Thursday, November 9

Familia ya Lissu yalia na Bunge

Familia ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu imeibuka kwa mara nyingine ikiliomba Bunge kutokukwepa wajibu wa kugharimia matibabu ya ndugu yao kwa kuwa si hisani bali ni stahiki anazopaswa kupewa.
Pia, familia hiyo imesisitiza wito wake kwa Serikali wa kuruhusu uchunguzi kutoka nje ili ukweli ujulikane kuhusu waliohusika kumjeruhi kwa risasi Lissu Septemba 7, mjini Dodoma.
Imesema haiwezekani miezi miwili imepita tangu aliposhambuliwa lakini hakuna taarifa za kukamatwa kwa mtu yeyote.
Vincent Mughwai, ambaye ni mdogo wa Lissu alisema hayo jana katika ofisi za Mwananchi, Tabata- Relini jijini Dar es Salaam.
Kwa mwezi wa pili sasa Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.
“Miezi miwili imepita gharama za matibabu ziko juu na ni wananchi wa Tanzania ndiyo wamezilipa. Mshangao wetu ni kuwa, Lissu ni mbunge na kama kiongozi ana haki ya kutibiwa na si kubaguliwa,” alisema Mughwai.
Alisema, “Lissu ana bima, bado hajaweza kupata msaada na sisi tunasema kulikoni, kama viongozi wengine wakiugua gharama zao zinalipwa na Bunge, huyu pia ni mbunge kwa nini kunakuwa na double standard kwa ndugu yetu.”
Mughwai alisema kikao walichokaa na uongozi wa Bunge, Oktoba 2 kujadili matibabu kilikwenda vizuri na wao kama familia walieleza kutokuwa na pingamizi la ndugu yao kugharamiwa lakini tangu siku hiyo mpaka sasa hakuna taarifa zozote kutoka kwa Bunge.
“Familia hatujajulishwa ingawa tuliandika si barua bali ujumbe kwamba familia haina tatizo Bunge kulipa gharama za matibabu ya Lissu lakini kimya, Bunge wanajua huyu mgonjwa anaishije huko? Tunaomba apate stahiki zake kama anavyostahili,” alisema.
Kauli hiyo ililifanya Mwananchi kumtafuta Spika wa Bunge, Job Ndugai lakini hakuweza kupatikana huku Katibu wa Bunge, Stephen Kigaigai akisema ‘’mimi sijui na sijapata taarifa kuhusu suala hilo kwani mazungumzo yalipofanyika mimi sikuwapo.”
Mdogo huyo wa Lissu alisema ‘’sisi tunaendelea kuwashukuru Watanzania kwa kujitoa, Chadema kikiongozwa na Mbowe (Freeman Mbowe-Mwenyekiti wa Chadema) ambao mpaka sasa wapo Nairobi, hatuna cha kuwalipa, tunaomba muendelee kumwombea na kutoa michango kupitia akauti za Chadema ili ndugu yetu aweze kupona.”
Kuhusu uchunguzi, Vicent alisema, “Tunaendelea kusisitiza Serikali iruhusu uchunguzi kutoka nje, waje washirikiane na jeshi letu la polisi, huu uvumi kwamba anayehusika ni fulani utamalizika, kama ni Chadema wamehusika watajukikana, kama ni nani watajulikanani hofu iko wapi,” alihoji Vicent
Alitolea mfano, Meja Jenerali mstaafu Vicent Mribata aliyepigwa risasi maeneo ya Ununio- Tegeta jijini humo kuna watuhumiwa walikamatwa lakini tukio la Lissu mpaka sasa hakun taarifa zaidi ya magari kumi aina ya Nissan kukamatwa nayo haijulikani yalipo.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi limekuwa likieleza kwamba uchunguzi wa suala hilo unaendelea na hauwezi kuwekwa hadharani kila hatua na mara baada ya kukamilika wataueleza umma.

