Monday, June 26

DKT SHEIN AONGOZA BARAZA LA EIDD EL FITRI MJINI UNGUJA,ZANZIBAR


 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Wananchi mbali mbali baada ya Swala ya Eidd Fitri iliyoswaliwa leo katika uwanja wa Maisara Suleiman Mjini Unguja katika kusherekekea kumalizika kwa Mfungo wa MweziMtukufu wa Ramadhan.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein akisalimiana na Wananchi mbali mbali baada ya Swala ya ElIdd Fitri iliyoswaliwa leo katika uwanja wa Maisara Suleiman Mjini Unguja katika kusherekekea kumalizika kwa Mfungo wa MweziMtukufu wa Ramadhan,[Picha na Ikulu.] 26/06/2017.
 Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga   alipokuwa akitoa khutba baada ya Swala ya El Idd elfitri iliyoswaliwa katika Uwanja wa Maisara Suleiman Mjini Unguja katika kusherehekea Sikukuu ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan aliyohudhuriwa na Viongozi  wa Kitaifa na Waislamu mbali mbali wa Mkoa wa Mjini Magharibi  leo.
 Waislamu wanawake wakiwa katika Swala ya Eid  el fitri iliyoongozwa na Sheikh Fadhil Soraga katika Uwanja wa Maisara Suleiman Mjni Unguja leo katika Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo  Viongozi  wa Kitaifa na Waislamu mbali mbali walihudhuria [Picha na Ikulu.] 26/06/2017.
 Baadhi ya waislamu wanaume waliohudhuria katika swala ya EId elfitri wakimsikiliza  Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar  Sheikh Fadhil Soraga aklipokuwa akitoa khutba ya Swala ya El Idd elfitri iliyoswaliwa katika Uwanja wa Maisara Suleiman Mjini Unguja katika kusherehekea Sikukuu ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan,[Picha na Ikulu.] 26/06/2017.

MAMBO YA KUSTAAJIBISHA AMBAYO YANAPATIKANA TANZANIA


Na Jumia Travel Tanzania
Inastaajabisha kuona watu wa mataifa ya nje wanajua vitu vingi zaidi vinavyopatikana Tanzania kuliko watanzania wenyewe. Sijui ni ile hulka ya kutopenda kufuatilia mambo au ni dhana kwamba waache wageni waje kushangaa maana hivyo vitu vitaendelea kuwepo tu.

Nchi yetu imebarikiwa na inaendelea kubarikiwa kugunduliwa kwa mambo mengi zaidi ya kustaajabisha ambayo hayapatikani kwingineko duniani. Jumia Travel ingependa kukufumbua macho kwamba yafuatayo ni baadhi tu ya mambo yanayopatikana na unaweza kuyashuhudia ukiwa nchini Tanzania.


Mti mrefu zaidi barani Afrika. Hivi karibuni mtafiti kutokea Chuo Kikuu cha Byreuth cha nchini Ujerumani, Dkt. Andreas Hemp baada ya utafiti wa takribani miaka 20 amethibitisha kuwa Tanzania ina mti mrefu zaidi kuliko yote barani Afrika ukiwa na urefu wa mita 81.5. Mti huo kwa jina la kitaalamu unajulikana kama ‘Entandrophragmaexcelsum’, ni aina adimu sana ya miti na inaweza kuwa na umri wa zaidi ya miaka 600. Ili kuweza kuuona mti huo unaopatikana katika safu ya misitu ya Mlima Kilimanjaro na kuwa kivutio kikubwa kwa watalii hivi sasa, itakupasa utembee umbali wa masaa 2.30 mpaka kutokea kijiji cha Tema ili kuufikia.

Twiga mweupe aonekana kwa mara ya kwanza.  kubisha kwamba hiko kitu hakiwezekani lakini ndio maajabu ya Mungu hayo, twiga mweupe ameonekana Tanzania. Takribani mwaka mmoja uliopita, mwanzilishi na mwanasayansi katika Taasisi ya Misitu Asilia katika hifadhi ya taifa ya Tarangire inayopatikana mkoani Manyara, Dkt. Derek Lee alimuona twiga mwenye rangi nyeupe. Twiga huyo ambaye alikuwa na umri wa miezi 15 amepewa jina la ‘OMO,’ rangi yake inaonekana kama vile imechubuliwa tofauti na rangi asilia ya twiga tunaowajua. Mtafiti huyo amesema kuwa twiga huyo anasumbuliwa na ‘leucism,’ ni hali inayosababisha kupotea kwa baadhi ya rangi. Licha ya utofauti huo na wenzake lakini bado mnyama huyo anajichanganya na wengine na wenzie kutojali utofauti huo kabisa.   
 
