Saturday, March 3

Vigogo Maliasili watoa kauli kinzani kifo cha faru

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi. 
Dar es Salaam. Licha ya mauaji ya faru mmoja katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kutokea Desemba mwaka jana, hadi sasa hakuna taarifa kamili iliyotolewa huku watendaji waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wakitoa kauli zinazokinzana.
Wakati katibu mkuu, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akisema kunafanyika uchunguzi wa kawaida, Naibu Waziri Japhet Hasunga amekaririwa akisema unafanyika uchunguzi wa kina ukihusisha kuundwa kwa kamati maalumu.
Licha ya kusema kuna uchunguzi wa kawaida, Meja Jenerali Milanzi amekanusha pia madai ya kuhojiwa viongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Chanzo cha taarifa kimelieleza Mwananchi kuwa baada ya wizara kupata taarifa iliundwa kamati ya kuchunguza tukio hilo ambayo pia iliwahoji maofisa wa Tanapa na kwamba kazi hiyo imekamilika.
Alipopigiwa simu na kuulizwa kuhusu suala hilo juzi, mkurugenzi mkuu wa Tanapa, Allan Kijazi alimtaka mwandishi ampigie baada ya saa moja kwa maelezo hakuwa sehemu nzuri.
Baada ya muda huo kupita, meneja mawasiliano wa Tanapa, Pascal Shelutete alimpigia simu mwandishi akisema ametumwa na bosi wake kumsikiliza.
Alipoulizwa taarifa za mauaji ya faru huyo katika Hifadhi ya Serengeti na kwamba kuna maofisa wa Tanapa wamehojiwa na wizara, Shelutete alikiri kutokea kwa mauaji lakini alikanusha maofisa kuhojiwa.
“Taarifa hizo ni za kweli na ziko mikononi mwa vyombo vya dola zinashughulikiwa. Si kweli kwamba tulichelewesha taarifa, tulitoa mapema tu,” alisema Shelutete alipoulizwa ni kwa nini taarifa za kuuawa kwa faru huyo hazikutolewa mapema.
Shelutete alimwahidi mwandishi kuwa atampigia tena baadaye. Baada ya saa tano kupita bila simu kupigiwa, mwandishi alimpigia tena lakini hakupokea bali alituma ujumbe wa maandishi akiandika, ‘Nakupigia’.
Meneja huyo hakupiga simu badala yake alitoa taarifa kwa vyombo vya habari juzi kuhusu tukio hilo ikisema Tanapa inawashikilia watuhumiwa wanne wanaodaiwa kuwa miongoni mwa mtandao wa ujangili na mauaji ya faru katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Desemba mwaka jana.
“Pamoja nao, shirika pia limefanikiwa kukamata bunduki aina ya rifle inayoaminika kutumika katika tukio hilo. Shirika linaendelea kushirikiana kwa karibu na vyombo vingine vya dola kukamilisha uchunguzi utakaopelekea kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wahusika,” imesema taarifa ya Tanapa.
Jana alipopigiwa simu, Shelutete alisema lengo la kutotoa taarifa hiyo mapema ilikuwa ni kulinda uchunguzi unaoendelea.
“Hata hiyo taarifa unaiona tumeitoa kwa ufupi kwa sababu the more you reveal to the public, (kadri unavyotoa taarifa kwa umma) the more unapoteza chance (nafasi) za kuwakamata hao majangili, kwa sababu ni mtandao mkubwa. Naomba muwe wavumilivu, uchunguzi ukikamilika tutawapa taarifa,” alisema Shelutete.
Ufafanuzi wa wizara
Akizungumza kwa simu, Meja Jenerali Milanzi alikiri kutokea kwa mauaji akisema ni ya kawaida na kwamba kuna uchunguzi wa kawaida unaendelea kuhusu hilo.
“Ni kweli. Mara nyingi huwa ni ‘routine investigation’ inafanyika lakini si kuwahoji viongozi wa Tanapa. Ikitokea ‘incident’ (tukio) yoyote kama mnyama amekufa au ameuawa kunakuwa na ‘routine investigation’. Huwa ni kwenda field pale wanapotupa taarifa. It’s a normal investigation (ni uchunguzi wa kawaida).
Meja Jenerali Milanzi alisema Tanapa waliwapa taarifa mapema na walishaanza kufuatilia.
Alisema licha ya mauaji ya mnyama huyo, bado faru wapo wengi ijapokuwa hakutaja idadi.
“Faru bado wapo hawawezi kwisha. Hata tembo wanapokufa huwa tunachunguza ametoka familia gani. Mnyama akifa ni kawaida mzoga wake kuliwa, lakini hawa wakubwa tunawalinda hata wasiliwe na ‘predators’ (wanyama wanaokula nyama)”.
Alipoulizwa sababu ya Tanapa kuchelewesha taarifa kwa vyombo vya habari alisema, “Kwani ulitaka tufanyeje? Huo ukimya mimi sifahamu kwa nini, labda nitazungumza na Tanapa, lakini naona wametoa taarifa yao jana (juzi).”
Lakini Naibu Waziri Hasunga alisema baada ya kupata taarifa kutoka Tanapa waliunda kamati kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kina.
“Tuliunda kamati kupata taarifa za kina baada ya kupata taarifa ya Tanapa. Hawakuchelewesha taarifa, ila tuliona kuna haja ya kujiridhisha zaidi,” alisema Hasunga.

