Monday, September 9

CUF: Ndugai anahujumu

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (Cuf), kimesema kitendo cha Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai kukataa kumpa nafasi Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na kuamuru askari wa Bunge wamtoe nje ya ukumbi huo ni kumhujumu Rais Kikwete kwenye azma yake ya kupata Katiba Mpya.
Pia, chama hicho kimesema kinafanya juhudi za kuwasiliana na viongozi wa vyama vingine ili kuweka mkakati wa pamoja wa kukabiliana na hujuma dhidi ya mchakato wa kupata Katiba Mpya na kuimarisha umoja wa kitaifa  kwenye kipindi hiki cha kukabiliana na changamoto za nchi jirani.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba alisema, Cuf inalaani vitendo vya kuwanyanyasa na kuwadhalilisha wabunge wa upinzani akiwamo Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na kudai kuwa inaonyesha wazi CCM wanampango wa kutengeneza katiba ya upande mmoja.
“Kwa mfumo wa mabunge ya Jumuiya ya Madola, kwa Tanzania Waziri Mkuu na kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ndiyo wanawakilisha pande mbili ndani ya Bunge, hivyo kumnyima Mbowe fursa ya kuzungumza ni unyanyasaji na udhalilishaji na kwamba kitendo hicho hakikubaliki,” alisema.
Profesa Lipumba alisisitiza muswada uliokuwa unajadiliwa  ulikuwa na utata, Serikali imeubadili kwa nguvu na kuondoa maoni muhimu ya wadau.


Tutatumia nguvu ya umma kukwamisha Katiba

Dodoma. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kitatumia nguvu ya umma kuikataa Katiba Mpya endapo CCM na Serikali yake: “vitaendeleza hila na ubabe katika mchakato unaoendelea.”
Pia chama hicho kikuu cha upinzani nchini, kimeitaka Serikali kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura kabla ya upigaji wa kura ya maoni ya Katiba Mpya huku kikisema kinyume chake suala hilo litaibua mgogoro mkubwa.
Kauli hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa chama hicho, John Mnyika katika mahojiano yaliyofanyika Mjini Dodoma mwishoni mwa wiki.
Mnyika alisema baada ya CCM kuhodhi muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na hivyo kulifanya Bunge la Katiba liwe ni hodhi ya chama hicho tawala karata pekee waliyobakiwa nayo ni kura ya maoni... “Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, ndiye atakayeteua wajumbe 166 kutoka taasisi na makundi na kufanya Bunge zima la Katiba kuwa na wajumbe zaidi ya 600.”
Alisema kwa sasa, Tanzania Bara hakuna utaratibu wa kikatiba wa namna ya kuendesha kura ya maoni na kuongeza.
“Wenzetu Zanzibar katika Katiba yao wanao mfumo wa kura ya maoni, sisi haupo ni lazima tutengeneze sheria ya kura ya maoni ya Katiba Mpya na Sheria ya kura ya maoni ya Muungano,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema Kamati ya Bunge la Katiba, Sheria na Utawala inapaswa kuanza kukutana kwa dharura kupata maoni ya wadau kuhusu kura ya maoni na ianze na Zanzibar ambayo haikushirikishwa.
“Kamati ianze sasa, isisubiri Bunge la Oktoba 29 maana kati ya mambo yaliyoifanya Serikali kuondoa muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni ni mgongano wa kikatiba kati ya Zanzibar na Muungano,” alisema.
Alisema pia Tanzania inahitaji kuwa na Katiba ya mpito ambayo itaweka chombo huru kitakachosimamia upigaji wa kura ya maoni badala ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Mbowe alisema Serikali ya CCM inatumia hila na ubabe kuhakikisha inapatikana Katiba Mpya itakayobeba masilahi ya chama hicho kwa gharama yoyote.
 “Endapo CCM itaendelea na hila zake hizi niwaambie Chadema tumejipanga… Tutatumia teknolojia ya kisasa kuwafikia Watanzania hata ikibidi kutumia helikopta nne ili waikatae wakati wa kupiga kura ya maoni,” alisema Mbowe na kuongeza: “Hila yoyote itakayotokea kwenye Katiba tutahamasisha Watanzania kuikataa, wasifikiri wanachokifanya ni salama kwao… Wanageuza mchakato kuwa wa kichama badala wa wananchi.”
Alisema msimamo wa CCM kukataa mapendekezo ya muundo wa Serikali tatu si wa wanachama wake wa kawaida, bali matakwa ya viongozi wake wa juu.

“Tunapozungumzia kumdhibiti Rais, wao (CCM) wanafikiri tunamzungumzia Rais Kikwete (Jakaya)… Tunataka kudhibiti madaraka ya Rais yeyote ajaye awe wa  Chadema, CCM au NCCR”.
Alisema mapendekezo ya wananchi kuhusu Serikali tatu yalianzia wakati wa Rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe mwaka 1984 na baadaye mwaka 1991 wakati wa Tume ya Jaji Mkuu Francis Nyalali.
Alisema pamoja na kutotekelezwa kwa mapendekezo hayo ya wananchi, bado wabunge wa G55 walianzisha vuguvugu hilo lakini likazimwa kwa kutumia nguvu kubwa.
“Tume ya Jaji Robert Kisanga nayo ilikuja na mapendekezo hayohayo na sasa Tume ya Jaji Joseph Warioba na bado CCM haitaki kuamini ni ya wananchi,” alisema.
Mbowe alisema ndiyo maana Chadema sasa kimeamua kujitoa mhanga kuwahamasisha hadi wanachama wa CCM kuikataa Katiba Mpya endapo itapatikana nje ya matakwa ya Watanzania... “ Nia tunayo, sababu tunayo na uwezo tunao.”
Alisema matumizi ya polisi hayatalipatia taifa Katiba Mpya na nzuri. “Wajue kuwa wako Watanzania wenye busara kwa mamilioni walioko nje ya Bunge ambao wana sauti katika Katiba yao na CCM wasifikiri wao ni alfa na omega (mwanzo na mwisho),” alisema Mbowe.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amesema hata kama Tanzania haitapata Katiba Mpya hadi ifikapo 2015, bado ya sasa haitafaa kutumika.
“Hata kama tutashindwa kupata Katiba Mpya hatuwezi kwenda kwenye uchaguzi na katiba hii ya sasa kwa sababu katiba mpya ya Zanzibar imejiingiza katika mgogoro na Katiba ya Muungano,” alisema.
Alisema kama dalili za kutopatikana kwa Katiba Mpya zimeanza kuonekana, ni vyema ikatumika busara na hekima katika kuvuka kikwazo hicho na njia pekee ni meza ya mazungumzo.
“Sisi siyo tutakaoifanya Tanzania isitawalike, bali CCM…  Tunafanya haya kwa nia njema kabisa, hatutaki damu ya Watanzania imwagike kwa jambo linaloepukika,” alisema.

