Thursday, June 8

ADIOS AMIGO,BRAZA CISCO



Na Ankal - issa michuzi blog
Hebu jaribu kulielezea jiji la Dar, au la Arusha, ama la Mwanza,  Mbeya  ama jiji lolote lile, tena  kwa kutumia ukurasa mmoja tu na uwe umefanikiwa kulieleza kinagaubaga kiasi hata mtu ambaye hajawahi kufika hapo ajione kama keshafika na anapafahamu vizuri.

Basi huo ndio mtihani nilionao wakati naandika haya, tena kwa moyo mzito, nikijaribu kumwelezea rafiki yetu, kaka yetu, ndugu yetu, jamaa yetu au vyovyote vile upendavyo kumwita mtu kama Balozi Abdulcisco  Omar Mtiro almarufu kama CISCO.
Labda uamue kuzungumzia kamtaa  kamoja tu katika kitongoji kimoja, ndipo kidooooogo unaweza kufanikiwa kueleza vitu vikaeleweka. nami ndivyo najaribu kufanya hapa, kwa kudonyoa kasehemu tu ka Braza Cisco.

Ni kweli kwamba mtu akitangulia mbele ya haki huwa kuna hulka ya kumsifia na kumuenzi mtu huyo. Lakini si uwongo kwamba haya niandikayo hapa, japo yalikuwa nyuma ya ubongo wa wengi wetu siku zote, ni halisi na wala sio kwa sababu Cisco hatunaye tena. 

Kwa wengi alikuwa mkarimu na mwingi wa bashasha saa zote. Kwa tuliobahatika kuwa karibu naye, Cisco alikuwa hivyo na zaidi. Pamoja na kuwa na wadhifa mkubwa serikalini (Balozi wetu nchini Nigeria na Malaysia katika nyakati mbalimbali na baadaye Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje), Cisco alikuwa mtu wa kujichanganya na kila mtu bila kujali hali ama mali zake. Hakuwa na makuu wala makidai. Alikuwa mtu mmoja 'freshi' sana, wanasema vijana wa mjini.

Unapomkuta na wanachama wenzie wa Klabu ya michezo ya TAZARA pale Leaders Club ama kwa Octa (kijiwe maarufu  jirani na ubalozi wa Ufaransa) ilikuwa huwezi kuamini kwamba huyu mtu mchana ametoka kusuguana mabega na viongozi wakuu wa nchi na wageni wao ambao, akiwa kama Mkuu wa Itifaki,  jukumu lake lilikuwa kuratibu na kusimamia kila kitu. 

Ubaya, ama uzuri wake, hukumsikia hata mara moja akizungumzia kazi yake ama wadhifa wake. Huko alikuwa serious kama askari wa Mjerumani. Lakini afikapo kijiweni, kama mlivyo nyinyi wakati huo, na yeye  pia alijitosa kuogelea nanyi kwenye soga za siku kama vile kandanda,  stori zote za mjini, pamoja na muziki ambao alikuwa anaupenda sana – hasa hasa Jazz, Classics, Old Skul na Chachacha.

Sifa yake kubwa akiwa nasi kijiweni ilikuwa ni utani na vichekesho vya kuvunja mabvu. Yaani Cisco alikuwa hakosi kuja na ‘mpya’ hata kabla ya kuketi kitini, na wakati wa kuondoka kwenda kupumzika alikuwa hakosi kuwaacha na ‘kibomu’ kingine cha kuchana mbavu. Vile vile kila ukutanapo naye lazima ‘akuchape’ na kitu kipya. 

Na hiyo ilikuwa hivyo kwa takriban miongo yote miwili ambayo nilibahatika kuwa karibu naye. Angeweza kuandika vitabu lukuki vya utani na vichekesho na bado akabaki hajaishiwa.