Mwisho wa migogoro ya ardhi wakaribia

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akipokea malalamiko ya kudhulumiwa ardhi kutoka kwa mkazi wa wilayani Mvomero, mkoani Morogoro. 
Matumizi ya ardhi ni mabadiliko yanayofanywa na binadamu kwa mazingira ya asili au jangwani kulingana na mahitaji, lakini lengo ni kuwa na mazingira yaliyojengwa kama mashamba, malisho na makazi.
Hata hivyo, inaelezwa matumizi ya ardhi na usimamizi wake wakati mwingine huwa na athari kubwa kwa mazingira kwa maana ya maliasili, vyanzo vya maji, udongo, virutubishi, mimea na wanyama.
Kwa mfano, vyanzo vya maji katika eneo lililokatwa miti ovyo au kwenye mmomonyoko, itakuwa na tofauti ya ubora kuliko yale ya maeneo yenye miti mikubwa na misitu ya kutosha.
Kulingana na ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula  Duniani (FAO),  uharibifu wa ardhi umeongezeka kwa kiwango kikubwa karibu katika nchi nyingi duniani.
Tatizo hilo linadaiwa kusababishwa na  kukosekana kwa mipango muhimu  ya matumizi bora ya ardhi.
Tanzania yachukua hatua
Hata hivyo, baada ya Tanzania kulibaini hilo, tayari Serikali imeanzisha Mfumo Unganishi wa Taarifa za Ardhi, Kiingereza maarufu kwa jina la ‘ Integrated Land Management Information System (ILMIS), utakaosaidia kutoa taarifa muhimu za ardhi kwa wananchi.
Akizungumza hivi karibuni, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema mradi huo unatekelezwa na wizara yake.
Anasema ILMIS inalenga kuboresha usalama na kiwango cha kuaminika cha shughuli za ardhi kwa kuanzisha mfumo wa taarifa za ardhi.
Lukuvi anasema mradi huo ni salama na unaoaminika, kwani utawezesha kutoa huduma za ardhi zenye gharama nafuu na zenye kuleta imani zaidi kwa wananchi kutokana na ulivyoundwa.
Akizungumza wakati wa warsha ya mafunzo ya uboreshaji utendaji wa wadau wa ILMIS iliyofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya New Africa, Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Moses Kusiluka alisema changamoto katika sekta ya ardhi zinaikabili Tanzania kwa kadiri kumbukumbu za binadamu zinavyoweza kurudi nyuma.
Anasema tayari majaribio kadhaa yameshafanywa miaka michache iliyopita kwa lengo la kukabiliana na changamoto hizo.
Dk Kusiluka anasema katika muongo mmoja uliopita, kumekuwapo na majaribio kadhaa ya Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, kuweka taarifa na rekodi za ardhi katika mfumo wa kompyuta.
Akitoa mifano ya majaribio hayo ya Serikali kutafuta majawabu ya changamoto za ardhi, Naibu Katibu Mkuu alisisitiza:
“Huko nyuma, Serikali ilibuni na kutekeleza miradi ya Mfumo wa Taarifa za Ulipaji Kodi za Ardhi (LRMS), Mfumo wa Menejimenti ya Taarifa za Ardhi (Molis) na Mfumo wa Kusajili Maeneo ya Ardhi Yaliyopimwa (SRS), kwa kutaja machache tu. Lakini katika majaribio hayo yote kila mfumo ulikuwa unajitegemea na kusimama peke yake bila kuunganika ama kuwasiliana na mwingine.”
Dk Kusiluka anaongeza: “Hakuna shaka kuwa mifumo hii ilisaidia uwekaji taarifa na kuboresha mifumo ya kibiashara ya ardhi wizarani, lakini bado uunganishaji taarifa na uwezo wa kubadilishana taarifa hizo kwa wepesi ilibakia changamoto yetu kuu. Mifumo hiyo iliyokuwapo haikuweza kufanikiwa ipasavyo kutatua changamoto za jinsi ya kutunza, kuweka na kubadilisha taarifa za ardhi kwa urahisi na kwa wepesi.”
Hata hivyo, Juni 25 mwaka huu, kikosi kazi cha masuala ya matumizi ya ardhi kilichokuwa kimejumuisha wadau kutoka serikalini na asasi za kiraia, kilikutana na kukamilisha rasimu ya mkakati wa kukabiliana na changamoto za matumizi ya ardhi nchini.
Mkakati huo uliwasilishwa katika ngazi ya juu kwa utatekelezwa, kusimamiwa na kufuatiliwa.
Kwa mujibu wa Dk Stephen Nindi, aliyezungumza kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi (NLUP), Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zenye utulivu wa migogoro ya ardhi iwapo mpango huo utatekelezwa.
