Saturday, August 19

Mwanzo wa mwisho wa dunia utakuwa Jumatatu 21 Agosti?

Jua litapatwa na mwezi kikamilifu Amerika kaskazini kwa mara ya kwanza kabisa Jumatatu tangu 1918Haki miliki ya pichaALAMY
Image captionJua litapatwa na mwezi kikamilifu Amerika kaskazini kwa mara ya kwanza kabisa Jumatatu tangu 1918
Mnamo Jumatatu tarehe 21 Agosti, tukio lisilo la kawaida litashuhudiwa Amerika Kaskazini, ambalo limewavutia watu zaidi ya milioni saba wanaotarajia kulishuhudia katika miji mbalimbali Marekani.
Kwa mara ya kwanza tangu 1918, jua litapatwa kikamilifu na mwezi Marekani.
Bara lote la Amerika Kaskazini litafunikwa na giza totoro mchana.
Ingawa baadhi ya watu wanalitazama tu kama tukio la kuvutia, kwa wengine, hili linaashiria mwisho wa dunia kama tunavyoifahamu kwa sasa.
Makundi mbalimbali ya Kiinjilisti nchini Marekani kwa mfano, yameanza kuhubiri kwamba tukio hilo linaashiria kukaribia kwa mwisho wa dunia.
Tovuti moja ya unabii wa Kikristo kwa jina Unsealed imedai kwamba tukio hilo la Jumatatu litaanzisha kipindi cha Majonzi, kipindi cha miaka saba ambapo katika kipindi hicho asilimia 75 ya watu wote duniani wataangamizwa.
Kwa wengine hata hivyo, ni tukio ambalo wamesubiri sana kwa hamu majira haya ya joto.
Kuna watu 12 milioni ambao wanaishi eneo la upana wa maili 70 9kilomita 112) kutoka Oregon hadi Carolina Kusini ambapo mwezi utalifunika kabisa jua.
Utalii wa "kutazama kupatwa kwa jua" unatarajiwa kuwazolea pesa nyingi sana, utalii ambao ulianza kupata umaarufu karne ya 18 ambapo watu wengi walisafiri hadi miji ambayo jua lingepatwa na mwezi Ulaya.
Lakini ni kwa nini tukio hili nadra sana linavutia watu wengi na pia kwa wengine kuibua wasiwasi?

Wasiwasi zama za kale

Katika karne ya 7 kabla ya kuzaliwa kwa yesu Kristo, mshairi maarufu Archilocus aliandika kuhusu kutokea kwa tukio hilo katika ksiiwa cha Paros, Ugiriki: " Hakuna jambo linaloweza kunishangaza tena duniani sasa. Kwani Zeus, babake Olympian, amegeuza mchana kuwa usiku wa giza kwa kulifunika jua, na sasa ukatili wa giza unawakodolea macho binadamu. Jambo lolote linaweza kutokea."
Tangu zamani tukio la jua kupatwa na mwezi limekuwa likizua wasiwasi wa mwisho wa duniaHaki miliki ya pichaALAMY
Image captionTangu zamani tukio la jua kupatwa na mwezi limekuwa likizua wasiwasi wa mwisho wa dunia
Watu wengi hawakufahamu kabisa nini kilitokea wakati wa jua kupatwa na mwezi, hadi karne ya 17, anasema Edwin Krupp, mkurugenzi wa kituo cha kutafiti anga za juu cha Griffith jimbo la California.
Wagiriki hawakuwa peke yao katika kuingiwa na wasiwasi.
Ingawa kuna wasomi kadha kuanzia karne ya 8 tangu kuzaliwa kwa Yesu ambao walianza kufahamu jua hupatwa vipi na mwezi, kwa miaka mingine 2,000, watu wengi duniani walihusisha tukio hilo na miungu.
Krupp anasema kwa muda mrefu, watu walijaribu kufafanua yaliyokuwa yakitokea na mambo na vitu vilivyowazunguka.
Hadi wa leo, baadhi ya maeneo duniani bado kuna itikadi kuhusu tukio la mwezi jua kupatwa na mwezi.
Nchini India, kuna baadhi ya wajawazito hawawezi kutoka nje ya nyumba zao wakati wa tukio hilo kwa sababu wanaogopa wanaweza kupatwa na madhara.
Ili kukabiliana na wasiwasi huo, baadhi ya jamii zilianza kufanya matambiko, wakijaribu kuwasiliana na nguvu au mashetani ambao waliamini walihusika katika kuliziba jua.
Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image caption"Tubuni; kwani Ufalme wa Mungu unakaribia," unasoma ujumbe katika bango hili lililobebwa na mmoja wa wanaoamini mwisho wa dunia unafika mjini Washington DC mwezi jana.
Moja ya itikadi za wakati huo ni kwamba kulikuwa na nduli aliyekuwa anashambulia Jua au Mwezi.
Asia magahribi, watu waamini jua kupatwa na mwezi kulitokana na zimwi kulishambulia jua. Wangepiga ngoma kubwa kujaribu kumtia woga nduli huyo aliache jua. China waliamini mbwa ndiye alikuwa analishambulia jua. Peru nako, wakazi waliamini mnyama mkubwa aina ya puma ndiye aliyekuwa analishambulia jua. Ulaya, maharamia wa Scandinavia maarufu kama Viking waliamini mbweha angani wlaikuwa wanashambulia jua. Si ajabu kwamba neon la kale zaidi kuhusu jua kupatwa na mwezi nchini China ni shih, ambalo lina maana ya "kula".

