Saturday, October 21

SEKTA YA VIWANDA INAHITAJI WAHANDISI WENGI


Mwenyekiti wa ALAT Taifa ambaye pia ni Mshtahiki Meya wa Shinyanga, Gulam Hafeez Mukadam wa pili kulia akipokea mifuko ya saruji 500 kutoka kwa Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Saruji ya Simba Cement Benedict Lema katikati ni Katibu Tawala Msaidizi Rasilimali watu na Utawala Mkoa wa Tanga, Radhiya Msuya ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga kulia ni Meneja Uhusiano na Mawasiliano ya Nje wa Simba Cement, Noor Mtanga.
Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Saruji ya Simba Cement Benedict Lema wa pili kushoto akimkabidhi mifuko ya saruji 500 Mwenyekiti wa ALAT Taifa ambaye pia ni Mshtahiki Meya wa Shinyanga, Gulam Hafeez Mukadam wa pili kutoka kulia kwa ajili ya ujenzi miundombinu katika sekta ya elimu katikati ni Katibu Tawala Msaidizi Rasilimali watu na Utawala Mkoa wa Tanga, Radhiya Msuya ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga kulia ni Meneja Uhusiano na Mawasiliano ya Nje wa Simba Cement, Noor Mtanga.
Sehemu ya Saruji iliyokabidhiwa leo.


IMEELEZWA kuwa sekta ya viwanda inahitaji wahandisi ambao watashiriki katika shughuli mbalimbali baada ya wale waliopo hivi sasa kustaafu kwa kuwekewa mazingira mazuri wanaochipukia katika uimarishaji wa miundombinu shuleni.

Hayo yalisemwa leo na Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Saruji cha Tanga (Tanga Cement),Benedict Lema wakati akikabidhi mifuko 500 ya Saruji kwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Shinyanga Gulam Hafeez Mukadam kwa ajili ya shule zao katika kuboresha maendeleo na ujenzi wa vyoo vya wanafunzi na maeneo mengine ya elimu na afya.

Mifuko hiyo ina zaidi ya thamani ya milioni 6 iliyotolewa Halmashauri ya Shinyanga kwa ajili ya kuweza kukabiliana na uhaba wa miundombinnu ya shule ikiwemo vyoo. Lema alisema ili kuweza kusaidia harakati za kuelekea Tanzania ya Viwanda ndio sababu kubwa wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali kuwezesha kupunguza baadhi ya changamoto zilizopo ili kuhakikisha zinakwisha.



Aidha alisema wanafunzi wanapaswa kuongeza bidii ili kuweza kufanikiwa katika masomo yao jambo ambalo litawezesha kupatikana kwa wahandisi wengi ambao watasaidia sekta ya viwanda.

Awali akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tanga ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Rasilimali watu na Utawala Mkoa wa Tanga, Radhiya Msuya aliishukuru kampuni ya Tanga Cement kwa mchango wao mkubwa wanaoutoa katika kusaidia sekta ya elimu ya vijana wetu ambao watakuwa wataalamu kwenye maeneo mbalimbali.

Alisema mchango wao huyo ni mkubwa kwa sababu unasaidia katika harakati za kuelekea Tanzania ya Viwanda kwa kuona mbali kwa kuwekeza kwenye sekta ya elimu ambayo ndio nguzo muhimu kufikia malengo hayo.

Naye kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT ) Taifa ambaye pia ni Mshtahiki Meya wa Shinyanga, Gulam Hafeez Mukadam aliishukuru kampuni hiyo kwa kuthamini harakati za kuinua elimu hapa nchini kwa kusaidia mifuko hiyo ya saruji ambayo itakuwa ni chachu kubwa kufikia malengo yao kielimu.

Alisema anawashukuru sana kwa kuunga mkono agizo la Rais kuelekeza nguvu kwenye sekta ya elimu katika kutatua changamoto za madawati na vyoo ili kusaidia harakati za elimu ambazo zinafaida. Hata hivyo alisema wataendelea kuwahimiza vijana kuhakikisha wanasoma kwa bidii ili kuweza kupatikana wahandisi wengi ambao watakuwa ni chachu kubwa baada ya waliopo kustaafu.