Friday, September 6

‘Marekebisho yanazungumzika bungeni’




Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema Serikali haitauondoa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa sababu mambo ambayo Kambi ya Upinzani Bungeni inayadai, yanazungumzika na yanaweza kubadilishwa kwa mamlaka ya wabunge.
Pinda alikuwa akijibu swali la nyongeza la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe katika kipindi cha Maswali ya Kwa Waziri Mkuu Bungeni, Dodoma jana.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema), alisema yapo matukio ya kibabe, kejeli, matusi na ya dharau ambayo yamekuwa yakifanya kuchelewa kwa utaratibu mzima wa utungaji wa sheria... “Pamoja na rai mliyoiondoa, sisi tunasema yapo maeneo mengi yasiyo na tija ambayo yanafanya msingi wa marekebisho ya sheria mlioleta jana (juzi), kuwa hayana tija kwa mchakato huu.”
Akijibu swali hilo, Pinda alisema: “Hivi kweli Mbowe una ngoja hadi muswada unafika ngazi ya Bunge, ndipo unakuja na hoja hiyo wakati tulikuwa na fursa kubwa?”
Alisema kwa mambo ambayo alielezwa kuwa ndiyo yaliyosababisha wabunge wa kambi ya upinzani kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge juzi, hakuna atakayeona umuhimu wa kuondoa muswada huo.
“Kwa sababu ni vitu ambavyo ndani ya Bunge hili vinazungumzika na vinaweza kubadilishwa kulingana na mamlaka mliyopewa,” alisema.
Katika swali la msingi, Mbowe alisema mchakato wa Katiba Mpya unahitaji ustahimilivu, ushirikiano, uwazi, dhamira njema na kwamba wabunge wanapaswa kutambua kuwa wapo wadau nje ya Bunge wanahitaji ushirikiano.
Pinda alisema: “Mategemeo ni wabunge tulio ndani tutaujadili muswada huu kikamilifu na maeneo yote ambayo yanadhaniwa yanaweza yasiwe na tija, neema kwa nchi yetu, ni jukumu letu kujadili kwa uwazi, uaminifu na kiukweli.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia (NCCR –Mageuzi), alihoji kama Serikali haioni ni busara mazungumzo ya kisiasa kufanyika kwanza kisha yakafuatiwa na sheria ambayo itasaidia kuunda dhana ya dola. Alisema kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa Katiba kwa kuruhusu mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar.
Kuhusu hilo, Pinda alisema kulikuwa na mashauriano makubwa kati ya vyama, taasisi na pande mbili za Muungano kabla muswada huo kufikishwa bungeni na kwamba Katiba Mpya itameza yote yaliyomo katika katiba hiyo ya zamani na kuja na mawazo mapya ambayo itaongoza Taifa.

Mheshimiwa SUGU anasakwa na polisi kwa kosa la kuwakashifu walinzi wa Bunge

Taarifa kutoka Dodoma zinadai kuwa kuna Askari mmoja ambaye ni miongoni mwa walinzi wa Bunge ameenda kufungua faili Polisi Dodoma na kusema kuwa ametishiwa kupigwa na Mbunge Sugu...
Baada ya kufungua Jalada hilo polisi wamechukua Difenda 6 na wameingia mitaani kumtafuta ili awekwe ndani mpaka kesho ndio afikishwe mahakamani asubuhi.

"Mbowe ni Mjinga na Mpuuzi"...Hii ni kauli ya Kigwangalla bungeni

Mbunge wa Nzega Dr. Kigwangalla, ametumia muda wake karibu wote wa kuchangia Muswada wa Katiba kwa kumshambulia Mwenyekiti wa CHADEMA, Mhe. Mbowe kuwa ni Mjinga, Mpuuzi, ametia aibu aibu 
Kigwangalla  amempongeza  Naibu  Spika  kwa  kumtimua  Mbowe  bungeni  na  kusema  kuwa  kitendo  hicho  kimemshikisha  adabu...
Aidha, mbunge  huyo  wa  Nzega amedai kuwa Mbowe sio Mchaga bali ni mhuni fulani  aliyejivika  sura  ya  Uchaga  kwa  masilahi  yake  binafsi !.
Kigwangalla  alihitimisha  mchango wake  kwa  kudai  kuwa wapinzani wana akili za shetani  zisizovumilika!

Wananchi walilaani Bunge la Tanzania kutokana na vurugu zinazoendelea

Baada ya kuibuka mvutano mkali bungeni jana, kati ya Naibu Spika, Job Ndugai na wabunge wa Kambi ya Upinzani, wasomi, wanaharakati, Chama cha Madaktari Tanzania (Mat), Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), vimesema kinachoendelea sasa ndani ya Bunge ni masilahi ya vyama vya siasa siyo taifa.
 

Walitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuwataka askari kumtoa nje ya Ukumbi wa Bunge, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
 

Mbowe aligoma kukaa chini na kuungwa mkono na wabunge wa upinzani, akishinikiza kuahirishwa kujadiliwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, hadi hapo Zanzibar itakaposhirikishwa, muda mfupi baada ya wabunge kupiga kura na 156 kutaka ujadiliwe na 56 wakitaka uondolewe.
 

Wabunge hao wa upinzani kutoka vyama vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi, juzi walitoka nje ya Ukumbi wa Bunge wakishinikiza kuahirishwa kujadiliwa kwa muswada huo. 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally alisema mvutano huo umejaa masilahi ya wanasiasa kwa kila upande kujaribu kuvutia kwake.
 

“Mvutano ule hauzungumzi kabisa mwafaka wa Bunge la Katiba, binafsi nadhani Bunge la Katiba linatakiwa kuwa na wabunge wapya kabisa na wasiotoka katika chama chochote cha siasa,” alisema
 

Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya alisema: “Marekebisho hayo yanafanyika kwa ajili ya mustakabali wa Muungano wetu, kama Zanzibar hawakushirikishwa, uwekwe utaratibu wa jambo hilo kufanyika ili kipatikane kitu bora, siyo bora Katiba.”
 

Alisema nchi zilizoendelea zimepata mafanikio kwa kuwa zina Katiba nzuri ambazo zinaweza kudumu kwa miaka 100 kabla ya kufanyiwa marekebisho..

Ripoti maalumu ya gazeti la MWANANCHI kuhusu vurugu zilizotokea jana bungeni


Jana, Bingwa wa Dunia wa uzani wa kati (super middle), unaotambuliwa na Shirikisho la Ngumi Duniani (WBF), Francis Cheka alitembelea Bunge baada ya kutwaa taji hilo karibuni na jana hiyohiyo, Bunge hilo lilishuhudia ngumi kavukavu katika vurugu kubwa pengine kuliko zote zilizowahi kutokea katika ukumbi wake. 

Katika masumbwi hayo yasiyo rasmi, Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ anadaiwa kumpiga kichwa Askari wa Bunge na kumchania sare na kung’oa kipaza sauti.
 

Mbilinyi jana alisema alikuwa anatafutwa na polisi huku akisema hilo limemshangaza akidai kwamba yeye ndiye aliyeshambuliwa na askari huyo.
 

Vurugu hizo zilitokea baada ya Naibu Spika, Job Ndugai kuamuru kutolewa nje kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.
 

Katika vurugu hizo Mbilinyi alibebwa juujuu na polisi hadi nje ya ukumbi huku akiwa hana viatu.
 

Pamoja na tafrani hiyo, Ndugai alisema wakati akihitimisha kikao cha Bunge kipindi cha asubuhi kuwa amewasamehe wabunge wote waliohusika na kosa hilo la utovu wa nidhamu na kuwaruhusu kurejea kipindi cha jioni kuendelea na Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. 

Hata hivyo, wabunge wote CUF, NCCR-Mageuzi na Chadema ambao baada ya tukio hilo walitoka nje ya ukumbi, hawakurejea na baadaye walitoa msimamo wa pamoja wakisema hawatashiriki katika mjadala huo.
 

Msimamo huo ulitolewa na Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na Mbunge wa CUF, Habib Mnyaa.
 