'Mapenzi ya Jua na Mwezi

Si watu wote hata hivyo walioogopa tukio hilo. Watu wa jamii ya Batammaliba nchini Togo na Benin walikuwa wakitazama tukio hilo kama vita kati ya Juan a Mwezi. Wangewahimiza kuacha vita na kutumia wakati huo kumaliza uhasama wa tangu jadi na kusameheana. Watu asilia wa kusini mwa Pasifiki na Amerika kaskazini magharibi walitazama tukio hilo kama wakati wa mapenzi. Waliamini Jua na Mwezi zilikuwa zinajificha nyuma ya pazia kushiriki mahaba faraghani.
Jarita Holbrook, mtaalamu wa anga za juu, anasema watu walitazama tukio hilo kwa kutegemea utamaduni wao. Katika maeneo ambayo kuna joto na chakula, miungu si wakatili na hivyo unalitazama kwa upande wa mema.
Lakini iwapo utamaduni wenu una dini ambapo miungu wanawatazama na wanaweza kuwaadhibu, basi utaogopa tukio kama hilo na kulihusisha na maafa "na mwisho wa dunia."
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Ulaya nyakati za Ukristo. Baada ya kuhangaishwa na tauni, vita na pia baada ya kufahamu vyema Biblia, fikira zao wakati wa tukio la jua au mwezi kupatwa zilikimbilia katika kitabu cha Ufunuo ambacho kinatabiri wakati ambapo Jua litageuka na kuwa giza nao mwezi ubadilike na kuwa rangi ya damu.
"Ni rahisi sana kuelewa ni kwa nini watu hufikiria hivi," anasema Chris French, profesa anayeangazia masuala ya saikolojia.
"Kitendo cha Jua kutoweka angani wakati wa jua kupatwa na wezi, kuna mambo mengi kiishara yanayohusishwa na hilo. Wakati wa mweiz kupatwa na jua, jua hugeuka na kwua rangi nyekundu. Na unagaa kukumbuka kwamba kwa watu wengi, hili ni jambo ambalo hawajawahi kuliona. Muda wa kuishi ni mfupi, na kwa hivyo haya si matukio ya kawaida."
Wahispania walipoteka himaya ya Aztec katika karne ya 16, kulikuwa na mtawa wa kundi la Francisca kwa jina Bernardino de SahagĂșn, ambaye sasa hcuhukuliwa kama mmoja wa wanaanthroporojia wa kwanza kabisa.
Anazungumzia wenyeji walivyopokea tukio la jua kupatwa na mwezi:
"Wote waliingiwa na wasiwasi na kuanza kulia. Watu wa kawaida walilia, kwa sauti. Kelele zilitanda kote. Watu wa rangi ya maji ya kunde walichinjwa kama kafara. Mateka waliuawa. Wote walitoa damu zao. Katika mahekalu yote, watu waliimba na kucheza zaburi. Kulikuwa na nyimbo za vita. Baadhi walsiema, iwapo hii itakamilika, basi kutakuwa na giza daima. Mashetani wa giza watashuka na kuwala binadamu."

