombo vya dola, viongozi wa kijamii na viongozi  wa dini kukemea wale wanaotaka kulivuruga taifa letu kwa kujua ama kutojua.

Watu hawa wachache ni vyema kutambua kuwa katika nchi za kidemokrasia, hakuna ushindi wa kweli unaopatikana kwa risasi ama mabavu bali ushindi hupatikana kwa hoja na maridhiano.

Mungu ibariki Tanzania. Mussa juma ni mwandishi mwandamizi wa gazeti la mwananchi anapatikana 0754296503

Wabunge wanawake wabebeshwa zigo kodi za ‘pedi’


Spika wa Bunge, Job Ndugai amewataka wabunge wanawake kusimamia kuondolewa kodi katika taulo za usafi za kike ‘pedi’
Amesema kodi hiyo imekuwa kero, hivyo amemtaka mwenyekiti wa wabunge wanawake, Magreth Sitta kubeba jukumu hilo.
Spika ametoa kauli hiyo kutokana na majibu ya Serikali kutoeleza moja kwa moja ni lini itaondoa kodi kwa taulo hizo.
Akijibu swali bungeni, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla amesema  maombi ya kuondoa kodi hiyo yamewahi kuwasilishwa na watumiaji na wauzaji wa bidhaa hiyo.
Dk Kigwangalla alikuwa akijibu swali la msingi la mbunge wa Viti Maalumu, Stella Alex aliyetaka Serikali ihakikishe inaondoa kodi kwenye taulo hizo.
Naibu waziri amesema uamuzi wa suala hilo umechelewa baada ya kubaini kuwa bidhaa hiyo haikuwa miongoni mwa orodha ya vifaa vya matibabu (vifaa tiba) ambavyo huondolewa kodi.
Hata hivyo, amesema taulo hizo zimeondolewa ushuru wa forodha lakini aina zingine za kodi zinalipwa kama bidhaa zingine.
Amesema Wizara ya Afya imeshaandika barua kwa Wizara ya Fedha na Mipango kuona namna ya kuondoa kodi katika bidhaa hiyo.
“Majadiliano yanaendelea kuwezesha bidhaa hii iunganishwe katika orodha ya vifaa tiba ili viweze kupata msamaha wa kodi na vifaa vingine vya tiba,” amesema.
Naibu waziri amesema kuondolewa kwa kodi kutawezesha kupunguza gharama za taulo hizo, hivyo kuuzwa kwa bei inayokubalika na wengi kumudu kuzinunua.

Mkuu wa majeshi atoa onyo


Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (CDF), Jenerali Venance Mabeyo ametoa tahadhari kwa wananchi kwamba kuna matapeli wanaojifanya wanaajiri vijana kujiunga na jeshi.
Amesema watu hao wanadai fedha ili kuwasajili vijana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jambo ambalo ni kinyume na taratibu za jeshi kuajiri vijana kwa JWTZ na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Mabeyo ameonya kwamba mtu yeyote atakayetapeliwa na watu hao basi naye atahesabika kama mmoja wa watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na kuchukuliwa hatua mara moja.
"Maongezi ya mtu na mtu hatuyatambui, ukitapeliwa nyamaza kimya kwa sababu ukilalamika kwetu na wewe utachukuliwa kama sehemu ya watoa rushwa," amesema Jenerali Mabeyo.

Mkuu huyo wa majeshi amebainisha njia mbalimbali ambazo wanazitumia kuajiri vijana jeshini kuwa ni kuwachukua wale waliopitia mafunzo ya JKT au pale wanapotaka watu wenye taaluma adimu kama vile madaktari, wahandisi au wanasheria.
Amebainisha kwamba jeshi linapokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na wanachukua hatua kila wanapopata taarifa ikiwa ni pamoja na kuwatafuta wahusika na kuwakamata.