Mbinu za kuwaepuka madalali wa mazao


Wiki iliyopita jarida hili lilichapisha makala kuhusu kilio cha wakulima, wakiwalalamikia madalali wa mazao kuwa ni kikwazo cha maendeleo yao.
Katika makala haya, wakulima wanaeleza jinsi ambavyo baadhi ya nyakati, wanavyoweza kuwaepuka madalali hao ambao uwepo wao katika masoko unaonekana kuwa kama mfumo rasmi wa uendeshaji wa masoko nchini.
Mkulima wa matunda kutoka wilayani Bagamoyo, Lucy Salema anasema : “Hawa mbona kuwaepuka ni kazi rahisi tu ilimradi tu kuwepo na utaratibu maalum kwenye haya masoko makubwa mfano Kariakoo ili madalali wasiwepo kabisa.”
Anasema kuwa kinachotakiwa kwa mkulima ni kutoa taarifa mapema kwa kiongozi wa soko kabla hajapeleka mazao sokoni, ili kiongozi huyo ajue kwamba ni wakulima wangapi wataingiza mazao sokoni na taarifa hiyo itolewe mwezi mmoja kabla.
Utaratibu huo utampa nafasi kiongozi wa soko kujua ni wakulima wangapi wataleta mazao ya aina moja na wangapi wataleta aina nyingine. Ni utaratibu ambao utasaidia kuondoa msongamano wa wingi wa watu wanaopeleka mazao.
“Wakulima tukienda sokoni wengi, madalali wanapata nafasi nzuri ya kutuumiza, kwa sababu wanajua mkulima hawezi kumkataa maana matunda ukikaa nayo sana yanaharibika, lakini kiongozi wa soko akisimama imara hatuwezi kunyanyaswa na watu hawa,” anasema.
Kwa mkulima, Salim Magege anayeishi mkoani Mwanza, anasema kinachotakiwa kufanywa ni ushirikiano kati ya mkulima, kiongozi wa soko na mnunuzi bila hivyo hawawezi kumaliza tatizo hilo la madalali sokoni wanaokandamiza haki za wakulima.
“Uwezekano wa kutotumia madalali sokoni upo tena mkubwa tu, yaani ni bora kama kuna ushuru mkulima nilipe moja kwa moja kwa uongozi wa soko na uongozi wa soko unikutanishe moja kwa moja na mnunuzi,” anasema.
Anasema kinachofanyika sasa ni kwamba madalali wanachukua fedha, uongozi wa soko nao wanachukua fedha kwa hiyo kuna mlolongo mkubwa ambao mkulima anapitia.
“Ukiangalia kiashiria kikubwa kuwa madalali wanatudhulumu ni kushusha bei. Kwa mfano, mkulima anaenda soko kuu la Kariakoo kwa lengo la kuuza vitunguu Sh 150,000 kwa gunia, lakini ukikutana na dalali unaambiwa uuze kwa 130,000,”anaeleza.
Anasema kuwa madalali wakipanga bei, hawataki mabishano kwani ukifanya hivyo huwezi kupata mteja na bidhaa yako itaoza.
Viongozi wa masoko wawazungumzia madalali
Saidi Mzuzure ni mjumbe wa kamati ya soko la Sterio wilayani Temeke anasema: “Sio kweli kuwa tunawabeba madalali kwa sababu kiongozi wa soko ni kiongozi wa mteja na mkulima kwani bila wao hakuna soko.’’
Akielezea taratibu za soko lao, anasema madalali nao ni wakusanya kodi, kwa kuwa mkulima anapouza bila ya kumtumia dalali Serikali ya wilaya inakosa mapato.
“Tukisema pia hawa wakulima wauze bila kupitia kwa dalali hatuwezi kukusanya ushuru, kwa sababu mkulima anapokuja hapa na kuuza mazao yake bila dalali akipata tu mtu akamuuzia utakuta mkulima yule anaondoka na yule mnunuzi anaondoka na mwishowe Manispaa haipati mapato,”anasema.
