Thursday, November 30

WAZIRI MBARAWA ATAKA BODI YA TPA KUFANYA MAAMUZI KWA WAKATI


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa wajumbe wa Bodi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA), na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Mhandisi Deusdedit Kakoko, kukamilisha Skana mpya (haipo pichani), ambayo inajengwa kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo inayoingia Bandarini hapo ambayo haijakamilika hadi sasa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amesema anasikitishwa na utendaji wa Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), kutofanya maamuzi kwa wakati hali ambayo inachangia malalamiko kuongezeka Bandarini hapo. Aidha, Mbarawa amesema Serikali inapeleka Naibu Mtendaji Mkuu mpya wa shughuli za Uendeshaji Bandarini hapo kutokana na aliyekuwepo kushindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo.

Profesa Mbarawa amesema hayo leo wakati wa ziara ya kushtukiza aliyoifanya bandarini ikiwa ni siku chache baada ya Rais John Magufuli, na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, kufanya ziara ya kustukiza na kubaini madudu bandarini hapo.   Ziara ya Waziri Mbarawa ni mwendelezo wa ziara mbalimbali bandarini hapo kubaini uendeshaji na utendaji wa shughuli zinazotolewa na Mamlaka hiyo.
Muonekano wa Skana mpya ambayo inajengwa kwa ajili ya ukaguzi wa mizigo inayoingia Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ambayo haijakamilika hadi sasa.

“Nimelazimika leo kuwaita Watendaji na Bodi ya TPA ili kuwaeleza kasoro zenu ambapo inaonesha wazi kuwa asilimia kubwa ya mambo yanayotokea humu ni kuwa mnakuwa wazito katika kutoa maamuzi”, amesema Profesa Mbarawa.   Amesema katika bandari hiyo ipo mizigo ya kahawa ambayo imefika bandarini tangu mwaka 2014 huku kukiwa hakuna sababu za kueleweka za wenye mali kutochukuwa mizigo yao.  

Profesa Mbarawa amesema hahitaji wasaidizi ambao wanakaa katika vikao na kulipana posho ila wanapaswa kufanya kazi ya kuangalia shughuli zote za bandari.   “Kama hamtabadilika nitaendelea kuja katika bandari hii ili kuchukua hatua pale ambapo inaonekana kwani haipendezi kila kukicha malalamiko kutokea,” amesisitiza Waziri Mbarawa.  
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Profesa Ignatus Rubaratuka (Wakwanza kushoto), wakati akikagua shehena ya kahawa iliyohifadhiwa Bandarini hapo kwa muda mrefu.

Aidha, Waziri Mbarawa ameitka bodi na menejimenti kuhakikisha kuwa inatatua changamoto iliyopo katika bandari ya kushusha na kupakia mizigo kutoka Zanzibar na kuingia Tanzania Bara ambapo wafanyabiashara wanalalamikia utaratibu unaotumika kuwahudumia.   Amesema haingii akilini kuona mizigo inayotoka au kwenda Zanzibar kutozwa kodi baada ya masaa huku inayotoka nje ya Tanzania ikitozwa baada ya siku saba.   

Kuhusu ujio wa Naibu mtendaji Mkuu mpya Mbarawa aliitaka Bodi na menejimenti kumpa ushirikiano ili aweze kutoa matokeo chanya kwenye bandari.   “Tunaleta Naibu Mtendaji Mkuu mpya ambaye atasimamia operesheni, naomba apewe ushirikiano ili kusaidia Serikali huyu ambaye anakaimu tunamuondoa ameshindwa kwenda na kasi yetu,” amefafanua Profesa Mbarawa.  
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akikagua shehena ya kahawa iliyohifadhiwa tangu mwaka 2014 hadi sasa katika ghala iliyopo katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Dar es Salaam. Pembeni yake ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka hiyo, Profesa Ignatus Rubaratuka akishuhudia ukaguzi huo.