Balaa la vunja mbavu liliongezeka maradufu pale alipokutana na marafiki  wengine wa karibu kama vile Balozi Mohamed Maharage (aliyekuja kumwachia kiti cha Mkuu wa Itifaki pale alipostaafu rasmi kazi takriban miaka mitatu iliyopita) kina Mudhihir Mudhihir, Job Juma, Max Rutihinda, David Mgwassa, Muddy Pizzaro, Makongoro Nyerere, Ronnie Mtawali, Wendo Mwapachu, Balozi Patrick Tsere, Balozi Amy Mpungwe, Zainnul Dossa, Henry Tandau, Philemon Ntahilaja na wengine wengi ambao nashindwa kuwataja wote kwa ufinyu wa nafasi. Hawa wakutanapo unakuwa hutaki kuondoka…

Yote tisa. Cisco pia alikuwa hodari katika kuhamasisha wadau kushiriki katika shughuli za mwenzetu wakati wa shida ama  raha, iwe harusi ama msiba. 

Huyu braza hatosahaulika pale alipoasisi kufanyika kwa michezo baina ya timu za veteran kutoka kila pembe ya jiji iliyokuja kujulikana kama Sunday Soccer Bonanza. Yaani kila Jumapili  wachezaji wa vilabu vya Veterans kutoka Sinza, Kinondoni, Ilala, Temeke walikutanika Leaders Club na kuchuana katika mchezo wa soka na baada ya hapo burudani ya muziki wa aidha Msondo ngoma ama Twanga Pepeta ilifuata. Umati uliokuwa unajaa hapo mahali si mchezo. Hakika Bonanza hilo lilifanikisha kwa kiasi kikubwa kuunganisha na kudumisha undugu miongoni vijana na watu wazima wa sehemu mbalimbali za Dar es salaam. Kama kuna mtu aliyekuwa ananung’unika san asana kwa kufifia kwa Bonanza hilo hivi sasa, basi  wa kwanza alikuwa Cisco.

Kama hilo Bonanza lilikuwa halitoshi, Cisco na wanachama wenzie wa TAZARA Club wakabuni hadhara ya kukutana mara moja kila mwaka kuwakumbuka na kuwaombea wenzetu wote waliotangulia mbele za haki kwa kisomo na dua za dini zote. Baada ya hapo ‘mpunga’ ulifinywa huku Balozi akichana mbavu za wadau kutwa nzima kwa vichekesho na stori za mjini. 

Nashindwa kukubali kwamba katika kisomo kifuatacho hapo Leaders Club jina la Abdul Omar Cisco Mtiro litatajwa katika orodha ya kuwarehemu wenzetu wote waliotangulia mbele ya haki.

Kama nilivyosema hapo awali, ugumu wa kumueleza mtu kama Cisco hauna tofauti na kuelezea jiji lolote kwa kutumia ukurasa mmoja tu. Yaani naweza kuandika kurasa mia kama hizi lakini bado nisiweze kusimulia robo tu  ya Cisco alikuwa ni mtu wa aina gani huku 'uraiani'.

Itoshe tu kusema kwamba kifo kimetupoka  mtu mmoja muhimu sana sana katika maisha yetu, na daima jina lake litabaki kuwa midomoni na ndani ya vilindi vya mioyo yetu daima.

ADIOS AMIGO, BRAZA CISCO!


 
 Cisco akiwa katika kutekeleza majukumu yake kama Balozi akiwa Malaysia

 Cisco aliketi pembeni yangu kuniliwaza nilipoondokewa na mwanagu Maggid mwaka jana

 Cisco akitaniana na Franco Kabigi (RiP) wakati wa 'kuufinya' baada ya kisomo cha kurehemu waliotangulia mbele ya haki Leaders  Club 

 Umati wakati wa Sunday Soccer Bonaza Leaders Club

 Mwadila Investments ilikuwa mojawapo ya timu za Kinondoni zilizoshiriki Bonanza hilo

 Uncle Phil akiwa tayari 'kuufinya'

 Wadau kutoka kila pembe ya jiji walishiriki hafla ya kurehemu waliotangulia mbele ya haki

 Umoja wa wana Dar es salaam usioweza kusahaulika

 Mpunga ukifinywa

 Umoja wa wana Dar es salaam

 Cisco (kulia, mwenye shati la Bluu) akipiga stori zake

 Cisco akiwa kazini siku Rais wa Marekani Bill Clinton alipozuru Tanzania

 Balozi Cisco akiwa kazini Lagos, Nigeria, kwenye mkutano uliohudhuriwa na Baba wa Taifa ma viongozi wengine wa Afrika