Isihaka Ofiole ambaye ni Kaimu Katibu wa soko la Buguruni, anasema wanatambua uwepo wa madalali katika soko hilo ila kuhusu wakulima kudhulumiwa hawalitambui hilo kwani makubaliano hufanywa kati ya wakulima wenyewe na madalali.
“Hilo la kudhulumiwa sijapata malalamiko, lakini kwa kucheleweshewa malipo inatokea mara kwa mara na hii ni kutokana na wakulima na madalali kutotoa taarifa kwa uongozi wa soko pindi wanapokabidhiana mazao yao,” anasema.
Ofiole hata hivyo, anasema madalali wanatokana na wakulima wenyewe kwa kuwa ndio wanaowapa mzigo. Anasema kilichozoeleka ni ule utamaduni waliojiwekea wakulima wa kuuza kupitia kwa dalali hasa kwa wale wanaoleata mzigo mkubwa.
“Lakini pia wakati mwingine mkulima ni mgeni, labda ametokea mkoani kwa hiyo huyu huwezi tu ukamwachia auze vinginevyo watu watamzunguka huko nje na hatimaye matapeli watamuibia, ndiyo maana tunamkabidhi kwa dalali,” anasema.
Anasema dalali anapokabidhiwa mzigo na mkulima na kuuhifadhi anabeba jukumu la kuulinda, kuuhifadhi na hata kulipia ushuru. Ni jukumu lake kwa kuwa yeye ndiye muuzaji.
Ofiole anawashauri wakulima kuwaona viongozi wa masoko kabla ya kuwapa mzigo madalali. Anasema kosa wanalolifanya wakulima ni kukabidhi mzigo kwa dalali bila kuwa na hati ya maandishi, hivyo uongozi unashindwa kuingilia kati kwa sababu hakuna uthibitisho unao onyesha kuwa wawili hao walikabidhiana mzigo.
Wenyewe wajitetea
Dalali wa mbogamboga katika soko la Temeke Sterio, Amosi Kimbute, anasema wanachakifanya wao ni utekelezaji wa majukumu yao, kwani hata kama wasingekwepo bado wakulima wangelalamika.
‘’Ukweli ni kwamba bila sisi hawawezi kuuza mazao yao. Nasema hivyo kwa sababu madalali tuna mtandao mkubwa na tunajua wapi kuna wanunuzi na yupi mnunuuzi wa kweli,”anasema.
Kuhusu bei anasema ni suala la makubaliano kati yao na wakulima na hata wanapopanga wao madalali, lazima wawaulize wenyewe wakulima kama wameridhia au hawajaridhia.
“Sawa tunapanga bei lakini huwa hatulazimishi mtu kukubaliana na bei ile kama akikataa basi na mara nyingi wakikataa tukiwaacha wanaanza kulalamika na ku tubembeleza,”anaongeza.
Anasema kwa mkulima anayelalamika kutapeliwa basi amekutana na dalali ambaye hatambuliki katika soko, kwa sababu madalali wanajuana na wanahakikisha hakuna mkulima anayedhulumiwa.
‘’Unakuta mkulima analeta tikiti zaidi ya 2000 na unapomtafutia mteja dalali anachukua Sh200 pekee sasa hapo namdhulumu vipi?anahoji.
Naye Omari Othman ambaye ni dalali wa matunda katika soko la Buguruni, anasema madalali hawapangi bei ila wanapanga pamoja kati yao na mkulima.
“Kwa wale wanaokwenda shamba sawa lakini sisi wa sokoni inategemea ila mara nyingi bei tunapanga pamoja na mkulima na tunauza pamoja hadi pale matunda yatakapokwisha,”anasema Othman na kuongeza:
“Changamoto iliyopo ni kwamba wanunuzi wanachelewa kulipa fedha, lakini pia hata matunda yanayokuja mengine hayana viwango hivyo unakuta tunayagawanya katika madaraja. Sasa lawama zinakuja unapomweleza kuwa matunda yako yapo daraja la mwisho, hivyo unatakiwa kuuza kwa bei hii. Sisi huwa tunayagawa katika madaraja matatu yaani la kwanza la pili na la tatu”