Akizungumza baada ya ziara hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya TPA Ignas Rugaratuka, amesema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa wanaitendea haki nafasi waliyopewa kwa kusimamia mabadiliko ndani ya bandari.   Amesema tangu waingie wamekuwa wakipambana kuhakikisha kuwa mapungufu ya TPA yanaisha ambapo wamefanikiwa kurekebisha kwenye utawala kwa kutoa mafunzo kwa watumishi na kuzuia wizi ambao ulikuwa umekithiri.   

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, amesema kuwa tangu aingie katika mamlaka hiyo wamekuwa wakifanya jitihada za kurekebisha mapungufu na kumuahidi waziri kuwa ataongeza jitihada zaidi.

  “Kama ni mabadiliko tumefanya makubwa sana hasa katika utawala na uongozi ila kila anayehusika katika sekta hiyo anapaswa kutoa msaada,” amesema Mkurugenzi Mkuu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alipofika Bandarini hapo leo wakati wa ziara ya kushtukiza kuangalia uendeshaji wa huduma Bandarini hapo.

CHINA YAAHIDI KUFADHILI UJENZI WA RELI KWA KIWANGO CHA KIMATAIFA (SGR)

BALOZI wa China hapa nchini, Wang Ke amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango na kuahidi kuwa nchi yake iko tayari kushawishi taasisi za fedha ikiwemo Benki ya EXIM ya nchini humo kushiriki ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa baada ya kufanyika kwa upembuzi yakinifu wa mradi huo.

Alisema kuwa kutokana na ukubwa wa mradi huo, unaokadiriwa utagharimu Dola za Marekani bilioni 7.6 hadi kukamilika kwake, utahitaji kufanyiwa upembuzi yakinifu ili kukidhi masharti ya kupata mkopo kupitia Benki ya Exim na taasisi nyingine zitakazotaka kujenga mradi huo muhimu. 

“Mradi huu ni muhimu na wa kihistoria kwa nchi hizi mbili, China ingependa kuona mradi huo unaboreshwa ili uweze kutoa huduma ya kusafirisha mizigo na abiria na kwamba kuimarika kwake kutaokoa miundombinu ya barabara kwa kuwa shehena kubwa ya mizigo itasafirishwa kupitia reli hiyo.

Aidha, Balozi Ke alisema kuwa nchi yake inasubiri pia kukamilika kwa taratibu za ndani kati yake na Tanzania ili mradi wa reli ya TAZARA uanze  ili kuboresha usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria kati ya Tanzania na Zambia pamoja na nchi za maziwa makuu.

Balozi Ke alitumia fursa hiyo kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kukusanya kodi, kusimamia matumizi adili ya fedha za umma, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kupambana na rushwa.

Akizungumza mara baada ya mazungumzo na mgeni wake, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango alisema kuwa Serikali imeridhia uamuzi wa China wa kufanya upembuzi yakinifu wa mradi huo wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR) ili China kupitia taasisi zake iweze kujenga sehemu ya mradi huo.

“Tayari mradi umeanza kujengwa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, kwahiyo kujitokeza kwa China kutaka kufadhili ujenzi wa mradi huo kutasaidia kukamilisha mradi huo muhimu kwa haraka na kwa wakati” Alisema Dkt. Mpango.

Alisema pia kuwa China imeonesha nia ya kusaidia kuujenga na kuupanga mji wa Dodoma kutokana na nchi hiyo kuwa na uzoefu wa kupanga miji ambapo nchi hiyo imeonesha nia ya  kujenga miundombinu ya elimu, barabara, uwanja wa ndege wa kimataifa-Msalato, kujenga mfumo wa maji safi na maji taka pamoja na majengo ya kisasa.

Kuhusu biashara, Dkt. Mpango alisema wamekubaliana kuwa China itaisaidia Tanzania kukuza kiwango cha biashara ambapo takwimu zilizoko zinaonesha kuwa urari wa biashara kati ya nchi hizo unaonesha kuwa Tanzania imekuwa ikinunua bidhaa nyingi kutoka nchini humo kuliko inavyo uza bidhaa na huduma zake.

“Mwaka 2016 Tanzania iliuza China bidhaa na huduma zenye thamani ya Dola za marekani milioni 460 wakati China iliuza hapa nchini bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.2, kiwango ambacho ni kikubwa karibu mara 5 ya kile tulichowauzia” Alisema Dkt. Mpango.