"Kuna mmoja alikusanya vijana 15 na kila kijana akatakiwa kulipa Sh1 milioni. Aliwapangia chumba sehemu kisha akatoweka," amesema Mabeyo na kusisitiza kuwa wengi wanaofanya vitendo hivyo ni raia, wanajeshi ni wachache na wanachukuliwa hatua za kinidhamu mara moja.
Kuhusu matukio ya watu kupigwa risasi, CDF amesema wakati wote yanapotokea matukio hayo, vyombo vya ulinzi na usalama vinakabiliana nayo mara moja na hali inakuwa shwari.

"Kwa ujumla hali iko shwari, huwezi kusema Tanzania siyo salama kwa sababu ya matukio mawili ya kijambazi. Mambo tunayotaka kujiridhisha nayo kwa sasa ni wapi wanapata silaha na wanatoka wapi," amesema Mabeyo.

Utafiti: Nyama ya nguruwe ni hatari kwa afya yako



Nchini Tanzania nyama ya nguruwe ni maarufu katika maeneo mbali mbali ya starehe na imepewa majina mengi ,kama vile mkuu wa meza, kiti moto na mengineyo mengi.
Hata hivyo utafiti wa kisayansi kutoka chuo kikuu cha kilimo cha sokoine ( SUA), umebaini kuwa walaji wa nyama ya nguruwe wako katika hatari ya kupata magonjwa kama vile kifafa kutokana na mnyoo Tegu uliopo kwenye nyama ya nguruwe.
Mwandishi wa BBC Maximiliana Mtenga amezungumza na mtafiti wa magonjwa ya binadamu na wanyama Dkt. Boa Mathias Emanuel kutoka chuo kikuu cha SUA, na kwanza amemuuliza ueneaji wa ugonjwa huu.

Wabunge wapewa haki, wanyang’anywa


Serikali imefanyia marekebisho Sheria ya Petroli nchini kwa kufuta sura 392 ambayo ilikuwa inaweka masharti kuwa mkataba wa mafuta hautaanza kazi hadi uridhiwe na Bunge, ikiwa ni miezi miwili tangu kupitishwa fursa hiyo.
Marekebisho hayo yanakuja miezi miwili baada ya Mkutano wa Saba wa Bunge (bajeti) kupitisha Muswada wa Sheria Mbalimbali, pamoja na mambo mengine sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho.
Marekebisho hayo yaliyowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju na kuridhiwa na Bunge jana yapo katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 3 wa Mwaka 2017.
Masaju alisema kifungu hicho kwa namna kilivyoandikwa kinapingana na masharti ya Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Maliasili na Raslimali za Nchi ya Mwaka 2017 na Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba inayohusu Maliasili ya Nchi Mwaka 2017.
Alisema sheria hizo zinaainisha kuwa Bunge linaweza kupitia mikataba iliyoingiwa na Serikali kuhusiana na maliasili na rasiliamali za nchi, si kutoa kibali cha kuanza kutumia.
“Hivyo ibara ya 16 ya muswada huu inapendekeza kifungu hicho kifutwe. Lengo la marekebisho haya ni kuwianisha masharti ya sheria hizo kuhusiana na nafasi ya Bunge kutekeleza ipasavyo wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri ipasavyo Serikali, kwa mujibu wa ibara 63(2) ya Katiba,” alisema Masaju.
Akitoa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh Ally alihoji sababu ya Serikali kufanya tena marekebisho ya kifungu hicho kwa kuondoa mamlaka kwa Bunge.
“Ni mwezi wa pili sasa, Sheria ya Petroli ifanyiwe marekebisho na kuongeza kifungu kidogo cha sita na kulipatia Bunge mamlaka ya kuridhia mikataba yote ambayo inahusiana na rasilimali ya mafuta ya petroli.” alisema Saleh na kuongeza:
“Marekebisho ya Sheria mara nyingi huletwa baada ya mamlaka za Serikali kupata uzoefu wa utekelezaji wa sheria husika, suala la kuhoji hapa ni kuwa ni uzoefu gani ambao Serikali imepata ndani ya miezi miwili baada ya kutungwa kifungu hiki?”
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mohamed Mchengerwa alisema kamati imekubaliana na mabadiliko hayo.
Alisema kama Bunge litapitisha mikataba hiyo hakutakuwa na dhana ya kuisimamia katika mihimili ya dola, hivyo kulifanya Bunge kuwa Sehemu ya makosa au matatizo yanayotokana na mikataba hiyo.
Akichangia Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alisema marekebisho ya sheria hiyo yaliletwa Bunge hivi karibuni na wao wakalalamikia kuletwa kwa dharura.
“Nguvu kubwa inayotumika hapa. Wakati ujao hii habari ya dharura tuache, tuzingatie utaratibu tupokee ushauri tusiangalie sura yake wala chama chake, dharura imeligharimu Taifa hili, imetuumiza na hili tatizo linaendelea kujirudia,” alisema.
Naye Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali alisema wapo mawaziri waliopita kwa kukosea kidogo tu na pengine kwa kushauriwa na wanasheria, hivi sasa wapo matatani. “Kwa nini huyu Mwanasheria Mkuu wa Serikali naye asiwajibishwe, ameiabisha Serikali lakini analeta sheria zinazopingana na nyingine. Naamini sheria zote zinazokuja hapa zinapitia mezani kwako na wewe unazipitia,” alisema.

