Friday, November 17

SERIKALI YADHAMIRIA KUIMARISHA KAMPUNI YA TTCL

SERIKALI ya Tanzania chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, imedhamiria kuiimarisha Kampuni ya Simu nchini (TTCL) iIi iweze kuingia kwenye ushindani wa kibiashara dhidi ya makampuni mengine ya simu.
Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa shirika hilo, Waziri Kindamba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya TTCL jijini Dar es Salaam.
Kindamba alisema hayo kufuatia Novemba 14, mwaka huu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujadili na kupitisha miswada ya mapendekezo ya mabadiliko ya sheria yanayofuta sheria iliyounda Kampuni ya Simu ya TTCL (Tanzania Telecomunication Company, Incoporation Act 2002) na kutunga sheria inayounda Shirika la Mawasiliano Tanzania (Tanzania Telecommunication Corporation Act 2017).
Aliongeza kuwa, kujadiliwa na kupitishwa kwa muswada huu bungeni kunafuatia hatua za awali za miswada ya serikali ambapo maoni ya wananchi na wadau wa huduma za mawasiliano yalikusanywa na kuchambuliwa.
Aidha, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni zilichambua muswada huu na kuutolea mapendekezo yao, ambapo Kindamba alisema mambo muhimu yanayotajwa katika sheria hiyo mpya ni pamoja na; Kuweka utaratibu utakaowezesha TTCL kutekeleza majukumu yake kama shirika la Umma. Kuweka jukumu la ujenzi, usimamizi na uendeshaji wa miundombinu ya kimsingi ya Taifa, Kuweka mazingira ya kinga ya mali (Asset) na miundombinu muhimu ya mawasiliano ya shirika na Kuanzishwa kwa shirika na kuainisha uongozi wa shirika.
Mambo mengine ni pamoja na Kuanisha vyanzo vya mapato na mtaji wa shirika, Kuanisha sheria zingine zitakazoguswa, Sheria kutumika pande zote za muungano na Kufuta kampuni ya simu Tanzania na kuanzisha shirika la mwasiliano Tanzania.
Kindamba aliongeza kuwa, katika mapendekezo ya sheria mpya yaliyoridhiwa na Bunge, Shirika la Mawasiliano Tanzania linapewa jukumu la msingi la kutoa huduma za mawasiliano kwa Taifa na kuhakikisha kuwa huduma hizo zinatolewa kwa viwango vya juu vya ubora.
Aidha, Kindamba alisema sheria mpya inataja jukumu jingine kuwa ni kusimamia na kuendeleza miundombinu ya Ki-Mkakati ya Mawasiliano kama vile Mkonga wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), Kituo Mahiri cha kutunzia kumbukumbu (National Data Centre) na miundombinu mingine itakayokuja siku za usoni.
Awali majukumu hayo yalikuwa yanafanywa na TTCL kwa niaba ya serikali bila kutajwa katika sheria. Amesema, miongoni mwa upungufu ulioonekana katika sheria ya awali ni kuwa, sheria hiyo ililenga kuwezesha mazingira ya ubia ndani ya TTCL, hitaji ambalo sasa halipo tena kutokana na TTCL kurejea mikononi mwa serikali kwa asilimia mia moja.
Kupitia utaratibu huo wa ubia, kwa kipindi cha miaka 15, TTCL ilimilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 65 na Kampuni ya Bharti Airtel ya India kwa asilimia 35.
Kaimu ofisa mtendaji huyo mkuu wa TTC L amesema, ubia huo ulifikia ukomo Juni 2016 baada ya Bharti Airtel ya India kulipwa jumla ya Tsh 14.7 Bilioni na kuondoka ndani ya TTCL.
Kindamba amesema hoja mahususi ni kwamba Shirika la Mwasiliano ni chombo muhimu katika ustawi wa nchi na kuongeza kuwa sheria mpya itaongeza ufanisi na tija katika shirika hilo ili liweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya Watanzania wote.
“TTCL ni taasisi yenye hazina kubwa ya watendaji wenye weledi na uzoefu mkubwa wa shughuli za mawasiliano hapa nchini,” alisema Kindamba na kuongeza; TTCL imeonesha weledi na uzoefu mkubwa katika kusimamia na kuendesha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye mtandao wa takriban kilomita elfu saba na mia nne nchi nzima.
Aidha, Kindamba amesema TTCL inasimamia na kuendesha kwa ufanisi mkubwa kituo mahiri cha kuhifadhi kumbukumbu (National Data Centre) kinachohudumia taasisi 28, taasisi 19 za serikali na taasisi 8 za sekta binafsi hadi sasa. “Makampuni yote ya mawasiliano na wadau mbalimbali wa biashara wanaotumia huduma zaTTCL wanaridhika sana na huduma inayotolewa,” alisema Kindamba na kuongeza;
“Kuhusu kuipa mtaji TTCL, serikali imeandaa mpango mkakati wa miaka mitano 2017/18-2021/2022 ambao pamoja na mambo mengine utaainisha mtaji unaohitajika na serikali ambapo serikali itatekeleza mpango huo.”
Aliongeza kuwa, kuhusu idadi ya wajumbe wa bodi kutoka Zanzibar, serikali imeridhia idadi hiyo kuongezeka kutoka mjumbe mmoja na kuwa wawili.

