Saturday, March 3

Waandamanaji wakabiliana na Polisi Ukraine

Takriban watu 100 wamekamatwa na Polisi baada ya kutokea vuruguHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionTakriban watu 100 wamekamatwa na Polisi baada ya kutokea vurugu
Watu kadhaa wamejeruhiwa mjini Kiev nchini Ukraine, wakati wa makabiliano kati ya waanamanaji wanaoipinga serikali na Polisi.
Vyombo vya habari nchini humo vimesema makabiliano hayo yalianza wakati waandamanaji walipowasha moto matairi ili kuwazuia maafisa wasifanyie ukaguzi Kambi ya waaandamanaji iliyokuwa nje ya Bunge.
Polisi wa Ukraine wamesema watu 50 wamekamatwa.Wamesema walikuwa wanafanyia uchunguzi kambi hiyo ili kupata ushahidi kuhusu makabiliano yaliyofanyika jumatatu iliyopita na kusababisha maafisa polisi kadhaa kujeruhiwa.
Katika kamatakamata hiyo Polisi wamekamata maguruneti ya kurushwa kwa mkono yaliyokuwa kwenye turubai la kambini hapo.

RAIA WA CHINA ALIPA MILIONI 110/- KUKWEPA KWENDA JELA MIAKA 20


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Raia wa China, Liu Xiu Feng kutumikia kifungu cha miaka 20 jela ama kulipa faini ya Sh.milioni 110 baada ya kukiri kosa la kukutwa na meno ya Simba mawili.

Hukumu hiyo imesomwa leo na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi kueleza mshtakiwa huyo amekiri kosa.

Hakimu Shaidi amesema kutokana na mshtakiwa huyo kukiri kosa Mahakama inamuhukumu kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani ama kulipa faini ya sh.milioni 110."Mahakama inakuhukimi kutumikia kifungo cha miaka 20 jela ama ulipe faini ya Sh.milioni 110," amesema Hakimu Shaidi.

Baada ya kutolewa hukumu hiyo, mshtakiwa Feng aliepuka kwenda jela baada ya kulipa faini hiyo ya Sh.milioni 110.

Raia huyo wa China alikuwa akikabiliwa na kosa la kukutwa na meno mawili ya Simba katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).Alikutwa na meno hayo Februari 7,mwaka 2018 ambapo yanathamani ya Sh.milioni 11, 029,900.

ALIYEKUWA MWANAJESHI, WENZAKE WAHUKUMIWA KWENDA JELA MIAKA 20


ALIYEKUWA mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ),Ex MT 66807 na wenzake watatu wamehukumiwa kwenda jela miaka 20 baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na meno ya Tembo yenye thamani ya Sh.198.

Hukumu hiyo imesomwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi  Kasonde.Watuhumiwa wengine waliohukumiwa kifungo hicho ni Bakari na Shafii Muhibu Muhibu.

 Hata hivyo, Mahakama imemuachia huru Asha Hassan Ulaya, aliyekuwa akishtakiwa na wenzake hao baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka bila ya kuacha shaka yoyote kuwa naye alihusika kwenye tukio hilo.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Kasonde amesema upande wa mashtaka kupitia mashahidi wake nane wameweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa hao watatu pasipo kuacha shaka yoyote kuwa wametenda kosa.

"Mahakama inawahukumu washtakiwa wote watatu kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja kwenye shtaka la kwanza na vilevile shtaka la pili miaka 20,"amesema Hakimu Kasonde.Pia Mahakama imeamuru meno ya Tembo yarudishwe kwa Mkurugenzi wa Wanyama pori na gari aina ya Suzuki waliyokamatwa washtakiwa waliyotumia kubebea meno hayo itaifishwe na Serikali.

Katika hati ya mashtaka, inadaiwa, Juni 2, mwaka 2016 huko Mbagala Kibondemaji wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote walikamatwa na vipande 10 vya meno ya Tembo.Pia washtakiwa hao walikuwa wanadaiwa kukubali kisafirisha meno hayo ya Tembo yenye thamani ya Sh. milioni 198,mali ya Serikaliya Tanzania.

Washtakiwa hao wanadaiwa kukutwa na nyara hizo za Serikali bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa wanyama pori.

UCHAGUZI K’NDONI, SIHA: RIPOTI YAFICHUA MAZITO



ZIKIWA zimepita siku kadhaa tangu ulipofanyika uchaguzi mdogo katika majimbo ya Kinondoni na Siha, taarifa ya tathmini ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), imeibua mazito.
Kati ya yaliyobuliwa katika taarifa hiyo ni tukio la kuibwa kwa sanduku la kura na watoto wadogo kupandishwa kwenye majukwaa ya kampeni jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Mbali na hilo, katika ripoti hiyo ya tathmini inadaiwa baadhi ya viongozi wa Serikali akiwamo waziri mmoja (jina linahifadhiwa), alitumia gari la Serikali katika kampeni kwenye uchaguzi wa Kinondoni.
Kutokana na hali hiyo, tathmini ya LHRC imetoa kasoro 11 katika uchaguzi huo wa marudio ambao walidai vyama vya upinzani viligandamizwa tofauti na chama tawala.