Rais Magufuli aivunja KDA


Rais John Magufuli ameivunja Mamlaka ya Usimamizi wa Mji Mdogo wa Kigamboni (KDA) na  sasa shughuli zake zinahamishiwa katika Manispaa ya Kigamboni.
Akizungumza leo Jumatano,Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema ametumwa na Rais Magufuli kutangaza uamuzi huo.
"Kumekuwa na mgongano katika usimamizi wa ardhi kati ya KDA na Manispaa ya Kigamboni, Rais ameliona hilo na kuamua kuivunja mamlaka hiyo,"amesema.
Lukuvi amesema jukumu la KDA lilikuwa kusimamia upangaji wa mji wa Kigamboni wakati hilo pia ni jukumu la manispaa hiyo.
Lukuvi ametoa miezi sita kwa watendaji wa KDA kukamilisha makabidhiano ya nyaraka na wao kuripoti kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa amesema mgongano wa usimamizi wa ardhi Kigamboni ulisababisha migogoro mingi ya ardhi.
Amesema pia manispaa hiyo ina upungufu wa maofisa mipango miji.
Amesema manispaa ina maofisa mipango miji watatu badala ya saba wanaohitajika.

Rahco yabisha hodi Kilimanjaro, kubomoa zaidi ya nyumba 100


Siku chache baada ya bomoabomoa inayoendeshwa na Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (Rahco) kutikisa mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma na Tanga, sasa ni zamu ya Kilimanjaro ambako zaidi ya nyumba 100 zimewekwa alama ya X ikiwa ni hatua ya awali ya kubomolewa.
Nyumba hizo ambazo zimewekwa alama ya X na Rahco ikiwa ni operesheni ya nchi nzima kubomoa nyumba za waliovamia maeneo ya reli, zipo Mtaa wa Arabika, Kata ya Miembeni.
Akizungumzia hatua hizo juzi, Ofisa Uhusiano wa Rahco, Catherine Moshi alisema watu wote waliovamia na kujenga maeneo ya reli lazima waondoke ili kupisha ujenzi wa reli.
Moshi alisema kampuni hiyo ilitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari Aprili 24 mwaka jana, kwamba watu waliovamia na kujenga maeneo hayo waondoke mara moja.
Alisema lazima wayachukue maeneo yao yaliyovamiwa na watu na kwamba, watahakikisha yamerudi mikononi mwa mamlaka husika kwa ajili ya kuendeleza reli.
“Watu walifikiri kwamba reli ilikufa ndiyo maana wakavamia na kujenga, lazima watupishe katika maeneo yetu ili tuyaendeleze na hii ni operesheni ya nchi nzima,” alisema Moshi.
Akizungumzia operesheni hiyo, Diwani wa Miembeni, Mbonea Mshana alikiri kuwapo nyumba zilizotangazwa na Rahco nchi nzima na kwamba, wote waliowekewa alama ya X wamepewa siku 30 kuondoka.
Hata hivyo, Mshana alisema amezungumza na ofisa mipango miji wa Manispaa ya Moshi kuona namna ya kushughulikia suala hilo.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi alisema hawajatoa hatimiliki na kuweka mawe ya mipaka maeneo hayo na kwamba, waathirika wameingizwa matatani na wahuni.
“Its very sad news (ni habari mbaya), reli hiyo ilikuwapo hata kabla ya uhuru. Watu hao waliingizwa mkenge (matatani) na wahuni, lazima atajulikana aliyefanya uhuni huo hata kama ilikuwa ni muda mrefu labda kama amekufa, lakini atajulikana tu,” alisema Mwandezi.
Machi 23, 2016 Rahco ilitoa notisi ya siku 30 kwa waliojenga kwenye maeneo ya reli kuondoka kupisha ujenzi wa reli ya Standard Gauge. Hata hivyo, Machi 11 ikiwa ni takriban mwaka mmoja kupita bila wahusika kubomoa kwa hiari, Rahco walianza kazi hiyo jijini Dar es Salaam na kuendelea mikoa ya Kigoma, Mwanza, Tabora na Tanga.