Ili kuvutia Sekta ya utalii, Tanzania imeiomba China kuanzisha safari ya ndege wa moja kwa moja kutoka China hadi Tanzania ili kuvutia watalii wengi kutoka nchini humo na kwamba utaratibu utafanyika ili Mamlaka ya usafiri wa anga iweze iratibu na kusaini makubaliano ya ushirikiano na hivyo kufanikisha jambo hilo.

“China imeandaa maonesho makubwa ya uwekezaji na biashara ya bidhaa na huduma mbalimbali mwezi Novemba, 2018, hivyo wafanyabiashara wa Tanzania pamoja na  Bodi ya Utalii nchini wahakikishe wanashiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo ili kutumia nafasi hiyo kujitangaza” Alisistiza Dkt. Mpango.

Aidha, Dkt. Mpango alieleza kuwa Balozi Wang Ke, amesema kuwa Nchi yake itashiriki katika ujenzi wa miradi ya bandari ili kukuza masuala ya usafiri kwa kuboresha bandari za Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Bagamoyo, Dar es Salaam, Mtwara na katika Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.

Waziri huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alitoa wito kwa wawekezaji kutoka China na nchi nyingine kuja kuwekeza nchini katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaipeleka nchi katika uchumi wa viwanda.

Miradi mikubwa ambayo China imewekeza na kufadhili hadi sasa hapa nchini ni Reli ya TAZARA, Kiwanda cha Urafiki, ujenzi wa barabara, majengo, ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi dar es Salaam, Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Jijini Dare Salaam, Ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na miradi mingine kadha wa kadha.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati),  Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke (wa pili kulia), Mwakilishi wa masuala ya Uchumi na Biashara wa Ubalozi wa China Bw. Lin Zhiyong (wa pili kushoto) pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango  wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa Mkutano kati ya pande hizo kuhusu Biashara, uwekezaji na ushirikiano, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Kulia) na mgeni wake Bi. Wang Ke, wakitoka nje ya Jengo la Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa mkutano kati yao uliohusu masuala mtambuka ya ushirikiano kati ya Tanzania na China.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) na Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke,  wakiagana   baada ya kumalizika kwa Mkutano kati yao ambapo balozi huyo aliahidi kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kati nchi hizo mbili, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam. 
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akiagana na Mwakilishi wa masuala ya Uchumi na Biashara wa Ubalozi wa China  nchini Tanzania Bw. Lin Zhiyong baada ya kumalizika kwa Mkutano kati ya Waziri huyo na Balozi wa nchi hiyo Bi. Wang Ke (hayupo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
 Kamishina wa Fedha za Nje Bw. John Rubuga (kushoto) na Afisa anayeshughulikia masuala ya nje katika dawati la China Bw. Alfonce Mayala kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wakifuatilia kwa makini majadiliano kati ya Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke,  na Waziri wa Fedha na Mipango (hawapo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), wa pili kulia akieleza kuhusu fursa zilizopo katika Sekta ya Utalii wakati wa  Mkutano kati yake na Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke, (hayupo pichani), Jijini Dar es Salaam, kulia ni Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. John Rubuga.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), wa tatu kulia akiwa katika mkutano na  Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke (wa pili kushoto) ambapo walikubaliana kuendeleza ushirikiano katika Biashara na uwekezaji kwa manufaa ya pande hizo mbili, mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akieleza kuhusu kuwa na uwiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China kwa manufaa ya pande hizo mbili wakati wa mkutano kati yake na Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke, (hayupo pichani), Jijini Dar es Salaam.
 Balozi wa China hapa Nchini Bi. Wang Ke, (katikati) akiongoza maafisa wake wa ubalozi wa nchi hiyo hapa nchini wakati wa mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), Jijini Dar es Salaam.
Balozi wa China hapa nchini, Bi. Wang Ke, akisisitiza jambo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), Jijini Dar es Salaam.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango)