Asilimia 30% ya ardhi ya Tanzania ni hifadhi za wanyama pori. Kama ulikuwa haujui basi ni kwamba nchi ya Tanzania sehemu ya asilimia 30 ya ardhi yake ni hifadhi za wanyama pori wa aina mbalimbali duniani. Tanzania inazo hifadhi za taifa 16 ambazo zinasimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ambapo kwa ujumla wake zina ukubwa wa kilometa za mraba takribani 42,000. Kwa mfano, hifadhi ya taifa ya mbuga ya Serengeti ni mojawapo ya mbuga maarufu na inayopendwa zaidi duniani, ni makazi ya aina mbalimbali za wanyama zaidi ya milioni moja. Pia imetangazwa kuwa ni Eneo la Urithi wa Dunia na kutajwa mojawapo ya sehemu ya Maajabu Saba ya Dunia.
 
Takribani wanyama milioni 2 hushiriki tukio la kuhama linalotokea kila mwaka mbuga ya Serengeti. Kila mwaka watalii hushuhudia tukio la kipekee la uhamaji wa makundi ya wanyama wa aina ya pundamilia na nyumbu zaidi ya milioni 1.5. Tukio hilo hutokea kati ya Kusini mwa bonde la mbuga ya Serengeti nchini Tanzania kuelekea eneo la Kaskazini mwa mbuga ya Masai Mara iliyopo Kenya. Lengo kubwa la tukio hilo ni katika harakati za kutafuta malisho mazuri kwa wanyama hao ambalo hutukia mnamo miezi ya Mei mpaka Desemba ingawa muda huwa unaweza kubadilika. Sehemu inayosisimua zaidi ni pale wanyama hao wanakatisha mto Mara kuuvuka kuelekea Masai Mara, wanyama hao kwa makundi na ujasiri mkubwa huvuka licha ya kuwa na mamba wakali.   
 
Mbuyu unaweza kuishi mpaka miaka 1,000. Mibuyu ni miti mikubwa na inayovutia zaidi, hapa nchini Tanzania unaweza kuiona vizuri zaidi ukitembelea hifadhi ya taifa ya Tarangire. Kama ulikuwa haufahamu ni kwamba baadhi ya aina ya miti ya mibuyu huweza kuishi kwa takribani miaka 1,000 au zaidi. Inasemekana mbuyu mkongwe zaidi unapatikana nchini Afrika ya Kusini ni unaaminika kuwa na miaka takribani 6,000.  
 
Uwepo wa vitu hivyo Tanzania ni uthibitisho wa namna nchi hii ilivyobarikiwa na vivutio mbalimbali ambavyo watu wengi hawavifahamu bado. Kwa hayo machache Jumia Travel inaamini utakuwa umejifunza na kupata shauku ya kutembelea maeneo hayo pamoja na kukuongezea ari ya kujifunza mengineyo zaidi.

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AHUTUBIA BARAZA LA EID KITAIFA MKOANI KILIMANJARO

*Ahimiza nyumba za ibada zisaidie vita ya dawa za kulevya 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepiga marufuku usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi kuanzia leo. “Kuanzia leo, ni marufuku kwa mtu yoyote kusafirisha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi bila ya vibali. Serikali inahamasisha uwekezaji kwenye ujenzi wa viwanda nchini. Kama tutatoa vibali, ni lazima mtu alazimike kusaga nafaka ili kutoa ajira nchini,” amesema. 

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatatu, Juni 26, 2017) wakati akitoa nasaha kwenye Baraza la Eid lililofanyika kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro mara baada ya kuswali sala ya Eid. 

“Jana nimeona kwenye televisheni taarifa kuhusu malori 10 yaliyokamatwa Tarakea yakiwa na mahindi tayari kuvushwa mpaka. Mheshimiwa RC akasema chakula hicho ni lazima yarudishwe kwa ajili ya usagaji.”