Kindamba amesema ieleweke kwamba mabadiliko haya ya sheria kutoka Kampuni ya Simu Tanzania kuwa Shirika la Mawasiliano Tanzania hayaathiri mikataba na makubaliano ya kibiashara yaliyofikiwa awali kati ya TTCL na wateja na wadau wa huduma zake.
Amesema madeni ambayo TTCL inadai wateja wake na ambayo TTCL inadaiwa na watoa huduma mbalimbali yapo palepale na yataendelea kufanyiwa kazi kwa mujibu wa makubaliano na mikataba ya kiabishara iliyofikiwa.

“TTCL ipo imara na thabiti zaidi kuliko ilivyokuwa awali kwa kuwa sasa inatarajia kupata mamlaka zaidi na uwezo zaidi wa kuhudumia umma,” alisema Kindamba.
Akielezea mustakabali wa ajira za wafanyakazi wa kampuni hiyo baada ya mabadiliko hayo, Kindamba amesema ajira zao ikiwa ni pamoja na mali na miuondombinu viko salama.

Kindamba amesema huduma zinazotolewa na TTCL yaani simu za mezani, simu za kiganjani, data na TTCL PESA zinaendelea kutolewa kwa ufanisi mkubwa na kuongeza kuwa huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo mahiri cha kutunzia kumbukumbu (National Data Centre) pia zinaendelea kutolewa kama kawaida na kwa weledi wa hali ya juu.
“Kilichobadilika ni sheria ya kampuni ya simu Tanzania ambayo sasa ni shirika la mawasiliano Tanzania ambapo mapendekezo haya yanasubiri idhini ya mheshimiwa rais ili kuwa sheria kamili,” amehitimisha Kindamba.

KESI YA JALADA LA VIGOGO WA SIMBA LAREJESHWA TAKUKURU.


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Novemba 17, imeambiwa jalada la kesi inayowakabili vigogo wa Klabu ya Simba Evans Aveva na Godfrey Nyange maarufu "Kaburu" limeisharudi kutoka kwa (DPP) na limerejeshwa TAKUKURU

Hayo yameelezwa na wakili wa Takukuru, Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa, wakati shauri hilo lilipokuja kwa kwa kutajwa.Wakili Swai alidai jalada hilo lilirudishwa juzi kutoka kwa DPP ambaye ametoa maelekezo ya kukamilisha zaidi upelelezi.

Upande wa jamhuri ulieleza hayo baada ya Wakili wa utetezi, Philemon Mutakyawa, kuhoji kuhusu jalada hilo la kesi ambalo lilielezwa kuwa kwa DPP, hivyo alitaka kujua lilipofikia.

Kesi hiyo imahirishwa hadi Novemba 30, mwaka huu,

Washtakiwa wanakabiliwa na mashtak uhujumu uchumi ikiwa na mashitaka matano na ya utakatishaji wa fedha

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha wa Dola za Marekani (USD) 300,000.

WANAODURUFU KAZI ZA SANAA KUFIKISHWA MAHAKAMANI.



 Kampuni ya Udalali ya Msama Auction Mart imethibitisha kuwa Watuhumiwa wote waliokwamatwa kushiriki kufanya biashara ya kazi feki za sanaa watafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Msama Auction Mart, Alex Msama amesema kuwa Watuhumiwa hao watapelekwa Mahakamani kutokana na kuwa na kesi ya kujibu.