iPhone X: Matukio 10 makuu katika mwongo mmoja wa iPhone

iPhoneHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionWatu hawakuruhusiwa kuigusa hata kidogo simu ya kwanza ya iPhone ilipozinduliwa
Kampuni ya Apple inaadhimisha miaka 10 tangu kuzinduliwa kwa simu zake za kisasa aina ya iPhone na inatarajiwa kwamba watazindua simu nyingine itakayokuwa na mabadiliko makubwa tangu kuzinduliwa kwa simu hizo.
Miongoni mwa mengine, muundo wa simu zenyewe unatarajiwa kubadilika, zitakuwa na uwezo wa kumtambua mtu kwa kuchunguza uso wake na pia kutakuwa na mabadiliko mengine kuongeza mtazamo wa uhalisia kwenye simu zenyewe.
Wachanganuzi kadha wamedokeza kwamba huenda bei ya simu hizo ikapanda zaidi.
Katika ulimwengu ambao simu za smartphone zimekuwa kama sehemu ya binadamu, ni rahisi kusahau jinsi simu za iPhone zilipozinduliwa na Steve Jobs mwongo mmoja zilivyowashangaza wengi na jinsi mjadala mkali ulivyozuka kuhusu iwapo zingebadilisha teknolojia mbalimbali za simu.
Kuadhimisha miaka 10 ya iPhone, tumechagua matukio makuu 10 katika kipindi hicho ambayo yalibadilisha sana mambo.

1. 2004: Kuzaliwa kwa Project Purple
Project Purple designHaki miliki ya pichaAPPLE
Image captionMuundo huu - ambao ulipewa jina Purple - uliundwa na wabunifu wa Apple Agosti 2005
Baada ya kufanikiwa kwa iMac na baadaye iPod, Apple walianza kuunda tabiti kama bidhaa waliyotarajia ingewafanikiwa sana.
Lakini 2004 hivi, mkuu wa zamani wa iOS Scott Forstall anakumbuka akiwana na mazungumzo ya kina na afisa mkuu mtendaji Steve Jobs wakila chakula.
"Sote tulikuwa tunatumia simu ambazo hazikutufurahisha," aliambia mkutano mmoja mapema mwaka huu.
2Tulitazama watu waliokuwa karibu nasi, na karibu kila mtu alikuwa na simu, na kila mtu alionekana kutofurahishwa na simu hizo.
"Na Steve akasema, 'Unafikiri kama tunaweza kubadilisha majaribio hayo tunafanya ya tabiti na kifaa cha kudhibitiwa kwa kugusa kwa vidole na badala yake tuunde kifaa kidogo kinachoweza kutoshea kwenye mfuko wako?'"
Hili liliwafanya wahandishi kuunda programu tumishi ya kuhifadhi nambari za simu ambayo ilitumia nafasi ndogo tu kwenye kona ya skrini.
"Punde tu [Steve Jobs] alipoona muundo huo, alijua tumefika," Bw Forstall anasema. "Hakukuwa na shaka. Hivi ndivyo simu zilifaa kuwa."
Kama nyaraka zilizowasilishwa kortini baadaye zilivyofichua, kufikia Agosti 2005 wahandisi wa Apple walikuwa wamepiga hatua sana katika kukuza dhana ya simu hizo - ambayo ilifahamika kama mradi wa Purple.
Dhana hiyo sasa inatambuliwa kama chanzo halisi cha simu hiyo ambayo ilifuata.