“Mimi nasema kuanzia leo, yeyote atakayekamatwa akitorosha chakula kwenda nje ya nchi, chakula hicho kitataifishwa na kupelekwa ghala la Taifa na gari lake tutalitaifisha na litaishia Jeshi la Polisi. Tunafanya hayo kwa lengo la kuwalinda Watanzania tusikumbwe na baa la njaa.” 

Akitoa tahadhari kuhusu uuzwaji wa chakula nje ya nchi, Waziri Mkuu amesema kumekuwa na wimbi kubwa la usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi bila kibali. “Hilo ni kosa kubwa kwa sababu litasababisha nchi yetu kupata baa la njaa huko mbele,” amesema.

Amesema mipaka ya Tarakea, Holili, Mwanga, Horohoro, Siha, Namanga na Sirari imekuwa inapitisha kiasi kikubwa cha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi jambo ambalo ni hatari sana. “Hii ni kwa sababu chakula cha ndani hakitoshelezi mahitaji. Kwa sababu nchi zote za jirani hazina chakula cha kutosha. Tusipokuwa makini, tutabaki tunalia njaa.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi wafanyabiashara wa ndani, wachukue mahindi kutoka maeneo yenye mavuno mengi na kuyapeleka kwenye sehemu zenye mavuno kidogo. “Watanzania tushirikiane, kama ni biashara tutoe huku kwenye mavuno mengi na tuyapeleke Shinyanga na Geita ambako wanayahitaji au tukanunue Sumbawanga na kuyapeleka kwenye mikoa mingine yenye upungufu,” alisisitiza. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa dini waisadie Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kupitia kwenye nyumba za ibada. “Naomba tuendelee kushirikiana kupambana na janga hili la dawa za kulevya kwa ustawi wa nchi yetu. Naamini viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa katika mapambano haya, kwa kuwafunda vijana wetu kuishi katika maadili ya kidini na kutojiingiza kwenye janga hilo.”

Alisema Serikali kwa upande wake itaendeleza mapambano hayo bila ajizi wala mzaha. “Tunaomba wananchi wote watuunge mkono kwa kutoa taarifa sahihi za wanaojihusisha na uzalishaji, utengenezaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya pindi tu wanapowabaini.”

Wakati huo huo, akitoa tafsiri ya Qur’aan tukufu kwenye Baraza la Eid, Sheikh wa Mkoa wa Arusha, Sheikh Shaaban Juma alisema kila nguzo katika Uislamu inapaswa kufuatwa na kwamba mtu akiharibu nguzo moja tu anakuwa ameharibu nguzo zote tano.

Alisema siku ya kiyama, watatokea watu wenye thawabu kama milima ya Usambara ama Upareni na akawataka Waislamu wote nchini wadumu katika kutenda mema ili wapate thawabu.

Mapema, akitoa khutba katika swala ya Eid el Fitr iliyoswaliwa kwenye msikiti huohuo wa Masjid Riadha, Sheikh Mlewa Shaban alisema sikukuu ya Eid ni siku ya kujiepusha na madhambi kama ulevi, kamari na lugha chafu, bali aliwataka waumini wote waitumie siku hiyo kuwapa furaha maskini, yatima na wajane.

“Mtu asiseme mwezi wa Ramadhan umepita, sasa narudia mambo yangu ya zamani. Adhabu za Mwenyezi Mungu hazina mipaka na wale waliotulizana watapata thawabu yao, kumbukeni neema na Mwenyezi Mungu na mcheni Mwenyezi Mungu.”