Ameendelea kusema ni kosa kuuza Kazi za Wasanii hao ambazo hazina Stika ya TRA, kwani zinawakosesha Mapato Wasanii hao na Serikali kwa ujumla.

Amesema wataendelea na zoezi hilo kwa kupita maeneo yote kuhakikisha wanadhibiti uuzwaji wa kazi hizo feki.Kwa jana zoezi letu liliendelea maeneo ya Mbande, Mbagala, Buza Tandika na Chanika", amesema Msama.

Amesisitiza kuwa kazi za nje na ndani lazima ziwe na Stika ya TRA, pia amesema ni marufuku kuweka nyimbo za Wasanii, Kuburn CD na kuweka kwenye Flash.
 Kampuni ya Udalali ya Msama Auction Mart inashirikiana na Jeshi la Polisi kwa ajili ya usalama, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuendelea na kuikamisha shughuli hiyo,ambayo pia inatarajiwa kufanyika katika mikoa mbalimbali.
  Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya Msama Auction Mart ya jijini Dar es salaam,Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari katika kituo kikuu cha Kanda Maalum Dar es salaam jana kabla ya kuanza kwa zoezi la kukamata wauzaji wa CD Feki katika maeneo mbalimbali ya ikiwemo eneo hatarishi kwa bishara hiyo la Kariakoo .
Baadhi ya watuhumiwa wakipandishwa kwenye gari na vifaa vyao.
 Mkurugenzi wa Kampuni ya Udalali ya Msama Auction Mart ya jijini Dar es salaam,Alex Msama akikagua baadhi ya CD kwenye moja ya duka.
Mmoja wa watuhumiwa akichukuliwa na na Askari baada ya kugundulika akiuza katika duka lake.
"Mfano huyu mmiliki wa duka hili, Leseni yake imeisha tangu 2014 mpaka leo na hajui taratibu zozote za kupata leseni mpya wala TIN number,bado anaendelea na biashara yake,kinyume cha sheria",alisema Alex Msama.

KWA MARA YA KWANZA UPASUAJI WA KUZIBUA MISHIPA YA MOYO KUPITIA MSHIPA WA DAMU WA MKONO (CATHETERIZATION) WAFANYIKA KATIKA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIKWETE (JKCI)

16/11/2017 Jumla ya wagonjwa 20 wamefanyiwa upasuaji wa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa upasuaji wa aina hiyo kufanyika hapa nchini.

Akiongea na Waandishi wa Habari leo jijini Dar Salaam Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge alisema upasuaji huo unafanyika katika kambi ya matibabu ya Moyo inayofanywa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na madakatari kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini Saudi Arabia.

Dkt. Kisenge alisema kuwa kambi hiyo inaenda sambamba na utoaji wa elimu na kubadilishana ujuzi wa kazi kati ya wafanyakazi wa Taasisi hizo mbili ikiwemo aina mpya ya upasuaji wanaoufanya kitu ambacho kinawajengea uwezo zaidi. ”

“Faida ya upasuaji huu ni kumwezesha mgonjwa kutoka chumba cha upasuaji akiwa anatembea na baada ya masaa manne kama hali yake inaendelea vizuri anaweza kuruhusiwa.“Tofauti na upasuaji wa kutumia mshipa wa paja ambao tulikuwa tunaufanya, baada ya upasuaji mgonjwa ni lazima akae Hospitali kwa zaidi ya masaa 24 ili kuangalia maendeleo ya afya yake”, alisema Dkt. Kisenge.

Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya IIRO Ali Al Masoud alisema kambi hiyo inaendelea vizuri kwani kwa siku wanatibu wagonjwa 10 na baada ya matibabu afya zao zinaimarika tofauti na ilivyokuwa kabla ya matibabu.Dkt. Masoud aliongeza kuwa wamekuja na utaalam mpya wa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono ambapo kabla ya hapo matibabu yaliyokuwa yanafanyika ni ya kutumia mshipa wa damu wa kwenye paja.

Alifafanua, “Hivi sasa tunafanya upasuaji wa Moyo wa bila kufungua kifua kitu ambacho wenzetu hawa walikuwa wanakifanya. Sisi tumewaongeza utaalam mpya wa kutumia mshipa ya mkononi badala ya mshipa wa paja.