Mbowe alisema wameamua kususia majadiliano hayo kuonyesha msimamo wao wa kupinga kupitisha mambo yasiyo na masilahi kwa nchi.
  
“Hatuko tayari kushiriki katika uchakachuaji wa Katiba... Matumizi ya nguvu ya polisi kamwe hayatatupatia Katiba nzuri,” alisema. Alisema kambi rasmi ya upinzani inalaani vikali kitendo cha Ndugai kuruhusu Bunge kunajisiwa kwa kuruhusu polisi kuingia ndani kinyume na kanuni.
 

Mnyaa alisema kitendo cha wadau wa Zanzibar kutoshirikishwa katika kutoa maoni yao katika muswada huo wa marekebisho ni dharau kubwa.
 

Mbatia alisema Tanzania haiwezi kuingia Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kutumia Katiba ya sasa kwa sababu tayari kuna mgongano wa kikatiba kati ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 

Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alimtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kutoa ushahidi kama Rais aliteua wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kulingana na mapendekezo ya taasisi zao.

Kuanza kwa tafrani
Sakata hilo lilianza saa 6:45 mchana muda mfupi baada ya kukamilika kwa kura kuamua kama Bunge liahirishwe au la kutokana na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Mkoani (CUF), Ali Hamisi Seif (CUF). Waliotaka liahirishwe walipata kura 59 na waliokataa 159.

Baada ya Ndugai kutangaza matokeo hayo na kutaka shughuli za Bunge ziendelee, Mbowe aliposimama na kusema ana hoja Naibu Spika alimwamuru akae chini.

Baada ya Mbowe kusisitiza ana hoja na kumwomba Spika amsikilize ndipo Ndugai alipomwamuru atoke nje na alipokaidi alisema:” Naomba askari wote waliopo katika mazingira haya (ya Bunge) waingie ndani ya ukumbi wa Bunge”.

Baada ya kitambo kifupi, Mbowe akiwa bado amesimama alitoa maagizo atolewe nje: “Kiongozi wa upinzani atolewe nje.”

Polisi waliingia ndani ya Ukumbi wa Bunge lakini Wabunge wa Kambi ya Upinzani kwa umoja wao, walimzinga Mbowe asifikiwe na askari hao.

Baada ya kuona polisi wanaelekea kushindwa, Ndugai alitoa maagizo mengine: “Askari hamjaletwa humu ndani kufanya majadiliano mnatakiwa kuhakikisha kiongozi wa upinzani anatolewa nje”.

Alisema yeye ndiye anayeendesha kikao hicho hivyo lazima Mbowe atolewe nje.

Hapo ndipo wabunge hao wa upinzani walipoanza kuimba: “Hatutaki kuburuzwa hatutaki kuburuzwa… hatutaki kuonewa,” huku wakiendelea kumzinga Mbowe.

“Askari wote mliopo humu ndani naomba mnisikilize… Sasa naagiza kwa mara ya mwisho... nasema kiongozi wa upinzani atolewe nje.”

Ngumi zarushwa
Baada ya kauli hiyo ya Ndugai, ndipo polisi walipotumia nguvu hasa kwa Mbilinyi na Mbunge wa Maswa Mashariki (Chadema), Silvester Kasulumbai.

Katika patashika hiyo, inadaiwa kwamba Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alipigwa ngumi ambayo ilimfanya apepesuke hadi sakafuni.

Kilichomponza Mbilinyi ni hatua yake ya kusogelea Siwa. Polisi waliokuwa karibu, walimbeba juujuu hadi nje ya ukumbi.

Wakati akitolewa nje ya ukumbi, alijaribu kujizuia kwa kushika kipaza sauti kinachotumiwa na upande wa upinzani hadi kikang’oka.

Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Mozza Abeid, alivuliwa hijabu katika vurumai hizo wakati polisi walipokuwa wakitumia nguvu ili kumfikia Mbowe.

Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, Mbowe aliamua kutoka nje huku akisindikizwa na polisi pamoja na wabunge wa vyama hivyo na alipofika nje ya ukumbi alipokewa na polisi wa kawaida waliomweka chini ya ulinzi kabla ya kumwachia baada ya ombi la Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini.

Kutokana na hali ya mambo kuwa tete, askari wa Bunge waliwaondoa wageni waliokuwa wamekaa katika kumbi za wageni wakiwamo wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari huku baadhi ya wabunge wa CCM waliokuwa na simu za kisasa za mkononi na kompyuta mpakato (Ipad) wakichukua picha za tukio zima.

Inadaiwa kwamba baada ya kutoka nje ya ukumbi, Mbilinyi alimtwanga ngumi mmoja wa askari waliomtoa kwa nguvu kabla ya kuamuliwa na wabunge na polisi.
Wakati wote huo, wafanyakazi wa Bunge na wageni walionekana wakiwa wamejikusanya katika makundi wakitafakari na kushangaa yaliyokuwa yakitokea.

Balaa lilivyoanza
Akitumia Kanuni ya 69(1), Mbunge wa Mkoani (CUF), Ali Hamisi Seif, alitaka kuahirishwa kwa mjadala wa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013 kutokana na ukweli kuwa Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala ya Bunge ilipaswa kukusanya maoni ya wadau mbalimbali nchini ikiwamo upande wa Zanzibar jambo ambalo halikufanyika wakati wa maandalizi ya muswada huo.

“Ilipaswa sheria hii inapotaka kufanyiwa marekebisho iende tena kulekule Zanzibar lakini jambo la kusikitisha kamati inayohusika na masuala ya Katiba haikwenda. Mimi ni mjumbe wa kamati na tuliitwa Dar lakini ratiba waliyotupa haikuonyesha kama tungekwenda Zanzibar,” alisema. 

Mkosamali naye aliomba mwongozo kwa Spika, akisema kwa kuzingatia matakwa ya kiapo cha Spika au Naibu alipaswa kuendesha Bunge kwa haki bila upendeleo.

“Kanuni inasema Spika ama Naibu Spika ama Mwenyekiti ataendesha shughuli za Bunge kwa haki, uadilifu, bila chuki wala upendeleo wowote kwa kuongozwa na Katiba ya nchi,” alisema na kuongeza: “Kwa kuwa sisi tumekuweka hapo ili uendeshe Bunge kwa uadilifu, usiburuzwe na chama chako na uzingatie miongozo yote kwa wakati. Kwa nini usitumie mamlaka yako kuondoa muswada huu”?

Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenister Mhagama aliomba mwongozo kwamba kwa kuwa bado kuna malalamiko basi waipe Serikali nafasi ya kuthibitisha kwamba majadiliano ya kamati yalikamilika.

Lissu katika kuomba mwongozo wake, alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala, Pindi Chana alilidanganya Bunge alipowasilisha maoni ya kamati kwamba wadau wa muswada huo walishirikishwa jambo ambalo alisema si kweli.

Lissu alisema hakuna Mzanzibari aliyefika mbele ya kamati hiyo kutoa maoni kuhusu muswada wowote.

Hata hivyo, Chana alijibu akisema wadau wa Zanzibar walitoa maoni yao na kukabidhi nyaraka mbalimbali kwa Spika kuthibitisha kauli yake hiyo. Alivitaja vyama vya Jahazi Asilia na ADC kuwa vilihojiwa.

Kwa upande wake, Lukuvi alimshambulia Lissu kwa kauli yake ya juzi kwamba uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete ulikuwa na walakini. “Lissu alisema jana (juzi) kwamba wapo wadau ambao walisema ijapokuwa waliandikiwa barua ya kuwasilisha majina matatu kila moja ili Rais ateue mmoja lakini hakuna mjumbe aliyeteuliwa”.