Nguvu za kisiasa

Kwa watu wachache waliofahamu kilichokuwa kinaendelea, walitumia tukio hilo kujifaa kisiasa.
Mwaka 1504, wanabaharia wake walipokuwa karibu kufa njaa baada ya meli yao kuzama pwani ya Jamaica, Christopher Columbus alikomesha maasi kwa kutumia tukio la mwezi kupatwa na jua kuwafanya wenyeji wa jamii ya Arawak kwamba alikuwa amedhibiti mbingu. Aliwashurutisha kumpa chakula.
Miaka 300 baadaye, alipokuwa anaunga ufalme wa Wazulu, Shaka kaSenzangakhona aliimarisha utawala wake kwa kuwashawishi watu wake kwamba alikuwa na uwezo wa kulidhibiti jua.
Moja ya sababu ambazo hufanya imani ya mambo kutokea kutokana na jua kupatwa na mwezi ni sadfa tu.
Kwa watu ambao wanaamini katika nguvu za nyota na unajimu, na kwamba mpangilio wa nyota huwa na ujumbe fulani, bila shaka kutakuwa na sadfa ambapo tukio la watu kuona kimondo na kifo cha mtu au kuzaliwa kwa moto vitatokea wakati mmoja.
French anasema kwa wale ambao hawaamini mambo kama hayo yanaweza kutokea kwa pamoja kwa kawaida, hilo huwapa sababu zaidi ya kuamini katika unajimu.
Sababu nyingine ni kwamba miili ya binadamu hubadilika kutokana na tukio lisilo la kawaida mfano jua kupatwa na mwezi.
Holbrook anasema. "Mapigo ya moyo wako huongezeka, kuna mabadiliko katika kiwango cha joto mwilini, kupumua, mboni za macho na pia kutokwa na jacho. Kunao wanaoamini kwamba hili hutokea kwa sababu binadamu huzaliwa na uwezo asilia wa kutambua yanayojiri duniani, na unapokumbana na jambo ambalo kawaida huwa haliwezekani, hilo huufanya ubongo kchukua hatua."
"Miili yetu huchukua hatua kwa njia sawa, lakini jinsi hayo hufasiriwa hutegemea utamaduni."

