Wednesday, August 12

MBOWE: Ninaendelea vema

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Freeman Mbowe amesema uchovu ndiyo sababu iliyomfanya kuugua ghafla jana na kulazwa katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili, jijini Dar es Salaam.
Akiwa katika maandamano ya kumsindikiza mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa, kuchukua fomu jana, Mbowe aliugua ghafla eneo la Manyanya, Kinondoni na kulazimika kukimbizwa Muhimbili ambako amelazwa hadi leo.
Hata hivyo, mwanasiasa huyo ambaye anawania ubunge katika jimbo la Hai kupitia Chadema amewahakikisha wanachama na wafuasi wa Ukawa kuwa afya yake ni njema na huenda akaruhusiwa kutoka hospitalini ndani ya saa 48.
Akizungumza na Mwananchi jana, Ofisa Uhusiano wa Muhimbili Aminieli Aligaesha pamoja na kukiri kulazwa kwa mwanasiasa huyo, hakutaka kuweka hadharani kilichokuwa kinamsumbua Mbowe.

Monday, August 10

Lowassa: CCM hodari wa kuiba kura

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na mgombea urais wa muungano wa Ukawa, Edward Lowassa wakiwapungia mkono wananchi waliofurika makao makuu ya CUF, 
Buguruni jijini Dar es Salaam jana. 