Alitaja majina ya walioteuliwa kuwa ni Maria Kashonda (Tec), Jesca Mkuchu (CCT), Humphrey Polepole (Civil Society) na Profesa Palamagamba Kabudi (Kundi la Wasomi).

Lukuvi aliwataja wengine waliopendekezwa na taasisi zao na Rais kuwateua kuwa ni Mwamtumu Malale (Bakwata) na Dk Sengondo Mvungi (NCCR) na Profesa Mwesiga Baregu wa Chadema.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Fredrick Werema alisema katika mchakato wa muswada huo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) iliwasilisha maoni yake mbele ya kamati.

Alisema Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi aliwasilisha kwa kamati mapendekezo ya SMZ, Mei mwaka huu na mapendekezo hayo ikiwamo uteuzi wa wajumbe 166 yalizingatiwa.


Waacha muswada, wapiga vijembe
Baada ya kurejea katika kikao cha Bunge cha jioni jana, wabunge wa CCM waliopewa fursa ya kuchangia mjadala wa muswada huo walitumia muda mwingi kuwajadili wabunge wa kambi ya upinzani.

Thursday, September 5

Rais Kikwete na Paul Kagame wakutanishwa na Rais wa Uganda

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ameitisha mkutano wa dharura wa marais wa nchi za Maziwa Makuu (ICGLR), kujadili hali ya usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. 

Rais Jakaya Kikwete ni miongoni mwa waalikwa kwenye mkutano huo ambao pia unatarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.
 

Wakati hali ya usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikidhoofika, katika siku za karibuni, uhusiano wa Tanzania na Rwanda umekuwa wa shaka hasa baada ya Rais Kikwete kuishauri Serikali ya Rwanda kukaa na wapinzani ili kumaliza mzozo uliolikumba eneo la Maziwa Makuu.
 

Rais Kikwete alitoa ushauri huo wakati akiwa katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja wa Afrika (AU), zilizofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia. Mkutano wa leo utafanyika kwenye Ukumbi wa Commonwealth Resort, Munyonyo katikati ya Jiji la Kampala.
 

Kwa mujibu wa taarifa Rais Museveni ameitisha mkutano huo hasa kuzungumzia hatua ya Umoja wa Mataifa kupambana na Kundi la Waasi wa M23.
 

Mbali na viongozi hao wa Tanzania na Rwanda, viongozi wengine wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo wanatoka Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Sudan, na Zambia.

Kesi ya waziri mkuu Mizengo Pinda kutajwa septemba 16 mwaka huu...DPP adai kuwa hiyo ni kesi FEKI

KESI ya kikatiba iliyofunguliwa dhidi ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutokana na kauli yake ya kuruhusu wanaokaidi maagizo ya Dola wapigwe, itatajwa Septemba 16 mwaka huu katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Kesi hiyo ilifunguliwa Agosti mosi mwaka huu na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), dhidi ya Waziri Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakipinga kauli hiyo iliyotolewa bungeni.

Itasikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, likiongozwa na Jaji Kiongozi Fakhi Jundu wengine ni Jaji Augustine Mwarija na Dk Fauz Twaib.

Inadaiwa Mei 20 mwaka huu, Pinda akiwa bungeni katika nafasi yake ya Waziri Mkuu, kinyume na Katiba ya Nchi alitoa kauli ya kuruhusu askari wa Jeshi la Polisi kuwapiga raia ambao hawatatii amri yao kunapokuwa na vurugu.

“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki, unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ndio jeuri zaidi watakupiga tuu na mimi nasema muwapige tu kwa sababu hakuna namna nyingine, eeh maana tumechoka sasa,” sehemu ya hati ya mashitaka iliyonukuu kauli ya Waziri Pinda.

Katika hati hiyo inadaiwa kwa mujibu wa utekelezaji wa Sheria za Jinai, kauli inayotolewa na kiongozi wa nafasi ya Waziri Mkuu, inaonekana kama amri inayopaswa kutekelezwa na vyombo vya Dola kama Polisi, hivyo itachukuliwa kama amri halali na kusababisha waendelee kuwatesa na kuwapiga wananchi wasio na hatia.

Aidha inadaiwa Pinda alivunja ibara ya 100 ya Katiba inayompa kinga mbunge anapotoa jambo lolote bungeni, kwa kuwa yeye hakuzungumza bungeni kama mbunge, bali alikuwa anatoa msimamo wa Serikali yake.

Akizungumza hivi karibuni, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) alisema hakuna uhalali wa mashitaka hayo kwa sababu kauli ya Pinda kuwa pigeni haikuwa piga ua, alichosema ni kupiga wale wasiotaka kutekeleza amri halali na kuna sheria inayoruhusu wananchi kupigwa pindi wanapokaidi amri.

