Thursday, June 8

PSPF YASAJILI WANAFUNZI ZAIDI YA 250 WA VYUO VIKUU JIJINI DAR ES SALAAM, WAJIUNGA NA MPANGO WA UCHANGIAJI WA HIARI, (PSS).


Afisa Mfawidhi wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Neema Lowassa,(wapili kulia), na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Mfuko huo, Bw. Abdul Njaidi wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali za wanavyuo wa elimu ya juu mkoa wa Dar es Salaam, wakionyesha vipeperushi vyenye melezo ya Mfuko huo, baada ya semina ya siku moja iliyoandaliwa na PSPF kuelimisha wanafunzi shughuli mbalimbali za Mfuko na fursa zilizopo. Semina hiyo imefanyika leo Juni 8, 2017.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSPF, Bi. Costantina Martn, akifungua semina hiyo leo Juni 8, 2017

NA K-VIS BLOG/Khalfan Said

ZAIDI ya wawakilishi 250 wa wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu kutoka jijini Dar es Salaam wamejiunga na Mfuko wa Pensheni wa PSPF, kupitia mpango wake wa uchangiaji wa hiari (PSS), baada ya kushiriki semina ya siku moja makao makuu ya Mfuko jijini Dar es Salaam Juni 8, 2017.

Wanafunzi hao kutoka taasisi 20 za elimu ya juu, wamehudhuria semina hiyo ya siku moja iliyoandaliwa na PSPF kwa uratibu wa Taasisi ya Elimu ya Vyuo Vikuu Tanzania, (TAHILISO), ili kuwapatia elimu wanafunzi hao kuhusu shughuli za Mfuo na faida azipatazo mwanachama ikiwemo mafao mbalimbali.

Kabla ya zoezi hilo la kujiunga na Mfuko, awali Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSPF, Bi. Costantina Martin, aliwaasa wanafunzi hao kujijengea utamaduni wa kuweka akiba kwani manufaa yake huonekana katika kipindi kifupi.

“Mimi nina mototo yuko chuo kikuu huwa ninampatia fedha kidogo za kujikimu lakini namueleza aweke akiba, ningependa kuwahamasisha vijana mjenge utamaduni wa kujiwekea akiba kidogo kidogo,zile posho mnazopata, na fedha kutoka kwa wazazi wenu, mnaweza kutenga sehemu ya fedha hizo na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ili kujiwekea akiba.” Alsoema Bi. Costantina Martin, wakati akifungua semina hiyo.

Alisema, PSPF, kama Mfuko wa hifadhi ya jamii, moja ya malengo yake ni kuandikisha wanachama wapya , kukusanya michango, kuwekeza na kuwalipa mafao na pensheni wastaafu na wategemezi iliw aweze kupata fedha kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.

Aliwashauri wanafunzi hao kujiunga na mpango wa uchangiaji wa hiari, ili hatimaye waanze kufaidi mafao mbalimbali ikiwemo faola matibabu ambapo mwanachama anapatiwa bima ya afya itakayomuwezesha kutibiwa yeye mwanachama na wategemezi wake.

Ili kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa salama, PSPF inaendesha mipango ya aina mbalimbali ya uchangiaji, mpango wa lazima na mpango wa hiari ili kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa salama katika Hifadhi ya PSPF.

“Najua wataalamu wetu watawapa elimu ya kutosha kuhusu aina za wanachama kwani hata ninyi mnaweza kuwa wanachama wetu kupitia mpango wa uchangiaji wa hiari PSS, ambapo mnaweza kujiunga na kupatiwa kadi zenu leo hii baada ya semina.” Alsiema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Elimu ya Vyuo Vikuu Tanzania, (TAHILISO), Bw.Stanslaus Peter Kadugalize, ameishukuru PSPF kwa kuwa mshirika mzuri na kukubali ombi la wanafunzi hao kupatiwa elimu juu ya hifadhi wa jamii.