Wachumi watoa jibu Taifa kuondokana na utegemezi


Wakati kiwango cha utegemezi kiumri kwa Watanzania ni asilimia 92, wataalamu wa uchumi wameshauri mbinu zinazoweza kutumika kuondokana na hali hiyo ili kufikia Tanzania ya uchumi wa viwanda.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi jana, wachumi hao walisema ni hatari kwa Taifa lolote duniani kuwa na kiwango kikubwa cha utegemezi pamoja na kuwatumia wataalamu maeneo sahihi ya taaluma zao.
Juzi, taarifa ya makisio ya idadi ya watu nchini iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na kuzinduliwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ilieleza kuwa Tanzania inakadiriwa kuwa na idadi ya watu 54.2 milioni huku ongezeko kwa mwaka likiwa ni wastani wa watu 1.6 milioni.
Dk Mpango alisema kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, kiwango cha utegemezi kinaonyesha kati ya Watanzania 100 wenye umri wa miaka 15 hadi 64 wanategemewa na watu 92 wenye umri wa chini ya miaka 15 na juu ya 65 ikilinganishwa na asilimia 40 ya nchi zinazoendelea.
Alisema kiwango kikubwa cha utegemezi kinachotokana na idadi kubwa ya watoto ni changamoto kwa maendeleo ya nchi yoyote duniani, huku akieleza kwamba sera ya maendeleo ya watu hailazimishi kuzaa idadi fulani ya watoto isipokuwa inatahadharisha wazazi kupata watoto wanaoweza kumudu kuwalea.
Jana, walipotakiwa kuchambua utegemezi huo na maana yake kiuchumi, Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salam (UDSM), Benedict Mongula alisema suala la utegemezi si geni hasa katika suala la idadi ya watu huku akieleza namna ya kulitatua.
“Tukuze uchumi wetu kwa kuongeza uwekezaji na uzalishaji ikiwamo kuongeza juhudi na maarifa, kuongeza tija ya uzalishaji katika eneo la kilimo ili kisaidie na tunapoingia katika uchumi wa viwanda tuingie kwa makini tusije kuingia na kurudi kama huko nyuma,” alisema Profesa Mongula na kuongeza:
“Tuongeze uwekezaji hasa wa Watanzania wenyewe na kutoka nje, viwanda vyetu tunavyoanzisha tuvitafutie soko la kutosha. Tuhakikishe kunakuwa na sera maalumu ya kuvisaidia viwanda kuendelea. Sera nzuri katika kilimo ili wakulima wadogo na wakubwa waweze kunufaika.”
Profesa Mongula anaungwa mkono na Profesa mwingine wa uchumi wa chuo hicho, Haji Semboja aliyesema hakuna haja ya kulalamika na utegemezi kwani Tanzania imejaliwa kuwa na rasilimali nyingi ikiwamo ardhi, madini, bahari na nyinginezo ambazo zikitumika vizuri zitamaliza suala la ukosefu wa ajira.
Alisema kinachotakiwa kufanyika ni Bunge, Mahakama na Serikali kusimamia na kutekeleza sera na sheria zilizopo kwa ukamilifu na watendaji wanaosimamia taasisi mbalimbali kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
“Wakati mwingine mambo yanashindwa kutekelezwa na kubaki kurukaruka au kurukia rukia kutokana na aina ya watendaji tuliona nao, mfano mimi ni Profesa wa eneo fulani, lakini nakuwa nasimamia taasisi isiyoendana na taaluma yangu, ndiyo utakuta narukaruka au narukiarukia mara hili mara lile,” alisema Profesa Semboja na kuongeza:
“Tanzania haina tatizo sasa na kwamba ni maskini hapana, rasilimali tulizonazo na namna tunavyozitumia. Tatizo ni ku- transform (kubadilisha) tulichonacho. Kuna maeneo mengine hayaendi vizuri. Ukiona hayaendi ukifuatilia ni suala la utawala. Wanaopaswa kukaa pale utagundua si wa professional (wataalamu wa fani) yao na ingependeza kuona watu sahihi eneo fulani ili kuepuka kurukiarukia mambo.”
Mchumi kutoka Taasisi ya Tanzania Music (Tamufo), Dk Donald Kisanga alisema kiuhalisia baadhi ya mila na desturi zilizopo zinachangia kuwapo kwa kundi kubwa la utegemezi jambo linalohatarisha uchumi.
“Serikali inahitaji rasilimali watu iliyoelimika, hivyo lazima kuwekeza kwenye elimu,” alisema.
Pia, alishauri kuwapo kwa mfumo wa kuandaa mazingira mazuri ya watu kujiajiri badala ya kubweteka na kusubiria ajira rasmi zinazowafanya waendelee kuwa tegemezi wakati zinapokosekana
Mtaalamu wa uchumi kutoka Taasisi ya Nnyaka Production, Dk Godwin Maimu alisema athari za utegemezi ni kubwa hasa wakati huu ambao Serikali ina mikakati ya kuingia kwenye uchumi wa viwanda. “Utegemezi unaathiri mitaji, unahamisha fedha za uwekezaji kuwa za matumizi na hii ni hatari kubwa kiuchumi, wanaotegemewa hawataweza kuendelea kuzalisha kwa sababu kila kinachopatikana kinaingia kwenye matumizi,” alisema.
Alisema hakuna taifa lolote linaloweza kuendelea duniani kama kundi la utegemezi ni kubwa kuliko la wanaotegemewa.
Ili kuondokana na dhana hiyo ya utegemezi, Dk Maimu alisema lazima Serikali ikubali kubadilisha mitalaa yake ya kufundishia na kuwekeza kwenye elimu ya vitendo badala ya nadharia inayotumika sasa.
Dk Maimu alisema wanafunzi wanapomaliza masomo yao wanapaswa kuwa na ujuzi utakaowasaidia kujitegemea, kwa sababu wengi watakuwa wamefundishwa ili wanapohitimu waweze kujitegemea. “Wanafunzi wasifundishwe kukariri, walau elimu nadharia iwe kwa asilimia 30 tu na vitendo iwe asilimia 70. Hii itasaidia kuondokana na utegemezi kwa sababu baada ya miaka kadhaa wanafunzi watakaokuwa wanahitimu watakuwa na ujuzi,” alisema.
Alisema hakuna taifa lolote linaloweza kujivunia kasi ya maendeleo kama watu wake wataendelea kuzaliana kupita kiasi.
Dk Maimu alisema utegemezi unanyima wigo mpana wa uwekezaji kwa sababu wanaotegemewa kuwekeza hubaki kwenye hatua ya chini, hivyo kutoingia kwenye ushindani wa kiuchumi kwa kuwa mitaji yao haitaweza kukua.
Alisema ipo haja kwa jamii kuelimishwa namna ya kuwaandaa watoto wao kujitegemea hasa wanapofikia umri wa kutakiwa kufanya hivyo.
“Kuna wategemezi ambao umri wao sio wa kuwa tegemezi hawa lazima watengenezewe mazingira ya kutokuwa tegemezi, hata kwa kupelekwa kwenye vyuo vya ufundi ili mwisho wa siku, utegemezi huu uondoke,” alisema.
Katika ukurasa wetu wa facebook, baadhi ya wachangiaji wamezungumzia idadi hiyo ambapo Leung Ka Yan alisema “lugha rahisi asilimia 92 ya watanzania hawana uwezo wa kuishi kwa kujitegemea wenyewe.”