 Cisco akiwa katika kisomo klabu ya Saigon ambako alikuwa mwanachama 

 Cisco akiwa kazini kama mkuu wa Itifaki

Cisco akiwa na Mwalimu na Madiba

Ndege ya jeshi la Burma yapotea na watu 100 ndani




BBC,Burma. Ndege ya jeshi la Burma, iliyokuwa imewabeba zaidi ya watu 100, imetoweka.
Taarifa zilizotolewa na viongozi wa kitaifa wa Burma, zimeeleza kuwa ndege hiyo ya kijeshi, ilikuwa imeruka kati ya Yangon (Rangoon) na mji ulioko Kusini mwa nchi hiyo wa Myeik. Shughuli za kutafuta ndege hiyo.
"Tulipoteza mawasiliano na ndege hiyo kuanzia saa 4:35 leo asubuhi (saa za Afrika Mashariki),   ndege hiyo ilipofika maili 20 Magharibi mwa Mji wa Dawei," jeshi la Burma limetoa taarifa hiyo 
Inaelezwa kuwa ndege hiyo ilikuwa na abiria 105 na wafanyakazi 11.
Ndege za wanajeshi pamoja na helikopta zimetumwa katika eneo hilo katika shughuli za kuwatafuta manusura au mabaki ya ndege hiyo ambayo mpaka sasa inaaminika kuwa imeanguka.
Taarifa zinaongeza kuwa, ndege hiyo ilikuwa angani ikivuka bahari ya Andaman dakika chache baada ya kutoweka.

MKUU WA WILAYA YA ILALA, SOPHIA MJEMA AMEPOKEA MSAADA WA VYAKULA KWA AJILI YA WATU WASIOJIWEZA NA MAYATIMA

Ubalozi wa Kuwait nchini kwa kushirikiana na Taasisi  ya Human Relief wamekabidhi msaada wa vyakula mbalimbali kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema kwa ajili ya watu wasiojiweza na mayatima ili kupata futari katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo mapema leo, Mjema amesema, chakula hicho kitapelekwa katika vituo vya watoto yatima na wasiojiweza ili waweze kuufurahia mwezi wa Ramadhani.

"Chakula hiki tunaenda kuwapa wananchi ambao hawana uwezo na familia ambazo kwa kweli tunaona hwana uwezo," alisema Mh. Mjema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya Bigbon, Mohammed Bahashwan amesema, taasisi hiyo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali na hasa kwa mayatima bila kujadili dini zao,amesema na kuongeza kuwa kuwa mbali na kutoa misaada hiyo lakini pia taasisi hiyo imekuwa ikijenga visima na misikiti katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, balozi wa Kuwait nchini, Mhe Jaseem Al Najem amesema kuwa, nchi hiyo itaendelea kushirikiana na serikali katika mambo mbalimbali ya kusaidia jamii.

Amesema msaada huo wameanza na wilaya ya Ilala lakini watakuwa wakitoa misaada na maeneo mengine kulinga na uhitaji wa mambo mbalimbali katika jamii nzima kwa kushirikiana na serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala ,Sophia Mjema (kulia) akipokea Msaada wa vyakula mbalimbali kutoka kwa Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Jaseem Al Najem.Pichani kushoto ni Katibu Tawala wilaya ya Ilala,Edward Mpogolo.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala ,Sophia Mjema Akizungumza wa Globu ya jamii baada ya kupokea msaada huo.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala ,Sophia Mjema na Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Jaseem Al Najem wakiwa katika picha ya pamoja. leo Jijini Dar es Salaam.Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya jamii.
Balozi wa Kuwait nchini Tanzania Mhe. Jaseem Al Najem akiwasili katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala ,Sophia Mjema.