Uchaguzi Kenya: Upinzani wawasilisha kesi ya kupinga ushindi wa Kenyatta

Odinga anadai mitambo ya tume ya uchaguzi ilidukuliwa kumfaa KenyattaHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionOdinga anadai mitambo ya tume ya uchaguzi ilidukuliwa kumfaa Kenyatta
Muungano wa upinzani nchini Kenya National Super Alliance umewasilisha kesi ya kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 8 Agosti.
Mawakili wa muungano huo wamewasilisha nyaraka za kesi hiyo na ushahidi katika majengo ya Mahakama ya Juu mjini Nairobi takriban saa moja unusu kabla ya muda ulioruhusiwa kumalizika.
Nyaraka na stakabadhi za ushahidi zilizowasilishwa na muungano huo ni za kurasa 9,000.
Kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyotangazwa Ijumaa wiki iliyopita ilifaa kuwasilishwa kabla ya saa sita usiku leo, kabla ya kumalizika kwa siku saba tangu kutangazwa kwa matokeo.
Mgombea urais wa chama hicho waziri mkuu wa zamani Raila Odinga alikuwa ameapa kutopinga matokeo ya urais tena kortini kabla ya uchaguzi kufanyika na baada ya matokeo kutangazwa.
Lakini alibadilisha uamuzi huo na kutangazwa Jumatano wiki hii kwamba muungano wake ungefika kortini kupinga matokeo hayo.
Bw Odinga alisema ingawa muungano huo ulikuwa umeapa kutowasilisha kesi kortini wakati huu, waliona ni heri kufanya hivyo "kufichua uovu uliotokea wakati wa uchaguzi mkuu."
"Tumeamua kwenda kortini kufichua jinsi uongozi wa kompyuta ulivyofanikishwa...Hawa ni viongozi wa kompyuta. Kompyuta ndiyo iliwataga, kompyuta iliangulia, kompyuta iliwatoa. Vifaranga vya kompyuta."
Wafuasi wa upinzani wamekusanyika katika barabara za kuelekea majengo ya Mahakama ya Juu
Image captionWafuasi wa upinzani wamekusanyika katika barabara za kuelekea majengo ya Mahakama ya Juu
Bw Odinga alisema mitambo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC ilidukuliwa na matokeo kuvurugwa kumfaa Bw Kenyatta ambapo kulikuwa na pengo kiasi fulani kati yake yeye na Bw Kenyatta muda wote wa kutangazwa kwa matokeo.
Aidha, kiongozi huyo aliishutumu tume ya uchaguzi akisema ilikuwa ikitangaza matokeo ya uchaguzi bila kutoa Fomu 34A za kuonyesha matokeo yalivyokuwa katika vituo vya kupigia kura.
Jamii ya kimataifa ilikuwa imehimiza upinzani, pamoja na wagombea wengine ambao hawakuwa wameridhishwa na uchaguzi, kutumia mifumo iliyowekwa kikatiba kutafuta haki.
Kwa mujibu wa matokeo ya IEBC, Rais Kenyatta alipata kura 8,203,290 huku naye Raila Odinga akipata kura 6,762,224.

Matokeo na mshindi kila kaunti uchaguzi wa urais 2017

Bofya kwa maelezo zaidi
Chanzo: IEBC

Tarehe muhimu kesi ya kupinga uchaguzi wa rais

  • Agosti 18: Siku ya mwisho ya kuwasilsiha kesi
  • Agosti 20: Siku ya mwisho ya kuwasilisha nyaraka za kesi kwa wanaofaa kujibu kesi
  • Agosti 24: Siku ya mwisho kwa wanaofaa kujibu kesi kuwasilisha majibu
  • Septemba 1: Siku ya mwisho kwa Mahakama ya Juu kutoa uamuzi.
Uamuzi wa Mahakama ya Juu kuhusu kesi hiyo ni wa mwisho. kwa mujibu wa Katiba ya kenya, iwapo mahakama hiyo itaidhinisha ushindi wa Bw Kenyatta kiongozi huyo ataapishwa kuongoza kwa muhula mwingine tarehe 12 Septemba, siku saba baada ya kutolewa kwa uamuzi.
Iwapo mahakama hiyo itakubali malalamiko ya upinzani na kubatilisha ushindi wa Bw Kenyatta, basi uchaguzi mpya utafanyika katika kipindi cha siku 60 baada ya uamuzi kutolewa, kufikia tarehe 31 Oktoba.