“ Ninachoomba, PSPF inaweza kuangalia namna gani inaweza kusaidia wanafunzi katika ushiriki wao kwenye elimu, kwa mfano mnaweza kutusaidia hata kutujengea vimbweta kwenye vyuo vyetu, lakini pia mnaweza,uwekeza kwenye ujenzi wa hosteli ambazo sisi wanafunzi tutalipa kodi.” Alsiema.

Maafisa wa PSPF, walitoa mada mbalimbali ambazo miongoni mwake ni pamoja na jenga career na PSPF, ambao ni mkopo wa elimu, Jipange kimaisha na PSPF, ambapo PSPF hutoa mikopo kwa mwajiriwa mpya,

Hata hivyo wanafunzi hao waliiomba PSPF kutengeneza mfumo ambao unaweza kuwasaidia wanafunzi kuwawezesha nkushiriki kwenye elimu bila matatizo. “Wanafunzi hawahitaji fedha nyingi, mnaweza kuweka mfumo utakaowawezesha wanafunzi kupata mikopo midogo ya fedha ili kuwawezesha kujikimu wawapo vyuoni na hatimaye wanafunzi hao wanaweza kurejesha fedha hizo kwa utaratibu utakaokubaliwa na pande mbili.
Mwenyekiti wa TAHILISO, Bw.Stanslaus Peter Kadugalize,(aliyesimama), akifafanua baadhi ya mambo mwishoni mwa semina hiyo. Wengine kutoka kushoto, ni Katibu Mkuu wa TAHILISO, Bi. Zuhura A. Rashid, Afisa Mfawidhi wa PSPF mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Neema Lowassa, na Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Mfuko huo, Bw. Abdul Njaidi.
Katibu Mkuu wa TAHILISO, Bi.Zuhura A.Rashid, (kushoto), akijaza fomu ya kujiunga na PSPF kupitia mpango wa uchangiaji wa hiari (PSS)
Viongozi wa wanafunzi wakijaza fomu za kujiunga na PSPF
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PSPF, Bi.Costantina Martin,akifungua semina hiyo
Kely Malinga, wa call centre ya PSPF akiwa kazini
Afisa Mfawidhi wa PSPF Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Neema Lowassa, akizungumza kwenye senima hiyo
Afisa Mfawidhi wa PSPF Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Neema Lowassa, akizungumza kwenye senima hiyo
Afisa Matekelezo wa PSPF, Bw. David Mutabazi, akitoa mada yake jinsi masuala ya hesabu za kulipa mafao zinavyofanyika
Bi. Neema na Bw. Njaidi wakiwaongoza washiriki wa semina hiyo, kutembelea pfisi za PSPF ili kujionea utendaji kazi wa ofisi hizo kabla ya kuanza semina
Washiriki wakijisajili
Afisa Uhusiano Mwandamizi wa PSPF, Bw. Abdul Njaidi, akizunguzma na baadhi ya viongozi wa wanafunzi wa elimu ya juu, walipotembelea kuona jinsi utunzaji taarifa za wanachama wa Mfuko zinavyohifadhiwa. Hii ilikuwa ni sehemu ya semina waliyopewa viongozi hao na maafsia wa PSPF jijini Juni 8, 2017
Washiriki wakionyeshana fomu za PSS, za wanachama wa mpango wa uchangiaji wa hiari
 Afisa wa PSPF anayeshughulikia masoko, Bw. Magira Werema akizungumza wakati wa kutoa elimu viongozi hao wa wanafunzi