Dar es Salaam. Mgombea wa urais kupitia Chadema, Edward Lowassa ameituhumu CCM kuwa ni hodari wa kuiba kura hivyo akawataka wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura ili hata sehemu ya kura hizo ikiibiwa, Ukawa ishinde kwa kishindo.
Lowassa ambaye ni waziri mkuu wa zamani aliuambia umati wa wafuasi wa Ukawa uliojitokeza jana kumpokea katika ofisi za makao makuu ya CUF yaliyopo Buguruni kuwa ili kufanikisha ushindi wa kuwawezesha kuingia ikulu hawana budi kushikamana, kushawishiana kupiga kura kwa wingi na kuzilinda Oktoba 25.
Kauli hiyo ya Lowassa ambaye amelelewa kisiasa na CCM tangu alipojiunga akiwa mdogo mwaka 1977, inaendeleza tuhuma ambazo hutolewa na vyama vya upinzani kuwa chama hicho huchakachua matokeo wakati wa uchaguzi.
Hata hivyo, Lowassa hakuwa na vielelezo wala kuthibitisha kuhusu tuhuma hizo dhidi ya chama chake cha zamani.
“Tukiwa na umoja, tukiwa na mshikamano tutawaondoa Jumapili asubuhi sana. Tutahitaji mshikamano, tatahitaji ushawishi wa kupiga kura tupate angalau asilimia 90 ili wakiiba asilimia 10 tuwasamehe,” alisema Lowassa katika hotuba yake iliyokuwa inakatishwa na kushangiliwa na na salamu ya CUF ya “Hakiii” na kujibiwa “kwa wote.”
“Hodari sana wa kuiba CCM kura. Sasa tupate kura nyingi za kutosha hata wakiiba kura hausikii na kuna usemi wa Chadema unaosema ‘piga kura, linda kura’ na sisi CUF ni hodari sana wa mambo hayo.”
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipotafutwa kwa simu kuhusu madai hayo, alijibu kwa ujumbe wa maneno kuwa asingeweza kuzungumza bali atumiwe ujumbe, na alipotumiwa ujumbe huo hakujibu.
Lubuva: Aeleze wanaibaje
Akizungumzia madai hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)  Jaji mstaafu, Damian Lubuva alisema Lowassa angeeleza jinsi wanavyoiba kura.
“Ili kutoa majibu ya uhakika naomba tufanye utafiti wa kutosha juu ya tuhuma hizo, lazima tujue ni njia zipi watu wanaiba, vinginevyo nitaeleza kitu ambacho sina ufahamu nacho. Yeye (Lowassa) kama mtu aliyekuwa serikalini lazima ana ufahamu walikuwa wanaiba vipi, angeeleza.”
Tume huwa inaendesha uchaguzi kwa mujibu wa taratibu na sheria na iwapo kuna mtu anasema kura zinaibwa ajitokeze aeleze kinagaubaga ili ofisi yake ifanye utafiti wa kina.
“Naomba nieleweshwe kura huwa zinaibiwa vipi? Hii imekuwa ni hisia, wengine wanasema tutaibiwa kura zetu wakati upande mwingine unasema hawa wataleta fujo kwa visingizio vya kuibiwa kura,” alisema Jaji Lubuva.
Lowassa ambaye alihamia Chadema siku 11 zilizopita na baadaye kuteuliwa kugombea urais kwa mwamvuli wa Ukawa kupitia Chadema, alisema safari ya Ikulu itafanikishwa kwa kupiga kura na siyo maandamano, hivyo Watanzania watunze shahada za kupigia kura. Hata hivyo, hakuendelea kueleza undani kuthibitisha ni namna gani CCM huiba kura.
Kiongozi huyo aliyeonekana mwenye furaha, aliwataka wanawake nao kujitokeza kwa wingi siku ya upigaji wa kura huku wakiwa wameshapika vyakula majumbani mwao ili nao wapate fursa za kupiga na kulinda kura.
Lowassa alisema ameingia Ukawa ili kuandika historia ya nchi kukuza uchumi na kuondoa umaskini na kutekeleza kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya “mabadiliko ya kweli yatapatikana nje ya CCM.”
Ukawa kutoyumba
Mbunge huyo wa Monduli anayemaliza muda wake, alisema Ukawa ipo imara haitayumbishwa kirahisi na wafitini, licha ya baadhi ya watu kujipitisha kwa viongozi wa juu na kutaka kuwarubuni ili umoja huo utetereke.
“Wanakuja kupitisha hela na kuhongahonga lakini viongozi wapo imara…hawahongeki hawa! Wanapita na maneno kwenye magazeti ya ufukuzi ufukuzi, nawaambia muwapuuze,” alisema Lowassa bila kuwataja wahusika.
Alisema kuna baadhi ya watu wanaleta propaganda kuwa Ukawa ikiingia madarakani nchi haitatawalika kiasi cha kuwatisha wafanyabiashara kukimbiza fedha zao nje ya nchi, jambo ambalo si la kweli.
“Waongo wakubwa hao…nchi itatawalika kuliko awali, Ukawa ikiingia madarakani nchi itatulia tuli, wasiwadanganye mkimbize hela zenu..tupo imara,” alisema.
Juma Duni afafanua
Mgombea mwenza wa urais wa Ukawa, Juma Duni Haji alisema hajahamia Chadema kutafuta vyeo kwa kuwa ameondoka akiwa Makamu Mwenyekiti wa CUF na waziri katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na hatua yake hiyo ni kutimiza za kuing’oa CCM madarakani.
“Ni vizuri mkaelewa kwamba tutafanya kosa kubwa tusipofika ikulu mwaka huu, tutahitaji kusubiri miaka 50 zaidi maana jamaa hawa wakija kutulia balaa yao ni mara 100 ya wanayoyafanya. Wanaoleta mabadiliko ni vijana siyo wazee,” alisema Duni Haji.
Alisema Ukawa wanatakiwa kushirikiana kwa dhati na Watanzania kwa ujumla kwa kuwa mwaka huu ni wa mageuzi na kila mmoja ana wajibu wa kufanya kampeni ya kuiondoa CCM ili kutafuta hatima bora ya nchi.
Kauli ya Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuna nguvu nyingi zinatumika kuivunja Ukawa lakini umoja huo utabaki kuwa imara na kutimiza malengo yake ya kushika dola mwaka huu kwa nguvu za Mungu.
Alisema vyama vya upinzani vimefanya siasa zao kwa shida kwa miaka 25 huku baadhi ya makada wakifungwa, kufukuzwa kazi, ndoa kuparaganyika, kufungwa au kufunguliwa kesi mahakamani lakini miezi minane iliyopita imekuwa migumu zaidi kutokana na baadhi ya watawala kupatwa na hofu baada ya Ukawa kujiimarisha.
“Safari yetu imebaki kidogo tufike tunakoelekea. Sasa akitokea kiongozi mmoja wetu bila kujali ni wa chama gani akaona kwamba malengo yetu siyo ya muhimu kuliko fursa binafsi, huyo hatufai,” alisema Mbowe na kushangiliwa.
Alisema maandamano ya leo kumsindika Lowassa kuchukua fomu yataanzia CUF na kupitia ofisi za Makao Makuu ya NCCR-Mageuzi Ilala hadi NEC kabla ya kurudi ofisi za Chadema Kinondoni.
Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi aliwataka wafuasi wa Ukawa kujitokeza kwa wingi kumsindikiza mgombea wa urais kupitia umoja huo na ikiwezekana kila mfuasi apeleke watu 10.
Mbatia amvaa JK
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema Ukawa itaendelea kuhubiri amani siku zote ili CCM na vyombo vya dola visipate sababu ya kuwatuhumu na kwamba Uchaguzi Mkuu utafanyika kwa amani.
Alisema Rais Jakaya Kikwete alihubiri chuki dhidi ya wapinzani kwa kuwaita maadui siku alipozungumza na wafuasi wa CCM baada ya kumpokea mgombea wa urais kupitia chama hicho, Dk John Magufuli alipotoka kuchukua fomu za kuwania.
 “Sikuamini kama Rais Kikwete angesema maneno yale eti anawaambia wana-CCM wana mikakati ya kila aina ya kushinda na kwamba ‘msiogope kujihadhari na nguvu za adui’. Yaani sisi wapinzani ni adui? Ukianza kuwaita wenzio adui wakati wewe ni amiri jeshi mkuu, nchi hii unaipeleka wapi?” alihoji Mbatia.
Malim Seif apongeza
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, aliwashukuru wafuasi wa Ukawa waliojitokeza kumpokea Lowassa wakati wa ziara ya kutembelea ofisi zao na kwamba moyo huo uendelee hadi Oktoba 25 siku ya kupiga kura.
“Hakuna silaha kubwa kuliko umoja, ushirikiano na mshikimano. Tukishirikiana tukawa wa kweli wa nafsi zetu bila shaka Lowassa anasubiri kuapishwa tu na sisi Zanzibar tumeshamaliza kazi,” alisema Maalim Seif na kushangiliwa na umati wa wafuasi hao.
Hali ilivyokuwa
Mapema kabla ya Lowassa hajawasili Buguruni wafuasi wa CUF walianza kujikusanya taratibu saa 4 asubuhi kwa kuzunguka na ngoma barabara za Uhuru na za mitaa kuingia ofisi za chama hicho.
Baadaye umati huo uliongezeka kiasi cha kufunga barabara ya Uhuru kwa muda wakati Lowassa anaingia saa 6:20 mchana na kupokelewa na Maalim Seif, Makaidi, Mbatia na viongozi waandamizi wa Ukawa.
Idadi hiyo ya watu iliwapa kibarua maofisa usalama wa Ukawa walioonekana wakihaha kutengeneza njia ili viongozi hao wapite.
Baada ya viongozi hao kuwahutubia wafuasi hao, waliingia katika ukumbi wa Mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi saa 7:15 mchana na kufanya mazungumza ya takriban saa moja na baadaye viongozi kutoka nje ya CUF kuondoka.
Nafasi ya Lipumba
Kikao cha Baraza Kuu kilijadili nafasi ya mwenyekiti iliyoachwa na Profesa Lipumba na suala hilo liliachiwa Mkutano Mkuu wa chama ambao utaitishwa baada ya miezi sita kwa kuwa ndio wenye uwezo wa kufanya uchaguzi huo kwa mujibu wa katiba ya CUF.
Akitoa taarifa ya kikao hicho, Maalim Seif alisema Baraza Kuu limeunda kamati maalum ya watu watatu itakayofanya kazi na katibu mkuu kwa miezi sita kabla ya Mkutano Mkuu kukaa na kumchagua mwenyekiti na makamu wake, nafasi ambazo ziko wazi.
Waliochaguliwa kwenye kamati hiyo ni Twaha Taslima ambaye ni mwenyekiti na wajumbe wawili ambao ni Aboubakary Khamis Bakary (Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar) na Sererina Mwijage (mbunge mstaafu wa viti maalumu.