2. Julai 2008: App za kwanza za iOS App Store zatolewa
MooHaki miliki ya pichaERICA SADUN
Image captionMoja ya app asili za iPhone ambazo bado zinapatikana katika App Store
Kwa sasa, kuna zaidi ya programu tumishi (app) zaidi ya milioni mbili katika mfumo endeshi wa simu za iPhone wa iOS.
Lakini zilipozinduliwa kwanza, zilikuwa chache sana, kwa sababu watengenezaji wa app wa nje walitakiwa kuunda app ambazo zilifanya kazi katika kisakuzi za simu yenyewe.
Jobs aliamini ingekuwa vigumu sana kufuatilia soko la app.
Ilikuwa ni hadi zaidi ya mwaka mmoja baadaye ambapo App Store ilizinduliwa.
Historia iliandikishwa tarehe 9 Julai Apple walipozindua app kadha kabla ya kufanywa wazi kwa soko lake la App.
Miongoni mwa app hizo kulikuwa na Moo - app ya kuiga mlio wa ng'ombe - ambayo ilikuwa imetengenezwa na mtayarishaji wa app kutoka Denver kwa jina Erica Sadun.

3. Septemba 2008: Kuzinduliwa kwa HTC Dream
HTC DreamHaki miliki ya pichaHTC
Image captionSimu za kwanza za Android hazikuwa na uwezo wa kugusa maeneo mengi kwenye skrini kwa kidole
Wajua kwamba afisa mkuu mtendaji wa Google alikuwa wakati mmoja kwenye bodi ya wakurugenzi wa Apple?
Eric Schmidt hakujiuzulu hadi 2009, lakini alikuwa njiani baada yake kuanza kuuza simu zake za kwanza za Android.
Mfumo huo endeshi uliotumiwa kwenye simu ya HTC Dream ulikuwa na mambo ambayo iPhone ilikuwa haina mpano uwezo wa 'kunakili' na 'kubandika', Street View na kuweza kutuma ujumbe wenye picha na video.
Wengi walipendekezwa na mfumo huo endeshi simu hizo, na Google walitambua uwezo mkubwa wa kufungua simu za kisasa jambo ambalo lingeipa Android nafuu zaidi ukilinganisha na iOS.
Simu hizo ziliweza kupokea maelezo wa kuguswa kwa vidole kadha - simu ingetambua ni vidole vingapi vilivyokuwa vinatoa maelekezo.
Lakini uwezo huo haukuwezeshwa, pengine kutokana na hali kwamba Apple walikuwa wamesajili hakimiliki ya teknolojia hiyo.
HTC walipoongeza uwezo huo katika simu nyingine mwaka 2010, Stev Jobs alikereka.
"Nitaiangamiza Android, kwa sababu ni bidhaa ya wizi," alimwambia mwandishi wa wasifu wake Walter Isaacson.
"Niko tayari kupigana nao vita vya nyuklia."

4. Februari 2010: App ya Siri yazinduliwa na SRI
SiriHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionSiri waliiwezesha Apple kuingia soko la Kutafuta habari mtandaoni
Siku hizi Apple hutumia mamilioni ya pesa wakitayarisha matangazo yanayosirikisha Siri na Dwayne "The Rock" Johnson, miongoni mwa waigizaji wengine.
Lakini app hiyo inayopokea maelezo ya sauti kutoka kwa anayetumia simu ilipozinduliwa kwenye iOS, ilikuwa ni app ambayo haikuangaziwa sana.
Ilikuwa imetayarishwa na taasisi ya utafiti kutoka California ambayo ilikuwa kwa sehemu fulani imefadhiliwa na Pentagon.
Muundo wake wa kibiashara ulikuwa ni kutoza migahawa na waandaaji wa hafla mbalimbali ada kwa kila oda ambayo ilitolewa kwa kutumia sauti kwa biashara zake.
Mpango ulikuwa wa kutoa aina nyingine tofauti za programu hiyo za kutumiwa na simu zinazotumia Android na Blackberry.
Lakini mpango huo ulibadilishwa miezi miwili baada ya kuzinduliwa kwake, Apple waliponunua teknolojia hiyo kwa takriban $200m (£150m).
App hiyo iliendelea kuuzwa kwenye App Store hadi Oktoba 2011, ambapo iliongezwa kama kiungo cha kununuliwa na simu, simu za iPhone 4S zilipozinduliwa.