Katiba moto, Chadema, CUF watoka nje

Dodoma.Wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni jana jioni walitoka ndani ya Ukumbi wa Bunge, baada ya kupuuzwa kwa mwongozo wao wa kutaka kuahirishwa kujadiliwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, hadi hapo Zanzibar itakaposhirikishwa.
Wabunge waliotoka bungeni jana yapata saa 12.15 ni kutoka vyama vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi huku Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP, Augustine Mrema akiendelea kubaki ukumbini.
Kitendo cha wabunge hao wa upinzani kilionekana kuwakera baadhi ya wabunge wa CCM, ambao walisikika wakiwakejeli kwa kupiga meza huku wakisema: “Kwendeni zenu, tumewazoea.”
Wakati wabunge hao wakiondoka, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alikuwa akiwasisitiza wabunge wanaobakia wawe watulivu, maana kuna usalama wa kutosha ndani ya ukumbi huo.
“Mnaotoka nimewaona wote na mnanijua,” alisikika Naibu Spika Ndugai akiwatahadharisha wabunge wa upinzani waliosusa mjadala huo.
Wabunge wa CCM waliendeleza vituko ambapo baada ya wapinzani kutoka, wabunge Juma Nkamia (Kondoa Kusini), Hilary Aeshi ( Sumbawanga Mjini) na Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini) walikwenda kukaa katika viti vya kambi ya upinzani.
Kabla ya kutoka kwa wabunge hao wabunge wawili kutoka CUF waliomba mwongozo wa Spika, wakitaka muswada huo kuondolewa ili kuwapa nafasi Wanzanzibar kutoa maoni yao.
Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mohamed Mnyaa (CUF) aliomba mwongozo akitaka muswada huo uondolewe, hadi hapo Wazanzibar watakaposikilizwa.
Alisema kuwa kwa maoni ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala wamesikiliza maoni ya wadau wengi, lakini Zanzibar hawakwenda kuwasikiliza wadau wa eneo hilo.
“Na hili suala zima katika masuala ya katiba linahitaji usawa wa washirika, tunazungumza kitu kinachohusiana na Zanzibar na Tanzania Bara, ili kupata maoni ya nchi nzima kuna uhalali gani wa Bunge hili kuendelea na mjadala huu?” alihoji.
Hata hivyo, alikatizwa na kelele za Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana (CCM), ambaye alitoa taarifa kuwa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ilialika wajumbe mbalimbali ikiwamo Zanzibar.
“Miongoni wa wajumbe walioalikwa ni pamoja na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar pamoja na wadau mbalimbali ambao walikuja mbele ya Katiba,” alisema Pindi ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo.
Mbunge wa Konde, Khatibu Said Alli (CUF), alitaka mwongozo wa Spika kuhusiana na ujumbe mfupi wa maneno ambao aliupokea ukimtisha, kutokana na kitendo chao cha kumuunga mkono Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu.
“Unashabikia mambo ya Tundu Lissu leo, endelea ila mtashughulikiwa,” aliunukuu ujumbe huo na kuongeza kuwa hafahamu umetoka kwa mbunge gani ila wahudumu wa Bunge ndio waliompelekea.
Akijibu mwongozo huo, Ndugai alisema kuwa ni miongoni mwa mambo ambayo anayachukua na kuyafanyia kazi ni suala hilo. Pia Ndugai aliomba ujumbe huo apelekewe.
“Hii ni demokrasia mara nyingi imeshatolewa miongozo, jibu linatolewa hapo hapo ama baadaye na kwa hoja zilizotolewa inakilazimu kiti kupata ushauri hapo baadaye,” alisema Ndugai.
Hata hivyo, baada ya Ndugai kutoa majibu hayo, wabunge wa upinzani waliamua kutoka ndani ya ukumbi huo.
Baada ya wabunge hao kutoka Naibu Spika Ndugai aliendelea na ratiba ya Bunge kwa kusema, jambo hilo halikupangwa kumalizika jana na kwamba litaendelea kujadiliwa hata ikibidi hadi keshokutwa.
Hata hivyo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama kabla ya mjadala kuendelea na kutetea hoja kuwa makundi yote yalisikilizwa tofauti na inavyodaiwa na wapinzani.
“Hata katika marekebisho ya sheria mbili hizi, mimi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tumekutana na viongozi wengi na mawaziri na ndiyo maana tumeahirisha Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni,” alisema.
Alisema, yeye (Lukuvi) alikuwa Mwenyekiti wa ujumbe uliotumwa na Rais kuitisha makundi ya siasa ambayo yalijadili muswada huo. Lukuvi alisema kuwa, pande zote zimeshiriki kikamilifu katika kutoa maoni yao, “kama hizi ni sarakasi za kisiasa mimi sijui.”
Baada ya kutoka, wabunge wa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi walifanya mkutano wa pamoja kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa. Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa, wabunge hao walikubaliana kufanya kila njia kuhakikisha wanazuia mjadala huo leo.
Pia wabunge wa CCM nao walikutana nao mara baada ya Ndugai kuahirisha kikao cha jioni.
Lissu achafua hali ya hewa
Hotuba ya Lissu ndiyo iliyochafua hali ya hewa baada ya kuituhumu Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kwa kutohoji watu wa Zanzibar wakati wakikusanya maoni kuhusu muswada huo.
Alisema licha ya kamati hiyo kukusanya maoni ya taasisi za kidini na za kiraia, taasisi za elimu ya juu na za kitaaluma, vyama vya siasa na asasi nyingine, lakini bado haikwenda Zanzibar kukusanya maoni ya watu wa huko.
“Wadau pekee walioshirikishwa kutoa maoni yao juu ya muswada huu ni Watanzania Bara tu. Wazanzibari hawakupatiwa fursa hiyo na hawakushirikishwa kabisa, licha ya sheria yenyewe kuwa na mambo mengi yanayoihusu Zanzibar,” alisema Lissu.
Pamoja na suala hilo, Lissu alitaka pia Rais wa Jamhuri ya Muungano aondolewe madaraka ya kuteua Wajumbe wa Bunge Maalumu wasiokuwa wabunge au wawakilishi kuwa inavuruga au kuondoa kabisa dhana ya uwakilishi wa wananchi na uhalali wa kisiasa katika mchakato wa Katiba Mpya.
Pia alipendekeza kuongezwa kwa idadi ya wajumbe ifikie 792, kwani Tanzania ina idadi ya watu milioni 45 kwa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012.
Lissu pia alitaka wawakilishi wa Zanzibar waongezwe bungeni, kwa Zanzibar itakuwa na wajumbe 219 kwenye Bunge lenye wajumbe 604, sawa na takriban 36% ya wajumbe wote. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka idadi iwe nusu kwa nusu kati ya pande mbili za Muungano.
Wajumbe 166
Kutakuwa na wajumbe 166 wasiotokana na Bunge na Baraza la Wawakilishi watateuliwa na Rais. Kutakuwa na Wabunge 357 na Wawakilishi 81 na kufanya Bunge Maalumu kuwa na jumla ya wajumbe 604.
Chikawe asoma muswada
Mapema akisoma muswada huo, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe alisema Rais atakaribisha makundi mbalimbali kuwasilisha majina yasiyozidi matatu kila kundi ambao watateuliwa kama wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba. Alisema pia Kifungu cha 27 (2) kitatoa fursa kwa uhuru wa maoni katika mijadala ya Bunge Maalumu na maoni hayo hayatahojiwa mahakamani au sehemu yoyote nje ya Bunge Maalumu.
Chikawe alisema Bunge Maalumu la Katiba litakaa kwa siku 70 mfululizo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili rasimu hiyo. Hicho kitakuwa kikao kirefu zaidi cha Bunge kuwahi kukaa nchini Tanzania.
“Kutokana na unyeti wa suala lenyewe muswada huo unampa nguvu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuongeza siku 20 ili kujadili katiba,” aliongeza Chikawe.
Imeandikwa na Daniel Mjema na Sharon Sauwa - mwananchi 

Breaking news: Freeman Mbowe atimuliwa bungeni

Kiongozi wa kambi rasmi ya Upinzani Bungeni Mh Mbowe ametolewa nje ya Bunge, baada ya kukaidi amri ya Naibu spika Mh Ndugai alipomwamuru akae na Mh Mbowe kutokutii amri hiyo. 

Mh ngudai aliamuru askari wa Bunge kumtoa nje, hata hivyo baadaye wabunge karibu wote wa upinzani walitoka pia isipokuwa Mh. Augustin Mrema wa TLP. 

Upinzani Bungeni unadai muswada wa katiba 2013 unamapungufu.

Wednesday, September 4

‘Mvua za Lowassa’ zagonganisha mawaziri

Dodoma.Suala la mvua za kutengeneza kutoka nchi ya Thailand maarufu kwa jina la ‘Mvua za Lowassa’ liliwagonganisha mawaziri wawili wa Serikali bungeni jana.

Ubishi mkali ulizuka baina ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira, Dk Terezya Huvisa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi waliokuwa wakivutana juu ya ukweli kuhusu teknolojia hiyo.

Wakati Waziri Huvisa akisema kwamba hakuna utaalamu wa aina hiyo, Lukuvi alisimamia kumpinga na kusisitiza kuwa jambo hilo lipo.

Suala la mvua hizo lililetwa nchini na aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa mwaka 2007, baada ya kufanya ziara Thailand ambako alivutiwa na utaalamu wa kutengeneza mvua na kuahidi kuuleta nchini.

Kutokana na mvutano wa mawaziri hao, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM), alipewa dakika moja na Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama kutoa ufafanuzi ambapo aliunga mkono hoja ya Lukuvi.

Malumbano hayo yalisababishwa na swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Lyimo ambaye alihoji mpango wa kutengeneza mvua ulipoishia kwa kuwa Serikali imekuwa kimya.

“Sasa ni miaka takriban sita au saba tangu Serikali ilipokuja na mpango wa kutengeneza mvua ambao iliuchukua kutoka nchi za wenzetu, mpango huo umefikia wapi?” aliuliza.