RAIS DKT. MAGUFULI AMTEUA BI. STELLA CHAGI KUWA MSAJILI WA MABARAZA YA ARDHI NA NYUMBA WA WILAYA

KAMANDA WA POLISI MKOA WA MWANZA AKANUSHA TAARIFA ILIYOPO KATIKA GAZETI LA MWANANCHI LA TAREHE 30/11/2017

LEO TAREHE 30.11.2017 KAMANDA WA POLISI MKOA WA MWANZA NAIBU KAMISHINA WA POLISI AHMED MSANGI (PICHANI), AMEKANUSHA TAARIFA ILIYOPO KATIKA GAZETI LA MWANANCHI LA TAREHE 30/11/2017, TOLEO NAMBA 6334, UKURASA WA TATU, INAYOSEMA KUWA AMETHIBITISHA JUU YA KUWEPO HEWA YA SUMU NDANI YA UKUMBI WA CITY MALL AMBAPO KULIKUWA KUKIFANYIKA MKUTANO MKUU WA UCHAGUZI WA VIJANA WA CCM (UVCCM) MKOA WA MWANZA.


AIDHA KAMANDA MSANGI ANASEMA, UKWELI NI KUWA ALIPIGIWA SIMU NA MWANDISHI WA GAZETI HILO TAREHE 29/11/2017 MAJIRA YA SAA 15:00 MCHANA ALIYETAKA KUTHIBITISHIWA TAARIFA YA KUWEPO HEWA YA SUMU NDANI YA UKUMBI WA CITY MALL  AMBAPO KULIKUWA KUKIFANYIKA MKUTANO TAJWA HAPO JUU. 


KAMANDA ALIMJIBU KUWA HANA TAARIFA NA HAWEZI KUTHIBITISHA KWANI HAJAPATA TAARIFA YEYOTE KUHISIANA NA YALIYOTOKEA KATIKA MKUTANO HUO, NA YEYE YUPO KWENYE KIKAO CHA KAMATI YA ULINZI NA USALAMA OFISI YA MKUU WA MKOA.

PIA KAMANDA HAKUFIKA ENEO TAJWA KAMA TAARIFA HIYO  INAVYOSEMA, HIVYO INAONEKANA MWANDISHI WA TAARIFA HIYO ALIAMUA KUANDIKA MANENO HAYO KWA MANUFAA YAKE BINAFSI HIVYO JESHI LA POLISI MKOA WA MWANZA LINAOMBA GAZETI HUSIKA KUREKEBISHA. PIA ANAOMBA WAELEWE KUWA MATUKIO YA AINA KAMA HIYO YANAHITAJI YAWE NA MAJIBU YA KITAALAMU TOKA KWA WANASAYANSI PINDI YANAPOTOKEA. 

AIDHA JESHI LA POLISI MKOA WA MWANZA LINANAEDELE KUOMBA USHIRIKIANO TOKA KWA WAANDISHI WA HABARI KWA KUFANYA KAZI KWA PAMOJA ILI KUWEZA KUENDELEA KUDUMISHA USALAMA NA ULINZI KATIKA MKOA WETU. PIA JESHI LINAWAOMBA WAANDISHI WA HABARI KUFANYA KAZI KWA KUFUATA TAALUMA YA UANDISHI WA HABARI, UWELEDI NA MAADILI YA UANDISHI WA HABARI ILI KUEPUSHA HABARI ZA AINA KAMA HII AMBAZO ZINALETA PICHA MBAYA KWA JESHI NA MKANGANYIKO KWA JAMII.

IMETOLEWA NA;
DCP: AHMED MSANGI
KAMANDA WA POLISI (M) MWANZA.