“Kitu tunachopaswa kufanya kila wakati ni kumcha Mwenyezi Mungu. Lazima tupendane, tuondoe tofauti zetu na tuujenge Uislam. Hatuwezi kuujenga uislam kama hatupendani. Lazima tuilinde ibada yetu kwa sababu hatuna garantii, ni lini tutaondoka,” alisema.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally; Wajumbe wa Baraza la Ulamaa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe; Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mama Anna Mghwira; IGP Mstaafu, Bw. Said Mwema; Mbunge wa Moshi Mjini, Bw. Jaffary Michael; Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa nasaha kwa waumini (hawapo pichani) waliohudhuria Swala ya Eid el Fitr na Baraza la Eid Kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waumini wa dini ya Kiislamu waliohudhuria Swala ya Eid el Fitr na Baraza la Eid Kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akitoa nasaha za Eid, tarehe 26 Juni, 2017. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiteta jambo na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally wakati wa stafutahi kwenye Ikulu ndogo ya Moshi, mara baada ya Swala ya Eid el Fitr na Baraza la Eid Kitaifa mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiagana na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally mara baada ya stafutahi kwenye Ikulu ndogo ya Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisaini kitabu cha maombolezo, nyumbani kwa marehemu Dk. Philemon Ndesamburo, eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa pole na neno la faraja kwa wanafamilia, nyumbani kwa marehemu Dk. Philemon Ndesamburo, eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro tarehe 26 Juni, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimpa pole mjane wa marehemu, mama Ndehorio P. Ndesamburo alipofika nyumbani kwao eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro kuwafariji kutokana na msiba wa Dk. Philemon Ndesamburo, leo tarehe 26 Juni, 2017. 
Kaka wa marerehemu Dk. Philemon Ndesamburo, Bw. Zablon Sindato Kihwelu akimshukuru Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyefika nyumbani kwao eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro kuwafariji kutokana na msiba wa Dk. Philemon Ndesamburo, leo tarehe 26 Juni, 2017.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bibi Anna Mgwira (wa tatu kushoto), mjane wa marehemu na Kaka wa marehemu wakiomba dua na wanafamilia kwenye kaburi la Dk. Philemon Ndesamburo, aliyezikwa nyumbani kwake eneo la Kiboriloni, Moshi, mkoani Kilimanjaro. Wa kwanza kulia ni mtoto wa marehemu.

RAIS DKT.MAGUFULI AONGOZA KIKAO CHA BARAZA LA MAWAZIRI IKULU JIJINI DAR ES SALAAM


Picha mbalimbali zikimuonesha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza kikao cha Baraza la Mawaziri leo tarehe 26/06/2017 Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU

Lowassa aitwa ofisini kwa DCI

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ameitwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Boaz.
Lowassa akizungumza na Mwananchi leo (Jumatatu), amesema ameitwa kwa DCI lakini hajui anachoitiwa.
Hata hivyo, amesema anahisi ni kauli yake kuhusu mashehe wa kikundi cha Uamsho cha Zanzibar wanaoshtakiwa kwa tuhuma ya ugaidi.
 “Ni kweli nimetakiwa niripoti kesho saa 4:00 asubuhi katika ofisi ya DCI. Sijui wananiitia nini, lakini nahisi ni kuhusu nilichosema kuhusu mashehe wa Uamsho,” amesema Lowassa.
Jana katika taarifa kwa vyombo vya habari, Lowassa alikaririwa akimtaka Rais John Magufuli kuwaachia huru mashehe hao wanaoshikiliwa kwa zaidi ya miaka minne sasa.
Taarifa hiyo ilisema Lowassa alitoa ombi hilo alipozungumza katika futari iliyoandaliwa na mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara.

Boti yazama, sita wafariki dunia

Watu sita wamefariki dunia na wengine 16 hawajulikani walipo baada ya boti ya abiria kuzama jana, Jumapili katika mji wa Kaskazini Magharibi mwa nchini ya Colombia.
Polisi nchini humo wamethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa juhudi za kuwatafuta abiria wengine waliokuwa kwenye boti hiyo zinaendelea.
Kwenye uokoaji huo boti ndogo, helikopta zilitumika kuhakikisha majeruhi wanaokolewa haraka. Zaidi ya watu 20 wamekimbizwa hospitalini katika mji wa Guatapé.
Imeelezwa kuwa boti hiyo iliyozama muda mfupi baada ya kung’oa nanga ilikuwa imebeba abiria 150.
Hata hivyo, kiongozi wa idara ya zimamoto waliokuwa wanafanya harakati za uokoaji, Luis Morales amesema chanzo cha ajali hiyo bado hakifahamika.
"Hatujafahamu kama kiini cha ajali hiyo ni tatizo ya kimitambo, ubeba watu kupita kiasi au mawimbi ziwani,"amesema.