JK, Magufuli waendelea kunguruma Kusini


Rais Jakaya Kikwete akibonyeza kitufe kuzindua rasmi Kivuko cha MV Mafanikio 
katika eneo la Msangamkuu mjini Mtwara jana. Picha na Freddy Maro wa Ikulu.

Mtwara. Rais Jakaya Kikwete akiwa na Waziri wa Ujenzi na mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli jana aliendelea kuunguruma katika mikoa ya Kusini na kuzindua Kivuko cha MV Mafanikio cha Mtwara kilichogharimu Sh3.3 bilioni.
Kivuko hicho chenye uwezo wa kubeba watu 100 na magari sita kinamaliza kero iliyokuwa ikiwakabili wananchi wanaovuka kutoka Pwani ya Mtwara Mikindani kwenda Pwani ya Msangamkuu, kilizinduliwa siku moja baada ya kuzindua kipande cha barabara ya Ndundu-Somanga mkoani Lindi.
Kuzinduliwa kwa kipande hicho cha barabara kumeifanya Serikali kukamilisha ujenzi wa miradi 13 mikubwa katika Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara.
Vilevile, kwa kukamilisha kipande hicho cha barabara ambayo ni sehemu ya Barabara Kuu ya Dar es Salaam-Kibiti-Lindi hadi Mingoyo, kunaifanya Serikali kutumia Sh9 trilioni katika miaka 10 ya uongozi wa Rais Kikwete.
Kilomita 60 za kipande cha Ndundu-Somanga ni sehemu pekee iliyokuwa imebakia kukamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami, ambayo imekuwa kero kwa wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara.
Baada ya tukio hilo juzi, Rais Kikwete jana aligeukia kivuko hicho na kusema kuwapo kwake ni utekelezaji wa ahadi alizotoa kwa wananchi.
Aidha aliwataka wananchi na wasafirishaji kuzingatia maadili ya kiwango cha uzito wa kivuko hicho.
“Suala la kivuko lilikuwa kero kubwa sana na tuliliona hasa watu walipokuwa wakivuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine. Jambo muhimu ni kukitunza kivuko kwa kubeba watu na mizigo kwa kiwango kinachokubalika” alisema Rais Kikwete.
Awali, Dk Magufuli akimkaribisha Rais Kikwete alisema watu wa Mtwara walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kivuko.
“Mheshimiwa Rais, wakati unaingia madarakani tulikuwa na vivuko 13, lakini kwa kipindi chako tumeongeza vivuko vingine 15 na kukamilisha idadi ya vivuko 28 vyenye uwezo wa kubeba tani tofauti tofauti, kikiwamo hiki cha Mtwara ambacho gharama yake ni Sh3.3 bilioni na tumekarabati vivuko vingine saba,” alisema Dk Magufuli.
Akizungumzia viwango vya nauli vilivyopangwa, Dk Magufuli alisema ni Sh300 kwa mtu mzima, wanafunzi hawatatozwa, huku watoto na wanafunzi wasiovaa sare za shule watalipa Sh100.
Kuhusu miradi mingine ya Kusini, Waziri Magufuli aliitaja kuwa ni Daraja la Umoja lililokamika ujenzi wake, ujenzi wa barabara za lami ya Songea-Namtumbo; Peramiho Junction-Mbinga, Masasi-Mangaka na usanifu wa kina kwa ajili ya ukarabati wa Barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi yenye urefu wa kilomita 200, ambao umekamilika.
Miradi mingine inayoendelea ni ujenzi kwa barabara za lami za Mangaka-Mtambaswala, Mangaka-Nakapanya, Nakapanya-Tunduru-Matemanga na Matemanga-Kilimasera yenye urefu wa kilomita 68.2.
Waziri Magufuli aliitaja miradi mingine inayoendelea ya ujenzi wa kiwango cha lami ni barabara za Kilimasera-Namtumbo, upembuzi yakinifu wa barabara ya Mtwara-Newala-Masasi na kuwa zabuni tayari imetangazwa kwa ajili ya ujenzi sehemu ya barabara ya Mtwara-Mnivata.
Madaraja 12 yajengwa
Kama ilivyo kawaida yake kutaja bila kusoma popote miradi anayojengwa na Serikali, Dk Magufuli alisema Serikali katika kipindi hicho imejenga madaraja makubwa 12, ambayo ni Rusumo (Kagera), Umoja (Mtwara), Mwanhuzi (Simiyu), Kikwete (Kigoma), Nangoo (Mtwara), Ruhekei (Ruvuma), Mbutu (Tabora), Mwatisi (Morogoro), Ruvu (Pwani), (Nanganga (Mtwara), Maligisu (Mwanza) na daraja la waendao kwa miguu la Mabatini (Mwanza).
Dk Magufuli pia alisema madaraja mengine madogo zaidi ya 7,200 yamejengwa na kukamilika katika kipindi cha uongozi wa Rais Kikwete, huku mengine makubwa saba yakiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi ambayo ni Kigamboni (Dar es Salaam), Kilombero (Morogoro), Kavuu (Katavi), Sibiti (Singida), Ruvu Chini (Pwani), Lukuledi 11, (Mtwara) na Kolo  la Dodoma.
Kana kwamba haitoshi, alisema kuna madaraja mengine makubwa ambayo yako katika maandalizi ya kujengwa.
Ni pamoja na Momba, Mwiti, Simiyu, Wami, Ruhuhu, Daraja jipya la Salendar, Daraja jipya la Wami Chini, Pangani na daraja la wandeao kwa miguu la Furahisha.