Akijibu swali hilo, Waziri Huvisa alisema: “Mimi ni Rais wa Mazingira wa Afrika, nasema hakuna kitu kama hicho, si Marekani wala Malaysia ambao wanaweza kutengeneza mvua, hayo ni mabadiliko ya tabianchi tu.”

Waziri Lukuvi alionyesha kutokuridhishwa majibu hayo, ndipo aliposimama kutoa ufafanuzi na kusema Lowassa alikwenda Thailand ambako kuna utaalamu huo na kusisitiza kwamba upo na bado unaendelea kutumika hata Ujerumani wanakotumia mitambo ya kijeshi kusambaratisha mawingu.

Alisema kilichokwamisha mpango huo nchini ni ufinyu wa bajeti ya Serikali.

Baada ya majibu hayo, Lowassa alisimama akitaka kutetea wazo lake. Hata hivyo, kabla ya kumruhusu, Mhagama alimwomba akae chini kwanza ili atoe maelekezo.

“Mheshimiwa Lowassa, yeye siyo waziri na hivyo hastahili kutoa majibu ya Serikali, lakini kwa kutumia kanuni zetu bungeni kuhusu kutengeneza utaratibu mzuri wa kuongoza Bunge, naomba Lowassa usimame sasa walau kwa dakika moja au mbili utoe ufafanuzi,” alisema Mhagama.

Aliposimama Lowassa alizungumza kwa ufupi; “Nakushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kukazia tu kuwa jibu lililotolewa na Mheshimiwa Lukuvi ndilo jibu sahihi.”

Majibu hayo yalisababisha Bunge kulipuka kwa shangwe.

Mara baada ya majibu ya Lowassa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza naye alisimama akitaka kutoa maelezo. Hata hivyo, Mhagama alisema inatosha na kuwaagiza mawaziri hao kukutana kuliangalia jambo hilo badala ya kuwa na majibu kinzani.

Awali, katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Rachel Mashishanga alitaka kujua ni kwa nini Serikali isirasimishe utaalamu wa kuleta mvua kutoka kwa waganga wa jadi walioko Mikoa ya Katavi na Rukwa ili maeneo yanayokabiliwa na ukame yapate mvua?

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, alipinga mpango huo na kusema hakuna kitu kama hicho isipokuwa wapo watu wenye utaalamu wa kuangalia mawingu yanayoendana na mvua.

Alisema watu wote wanaosema kuwa wanaweza kutengeneza mvua kwa imani za kishirikina ni waongo na hivyo hawapaswi kuaminiwa.

Alisema siyo wakati mwafaka kwa Serikali kushinikizwa kurasimisha utaalamu huo wa kuleta mvua kwa kuwa hakuna tafiti zozote zilizofanyika na kuthibitisha kuwapo kwake.

Wabunge Z’bar wakwamisha Muswada wa kura za Maoni - mwananchi

Dodoma. Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni wa mwaka 2013 uliokuwa ujadiliwe katika mkutano wa 12 wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma, umeondolewa na sasa utajadiliwa Bunge lijalo.

Habari za uhakika zilizopatikana jana, zilisema kwamba kuahirishwa huko kumetokana na wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge wanaotoka Zanzibar kupinga vikali kura ya maoni kupigwa visiwani humo kwa kuwa tayari huko kuna sheria hiyo.

Muswada huo ulikuwa ujadiliwe na wabunge katika kikao cha Bunge kinachoendelea ukitanguliwa na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013.

“Ukisoma huu Muswada unasema kura hiyo itapigwa Tanzania Bara na Zanzibar sasa sheria hii ina apply vipi (inatumikaje) Zanzibar wakati kule tuna sheria yetu tayari?” alihoji Mbunge mmoja wa Zanzibar.

Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alipoulizwa jana, alithibitisha kuondolewa kwa muswada huo wa kura ya maoni kusema na utakaojadiliwa ni ule wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba pekee.

“Bunge litaahirishwa Ijumaa (keshokutwa) na ni kweli huo Muswada wa Kura ya Maoni umeondolewa kwa sababu bado uko kwenye ngazi ya kamati,” alisema Joel.

Alipoulizwa sababu za kuondolewa kwa muswada ambao ulishaingizwa kwenye ratiba ya Bunge, alitaka swali hilo aulizwe Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.

Waziri Lukuvi alithibitisha kuondolewa kwa muswada huo na kusema utajadiliwa katika Mkutano wa Bunge wa Oktoba.

“Ni kweli muswada huu hautajadiliwa na Bunge hili bado kuna mashauriano yanaendelea kati ya SMZ (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

Kwa upande wake, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alisema wabunge wa Zanzibar ndiyo waliokwamisha muswada huo kutokana na mgongano wa sheria.

“Wao wanasema masuala ya kura ya maoni siyo ya Muungano kwa sababu wao tayari wana sheria yao ya kura ya maoni. Sasa wanahoji inakuwaje sheria hii itumike tena hadi Zanzibar? Huu ni mgongano,” alisema.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), alisema tangu mwanzo aliliona suala hilo na kuitahadharisha Kamati ya Bunge kwamba mapendekezo hayo yana upungufu.

Muswada pekee uliobaki wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba unatarajiwa kuwasilishwa leo huku ukitarajiwa kuibua mjadala mzito kutokana na misimamo ya baadhi ya wabunge.

Muswada huo unawasilishwa wakati CCM kikiwa kimeweka msimamo wa kupinga baadhi ya mambo katika Rasimu ya Katiba.



Yanayotarajiwa kuzua mjadala

Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe amekiri kupokea mapendekezo kutoka kwa wabunge na hasa kwenye Sheria ya Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba akisema wametaka kuangaliwa upya kwa kipengele cha Kamati ya Uteuzi ya viongozi wa Bunge la Katiba. Alisema sasa wataweka sifa za mwombaji wa nafasi hizo na wasiokuwa nazo hawatagombea.

Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba unataka wawakilishi kutoka makundi ya jamii kuwa 166 katika Bunge la Katiba, lakini wabunge wanataka idadi iwe 200.

Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) alisema uzoefu katika nchi nyingine unaonyesha kuwa mabunge ya Katiba hushirikisha watu wengi ili kupata uwakilishi mpana tofauti na mapendekezo yaliyotolewa.

Mkosamali ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, alisema ni vyema sheria ikasema wajumbe wa Bunge hilo watatoka katika taasisi zipi.

Kifungu kingine ni kile kinachohusu Kamati ya Uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu wake ambao kwa mujibu wa muswada itaundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (AG) na yule wa SMZ, Waziri wa Katiba na Sheria Tanzania Bara na Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar na Kiongozi Rasmi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Mkosamali alisema muswada huo wa Mabadiliko ya Katiba unasema mwenyekiti wa muda atakuwa Spika wa Bunge lakini akataka: “Mwenyekiti wa muda atokane na Chama cha Majaji wastaafu maana wao hawafungamani na upande wowote.”

KASHFA YALIKUMBA JESHI LA POLISI TENA-CCTV ZAZIMWA KURUHUSU UJAMBAZI

SIKU chache baada ya tukio la wizi mkubwa wa fedha katika Benki ya Habibu mjini Dar es Salaam, siri nzito zimeanza kuvuja kuwa polisi wanadaiwa kuhusika katika tukio hilo kwa kuhujumu kamera za usalama za CCTV zinazomilikiwa na jeshi hilo.

Katika tukio hilo, watu wanaodaiwa kuwa majambazi walipora dola za Marekani 20,000 ambazo ni sawa na Sh milioni 32 za Tanzania.