Mshiriki akijaza fomu za kujiunga na PSS
Washiriki wakiwa kwenye foleni ya kupiga picha za vitambulisho vya kadi za uanachama wa PSPF kupitia mpango wa PSS
Afisa mwandamzi wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Bw. Delphis Richard, (kushoto), akitoa mada iliyoelezea faida mbalimbali azipatazo mwanachama wa Mfuko huo kwa washiriki
Washiriki wakijaza fomu za kujiunga na mpango wa PSS
Bi. Neema(kushoto), akimuelekeza jambo mshiriki huyu wa semina
Mkuu wa idara ya call centre, Bi Queen, (katikati), akitoa maelezo kwa washiriki walipotembelea ofisi za huduma kwa wateja, za PSPF makao makuu 
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PSPF, Costantina Martin, (katikati), akiongozana na Afisa Mfawidhi wa Mfuko wa Pensehni wa PSPF, Mkoa wa Dar es Salaam, Neema Lowassa, (kulia) na Afisa Mwandamizi wa Utafiti, Mapesi Maagi. Kuelekea kwenye ukumbi wa mkutano ambako kulifanyika semina ya siki moja ya viongozi wa serikali za wanafunzi wa elimu ya juu jijini Dar es Salaam jana Juni 8, 2017.
Afisa mwandamizi wa kitengo cha utunzaji kumbukumbu (record keeping), Bw. Gwamaka A. Ngomale, (mwenye kofia), akiwaeleza washiriki hao namna PSPF inavyotunza kumbukumbu kwenye mfumo wa kielektroniki wa makabati (electronic shelves)
Katibu Mkuu wa TAHILISO, Bi.Zuhura A. Rashid, akitoa neno la shukurani baada ya semina kumalizika

Road License yafutwa, sasa kulipwa mara moja

Dodoma. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ametangaza kufutwa rasmi kwa ada ya mwaka ya leseni ya magari.
Amesema uamuzi umechukuliwa ili ada hii ilipwe mara moja pale gari linaposajiliwa na baada ya hapo iendelee kulipwa katika ushuru wa bidhaa  katika mafuta ya petroli na dizeli.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi bungeni na Waziri Mpango wakati akiwasilisha bajeti ya mwaka 2017/18.
Pamoja na hayo, Waziri Mpango ameshuha ushuru  kwa mvinyo  unaotengenezwa kwa zabibu zinazozalishwa  ndani kutoka Sh2O2  kwa lita hadi Sh200 kwa lita.
Kadhalika ushuru wa bia zinazotengenezwa kwa nafaka za ndani umepanda kutoka Sh429 hadi 450 kwa lita.
 Wakati huo, ushuru wa  bia zisizo na kilevi na vinywaji vya kuongeza nguvu kutoka Sh534 hadi Sh564 kwa lita.

ADIOS AMIGO,BRAZA CISCO



Na Ankal - issa michuzi blog
Hebu jaribu kulielezea jiji la Dar, au la Arusha, ama la Mwanza,  Mbeya  ama jiji lolote lile, tena  kwa kutumia ukurasa mmoja tu na uwe umefanikiwa kulieleza kinagaubaga kiasi hata mtu ambaye hajawahi kufika hapo ajione kama keshafika na anapafahamu vizuri.

Basi huo ndio mtihani nilionao wakati naandika haya, tena kwa moyo mzito, nikijaribu kumwelezea rafiki yetu, kaka yetu, ndugu yetu, jamaa yetu au vyovyote vile upendavyo kumwita mtu kama Balozi Abdulcisco  Omar Mtiro almarufu kama CISCO.
Labda uamue kuzungumzia kamtaa  kamoja tu katika kitongoji kimoja, ndipo kidooooogo unaweza kufanikiwa kueleza vitu vikaeleweka. nami ndivyo najaribu kufanya hapa, kwa kudonyoa kasehemu tu ka Braza Cisco.

Ni kweli kwamba mtu akitangulia mbele ya haki huwa kuna hulka ya kumsifia na kumuenzi mtu huyo. Lakini si uwongo kwamba haya niandikayo hapa, japo yalikuwa nyuma ya ubongo wa wengi wetu siku zote, ni halisi na wala sio kwa sababu Cisco hatunaye tena. 