MWAMUZI MTANZANIA KUCHEZESHA KOMBE LA DUNIA KWA WANAWAKE 2018 NCHINI URENO

\\\
Mtanzania Jonesia Rukyaa Kabakama ameteuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), kuchezesha fainali zijazo za Kombe la Dunia kwa wanawake (Algarve Cup) zitakazofanyika nchini Ureno, mwezi Februari, mwakani.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka TFF, Jonesia, ambaye ni mwanamke, ameteuliwa kupuliza filimbi katika fainali hizo ambazo hukutanisha timu mahiri zilizofanya vema katika michuano ya kila Bara.
Lakini kabla ya kwenda Ureno, Jonesia anatarajiwa kushiriki semina maalumu iliyoandaliwa na FIFA. Semina hiyo itafanyika Doha, Qatar kuanzia Februari 12- 16, mwakani.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania limempongeza Mwamuzi Jonesia kwa kuteuliwa na FIFA kuchezesha fainali za Kombe la Dunia na kuhudhuria semina hiyo muhimu kwa maendeleo ya mpira wa miguu.
Waamuzi wengine walioteliwa kutoka Afrika Lidya Abebe wa Ethiopia, Glady Lengwe wa Zambia na Salima Mukansanga wa Rwanda.

WCF YAPATA HATI SAFI KATIKA UKAGUZI WA TAARIFA YA FEDHA ULIOFANYWA NA CAG

 Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF), Bw. Masha Mshomba, akifafanua baadhi ya mambo wakati viongozi wa Mfuko walipokuwa wakiwasilisha taarifa za utendaji wake kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Mwaka wa Wadu kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa, AICC, jijini Arusha leo Novemba 30, 2017.



MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi, (WCF) umepata hati safi katika taarifa ya hesabu zake za fedha katika kipinmdi cha mwaka 2015-2016 ikiwa ni mwaka mmoja tu tangu kuanzishwa kwake.

Katika taarifa hiyo mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2016 (mwaka wa kwanza tangu kuaza kufanya kazi zake), thamani ya Mfuko ilifikia shilingi bilioni 65.68 na mfanikio haya yaliweza kufikiwa kutokana na ubunifu na ushirikiano mkubwa kati ya Mtendaji Mkuu wa Mfuko na Bodi ya Udhamini, Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Mfuko huo, Bw.Bezil Kwala, aliwaambia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Kwanza wa Wadau wa Mfuko huo unaoingia siku yake ya pili nay a mwisho kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa, AICC jijini Arusha, wakati akiwasilisha taarifa hiyo ya fedha leo Novemba 30, 2017.

Amesema Mfuko umekuwa ukiaandaa hesabu zake kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya uaandaji wa hesabu za fedha na kwa mujibu wa sheria CAG ndiye mwenye mamlaka ya kufanya ukaguzi na Hati Safi ni uthibitisho wa taarifa ya fedha za Mfuko kuonyesha hali halisi na kutokuwa na dosari ya aina yoyote.
Amesema katika ukaguzi huo, CAG alishirikiana na kampuni ya PricewaterhouseCoopers (PwC). Mwakilishi wa kutoka Ofisi ya CAG, Bw…….. amethibitishia wajumbe usahihi wa taarifa hiyo ya fedha ya WCF.
Mkutanmo huo ambao umeanza Novemba 29, 2017 na kubeba kauli mbiu isemayo, "Mafao ya Fidia: Haki ya Mfanyakazi na chachu katika kukuza uchumi wa viwanda”, pia ulipokea taarifa ya mipango ya uwekezaji ambapo Bw. Kwala aliwaambia wajumbe kuwa, katika kipindi kati ya mwaka 2017/18 – 2021/22, Mfuko umepanga kuwekeza kwenye miradi mbalimbali itakayoleta faida kwa mujibu wa tathmimi za kitaalamu zitakazofanyika.
“Maeneo tuliyoyaanisha katika uwekezaji kwenye sekta ya viwanda ni pamoja na kiwanda cha Grape Processing Factory kwa ushirikiano kati ya  GEPF na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, kiwanda cha Madawa mkoani Simiyu kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Kiwanda cha Morogoro Canvas Mills kwa kushirikiana na mifuko ya WCF, NSSF, PSPF, GEPF, na LAPF”. Alifafanua.
Akifafanua zaidi kuhusu umuhimu wa Mfuko kuwekeza, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw.Masha Mshomba alisema, fedha zitokanazo na michango ya Wanachama ni kidogo ukilinganisha na mahitaji halisi ya ulipaji Mafao ya fidia na kwa hali hiyo, ni muhimu Mfuko kuwekeza ili kupanua wigo wa kuongeza mapato na hivyo kuendelea kutoa Mafao ya Fidia bila ya shaka yoyote.
 Baadhi ya Wakurugenzi na Wakuu wa Idara wa WCF wakiwa kwenye mkutano huo.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya WCF, Bw. Emmanuel Humba, akizungumza
 Mkurugenzi wa Fedha WA WCF, Bw.Bezil Kwala, akiwasilisha ripoti ya fedha ya Mfuko kwa mwaka wa 2015-2016.
 Msaidizi wa Mkaguzi Mkuu wa Ofisi ya Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Johanes Joel Kisiri, akisikiliza uwasilishaji wa taarifa hiyo ya fedha.
 Mkuu wa Kitengo cha Sheria cha WCF, Bw.Abraham Siyovelwa, akitoa mada kuhusu Sheria juu ya kuanzishwa kwa Mfuko na jinsi unavyofanya kazi zake. Pamoja na mambo mengine Bw. Siyovelwa aliwaambia wajumbe kuwa,   Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoazishwa kwa mujibu wa kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Sura Na. 263 (Marejeo ya 2015) na kuanza kazi rasmi tarehe 1 Julai 2015. Lengo la kuazishwa kwa Mfuko ni kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika sekta rasmi (Binafsi na Umma) Tanzania bara ambao wataumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi
 Mkurugenzi wa Uendeshaji wa WCF, Bw. Anslem Peter, akiwasilisha taarifa ya uendeshaji ya Mfuko katika kipindi cha uahai wake, ambapo alisema Mfuko umekuwa ukifanya vizuri ikiwa ni pamoja na usajili wa wanachama " katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015-2017 jumla ya Waajiri 5,178 walisajiliwa ikiwa ni asilimia 71.92 ya lengo la kusajili waajiri 7,200