5. Juni 2010: iPhone ya kwanza ya selfie
iPhone 4Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionKamera ya upande wa mbele ya iPhone 4 ilikuwa inapiga picha ya megapikseli 0.3
iPhone 4 ilipozinduliwa, ilikuwa na kamera nyingine ya ziada upande wa mbele ambayo iliangazia zaidi kupiga simu za video badala ya kujipiga picha.
Ingawa neno "selfie" lilikuwa tayari limebuniwa, halikuwa limevuma sana.
Ingawa iPhone 4 haikuwa ya kwanza kuwa na kamera pande zote mbili - Sony Ericsson waliunda simu kama hiyo 2003 - wanaweza kusema ndio waliochangia kuvuma zaidi kwa picha za kujipiga, maarufu kama selfie.
Siku hizi, badala ya watu kuwaomba nyota wao wawawekee saini kwenye nguo, vitabu au vitu vingine vya thamani, imekuwa watu ni kujaribu kujipiga picha ukiwa nao.

6. Oktoba 2011: Kifo cha Steve Jobs
Steve JobsHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionSteve Jobs alifariki kutokana na saratani nadra ya kongosho
Tim Cook - badala ya Steve Jobs - alipozindua 4S mamo 4 Oktoba2011, alikosolewa sana kutokana na alivyoendesha hafla hiyo.
BBC hata wenyewe walisema hakuwavutia watu.
Kitu ambacho wengi walikuwa hawafahamu ni kwamba huenda Cook alikuwa anafahamu kwamba mlezi wake na rafiki mkuu Steve Jobs alikaribia kufariki.
Alifariki dunia siku iliyofuata.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba Apple ingelisambaratika iwapo Jobs hangeamua kurejea katika kampuni hiyo aliyosaidia kuianzishwa mwaka 1997. Hii ina maana kwamba huenda hakungewahi kuwa na iPhone.
Au labda iwapo hangeondoka wakati mmoja Apple, wahandisi wa kampuni hiyo wangelifuata muundo tofauti wa simu uliofuatana na iPod.
Tangu kifo chake, Apple hawajawahi kuzindua bidhaa iliyokaribia ufanisi wa Apple.
Jobs alionekana mara ya mwisho hadharani Cupertino City Council Juni 2011, ambapo aliomba idhini ya kujenga makao makuu mapya ya Apple.
Simu mpya za iPhone zitazinduliwa katika makao makuu hayo, eneo linaloitwa Ukumbi wa Steve Jobs.

7. Aprili 2012: Facebook kununua Instagram kwa $1bn
InstagramHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Iwapo bado kulikuwa na shaka kuhusu athari za iPhone katika uchumi, ununuzi wa iPhone ulimaliza mashaka hayo.
App hiyo ilikuwa imedumu miezi 18 pekee sokoni ununuzi wake ulipotangazwa.
Ilikuwa na wafanyakazi 13 pekee na ilikuwa inatumiwa kwenye iOS pekee hadi wiki moja kabla ya ununuzi.
Ununuzi huo ulibadilisha mambo kwa wawekezaji wa Instagram na app nyingine za simu ambao walikuwa wanatafuta pesa.
Wengi walidhani Facebook walilipa pesa nyingi kupita kiasi. Sasa, Instagram wameanza kupokea pesa nyingi sana za matangazo na kuwa faida kuu.
App nyingine ambazo zilianza katika iPhone - zikiwemo Uber, Deliveroo na Airbnb - zimebadilisha sekta nyingi.
Baadhi ya wachanganuzi wanakadiria kwamba jumla ya thamani ya biashara za app - mauzo, utangazaji na biashara kwenye simu - ilikuwa ya jumla ya $1.3tn (£993bn) mwaka jana.