Taasisi tatu nchini zatupiana mpira mabasi 70 Dart kuingia barabarani


 Taasisi tatu zote zikiwa na masilahi katika usafiri na usafirishaji zimegongana huku Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu na Majini (Sumatra) wakidai hawajapata maombi ya kibali cha kuruhusu magari mapya 70 kuingia barabarani.
Dart na Sumatra zimelaumiwa kupitia taarifa iliyotolewa juzi baada ya Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (Udart), kusema kuchelewa kuingia barabarani kwa mabasi hayo waliyoyaleta hivi karibuni kunatokana na uchelewaji wa kibali kutoka Sumatra na Dart.
Akizungumza jana na gazeti hili, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Udart, Deus Bugaywa alisema mabasi hayo yataingia barabarani mara tu baada ya kupata vibali kwa mamlaka zinazohusika.
Alizitaja mamlaka hizo kuwa ni Dart ambao anadai ndio hasa wasimamizi wa mradi na Sumatra wenye mamlaka ya kutoa leseni za mabasi kuingia barabarani.
“Ni imani yetu kwamba vibali hivyo vikitoka, basi tutawaondolea kero abiria wetu na tunawaomba kuwa na subira kwani ili mradi mabasi hayo tayari yapo hapa nchini hakuna litakaloshindikana, ni muda tu,” alisema.
Hata hivyo, gazeti hili liliwatafuta kwa nyakati tofauti na kwa njia ya simu wakurugenzi wa mamlaka hizo ili kujua sababu ya kuchelewa kutoa vibali hivyo, ikizingatiwa mabasi hayo yana wiki mbili hadi sasa tangu yaingizwe nchini ambapo yule wa Dart, Ronald Lwakatare alisema anachojua ni kuwa hajapata maombi ya kuombwa kibali kwa ajili ya mabasi hayo na kuahidi kwamba endapo yatamfikia ataharakisha kukitoa. “Hapa wewe ndio unaniambia kuwa mabasi hayo hayajaingia barabarani kwa sababu ya kibali, lakini kwa kumbukumbu yangu mpaka sasa sijaona maombi yoyote mezani kwangu yanayohusu mabasi hayo kutaka kuruhusiwa kuingia barabarani, labda kama yamekuja muda huu ambao nipo nje ya ofisi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe alisema hajapata maombi yoyote na kwamba, kwa kawaida wanayapata kupitia Dart ambao ndio wasimamizi wakuu wa mradi.

Asilimia 90 ya wanyamapori watoweka kwa ujangili


Ujangili unaofanyika katika jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori Wami Mbiki iliyopo mkoa wa Pwani na Morogoro, haujawahi kufanyika hifadhi zingine zozote nchini, imeelezwa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori, Omary Tofiki alisema miaka iliyopita hifadhi hiyo ilikuwa na wanyama wa aina zote kasoro faru, lakini kutokana na kukithiri kwa ujangili wanyama waliobaki asilimia kumi.
Tofiki alisema licha ya doria zinazofanywa mara kwa mara, wapo baadhi ya askari wamekuwa wakitoa taarifa kwa majangili hivyo kukwamisha mapambano. “Ujangili unaofanywa katika hifadhi hii haufanywi mahali popote nchini, mara kadhaa nimeshatoa taarifa za ujangili huu kwa viongozi mbalimbali lakini hali ni mbaya,” alisema Tofiki.
Naye ofisa wanyamapori mwandamizi wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (Tawa), Abraham Jullu alisema hifadhi hiyo ni muhimu kwa ustawi wa wanyama kwani imekuwa ikitumika kama sehemu ya mazalia ya wanyama wanaotoka hifadhi za jirani ambazo ni Saadani, Mikumi na Selou.
Alisema kuwa kama hifadhi hiyo haitasimamiwa na kupewa ulinzi madhubuti idadi ya wanyama katika hifadhi hizo itapungua kwa kuwa wanyama wengi watauawa wakiwa Wami mbiki.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Alhaji Majid Mwanga alisema kuwa sehemu ya hifadhi hiyo ya Wami mbiki iko kwenye wilaya yake na kwa kiasi kikubwa kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya hiyo imefanyakazi ya kuendesha doria na misako katika hifadhi hiyo.
Alisema kuwa katika misako hiyo pia walifanikiwa kuwaondoa wafugaji waliovamia katika hifadhi hiyo hata hivyo kwa sasa wafugaji wameanza kurudi na kuweka makazi tena wakiwa na makundi makubwa ya mifugo.