Maofisa utamaduni mnafanya kazi yenu au anawafanyia waziri?



Anko Kitime
Anko Kitime 
Wiki imemalizika kwa amri ya kuzuia nyimbo kadhaa za ‘Bongo Fleva’ kurushwa kwenye vyombo vya utangazaji nchini. Kwa wengi hili halikuwa jambo la kushangaza, kuna wengine walikuwa wanashangaa kwanini baadhi ya nyimbo zinaendelea kusikika hewani. Na hakika kuna wengi wametetea kuwa nyimbo hizo hazina tatizo ziendelee tu kurushwa watu wafurahi.
Tatizo liko wapi? Binafsi naona kuwa hatua ya kufungia nyimbo hizi haitamaliza tatizo kwani hatua iliyofanyika ni kubandika tu bandeji kwenye kidonda kilichooza. Pengine tujiulize kwanini nyimbo ambazo zinasemekana ‘hazina maadili’ ziliweza kutungwa na kurekodiwa? Kwanini ziliweza kurushwa kwenye vyombo vya utangazaji bila kuonekana shida yoyote mpaka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na TCRA waingilie kati? Kwanini vijana wengi hawaoni tatizo la nyimbo hizo?
Kuna usemi maarufu usemao ‘Sanaa ni kioo cha jamii’. Ukiangalia kwenye kioo na kukuta sura mbaya inakuangalia basi ujue hivyo ndivyo ulivyo, kuvunja kioo au kubadili kioo hakutabadili sura yako.
Unaweza ukaikubali sura hiyo au ukaanza mkakati wa kutumia vipodozi kujipa mvuto unaoutaka. Kazi za wasanii zinaonyesha tu jamii ilivyo.
Mtoto aliyelelewa na wazazi wenye mdomo mchafu haiwi taabu kwake kuwa na mdomo mchafu, tena anashangaa sana akianza kukatazwa kutoa maneno machafu, anaona anaonewa kwa kuzibwa mdomo bila sababu za msingi. Hivyo kutunga wimbo uliojaa matusi au dalili za matusi kwake si tatizo, ndivyo jamii yake ilivyomlea.
Na wimbo huo utapokelewa vizuri tu na jamii yake kwani hayo ndio maisha yao ya kila siku. Niliwahi kuongea na mzazi wa mwanamuziki mmoja ambaye wimbo wake umeingia katika orodha ya kupigwa marufuku, mama yule alikuwa anajisifu kuwa yeye ndiye aliyeutunga wimbo anaoimba mwanae.
Turudi nyuma miaka 23 iliyopita. Uongozi wa awamu ya tatu ulipoingia madarakani, Wizara ya Utamaduni ilipata pigo ambalo matokeo yake yanaonekana sasa. Katika awamu hii maofisa utamaduni, mkoa na wilaya walifutika. Na baadaye kufufuka kinyemela wakiwa chini ya Idara ya Elimu katika halmashauri mbalimbali.
Hata huko walifufuliwa baada ya kuonekana kunahitajika mtu atakayekuwa akishughulikia kuratibu shughuli kama za Mwenge na sherehe mbalimbali.
Ofisa Elimu alimteua mwalimu aliyemuona anapenda sanaa na kumpa cheo cha uofisa utamaduni.
Maafisa hawa hadi leo bado ni utata, hawana bajeti, hawahusishwi kwenye vikao mbalimbali vya halmashauri, kila wilaya au halmashauri ikiwa na utaratibu wake. Mfano hapa Dar es Salaam kuna halmashauri za Ubungo, Kinondoni, Ilala na Temeke, ni halmashauri ya Kinondoni tu yenye sheria ndogo zinazohusu mambo ya sanaa na burudani, na sheria hizo zinahusiana zaidi na utoaji vibali tu kwa shughuli mbalimbali. Ukiona mkanganyiko huu kwa maofisa utamaduni wa jiji hili tu, je hali ikoje katika halmashauri za nchi nzima?
Waziri anayehusika na Utamaduni hawaongelei maofisa utamaduni hawa kwani hawako katika wizara yake na Waziri wa Tamisemi hawaongelei kwani hawana umuhimu huo kwake. Lakini hawa watu ndio kiungo muhimu sana katika kulinda na kuelekeza ‘maadili’ ya Kitanzania.
Awali walikuwa chini ya Wizara ya Utamaduni walikuwa ndio watekelezaji wa Sera ya Utamaduni, kwa sasa hawawajibiki kwa hilo, hivyo sera ya Utamaduni ni kitabu kiko katika makabati ya Wizara ya Utamaduni tu. Katika miaka hiyo ya nyuma nchi ilikuwa japo na maono kuwa inataka kwenda wapi kimaadili, na ikawa na utekelezaji wa pamoja wa maono hayo.
Kupotea kwa maofisa hawa kulikuja wakati mmoja na kuongezeka kwa vyombo vya utangazaji, luninga na redio.
Vyombo hivyo ndivyo vikaanza kubeba pengine bila kujua au kwa makusudi nafasi ya kulea maadili ya watoto wa Kitanzania. Malezi ya miaka mingi sasa yanatoa matunda, vijana waliokuwa na umri wa miaka 10 au chini zaidi mwaka 1995 na waliozaliwa baada ya hapo, ndio hao watunzi wa nyimbo ambazo zinaonekana hazina maadili, ni vigumu kwao kueleza au kujua maadili ya Kitanzania ni yepi.
Wanamuziki, watangazaji, waandishi, maproducer, mameneja wa wanamuziki na kadhalika wengi ndio waliozaliwa katika kipindi hiki.
Teknolojia imewezesha kazi ya muziki kuwa rahisi sana, ukiwa na kompyuta na microphone moja unaweza kujifungia chumbani kwako ukarekodi wimbo na kuutuma kwa barua pepe mpaka kwa mtangazaji na wimbo ukaanza kurushwa hewani katika kipindi cha masaa kadhaa.
Hivyo kama hakuna aliyelelewa kuona ukakasi katika wimbo basi umma bila kujali umri au uhusiano unajikuta ukisikiliza maneno ambayo kwa kawaida huwa faragha na kwa watu wazima wenye aina fulani ya mahusiano tu, maneno hayo yanatamkwa hadharani bila kumumunya.
Kuna haja kubwa ya Wizara inayohusika na Utamaduni kujiangalia upya na kujipanga upya ili kukabiliana na hali hii na si kuishia kufanya kazi rahisi ya kufungia nyimbo tu.

Makatibu wakuu 12 watembelea Hifadhi ya Ziwa Manyara

Mwenyekiti wa makatibu wakuu hao, Katibu mkuu
Mwenyekiti wa makatibu wakuu hao, Katibu mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Maimuna Tarishi  
Arusha. Makatibu wakuu wa wizara 15 pamoja na baadhi ya watendaji wa wizara hiyo watembelea Ziwa Manyara kuona hali halisi ya uharibifu wa ambao unatishia kukauka kwa ziwa hilo.
Mwenyekiti wa makatibu wakuu hao, Katibu mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Maimuna Tarishi amesema lengo la ziara hiyo ya kazi ni kujionea uharibifu wa ziwa na kuishauri Serikali.
Amesema hivi karibuni mawaziri ambao wizara zao zinahusiana na ziwa hilo walikutana na kupokea changamoto za ziwa hilo na waliagiza makatibu wakuu kutembelea na kupata hali halisi na baadae kuishauri Serikali.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Allan Kijazi amesema ziwa Manyara lipo hatarini kukauka kutokana na kuongezeka shughuli za kibinaadamu pembezoni mwa ziwa.
Amesema shughuli hizo pia zimeathiri mapito na mtawanyiko wa wanyama katika eneo la ikolojia ya hifadhi za Manyara na Tarangire.
Ziara ya makatibu wakuu inaendelea muda huu na inashirikisha watendaji wa Serikali, ofisi ya mkuu za wakuu wa mikoa Arusha na Manyara, ofisi ya mwanasheria mkuu wa Serikali na maofisa wa  wizara hizo.