Odinga: Hakutakuwa na uchaguzi Kenya 26 Oktoba

Odinga: Hakutakuwa na uchaguzi Kenya 26 Oktoba

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amesisitiza kwamba muungano wake hautashiriki uchaguzi wa marudio wa urais ambao umepangiwa kufanyika Alhamisi.
Amesema kwamba haamini kwamba utakuwa huru na wa haki.
Bw Odinga aliongoza mkutano wa kisiasa Bondo, magharibi mwa Kenya Rais Kenyatta alipokuwa anaongoza maadhimisho ya sikukuu ya Mashujaa jijini Nairobi.
Ameahidi kutoa tangazo kwa wafuasi wake Jumatano.

Lupita naye amlalamikia Weinstein

Harvey Weinstein
Mcheza filamu na mshindi wa tuzo ya Oscar Lupita Nyong’o, raia wa Kenya, amejitokeza kuungana na wacheza sinema wengine kadhaa wanawake waliotoa shutuma za udhalilishaji wa kingono dhidi ya mzalishaji maarufu wa filamu wa Hollywood Harvey Weinstein.
Katika Makala iliyochapishwa kwenye majarida kadha ikiwa ni pamoja na gazeti mashuhuri la New York Times.Nyong’o anaeleza uamuzi wake wa kusimulia kisa kilichomkuta hivi sasa akiungana na sauti za wanawake wengine ambao walikuwa wamebughudhiwa na kudhalilishwa kimapenzi.
“Nilikuwa nimeweka dukuduku langu dhidi ya Harvey mbali kabisa na akili yangu, na kujiunga na wale waliokubaliana kunyamaza dhidi ya uovu huu ambao umempa nafasi mwindaji huyu wa ngono kuwadhalilisha wanawake kwa miaka mingi. Nilikuwa najihisi niko peke yangu wakati udhalilishaji huu ulipotokea, na nilijilaumu kwa yaliyotokea, kama vile ilivyokuwa kwa wanawake wengine ambao wamesimulia dukuduku lao.
Lakini kwa vile hivi sasa suala hili linazungumziwa kwa uwazi sikuweza kujizuilia na kumbukumbu zangu juu ya udhalilishaji huu zilizojitokeza. Nilijisikia ndani ya tumbo langu kuwa ninaumwa. Nilihisi vile hasira zinavyonipanda ni kitambua kuwa simulizi yangu siyo ya kipekee bali ni sehemu ya mfumo wa kitabia.”
Weinstein inadaiwa kuwa kwanza alijaribu kumlazimisha Nyong’o wawe na mahusiano wakati alipojitokeza kutathminiwa katika shindano la filamu katika makazi yake mzalishaji huyo huko Westport, Connecticut. Wakati huo Nyongo alikuwa bado ni mwanafunzi wa Sanaa ya kuigiza chuo cha Yale. Nyong’o anaelezea:
“Harvey alinipeleka chumbani- chumbani kwake- na akatangaza kuwa alikuwa anataka kunifanyia massage (kunikanda). Nilidhani kuwa alikuwa anatania hapo awali. Ilikuwa siyo hivyo. Kwa mara ya kwanza tangu nikutane naye nilijihisi siko salama. Nilishtuka kidogo na kufikiria haraka jinsi ya kumuepuka na kuweza kujihami nafsi yangu, kujua hasa sehemu gani mikono yake ilikuwa inataka kushika wakati wote huo.