Watoto wanne wa familia moja wateketea kwa moto


Watoto wanne wa familia moja wamefariki dunia kwa kuteketea kwa moto walipokuwa wamelala chumbani katika mtaa wa Geita Road mjini Sengerema.
Akizungumzia tukio hilo jana, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alisema tukio hilo lilitokea saa 5:00 usiku wa Februari 28 (kuamkia jana).
Aliwataja watoto hao kuwa ni Lydia Elias (10), Modesta Elias (9), Steven Deogratias (9) na Kizengela Elias (8).
Alibainisha kuwa wakati moto huo uliotokana na mshumaa kushika chandarua na kuunguza godoro walilokuwa wamelalia, mama yao alikuwa amelala kwenye nyumba nyingine ya familia hiyo.
“Watoto wote ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Pambalu na wanatarajiwa kuzikwa kesho (leo),” alisema Kipole.
Mmoja wa majirani wa familia hiyo, Amas Juma aliwataka wazazi kuwa makini wanapolazimika kuwawashia watoto mishumaa kwa kuhakikisha inazimwa kabla ya kulala.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo na kutoa wito kwa wazazi na walezi kuchukua tahadhari watoto wanapobaki wenyewe nyumbani.

Shule yafungwa baada ya wanafunzi kuvamia, kuharibu nyumba ya mwalimu


Katika hali isiyo ya kawaida, Shule ya Sekondari ya Lyamungo wilayani Hai imefungwa kwa wiki mbili baada ya kutokea vurugu zilizofanywa na wanafunzi na kusababisha uharibifu wa nyumba ya mwalimu wa nidhamu, Safari Rasin.
Taarifa ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Yohana Sintoo aliyoitoa jana inaeleza kuwa shule hiyo imefungwa baada ya wanafunzi zaidi ya 400 kuvamia nyumba ya mwalimu huyo na kufanya uharibifu kwa madai kuwa amekuwa akiwatukana matusi ya nguoni jambo ambalo limekuwa likiwakera.
Sintoo alisema Februari 27, wanafunzi hao walikuwa na uchaguzi wa serikali yao na mmoja wao aliandika matusi kwenye karatasi ya kura, hali iliyowafanya walimu kuwataka kila mmoja achukue karatasi yake ili kumbaini mhusika.
Alisema karatasi zilichukuliwa na ikabaki moja iliyoandikwa matusi, huku mwanafunzi mmoja akikosa karatasi yake aliyopigia kura, na katika kufuatilia walibaini iliyobaki ni ya kwake hivyo taratibu za nidhamu zilichukuliwa ikiwamo kumsimamisha shule.
Sintoo alisema mwanafunzi aliyeandika matusi aliadhibiwa kwa kusimamishwa masomo kwa muda, hali iliyoibua taharuki kwa wenzake na kwenda kuvamia nyumba ya mwalimu huyo kwa madai kuwa ndiye amekuwa akiwatolea matusi.
Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Hamisi Issah alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 4:00 asubuhi.
Issah alisema miongoni mwa mali zilizoharibiwa ni milango, madirisha, mabati na migomba yote inayozunguka nyumba hiyo ambayo ipo eneo la shule.

Lukuvi, naibu wake wapishana msituni


Unaweza kusema ni mwendo wa mbio za nyika namna mambo yanavyokwenda katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Wakati Waziri William Lukuvi akiwa ameanzia mkoani Kagera na Shinyanga ambako ameacha vumbi likitimka dhidi ya maofisa ardhi na matajiri waliokuwa wakionea maskini kwa kuwanyang’anya maeneo yao, naibu wake Angelina Mabula alianzia Mwanza baadaye Mara na sasa yupo Kilimanjaro.
Akiwa Kilimanjaro, juzi Mabula alikabidhiwa na CCM migogoro miwili ya ardhi mjini Moshi ikitaka asaidie kuipatia ufumbuzi.
Migogoro hiyo ni wa Pasua Block JJJ ambako zaidi ya watu 100 waligawiwa viwanja na Manispaa ya Moshi, lakini kampuni ya Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), inadai ni mali yake.
Septemba 14 mwaka jana, Rahco iliweka alama X katika nyumba hizo ikiwataka wazibomoe ndani ya siku 30, lakini halmashauri inadai Rahco hawajawahi kumiliki eneo hilo wala hawakuwahi kupewa na kwamba, halmashauri wakati ikiandaa mpango kabambe wa mji (master plan) mwaka 1962, ilitenga tu eneo la kujenga viwanda na ikatenga kipande cha ardhi cha kujenga reli kuhudumia viwanda hivyo.
Hata hivyo, viwanda hivyo havikujengwa na eneo lote kujengwa makazi hivyo halmashauri ikaomba kubadili matumizi ya kipande cha ardhi kilichokuwa kijengwe reli, maombi yaliyoridhiwa na wizara.
Akiwasilisha nyaraka za mgogoro huo ikiwamo hati miliki, katibu wa CCM Mkoa Kilimanjaro, Jonathan Mabhia alisema mgogoro huo ni kero inayohitaji majibu.
“Wananchi wangependa wapatiwe majibu ya uhakika wa kuendelea kuishi na unavyojua migogoro ya ardhi ni kero kubwa,” alisema Mabhia na kuongeza: “Maana tunaonekana kama hatushughuliki na matatizo ya wananchi. Ni matumaini yangu utatusaidia kushughulikia tatizo hilo ambalo kwa kweli ni kero kubwa kwa wananchi.”
Katibu huyo alisema kwa kutambua CCM ndio kimbilio la Watanzania, wapo wananchi waliompelekea barua yeye na wengine walituma barua hizo kwa katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Mgogoro mwingine aliouwasilisha ni wa Meresini katika mji mdogo wa Himo, ambako wananchi wananyimwa viwanja vikiwamo vya kujenga shule na kupewa watu wengine akiwamo mwekezaji.
Akijibu maombi hayo, Mabula alisema kwa kuwa mgogoro wa Pasua Block JJJ umewasilishwa ukiwa na nyaraka, atazipitia na kumkabidhi Kamishna wa Ardhi.
Kuhusu mgogoro wa Mieresini, alisema nalo amelichua ili alifuatilie aone namna ugawaji huo ulivyofanyika na kilio cha wananchi.