Refa wa kandanda apigwa risasi na kuuawa Mogadishu, Somalia

Dirah amepigwa risasi akiondoka msikitini kurejea kwake nyumbaniHaki miliki ya pichaSHIRIKISHO LA SOKA LA SOMALIA
Image captionDirah amepigwa risasi akiondoka msikitini kurejea kwake nyumbani
Mwamuzi maarufu katika mchezo wa kandanda nchini Somalia amepigwa risasi na kuuawa karibu na nyumbani kwake mjini Mogadishu.
Osman Jama Dirah, ambaye alisimamia mechi za kanda na kimataifa, aliuawa akiondoka msikitini kurejea kwake nyumbani katika mtaa wa Wardhigley.
Taarifa zinasema wanaume wawili waliokuwa na bastola walimfatulia risasi mara kadha.
Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Somalia Anas Ali Mohamud amenukuliwa akisema aliwaona washambuliaji wakiondoka eneo la mauaji.
Anasema maafisa wa usalama walifika eneo hilo baadaye lakini kufikia sasa hawajafanikiwa kuwakamata wahusika.
Mwandishi wa BBC Somali Ahmed Adan anasema kuuawa kwa Osman Jama Dirah ni pigo kubwa sio tu kwa tasnia ya soka nchini Somalia bali kwa sekta yote ya michezo nchini humo.
Alikuwa miongoni mwa marefa maarufu zaidi nchini humo tangu kusambaratika kwa serikali kuu miaka 27 iliyopita.
Dirah alifahamika kama mwamuzi bora zaidi na alihudumu katika kamati ya waamuzi katika Shirikisho la Soka la Somalia.
Alisimamia mechi za kanda na kimataifa na alihduumu kama mwamuzi kwa zaidi ya miaka 25.
Alianza kushiriki katika kandanda mwaka 1979, kama mlinda lango wa timu ya Galgadud, na baadaye akajiunga na timu ya taifa kama mlinda lango.
Mwaka 1997, aliteuliwa kuwa mwamuzi na FIFA nchini Somalia.
Sababu ya kuuawa kwake bado haijabainika, na kufikia sasa hakuna aliyedai kuhusika.
Kuuawa kwa watu mashuhuri hata hivyo si jambo geni lakini haijulikani ni kwanini afisa wa soka alilengwa.
Mwili wa Dirah utazikwa baadaye leo mjini Mogadishu.

MAKAMU WA RAIS AHUDHURIA MKUTANO WA TROIKA MBILI MJINI PRETORIA,NCHINI AFRIKA KUSINI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassana , leo tarehe 18 Agosti 2017 amehudhuria Mkutano wa Troika Mbili za Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC na Troika ya SADC kwa ajili ya kujadili hali ya Siasa , Ulinzi na Usalama katika Kanda. 
Mkutano huu umejadili zaidi hali ya Siasa nchini Lesotho na namna ya kuisaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo inatarajiwa kufanya Uchaguzi Mkuu. 
Taarifa kamili ya Mkutano huu itawasilishwa leo Jumamosi tarehe 19 Agosti 2017, katika Mkutano wa 37 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC. 
Double Troika inahusisha nchi wanachama Sita ambao kwa sasa ni Swaziland, Tanzania, Afrika Kusini, Angola, Botswana na Msumbiji.



 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kabla ya Mkutano wa Troika Mbili za Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika  SADC na Troika ya SADC kwa ajili ya kujadili hali ya Siasa , Ulinzi na Usalama katika Kanda.
Mkutano huo unafanyika mjini Pretoria, Afrika Kusini. 



 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akijadiliana jambo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kulia) kabla ya Mkutano wa Troika Mbili za Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika  SADC na Troika ya SADC kwa ajili ya kujadili hali ya Siasa , Ulinzi na Usalama katika Kanda.
Mkutano huo unafanyika mjini Pretoria, Afrika Kusini.(Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).



 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasili kwenye ukumbi wa OR Thambo mjini Pretoria,Afrika ya Kusini tayari kuhudhuria Mkutano wa Troika Mbili za Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika  SADC na Troika ya SADC kwa ajili ya kujadili hali ya Siasa , Ulinzi na Usalama katika Kanda

WAFANYAKAZI MUHIMBILI WAPATIWA MAFUNZO YA HUDUMA KWA WATEJA



 Kaimu Mkurugenzi Mkuu Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Makwaia Makani akifungua mafunzo ya Huduma Kwa Wateja yaliofanyika katika hospitali hiyo jana. Kushoto ni mtoa mada, Elizabeth Fupe na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano katika Hospitali hiyo, Neema Mwangomo. Wafanyakazi wametakiwa kutumia lugha nzuri wakati wa kuwasiliana na wagonjwa pamoja na ndugu zao ili kurahisisha utuoaji wa huduma za matibabu.