Mratibu wa programu ya ardhi wa shirika la kimataifa la Care, Mary Ndaro anasema maeneo mengi yakipimwa yatasaidia kuwapo kwa usalama wa miliki na hati miliki hususani kwa wananchi wa vijijini  ambao karibia asilimia 60 wanategemea ardhi kwa ajili ya kujipatia kipato.
Hivyo uamuzi unaochukuliwa sasa na Serikali wa  kuwekeza katika upangaji wa matumizi bora ya ardhi, utasaidia kupunguza kama siyo kumaliza kabisa migogoro ya ardhi nchini.
Wakati wadau hao wakizungumza hayo, Serikali inasema ili kutafuta jibu la pamoja la changamoto za namna ya kuweka taarifa za ardhi linalofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Ardhi, imemwajiri mtaalamu ambaye atatekeleza kwa majaribio mpango wa kubuni, kuendeleza, kufunga na kuanza kutumia mfumo wa ILMIS, mradi unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).
Mfumo huo unatekelezwa kwa majaribio katika Halmashauri za Kinondoni na Ubungo, mkoani Dar es Salaam.
Dk Kusiluka anasema ILMIS itaunganisha shughuli zote za menejimenti ya ardhi, usajili na uandikishaji wa shughuli zote.
“Mfumo huo pia utasaidia kazi ya kubadilisha rekodi za ardhi na ramani kutoka kwenye rekodi za makaratasi na kuzigeuza kuwa za kidigitali,” anasema.
Kwa mujibu wa Dk Kusiluka kazi hiyo iliyoanza Julai mwaka jana, itakamilika Julai mwaka 2018.
Anasema kipindi hicho kitafuatiwa na cha mwaka mmoja cha kuendelea kuangalia utendaji wa mfumo kabla ya kuanza kusambazwa nchi nzima.
 “Shabaha kuu ya ILMIS ni kujenga mfumo halisi, wenye kubeba taarifa zote za ardhi sehemu moja ili kuongeza usalama wa taarifa hizo na imani ya wananchi hivyo kuongeza huduma kwao,” anasema.
Nini kifanyike ili kukamilisha mpango huo?
Ili kufanikisha shabaha hiyo, hatua kadhaa zitachukuliwa wakati wa utekelezaji wa awamu kwa awamu.
Hatua hizo zitakuwa ni kubuni majawabu ya changamoto za ardhi ambazo zitawezesha kuboreshwa kwa huduma zote za ardhi kwa kuchukua hatua za kitaalamu, kusudi kuleta utulivu na usalama katika mfumo wa utoaji huduma za ardhi.
ILMIS itahakikisha inabadilisha mfumo wa kazi kutoka kwenye mfumo wa kutumia makaratasi na mafaili na kuweka kidigitali ili kurahisisha upatikanaji wa kwa kutumia kompyuta. 
Hata hivyo, inaelezwa ujenzi wa mfumo huo utakapokamili na kuanza kufanya kazi kwa ukamilifu, muda wa kuhakiki na  kuboresha taarifa za ardhi na hata kuhamisha miliki ya ardhi utafupishwa kuliko ilivyo sasa.
Dk Kusiluka anasema ILMIS utasaidia kulinda ardhi ya umma kwa kuzuia uvamizi wa maeneo tengefu, misitu, hifadhi ya barabara na ardhi nyingine ya umma.
Uvamizi wa ardhi ya umma, imekuwa changamoto kubwa nchini. Hivyo, ILMIS itaongeza uendeshaji na ulinzi wa ardhi ya maeneo ya hifadhi na maliasili.
Pengine kubwa zaidi kwa wananchi ni kwamba, ILMIS itawasaida kupunguza kero za rushwa zinazohusishwa na uhakiki, usajili na uandikishaji na uhamishaji wa miliki ya ardhi, anasema Dk Kusiluka.
Tatizo la rushwa
Kama liko jambo moja ambalo pengine kila Mtanzania anayemiliki ardhi nchini amekumbana nalo katika kuweka kumbukumbu zake za miliki ya ardhi ni rushwa.
Lakini Dk Kusiluka anasema ILMIS itaongeza uwezo wa Serikali na Taifa  kupambana na kero ya rushwa katika shughuli za ardhi.
Ni dhahiri kuondoka kwa kero ya rushwa kutaiwezesha ILMIS kuleta manufaa mengine kwa umma ambayo ni ongezeko la imani ya wananchi katika mfumo wa uendeshaji wa shughuli za ardhi, jambo ambalo kwa sasa halipo kwa sababu ya wingi wa changamoto katika uendeshaji wa shughuli za ardhi nchini. 
Kusiluka anaongeza pia kuwa ILMIS itaongeza uhusiano na mawasiliano kwa kuambatanisha wamiliki wa mali kwenye mali zao, na mali zenyewe.
Mpango huo pia utawasiliana moja kwa moja na kutoa taarifa za miliki na menejimenti ya shughuli za ardhi kwa njia ya kielektroniki kwa taasisi nyingine zitakazoteuliwa, zikiwamo benki, taasisi za kutoza kodi, kampuni na taasisi zinazofanya biashara ya kujenga, kuuza na kununua nyumba.