Jinsi ya kutengeneza mtandao bora wa ajira na biashara


Shughuli nyingi duniani zinafanikiwa kwa kutegemeana. Hauwezi kufanikiwa kwa kuamua kufanya kila kitu peke yako pasipo kuwashirikisha au kujifunza kutoka kwa wengine.
Hii inatulazimu kuhakikisha tunatengeneza mitandao ya watu watakao kuwa na tija kwenye mafanikio ya shughuli zetu.
Kila siku kuna jambo jipya la kujifunza linaloweza kukusogeza hatua moja mbele katika mafanikio ya kile unachofanya. Njia nzuri ya kujifunza ni kuwa karibu na wale waliofanikiwa tayari. Lengo la kutengeneza mtandao wa kiajira au biashara siyo kujifunza pekee bali kupata fursa mbali mbali zinazoweza kuwa matokeo ya kuwa karibu na wale wanaoweza kuwa msaada katika kukupa fursa mbali mbali ikiwemo taarifa.
Wewe kama ni mfanyabiashara kuna wafanyabiashara wengine ambao wanaweza kusadia biashara yako kwa namna moja ama nyingine. Hawa ni watu kuwaweka karibu sana.
Kama unatarajia kufanya kazi kampuni fulani hapo baadaye ni vyema kutafuta mtu au watu wanaoweza kuwa msaada kufikia lengo hilo.
Mtandao wa kiajira au kibiashara ni jumla watu wako wa karibu unaowasiliana nao mara kwa mara huku uhusiano wenu ukiwa umejengwa kwa lengo la wewe kunufaika au kunufaishana katika shughuli mnazofanya au mnazotarajia kufanya.
Je, ni nani wa kumuweka kwenye mtandao wako?
Sio kila mtu anastahili kuwa kwenye matandao wako. Kuna mambo kadhaa ya kuzingatia unapoamua kumuingiza mtu kwenye aina hii ya mtandao lakini kigezo kikubwa ni mtu anayaweza kukupa fursa au mwenye uwezo wa kukuunganisha na fursa au watu wengine wenye fursa au yeye mwenyewe ni fursa katika mafanikio ya shughuli zako.
Usimuweke mtu kwenye mtandao wako ambaye si msaada na wala hatakuwa msaada katika shughuli zako sababu mwisho wa siku anaweza kuwa mzigo pia.
Ukiwa unatamani kuwa mshehereshaji (MC) mwenye mafanikio ni vyema kuanza kufanya utafiti ili kujua ni watu gani wamefanikiwa katika eneo hili na kuwaweka karibu.
Wakati mwingine itakubi kuwaomba ufanye nao kazi hata bila malipo ili uweze kujifunza na kuunganishwa na watu wengine wanaoweza kuwa msaada katika shughul hii.
Mbinu hii inawafaa sana wale walio kwenye mchakato wa kutafuta ajira. Ni vyema kuwa karibu na wale wanaoweza kuwa ngazi ya mafanikio yako kama siyo sasa basi ni ya baadaye.
Unawezaje kuwapata watu sahihi wa kuwaweka kwenye mtandao?
Kile unachokifanya au unataka kukifanya mara nyingi kinakuwa tayari kimeshafanywa na watu wengine na wameshafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Ukitaka kuanzisha biashara ya kuafirisha nafaka kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine wapo watu wamekuwa wakiifanya biashara hii kwa miaka mingi na wana uzowefu.
Tafuta wawasilino yao na omba kuonana nao ana kwa ana kama inawezekana.
INAENDELEA UK 26
Kama ni ngumu kuonana nao zungumza nao kwa simu au barua pepe ukieleza lengo la wewe kutaka kujifunza kutoka kwao. Inawezekana wapo wanaoweza wasipende wazo hili lakini pia wapo wanaoweza kuonesha moyo wa kusaidia.
Katika masuala ya biashara wateja wako wa sasa na wateja wako watarajiwa ni watu muhimu sana kuwaweka karibu ili wawe msaada kwenye biashara yako.
Wapo wafanyabiashara waliojiwekea utaratibu wa kuwajulia hali wateja wao na kufanya ufuatiliaji wa mrejesho wa huduma au bidhaa wanayo uza.
Kumbuka ni vyema kuwa mtu wa kujichanganya na kujitambulisha kwa watu tofauti ili wajue unafanya shughuli gani na kama ni mtafuta ajira wajue sifa ulizo nazo. Umeenda kwenye kongamano na umekutana na watu mbali mbali, wasalimie, ongea nao ili ujue shughuli waazofanya na mwisho ubadilishane nao mwasiliano na ukumbuke kuwasiliana nao muda mfupi baada ya kuachana nao.
Jinsi ya kuimarisha mtandao wako
Unapoamua kuanzisha mtandao au kumuweka mtu kwenye mtandao wako ni vyema kuzingatia kuwa ili mtandao uwe na tija ni lazima uimarishwe.
Njia kuu ya kuimarisha mtandao wa aina hii ni mawasilinao ya mara kwa mara. Mawasiliano haya yanaweza kuwa kwa njia ya simu, barua pepe na njia nyingine za mawasilinao lakini kukutana ana kwa ana pale inapowezekana.
Wasiliana na wadau wako hasa wateja. Unaweza jiuliza, kama nina wateja wengi sana huo muda wa kumjulia hali mmoja mmoja au kujua kama wamelidhika na huduma ua bidhaa yangu nitautoa wapi? Si lazima ufanye wewe lakini pia teknolojia imerahisisha mawasilino kwani waweza tuma barua pepe moja kwa mamia ya wateja wako au kwa kuwatumia ujumbe mfupi wote kwa pamoja.
Kwa wale wadau wako wakuu au wa karibu sana ni vyema kufanya mawasilino ya moja kwa moja na ikiwezekana kukutana nao mara kwa mara.
Suala jingine ni kuhakikisha kuwa unakuwa mwaminifu. Si vyema kutoa taarifa za uongo na ahadi usizowezo kuzitekeleza. Mambo haya yana athari kubwa sana katika mtandao na yanaweza kukuharibia sifa njema na kuondoa imani kutoka wadau mbali mbali.
Angalizo
Kwa kuzingatia kuwa mawasiliano ndiyo msingi wa mtandao bora ni vyema kuhakikisha kuwa mawasiliano yanafanywa kwa uangalifu.
Watu hututathamini kwa namna tunavyowasiliana nao. Hakikisha kuwa mawasilino yako hayawi kero au usumbufu kwa watu kwenye mtandao wako.
Ni vyema kuzingatia muda wa kufanya mawasilino; si kila wakati ni muda muafaka wa kufanya mawasilino.
Wapo ambao hawapendi kufanya mawasiliano usiku wanapokuwa na familia zao na hupenda kufanya hivyo muda wa kazi pekee.
Mtandao bora ni ule ambao ni kutegemeana na siyo wa kunufuisha upande mmoja hivyo ni vyema kuhakikisha unajitahidi kuangalia mtandao wako utawanufaishaje watu kwenye mtandao wako. Inawezekana hauwezi kutoa ajira lakini unaweza kutoa taarifa zinazoweza kuwa msaada kwa watu wengine kwenye mtandao wako.