 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Dkt.Irene Isaka.
 Kiongozi wa chama cha Waajiri nchini (ATE), Bw. Aggrey Mlimuka, akizungumza kwenye mkutano huo.
 Bw. Hiroshi Yamabana kutoka Shirika mla Kazi Duniani, (ILO), akiuliza masuala mbalimbali kuhusu upembuzi juu ya usalama mahala pa kazi
 Tommie Dounball, kutoka kampuni ya Argen ya Afrika Kusini, akizungumzia uzoefu wa masuala ya Mfuko wa Fidia kutoka nchini kwake


 Bw. Mshomba (kushoto), akizungumza jambo wakati wa mkutano huo. Kulia ni Bw.Tommie Dounball, kutoka kampuni ya Argen ya Afrika Kusini,


 Mbunge wa jimbo la Mlalo Mkoani Tanga, Mhe. Rashiud Shangazi, (kushoto), akimsikiliza Meneja Uhusiano wa PPF, Bi. Lulu Mengele. Wote hao ni miongoni mwa wadau walioalikwa kushiriki mkutano huo.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Wdhamini ya WCF, Bw. Emmanuel Humba, (kulia), akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mkuu wa Taifa wa Bima ya Afya, (MHIF), Bw. Afya, Bw. Bernard Konga.

Mkurugenzi wa Matekelezo na Uandikishaji wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Bi. Lightness Mauki

FINLAND YAIPATIA TANZANIA MSAADA WA BILIONI 75 KUENDELEZA MISITU, MAFUNZO YA UONGOZI NA UBUNIFU


Serikali ya Tanzania na Finland zimetiliana saini mikataba mitatu yenye thamani ya Euro milioni 28.8 sawa na Shilingi bilioni 75 kwa ajili ya kuendeleza misitu, ubunifu na masuala ya uongozi.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mikataba hiyo, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James amesema, msaada huo kutoka Finland umetolewa ili kuendeleza  uwezo wa viongozi na kufanya maamuzi sahihi yenye tija kwa ukuaji wa uchumi wa Taifa, mradi ambao unasimamiwa na Taasisi ya Uongozi, ambapo kiasi cha Euro milioni 9.90 zimetolewa kuendeleza mradi huo.