Kwa wengi alikuwa mkarimu na mwingi wa bashasha saa zote. Kwa tuliobahatika kuwa karibu naye, Cisco alikuwa hivyo na zaidi. Pamoja na kuwa na wadhifa mkubwa serikalini (Balozi wetu nchini Nigeria na Malaysia katika nyakati mbalimbali na baadaye Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje), Cisco alikuwa mtu wa kujichanganya na kila mtu bila kujali hali ama mali zake. Hakuwa na makuu wala makidai. Alikuwa mtu mmoja 'freshi' sana, wanasema vijana wa mjini.

Unapomkuta na wanachama wenzie wa Klabu ya michezo ya TAZARA pale Leaders Club ama kwa Octa (kijiwe maarufu  jirani na ubalozi wa Ufaransa) ilikuwa huwezi kuamini kwamba huyu mtu mchana ametoka kusuguana mabega na viongozi wakuu wa nchi na wageni wao ambao, akiwa kama Mkuu wa Itifaki,  jukumu lake lilikuwa kuratibu na kusimamia kila kitu. 

Ubaya, ama uzuri wake, hukumsikia hata mara moja akizungumzia kazi yake ama wadhifa wake. Huko alikuwa serious kama askari wa Mjerumani. Lakini afikapo kijiweni, kama mlivyo nyinyi wakati huo, na yeye  pia alijitosa kuogelea nanyi kwenye soga za siku kama vile kandanda,  stori zote za mjini, pamoja na muziki ambao alikuwa anaupenda sana – hasa hasa Jazz, Classics, Old Skul na Chachacha.

Sifa yake kubwa akiwa nasi kijiweni ilikuwa ni utani na vichekesho vya kuvunja mabvu. Yaani Cisco alikuwa hakosi kuja na ‘mpya’ hata kabla ya kuketi kitini, na wakati wa kuondoka kwenda kupumzika alikuwa hakosi kuwaacha na ‘kibomu’ kingine cha kuchana mbavu. Vile vile kila ukutanapo naye lazima ‘akuchape’ na kitu kipya. 

Na hiyo ilikuwa hivyo kwa takriban miongo yote miwili ambayo nilibahatika kuwa karibu naye. Angeweza kuandika vitabu lukuki vya utani na vichekesho na bado akabaki hajaishiwa.

Balaa la vunja mbavu liliongezeka maradufu pale alipokutana na marafiki  wengine wa karibu kama vile Balozi Mohamed Maharage (aliyekuja kumwachia kiti cha Mkuu wa Itifaki pale alipostaafu rasmi kazi takriban miaka mitatu iliyopita) kina Mudhihir Mudhihir, Job Juma, Max Rutihinda, David Mgwassa, Muddy Pizzaro, Makongoro Nyerere, Ronnie Mtawali, Wendo Mwapachu, Balozi Patrick Tsere, Balozi Amy Mpungwe, Zainnul Dossa, Henry Tandau, Philemon Ntahilaja na wengine wengi ambao nashindwa kuwataja wote kwa ufinyu wa nafasi. Hawa wakutanapo unakuwa hutaki kuondoka…

Yote tisa. Cisco pia alikuwa hodari katika kuhamasisha wadau kushiriki katika shughuli za mwenzetu wakati wa shida ama  raha, iwe harusi ama msiba. 

Huyu braza hatosahaulika pale alipoasisi kufanyika kwa michezo baina ya timu za veteran kutoka kila pembe ya jiji iliyokuja kujulikana kama Sunday Soccer Bonanza. Yaani kila Jumapili  wachezaji wa vilabu vya Veterans kutoka Sinza, Kinondoni, Ilala, Temeke walikutanika Leaders Club na kuchuana katika mchezo wa soka na baada ya hapo burudani ya muziki wa aidha Msondo ngoma ama Twanga Pepeta ilifuata. Umati uliokuwa unajaa hapo mahali si mchezo. Hakika Bonanza hilo lilifanikisha kwa kiasi kikubwa kuunganisha na kudumisha undugu miongoni vijana na watu wazima wa sehemu mbalimbali za Dar es salaam. Kama kuna mtu aliyekuwa ananung’unika san asana kwa kufifia kwa Bonanza hilo hivi sasa, basi  wa kwanza alikuwa Cisco.