Waziri Mkuu awashukia mawaziri kuhusu matamko

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akielezwa jambo na
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akielezwa jambo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi walipohudhuria kikao cha pili cha mkutano wa tisa wa Bunge, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 
Dodoma/ Dar. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka mawaziri kuacha kutoa matamko yasiyotekelezeka kwani kufanya hivyo kunasababisha mikanganyiko serikalini.
Akifungua kikao kazi cha mawaziri kilichofanyika juzi katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma, Waziri Mkuu aliwataka viongozi hao wakajiridhisha kwanza kama jambo wanalotaka kulitolea tamko halitakuwa na athari za kibajeti na kisera na kujiridhisha kama lipo katika bajeti za wizara zao.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri baada ya kikao hicho imesema Majaliwa pia amewataka viongozi hao wafanye kazi kwa kuzingatia maadili ya uongozi ili kuithibitishia jamii kuwa Rais John Magufuli aliwateua kutokana na uadilifu na uwezo wao kiutendaji.
“Tunao wajibu wa kuhakikisha kila mmoja wetu anafanya kazi kwa nguvu na bidii ili kutimiza matarajio ya Mheshimiwa Rais Magufuli na wananchi wote kwa jumla,” alisema.
Majaliwa, ambaye alikuwa naibu waziri wa Tamiseni na ambaye ni mtendaji mkuu wa Serikali, aliwataka viongozi hao wajiwekee utaratibu wa kusikiliza hoja na shida za wabunge na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria, utaratibu na kanuni.
Ndoa kwa cheti cha kuzaliwa
Ingawa Waziri Mkuu hakuwataja viongozi hao, mawaziri wamekuwa wakitoa maagizo tofauti, yanayoonekana kukinzana na sera na pia kutozingatia uwezo wa kibajeti.
Mapema mwaka huu, Dk Harrison Mwakyembe, akiwa Waziri wa Katiba na Sheria, alikaririwa akisema mwananchi ambaye hatakuwa na cheti cha kuzaliwa, hataruhusiwa kufunga ndoa.
Dk Mwakyembe alipiga marufuku watu kufunga ndoa ya aina yeyote, iwe ya Serikali, kimila au ya dini bila kuwa na cheti cha kuzaliwa, agizo ambalo alitaka lianze Mei Mosi.
Lakini nsiku moja baadaye, Rais John Magufuli alifuta agizo hilo akisema halitekelezeki.
“Dk Magufuli amesema Serikali haiwezi kuruhusu masharti hayo kutumika, kwa kuwa yatawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao hawana vyeti vya kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado unakabiliwa na changamoto nyingi kwa wanaohitaji,” inasema taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa.
Pia, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba aliwahi kuagiza kuwe na mizani maeneo yote ambako nyama inauzwa, zikiwemo sehemu za nyama choma ili wateja wanufaike na viwango halisi badala ya kukadiriwa. Hata hivyo, agizo hilo la mwaka 2016 wakati Kilimo kikiwa pamnoja na mifugop na uvuvi, halijatekelezwa,
Waziri mwingine ni Selemani Said Jafo wa Tamisemi ambaye aliagiza halmashauri 12 kuwa zimelipa madeni yake Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa ifikapo Desemba 30.
Waziri mwingine anayedaiwa kutoa kauli zenye utata ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Tamisemi), Joseph Kakunda ambaye aliwataka viongozi wa dini nchini kujihadhari kuwaozesha wasichana ambao hawajamaliza kidato cha nne.
Alisema watoto wa kike wanashindwa kumaliza masomo kwa sababu ya mimba au kuozeshwa jambo ambalo limeendelea kuisumbua Serikali katika juhudi zake za kuokoa maisha ya watoto wa kike ili waendelee na masomo.
“Haiwezekani mtu anamkamata mtuhumiwa anatakatisha Sh1 milioni anakosa dhamana, halafu mtu anampa mimba mwanafunzi kisha anapata dhamana siku hiyohiyo, hapa tutakuwa hatuthamini maisha ya mtoto wa kike.”
“Tunapoelekea watoto wote watasoma shule kuanzia darasa la kwanza mpaka form four, sera yetu mpya ambayo tutai –adopt hivi karibuni inasema mwaka mmoja wa shule ya awali, miaka sita shule ya msingi na miaka minne ya sekondari ni lazima. Kwa hiyo tunapoelekea, ili mtoto aolewe lazima aonyeshe cheti cha kumaliza shule ya sekondari... Ndiyo... ili uolewe uonyeshe living certificate au vinginevyo tujue wewe hujasoma kabisa ili tuwahoji wazazi..”
Hata hivyo, siku moja baada ya kauli hiyo ambayo ilisambaa katika mitandao ya kijamii, Serikali ilikanusha. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais ( Tamisemi ), Selemani Jafo alisema habari hizo kuwa msichana atatakiwa kuwa na cheti cha kidato cha nne kabla ya kuruhusiwa kufunga ndoa ni za upotoshaji.
Kufuatilia utekelezaji
Waziri Mkuu pia amewataka mawaziri kufuatiliaji na kutathmini ya utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo inayohusu sekta zao kwa kuwa ni wasimamizi wa utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Alisema mawaziri na manaibu wao wanatakiwa wasimamie utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa kuanzia mwaka 2016/17 hadi 2020/21 na utekelezaji wa ahadi zote zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 na ahadi alizotoa Rais Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Wasomi, wabunge wapongeza
Alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu agizo hilo la Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo Bisimba alisema hatua hiyo itawarejesha katika mstari mawaziri ambao walikuwa wanatoa matamko yasiyotekelezeka.
Alisema Waziri Mkuu ni kiongozi wa mawaziri hivyo ni vizuri kuwarudisha katika mstari ili kuhakikisha hawatoi matamko yatakayoiweka Serikali njia panda.
“Kuna waziri aliwahi kusema ili kuolewa ni lazima mtoto amalize kidato cha nne, hivi wasiofika ndiyo wasiolewe?” alihoji.
“Wengine wanasema watafanya mambo makubwa ya maendeleo ilhali wanajua kabisa hayatekelezeki, ni vizuri kusema kitu unachokiamini na unachoweza kukifanya.”
Mwingine aliyempongeza ni Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye alisema Waziri Mkuu amekuwa mwerevu hasa kipindi hiki cha vyama vingi ambacho Serikali inafanya kazi na upinzani kama paka na panya.
“Unapokuwa serikalini wewe ni panya na upinzani ni paka, hivyo mara zote kuwindana ni jambo la kawaida cha msingi ni kuwa makini na matamshi yako,” alisema.
Alisema kwa sasa mawaziri wengi ni wageni hivyo Waziri Mkuu akiwa kiongozi wao ni lazima ahakikishe anasimamia wanasema nini, wakati gani na yataleta madhara gani kwa jamii.”
Alitoa mfano wa kauli iliyotolewa bungeni hivi karibuni na waziri mmoja kwamba hata vyerehani vinne ni kiwanda, akisema haikupaswa kutolewa na waziri.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema) Peter Msigwa alisema agizo hilo ni zuri lakini ni gumu kulitekeleza.
Mbunge wa Biharamulo Magharibi (CCM), Oscar Mkasa alisema hiyo ni kanuni ya kawaida ya utawala ya Serikali kufanya uratibu katika shughuli zake.
“Ni agizo zuri kwa sababu wananchi watahoji matamko yaliyotolewa na Serikali hivyo ni namna nzuri ya kuratibu,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Kunti Majala alisema kutoa matamko ambayo hayatekelezeki ni mfumo ulioanza tangu zamani.