Aidha Serikali ya Finland imetoa kiasi cha Euro milioni 8.95 kwa mradi wa  kuiimarisha mfumo wa ubunifu nchini kwa kutengeneza mazingira rafiki kwa wabunifu ili kuweza kubuni na kuendeleza ubunifu wao na kuchochea ukuaji wa viwanda. 

Bw. James alisema fedha hizo zitatumika kuwasaidia wabunifu kwa kuwapatia vifaa na msaada wa kitaalamu ili kuyaendeleza mawazo yao na kuyafanya yawe ya kibiashara na kuweza kusaidia kubadili mawazo hayo kuwa viwanda. 

“Fedha hizi zitasaidia kutatua changamoto katika viwanda vilivyopo nchini ili vifanye kazi kwa ufanisi kwa kuwaunganisha wanataaluma mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na wabunifu wachanga, wataalamu kutoka vyuoni, wataalamu kutoka Serikalini na Sekta binafsi” Alisema Bw. Doto James

Eneo lingine lililonufaika na msaada huo ni programu ya misitu, ambayo imepatiwa Euro milioni 9.95 kwa lengo la utuzaji wa misitu na uongezaji thamani ya mazao yatokanayo na misitu ili kuongeza kipato kwa Wananchi, kupunguza umasikini na kulinda mazingira.

Katibu Mkuu amemshukuru balozi wa Finland Nchini, Mhe. Pekka Hukka kwa msaada walioutoa na kwa kuunga mkono shughuli za maendeleo za Serikali, na kuongeza kuwa Finland wamekuwa wakifadhili miradi mbalimbali nchini, ukiwemo mradi wa kilimo biashara Mkoani Lindi na Mtwara (LIMAS), uliogharimu Euro milioni 9, Mradi wa kuimarisha usambazaji na upatikanaji wa umeme wa uhakika Jijini Dar es Salaam, uliogharimu Euro milioni 25, na Programu ya maboresho ya Serikali za Mitaa, Euro milioni 10.5

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Profesa Joseph Semboja aliiishukuru Serikali ya Finland kwa kuendelea kuisaidia Taasisi hiyo.
‘Hii ni mara ya tatu Finland wamekuwa wakitusaidia kuendeleza jitihada zilizoanzishwa na Serikali yetu ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2012 ambapo walitupatia Euro milioni 7, mwaka 2014 Euro milioni 12 na sasa wametupatia Euro milioni 9.90 huu ni msaada mkubwa’ alisema Profesa Semboja.

Aidha kwa upande wake Balozi wa Finland Bw. Pekka Hukka, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano na Serikali yake, na kuongeza kuwa msaada huo ni muhimu sana katika kutimiza malengo ya maendeleo ya nchi.Amesema msaada huo ukitumika ipasavyo hasa katika kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu utasadia kuongeza ajira na kuongeza pato la Taifa.

Ameitaka Serikali kupitia Wizara ya nishati,  kushirikiana na sekta binafsi na kuitumia fursa hiyo ya kuboresha misitu ili kuiongezea nchi mapato zaidi yatakayotokana na makusanyo ya kodi.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia) akionesha kalamu aliyozawadiwa na Balozi wa Finland Bw. Pekka Hukka (kushoto) ambayo imetengenezwa kwa mbao, akionesha uzalendo wa matumizi ya misitu. Kutoka kulia ni Kamishna wa Bajeti Wizara ya Fedha na Mipango Bibi. Mary Maganga na Kamishna wa Fedha za Nje Bw. John Rubuga.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Dotto James (kulia) akitia saini moja kati ya mikataba mitatu yenye jumla ya shilingi bilioni 75 kama msaada kwa Tanzania, Kushoto ni Balozi wa Finland Bw. Pekka Hukka kwa pamoja wakisaini mikataba hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia) akibadilishana mkataba na Balozi wa Finland Bw.Pekka Hukka. Mkataba wa kwanza wa Euro milioni 9.9 ni kwa ajili ya kusaidia Taasisi ya Uongozi, wa pili wa Euro milioni 8.9 kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa ubunifu na watatu wa Euro milioni 9.5 ni kwa ajili ya program ya misitu.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia) pamoja na Balozi wa Finland Bw. Pekka Hukka (kushoto) wakionesha moja ya mikataba mara baada ya kumaliza kutia saini mikataba hiyo.
Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Prof. Joseph Semboja (Kulia) akiishukuru Serikali ya Finland kwa kuwapatia msaada wa Euro milioni 9.9 ambayo itawasaidia kuendesha shughuli mbalimbali za Taasisi hiyo. Kushoto ni Balozi wa Finland Bw. Pekka Hukka.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (katikati, waliosimama mbele) akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya hafla ya utiaji saini mikataba mitatu ya jumla ya shilingi bilioni 75. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