Profesa Lipumba: CCM ina wagombea wawili wa urais


“Ukweli ni kwamba  tumejiparaganyisha wenyewe ndani ya Ukawa. Kwa hiyo Watanzania watakuwa na wanaCCM wawili wanaogombea urais wakati Ukawa tulikuwa na wagombea watatu, na tulikubaliana Dk Slaa apeperushe bendera” Profesa Lipumba

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), kina wagombea wawili wanaowania kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Madai hayo mapya ya Profesa Lipumba yametolewa siku tatu baada ya kujiuzulu uenyekiti CUF, akisema hiyo ni moja ya sababu za kuachia nafasi yake kutokana na uamuzi uliofikiwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuhusu mgombea urais.
Akizungumza wakati akitangaza kujiuzulu wiki iliyopita, Profesa Lipumba alisema dhamira yake ilikuwa inamsuta kwa kuwaingiza ndani ya Ukawa watu kutoka CCM, waliokuwa wanapingana na maoni ya wananchi kuhusu rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na kuwapa fursa ya kuwania urais.
Juzi usiku katika mahojiano aliyoyafanya na Azam TV kutoka Kigali alikosema anafanya utafiti, Profesa Lipumba alisema kumpa nafasi waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa kuwania urais kupitia Chadema ndani ya Ukawa, ni sawa na CCM kusimamisha wagombea wawili (Lowassa) na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Katika mahojiano hayo ya simu, Profesa Lipumba ambaye wiki mbili zilizopita alimpokea Lowassa akisema ni mtu safi na kwamba, ufisadi ndani ya CCM ni mfumo  alisema katika kujiuzulu kwake hakutumiwa na CCM kuparaganyisha Ukawa, bali walikuwa tayari wameparaganyika.
“Ukweli ni kwamba tumejiparaganyisha wenyewe ndani ya Ukawa. Kwa hiyo Watanzania watakuwa na wanaCCM wawili wanaogombea urais wakati Ukawa tulikuwa na wagombea watatu... mimi, Dk Willibrod Slaa, (Katibu Mkuu wa Chadema) pamoja na Dk George Kahangwa (NCCR-Mageuzi) ambaye alikiri kuwapo makubaliano hayo.
“Tulikutana nyumbani kwangu tukakubaliana Dk Slaa apeperushe bendera ya Ukawa, lakini tumewekwa kando,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema yupo Rwanda kwa muda na anafanya utafiti kuona namna gani Tanzania inaweza kujifunza mambo ya kiuchumi kutokana na nchi hiyo kupiga hatua kubwa kiuchumi.
Pia alisisitiza kuwa hajahama nchi na kwamba wiki hii anatarajia kurejea nchini.
Agosti 6, mwaka huu Profesa Lipumba alijivua  uenyekiti wa CUF wakati mkakati wa vyama vya upinzani kushirikiana kushika dola ukiwa umeshika kasi.





Pinda: Nimeishia kuwa rais wa fikra


Waziri Mkuu Mizengo Pinda akipungia wakulima kwenye maonyesho ya Nanenane, 
Kanda ya Kusini yaliyofanyika jijini Mbeya juzi.

Mbeya. Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambaye alianguka katika hatua za awali za mbio za urais ndani ya CCM, amesema ameishia kuwa “rais wa fikra”.
Pinda, ambaye amekuwa Waziri Mkuu kwa takriban miaka minane, hakuweza kuingia katika orodha ya makada watano ambao majina yao yalipelekwa Halmashauri Kuu kwa ajili ya kupata majina matatu ya kupelekwa Mkutano Mkuu kwa ajili ya kupata mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala.
Baada ya mchakato huo kumalizika, mbunge huyo wa Katavi amekuwa kimya, lakini jana aliibuka na kuzungumzia mbio hizo zilizoacha majeraha kwenye chama hicho kikongwe.
Pinda alisema mchakato huo ulikuwa hauna kulala, wa haraka haraka, ambao uliisha kwa CCM kupata mgombea ambaye alimuelezea kuwa “ni chaguo la Mungu”.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa fupi ya Mkoa wa Mbeya kuhitimisha maonyesho ya Nanenane jijini hapa, Pinda alisema alitamani sana kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania.
“Mimi ninaamini Mungu ndiye anayepanga kwani  sikuzaliwa kuwa Waziri Mkuu wala kuwa Rais, lakini nilipangiwa uwaziri mkuu ambao nimefanya kazi hiyo hadi nimechoka,” alisema Pinda, ambaye alikuwa mmoja wa makada 42 wa CCM waliojitokeza kuwania ridhaa ya chama hicho kugombea urais.
“Baada ya mchakato ule, alipatikana mtu mahiri ambaye Mungu alimpanga, lakini tamaa yangu, ikaishia kuwa rais wa fikra tu.”
Alisema mchakato ulifanyika kwa kasi bila kulala na wakapatikana watano, mara watatu na hatimaye mmoja.
“Suala hilo halitakiwi kuwa sababu ya kugombana, kulaumiana na kutoana macho, kwani ni sawa na kugombana na Mungu,” alisema Pinda.
“Hata mimi nilitamani sana kuwa Rais, lakini sasa yamekwisha. Sina sababu ya kuwa na hasira  au kuhama chama kwani haina tija na hasira ni hasara.
“Sina sababu ya kuhama chama, nitabaki CCM na baada ya Oktoba nitakuwa mkulima mzuri ambaye nitashirikiana na wenzangu kuendeleza nchi.” Pinda alisema mgombea wa CCM, Dk John Magufuli ni mzuri na kwamba Mungu atamsaidia kujua mahitaji mengine ya Taifa na Watanzania.
Alisema ana uhakika kwamba ifikapo mwaka 2025, hali ya umaskini katika kaya itakuwa imepungua.
Aliwataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na maofisa wote wa Serikali waliogombea urais, ubunge na udiwani  ambao walishindwa katika kura mbalimbali, wakubali matokeo na wachape kazi bila kinyongo na kwamba Serikali ijayo itawafikiria kwa utendaji mzuri.
Awali, katika taarifa yake fupi, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro alisema yeye na viongozi wengine waliwania ubunge, lakini wameshindwa na wataendelea kuchapa kazi ya Serikali.
Kandoro alizungumzia utekelezaji wa maagizo mbalimbali aliyopewa na Waziri Mkuu likiwamo la kuwashughulikia wanaume waliowapa mimba wanafunzi wa sekondari na alisema  watu 176 walikamatwa na 53 kati yao, kesi zipo mahakamani wakati wengine walifungwa na wengine uchunguzi unaendelea.
Kuhusu agizo la kuhakikisha wanawake wanapimwa ili kujua hali ya kansa mkoani Mbeya, alisema wanawake 7,241 walipimwa na 200  kati yao walionekana kuwa na saratani ya shingo kizazi.