USAFIRI: Daladala jijini Dar es Salaam kuanza kutumia kadi maalum za malipo


Dar es Salaam. Daladala jijini hapa zitaanza kutumia kadi maalumu za malipo ili kuondokana na changamoto za kulipa kwa fedha taslim.
Matumizi hayo yanayoanza leo yanatokana na uzinduzi wa kadi hizo uliofanyika jana.
Kadi mpya aina ya ‘Uhuru Pay’ zimeanza kufanya kazi katika baadhi ya daladala ikiwa ni hatua ya majaribio na zimezinduliwa na kampuni ya BCX ya jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa BCX-Tanzania Seronga Wangwe alisema lengo la kubuni mfumo huo ni kutaka kuboresha ukusanyaji wa mapato ya vyombo hivyo na kuwapa uhuru watumiaji wa daladala kusafiri kwa utulivu.
“Tunataka kuondoa vurugu za kukosa chenchi na wizi unaofanywa kwenye daladala badala yake pesa iende moja kwa moja katika akaunti benki. Abiria na kondakta wasilazimike kuwa na fedha taslimu,” alisema.
Licha ya abiria na makondakta, alisema tofauti na ilivyokuwa awali hivi sasa wamiliki wa vyombo hivyo wataweza kupata faida katika uwekezaji wanaoufanya kutokana na udhibiti wa mapato ya makusanyo.
Alisema katika hatua za awali mfumo huo umeanza kujaribiwa katika mabasi kumi yanayofanya safari zake kati ya Tegeta Nyuki na Kivukoni kabla ya kuhamia katika maeneo mengine ya jiji.
“Tunataka kubaini changamoto zilizopo kabla ya kufanya maboresho kukidhi mahitaji ya watumiaji na mifumo yetu ina uwezo wa kuhudumia watu wengi bila kuzidiwa tofauti na mingine,” alisema
Mfumo huo utaunganishwa moja kwa moja na wamiliki wa mabasi ili waweze kufuatilia mauzo ya tiketi ya kila siku kitu walichokosa kwa muda mrefu kwenye biashara hiyo.
Meneja wa usalama barabarani na mazingira kutoka Mamlaka ya Usafiri Majini na Nchikavu (Sumatra), Godfrey Silanda alisema wamefanya marekebisho ya kanuni kuendana na mfumo huo.
“Kwa mujibu wa TBS, watu nane wanaruhusiwa kusimama katika mita moja ya mraba. Lakini kwa kuzingatia aina ya basi, kila moja litakuwa na utaratibu wake,” alisema Silanda.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni ya Christiania, Emmanuel Mlaponi alisema mfumo huo utasaidia kuongeza mapato kwa kupunguza wiziunaofanywa na madereva au makondakta wasio waaminifu.
“Ilikuwa ni taabu kufutilia mapato. iNililazimika kuwafuata hawa wenzetu na nikawaambia wafikirie ni jinsi gani wanaweza kuniondolea changamoto hii.  NKuanzia sasa fedha itakua haipiti katika mikono ya mtu na itaenda benki moja kwa moja,” alisema Mlaponi.

Airtel kuboresha mtandao wake

Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson
Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa programu mpya ya  Airtel U900 inayolenga kuimarisha ubora wa mtandao na kutoa huduma bora kwa wateja wake. Kulia ni Meneja Ubora wa huduma za Mtandao Emmanuel Luanda. 
Dar es Salaam. Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania imezindua programu ya kuboresha huduma za mtandao kupitia teknolojia ya iliyopewa jina la ‘Mradi wa U900’.
Progrtamu hiyo itasaidia kuimarisha ubora wa mtandao na kutoa huduma bora kwa wateja wake mahali popote nchini.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, programu hiyo inahusisha uwekezaji mkubwa unaolenga kuhakikisha uhakika wa upatikanaji wa huduma ya 3G, ujazo wa data kamili pamoja na kuongeza kasi ya intaneti.
Akiongea wakati wa kutangaza huduma hiyo jijini Dar es Salaamn leo Novemba 9, Meneja Ubora wa huduma za Mtandao Airtel, Emanuel Luanda, amesema Airtel imedhamiria kuimarisha huduma ya mtandao kutokana na ongezeko la matumizi ya simu za smartphone kulikosababsiah kukua kwa mahitaji ya huduma hiyo.
“Kutokana na uboreshaji wa mtandao wetu, wateja wote nchini watakuwa wakitapa huduma yenye kasi na hivyo kuwa na uhakika na huduma bora kutoka Airtel wakiwa popote,” amesema.
Kwa mijibu wa Luanda ripoti ya hivi karibuni ya mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inayotoa mchanganuo wa matumizi ya huduma za Intaneti inaweka wazi kuweko kwa ongezeko la watumiaji wa huduma za intaneti kutoka asilimia 34 ya watanzania mwaka 2015 hadi aslimia 40 mwaka 2016. 
“Hali hiyo ndio inatoa msukumo hata kwetu Airtel kuendelea kuwekeza zaidi katika teknolojia mpya  ili kuwapatia wateja wetu huduma bora zaidi,” ameongeza.
Kwa upande wake, Meneja wa Masoko Airtel Tanzania, Arnold Madale amesema: “Kwa kuwa Airtel tunatambua mahitaji ya wateja wetu na hali ya soko, tumekuwa tukifanikiwa kuleta bidhaa zenye ubunifu na mpangilio wa huduma zinazozingatia mahitaji ya mteja.”
, hii ni hatua kubwa sana hasa kwenye ushindani wa biashara. Tunao  wateja ambao wanatumia mtandao wetu kwa ajili ya intaneti tu, lakini pia kuna wale wanaotumia kwa kupiga na kupokea simu, tunazo bidhaa na huduma ambazo zinakidhi matakwa ya wateja hao kwa muda wote wakiwa mahali popote. Kwa sasa hivi tunaendelea pia kuboresha huduma yetu ya 2G ili kutoa huduma yenye uhakika wa hali ya juu ikiwemo huduma ya Airtel Money ili kuendelea kuwafikia Watanzania wengi waishio pembezoni  huduma za kibenki na huku tukitimiza sera ya serikali ya kushiriki katika uboreshaji wa huduma bora za kifedha vijijini.”
“Tunapotangaza huduma hii muhimu ya kuboresha mtandao wetu, tunayo furaha kutangazia huduma ya Bando la OFA KABAMBE ambayo inapatika kwa urahisi na kumfanya mteja kuwa na Uhuru zaidi wa kutumia Intaneti  yenye kasi kwa muda mrefu zaidi kwa kuwasiliana na ndugu, marafiki  au wadau katika biashara mahali popote. Wateja wetu wataweza kufaidi huduma hii ya bando kwa kupiga *150*60#  na kujipatia 1GB, dakika150 kupiga mitandao yote na kudumu nazo kwa muda wa siku saba, aliongeza Madale.
‘Nia yetu ni kuendelea kukua kupita Maelezo huku tukitengeneza ujuzi wa kuaminiwa na wateja wetu kwa kuwa na gharama nafuu. Mradi wa U900 unadhihirisha kuwa Airtel imeamua kuinua taifa letu kufikia lengo la kuishi kidigitali kwa kuwepo na huduma za kidigitali, aliongeza Madale.