HEKAYA YA MLEVI : Ukiona wanatupiana maandazi ujue wameshiba



GASTON NUNDUMA
GASTON NUNDUMA 
Babu mmoja aliokota jiwe. Akalibandika karatasi iliyosomeka: “Hili ndilo jiwe alilojisugulia Mkwawa”. Akampa mjukuu wake alitembeze kwenye mitaa ya uswazi kwa nia ya kujua thamani yake. Akamwambia kuwa watu wakiulizia bei asiongee neno zaidi ya kunyoosha vidole vitatu.
Mzee aliona mbali sana. Alijua wazee wa bandari wangejifanya kuwa wao walikuwa wakinywa “chimpumu” na Mkwawa halafu wangemhoji jinsi alivyolipata jiwe hilo. Hatimaye wangemnyang’anya na kulitia sokoni kwa maelezo yaleyale yaliyoandikwa na babu. Hivyo dogo akaekti ububu.
Watu walimsimamisha na baada ya kusoma sifa za jiwe wakamuuliza bei. Dogo akanyoosha vidole vitatu hewani. Wakasema “aha! Buku tatu. Bei ya mwisho je? Je bei ya kuuzia?” Dogo akarudia vidole vilevile vitatu.
Walipotaka kununua dogo aliondoka na jiwe lake na kurudi kwa babu. Babu akamwambia, “Sasa hivi nenda mitaa ya uzunguni. Ukiulizwa bei ufanye kama nilivyokuagiza.” Dogo akaingia Oysterbay na Masaki. Aliponyoosha vidole vitatu wakasema “Elfu thelathini? Niuzie…”
Akarudi tena kwa babu. akaambiwa “Sasa tembea kwenye balozi za mamtoni ukafanye vilevile. Lakini sasa usirudi nalo, liuze huko.” Dogo akaingia ubalozini.
Kama kawaida alipoulizwa bei akanyoosha vidole vitatu. Balozi akasema “Laki tatu? Tafadhali niuzie…” Akachukua hela na kurudi kwa babu. Maisha yakaendelea. Yule balozi alilipeleka jiwe Ulaya na kuliweka kwenye soko la vitu vya kale vilivyovumbuliwa barani Afrika.
Siku moja dalali wa Kiswahili alipita kwenye soko hilo, akalinunua jiwe hilo kwa dola zenye thamani ya shilingi milioni tatu za Kitanzania. Alijua kwa sifa za jiwe hilo asingekosa shilingi milioni thelathini kutoka serikalini ili jiwe likahifadhiwe kwenye Makumbusho ya Taifa.
Tunajifunza kuwa thamani ya kitu hupandishwa na watu kulingana na mazingira ya soko. Kuna koti ulitaka kuuziwa pale Tandika lakini ukalikwepa kwa madai ya viwango. Likapelekwa dry cleaner na ukaletewa ofisini kwako kule Kivukoni ukalinunua kwa bei mara kumi ya ile uliyotajiwa Tandika.
Au hujui kwamba zile kauzu za pakti unazozinunua shilingi elfu mbili Posta na Feri ndio zilezile zinazouzwa kwenye genge la jirani tena kwa shilingi mia tano tu? Au ni kwa sababu kwenye pakti kuna tangazo linalosema dagaa wanaongeza kinga ya mwili na nguvu za kiume? Yaleyale ya “jiwe aliloogea Mkwawa”.
Kwa hili nawapongeza wajasiriamali. Wanajua kuwa uongo wa sangoma ndiyo tiba ya mgonjwa. Lakini kwa leo inanibidi nirudi kuwa mzalendo mwenye kutazama maslahi mapana ya Taifa langu kwanza.
Mtu yeyote mwenye busara hakosi bustani ya mboga nyumbani kwake. Akikosa basi ni kwa sababu iliyo nje ya uwezo wake; pengine kiwanja alichoweza kununua kilimtosha kuinua mjengo tu bila kuacha mahali pa kucheza watoto.
Bustani ingembeba akapata angalau mboga orijino maana hizi za mtaani hazieleweki kabisa. Vilevile atapata utelezi kidogo wakati vyu… wakati hali imekuwa ngumu. Unaweza kuamka na maganda ya karanga mfukoni bila senti ukasonga unga uliobaki jana kwa tembele la bustanini kuliko kumsomesha mgogo buchani. akukopeshe nyama. Mwaka 1985 Mwalimu Nyerere alizindua kiwanda cha kutengeneza karatasi huko Mufindi Mkoani Iringa. Bila shaka alizingatia mahitaji ya karatasi yalivyokuwa yakipanda. Kwanza wasomi walikuwa wakiongezeka kila muhula. Wasomi wote (kuanzia vyuoni hadi chekechea) hawakuweza kufanya lolote pasipokuwa na karatasi. Hata huku mtaani wakati vita ya taka sugu kama plastiki ikipamba moto, karatasi ilikuwa mkombozi kwenye mifuko, na mapambo.
Pia kuna mtu alinieleza kuwa bi mkubwa wake alikuwa akitumia mkaa wa karatasi tangu akiwa mwanamwali. Aliloweka karatasi na maboksi kwa siku kadhaa, akayachanachana ndani ya maji na kuyakamua katika mfano wa matonge ya ugali. Kisha akayaanika juani. Kitu tayari. Huyu atunukiwe shahada ya mazingira.
Kile kiwanda kilifanya kazi nzuri kiasi kwamba Tanzania iliuza karatasi hadi nje. Lakini pia tulipata vifungashio vya bidhaa za viwandani (kwa maana ya maboksi na mifuko).
Lakini mwaka 2004 kiwanda kikauzwa kimya kimya kwa Wakenya kwa madai ya kutozalisha vizuri. Sijui ni nani anayeukata mkono wa mtoto wake kwa sababu ati kaunyea! Lakini kwa sababu yaliyopita si ndwele, tutazame yanayotokea sasa. Ukiyakosa maji ndipo utajua umuhimu wake.
Hivi sasa tunategemea karatasi za Afrika Kusini, lakini hasa za China. Kutokana na desturi ya Wachina, kuanzia tarehe 23 mwezi wa 12 hadi tarehe 15 mwezi wa Januari Wao huwa likizoni kuadhimisha sikukuu ya mwaka mpya wa kijadi.
Hali hii inatuathiri sana kwa sababu hakuna mizigo inayoingia wakati sisi hutumia makontena mengi sana ya karatasi katika muda mfupi. Kwa uhaba huo bei hupanda hadi mara tatu ya bei elekezi. Wengi wanashindwa kununua na elimu ya watoto wao inayumba kwa sababu wakizikosa wanafukuzwa shuleni.
Huwa najiuliza Wakenya waliona nini ambacho sisi wenye kiwanda tulishindwa kukiona. Bila shaka wao wana upeo wa babu aliyeuza jiwe. Tangu enzi zile walitukimbiza sana na bidhaa zao kama mafuta ya Blue Band dhidi ya Tan Bond yetu kwa jinsi walivyojua kuongeza thamani.
Japokuwa hatushadadii yaliyopita lakini “Tanzania ya Viwanda” isipofanya “ndwele” sijui kama tutafika.