Saturday, August 8

Dk Magufuli, Lowassa pambano la karne


Dk John Magufuli (Kushoto) na Edward Lowassa (kulia) 

Dar es Salaam. Wakati zikiwa zimesalia siku 14 kabla ya kuanza kwa kampeni za urais, ubunge na udiwani, macho na masikio ya wengi yanaelekezwa kwa wagombea wawili kutoka vyama vikuu vya siasa, Dk John Magufuli wa CCM na Edward Lowassa wa Chadema, ambao uchambuzi wa gazeti hili unaonyesha wana mengi yanayoshabihiana.
Wawili hao ni kati ya makada saba waliosimamishwa na vyama saba kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambao inaelekea kuwa ndiyo watakaochuana vikali, hasa kutokana na ukweli kuwa Dk Magufuli anatoka chama tawala na Lowassa, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, anaungwa mkono na vyama vinne vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wengine wanaowania urais ni Mchungaji Christopher Mtikila wa DP, Chifu Lutayosa Chemba (ADC), Macmillan Limo (TLP), Hashimu Rungwe (Chauma), Fahami Dovutwa (UPDP) na mgombea wa ACT Wazalendo ambaye bado hajateuliwa.
Pamoja na kwamba katika siasa lolote linaweza kutokea, wagombea hao watano hawatazamiwi kuweka ushindani mkubwa zaidi ya ule wa Dk Magufuli na Lowassa.
Dk Magufuli hakutarajiwa kupita kwenye mbio za urais ndani ya CCM, ambako Lowassa na vigogo wengine walikuwa wakipewa nafasi kubwa, lakini ushindi wake umemfanya awe mgombea wa chama chenye mtandao mkubwa nchini na hivyo mwanzoni kupewa nafasi kubwa ya kushinda.
Hata hivyo, uamuzi wa Lowassa kujivua uanachama wa chama kilichomlea na kilichompa umaarufu mkubwa, umebadili upepo na sasa vita ya kuingia Ikulu Oktoba 25 inaonekana kuwa ya watu hao wawili.
Gazeti la Mwananchi linaangalia sifa ambazo wawili hao wanashabihiana pamoja na tofauti zao, kwa kuzingatia maelezo ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa.
Wote wamesomea ualimu
Moja ya mambo ambayo wawili hao wanashabihiana ni kusomea ualimu, ingawa wa fani tofauti. Dk Magufuli, ambaye atakuwa akitimiza miaka 56 siku nne baada ya Uchaguzi Mkuu, ni mwalimu aliyejikita kwenye masomo ya kemia na hesabu.
Alipata diploma ya ualimu mwaka 1982 kwenye Chuo cha Elimu Mkwawa, kabla ya kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alipata shahada yake ya kwanza, ya umahiri na ya uzamiri akijikita kwenye somo la kemia.
Lowassa, ambaye Agosti 26 atakuwa akitimiza miaka 62, alisomea shahada ya ualimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1977, lakini shahada yake ya uzamili ilijikita kwenye masomo ya maendeleo ya jamii.
Dk Magufuli alitumia taaluma yake kufundisha kemia na hesabu kwenye Shule ya Sekondari ya Sengerema, lakini Lowassa hakufundisha.
Wote ni makini
Pengine ni kutokana na maadili ya ualimu, wawili hao wamedhihirisha kuwa ni watu makini katika utendaji wao, jambo ambalo limekuwa likiwafanya watu wanaofanya kazi chini yao kuwa na wasiwasi kila wanapowapeleka taarifa.
Dk Magufuli na Lowassa hutumia muda mwingi kujiridhisha na taarifa wanazopelekewa kabla ya kufanya uamuzi ambao wakati mwingine huonekana kama wamekurupuka.
Mhandisi mmoja ambaye amewahi kufungiwa leseni na Magufuli aliiambia Mwananchi kuwa kosa moja kubwa alilofanya ni kumwandikia Dk Magufuli taarifa ndefu, lakini iliyojaa mambo yasiyo sahihi.
Anasema kuwa aya hiyo ilikuwa ukurasa wa 20, lakini ndani ya muda mfupi Magufuli aliibaini na kibarua chake kiliota nyasi.
Hali ni kama hiyo kwa Lowassa, ambaye akiwa Waziri Mkuu aliwahi kumtimua mkandarasi wa Wilaya Temeke kwa kushindwa kukagua ujenzi wa maghorofa ikiwemo la Chang’ombe Village lililoporomoka na kusababisha maafa ya mtu mmoja na wengine kadhaa kujeruhiwa mwaka 2006.
Uchapakazi
Mbali na umakini, wawili hao wamedhihirisha kuwa ni wachapakazi hodari katika wizara na taasisi walizopitia kiasi cha kujijengea jina kubwa kwa wananchi.
Utendaji wa Dk Magufuli hauna shaka na ameshaeleza bayana kuwa hapendi wazembe na wasiowajibika sanjari, kama Lowassa ambaye hata siku ya kwanza alipoingia ofisini mwaka 2005 aliwataka wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Wakati Dk Magufuli alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, wengi walidhani kuwa amemaliza kisiasa, lakini mbunge huyo wa Chato alifanya kazi kubwa ya kutambua fursa za kiuchumi zilizoko hasa kwenye uvuvi na akafanikiwa kuonyesha ni kiasi gani Serikali ilikuwa ikipoteza fedha.
Wakati huo, Tanzania iliingia makubaliano na Afrika Kusini na nchi nyingine za ukanda huu kufanya doria kwa pamoja kwenye pwani ya Afrika Mashariki na juhudi hizo zilifanikiwa kunasa meli ya Tawaliq 1 iliyokuwa na samaki wenye thamani ya Sh20 bilioni.
Uchapakazi wake umedhihirika hasa kwenye ujenzi wa barabara, akiwa amefanikiwa kuunganisha takriban mikoa yote ya Tanzania katikja kipindi alichokaa Wizara ya Ujenzi.
Lowassa anaonekana zaidi katika kusimamia utekelezaji wa mradi wa maji ya Ziwa Victoria katika shughuli za maendeleo baada ya mpambano mkali dhidi ya Misri, ambayo ilikuwa na ukiritimba wa maji hayo kabla ya nchi tano kuungana na kusaini makubaliano ya matumizi ya maji hayo.