Wednesday, June 7

Mghwira atemwa uenyekiti ACT Wazalendo







Kaimu Kiongozi wa ACT, Samson Mwingamba
Kaimu Kiongozi wa ACT, Samson Mwingamba akizungumza na wanahabari leo Jijini Dar es salaam Kuhusu maamuzi hayo 
Chama cha ACT Wazalendo kimmevua uongozi aliyekuwa mwenyekiti wake, Anna Mgwhira ambaye ameteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Chama hicho kimefikia hatua hiyo kwa kuzingatia ibara ya 17 ya katiba yake ambayo inatamka kuwa kiongozi wa chama atakoma kuendelea na madaraka yake iwapo atashindwa kutekeleza majukumu yake.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Kaimu Kiongozi wa ACT, Samson Mwingamba alisema kamati ya uongozi wa ACT ulikutana leo lengo kuu ni kutafakari lililotokea kuona namna gani Mgwhira anaweza kutimiza majukumu yake kama Mwenyekiti na Mkuu wa Mkoa.
“Kama chama baada ya kutafakari kwa kina na baada ya mashauriano baina yake na viongozi kutumia katiba ya chama anakoma kuwa kiongozi kwa kuwa kutakuwa na mgongano wa majukumu, maslahi hivyo anakoma kuwa mwenyekiti,” alisema Mwigamba.
Mwigamba alisema kamati ya chama imemchagua Yeremia Maganja kuwa  Kaimu Mwenyekiti na kamati ilimpongeza Rais Magufuli kwa kumteua Mgwhira.
Hata hivyo, Mwigamba alisema Mghwira bado ataendelea kuwa mwanachama halali wa chama hicho.

WATOTO WENYE MATATIZO KUPATIWA MATIBABU NCHINI

WATOTO wenye matatizo ya usikivu watapata matibabu ya kupandikizwa vifaa vya usikivu hapa nchini katika Hospitali ya taifa ya Muhimbili badala ya kwenda nje ya nchi kwa matibabu kama ilivyokuwa awali.

Hayo yamesemwa na Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati alipozindua huduma hiyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili leo jijini Dar es salaam.

“Serikali haitapeleka mgonjwa mwenye matatizo ya kusikia nje ya nchi kwa ajili ya kupandikizwa vifaa vya kusikia na badala yake atatibiwa nchini ili kupunguza rufaa za wagonjwa wan je ya nchi” alisema Mh. Ummy.

Aidha Waziri Ummy amesisitiza juu ya umuhimu wakujiunga na mfuko wa Afya wa Jamii wa NHIF ili kupata fursa ya kutibiwa kwa gharama ndogo zaidi, huku akisisitiza kuwa wananchi wote watakaokuwa na kadi ya NHIF wataweza kupata matibabu ya upandikizaji wa kifaa cha kusikia bure kupata huduma hii.

Mbali na hayo Mh. Ummy ameahidi kuwa Serikali kupitia Wizara yake ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuunga mkono kwa kuisaidia hospitali ya Muhimbili ili kuendelea kufanikisha upasuaji wa Watoto hivyo kupunguza gharama inayopata Serikali kusafirisha Watoto hao nje ya nchi pindi wapatapo matatizo hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili Lawlence Mseru amsisitiza kuwa moja kati ya mipango ya Hospitali ya Muhimbili ni kuhakikisha kuwa wanapunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kila mara jambo linaloigharimu Serikali pesa nyingi. 

Aidha Dkt. Mseru aliongeza kuwa licha ya kufanikisha tukio hilo la Kihistoria wanaomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kusaidia kuboresha Wodi za Wagonjwa mahututi, ununuzi wa Vifaa tiba, kuongeza vyumba vya upasuaji jambo litalopunguza msongamano wa shughuli za hospitali pia kuongeza Wataalamu waendao nje ya nchi kwaajili ya mafunzo ili kuendeleza huduma katika nchi yetu jambo litakalosaidia kuwa na Wataalamu wengi hivyo kuweza kufanikisha huduma kwa wagonjwa wengi zaidi.

Nae Prof. Sunil Narayan Dutt kutoka Hospitali ya Apollo nchini India ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa jitihada inayoonesha hasa katika kutetea haki za watoto.

Kwa upande Bi. Hilda Bohela ambae ni mzazi wa Apulie Bohela aliyepata huduma hiyo nchini amewasihi wazazi wenzie kuwapeleka watoto kufanyiwa uchunguzi pindi waonapo hali isiyokuwa yakawaida kwa watoto wao na kuachana na mila potofu jambo linalopelekea watoto wengi kupata ulemavu .



waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watot, ummy Mwalimu (katikati) akizungumza leo jijini Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa Upasuaji wa Upandikizaji Kifaa cha Usikivu (Cochlear-Implant) kulishoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Profesa Lawrence Museru na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH), Profesa Charles Majinge.
waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ummy Mwalimu akiwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili leo jijini Dar es Salaam.
waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ummy Mwalimu akiwasili katika hospitali ya Taifa Muhimbili leo jijini Dar es Salaam. 
waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ummy Mwalimu akiwa katika picha ya pomoja na watendaji wa hospitali ya Taifa Muhimbili leo jijini Dar es Salaam.Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya jamii.