Muda siyo mrefu alisema anataka kuvua suruali yake. Nilimwambia asifanye hivyo na kuwa itanifanya niwe katika hali ya taharuki… nilifungua mlango na kusimama kwenye kizingiti. Alivaa shati lake na mara nyengine alisema jinsi nilivyokuwa mjeuri. Nilikubaliana naye huku nikicheka na kujaribu kuondokana na hali hiyo kwa salama.”
Kama Nyong’o anavyoeleza, sehemu ya mafunzo yake ilikuwa ni kujifunza namna ya kukanda na mazoezi ya viungo, lakini Weinstein amedai vitendo hivyo vilionyesha kuvuka mstari. Baadae, anaeleza jinsi alivyopitia katika mchakato wa kutambua jinsi atavyoweza kulishughulikia suala hili kwa umakini zaidi—“Nilikuwa naingia katika biashara ambayo mahusiano mazuri ni sehemu ya weledi na kwa hivyo kunajichanganya sana,” amesema. Baadae ameandika juu ya tukio – akiwa katika chakula cha usiku na kundi la watu—pamoja na Weinstein ambapo alimgundua kuwa ni mtu mwenye “mashara na ucheshi.” Bila shaka alikuwa ni mdhalilishaji, lakini pia anaweza kuwa mcheshi kweli kweli, kitu ambacho kilikuwa kinachanganya na kuvutia.” Nyong’o amesema.
Lakini baada ya kukutana naye mara kadha katika shughuli za kikazi za kawaida, Nyong’o anasimulia kukutana kwao katika chakula cha usiku ambapo alijikuta yuko peke yake na Weinstein (Nyong’o anasema kuwa msaidizi wake husubiri mpaka anapofika na kuondoka). Weinstein alimtongoza kwa mafumbo:
Kabla ya chakula cha utangulizi kufika [Weinstein] alisema: Twende katika mchezo. Nina chumba changu binafsi juu ambapo tunaweza kupata sehemu ya chakula cha usiku iliyobakia.
Nilishtuka. Nilimwambia nilikuwa napendelea kula katika mgahawa. Akaniambia acha utoto wako.
Iwapo nataka kuwa muigizaji, ni lazima niwe tayari kufanya vitu kama hivi. Alisema alikuwa ametembea na Muigizaji Maarufu X na Y na angalia wamefikia wapi katika fani hii.
Nyong’o ameandika kuwa “kwa upole alikataa pendekezo hilo” na kumshangaza Weinstein—anadai kuwa Weinstein alimwambia kuwa “ hatambui fursa gani anaipoteza
Baada akiendelea kupiga hatua katika fani hii ya uigizaji, na baada ya Nyong’o kuwa nyota katika filamu inayoitwa 12 Years a Slave, ambayo alipata tuzo ya Academy, Weinstein alimfuata Nyong’o baada ya tafrija ya sherehe hiyo huko Toronto. Weinstein alimwambia Nyong’o alikuwa anaona fedheha katika nafsi yake kwa kile alichomtendea na kuahidi kuwa atamheshimu kuanzia hapo. “Lakini niliweka ahadi moyoni kwamba sitafanya kazi na Harvey Weinstein milele,” ameongeza Nyong’o.
Na hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kukutana pamoja, Nyong’o amesema haraka sana kwamba yuko mbali na mtu pekee katika sekta ya filamu ambaye ametumia madaraka yake kinyume cha sheria.

Acacia wadai hawana pesa za kuilipa Tanzania

Rais Dr Magufuli na Mwenyekiti wa Barrick Gold Profesa Thornton
Mamlaka ya juu kabisa toka kwa kurugenzi ya fedha ya Gold miner Acacia Mining Plc  imesema haina uwezo wa kuilipa Tanzania Dola za Kimarekani milioni 300 kama ilivyokubaliwa katika mazungumzo baina ya Tanzania na Barrick Gold hivi karibuni.
Shirika la habari la Reuters limeripoti Ijumaa kuwa Mkuu wa Fedha Andrew Wray amesema wakati wa uchambuzi juu ya kutatua mgogoro huo Ijumaa kuwa haitoweza kufanya malipo hayo.
Alhamisi Serikali ya Tanzania ilisema kuwa mazungumzo kati ya magwiji wa sheria na mambo ya mikataba ya madini na timu ya wataalamu wa Barick yamefikia maelewano na tayari Barrick Gold imekubali kulipa 300$m.
Vyanzo vya habari nchini Tanzania vimesema kuwa mazungumzo hayo yamechukua muda Mrefu kutokana na unyeti wake.
Lakini wachambuzi wa mambo ya uwekezaji wanasema kuwa ni mapema sana kwa Tanzania kutangaza ushindi katika mazungumzo hayo.
Wanadai kuwa kuzungumza na Barrick Gold haitoshelezi kwani kampuni ya Acacia bado ni muhimu katika kufikia makubaliano katika mgogoro huo.
Rais Magufuli alisema Alhamisi kuwa Tanzania haitofanya mazungumzo yoyote na Acacia kwani wao sio wamiliki wakubwa wa uchimbaji huo, na kuwa mazungumzo yote yatafanyika baina ya Barrick Gold na Serikali ya Tanzania.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Barrick Gold amesema mbele bado kuna matumaini makubwa na wana kazi kubwa ya kufanya na maamuzi yote yanatakiwa yapitishwe na bodi ya wakurugenzi iliyopo Uingereza ambao wanamiliki 64% ya Acacia.