Lowassa pia anajinadi na mafanikio ya ujenzi wa shule za kata, ambazo kwa kiasi kikubwa zimefanikisha watoto wengi kupata elimu kwa gharama nafuu, ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma ambao aliufanya kwa kukutanisha mifuko ya hifadhi ya jamii na kuiamuru ichangia gharama za ujenzi.
Jambo lingine walilonalo Dk Magufuli na Lowassa ni misimamo. Dk Magufuli ni kiongozi mwenye misimamo isiyotia shaka na siku zote husimamia anachokiamini, sanjari na Lowassa, ni mwenye misimo yake na itakumbukwa alipokuwa Waziri wa Maji na baadaye Waziri Mkuu alionyesha misimamo.
Dk Magufuli alitofautiana hata na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati aliposimamia uendeshaji wa kivuko cha Kigamboni, na suala la kiwango cha mizigo inayobebwa na malori.
Moja ya kauli zilizonukuliwa sana ni ile ya “asiyekuwa na nauli ya kulipia kivuko, apige mbizi”, ambayo ilitafsiriwa kuwa ya kutojali wananchi, lakini faida zake ndio zinamfanya aonekane kuwa msimamo wake ulilenga kunufaisha wananchi.
Hali kadhalika Lowassa anajulikana kwa kusimamia uamuzi kama wa kubomoa maghorofa yaliyojengwa kinyume na sheria Masaki jijini Dar es Salaam. Msimamo wake pia kwenye suala la mkataba wa City Water iliyokuwa ikihusika na ugavi wa maji jijini Dar es Salaam ndio uliosababisha uvunjwe.
Ufuatiliaji
Lowassa na Dk Magufuli pia wanajulikana kwa kuwa wafuatiliaji wazuri kwa watu walio chini yao au wanaofanya kazi chini ya mamlaka zao. Dk Magufuli, ambaye anajulikana kwa kukariri tarehe, kiwango cha miradi, urefu wa barabara na kiwango cha fedha zilizotengwa kwenye miradi, hutumia talanta hiyo kufuatilia miradi mbalimbali na hasa muda wa kumalizika, hali inayomfanya kila mara atishia kuvunja mikataba na wakandarasi au kuivunja kabisa.
Hilo pia limekuwa likifanywa na Lowassa, ambaye akiwa Waziri Mkuu alikuwa akihakikisha wakuu wa wilaya na mikoa wako sehemu zao za kazi na yeyote ambaye alitaka kutoka alitakiwa awe na kibali, kwa mujibu wa baadhi ya watu waliofanya kazi naye.
Udhaifu
Mbali na sifa hizo nzuri, wanasiasa hao wanashabihiana katika udhaifu, hasa uamuzi wa papo kwa papo ambao pia husababishwa na kiu yao ya kutaka kuona kazi inafanyika.
Wote wawili hufanya uamuzi wa papo kwa pamo ambao wakati mwingine huwa na athari za kisheria. Uamuzi kama huo huwa na kadhia kwa wafanyakazi na makandarasi wanaopewa zabuni mbalimbali na Serikali.
Hawaachi mfumo wa utendaji
Udhaifu mwingine wa wawili hao ni hali ya kujituma wao bila ya kutengeneza mfumo ambao unaendeleza ufanisi na badala yake wanapoondoka, hali hubakia kama ilivyokuwa awali.
Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Dk Magufuli kwenye wizara alizopitia kama ya uvuvi na hali kadhalika kwa Lowassa.
Pia wanatofautiana
Tofauti kubwa kati ya Dk Magufuli na Lowassa ni mgombea huyo wa CCM kutokulia ndani ya chama na badala yake amekuwa kwenye nafasi za utendaji zaidi na uwaziri. Dk Magufuli amekuwa mwanachama wa CCM na mbunge, nafasi ambayo humuingiza kwenye kikao cha Halmashauri Kuu pekee.
Lakini Lowassa ameshika nafasi mbalimbali kwenye chama kuanzia katibu wa mkoa hadi mjumbe wa vyombo vya juu vya CCM.
Kauli za wachambuzi
Baadhi ya wachambuzi na wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (Udsm) wamesema kwa nyakati tofauti kwamba wagombea hao wanaonekana kuwa na tofauti kubwa zinazoweza kufanikisha ushindi katika uchaguzi huo.
Mohammed Bakari, ambaye ni mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema wagombea hao wanafanana katika kigezo cha utendaji kazi lakini kiuamuzi na uzoefu wanatofautiana.
“Dk Magufuli ana uamuzi wa kukurupuka ila Lowassa ametulia,” alisema. “Kuhusu uzoefu pia Lowassa ni mzoefu kiuongozi kuliko Dk Magufuli.”
Alisema suala la uadilifu siyo rahisi kupata kiongozi mwadilifu kwa wagombea hao na bila kuzitaja kashfa hizo, alisema wote wana kashfa. Aliongeza kwamba, Lowassa ni mgombea anayeweza kuleta mabadiliko kwa Taifa hili, lakini Dk Maghufuli hawezi kutokana na mfumo uliopo kwenye chama chake.
Mkuu wa Idara ya Sayansi ya Siasa wa Udsm, Dk Alexander Makulilo pia anaona sifa hizo zinazolingana.
Alisema wagombea hao wanafanana kwa utendaji mzuri wa kazi na uamuzi wa papo kwa hapo. Aidha, alisema Magufuli ni kiongozi anayeweza kuleta siasa mpya zisizokuwa na makundi.
Alisema Lowassa ni mgombea anayekabiliwa na changamoto ya Richmond iliyomfanya ajiuzulu uwaziri mkuu, wakati Dk Magufuli hana kashfa kubwa iliyowahi kujadiliwa bungeni.
“Lakini hali hiyo haiwezi kuwa changamoto kubwa kutokana na mwamko mkubwa wa kundi linalohitaji mabadiliko ya uongozi serikalini. Uchaguzi huu ninaufananisha na Zambia wakati chama cha UNIP kilipoondolewa madarakani kwa kuwa makundi ya kijamii yalikuwa yameamua kiondoke madarakani,” alisema.
Kuhusu mfumo kuibeba CCM, Dk Makulilo alisema ni sehemu ya changamoto kubwa inayoweza kufanikisha ndoto za Lowassa kuingia madarakani.