Tuesday, June 6

Cisco kuzikwa kesho Kisutu


Balozi Abdul Cisco Mtiro enzi za uhai wake 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi
Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Itifaki Ikulu katika Serikali ya awamu ya tatu na nne, Balozi Abdul Mtiro ‘Cisco’ utazikwa kesho, Jumatano, katika makaburi ya Kisutu jijini hapa.
Cisco ambaye pia aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Ufilipino, Cambodia na Singapore, alifariki juzi katika Hospitali ya Agha Khan alikokuwa akipatiwa matibabu.
Omar Mtiro ambaye  ni mtoto wa kwanza wa marehemu Cisco kati ya wanne, amesema mazishi  yatafanyika kesho  saa 7.00 mchana katika makaburi ya Kisutu.
Omar amesema kabla ya maziko, mwili wake utapelekwa nyumbani kwake Mikocheni B saa 5.00 asubuhi kwa ajili ya kufanyiwa kisomo na sala.
Kuhusu chanzo cha kifo chake Omar amesema, “suala la chanzo cha kifo chake nisingeependa kukizungumzia ibaki kuwa ‘privacy’ (faragha), lakini mzee aliumwa kwa wiki mbili hadi anafikwa na mauti.”
Kufuatia kifo hicho juzi Rais John Magufuli alituma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na mabalozi wengine kwa kuondokewa na mpendwa wao.


MAREHEMU NDESAMBURO AZIKWA LEO KIJIJINI KWAKE MKOANI KILIMANJARO


Gari lililobeba mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Phillemon Ndesamburo likielekea kwenye kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kiboriloni kwa ajili ya kuombewa. Maziko ya Marehemu Ndesamburo yanafanyika leo nyumbani kwake mtaa wa  KDC- Moshi,mkoani Kilimanjaro.
Gari lililobeba mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Phillemon Ndesamburo likiingia kwenye kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kiboroloni.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe akiiingia katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kiboroloni kwa ajili ya kumuaga aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Phillemon Ndesamburo.
Viongozi mbali mbali wa Chadema wakiingia katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kiboriloni.
Viongozi mbali mbali wa Chadema wakiingia katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kiboriloni. Waziri mkuu wa Zamani ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa akiingia kanisani.
Wabunge wa Chadema wakiwa wamejipanga kupokea mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Phillemon Ndesamburo katika kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kiboriloni.
Wajukuu wa Marehemu Phillemon Ndesamburo wakielekea kanisani.
Mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Phillemon Ndesamburo ukiingizwa kanisani.
Waziri mkuu wa Zamani ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa akibadilishana mawazo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi katika ibada ya kumuaga aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Phillemon Ndesamburo.
Viongozo wa Chadema wakiwa katika ibada ya kumuombea aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Phillemon Ndesamburo.
Mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Phillemon Ndesamburo ukiwa kanisani tayari kwa maombezi.
Mke wa Marehemu aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Kilimanjaro, Phillemon Ndesamburo (wa pili toka kushoto) akiwa kanisani.

RAIS DKT. MAGUFULI AMUAPISHA MHE ANNA ELISHA MGHWIRA KUWA MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO LEO



 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Anna Elisha Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Anna Elisha Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Ikulu jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Elisha Mghwira Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi ,Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Elisha Mghwira, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na viongozi wengine Ikulu jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara Rodrick Mpogolo akimkabidhi Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Elisha Mghwira huku Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ,Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Salum Hapi pamoja na wakuuu wa Wilaya za Ubungo na Ilala wakipiga makofi. Picha na IKULU

VIJANA WATOA SIRI KUFICHUA MITANDAO YA UHALIFU NCHINI


TAA 2















Zaidi ya vijana wapatao  1230  wametoa siri nzito kwa  Maaskofu na Mashekhe  kutoka katika Kamati ya Kitaifa ya Maadili , Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini  Nchini  kufichua mtandao  haramu  wa watu  wanaoendesha mauaji na uhalifu mwingine kwenye   mikoa  13, nchini kama njia muhimu ya kumpongeza IGP mpya, Saimoni Sirro.

 Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Askofu William Mwamalanga, siri hiyo imetolewa  jana  na vijana hao katika   siku ya  tatu  mkutano wa kujenga maadili kwa vijana unao fanyika Mbagala, jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha   vijana  wa madhehebu mbalimbali ya dini  kutoka katika  mikoa ya Pwani, Tanga, Lindi,  Morogoro,Dar es Salaam  ambapo wameyataja maeneo ya Mkuranga, Rufiji  Kigamboni, Kibiti, Msata, Tanga mjini, Pemba na Unguja kuwa maeneo hatari yanayowajengea vijana imani za  kigaidi.

 Aidha, Askofu Mwamalanga alisema kuwa vijana 147  wa kiislamu wanaohudhuria mkutano huo  wamewataja  baadhi ya watu  ambao ni   hatari  na wamekuwa wakieneza elimu ya mauaji  kwenye  misikiti mbali mbali nchini kwa kuiita Serikali ya Awamu ya Tano jina la katili na kwamba elimu hiyo imesambazwa kwa kasi  katika mikoa ya  Kagera, Tanga, Mwanza, Arusha, Pemba, Unguja, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Morogoro, Iringa, Singida, Dodoma, Pwani na Kigoma huku vikosi vya vijana vikiandaliwa kufanya mauaji  mara baada ya mufungo mtukufu wa Ramadhani kama yale ambayo yamekuwa yakifanywa  Mukuranga, Kibiti  na Rufiji. 

Vijana hao wanamuomba  IGP  Sirro kuwachukulia hatua kali maafisa wa jeshi hilo ambao wanatumia jeshi kupandikiza Umngiki, na  kwamba wana imani na IGP Sirro amabaye kwa mujibu wa hao vijana hatamwangusha Rais  Magufuli na watanzania kwa ujumla.

Akifunga  Mkutano huo  Askofu Mwamalanga  amemtaja IGP  Sirro kama polisi mahiri wa maadili na jemadali  mweledi wa mapambano hivyo amewataka  vijana kote nchini kumuunga mkono kwa kuwafichua polisi wote wanaoenzi uhalifu. “Tusipofanya hivyo tutakuwa  kama  pipa zuri  tunalo jaza maji wakati tukijua chini limetoboka”,alisema Askofu Mwamalanga na kuongeza kuwa raia wema ni asilimia 99.9  wahalifu ni 0.1   hii ina maana kuwa ukiondoa polisi wahalifu  ndani ya jeshi hilo wahalifu ni wachache mno  mitaani  watayeyuka wenyewe. 

Aidha,  Askofu huyo amewahimiza vijana na viongozi wa dini kushiriki kwenye mafunzo hayo kote nchini ili  wapewe ufahamu wa elimu ya maadili ya kweli  ili wawe walinzi wa taifa na kupenda amani  na kuweka uchu wa kuchukia rushwa  na kujiwekea  mitazamo ya kupenda kazi za baraka.

Kiongozi huyo wa dini amekemea vikali nyumba za ibada   kugeuzwa  eneo la mafunzo ya uhalifu kwani ni aibu kwa msikiti au kanisa kufanya  mafunzo ya kigaidi  ndani  ya  nyumba  za ibada  kufanya hivyo ni ibada ya sanamu, watu wa jinsi hiyo hawana uhusiano wowote na Mwenyenzi MUNGU ambaye kusudi lake ni kuondoa uovu kwa mwanadamu.

Hivi karibuni yametokea mauaji ya viongozi wa Chama Tawala maeneo ya Kibiti, Mukuranga na Rufiji na kufanya wakazi wa maeneo hayo kuishi kwa wasiwasi na mashaka juu ya maisha yao. Wakati akiipishwa kuwa IGP, Kamanda Simon Sirro alisema kupambana na kuondoa uhalifu kwa kushirikiana na raia wema ni moja ya vipaumbele vyake.