Mwenyekiti huyo Profesa John L. Thornton amesema kulikuwa na kutokukubaliana kati ya Tanzania na kampuni ya Acacia kuhusu masuala ya kodi, hata hivyo wamekubali kulipa dola milioni 300 kwa ajili ya kukuza uaminifu.

Kutokana na ugumu wa suala lenyewe wamekubaliana kuunda timu ndogo ambayo itashirikisha pande zote mbili kwa ajili ya kuendelea kushughulikia masuala machache yaliyobakia.
Lakini wachambuzi wanadai kuwa Acacia bado ni muhimu kushirikishwa katika mazungumzo hayo ili kufikia ufumbuzi wa kudumu kwani wao ndiyo wanahusika na shughuli za uchimbaji nchini Tanzania.
Wakati wa kupokea ripoti hiyo Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli alisema Barrick Gold wamekubali kulipa kile kinachostahili kwenye Halmashauri.
"Naomba Barrick walipe hizo Shilingi bilioni 700 haraka kwa sababu ninataka kuzitumia"

Pia aliwahikikishia Barrick Gold kwamba Serikali ya Tanzania sasa itaanza kufanya kazi moja kwa moja na kampuni hiyo.

"Barrick your true partner and your here to stay" akimaanisha Barrick nyinyi ni wabia wa kweli na mtaendelea kuwepo kufanya biashara hapa nchini,” aliwahakikishia Rais.

Rais pia aliiagiza Kamati hiyo iliyoshughulikia mgogoro wa Barrick Gold iendelee kufanya mazungumzo na makampuni yanayochimba Almasi na Tanzanite, kwa kutumia misingi ya mazungumzo yaliyofanywa na Barrick Gold, akiiagiza kuwa “kazi hiii ianze haraka na mapema"
Dkt Magufuli amesema kuwa kampuni hizo kama zikiwa hazitaki kuingia katika mazungumzo ili kufikia muwafaka juu ya uchimbaji madini ya almasi na tanzanite basi waondoke na kuiachia nchi madini yake.