Gesi kuanza kusafirshwa Dar baada ya siku 14


Mtwara. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), James Mataragio amesema kuwa gesi asilia itaanza kusafirishwa kwa njia ya bomba kutoka Mtwara kuelekea Dar es Salaam, baada ya siku wiki mbili kuanzia sasa.
Mataragio ametoa kauli hiyo jana baada ya kutembelea kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo kijiji cha Madimba Wilaya ya Mtwara mkoani hapa na kujionea sehemu kubwa ya mradi huo, ukiwa umekamilika kwa asilimia 100.
Hivi karibuni Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema umeme wa gesi utaanza kutumika mwezi ujao baada ya ujenzi wa bomba la kupitisha gesi hiyo kukamilika.
Mataragio alisema kuwa kutokana na kiwanda hicho cha kuchakata gesi asilia kukamilika kwa asilimia kubwa, Watanzania wategemee kuanzia mwezi ujao wataanza kutumia umeme unaotokana na Nishati hiyo ya Gesi Asilia.
“ Sisi kama TPDC kabla gesi haijaanza kusafirishwa tunajiridhisha kwanza kwa kufanya majaribio ya mitambo kwa sababu inakuwa bado haijaanza kufanya kazi, tunaangalia uwezo wake ili tuweze kujiridhisha ndiyo tuisafirishe kuelekea Dar es Salaam.” Alisema Mataragio.
Kadhalika Mkurugezi huyo alisema kuwa wananchi wa mkoani hapa watanuifaka na gesi hiyo kutokana na ujenzi wa kiwanda cha Saruji cha Dangote pamoja na shughuli mbalimbali zitakazowaongezea kipato kutokana na rasilimali hiyo.
Alisema kuwa wananchi hao watanufaika na kiwanda hicho cha kuchakata gesi asilia kwa kupata maji safi na salama, pamoja na kuwajengea kituo cha Afya ili kiweze kuwasaidia kupitia mradi huo.
Hata hivyo Mataragio alisema kuwa hadi sasa kuna visima ambavyo vimepatikana katika eneo la Mnazi Bay pamoja na Msimbati, na utafiti bado unaendelea kutafuta visima vingine.

NEC: Marufuku kutoa kadi ya kupigia kura

Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva 

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeonya kwamba mtu yoyote haruhusiwi kutoa kadi yake ya kupigakura au taarifa za kadi hiyo kwa ndugu, jamaa au mwajiri wake.
NEC imetoa onyo hilo wakati tayari kukiwa na tetesi kuwa baadhi ya wafanyakazi wa umma wakiwamo polisi, wanajeshi na askari magereza, wametakiwa kukabidhi kadi zao kwa viongozi wao wa ngazi za juu.
Wakati hayo yakisemwa, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika jana aliitisha mkutano wa vyombo vya habari akidai kuna tetesi serikali imeviagiza vyombo vya usalama, kupeleka namba za vitambulisho vya askari wote kwa wakuu wa vitengo jambo ambalo ni kunyume na utaratibu
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima Kombwey alitoa angalizo juu ya hilo na kusema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ambayo inazungumzia Daftari la Kudumu la Wapigakura, hairuhusiwi na haitakiwi kwa mtu asiyehusika na kadi ya mpigakura kuimiliki kadi hiyo.
Kombwey alisema hakuna sheria yoyote inayomlazimisha mtumishi wa umma kutoa kadi yake ya kupigiakura kwa mwajiri wake.
Akizungumzia suala hilo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga alisema taarifa hizo ni za uongo na hazina ukweli wowote kuwa wanajeshi wameombwa nambari za vitambulisho.
Msemaji wa Polisi, Advera Bulimba alipopigiwa simu kuhusu madai hayo, alisema hana hizo taarifa.
Ofisa Mawasiliano wa Magereza, Deodatus Kazinja alisema hizo ni tetesi na wala hazina ukweli wowote.
*Imeandikwa na Hussein Issa na Florid Mapunda, Suzan Mwillo