 Baadhi ya wafanyakazi wakifuatilia mafunzo hayo yaliofanyika katika hospitali hiyo.  


 Baadhi ya wafanyakazi wakifuatilia mafunzo hayo yaliofanyika katika hospitali hiyo.  



Wafanyakazi hao wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupatiwa mafunzo hayo.

RAIS MAGUFULI AMTEUA MHE. JAJI BARKE MBARAKA ABOUD SEHEL KUWA MWENYEKITI WA BARAZA LA USHINDANI



TAARIFA KUTOKA JESHI LA POLISI MKOA WA MWANZA



KWAMBA TAREHE 17.08.2017 MAJIRA YA SAA 11:00HRS ASUBUHI KATIKA ENEO LA UFUKWE WA ZIWA VIKTORIA LIITWALO MURUTANGA ULIOPO KATA YA IRUGWA WILAYA YA UKEREWE MKOA WA MWANZA, MARWA MWITA MIAKA 18, MVUVI NA MKAZI WA NYAMAZARA TARIME, ANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA TUHUMA ZA MAUAJI DHIDI YA MVUVI MWENZAKE AITWAYE ERNEST MAGERO, MIAKA 26, MVUVI NA MKAZI WA KIABAKARI – MARA, YALIYOTOKANA NA KUCHOMWA NA KITU CHENYE NCHA KALI KINACHOZANIWA KUWA NI KISU MAENEO YA SHINGONI NA KUSABABISHA KIFO CHAKE PAPO HAPO, KITENDO AMBACHO NI KOSA LA JINAI.


INADAIWA KUWA TUKIO HILO LA MAUAJI LIMETOKEA BAADA YA KUZUKA KWA UGOMVI KATI YA MAREHEMU NA MTUHUMIWA WA MAUAJI, AMBAPO INASEMEKANA KUWA MAREHEMU ALIKUWA AKIMTUHUMU MTUHUMIWA KUWA ANATABIA YA KUJIPENDEKEZA KWA BOSI WAO ALIYEWAPA MTUMBWI WA KUVULIA SAMAKI. INADIAWA KUWA BAADA YA MTUHUMIWA WA MAUAJI KUAMBIWA KAULI HIYO ALIKASIRIKA NDIPO ALICHUKUA KITU CHENYE NCHA KALI KISHA AKAMCHOMA MAREHEMU MAENEO YA SHINGONI NA KUPELEKEA MAREHEMU KUPOTEZA MAISHA PAPO HAPO.

WANANCHI/ WAVUVI BAADA YA KUONA TUKIO HILO WALITOA TAARIFA KITUO CHA POLISI, AMBAPO ASKARI WALIFANYA UFUATILIAJI WA HARAKA HADI ENEO LA TUKIO NA KUSHIRIKIANA NA WANANCHI NA KUFANIKIWA KUMKAMATA MTUHUMIWA. MTUHUMIWA YUPO KATIKA MAHOJIANO NA JESHI LA POLISI PINDI UCHUNGUZI UKIKAMILIKA ATAFIKISHWA MAHAKAMANI, MWILI WA MAREHEMU UMEHIFADHIWA HOSPITALI YA WILAYA YA UKEREWE KWA AJILI YA UCHUNGUZI, PINDI UCHUNGUZI UKIKAMILIKA UTAKABIDHIWA KWA NDUGU WA MAREHEMU KWA AJILI YA MAZISHI.

KAMANDA WA POLISI MKOA WA MWANZA NAIBU KAMISHINA WA POLISI AHMED MSANGI ANATO WITO KWA WANANCHI WA MKOA WA MWANZA AKIWATAKA KUACHA TABIA YA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI KWANI NI KOSA KISHERIA. AIDHA PIA ANAWAOMBA NDUGU WA MAREHEMU KUWA WATULIVU KATIKA KIPINDI HIKI AMBAPO JESHI LA POLISI LINAENDELEA NA UCHUNGUZI ILI BAADAE MTUHUMIWA AWEZE KUFIKISHWA KWENYE VYOMBO VYA SHERIA.