Ni rahisi kupata leseni ya biashara, itafute



Justine Kaleb
Justine Kaleb 
Leseni ya biashara ni kibali ambacho hutolewa na mamlaka husika kwa mfanyabiashara au mtoa huduma. Mwanzoni leseni za biashara zilikuwa zinatolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara pekee lakini hivi sasa halmashauri zinaruhusiwa kufanya hivyo kwa daraja fulani.
Kwa hivi sasa leseni zimegawanywa katika makundi mawili A na B. Katika kundi A kuna biashara zenye mtaji mkubwa ambapo hujumuisha leseni za uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, huduma za mawasiliano, bandari, vilabu vya usiku na uuzaji na usambazaji wa silaha na risasi.
Biashara nyingine ni usafirishaji wa mafuta mazito, bima, huduma za utalii, benki na taasisi nyingine za fedha pamoja na maduka ya kubadilishia fedha. Leseni za biashara za kundi hili hutolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).
Katika kundi B kuna biashara za migahawa na hoteli za kawaida, vyama vya ushirika, wakala wa bima, usafirishaji wa abiria, viwanda vidogo, udalali, vipuri, utaalamu au ushauri, uuzaji wa bidhaa jumla na rejareja.
Biashara za kundi B leseni zake hutolewa na halmashauri ya eneo husika ambako biashara inafanyika. Leseni hizi zinatolewa na Wizara ya viwanda na Biashara, halmashauri za mikoa na miji pamoja na wilaya chini ya Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Leseni za Biashara namba 25 ya 1972.
Gharama za leseni hizi hubadilika mara kwa mara kulingana na inavyopendekezwa na mamlaka husika. Kufanya biashara bila leseni ni kosa kisheria hivyo ni vyema kuchukua hatua za kurasmisha biashara yako kisheria.
Ili kupata leseni ya biashara muombaji anatatakiwa kuhakikisha nyaraka zote muhimu ili kuepuka usumbufu wa kurudishwa kuondoa mapungufu yaliyopo. Muombaji ni lazima ajaze fomu ya maombi ya leseni zinazopatikana Brela au ofisi za halmashauri.
Wakati wa kuirejesha itatakiwa kuambatanishwa na namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN), mkataba wa kodi ya pango kama sehemu ya biashara umepanga, cheti cha usajili wa kampuni au jina la biashara kutoka Brela, katiba ya kampuni, vitambulisho vya viongozi wa kampuni na cheti cha uthibitisho wa mlipa kodi.
Kwa muombaji wa leseni ya biashara ya huduma za kitaalamu atatakiwa pia kuambatanisha vyeti kutoka katika mamlaka husika mfano, TCRA (kwa leseni za mawasiliano), TFDA na TBS (kwa vyakula au dawa na ubora wake) au EWURA kwa uagizaji na usambazaji wa mafuta.
Pia katika masuala ya sheria, udaktari, uhandisi, urubani au unahodha ni lazima kuwa na hati ya kitaalamu (professional certificates) kuambatanishwa katika maombi ya leseni husika.
Kama nyaraka zilizoorodheshwa hapo juu zitaambatanishwa katika fomu ya maombi ya leseni, basi kuna uwezekano wa kupata leseni yako ndani ya muda mfupi ni mkubwa. Lakini ni lazima nyaraka zote ziwe kamili bila kasoro yoyote.
Kumbuka, leseni ya biashara hulipiwa kila mwaka mara moja tangu tarehe ilipotolewa mpaka ukomo wa matumizi yake.
Leseni utakayopatiwa itakuwa na taarifa zako muhimu mfano namba ya leseni, aina ya leseni, jina la mamlaka iliyotoa leseni hiyo, namba ya mlipa kodi (TIN), jina la kampuni au muombaji wa leseni na aina ya biashara.
Taarifa nyingine zitakazokuwamo ni mahali biashara itakapokuwepo, kiasi cha ada kilicholipwa na namba ya stakabadhi pamoja na tarehe ya malipo. Kutakuwa na maelezo kama leseni hiyo ni mpya au inaendelea, tarehe ya kutolewa na mwisho wa matumizi yake, sahihi ya mtoaji, jina na muhuri wa mamlaka husika.
Upatikanaji wa leseni utakunufaisha sana, kwani biashara yako itatambulika kisheria, itakusaidia wakati wa kufungua akaunti ya biashara, utaweza kukopa fedha kutoka katika taasisi mbambali za fedha, utaepukana na usumbufu wa kufungiwa biashara yako na kufikishwa kwenye vyombo vya dola kama muhujumu uchumi na utasaidia kukuza Pato la Taifa.
Ni muhimu kutambua kuwa kila leseni ni lazima itumike kwa biashara iliyoombewa na si vinginevyo. Kutozingatia hili nikosa ammbalo ukibainika unapaswa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Kwa kulitambua hilo, kila mfanyabiashara anaruhusiwa kuwa na zaidi ya leseni moja kulingana na wingi wa miradi aliyonayo. Kwa kutowekewa ukomo wa leseni unazoweza kumiliki, adhabu huwahusu wote wanaotumia lesenimoja kwa biashara zaidi ya moja iliyoombewa.
Leseni ni kinga ya biashara yako, epuka usumbufu nenda kachukue leseni yako katika mamlaka husika ili ujitendee haki wewe mwenyewe, biashara husika pamoja na wadau unaohusiana nao kufanikisha mafanikio unayoyakusudia.