Sunday, June 25

Polisi Dar mguu sawa sikukuu ya Eid


JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewahakikishia  hali ya usalama na amani wakazi, wananchi wa jiji la Dar es Salaam katika kipindi chote cha sikukuu ya Eid inayotarajiwa kuwa Jumatatu.
Lucas Mkondya, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam amesema kuwa askari wa jeshi hilo wamejipanga vyema kuhakikisha wananchi wa jiji la Dar es Salaam wanasherehekea sikukuu hiyo kwa kwa amani na utulivu pasipo bugudha za wahalifu.
“Uzoefu unaonesha kuwa, mara nying kipindi cha sikukuu kama hii watu wenye nia ovu hujiandaa kufanya vitendo vya kihalifu, ndiyo maana tumejipanga kukabiliana na aina yoyote  ya uhalifu kwa kuzuia au kuwatia nguvuni wote watakaoshiriki vitendo vya uvunjifu wa sheria,” amesema.
Kamanda Mkondya amesema polisi watafanya doria za masaa 24 katika maeneo yote ya jiji la Dar es Salaam hasa maeneo yenye korofi na yenye rekodi au viashiria vya uhalifu.
“Pia kutakuwa na doria katika maeneo ya misikiti, kumbi za starehe na maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu na tutatumia taarifa za kiintelijensia ili kuwabaini wahalifu wanaopanga kufanya matukio ya uhalifu.
“Tutaimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuhakikisha maeneo yote hatarishi yanadhibitiwa,” amesema Kamanda Mkondya.

Hizi ni mbinu za ubinafsishaji




Biashara imara huanzishwa kwa ufanya upembuzi yakinifu ambao hutoa fursa kutambua mambo mengi kuhusu biashara yenyewe na mazingira ambayo biashara hiyo itawekezwa.
Biashara kubwa za kampuni hutumia fedha nyingi kufanya maandalizi ya msingi kabla ya kujiridhisha kama biashara hiyo inaweza kufanyika na kuleta matokeo chanya kwa wamiliki na wadau wengine.
Hili linaweza kufanyika kwa biashara aina zote na kiwango chochote cha mtaji ili kuziweka biashara katika maeneo salama. Uwekezaji wa biashara zote ni muhimu kuangalia mambo yafuatayo,
Upatikanaji wa malighafi au bidhaa za msingi za Biashara husika, ni muhimu sana kufungua na kuanzisha biashara eneo ambalo kutakuwa na urahisi wa upatikanaji malighafi muhimu kwa uzalishaji wa bidhaa kuu na huduma zinazotolewa na biashara husika.
Ili uimudu biashara ni lazima kujihakikishia upatikanaji wa malighafi au mizigo unayochukua kuleta kuuza iwe ndani au nje ya nchi ni muhimu kuwa na uhakika wa upatikanaji wa huduma na bidhaa zako.
Kuwafahamu wapinzani wako kwenye biashara unayokwenda kuwekeza, ili kuweza kuipata nafasi yako kwenye soko la ushindani. Wafahamu watu wanaofanya biashara kama yako au nyingine zinazofanana na yako.
Kulifahamu soko la bidhaa na mahitaji ya wateja na wadau wako, ubunifu wa bidhaa zinazokwenda na wakati ni jambo la muhimu sana kwasababu sio kila bidhaa yako inafaa kutumika kwa watu wote.
Ni muhimu kulifahamu soko lako na ulichambue vizuri ili uweze kubuni bidhaa na huduma zinazokwenda na mahitaji yao. Mfano wa kampuni ya simu kwa ubunifu wao mzuri wa vifurushi vingi kama vile vya chuo ambako huko kuna wanafunzi wengi na wanatumia sana simu na vifaa vingine kufanya mawasiliano ya mtandao na kawaida, huu ni mfano wa biashara inayotambua soko lake na mahitaji ya wadau kutokana na mazingira.
Gharama za kuendesha Biashara yako, kuna wakati unaweza kuwa na wazo zuri sana la biashara lakini katika kufanya Uchunguzi na upembuzi ukagundua kuwa gharama za uendeshaji wa biashara yako zitakuwa juu na kukufanya upate hasara au kuendesha biashara isiyokuwa na tabia ya kupanuka ni vizuri kufikiria mara mbili kuhusu biashara hiyo.
Utaratibu wa ulipaji kodi na gharama nyingine, ni muhimu na lazima kulipa kodi kwa biashara yoyote ila kama biashara yako unaona inaingia kukupa gharama kubwa na mazingira yasiyokuwa rafiki kwenye ulipaji kodi ni vizuri kujitathimini na kuangalia upya mfumo wa kuingiza au kuendesha biashara yako.
Hali ya eneo lako la biashara. Moja kati ya vitu vya muhimu sana kwenye biashara inayoanza au ile inayoendelea ni kujiuliza kuhusu eneo ambalo biashara yako unahitajika kuiweka.
Biashara nzuri inategemea sana eneo ambalo ofisi na majengo yake yatakuwepo kama yatakuwa katika maeneo sahihi kwa watu na wadau wake kufika na kupata huduma basi biashara hii itakuwa inafanya kazi nzuri lakini ukichagua eneo baya na ambalo haliendani na aina ya biashara yako unaweza kujikuta unapunguza nguvu ya biashara yako kufanya vizuri na kukupa matokeo mazuri kwenye upande wa faida kifedha.
Mazingatio haya ni muhimu kwa biashara za aina zote kuanzia viwanda, biashara za kawaida za kuuza na kununua tulizozoea au sekta za fedha huwezi kuifanya biashara yenye mafanikio bila kuzingatia vitu hivi muhimu ili kuifanya biashara yako iwe na nguvu, mbinu hizi zinatumika kwa biashara mpya na zile zilizokuwepo.
Lakini pia katika hayo machache swala la Amani ya eneo la biashara ni muhimu kwenye kutengeneza biashara yenye nguvu.