Hospitali ya Misheni Rulenge yaomba msaada kuokoa maisha ya majeruhi


Ngara. Majeruhi 43 wa bomu lililolipuka katika Shule ya Msingi Kihinga wilayani Ngara mkoani Kagera, ambao wamelazwa katika Hospitali ya Misheni ya Rulenge baadhi wanahitaji kuongezewa damu ili kuokoa maisha yao.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Dk Revocatus Ndyekobora amesema kati ya majeruhi hao, wanafunzi ni 42 na mwalimu wao wa darasa wanahitaji uniti 50 za damu.
“Tayari wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Alfred Rulenge inayomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Rulenge wamechangia uniti 46 za damu kusaidia wenzao,” amesema.
Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo leo Alhamisi Novemba 9,2017 asubuhi, Dk Ndyekobora amesema timu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera imewasili Ngara kusaidiana na wenzao kuwafanyia uchunguzi na kuwatibu majeruhi hao.
“Watakaobainika kuhitaji huduma maalumu watahamishiwa hospitali zingine kulingana na taarifa ya madaktari,” amesema Dk Ndyekobora.
Mbali ya damu, majeruhi pia wanahitaji mashuka na mablanketi zaidi ya 50 kutokana na yaliyopo kutotosheleza mahitaji.
Amesema baadhi wamelazimika kulala sakafuni kutokana na vitanda kujaa.
“Msaada wa chakula pia unahitajika kwa ajili ya majeruhi hawa ambao wametoka maeneo ya mbali kiasi cha kutowezesha wazazi, ndugu, jamaa na marafiki kuwaletea chakula,” amesema Dk Ndyekobora.
Usafiri kwa ajili ya kuwahamishia hospitali zingine pia ni miongoni mwa mahitaji ya dharura yanayohitajika kuokoa maisha ya majeruhi hao.
Amesema baadhi wamebainika kuwa na vipande vya vyuma vilivyotokana na mlipuko wa bomu uliotokea jana Jumatano Novemba 8,2017 wakati wanafunzi hao wa darasa la kwanza wakiingia darasani.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Aidan Bahama amepiga marufuku biashara ya vyuma chakavu katika maeneo ya shule akionya kuchukua hatua dhidi ya mwalimu mkuu na wakuu wa shule watakaobainika kuruhusu biashara hiyo.
Amri ya Bahama imetokana na uchunguzi wa awali wa polisi kubaini mwanafunzi mmoja aliokota bomu na kulihifadhi kwenye begi lake kwa lengo la kuliuza kama chuma chakavu.
Halmashauri kugharamia mazishi
Bahama amesema halmashauri imechukua dhamana ya kugharimia majeneza na shughuli za mazishi ya watoto watano waliokufa katika tukio hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Erick Nkilamachumu na mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Ngara, George Lubagola wameiomba Serikali kuimarisha ulinzi na ukaguzi kwa watu wanaingia nchini kutoka Burundi ili kudhibiti uingiaji holela wa silaha na mabomu ya kutupa kwa mkono.
Kijiji cha Kihinga ni miongoni mwa maeneo yanayopakana na nchi jirani za Burundi na Rwanda na kuna mwingiliano wa watu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Uongozi Ubungo Plaza wazungumzia kutimuliwa Blue Pearl


Dar es Salaam. Uongozi wa Ubungo Plaza Limited umesema mpangaji wake, hoteli ya Blue Pearl alikoma kulipa kodi ya pango tangu Mei, 2014.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 9,2017, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Ubungo Plaza, Harun Mgude amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kushinda kesi Mahakama ya Ardhi.
"Blue Pearl amekuwa mpangaji wetu tangu mwaka 2006 na mkataba wake ulikuwa wa miaka 15 ambao ungeisha 2021. Alikuwa akilipa vizuri lakini tangu Mei 2014 aliacha kulipa," amesema Mgude.
Amesema kutokana hilo walikwenda kufungua kesi Mahakama ya Ardhi na Blue Pearl wameshindwa, hivyo kutakiwa kulipa au kutoka ndani ya jengo.
"Kama mnakumbuka tuliwahi kumtoa na akarudi kwa amri ya Mahakama ili kupisha kesi kuendelea, lakini Novemba 3,2017 kesi iliisha na ameshindwa na kutakiwa kulipa deni la Sh5.7 bilioni," amesema.
Amesema uongozi wa Blue Pearl umeomba kufanya kikao Jumatatu Novemba 13,2017 ili kujadili jinsi ya kulipa deni hilo.
"Baadhi ya wateja wamehamishiwa hoteli nyingine sijui ni wapi. Ila ieleweke kuwa robo tatu ya mali zilizokuwamo Blue Pearl ni za Ubungo Plaza Limited kama vile fenicha na vitu vingine," amesema Mgude.
Uongozi wa hoteli hiyo ulikuwa ukishughulikia kuwahamisha wateja na haukuwa tayari kuzungumzia suala hilo.