Kama hilo Bonanza lilikuwa halitoshi, Cisco na wanachama wenzie wa TAZARA Club wakabuni hadhara ya kukutana mara moja kila mwaka kuwakumbuka na kuwaombea wenzetu wote waliotangulia mbele za haki kwa kisomo na dua za dini zote. Baada ya hapo ‘mpunga’ ulifinywa huku Balozi akichana mbavu za wadau kutwa nzima kwa vichekesho na stori za mjini. 

Nashindwa kukubali kwamba katika kisomo kifuatacho hapo Leaders Club jina la Abdul Omar Cisco Mtiro litatajwa katika orodha ya kuwarehemu wenzetu wote waliotangulia mbele ya haki.

Kama nilivyosema hapo awali, ugumu wa kumueleza mtu kama Cisco hauna tofauti na kuelezea jiji lolote kwa kutumia ukurasa mmoja tu. Yaani naweza kuandika kurasa mia kama hizi lakini bado nisiweze kusimulia robo tu  ya Cisco alikuwa ni mtu wa aina gani huku 'uraiani'.

Itoshe tu kusema kwamba kifo kimetupoka  mtu mmoja muhimu sana sana katika maisha yetu, na daima jina lake litabaki kuwa midomoni na ndani ya vilindi vya mioyo yetu daima.

ADIOS AMIGO, BRAZA CISCO!


 
 Cisco akiwa katika kutekeleza majukumu yake kama Balozi akiwa Malaysia

 Cisco aliketi pembeni yangu kuniliwaza nilipoondokewa na mwanagu Maggid mwaka jana

 Cisco akitaniana na Franco Kabigi (RiP) wakati wa 'kuufinya' baada ya kisomo cha kurehemu waliotangulia mbele ya haki Leaders  Club 

 Umati wakati wa Sunday Soccer Bonaza Leaders Club

 Mwadila Investments ilikuwa mojawapo ya timu za Kinondoni zilizoshiriki Bonanza hilo

 Uncle Phil akiwa tayari 'kuufinya'

 Wadau kutoka kila pembe ya jiji walishiriki hafla ya kurehemu waliotangulia mbele ya haki

 Umoja wa wana Dar es salaam usioweza kusahaulika

 Mpunga ukifinywa

 Umoja wa wana Dar es salaam

 Cisco (kulia, mwenye shati la Bluu) akipiga stori zake

 Cisco akiwa kazini siku Rais wa Marekani Bill Clinton alipozuru Tanzania

 Balozi Cisco akiwa kazini Lagos, Nigeria, kwenye mkutano uliohudhuriwa na Baba wa Taifa ma viongozi wengine wa Afrika

 Cisco akiwa katika kisomo klabu ya Saigon ambako alikuwa mwanachama 

 Cisco akiwa kazini kama mkuu wa Itifaki

Cisco akiwa na Mwalimu na Madiba

Ndege ya jeshi la Burma yapotea na watu 100 ndani




BBC,Burma. Ndege ya jeshi la Burma, iliyokuwa imewabeba zaidi ya watu 100, imetoweka.
Taarifa zilizotolewa na viongozi wa kitaifa wa Burma, zimeeleza kuwa ndege hiyo ya kijeshi, ilikuwa imeruka kati ya Yangon (Rangoon) na mji ulioko Kusini mwa nchi hiyo wa Myeik. Shughuli za kutafuta ndege hiyo.
"Tulipoteza mawasiliano na ndege hiyo kuanzia saa 4:35 leo asubuhi (saa za Afrika Mashariki),   ndege hiyo ilipofika maili 20 Magharibi mwa Mji wa Dawei," jeshi la Burma limetoa taarifa hiyo 
Inaelezwa kuwa ndege hiyo ilikuwa na abiria 105 na wafanyakazi 11.
Ndege za wanajeshi pamoja na helikopta zimetumwa katika eneo hilo katika shughuli za kuwatafuta manusura au mabaki ya ndege hiyo ambayo mpaka sasa inaaminika kuwa imeanguka.
Taarifa zinaongeza kuwa, ndege hiyo ilikuwa angani ikivuka bahari ya Andaman dakika chache baada ya kutoweka.