Katika tukio hilo, Polisi Mkoa wa Ilala inamshikilia askari mmoja kwa kosa la kuhusika katika tukio hilo kutokana na kushindwa kuchukua hatua za haraka wakati tukio linatokea.

Habari za uhakika kutokana ndani ya jeshi hilo, zinasema siku ya tukio polisi waliokuwa zamu kuongoza mitambo hiyo, kwa namna moja au nyingine wanadaiwa kufanya hujuma hiyo, kwa lengo la kupoteza mawasiliano na maeneo mengi ya polisi.

Chanzo chetu hicho, kiliongeza kuwa siku ya tukio eneo lote la mzunguko wa barabara ya Uhuru na maeneo ya jirani na Kiwanda cha Bia Tanzania (TBL), sehemu zote hazikuwa na huduma ya kamera za usalama, jambo ambalo si la kawaida kutokea.

“Hatua iliyofikia sasa ni mbaya, huwezi amini siku ya tukio kamera za CCTV zinazotumiwa na polisi zilizimwa kabisa, kitendo hiki kilisababisha polisi makao makuu wasijue nini kinachoendelea pale.

“Ndiyo maana utaona kuna askari mmoja anashikiliwa katika tukio lile, haiwezekani kituo kikuu kishindwe kubaini uwapo wa tukio hili, wakati kuna mawasiliano ya kutosha, umefika muda wa kulisafisha jeshi letu kwa kasi,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo hicho, kilisema mitambo ya kamera hizo, ilizinduliwa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa mwaka 2004 na imekuwa ikifanya kazi bila matatizo yoyote.

“Nimekuwapo hapa tangu mwaka 2004, kamera hizi zilipozinduliwa rasmi na hazijawahi kuharibika hata siku moja, iwe siku ya tukio zisifanye kazi,” kilihoji chanzo chetu.

Askari aliyekamatwa katika tukio hilo, anadaiwa anafanya kazi katika kituo cha Oysterbay Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alithibitisha kukamatwa kwa askari huyo.

Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alipoulizwa na MTANZANIA jana, alisema ameipokea taarifa hiyo na wanaifanyia kazi haraka iwezekanavyo.

“Taarifa hii tumeipokea, tunaifanyia kazi haraka sana ili kupata ukweli, naomba tuwe na subira,” alisema kwa kifupi Kamishna Kova.

Alisema bado polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba watu waliokamatwa watafikishwa mbele ya vyombo vya dola.

Monday, September 2

KINGUNGE AMSHANGAA KAGAME



MWANASIASA mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru, amejitosa katika mgogoro wa kidiplomasia uliopo kati ya Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

Akizungumza na MTANZANIA Jumatatu mwishoni mwa wiki nyumbani kwake Kijitonyama jijini Dar es Salaam, Kingunge alimshangaa Rais Kagame kwa jinsi alivyouchukulia vibaya ushauri wa Rais Jakaya Kikwete, aliompa juu ya waasi wa nchini humo.

Alisema kwamba, kilichotolewa na Rais Kikwete juu ya waasi hao, ulikuwa ni ushauri ambao ulilenga kurejesha amani nchini Rwanda na wala si vinginevyo.

“Kutoelewana baina ya nchi jirani si jambo dogo na jema, hivyo si vizuri hali hiyo ikaachwa iendelee kwa muda mrefu bila kupatiwa suluhu.

“Nashauri jitihada zote zifanyike ili sintofahamu hii baina yetu na Rwanda ipate suluhu haraka iwezekanavyo, kwa sababu sisi ni majirani.

“Ushauri alioutoa Rais Kikwete kwa Rwanda ulikuwa sahihi na nauunga mkono, lakini maadam wenzetu Rwanda hawakuupokea vizuri, jawabu ni kufanya juhudi za kidiplomasia ili mtafaruku huo uishe.

“Hata hivyo, pamoja na mambo mengine, mgogoro huo hauna sababu ya kututoa au kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa sababu nchi zote tano zinahitajiana na tuna wajibu kwa wananchi wetu kushirikiana kwa faida ya nchi zote husika,” alisema Kingunge kwa kifupi.

Akizungumzia vyama vya upinzani nchini, Kingunge alisema safari yao katika kuchukua dola bado ni ndefu kutokana na kutokuwa na mtandao unaofikika nchi nzima.

Alisema vyama vikubwa vya upinzani vikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Wananchi (CUF), bado viongozi wake wana tabia ya kuhutubia na kuondoka badala ya kujenga chama chenye mtandao.

“Tatizo la vyama vyetu vya upinzani nchini, lilianza tangu mwaka 1992 vilipoanzishwa na tangu wakati huo, havijaweza kujirekebisha, viongozi wake wanafikiria kwenda Ikulu tu na hivyo wanajielekeza kwenye kushinda urais na kusahau nafasi nyingine.

“Lakini, ili kufika Ikulu, lazima uwe na watu wa kukufikisha huko na watu hao ni wanachama kutoka kwenye vijiji, kata, wilaya na taifani. Kama kule kwenye watu hao hawajaweza kujizatiti, suala la kwenda Ikulu litawachukua muda mrefu.

“Ili kuwa na nafasi ya kushinda uchaguzi, chama lazima kiwe kimejikita kwa umma wa wananchi na siyo kuzungukazunguka,” alisema Kingunge.

Alisema mikutano ya hadhara kwa vyama ni sahihi kufanyika na kwamba ndiyo kazi ya vyama vya siasa, kwani chama kinapata nafasi ya kueneza sera na kujipima kisiasa kupitia mikutano hiyo.

Pamoja na hayo, alisema mvuto huo wa kisiasa huwa si wa wakati wote kwani inawezekana chama kina tabia ya kuzungumza juu ya masuala ambayo wananchi wanapenda kuyasikia hata kama hawakubaliani nacho.

“Kupata watu wengi kwenye mkutano haimaanishi kwamba vyama vingine havipendwi au havikubaliki, inawezekana vyama vingine vikawa vinapendwa na kukubalika, lakini havina tabia ya kufanya mikutano.

“Lakini, kwa ujumla wake, ni kwamba vyama vyote hivyo vinaweza kushinda urais kama tu vinashinda kwenye majimbo ya ubunge, ila kwa hali jinsi ilivyo hivi sasa, safari yao bado ni ndefu hawawezi kuchukua nchi,” alisema mwanasiasa huyo.

Sakata la Mansour
Akizungumzia kuvuliwa uanachama kwa aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi Kisiwani Zanzibar, Mansoor Yussuf Himid, Kingunge alisema mwanasiasa huyo alistahili kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), alistahili adhabu hiyo.

“Chama kina sera ambazo tunazitekeleza na tunaziheshimu, tuna katiba inayotuongoza na kwa mujibu wa katiba yetu, tuna vikao vinavyofuatilia uadilifu wa wanachama wetu.

“Uadilifu huo ni pamoja na kuheshimu Katiba na sera za msingi wa chama na vikao vya mara kwa mara, kwa hiyo, mwanachama anayeonekana kwa kauli na vitendo vyake yuko kinyume na matakwa ya Katiba, Halmashauri Kuu ina madaraka ya kumvua uanachama, uongozi au kumpa adhabu nyingine.

“Kwa hiyo, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ilikuwa sahihi, hivi ni nani asiyemfahamu Mansour kwamba ni CUF? Hili suala liko wazi familia yao nzima ni wanachama wa CUF, kwa hiyo si ajabu kwake.