IMETOLEWA NA;
DCP: AHMED MSANGI

KAMANDA WA POLISI (M) MKOA

BENKI YA FINCA KUBORESHA HUDUMA ZA KIFEDHA KWA WATEJA WAKE


Benki ya Finca imeeleza kutoa huduma kwa wateja wake ambapo mpaka sasa  watanzania wapatao 800,000  wamepata huduma katika matawi  yake yote yaliyo katika Mikoa 24 nchi nzima. Finca inafikisha huduma kwa njia ya Mawakala wanaopatika nchi nzima, pia kutoa huduma hiyo ya kifedha kwa njia ya simu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo Issa Ngwegwe amesema kuwa wanatoa huduma za kifedha zinazowasidia wateja kuweza kutengeneza biashara ambazo zinawapatia kipato.
Ngwegwe amesema kuwa huduma hizo pia zitawasaidia wateja hao kutengeneza ajira kwa Watanzania wengine wasio katika Sekta Binafsi.Pia, ameongeza huduma hizo kuwapatia uwezo wa kujitambua na kuwafikisha katika malengo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Masoko wa Benki, Gershom Mpangala amesema kuwa Benki hiyo ina akaunti inayoitwa Mipango Pay Out inayolenga kwa Wastaafu zaidi ambazo zinaweza kumuingizia Mstaafu huyo Riba kubwa.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Issa Ngwegwe akizungumza na Waandishi wa Habari  kuhusu utaoaji huduma Benki ya FINCA kwa wateja wake kwenye ofisi zake jijini Dar es Salaam leo
Mkuu wa Masoko wa Benki ya Finca, Gershom Mpangala akizungumzia Mipango Pay Out inayolenga kwa Wastaafu zaidi ambazo zinaweza kumuingizia Mstaafu huyo Riba kubwa.

ZIARA YA MAKAMO WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR NCHINI CUBA



Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema mchango wa Cuba katika kuimarisha afya za wananchi wa Bara la Afrika unaimarika kila siku kutokana na misingi imara ya ushirikiano wa karibu na kiundugu ulioanzishwa na muasisi wa taifa hilo Fidel Castro Balozi Seif ameyasema haya Leo mjini Havana wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Afya ya umma mheshimiwa Roberto Morales Ojeda. 
 Amesema kutokana na uhusiano mzuri na kiundugu uliopo kati ya Tanzania na Cuba, Zanzibar imeweza kutoa madaktari wasiopungua 50 ambao wamefundishwa na madaktari kutoka Cuba. Amesema kupatikana kwa madaktari hao kumeiweka Zanzibar nafasi nzuri ya kufikia malengo yake ya kuwa na kituo cha afya chenye daktari kwa kila kilometa nne. 
 Balozi Seif ameiomba Serikali ya Cuba kuipatia Zanzibar madaktari 3 mabigwa katika fani ya figo (Nephrologist); masikio, pua na koo (ENT) na mionzi (Radiologist). Aidha ameitaka Cuba kuwapatia vijana waliomaliza mafunzo ya udaktari chini ya madaktari wa Cuba nafasi za mafunzo ya juu katika fani mbali mbali. 
 Naye Waziri wa Afya ya umma mheshimiwa Roberto ameeleza kuridhishwa kwake na uhusiano ulipo wa sekta ya afya kati ya Zanzibar na Cuba. Amesema Cuba iko tayari kuwapatia mafunzo ya juu vijana wa Zanzibar kwa gharama nafuu na kuitaka Wizara ya Afya ya Zanzibar kupeleka maombi yake mapema iwezekanavyo.
Kwa upande wa wataalamu wa Afya Waziri wa Cuba Mheshimiwa Roberto amesema Serikali yake itarifikia ombi hilo na itatoa jawabu hivi karibuni