‘Lipumba angetaka ningemwachia urais’

Profesa Ibrahimu Lipumba 
Dar es Salaam. Mgombea urais kupitia tiketi ya Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) Chifu Lutalosa Yemba, amemkaribisha aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kujiunga na chama hicho.
Chama hicho juzi kilifanya mkutano wa kuwatambulisha wagombea wake wa nafasi ya urais, Yemba anayewania urais wa muungano na mgombea mwenza wake Said Miraj Abdullah, pia alitambulishwa Hamad Rashid Mohamed, anayewania urasi wa Zanzibar.
Yemba kwenye mkutano huo alisema anaufahamu uwezo wa Lipumba katika siasa, ujasiri na uvumilivu wake, hivyo hatakuwa na kinyongo kufanya naye kazi ya kusukuma mbele gurudumu la siasa za upinzani.
Alisema hakujiunga na chama hicho kwa ajili ya kuwa rais, amejiunga kwa ajili ya kutengeneza dola ya uongozi itakayoondoa dhiki na mateso wanayopata Watanzania, hivyo kutokana na uzowefu alionao katika siasa anaamini watafanikisha hilo kwa ufanisi.
“Walinifukuza mwezi wa sita , mwezi wa nane Lipumba amejing’atua kwenye uongozi, watafahamu sasa kuwa kwenye chama kile kuna udhalimu, namkaribisha Lipumba na ninampongeza kwa uvumilivu wake, ingawa ninaumia kuona kiongozi shupavu aliyekuwa na uwezo wa kuhakikisha wananchi wanaamini katika vyama vingine vya upinzani kukatishwa tamaa na watu wachache wenye uroho wa madaraka, ”alisema Yemba.
Alisema kuwa anaingia katika kinyang’anyiro cha kuwania urais akipambana na chama kimoja tu, CCM, hivyo vilivyobaki hakuna wa kumtisha kwa sababu wenyewe kwa wenyewe wameanza kuvurugana.
“Sisi ADC kama bahari, tunachukua maovu yao tunameza, baadaye tunayatema, wakati ukifika wa kufanya hivyo tutafanya kwa sasa , nawaomba Watanzania mpime kwa makini na kuchagua kiongozi anayefaa.
“Mchagueni asiyekuwa mwizi, fisadi, mnyang’anyi asiye na kashfa na hakuna unapoweza kumpata kiongozi wa namna hiyo zaidi ya ADC, pimeni sikilizeni sera zetu, ilani yetu mtuunge mkono. ”alisema Yemba.
Jana, Yemba alichukua fomu za kuwania urais wa chama hicho, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), huku akiwasisitiza Watanzania kukipa nafasi chama hicho ili kuifanyia nchi mabadiliko ya haki na kuondokana na ukandamizaji.
Kabla ya kufikia uamuzi wa kuchukua fomu Nec, Yemba alinukuliwa akisema kama Lipumba angejitokeza jana, angemwachia nafasi ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano. Hata hivyo kuna taarifa Lipumba alisafiri juzi usiku kwenda nje ya nchi.
Said Miraj Abdulla
Kwa upande wa mgombea mwenza wa chama hicho Said Miraj Abdulla, alisema kuwa anamualika Maalim Seif awaeleze Watanzania anataka nini katika siasa, kwa nini anavuruga utaratibu wa kuwapo kwa upinzani wa kweli.
Alieleza kuwa pamoja na kuunga mkono kilichofanywa na Lipumba kutokana na udhalimu unaofanywa na wanasiasa wachache wanaokatisha tamaa wengine, lakini hafurahi kumuona au kusikia anakaa nje ya ulingo wa siasa.
“Nani asiyejua mchango wa Lipumba katika siasa za upinzani wa nchi, arudi kwenye siasa aje kuendeleza safari aliyoianza mwaka 1995, kukaa kwake nje ya siasa kunapunguza nguvu ya Watanzania kufikia kilele cha mafanikio ya kupata rais atakayejali shida zao, kuwasikiliza, kuwanufaisha na rasilimali zinazopatikana nchini mwao, ”alisema Abdulla.
Hamad Rashid Mohamed
Kwa upande wa mgombea urais wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed, aliwataka wananchi kuwa makini wanaposhabikia vyama na kuviepuka visivyoheshimu Katiba.
Alisema alipokuwa kwenye Bunge la Katiba alisema hakuna upawa wala Ukawa, matokeo yake ndiyo hayo watu wanalumbana, Wazanzibar wanahitaji mabadiliko wamekaa kwenye umasikini usiowahusu kwa sababu hakuna ajira.
Alieleza kuwa kwa wakazi wa Zanzibar wanaohitaji ajira, akijenga viwanda vitano tu hakutakuwa na kijana atakayekosa kazi na huo ndiyo mkakati wake katika miaka mitano ya uongozi.
“Watanzania shabikieni vyama huku mkiwapima wagombea wana nia gani na nyinyi, maslahi yao binafsi au kuwasaidia, maana “Tumbili akimaliza miti anakuja mwilini” kuweni makini, ”alisema.