Hoteli ya Blue Pearl yafungwa


Dar es Salaam. Kampuni ya Udalali ya Yono imeifunga Hotel ya Blue Pearl  kwa kudaiwa kodi na Ubungo Plaza.
Shughuli ya kufunga hotel hiyo imefanyika leo Novemba  9 asubuhi saa 12 huku wateja waliokuwa bado wamelala wakilazimika kuamshwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Scholastika Kevela amesema hotel hiyo inadaiwa kodi ya pango na Ubungo Plaza Sh.5.7 bilioni.
"Tunafunga na kukabidhi kwa mmiliki na shughuli hapa hazitaendelea tena hadi awe amelipa kodi," amesema Kevela
Mmoja wa wateja, Masoud Masoud akiwa na familia yake amesema''nimetoa hela nyingi na ilikuwa nikae kama wiki mbili na nimeingia jana, huu ni usumbufu."

Messi: Sitaki kupangwa na Hispania


Moscow, Russia. Wakati Hispania ikiwa kundi la pili katika upangaji wa ratiba ya Kombe la Dunia itakayofanyika Desemba 1, Lionel Messi amesema angependa Argentina isipangwe pamoja na Hispania.
Pamoja na kufuzu kwa shida kwa fainali hizo za 2018, Russia bado Argentina  imepangwa kundi la kwanza shukrani kwa kazi kubwa ya Messi aliyofanya katika mechi ya mwisho dhidi ya  Ecuador.
"Ningependa tusikutana na Hispania katika hatua ya makundi kwa sababu ni timu ngumu zaidi kucheza naye," aliimbia TyCSports.
Argentina kwa sasa inajiandaa kwa mechi mbili za kirafiki dhidi ya Russia na Nigeria.
Messi ametumia nafasi hiyo kuweka mambo sawa kuhusu tetesi kwamba yeye ndiye anayepanga wachezaji na makocha wa timu ya taifa.
"Wakati wanapozungumzia kuhusu marafiki wa Messi inanifanya nicheke tu," aliongeza. "Wanasema kuwa ndiye ninayechagua makocha na wachezaji wa kuchezea Argentina, huo ni uongo.
"[Javier] Mascherano, [Angel] Di Maria, [Lucas] Biglia ni wachezaji wakubwa duniani, madai hayo ni kuwavunjia heshima. Hivyo sivyo nilikuwa mimi hata kidogo.

Nyumba mbili za Lugumi zauzwa kwa mnada


Dar es Salaam. Nyumba mbili za Said Lugumi zilizoko  Mbweni JKT zimeuzwa kwa Dk Louis Shika.
Katika mnada uliofanyika leo Alhamisi Novemba 9,2017 nyumba moja imenunuliwa kwa Sh900 milioni na nyingine kwa Sh1.1 bilioni.
Nyumba hizo ambazo zina kila kitu ndani, zipo umbali wa takriban mita 100 kutoka moja hadi nyingine. Mnada umefanyika kuanzia saa 5:58 asubuhi na ulidumu kwa wastani wa dakika tano kwa kila nyumba.
Mnada huo umeendeshwa na kampuni ya udalali ya Yono ukifanyika kwa mara ya pili baada ya wa kwanza wa Septemba 7,2017 kukwama kutokana na wateja waliojitokeza kutofikia bei iliyohitajika.
Akizungumza na Mwananchi jana Jumatano Novemba 8,2017 Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Yono, Scholastica Kevela alisema lengo la mnada ni kufidia Sh14 bilioni ambazo mfanyabiashara Lugumi anadaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Nyumba hizo mbili ni kati ya tatu ambazo zitapigwa mnada. Nyingine iko Upanga,  jijini Dar es Salaam.

Magufuli apokewa na Rais Museveni Mtukula


Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameanza ziara rasmi ya kiserikali ya siku tatu nchini Uganda kwa mwaliko wa Rais Yoweri Museveni.
Dk Magufuli aliyeongozana na mkewe Janeth amewasili Mtukula mpakani mwa Tanzania na Uganda ambako amepokewa na mwenyeji wake Rais Museveni aliyeambatana na mkewe Janeth.
Katika mapokezi hayo leo Alhamisi Novemba 9,2017, Rais  Magufuli amepigiwa mizinga 21 na amekagua gwaride  lililoandaliwa kwa heshima yake.
Wakiwa mpakani, viongozi hao wawili watafungua kituo cha pamoja cha huduma za mpakani (One Stop Border Post - OSBP) kilichojengwa ili kurahisisha utaratibu wa forodha, uhamiaji na kuharakisha biashara kati ya nchini hizi mbili.
Taarifa ya Ikulu imesema baadaye leo, marais hao wataweka jiwe la msingi katika mradi wa bomba la mafuta ghafi linaloanzia Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Shughuli hiyo itafanyika katika Kijiji cha Luzinga, kilichopo mkoani Rakai nchini Uganda.
Baada ya ufunguzi, viongozi hao watazungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara utakaofanyika  wilayani Kyotera nchini Uganda.
Rais Magufuli jioni ya leo atahudhuria dhifa ya kitaifa iliyoandaliwa kwa heshima yake na Rais Museveni katika mji wa Masaka.