MKUU WA WILAYA YA ILALA, SOPHIA MJEMA AMEPOKEA MSAADA WA VYAKULA KWA AJILI YA WATU WASIOJIWEZA NA MAYATIMA

Ubalozi wa Kuwait nchini kwa kushirikiana na Taasisi  ya Human Relief wamekabidhi msaada wa vyakula mbalimbali kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema kwa ajili ya watu wasiojiweza na mayatima ili kupata futari katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo mapema leo, Mjema amesema, chakula hicho kitapelekwa katika vituo vya watoto yatima na wasiojiweza ili waweze kuufurahia mwezi wa Ramadhani.

"Chakula hiki tunaenda kuwapa wananchi ambao hawana uwezo na familia ambazo kwa kweli tunaona hwana uwezo," alisema Mh. Mjema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya Bigbon, Mohammed Bahashwan amesema, taasisi hiyo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali na hasa kwa mayatima bila kujadili dini zao,amesema na kuongeza kuwa kuwa mbali na kutoa misaada hiyo lakini pia taasisi hiyo imekuwa ikijenga visima na misikiti katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, balozi wa Kuwait nchini, Mhe Jaseem Al Najem amesema kuwa, nchi hiyo itaendelea kushirikiana na serikali katika mambo mbalimbali ya kusaidia jamii.

Amesema msaada huo wameanza na wilaya ya Ilala lakini watakuwa wakitoa misaada na maeneo mengine kulinga na uhitaji wa mambo mbalimbali katika jamii nzima kwa kushirikiana na serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala ,Sophia Mjema (kulia) akipokea Msaada wa vyakula mbalimbali kutoka kwa Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Jaseem Al Najem.Pichani kushoto ni Katibu Tawala wilaya ya Ilala,Edward Mpogolo.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala ,Sophia Mjema Akizungumza wa Globu ya jamii baada ya kupokea msaada huo.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala ,Sophia Mjema na Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Jaseem Al Najem wakiwa katika picha ya pamoja. leo Jijini Dar es Salaam.Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya jamii.
Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Mhe. Jaseem Al Najem akiwasili katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala ,Sophia Mjema.

Wednesday, June 7

Mghwira atemwa uenyekiti ACT Wazalendo







Kaimu Kiongozi wa ACT, Samson Mwingamba
Kaimu Kiongozi wa ACT, Samson Mwingamba akizungumza na wanahabari leo Jijini Dar es salaam Kuhusu maamuzi hayo 
Chama cha ACT Wazalendo kimmevua uongozi aliyekuwa mwenyekiti wake, Anna Mgwhira ambaye ameteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Chama hicho kimefikia hatua hiyo kwa kuzingatia ibara ya 17 ya katiba yake ambayo inatamka kuwa kiongozi wa chama atakoma kuendelea na madaraka yake iwapo atashindwa kutekeleza majukumu yake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Kaimu Kiongozi wa ACT, Samson Mwingamba alisema kamati ya uongozi wa ACT ulikutana leo lengo kuu ni kutafakari lililotokea kuona namna gani Mgwhira anaweza kutimiza majukumu yake kama Mwenyekiti na Mkuu wa Mkoa.
“Kama chama baada ya kutafakari kwa kina na baada ya mashauriano baina yake na viongozi kutumia katiba ya chama anakoma kuwa kiongozi kwa kuwa kutakuwa na mgongano wa majukumu, maslahi hivyo anakoma kuwa mwenyekiti,” alisema Mwigamba.
Mwigamba alisema kamati ya chama imemchagua Yeremia Maganja kuwa  Kaimu Mwenyekiti na kamati ilimpongeza Rais Magufuli kwa kumteua Mgwhira.
Hata hivyo, Mwigamba alisema Mghwira bado ataendelea kuwa mwanachama halali wa chama hicho.