460 wabainika kuugua saratani ya matiti Mara


Zaidi ya wanawake 460 kati ya 111,733 waliopimwa saratani ya matiti mkoani Mara mwaka jana na mwaka huu wamebainika kuwa na ugonjwa huo.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Francis Mwanaisi alisema mwaka jana wanawake 63,123 walipimwa saratani ya matiti na kati yao, 422, sawa na asilimia 0.7, walikutwa na ugonjwa huo.
“Kati ya Januari hadi Septemba, mwaka huu wanawake 48,610 wamepimwa na 47 kati yao, sawa na asilimia 0.7 wamegundulika kuwa na ugonjwa huo,” alisema Dk Mwanaisi.
Alifafanua kuwa uelewa mdogo wa jamii kuhusu upimaji wa afya umebainika kuwa miongoni mwa sababu za ugonjwa huo na kuwataka wananchi kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara ili kupata tiba mapema.
Hivi sasa, wanaogundulika kuwa na ugonjwa huo hupewa rufaa kwenda kutibiwa katika hospitali za rufaa za Bugando jijini Mwanza, Muhimbili na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, zote za jijini Dar es salaam.
“Kwa wale wagonjwa ambao hawajaathirika na ugonjwa sana, hospitali yetu inao uwezo wa kuwafanyia upasuaji na tayari tumefanikiwa kuwafanyia upasuaji wanawake wanne kati ya Januari hadi Septemba mwaka huu,” alisema Dk Mwanaisi.
Mkazi wa Manispaa ya Musoma, Felix Kalisa aliiomba Serikali kuboresha huduma na tiba ya saratani katika ngazi ya wilaya na mikoa ili kutoa fursa kwa wananchi wengi kufikiwa badala ya huduma hiyo kutolewa ngazi ya hospitali za rufaa.

Radi, moto na maji vyaua watu sita


Watu sita wamefariki dunia katika matukio tofauti likiwamo la mtoto Charles Samson (14), mkazi wa Kijiji cha Iseni wilayani Sengerema kupigwa radi.
Tukio hilo la mtoto Samson kupigwa na radi lilitokea juzi saa tano asubuhi wakati akiwa na wenzake 12 walipokuwa wakijisomea kujiandaa na masomo ya kidato cha kwanza mwakani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema mtoto Claud Mussa alijeruhiwa katika tukio hilo huku wenzao wakitoka salama licha ya kupata mshtuko wa kawaida.
Katika tukio lingine lililotokea wilayani Kwimba, moto ambao chanzo chake hakijajulikana uliteketeza nyumba ya Kaleb Swema iliyoko Mtaa wa Ngumo na kusababisha vifo vya watu wawili na kumjeruhi mmoja.
Waliofariki dunia ni Jackline Machumu (38) na mwanaye Juliana David (4), huku mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Jesca akijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Wakati huohuo, mtu mmoja ambaye jina lake halijajulikana amefariki dunia na wengine watatu kunusurika baada ya mtumbwi waliokuwa wakitumia kuvua samaki ndani ya Ziwa Victoria kupinduka kutokana na kupigwa na upepo mkali.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake juzi kuwa tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Nyamagaro.
Huko Igunga mkoani Tabora, wanafunzi wawili wa Shule ya Awali ya Ncheli wamefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye kisima cha maji walipokuwa wakirejea nyumbani kutoka shule.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa alisema kuwa tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Ncheli saa tano asubuhi ya Oktoba 17 na kuwataja marehemu kuwa ni Mwashi Yohana (6) na Wande Shija (6).
“Mwenzao, Kwimba Sanongo (6), waliyekuwa wameongozana alipoona wenzake wamezama kisimani alikimbia kurejea shuleni kutoa taarifa kwa walimu ambao hata hivyo walipofika na kuwaopoa walikuta tayari wamefariki dunia,” alisema Kamanda Mutafungwa.