TANTRADE YAWAKARIBISHA KATIKA MAONYESHO YA 41 YA BIASHAYA YA KIMATAIFA JIJINI DAR


Mwigulu apigilia msumari agizo la JPM

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amezionya taasisi zisizo za Serikali zinazohamasisha kudai haki ya mtoto anayepata mimba kurejeshwa shuleni kuacha mara moja na zikiendelea atazifutia usajili.
Mwigulu ameyasema hayo leo, Jumapili wakati alipomwakilisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Parokia ya Kisasa Mjini hapa.
Amesema Serikali haitaomba ushauri wala maoni kwa sababu maelezo yaliyotolewa na Rais, John Magufuli ni maagizo ya Serikali.
Waziri huyo amesema Serikali imetoa haki ya kila mtoto kupata elimu kwa kuifanya kuwa bure kwa hiyo atakayeikosa asitafute kisingizio.
"Rais ametoa haki hiyo sasa hivi elimu ni bure, halipi tuition wala nini, atakayeamua kuachana na haki hiyo asitafute kisingizio, asipeleke lawama kwa Serikali, "amesema.

Saturday, June 24

Mtoto atunukiwa zawadi ya kusafiri kwa ndege maisha yake yote


Shirika la ndege la binafsi nchini India limemtunuku safari za bure mtoto aliyezaliwa ndani ya ndege moja ya shirika hilo iliyokuwa safarini kutoka Saudi Arabia kuelekea India.
Mhudumu mmoja wa ndege, ambaye alikuwa amepata mafunzo ya uuguzi alimsaidia mama kujifungua mtoto wakati ndege hiyo ikiwa umbali wa futi 35,000 angani.
 Kutokana na tukio hilo, shirika hilo lilimpa zawadi ya kudumu maishani, ambayo itakuwa ni kusafiri bure kwa ndege ya shirika hilo katika maisha yake yote.
Mama na mtoto wake walipelekwa hospitalini baada ya ndege hiyo aina ya Boeng 737 kutua katika mji wa magharibi ya Mumbai.
Shirika hilo liliiambia BBC kuwa mama na mtoto wake walikuwa katika afya nzuri.
Kampuni iliwashukuru wahudumu kwa kumsadia mama kujifungua salama.
Shirika hilo lilisema kuwa hiyo ni mara ya kwanza mtoto kuzaliwa kwenye ndege zake.
Tukio kama hilo lilitokea nchini Uturuki ambapo mtoto wa kike alizaliwa katika ndege ya Shirika la Turkey Airline, Aprili mwaka huu.