Naye Bader Alanezi ambaye ni Mtaalamu wa magonjwa ya Moyo na mishipa ya damu kutoka IIRO alimalizia kwa kusema kuwa wamepata muda wa kujifunza vitu vingi na kupata uzoefu mpya wa baadhi ya magonjwa na mambo ya kiteknolojia ambayo katika nchi yao hakuna.

Jumla ya wagonjwa 40 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji katika kambi hiyo ya siku tano ambayo imeanza tarehe 14 hadi tarehe 18 mwezi huu.

Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini Saud Arabia wakimfanyia mgonjwa upasuaji wa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab katika kambi ya matibabu ya moyo inayoendelea kwenye Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa 40 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji katika kambi hiyo ya siku tano.


Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Peter Kisenge na mwenzake wa Taasisi ya Kimataifa ya Kiislamu ya Misaada (IIRO) ya nchini Saud Arabia Ali Al Masoud wakimfanyia mgonjwa upasuaji wa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab katika kambi ya matibabu ya moyo inayoendelea kwenye Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa 40 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji katika kambi hiyo ya siku tano.

Zoezi la kumfanyia mgonjwa upasuaji wa kuzibua mishipa ya moyo kupitia mshipa wa damu wa mkono (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab likiendelea. Picha na JKCI

Wakurugenzi wawili ndugu walivyopoteza maisha ajali ya ndege Ngorongoro

Maofisa wa vyombo vya usalama wakikagua mabaki
Maofisa wa vyombo vya usalama wakikagua mabaki ya Ndege iliyoanguka juzi eneo la Empakai ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha. Picha na Mussa Juma 
Ngorongoro. Ajali ya ndege ya kampuni ya Coastal Aviation iliyotokea juzi na kuua watu 11, imepoteza maisha ya wakurugenzi wawili wa kampuni maarufu ya utalii mkoani Arusha, Masai Wandering, Nassibu Mfinanga na Shatri Mfinanga.
Ndege hiyo yenye namba 5H-EGG aina ya Cessna Grand Caravan ilianguka baada ya kugonga kingo za Kreta ya Empakai umbali wa mita 3,250 kutoka usawa wa bahari ikitoka mkoani Kilimanjaro kwenda Hifadhi ya Serengeti kutokana na ukungu uliokuwa umetanda katika eneo hilo.
Wakurugenzi hao pamoja na mkuu wa idara ya kompyuta wa kampuni hiyo, Gift Lema walikuwa wakielekea Hifadhi ya Serengeti ambapo wanamiliki kambi za watalii kwa ajili ya kupiga picha ili kuboresha mtandao intaneti wa kampuni hiyo.
Wengine waliofariki ni pamoja na Joyce Mkama mfanyakazi wa Hoteli ya Serena, Simion Kombe ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya Mount Kilimanjaro na Moses Maina aliyekuwa mfanyakazi wa Hoteli ya Andbeyond.
Waliofariki wengine ni Mfalala Siyabonga aliyekuwa akifanyakazi Hoteli ya Bilila Serengeti na watalii Steinert Alexis, Lickttgen Katharina, Kauser Anita na Beranek Hubert.
Walifanya sherehe kabla
Akizungumza katika eneo la ajali, mpwa wa Nassibu, Rick Thomas alisema kabla ya safari hiyo Novemba 11, wakurugenzi hao walifanya sherehe maalumu ya kila mwaka na wafanyakazi wote na wageni iliyokwenda sambamba na kuchangia vituo vya watoto yatima jijini Arusha. Thomas alisema kampuni ya Masai Wondering inavilea vituo vya watoto yatima zaidi ya 10 katika mikoa ya Arusha na Manyara ambapo katika sherehe hiyo iliyopewa jina la ‘Asante Afrika’ kila tiketi iliuzwa Sh100,000.
Mfanyakazi mwingine wa kampuni hiyo, Mubarak Mkwepu alisema katika sherehe hiyo zaidi ya Sh15 milioni zilipatikana.
Alisema kuwa Nassibu ameacha mke na watoto wawili.
Ajali ilivyotokea
Kabla ya kuanguka ndege hiyo ilizunguka juu na kumwaga mafuta.
Mashuhuda waliozungumza na gazeti hili walisema kabla ya kuanguka ilizunguka angani kwa zaidi ya nusu saa katika eneo la milima ya bonde la Empakai ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Lunda Mollel na Lengio Kilembi ambao ni wakazi wa Kijiji cha Sendiu walisema wakiwa machungani waliiona ndege hiyo ikizunguka juu na baadaye kuanguka.
Hata hivyo, walisema walianza kutilia shaka baada ya kuona inachukua muda mrefu na baadaye kurejea eneo la Kreta ya Empakai kwa kasi na kisha kugonga mlima na kuanguka.
Kilembi alisema wakati ndege hiyo ikiwa juu inazunguka waliona ikimwaga mafuta, jambo ambalo liliwashangaza. “Nadhani yule rubani alishindwa kutoka katikati ya milima kutokana na ukungu na ndipo alishindwa kuidhibiti ndege na kuanguka,” alisema Mollel.
Hata hivyo, alisema washindwa kwenda katika eneo hilo kutokana na umbali, lakini majira ya saa 10 jioni ndipo walianza kuona magari yakienda na wao walikwenda na kukuta watu 11 wakiwa wamefariki dunia. Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema jeshi hilo kwa kushirikiana na mamlaka nyingine ikiwamo ya anga wanaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo.
“Uchunguzi umeanza kujua chanzo na tayari kisanduku maalumu cha mawasiliano kimechukuliwa na wataalamu waliofika mara tu baada ya ajali,” alisema.
Hiyo ni ajali ya pili kutokea ikihusisha ndege za Coastal Aviation kwani wiki mbili zilizopita ndege nyingine ya kampuni hiyo iliangika katika eneo la Lobo Serengeti na kujeruhi watu wanne.