Upelelezi bado kesi ya kina Rugemalira


Upande wa mashtaka katika kesi inayowakabili Habinder Sethi na James Rugemalira umedai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababisha Serikali hasara ya Dola 22.198 milioni za Marekani (Sh309.5 bilioni) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mwendesha mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),  Leonard Swai amedai hayo mahakamani leo Machi 2,2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati shauri lilipotajwa.
"Upelelezi wa kesi hii bado haujakamilika, hivyo tunaomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa," amesema Swai.
Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 16, 2018 itakapotajwa. Washtakiwa wamepelekwa rumande.

NCAA na Tato kushirikiana kukuza utalii nchini

Naibu Mhifadhi wa NCAA anayeshughulikia  huduma
Naibu Mhifadhi wa NCAA anayeshughulikia  huduma za shirika,  Asangye Bangu 
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Chama cha Mawakala wa Utalii (Tato), wamefikia makubaliano  ya kuondoa vikwazo na tofauti baina yao, hivyo kushirikiana katika kukuza utalii hapa nchini.
Makubaliano hayo, yalifikiwa leo Machi 2, katika kikao kilichofanyika Arusha,   kati ya  viongozi wa NCAA,Tato na  kampuni za utalii  ambazo hivi karibuni zilitajwa kuwa huenda zingezuiwa kuingiza watalii katika Hifadhi ya Ngorongoro.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Mhifadhi wa NCAA anayeshughulikia  huduma za shirika,  Asangye Bangu amesema  NCAA imejipanga kuboresha huduma kwa watalii na kuondoa changamoto zinazowakabili wenye kampuni za utalii.
"Kikao chetu kimekwenda vizuri, NCAA tutaendelea kuboresha mifumo ya malipo, kuboresha mawasiliano baina yetu na mawakala wa utalii lakini pia kutatua changamoto kadhaa, ikiwamo barabara ndani ya hifadhi,"amesema
Bangu amesema katika kukabiliana na kero ya barabara, Agosti 8 mwaka huu NCAA inatarajiwa kuanza ujenzi wa barabara ya kutoka geti la kuingia Ngorongoro hadi la Serengeti lenye urefu wa kilomita 83 kwa kuweka tabaka gumu juu.

"Hii ni kero ya muda mrefu ya kampuni ya utalii lakini sasa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO) limetukubalia kuijenga barabara hii na ikikamilika tuna imani barabara itadumu kwa zaidi ya miaka 40,"amesema.
Awali, Katibu Mtendaji wa Tato, Siriri Akko amesema katika siku za karibuni kuliibuka taarifa za kuwachanganya baadhi ya wanachama wao juu ya kuzuiwa kuingia Ngorongoro kupeleka watalii.
Hata hivyo, amesema baada ya kupata maelezo kutoka NCAA wamefikia makubaliano ambayo lengo lake ni kuboresha sekta ya utalii nchini na pia kuondoa changamoto zinazowakabili.
"Kikao chetu kimekwenda vizuri na ile hofu ya kampuni kuzuiwa sasa haipo na tuna imani kampuni zote zitafuata sheria na taratibu za kufanya biashara ya utalii hapa nchini,"amesema.
Akizungumza katika kikao hicho leo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Shidoria, Lazaro Mafie amesema ni muhimu kuwapo na mawasiliano ya mara kwa mara baina ya NCAA na kampuni za utalii ili kutatua kero.
Mafie amesema wao kama wamiliki wa kampuni za utalii, wateja wao ni watalii sawa na NCAA ambayo uwapo wao unategemea watalii, hivyo ni lazima kuwapo na mawasiliano mazuri baina yao.
"Kuna changamoto kadhaa ambazo tunakabiliana nazo lakini tuna imani sasa zitafanyiwa kazi ili kuboresha sekta ya utalii hapa nchini,"amesema.