Sirro aibukia Moshi mauaji ya Kibiti


Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro amesema mauaji ya polisi, viongozi na raia katika maeneo ya Kibiti, Rufiji na Ikwiriri ni ya muda na kusisitiza majibu yake yako mbioni kupatikana.
Sirro ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi) katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi (MPA), wakati wa kufunga mafunzo ya upandishaji vyeo kwa maofisa na askari 222 wa Jeshi la Uhamiaji nchini.
Kauli ya Sirro imekuja huku kukiwa na mfululizo wa mauaji ya polisi na raia katika maeneo hayo ambapo zaidi ya watu 35 wameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana wakiwamo polisi 13.
Hadi sasa, licha ya polisi kufanya operesheni kubwa katika maeneo hayo, bado halijaweza kubaini chanzo cha mauaji hayo na kwa nini wanawalenga polisi na baadhi ya watu na nani wanayatekeleza.
Tukio la hivi karibuni kabisa lililotokea Jumatano iliyopita, ambapo watu wasiojulikana waliwashambulia kwa risasi na kuwaua polisi wawili wa kikosi cha usalama barabarani huko Kibiti.
Akizungumza katika sherehe za kuhitimu mafunzo kwa maofisa na askari hao 222 wa Jeshi la Uhamiaji, Sirro amesema japokuwa nchi ni salama, lakini inakabiliwa na kitisho cha usalama eneo hilo.
“Tuna shida Kibiti Ikwiriri lakini wanasema sisi ni wengi wao ni wachache. Tusikubali hata siku moja makabila yetu, madhehebu yetu, majimbo yetu yatugawanyishe,” amesema Sirro na kuongeza;-.
“Umoja wetu ndio nguvu yetu. Suala la Kibiti ni la muda mfupi. Tunakwenda na tutapata majibu. Hatutakubali kikundi cha watu wachache wafanye Kibiti, Ikwiriri, Rufiji yasikalike,”.
Akizungumzia changamoto zinazolikabili Jeshi la Uhamiaji, Sirro aliyekuwa mgeni rasmi amesema moja ya changamoto kubwa ni uingiaji wa wahamiaji haramu wanaopitia njia zisizo rasmi kuingia nchini.
“Hili litawezekana kwa kuimarisha intelijensia. Mnapopanda vyeo sio mfurahie tu kupanda cheo mjue majukumu yanaongezeka pia. Idadi ya mnaoenda kuwaongoza sasa itaongezeka,”amesema Sirro.
“Kazi yenu Uhamiaji na sisi polisi hazitofautiani sana na mara nyingi tumekuwa tukifanya kazi za operesheni pamoja. Changamoto tunayokutana nayo ni usimamizi wa kazi”alisisitiza na kuongeza;-
“Askari anakosea huchukui hatua. Konstebo anafikia mahali anamtuma Koplo amletee soda na anakimbia anakwenda kumletea soda. Mnaona ni sawa hii?”alihoji na kujibiwa “Hapana”.
“Heshima yetu sisi askari ni kutokuwa waoga na unakuwa sio muoga kwa sababu kazi unaifahamu, unakuwa sio muoga kwa sababu unatii sheria na unasimamia sheria na hubabaiki,”amesema.
“Ninawaelekeza suala la uoga, suala la ulegelege katika awamu hii tusiipe nafasi,”ameongeza kusema na kusisitiza maofisa hao kufanya kazi kwa weledi pasipo kuwasumbua au kuwazungusha wananchi.
Kamishina Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji, Dk Anna Makakala, amesema mafunzo hayo ni ya kwanza katika historia ya jeshi lake baada ya Jeshi hilo kufanya maboresho ya kimuundo na sheria.
“Jeshi la Uhamiaji limefanya maboresho yakiwamo ya kimuundo na sheria ili kuliingiza Jeshi la Uhamiaji katika tume ya polisi na Magereza. Hatua hii imechangia kuwepo kwa mabadiliko,”amesema.
“Uhamiaji lina askari na watumishi wasiozidi 3,000, hawatoshi kutokana na ongezeko la majukumu ya uhamiaji. Ili kufanya kazi kwa ufanisi linalihitaji kuwa na askari wasiopungua 10,000,”amesisitiza.
Kamishina Jenerali hiyo amesema Taifa kwa sasa linakabiliwa na changamoto ya wahamiaji haramu wanaoingia kupitia njia zisizo rasmi, lakini akasema wanapata ushirikiano mkubwa toka polisi.

MAVUNDE ATOA RAI KWA BENKI NA TAASISI ZA FEDHA KUSOGEZA HUDUMA ZAO VIJIJINI ILI KUWAHUDUMIA WAKULIMA


 Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Mh Anthony Peter Mavunde, akizungumza wakati wa uzinduzi wa benki ya Microfinance Bank PLC katika kata ya Mngeta,Wilaya ya Kilombero,Mkoani Morogoro.
 Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Mh Anthony Peter Mavunde, wa kushoto  akiwa katika uzinduzi wa benki ya Microfinance Bank PLC katika kata ya Mngeta,Wilaya ya Kilombero,Mkoani Morogoro.