MTANDAO WA UTEPE MWEUPE (WHITE RIBBON) WAZUNGUMZA NA WAKAZI WA KIJIJI CHA MAORE JUUU YA VIFO VTOKANAVYO NA UZAZI KWA KINAMAMA NA WATOTO WACHANGA

Mratibu wa Mtandao wa Utepe Mweupe kitaifa  (The White Ribbon Alliance ) Rose Mlay akizungumza na wananchi katika kijiji cha Maore wilayani Same wakati wamkutano wa hadhara ulioandaliwa na Taasisi ya Utepe mweupe (White Ribbon)  kujadili vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga .
Baadhi ya Wakazi wa Kijiji cha Maore wilayani Same akifuatilia kwa makini majadiliano yaliyokuwa yakiendelea kuhusu vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga .
Mganga Mkuu wa wilaya ya Same,Dkt Godfrey Andrew akizungumza wakati wa mkutano na wananchi ulioandaliwa na Mtandao wa Utepe Mweupe (White Ribbon) kujadili  vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga .
Baadhi ya Wakazi wa Kijiji cha Maore wilayani Same akifuatilia kwa makini majadiliano yaliyokuwa yakiendelea kuhusu vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga .
Mkutano ukiendelea katika jengo la Mahakama lililopo katika kijiji cha Maore wilayani Same.
Baadhi ya kina mama wakiwa na watoto wao katika mktano huo.

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Maore wilayani Same wakichangia wakati wa mkutano uliondaliwa na Mtandao wa White Ribbon kuhusu vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga .

Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii ,Kanda ya Kaskazini.

WANANCHI katika kijiji cha Maore wilayani Same mkoa wa Kilimanjaro,wamesema tatizo la vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi pamoja na watoto wachanga vinachangiwa na upungufu wa watumishi katika zahanati ya kijiji pamoja na ufinyu wa wodi ya wazazi iliyopo.

Wakitoa maoni yao katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Taasisi ya Utepe mweupe (White Ribbon)  kujadili vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga katika kijiji cha Maore wilayani Same wananchi hao wameiomba serikali kuangalia namna ya kutatua changamoto hizo.

Mbali na changamoto hizo wakazi wa Maore wameeleza pia changamoto kubwa inayowakabili wanafunzi wa kike kupata ujauzito pindi wawapo shuleni kuna changiwa na wazazi kushindwa kuwaeleza ukweli  watoto wao kuhusu kuanza mahusiano wawapo shuleni .

Mganga Mkuu wa wilaya ya Same ,Dkt Godfrey  Andrew amesema vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi pamoja na watoto wachanga vimepungua wilayani Same hadi kufikia 15 mwaka huu ukilinganisha na vifo 60 vilivyotokea katika miaka miwili iliyopita ya 2015 na 2016 huku akibainisha mikakati iliyopo ya kupambana na changamoto za upungufu wa watumishi.

Mratibu wa Mtandao wa Utepe Mweupe kitaifa  (The White Ribbon Alliance ) Rose Mlay amesema  kuwekeza kwa mama mjauzito kunachangia kuzaliwa kwa kijana mwenye afya njema atakayechangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kulea maendeleo.

Same ni mojawapo ya wilaya saba zilizoko katika mkoa wa Kilimanjaro zinazokabiliwa na changamoto ya vifo vya akina mama wajawazito vitokanavyo na uzazi huku sababu ya vifo hivyo kwa kina mama ikielezwa kuwa ni Kifafa cha Mimba,kupasuka kwa mji wa mimba na kutokwa na damu nyingi.