Duce walia na deni la Sh700 milioni

Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi Duce, Profesa
Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi Duce, Profesa Rwekaza Mukandala 
Dar es Salaam. Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce) kinakabiliwa na deni la Sh700 milioni, lililotokana na mkopo uliotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) ikiwa ni gharama za kusomesha wanataaluma.
Rais wa chuo hicho, Profesa William Anangisye alisema hayo kwenye mahafali ya kumi ya Duce jijini Dar es Salaam.
Alisema ili kukabiliana na madeni kutoka bodi hiyo, chuo kimeanzisha utaratibu wa kuwachuja wanataaluma wanaoomba kusomeshwa na bodi.
“Tumeanzisha uhusiano na vyuo rafiki nje ya nchi ili vitusaidie kusomesha wanataaluma hawa,” alisema.
Anangisye alifafanua kuwa huu ni wakati wa wanataaluma kutafuta ufadhili kutoka taasisi nyingine za kimataifa zinazotoa ufadhili ili wasomeshwe.
Alisema wanatumia fedha nyingi kuwalipa wahadhiri wa muda chuoni hasa katika masomo ya Fizikia, Hisabati, na Infomatiki.
“Hii ni changamoto kwetu, hata hivyo tumeanzisha utaratibu wa kuandaa mpango wa usomeshaji wa wafanyakazi uitwao Staff Training Plan utaowezesha chuo kutathmini mahitaji ya usomeshaji,” alisema.
Pia, alifafanua kuwa chuo kinakabiliwa na uhaba wa mabweni na kwamba wanafunzi 4,888 kati ya 5,300 wamekosa nafasi za mabweni na kuishi katika vyumba vya kupanga.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi Duce, Profesa Rwekaza Mukandala aliwataka wahitimu kuacha kujenga mazoea ya kuajiriwa na badala yake watengeneze mazingira ya kujiajiri wenyewe ili kukabiliana na changamoto ya mrundikano wa wahitimu wasio na kazi mtaani.
“Mimi nasisitiza tu kuwa ni vizuri kwa wahitimu kufikiria kuajiriwa nje ya Serikali au sekta rasmi pekee,” alisema.
Alisema tatizo la wahitimu kutegemea ajira lipo katika nchi nyingi za Afrika na dunia kwa jumla, hivyo chuo kimeona ipo haja ya kuongeza mkazo katika elimu ya ujasiriamali ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri.
“Kwa idadi hii, leo tunategemea mtafanya kazi kwa bidii na nidhamu, na kwa wale watakaoenda kuwa wajasiriamali mna mchango pia katika jitihada za kuwezesha mikakati ya kitaifa ya kuleta maendeleo ya viwanda na uchumi wa kati,” alisema.
Mkuu wa chuo hicho, Jakaya Kikwete aliwatunuku wahitimu 1,443 shahada za fani mbalimbali.