Kufungiwa ‘chura wangu’ sielewi hadi sasa


Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Snura Mushi, amesema hadi sasa haelewi ni kwanini nyimbo zake mbili zimefungiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Akizungumza na MCL Digital, leo Machi 3, Snura amesema kufungiwa kwa nyimbo zake mbili ya ‘Chura’ na ‘Nimevurugwa’ kumemchanganya na wala haelewi hadi sasa nini sababu ya kufikiwa kwa hatua hiyo na mamlaka hiyo ya Serikali.
Akitolea mfano wa wimbo wa ‘chura’ Snura amesema video yake ilipofungiwa alitakiwa kuirekebisha na alifanya hivyo na kisha ikahaririwa na vyombo vyote ikiwamo Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na TCRA wenyewe na kumruhusu kuionyesha.
“Lakini juzi nashangaa kati ya nyimbo 15 zilizofungiwa yangu hiyo ya chura nayo ilikuwa mojawapo hadi najiuliza kumetokea nini hasa hadi wanipe adhabu hiyo kubwa kwangu,” amesema Snura.
Wakati kwa wimbo wake wa ‘Nimevurugwa’ amesema ana uhakika hakuna tusi lolote ndani ya wimbo huo na kueleza hata video yake haoni kama ina shida.
Pia msanii huyu ameeleza pamoja na yote hayo hajapewa barua hadi sasa kama ilivyo taratibu msanii unapotaka kufungiwa nyimbo yako na wala Basata haijamuita kumweleza tatizo lake ni nini hasa.
Kutokana na hatua hiyo, MCL Digital, pia iliweza kuongea na Mkurugenzi wa TCRA, Mhandisi James Kilaba, ili kujua ni vigezo gani walivyotumia katika kuzifungia nyimbo walizozitaja ukizingatia nyingine zilishafungiwa kipindi cha nyuma na wasanii kulipishwa faini.
Katika majibu yake, Mhandisi Kilaba, amesema swali hilo waulizwe Basata kwa kuwa wao ndio waliwapelekea malalamiko kuhusu nyimbo hizo na kwa kuwa moja ya  kazi yao ni kusimamia redio na televisheni ndio wakaamua kuchukua hatua hiyo ya kuviandikia barua vyombo hivyo kuacha kuzionyesha na kuzicheza.
Wakati Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza, amesema walichukua hatua ya kupeleka malalamiko yao TCRA, baada ya kuona pamoja na kuzifungia nyimbo hizo lakini bado baadhi ya vituo vya redio na televisheni ziliendelea kuzicheza na wao hawana mamlaka ya kuvichukulia hatua vyombo hivyo zaidi ya kuishia kwa wasanii.
Februari 28 TCRA iliandika barua kwa vituo vya redio na televisheni ikiviagiza visitishe kuonyesha nyimbo 15 za wasanii kadhaa kutokana na kuwa na maudhui ambayo yanaenda kinyume na maadili na kanuni za Huduma za Utangazaji (Maudhui) 2005.
Nyimbo hizo na jina la msanii aliyeimba kwenye mabano ni  Hallelujah na Wakawaka (Diamond), Kibamia (Roma Mkatoliki), Pale Kati patamu, Maku (Makuzi) na Mikono Juu (Ney wa Mitego), Hainaga Ushemeji (Manifongo), I am Sorry JK (Nikki Mbishi).
Nyingine ni Chura na Nimevurugwa (Snura), Tema mate tumchape (Madee), Uzuri wako (Jux), Nampa papa (Gigy Money), Nampaga (Baranaba) na Bongo Bahati mbaya (Young D).