8. Julai 2012: Apple yanunua AuthenTec
Touch IDHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionApplewalitumia mwaka mmoja hivi kuongeza teknolojia ya AuthenTec kwenye iPhones
Apple walinunua kampuni ya kutambua alama za vidole ya AuthenTec kwa miaka $356m mwaka 2012 na kuwasababishia matatizo Samsung.
Kampuni hiyo ya Korea Kusini ilikuwa inatumia baadhi ya vifaa vyake kwenye laptopu zake na ilikuwa imetangaza mkataba wa kuongeza baadhi ya viungo vyake vya usalama kwenye simu zake za Android phones.
Lakini ingawa walifurahia pia kuwashinda wapinzani wao wakuu, Apple walifaidi zaidi kwa kuweza kuzindua mfumo wake wa Touch ID kwenye iPhone 5S mwaka 2013.
Mwanzoni, ilitumiwa tu kufungua simu na kufanya ununuzi kutoka kwa Apple lakini baadaye, Apple waliweza kuanzisha Apple Pay na kuongeza usalama zaidi kwa kutumia alama za vidole bila kuhitaji mtu kuweka nywila.

9. Agosti 2013: Steve Ballmer alipong'atuka Microsoft
Steve BallmerHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionIngawa simu za Windows zilifanikiwa sana Ulaya, hazikutoa ushindani mkubwa sana kwa iPhone
Mwaka 1997, Microsoft waliisaidia Apple kwa kununua hisa za $150m katika kampuni hiyo ambayo ilikuwa haifanyi vyema.
Apple nao waliwafaa kwa kuzindua bidhaa ambayo Microsoft mwanzoni hawakuielewa vyema lakini baadaye walihangaika kushindana nayo.
Afisa mkuu mtendaji wa Microsoft Steve Ballmer alikuwa amewacheka Apple aliosikia wanazindua iPhone.
"Hii ndiyo simu ghali zaidi duniani, na haiwavutii wateja wa kibiashara kwa sababu haina kibodi," alisema 2007.
Miaka sita baadaye, alinunua biashara ya simu ya Nokia kwa kutumie euro 5.4bn ($6.5bn; £5bn) akijaribu kushindana na Apple.
Pesa hizo zilikuwa hasara mwaka 2015 baada yake kuondoka kwani mrithi wake alikubali kwamba Simu ya Windows haingefanikiwa.
Jambo la kushangaza ni kwamba iwapo Microsoft hawangekuwa wameuza hisa zao Apple chini ya Ballmer, hisa hizo sasa zingekuwa za thamani ya zaidi ya $40bn.

10. Julai 2016: Kuzinduliwa kwa Pokemon Go
Pokemon GoHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
'Homa' ya Pokemon Go kwa sasa imeisha, lakini app hiyo itaendelea kukumbukwa kwa muda mrefu.
Kuvuma kwake kulithibitisha kwamba app zinazoangazia maisha ya uhalisia zinaweza kuvuma sana.
Teknolojia hiyo ya kuoanisha maisha ya kubuni na maisha ya uhalisia (AR) chanzo chake ni mwaka 2009 kwenye iPhone, Mfaransa mmoja alipounda app ambayo ilikuwa inakuonesha maduka yaliyo karibu na maeneo mengine ya kuvutia Paris.
Lakini inakaribia kukomaa iOS itakapozinduliwa, ikiwa ni pamoja na ARKit - programu ambayo itarahisisha uundaji wa michoro na picha kwa njia rahisi zaidi.
Tayari kuna mifano ambayo imezinduliwa na imeonekana kupendeza.
Swali kuu linabaki kuwa iwapo wateja wataridhishwa na kujivunia matukio yanayokaribia uhalisia kwenye simu zao za iPhone pekee au Apple watahitajika kutoa vifaa vya kando vya kutumiwa na simu hizo.