“Mimi nastaajabu kwa sababu, kwanza baba yake alikuwa miongoni mwa watu 14 waliotekeleza Mapinduzi ya Zanzibar na hakuwa mkorofi, sijui imekuwaje Mansour naye akabadilika maana ninavyomfahamu hakuwa hivi,” alisema Kingunge.

Agosti 26, mwaka huu, kikao cha NEC, kilimvua uanachama Mansour kwa kushindwa kusimamia malengo ya CCM na kutekeleza masharti ya uanachama.

Msigwa amkalia kooni Waziri Kagasheki



Dodoma. Msemaji wa kambi ya upinzani wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa amesema kuna ugawaji holela wa maeneo katika Mamlaka ya Uendelezaji Bonde la Ngorongoro (NCAA) kwa kampuni za kitalii na kudai kwamba Waziri wake, Balozi Khamis Kagasheki anahusika.

Msigwa aliwaambia waandishi wa habari katika ofisi za kambi hiyo mjini Dodoma jana kuwa Balozi Kagasheki amerudia makosa yaliyofanywa na mtangulizi wake, Ezekiel Maige.

Hata hivyo, Waziri Kagasheki amejibu tuhuma hizo akisema hana mamlaka kisheria ya kugawa vitalu kama inavyodaiwa na kwamba kilichotolewa ni vibali kwa ajili ya kambi za watalii (tented camps).

“Katika Kamati ya Vitalu tulisema kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa ugawaji na Maige alipata wakati mgumu lakini huyu aliyemrithi hajabadili kitu,” alisema Msigwa, ambaye pia ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema). Mchungaji Msigwa alisema kampuni mbili za Leopard Tours na Masai Sanctuaries zilipewa vitalu vya utalii ndani ya eneo la NCAA kinyume na mpango wa miaka mitano wa ugawaji wa mamlaka.

Kwa kawaida wataalamu wa uhifadhi na uongozi NCAA hukutana kila baada ya miaka mitano ili kugawa vitalu katika eneo la Ngorongoro. Msigwa alisema Waziri Kagasheki alitakiwa kupata ushauri kutoka uongozi wa Ngorongoro kabla ya kufikia uamuzi wa kutoa vitalu hivyo.

“Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo nyaraka zinazoonyesha kuwa kampuni hizo zilipewa vitalu vya utalii vya Ndutu na Oloololo ambavyo havikuwa katika mpango wa ugawaji kama inavyotakiwa kisheria.”

Alidai kuwa katika moja ya barua ambazo kambi hiyo inazo, Waziri Kagasheki aliiandikia Kampuni ya Leopard Tours akiitaarifu kuwa tayari ameiagiza NCAA ipewe kitalu chenye ukubwa wa hekari tano.

“Alielekeza mamlaka kuipa kampuni hiyo ekari tano kwa Dola za Marekani 30,000 (Sh48 milioni) ambacho ni nusu ya kiwango cha kawaida cha Dola 60,000 (Sh95 milioni) kwa ekari 10,” alisema Msigwa.

Barua hiyo ya Julai 17, 2013 yenye kumbukumbu namba CAB.315/319/01B iliyosainiwa na Balozi Kagasheki inauelekeza uongozi wa NCAA kumpa viwango hivyo.

Waziri Kagasheki alisema alitoa punguzo hilo kwa kampuni hiyo ya Leopard si kwa ajili ya kitalu, bali tozo kwa ajili ya kambi yake ya watalii na kueleza kushangazwa na tuhuma zilizoelekezwa kwake akisema sheria haimruhusu kugawa vitalu hadi awasiliane na kamati husika. Alisema aliwapunguzia ada hiyo Leopard kwa kuwa walipewa mita za mraba 29.7 na kudaiwa Dola 60,000. Alisema wangetakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha kama wangepewa mita za mraba 60.

“Niliona hawa jamaa hawajatendewa haki kwani walitozwa ada kubwa kwa ajili ya nusu eneo,” alisema na kumtaka Msigwa kutoa ushahidi wa barua kama amegawa vitalu. Balozi Kagasheki alisema ugawaji wa vitalu utafanyika keshokutwa atakapokutana na kamati husika.

Haya hivyo, Mchungaji Msigwa alisema waziri alifanya uamuzi huo bila kuzingatia sheria na kanuni za ugawaji wa vitalu, pia akivunja sheria kwa kufanya uamuzi moja kwa moja na kampuni hiyo na kushusha viwango vilivyowekwa kisheria bila kutoa tangazo la Serikali.

Mke wa Kagasheki atuhumiwa

Mbali na tuhuma hizo, Mchungaji Msigwa pia amemtuhumu Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Catherine Magige akidai kwamba ametumia ushawishi wa mumewe, Balozi Kagasheki kupewa msaada wa Sh10 milioni na NCCA kupitia taasisi yake ya Catherine Foundation Development Ltd kinyume cha kanuni inayotaka isizidi Sh2 milioni.

“Mradi huu ulipewa fedha hizo huku dokezo la maombi ya msaada huo ukionyesha kuwa watendaji wa NCAA walitoa mapendekezo mara mbili kuwa hakuna bajeti ya kusaidia msaada huo,” alisema.

Msigwa alisema Kaimu Mhifadhi wa NCAA alinukuliwa akisema fungu la msaada halina fedha ya kutosha na kwamba Magige ashauriwe kusubiri mpaka mwaka wa fedha ujao 2013/2014... “Dokezo hili lilisainiwa tarehe 14.12.2012 lakini jambo la kushangaza na la kutia walakini... Mhasibu aliagizwa ilipwe kiasi hicho.”

Alisema pamoja na baadhi ya watendaji kueleza kwamba NCAA haikuwa na fedha, Kaimu Mhifadhi Mkuu alitoa agizo Juni 18,2013 la kutoa kiasi cha Sh10 milioni kwa taasisi hiyo.“Katika hili kuna mgongano mkubwa wa masilahi kwa sababu huwezi kumtenganisha Mheshimiwa Kagasheki na kazi zake za uwaziri na hii ya Catherine Foundation ambaye ni mke wake,” alisema.

Akizungumzia suala hilo, Balozi Kagasheki alikanusha vikali tuhuma hizo na kusema hakuwa na mamlaka ya kuishinikiza NCAA... “Nisingependa kuzungumzia masuala ya mke wangu maana kuna mambo mazito ya nchi ya kuzungumzia. Ila siwezi kushinikiza taasisi iliyo chini yangu itoe Sh10 milioni pengine labda ingekuwa Sh1 milioni.”

Kagasheki alisema hamshangai Mchungaji Msigwa kwani amekuwa na tabia ya kumzushia mambo na kukumbusha alivyoshinikiza ajiuzulu katika kikao kilichopita cha bajeti.

Naye Magige alipoulizwa kuhusu fedha hizo, alikiri taasisi yake kupewa lakini akasema walifuata taratibu zote katika kuomba kama wanavyofanya katika taasisi nyingine.

“Sisi tunaomba misaada katika taasisi mbalimbali na katika hili tulifuata taratibu zote na wakaamua watupe Sh10 milioni. Tungekataa wakati wanafunzi hawana madawati?” alihoji Magige.

Alisema kutolewa kwa fedha hizo kulikuwa hakuna shinikizo lolote kutoka kwa Waziri Kagasheki na kwamba kama ingekuwa hivyo, taasisi hiyo ingepewa fedha nyingi zaidi.

Alieleza kushangazwa na kauli za Msigwa dhidi yake na taasisi yake ambayo alisema imekuwa msaada mkubwa kwa shule za msingi Arusha ambazo zimekuwa na upungufu wa madawati.