Mbowe amuweka kiti moto Waziri Mkuu shambulio la Lissu, walioua Geita, watekaji

Dodoma. Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amehoji tena hatua ambazo Serikali imechukua dhidi ya watu walioshambulia, kuua na kumpoteza kada wa Chadema, lakini Serikali ikajibu kuwa vyombo vya dola vinaendelea kuwasaka wahusika na kwamba uchunguzi utachukua muda mrefu kukamilika.
Mbowe, ambaye ni mbunge wa Hai, alikuwa akimuhoji Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuhusu hatua ambazo Serikali imechukua dhidi ya mauaji ya mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Alphonce Mawazo, kutoweka kwa Ben Saanane, ambaye alikuwa msaidizi wake, na tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ambaye hivi sasa amelazwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.
Siku chache baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, Mawazo alitekwa akiwa katika kikao cha ndani cha Chadema na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa chama kimoja cha siasa, kisha kupigwa kwa silaha za jadi, na kumuua kwa kumkata kichwa kwa shoka.
Saanane, ambaye alikuwa msaidizi wa Mbowe, alitoweka siku chache baada ya kuandika makala ya kisiasa kwenye mitandao ya kijamii na hadi sasa hajulikani alipo.
Lissu alishambuliwa kwa risasi zipatazo 30 Septemba 7 mwaka huu akiwa ndani ya gari iliyoegeshwa nje ya makazi yake mjini Dodoma muda mfupi baada ya kuwasili akitokea bungeni. Pamoja na washambuliaji hao kufanya kitendo hicho mchana, Jeshi la Polisi halijaeleza hadi sasa kama limeshamkamata mtu yeyote kwa kumhusisha na shambulio hilo.
"Kumekuwa na matukio mengi yanayovunja usalama, yanayovunja amani na yanayojenga chuki miongoni mwa vyama vya siasa na kuharibu utengemano wetu wa kitaifa," alisema Mbowe.
Mbowe alisema tukio la Lissu kushambuliwa kwa risasi kwa nia ya kuua limezua hofu kubwa kwa Taifa, bara Afrika na Jumuiya ya Kimataifa.
"Nina hakika taharuki hiyo, imeharibu sana sura ya Taifa, heshima tuliyokuwa nayo kamaTaifa, na hatujaona kama Serikali inachukua hatua zozote kujaribu kufanya jambo hili lisiendelee kuharibu image (taswira) yetu kama Taifa)," alisema Mbowe.
Mbowe, ambaye chama chake kinataka uchunguzi huru wa shambulio shidi ya Lissu, alitaka kujua kama Serikali inachukua hatua zozote dhidi ya matukio hayo.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu alisema matukio hayo yako kote nchini kuanzia ngazi familia na kwenye mikusanyiko na kwamba shambulio dhidi ya Lissu si tukio pekee.
"Hatupendi matukio haya yatokee, lakini pia utakumbuka wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiki tumepoteza watu wengi," alisema Waziri Mkuu huku wabunge wakishangilia kwa makofi na sehemu ya wabunge baada ya kutaja mauaji ya wilaya hizo tatu za Mkoa wa Pwani.
"Lakini pia hata siku za karibuni, kamanda wetu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) naye alipigwa risasi pia. Kwa hiyo tuyazungumze haya kwa ujumla wake. Na tunapoyazungumza haya kwa ujumla wake.
"Na kwa utamaduni ambao tumeujenga nchi hii katika kujilinda wenyewe kuhakikisha kwamba nchi inaendelea kuwa salama, nataka kuhakikishia kwamba vyombo vyetu vya dola vinaendelea kufanya uchunguzi wa haya.
"Na uchunguzi huu hauwezi kuwa wa leoleo halafu ukapata ufumbuzi kwa sababu wanaotenda matendo haya wanafanya mbinu nyingi za kujificha."

Mkurugenzi Halmashauri ya Tunduru ang’olewa



Abdallah Mussa
Abdallah Mussa 
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED) ya Wilaya ya Tunduru, Abdallah Mussa kwa kushindwa kumudu majukumu yake.
Kutenguliwa kwa uteuzi wa mkurugenzi huyo leo Alhamisi Novemba 9,2017 kumefanyika siku tatu baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa wakurugenzi wengine wawili.
Taarifa ya Rebecca Kwandu, mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini katika ofisi ya Tamisemi imesema Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mussa Iyombe ndiye aliyotoa taarifa ya kutenguliwa kwa uteuzi huo leo mjini Dodoma.
Amesema kutokana na hatua hiyo, uteuzi wa mkurugenzi mwingine utafanyika baadaye.
Rais Magufuli Novemba 6,2017 alitengua uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri za Manispaa ya Bukoba, Erasto Mfugale na wa Halmashauri ya Bukoba, Mwamtumu Dau.
Viongozi hao walishindwa kutaja kiasi cha fedha za Mfuko wa Barabara zilizopokewa kwenye halmashauri zao walipoulizwa na Rais Magufuli wakati wa uzinduzi wa Uwanja wa Ndege wa Bukoba.
Alipoitwa mbele na kutakiwa kutaja kiasi halisi cha fedha zilizopokewa katika halmashauri kwa ajili ya mfuko huo, Mwantumu alijibu kuwa ana idara nyingi anazozisimamia hivyo isingekuwa rahisi kwake kukumbuka kila kitu, hivyo ni mpaka awepo mweka hazina. Pia, alisema hawezi kusema uongo.
Dk Magufuli katika mkutano huo alisema amewasamehe lakini baadaye Ikulu ilitoa taarifa ikieleza Rais ametengua uteuzi wao.

Samia kufunga maadhimisho ya polisi wanawake


Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameudhuria maadhimisho ya miaka 10 tangu kuanzishwa mtandao wa polisi wanawake yanayofanyika katika viwanja vya Chuo cha Polisi Kurasini, Dar es Salaam.
Baada ya kuwasili katika maadhimisho hayo yanayofanyika leo Alhamisi Novemba 9,2017, Makamu wa Rais amekagua gwaride maalumu na kupokea maandamano yakiongozwa na farasi na pikipiki.
Maadhimisho yamepambwa na vikundi mbalimbali vya wanawake, vikiwemo vikosi maalumu vya kupambana na uhalifu na cha komandoo wanawake.
Samia pia atatembelea mabanda na kukagua shughuli zinazofanywa na polisi wanawake.
Miongoni mwa  mabanda yaliyopo, lipo kwa ajili ya uchangiaji damu.