Majaliwa awataka wakulima wa ufuta kuuza zao hilo mnadani


Ruangwa. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakulima wa ufuta katika mikoa inayolima zao hilo nchini kuuza kwa kutumia njia ya minada na si mashambani.
Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Machi 03, 2018) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Nachihungo, Narung’ombe na Chikwale.
Waziri Mkuu ambaye yuko wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi amesema ili wakulima wapate tija ni vema wakauza ufuta wao kwa kupitia minada kama inavyofanyika katika zao la korosho.
“Usikubali kumuuzia mtu yeyote ufuta wako ukiwa shambani kwa sababu bei atakayonunulia ni ndogo kulinganisha na soko, naamini ufuta wote ukiuzwa katika minada mtaona faida,” amesema.
Kufuatia agizo hilo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Andrea Chezue aandae utaratibu wa maeneo ya kukusanyia ufuta na kufanyia minada.
Amesema ufuta unaolimwa nchini ni bora na unapendwa sana duniani hivyo wasiwe na wasiwasi. Baadhi ya mikoa inayolima ufuta kwa wingi ni Lindi, Pwani, Dodoma, Manyara, Kigoma na Singida.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema vijiji vyote visivyokuwa na umeme nchini vikiwemo vya wilaya ya Ruangwa vitaunganishiwa katika Mradi wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya tatu.
Amesema wananchi waendelee kuwa na subira kwa sababu tayari mkandarasi ameshaanza kazi ya kuunganisha umeme katika vijiji vingine vya wilaya hiyo na atafika kwenye maeneo yao.
Alibainisha kuwa mkakati wa Rais John Magufuli ni kuhakikisha wananchi wote nchini wanaunganishiwa nishati ya umeme kwenye majumba yao, hivyo waendelee kuwa na subira na kushirikiana na Serikali yao.
Kuhusu suala la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama alisema, “Huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo vijiji vyote vitapata maji.”
Pia alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kote nchini kutunza vyanzo vya maji ili kuliepusha taifa kugeuka jangwa pia miradi inayoletwa na Serikali iwe endelevu.

Mama ajifungua watoto wanne kwa mpigo Dar


Dar es Salaam. Ofisa Tarafa wa Kibamba, wilayani Ubungo, Beatrice Mbawala amejifungua watoto wanne kwa mpigo katika Hospitali ya Agha Khan, jijini hapa.
Beatrice amejifungua watoto hao wakiwa njiti mwezi mmoja uliopita.
Akizungumza hospitalini hapo, leo Machi 3, baba wa watoto hao, Julius Mbawalla amesema familia yake ina furaha kupokea watoto wanne na kwamba jukumu lake kubwa ni kuhakikisha mkewe anapata huduma muhimu ili aweze kumudu kuwanyonyesha.
Daktari Bingwa wa Watoto katika hospitali ya Agha Khan, Dk Mariam Mgonja amesema afya za watoto zimeimarika na tayari wameruhusiwa kwenda nyumbani.

Operesheni za UN zasitishwa mjini Rann,Nigeria

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa nchini Nigeria
Image captionWafanyakazi wa Umoja wa Mataifa nchini Nigeria
Umoja wa Mataifa umeeleza kwa kina kuhusu sababu za kusitisha operesheni za kibinaadam mjini Rann nchini Nigeria baada ya shambulio la siku ya Alhamisi ambalo linadaiwa kutekelezwa na wanamgambo wa kiislamu, Boko Haram.
Zaidi ya wafanyakazi 50 wa misaada walikuwa wakitoa usaidizi kwa takriban watu 80,000 mjini Rann, mji uliotengwa, hakuna mtandao wa simu.
Msemaji wa UN nchini Nigeria, Samantha Newport amesema shambulio la siku ya Alhamisi liligharimu maisha ya wafanyakazi wa misaada watatu, watatu walijeruhiwa, wengine hawajulikani walipo.
''kutokana na hilo Umoja wa Mataifa umeamua kusitisha kwa muda operesheni zake mjini Rann pekee kwa muda wa juma moja''.Ameeleza
Samantha amesema inaonekana shambulio hilo lilikusudiwa kulenga wanajeshi, hivyo kwa bahati mbaya wafanyakazi wa UN ilitokea tu walikuwepo hapo kwenye eneo baya na kwa wakati mbaya.

Ni kwa nini wacheza utupu huhudhuria mazishi nchini China

File photo of a pole dancer in ChinaHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionThe Chinese government is trying to crack down on what it calls "obscene performances"
Muziki unacheza kwa sauti, wacheza utupu wakicheza densi na umati ukishangilia. Katika sehemu zingine huko China hili ndilo unaweza kuliona wakati wa mazishi.
Mapema mwaka huu, China alianza tena kuwakamata wacheza utupu wanaocheza densi kwenye mazishi, harusi na kwenye mahekalu.
Hio sio mara ya kwanza mamlaka zimejaribu kuzuia tabia hizo lakini bado hazijanafikiwa

Mbona watu huwaajiri wacheza utupu?

Wacheza utupu hutumiwa kuwavutia watu wnaaohudhuria mazishi kwa sababu uwepo wa watu wengi kwenye mazishi huonekana kama heshima kwa marehemu.
Imani nyingine zinasema kuwa suala hilo na la kuabudu.
Imani nyingi ni ile kuwa kuwaajiri wacheza utupu kunaweza kuonekana kama ishara ya utajiri.
Maeneo ya vijijini nchini China ndiyo yenya tabia ya kutumia pesa nyingi hata kuliko mapata, kuwalipa wuigizaji, waimbaji, wachekeshaji na wacheza utupu kuwatumbuiza wale waliofiwa.

Shughuli hii ni maarufu?