Albino asiye na mikono yote kupanda Mlima Kilimanjaro


Wanawake wenye ulemavu wa ngozi barani Afrika akiwamo Mtanzania aliyekatwa mikono yote miaka 10 iliyopita kwa imani za kishirikina, Mariam Stanford watapanda Mlima Kilimanjaro ili kutoa ujumbe kwa dunia kwamba licha ya ulemavu walionao, wana uwezo wa kufanya jambo lolote.
Mpango huo wa kukwea Mlima Kilimanjaro umebuniwa na mwanaharakati wa haki za binadamu, Jane Waithera na kusimamiwa na Taasisi ya Under the Same Sun (UTSS).
Akizungumza katika mkutano leo Ijumaa, Machi 2, Waithera amesema wanawake hao watapanda kwa siku nane kuanzia Septemba 24, 2018.
Mariam amesema kutokana na changamoto alizozipata, anaona kazi ya kupanda mlima itakuwa rahisi licha ya ulemavu wake.
"Nimekatwa mikono miwili bila ganzi, nimeishi maisha ya hofu, sasa ninajiamini ninaweza kufanya jambo lolote linaloweza kufanywa na binadamu," amesema.
Amesema wanapanda Mlima Kilimanjaro ili, “Kuwaonyesha watu kwamba sisi ni wanawake wenye ulemavu wa ngozi lakini tunaweza.”
Katika kudhihirisha kwamba anaweza licha ya ulemavu wa aina mbili alionao, Mariam anatengeneza masweta ambayo yamekuwa yakimwingizia kipato na kumfanya awe na maisha mazuri.
Mwanzilishi wa taasisi ya UTSS, Peter Ash kutoka Canada amesema wanawake hao kupanda Kilimanjaro kama kielelezo kwamba wanaweza kujitegemea.
"Kupanda mlima ni njia nzuri ya kuwaonyesha watu kwamba tupo, tunajitegemea na tunaweza" amesema.
Mkurugenzi mtendaji wa UTSS, Vicky Ntetema amesema hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa wanawake wenye ulemavu wa ngozi kupanda Mlima Kilimanjaro.

Dk Mpango aiomba WB mkopo wa Dola 150 milioni za Marekani


Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango ameiomba Benki za Dunia (WB), kuipa Tanzania mkopo wa Dola 150 milioni za Marekani ili kuchochea ukuaji wa uchumi na utoaji wa huduma nchini.
Dk Mpango ametoa ombi hilo leo Machi 2 wakati alipokutana na Mkurugenzi wa Uchumi Mpana, Biashara na Uwekezaji wa Benki ya Dunia, Felipe Jaramilo katika ofisi za  Wizara ya Fedha na Mipango Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, Waziri wa Fedha na Mipango aliishukuru WB kwa kuendelea kuisaidia Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk John Pombe Magufuli katika kutekeleza miradi ya maedeleo nchini.
Dk Mpango ameeleza kuwa uchumi wa nchi umeendelea kukua kwa kiwango cha kati ya asilimia sita hadi saba kwa mwaka na hivyo kuiwezesha Serikali kuendelea na utoaji wa huduma za jamii na kuwekeza katika miradi ya maendeleo.
“Pamoja na ukuaji mzuri wa uchumi, Taifa bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ukosefu wa ajira kwa vijana, kiwango cha umaskini bado kiko juu, ukuaji  mdogo wa sekta ya kilimo na kupungua kwa mikopo ya benki za biashara kwa sekta binafsi,”amesema.
Wakati huohuo, Dk Jaramilo aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri inayofanya ya kusimamia uchumi mpana na kuongeza makusanyo ya ndani ambayo yanasaidia upatikana fedha kwa ajili ya kugharamia uwekezaji katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aliishauri Serikali kuwekeza zaidi katika rasilimali watu na miundombinu  ili  Taifa liweze kuhimili ushindani  wa kimataifa wa dunia na kujenga uchumi unaokua  na  endelevu.

Wizara kushauri uundwaji wa jeshi jipya mahsusi kwa misitu na wanyamapori


Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamis Kigwangalla amesema wizara ipo kwenye mchakato wa kumshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuunda Jeshi jipya litakalokuwa maalumu kwa usimamizi wa wanyamapori na rasilimali za misitu nchini ili kuboresha utendaji kazi katika sekta hiyo.
Amesema hatua hiyo inalenga kudhibiti na kusimamia sekta ya maliasili kutokana na kuingiliwa na majangili wanaosababisha rasilimali hiyo kuteketea. 
"Vikosi vya majeshi vilileta ushauri huo na sasa wizara tumeona jambo hilo lina tija kweli, hivyo tupo kwenye mchakato huo na tumefikia hatua nzuri tukikamilisha tunampelekea Rais kwa kumshauri aanzishe jeshi jipya kwa ajili wanyamapori na misitu, tunaamini jambo hili litazaa matunda,” amesema.
Amefafanua kuwa jeshi litakaloundwa litakuwa chini ya Rais mwenyewe na litasaidia kuleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji na kujenga nidhamu kwa watumishi.
Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Misitu Tanzania,(TFS) Professa Dos Santos Silayo amesema kwa sasa wameimarisha utendaji wa wakala huo tofauti na ilivyokuwa awali wa kusimamia mapato  tu.
Amesema hatua ya kubadili wakala huo na kuwa mamlaka kamili ya misitu itaongeza ufanisi na utendaji kazi katika sekta hiyo. 
"Mbali na kuweka mifumo mizuri ya udhibiti lakini tumeanza ushirikishwaji wa wananchi wanaoishi karibu na misitu ili kuweka ulinzi wa rasirimali hizo.”