Walimu waliolala nje na kujikuta wamenyolewa wageuziwa kibao


Buchosa. Wananchi wa Kisiwa cha Soswa halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema wamewatupia mpira walimu waliojikuta wamelala nje kwa madai ya imani za kishirikina kuwa ni tukio la kutengenezwa.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara ulioitishwa jana Alhamisi kwa dharura kujadili suala hilo lililojitokeza usiku wa kuamkia Novemba 15, mwaka huu, katika viwanja vya shule ya msingi Soswa wananchi hao walisema tukio hilo ni la kutengenzwa ili kuishinikiza Serikali iwape uhamisho kutokana na mazingira magumu wanayokaa.
Mzee wa kisiwa hicho, Mashinga Boniphace (80) alisema hakuna ukweli juu ya tukio hilo kwani yeye pamoja na wazee wenzake waliangalia vibuyu na damu iliyokuwa imetapakaa ndani ya nyumba za walimu hao sio ya kishirikina.
“Walimu hao waliamua kuua ndege aina ya nyagenyange ili na kutapakaza damu hizo ndani ya nyumba zao pamoja na kwenye vibuyu ili kushinikiza uongozi wa juu kuwahamisha kutokana na juhudi zao za kuhama kugonga mwamba,”alisema Boniphance
Kauli ya mzee huyo wa mila ilipingwa na mkazi mwingine wa kijiji hicho, Mjula Magafu ambaye alisema suala hilo liangaliwe kwa kina kwakuwa limezua sintofahamu ndani ya kisiwa hicho na Taifa kwa ujumla.
Alisema kama walimu ndio walitengeneza tukio hilo wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa kudanganya umma.
“Hapo awali lilipotokea tukio la nyumba zao kupondwa mawe walimu wote waliondoka na kubaki wawili ambapo hakukuwa na kitendo kama hicho, baadaye walimu waliokuwa wamesusia akiwemo mwalimu Daudi Shule na Wape Kisimu kitendo hicho kilijirudia tena na sasa wameamua kutengeneza tukio la kulazwa nje, tunapaswa kuchunguza kwa kina,” alisema Magafu
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na Mwananchi walisema tukio hilo limewaathiri kimasomo hivyo kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao.
Mwanafunzi wa darasa la tano, Malisela James aliiomba jamii ikubali kuwa walimu hao wamefanyiwa vitendo vya kishirikina na kwamba watafute namna ya kukukomesha ili kuwapa fursa ya kuendelea kusoma.
Mwenyekiti wa kamati ya shule, Lidia Buluba alilaani kitendo hicho ambacho kinahisishwa na imani za kishirikina huku akiwatupia lawama baadhi ya walimu waliotengeneza jambo hilo ili wapatiwe uhamisho kwa madai kuwa mazingira wanayoishi si mazuri.
Mwalimu Daudi Shule ambaye anapatiwa matibabu ya asili katika kijiji cha mwangakia yeye alidai alinyolewa sehemu za siri, mwalimu  Ernest Katunzi alithibisha kwa kumwona sehemu hizo kuwa amenyolewa pamoja na mwalimu Wape Kisumo aliyonyolewa nywele  kichwani  kwa pamoja walisema kuwa wanafanyiwa vitendo vya kishirikina  hata kipindi wanapondwa mawe jamii hiyo haikuamini.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Petro Lukas alisema maneno yanayosemwa na jamii hawawezi kuyaamini na haamini kama walimu wametengeneza mazingira ya tukio hilo ili wahame kwa kuwa kazi yao ni kufundisha.
Mtendaji wa Kata ya Bulyaheke, Musa Mwilomba alisema kuwa anaiomba jamii kutokutupiana mpira juu ya tukio hilo na kwamba wanatakiwa kusameheana na kusahau kilichotokea ili kuanza sura mpya na walimu waendelee kufundisha.
Mkaguzi wa shule wilayani Sengerema, Elly Msulu aliyefika katika Kisiwa cha Soswa kupata ukweli juu ya tukio hilo aliitaka uchunguzi zaidi ufanyike kujua ukweli wa tukio hilo na watakaobainika hatua kali za kisheria dhidi yao zitachukuliwa huku akiwaomba walimu kuwa wavumilivu wakati suala hilo linatafutiwa ufumbuzi.

PITIA VICHWA VYA HABARI KATIKA MAGAZETI YA LEO NOVEMBA 17,2017