WATOTO WENYE MATATIZO KUPATIWA MATIBABU NCHINI

WATOTO wenye matatizo ya usikivu watapata matibabu ya kupandikizwa vifaa vya usikivu hapa nchini katika Hospitali ya taifa ya Muhimbili badala ya kwenda nje ya nchi kwa matibabu kama ilivyokuwa awali.

Hayo yamesemwa na Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipozindua huduma hiyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili leo jijini Dar es salaam.

“Serikali haitapeleka mgonjwa mwenye matatizo ya kusikia nje ya nchi kwa ajili ya kupandikizwa vifaa vya kusikia na badala yake atatibiwa nchini ili kupunguza rufaa za wagonjwa wan je ya nchi” alisema Mh. Ummy.

Aidha Waziri Ummy amesisitiza juu ya umuhimu wakujiunga na mfuko wa Afya wa Jamii wa NHIF ili kupata fursa ya kutibiwa kwa gharama ndogo zaidi, huku akisisitiza kuwa wananchi wote watakaokuwa na kadi ya NHIF wataweza kupata matibabu ya upandikizaji wa kifaa cha kusikia bure kupata huduma hii.

Mbali na hayo Mh. Ummy ameahidi kuwa Serikali kupitia Wizara yake ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuunga mkono kwa kuisaidia hospitali ya Muhimbili ili kuendelea kufanikisha upasuaji wa Watoto hivyo kupunguza gharama inayopata Serikali kusafirisha Watoto hao nje ya nchi pindi wapatapo matatizo hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili Lawlence Mseru amsisitiza kuwa moja kati ya mipango ya Hospitali ya Muhimbili ni kuhakikisha kuwa wanapunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kila mara jambo linaloigharimu Serikali pesa nyingi. 

Aidha Dkt. Mseru aliongeza kuwa licha ya kufanikisha tukio hilo la Kihistoria wanaomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kusaidia kuboresha Wodi za Wagonjwa mahututi, ununuzi wa Vifaa tiba, kuongeza vyumba vya upasuaji jambo litalopunguza msongamano wa shughuli za hospitali pia kuongeza Wataalamu waendao nje ya nchi kwaajili ya mafunzo ili kuendeleza huduma katika nchi yetu jambo litakalosaidia kuwa na Wataalamu wengi hivyo kuweza kufanikisha huduma kwa wagonjwa wengi zaidi.

Nae Prof. Sunil Narayan Dutt kutoka Hospitali ya Apollo nchini India ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa jitihada inayoonesha hasa katika kutetea haki za watoto.

Kwa upande Bi. Hilda Bohela ambae ni mzazi wa Apulie Bohela aliyepata huduma hiyo nchini amewasihi wazazi wenzie kuwapeleka watoto kufanyiwa uchunguzi pindi waonapo hali isiyokuwa yakawaida kwa watoto wao na kuachana na mila potofu jambo linalopelekea watoto wengi kupata ulemavu .



waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watot, ummy Mwalimu (katikati) akizungumza leo jijini Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa Upasuaji wa Upandikizaji Kifaa cha Usikivu (Cochlear-Implant) kulishoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Lawrence Museru na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH), Profesa Charles Majinge.
waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ummy Mwalimu akiwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili leo jijini Dar es Salaam.
waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ummy Mwalimu akiwasili katika hospitali ya Taifa Muhimbili leo jijini Dar es Salaam. 
waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pomoja na watendaji wa hospitali ya Taifa Muhimbili leo jijini Dar es Salaam.Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya jamii.