Mwanamke aliyepambana na mamba afanyiwa upasuaji mkubwa wa mguu leo


Mwanamke aliyeshambuliwa na mamba, Martha Malambi (25) amefanyiwa upasuaji mkubwa wa mfupa mrefu wa paja baada ya majeraha aliyopata kutengemaa.
Martha aliyelazwa katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) baada ya kushambuliwa na mamba huyo wakati akiteka maji kwenye Mto Mgeta katika Kijiji cha Ukutu Kata ya Bwakilachini, Morogoro anaendelea vizuri kiafya baada za kufanziwa upasuaji huo leo Machi 2.
Mtaalamu mwandamizi wa upasuaji wa mifupa MOI, Dk Paul Marealle amesema Martha anaendelea vizuri na upasuaji huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
"Huu ni upasuaji mkubwa wa mfupa mrefu wa paja, umekamilika vizuri, amewekewa chuma maalumu ndani ya mfupa (sign nail)." amesema.

Friday, March 2

Tanzania yakanusha kuminya demokrasia


Serikali ya Tanzania imekanusha tuhuma kwamba inaminya demokrasia nchini humo na kusema kuwa imesikitishwa na matamko kadhaa yaliotolewa na Marekani na Umoja wa Ulaya (EU) na kuungwa mkono na baadhi ya balozi za nchi za Magharibi.
Taarifa ya serikalli ya Tanzania imefuatia matamko yaliyotolewa na nchi za magharibi wiki za hivi karibuni yakielezea wasiwasi wao kutokana na matukio ya kiusalama ambayo wameeleza yanatishia utawala wa kisheria na maadili ya kidemokrasia nchini Tanzania.
Katika wiki za hivi karibuni polisi wa Tanzania wameshutumiwa kwa kutumia nguvu za kupita kiasi kushughulikia mivutano ya kisiasa na pia wanasiasa kadha wa upinzani wakiwemo wabunge mara kwa mara wameitwa polisi kwa mahojiano kutokana na madai ya kufanya mikutano isiyo halali.
Mbunge wa upinzani Joseph 'Sugu" Mbilinyi na afisa mwingine wa chama cha Chadema mjini Mbeya walihukumiwa kifungo cha miezi mitano gerezani mwishoni wa Februari baada ya kukutwa na hatia ya kumkashifu Rais John Pombe Magufulu
Taarifa hiyo iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania pia imesema kuwa tayari nchi hiyo imechukua hatua kukubaliana na vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini. Nchi za magharibi ziliishutumu Tanzania kwa kukiuka vikwazo hivyo.
Hata hivyo Tanzania imesema tuhuma kwamba imekiuka vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya silaha za nyuklia za Korea Kaskazini na programu yao ya makombora ya balistika hazijaweza kuthibitishwa..
Taarifa hiyo imeeleza kuwa suala la utawala wa sheria na demokrasia katika tamko hilo la mabalozi linaonyesha sintofahamu iliyoko juu ya usalama na changamoto za kisiasa ambazo Tanzania imekuwa ikikabiliwa nazo kwa kipindi cha miezi 18 na kwamba matamko hayo yamekuwa sio tafsiri sahihi ya hali ya kisiasa na usalama iliyopo Tanzania.
“Ni kawaida kwa wanadiplomasia wa kigeni kufuatilia na kuripoti hali ya kisiasa na usalama inayoendelea katika nchi walizotumwa. Lakini tunashangazwa na ukimya uliowazi katika kipindi cha nyuma wa mabalozi hawa juu ya vitisho vya uvunjifu wa amani uliokuwa haujawahi kutokea na changamoto nyingine ambazo Tanzania imekuwa ikikabiliana nazo katika maeneo matatu ya Kibiti-Mkuranga –Rufiji yanayopakana,” limesema tamko hilo.
Wizara hiyo imeeleza kuwa vitisho hivyo vimewauwa watu wasio na hatia na kwa sadfa ya ajabu, wengi wa waliouwawa walikuwa kutoka chama tawala.
Mauaji hayo yalikuwa yametanguliwa na matukio kama hayo ya uvunjifu wa amani katika maeneo mbalimbali ya nchi yakiwa ya aina yake yalihusisha uvunjifu wa amani.
Kwa mujibu wa tamko hilo pamoja na kuwepo taarifa za matukio haya ya uvunjifu wa amani yalitolewa na vyombo vya habari nchini, hakukuwa hata na tamko lililolaani vitendo hivyo kutoka kwa mabalozi hao.
Wizara imehoji kuwa ni hivi sasa tu ndio EU inataja juu juu shambulizi la silaha lililotokea Mkoa wa Pwani katika kipindi cha miaka miwili.” Kuchelewa kutolewa kwa matamko hayo baada ya muda mrefu na wakati mgumu unastaajabisha.
Moja ya matamko yaliyotolewa na mabalozi wizara imesema ni jambo zuri kwa mabalozi wametambua wito wa Rais Magufuli akitaka uchunguzi ufanyike wa matukio mengine ya uvunjifu wa amani katika wimbi la operesheni ya Kibiti, Mkuranga na Rufiji.
Lakini wizara imesema kuwa matamko hayo ya mabalozi hayakutambua uhusiano uliokuwepo kati ya hatua za kishujaa ambazo zimechukuliwa na Rais Magufuli kuondoa ufisadi, madawa ya kulevya, ukwepaji kodi, ujangili wa nyara za serikali na kuhakikisha uwajibikaji katika sekta binafsi na za umma, na matukio ya usalama.
“Hatua za serikali ya awamu ya nne bila shaka zimewakasirisha watu wenye nguvu ndani na nje ya nchi ambao wanamaslahi binafsi katika hali ya uzembe iliokuwa inaendelea hapo awali nchini,” taarifa hiyo imesema.