Tamaduni hiyo inapatikana sana maeneo ya vijijini ya China na ni maarufu zaidi nchini Taiwan ambapo ilianzia.
"Tamaduni hii ya wacheza utupu kwenye mazishi kwanza lilipata umaarufu nchini Taiwan mwaka 1980," msomi wa chuo cha South Carolina Marc Moskowitz aliiambia BBC.
Tamaduni hii imepata umaarufu nchini Taiwan lakini nchini China serikali imeizuia na watu wengi hawafahamu kuihusu.
This picture taken on 3 January 2017 shows a pole dancer performing on top of a jeep during the funeral procession of former Chiayi City county council speaker Tung Hsiang in Chiayi City, southern Taiwan.Haki miliki ya pichaAFP/GETTY IMAGES
Image captionPole dancers have also performed in funeral processions in Taiwan

Makampuni yashinikizwa kutowekeza kwa watengeneza silaha Marekani

Makampuni yanayouza silaha yatakiwa kuhakikisha usalama wa matumizi ya silaha unakuwepo
Image captionMakampuni yanayouza silaha yatakiwa kuhakikisha usalama wa matumizi ya silaha unakuwepo
Kampuni kubwa ya usimamizi katika uwekezaji imeweka shinikizo dhidi ya makampuni yanayotengeneza na kuuza silaha baada ya tukio la mashambulizi katika shule ya Florida.
Kampuni ya Black Rock imekuwa ikiwashawishi wawekezaji kutowekeza kwenye makampuni ya kutengeneza silaha na amekuwa akiyauliza makampuni ni namna gani huwa wanachunguza matumizi salama ya silaha.
Shirika hilo limesema jambo linatakiwa kufanyika baada ya tukio la Florida ambapo watu 17 walipoteza maisha.
Shirika hilo ni mdau mkubwa katika viwanda vikubwa viwili vya kutengeneza silaha nchini Marekani.
Black Rock inaamini kuwa tukio hilo linahitaji mwitikio kutoka kwenye sekta zote, za uma na binafsi.

Mkuu wa Kampuni ya Nishati ashutumiwa kumuua mwanaharakati wa mazingira

Mwanaharakati Caceres ni miongoni mwa wengine 100 waliouawa katika kipindi cha muongo uliopitaHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionMwanaharakati Caceres ni miongoni mwa wengine 100 waliouawa katika kipindi cha muongo uliopita
Polisi nchini Honduras inamshikilia Mkuu wa Kampuni ya masuala ya nishati akishukiwa kupanga mauaji ya mwanaharakati wa mazingira.
Berta Caceres aliuawa kw kupigwa risasi nyumbani kwake miaka miwili iliyopita
Mwanamama huyo alipinga vikali mradi wa ujenzi wa bwawa.
Roberto David Castillo ni rais wa Kampuni iitwayo Desa, kampuni hiyo ilikuwa inajenga bwawa.
Kampuni hiyo imeshutumiwa na kukemewa vikali kimataifa pia zilifanyika kampeni za mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali yakikemea tukio hilo.
Imeripotiwa kuwa Castillo alikua mwanajeshi, afisa wa intelijensia.
Mkuu wa Kampuni ya Nishati anayeshutumiwa kupanga njama za mauajiHaki miliki ya pichaAFP
Image captionMkuu wa Kampuni ya Nishati anayeshutumiwa kupanga njama za mauaji
Watu wengine wanane wameshtakiwa kutokana na mauaji hayo, wakiwemo polisi na wafanyakazi wa Desa.
Familia ya Caceres imesisitiza kuwa aliuawa kwa sababu za kiuchumi.
Inasema Caceres kwa miezi mingi amekuwa akipata vitisho kutoka kwa Polisi,wanasiasa na Kampuni za ujenzi.
Mwezi Novemba mwaka 2017, ripoti ya kurasa 92 kutoka kwa wataalamu wa kimataifa ilihitimisha kuwa Kampuni hiyo na mawakala walipanga kumuua mwanaharakati huyo.
Mwanaharakati Caceres atakumbukwa kwa kupigania haki za jamii ya wachache katika hali ya amani na mwaka 2015 alishinda tuzo ya Goldman, moja kati ya tuzo muhimu za masuala ya mazingira.
Majaji wa walisema kuwa aliongoza kampeni ya watu wa jamii ya Lenca nchini Honduras kampeni ambayo ilifanikiwa na kushinikiza mjenzi wa bwawa kubwa zaidi duniani kuondoka kwenye bwawa la Agua Zarca.
Bwawa hilo lingeleta madhara kama mafuriko na kukata miundo mbinu ya kusambaza maji, chakula dawa kwa ajili ya jamii ya Lenca.
Caceres ni mmoja kati ya wanaharakati 100 wa masuala ya ardhi waliouwawa nchini Honduras katika kipindi cha muongo uliopita.

Waandamanaji wakabiliana na Polisi Ukraine

Takriban watu 100 wamekamatwa na Polisi baada ya kutokea vuruguHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionTakriban watu 100 wamekamatwa na Polisi baada ya kutokea vurugu
Watu kadhaa wamejeruhiwa mjini Kiev nchini Ukraine, wakati wa makabiliano kati ya waanamanaji wanaoipinga serikali na Polisi.
Vyombo vya habari nchini humo vimesema makabiliano hayo yalianza wakati waandamanaji walipowasha moto matairi ili kuwazuia maafisa wasifanyie ukaguzi Kambi ya waaandamanaji iliyokuwa nje ya Bunge.
Polisi wa Ukraine wamesema watu 50 wamekamatwa.Wamesema walikuwa wanafanyia uchunguzi kambi hiyo ili kupata ushahidi kuhusu makabiliano yaliyofanyika jumatatu iliyopita na kusababisha maafisa polisi kadhaa kujeruhiwa.
Katika kamatakamata hiyo Polisi wamekamata maguruneti ya kurushwa kwa mkono yaliyokuwa kwenye turubai la kambini hapo.