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu Mh Anthony Peter Mavunde amezitaka benki na Taasisi za Fedha kusogeza huduma zao katika maeneo ya Vijijini ili kuwafikia watanzania wengi ambao wanajihusisha na shughuli za uzalishaji mali kama vile kilimo na Ufugaji.


Mavunde alitoa rai hiyo jana wakati wa uzinduzi wa benki ya Yetu Microfinance Bank PLC katika kata ya Mngeta,Wilaya ya Kilombero,Mkoani Morogoro kwa kuzitaka Taasisi hizo za fedha zisaidie katika utoaji wa mikopo nafuu kwa wakulima ikiwemo mikopo ya fedha taslimu,mikopo ya zana za kilimo na mashine za uchakataji wa mazao kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali kupitia uchumi wa Viwanda.


Mavunde amewataka wananchi wa kata ya Mngeta kuitumia hiyo fursa kuboresha kilimo chao kwa kulima kwa njia za kisasa na pia kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya uchakataji mazao.


Aidha,Mkurugenzi Mtendaji wa Benki Bwana Millinga alimuelezea Naibu waziri kwamba wameshaanza mchakato wa kuwakopesha wakulima mashine za uchakataji wa mazao na watatanua wigo zaidi ili kuwafikia wakulima wengi zaidi.

MUFTI MKUU WA TANZANIA AWASILI MKOANI KILIMANJARO KWA AJILI YA SWALA YA EID EL FITRI


Mufti Mkuu wa Tanzania,Sheakh Aboubakary Zubeiry Ali akiwa na waliompokea katika lango la kutokea eneo la watu mashuhuri katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) alipowasili jana mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya Swala ya Idd El- Fitr inayotaraji kufanika kitaifa mkoani humo.
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali akitia aini katika kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kilimajaro (KIA).
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali  akiteta jambo na Shekh Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro mara baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Gari maalumu kwa ajili ya Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali 
Msafara wa Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali   ukitoka katika uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) .
Gwaride la vijana katika kumpokea Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali 
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali akiwa na viongozi pamoja na waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya kuwasili mkoani Kilimanjaro.
Baadhi ya wanawake wa Dini ya Kiislamu walipofika kwa ajili ya kumpokea Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali 
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali  akiwasili katika mmoja wa miskiti iliyopo wilayani Hai kwa ajili ya uwekaji wa jiwe la Msingi. 
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali akifungua kitambaa katika jiwe la Msini kuashiria kuendelea kwa ujenzi wa jengo hilo litakalotumika kama Madrasa.
Mapokezi mwakubwa kwa Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali 
Jengo la Ofisi za BAKWATA wilaya ya Hai ambalo Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali  amefika kwa ajili ya uzinduzi wake.
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali  akisalimiana na waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya kuwasili katika ofisi za Bakwata wilaya ya Hai ka ajili ya ufunguzi wake.
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali  akisalimiana na waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya kuwasili katika ofisi za Bakwata wilaya ya Hai ka ajili ya ufunguzi wake.
Furaha ya kutembelewa na Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali 
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali  akizindua rasmi ofisi za BAKWATA wilaya ya Hai.
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali akitia saini katika kitabu cha wageni mara baada ya kufungua rasmi ofisi za BAKWATA wilaya ya Hai.
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali akiondoka baada ya kufungua rasmi ofisi za BAKWATA wilaya ya Hai.
Msikiti wa Masjid Shafi uliopo wilayani Hai
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali akitia saini katika kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili katika msikiti wa Masjid Shafii kwa ajili ya uzinduzi.
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali akikata utepe kuuzindua rasmi Msikiti wa Masjid Shafi uliopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
 Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Aliakizindua rasmi Msikiti wa Masjid Shafi uliopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
Katibu wa Bakwata wilaya ya Hai,Mwl Mohamed Mbowe akisoma risala mbele ya Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali wakati wa uzinduzi rasmi wa msikiti wa Masjid Shafi uliopo wilayani Hai.
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali akipokea risala hiyo
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ali akizungumza mara baada ya kuzindua Msikiti wa Masjid Shafi uliopo wilayani Hai.
Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii, Kanda ya Kaskazini.