VETA NA UJERUMANI WATILIANA SAINI

VETA NA UJERUMANI WATILIANA SAINI MAKUBALIANO YA MAFUNZO YA UWANAGENZI KATIKA TEKNOLOJIA YA UFUNDI WA ZANA ZA KILIMO NA MITAMBO YA UJENZI

Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii.
Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imetiliana saini makubaliano yenye thamani ya Euro 900,000 (zaidi ya shilingi bilioni 2.3) na Chemba ya Baraza la Ufundi Stadi ya Ujerumani (WHKT) kwa ajili ya mafunzo ya uwanagenzi yenye lengo la kuimarisha ufundi wa zana za kilimo na teknolojia ya mitambo ya ujenzi.
Makubaliano hayo yalitiwa saini na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Moshi Kabengwe kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk Leonard Akwilapo na Ujerumani aliyetia saini ni ni Mtendaji Mkuu wa Ujerumani , Reiner Nolte na kushuhudiwa na Barozi wa Ujerumani nchini, Dk. Detlef Waechter, Mwenyekiti wa Board ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi,Peter Maduki, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dk. Bwire Ndazi na Maafisa wengine waandamizi wengine wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, VETA na Ujerumani.
“ujuzi wa mafundi na wakulima utaboreshwa kupitia kozi zitakazotolewa na VETA kwa mfumo wa uwanagenzi. Kozi hizo ni pamoja ufundi zana za kilimo, ufundi mitambo ya ujenzi na mafunzo ya vitendo katika teknolojia ya kupunguza upotevu wa mavuno ya mazao ya kilimo katika maeneo yatakayoainishwa,” inaeleza sehemu ya waraka wa makubaliano.
Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo, Balozi wa Ujerumani nchini Dk. Detlef Waechter alisema anatarajia kuwa ushirikiano katika mradi huo utawasaidia kwa kiasi kikubwa Watanzania wengi, hususani vijana katika kupata ujuzi wa kuutumia kwenye kuongeza tija kwenye kilimo nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimani watu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Moshi Kabengwe aliishukuru serikali ya Ujerumani kwa msaada na ushirikiano na kusema kuwa utawasaidia vijana wengi kuajirika na kuwa na ujuzi wa kutumia teknolojia za kisasa katika kilimo.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk. Bwire Ndazi aliishukuru serikali ya Ujerumani kwa kuendelea kuiamini VETA na kuendeleza ushirikiano nayo katika utoaji mafunzo kwa mfumo wa uwanagenzi. Amesema, ushirikiano katika miradi ya nyuma umeendelea kuwanufaisha vijana wengi kupata ujuzi na kuweza kuajirika kwa urahisi.

Mafunzo ya uwanagenzi uendeshwa kwa mfumo wa ngwe za mzunguko kati ya chuo cha ufundi stadi na sehemu ya kazi ambapo mwanafunzi hupata mafunzo ya ujuzi kwenye karakana za chuo na uzoefu wa hali halisi mahala pa kazi, hivyo kumwongezea umahiri pamoja na maarifa zaidi na utamaduni wa ya mazingira ya kazi husika.



Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Moshi Kabengwe akisaini makubaliano ya uendelezaji wa mafunzo ya uwanagenzi kulia ni ni Mtendaji Mkuu wa Ujerumani , Reiner Nolte na wanaoshuhudia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk. Bwire na Balozi wa Ujerumani nchini, Dk. Detlef Waechter.


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk. Bwire Ndazi akizungumza katika mkutano wa kutiliana saini ya makubaliano kati ya Ujerumani na VETA kwa ajili mafunzo ya uwanagenzi yenye lengo la kuimarisha ufundi wa zana za kilimo na teknolojia ya mitambo ya ujenzi.
Picha ya Pamoja Balozi wa Dk. Detlef Waechter akipeana mkono Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimani watu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloji, Moshi Kabengwe pamoja na watendaji wa VETA Wawakilishi Ujerumani baada ya kusaini makubaliano ya kuendeleza wanagezi.