Ufaulu darasa la saba wapanda


Dar es Salaam. Kiwango cha ufaulu katika mtihani wa darasa la saba kimeendelea kupanda kwa miaka mitatu mfululizo.
Ufaulu umepanda kwa zaidi ya asilimia mbili, mwaka 2015 ukiwa asilimia 67.84, mwaka 2016 (asilimia 70.36) na mwaka 2017 (asilimia 72.76).
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa jana na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), wanafunzi 662,035 kati ya 909,950 waliofanya mtihani wa darasa la saba, wamefaulu.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana, katibu mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema watahiniwa waliofaulu wamepata alama 100 au zaidi kati ya alama 250 wanazopaswa kupata.
Msonde alisema idadi hiyo ya waliofaulu ni sawa na asilimia 72.76. Alisema kati yao wasichana ni 341,020 ambao ni sawa na asilimia 70.93 na wavulana ni 321,015 (asilimia 74.80).
Dk Msonde alisema mwaka 2016 waliofaulu walikuwa asilimia 70.36, hivyo kuna ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.40.
Akizungumzia takwimu za matokeo, Dk Msonde alisema ufaulu katika masomo ya Kiswahili, Kiingereza na Hisabati umepanda kwa asilimia kati ya 4.25 na asilimia 10.05 ikilinganishwa na mwaka 2016.
“Kwa masomo ya Sayansi na Maarifa ya Jamii, ufaulu umeshuka kwa asilimia kati ya 3.56 na asilimia 13.97 ikilinganishwa na mwaka 2016,” alisema.
Dk Msonde alisema watahiniwa wamefaulu zaidi katika somo la Kiswahili, ambalo kiwango cha ufaulu ni asilimia 86.86, lakini kiwango cha Kiingereza ni asilimia 40.30.
Katika matokeo hayo, Msonde alizitaja shule 10 bora kitaifa kuwa ni St Peter, St Severine, Mwanga na Rweikiza zote za Mkoa wa Kagera, Alliance (Mwanza), Sir John (Tanga), Palikas (Shinyanga), Hazina na St Anne Marie (Dar es Salaam) na Martin Luther (Dodoma).
Dk Msonde alizitaja shule 10 ambazo hazikufanya vizuri kuwa ni Nyahaa, Mntamba na Ikolo zilizopo mkoani Singida, Bosha, Kishangazi na Mkulumuzi (Tanga), Ntalasha (Tabora), Kamwala (Songwe), Kibutuka (Lindi) na Kitwai A (Manyara).
Aliitaja mikoa 10 iliyoongoza kitaifa kuwa ni Dar es Salaam, Geita, Kagera, Iringa, Kilimanjaro, Njombe, Arusha, Mwanza, Katavi na Tabora.
Dk Msonde aliwataja watahiniwa 10 bora kuwa ni Hadija Azizi Ally, Naseem Kareem Said na Insiyah Kalimuddin wote kutoka shule ya Sir John.
Wengine ni Ibrahim Shaban kutoka shule ya Tusiime, Kadidi Mkama Kadidi (Paradise), Mahir Ally Mohamedy na Mbarak Faraj (Feza), Colletha Masungwa na Philimon Damas (St Achileus) na Acius Job Missingo (St Peter Claver).
Aliwataja wasichana 10 bora kitaifa kuwa ni Hadija Azizi Ally, Naseem Kareem Said, Insiyah Kalimuddin, Linah John Lameck, Saada Ahemd Omary na Khadija Salim Omary wote kutoka shule ya Sir John; Colletha Masungwa (St Achileus), Hannat Ramadhani (Dar-Ul-Muslimeen), Efrosina Geofrid (Omukaliro) na Nancy Elirehema Mejooli (Tusiime).
Wavulana 10 bora kitaifa ni Ibrahim Shaban wa Tusiime, Kadidi Mkama Kadidi (Paradise), Acius Job Missingo (St Peter Claver), Mahir Ally Mohamedy (Feza), Mbarak Faraj (Feza), Philimon Damas (St Achileus), Huruma Godfrey (Mwanga), Hamza Azael Almas (Hazina), Gobbons Roy (Fountain of Joy) na Erastus Joseph (St Peter Claver).
Dk Msonde alizitaja halmashauri 10 zilizoongoza kitaifa kuwa ni Kinondoni, Moshi, Arusha, Ilala, Mafinga Mji, Mlele, Kigamboni, Nzega Mji, Mpanda na Chato.
Katika hatua nyingine, Necta imezuia matokeo ya watahiniwa 65 waliougua au kupata matatizo na kushindwa kufanya mitihani yao yote au baadhi ya mitihani.
Wanafunzi hao wamepewa fursa ya kufanya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi mwakani.
Necta pia imefuta matokeo yote ya watahiniwa 10 waliofanya udanganyifu.

Walioshindwa uchaguzi CCM wapinga matokeo


Mwanza. Matokeo ya uchaguzi wa Wenyeviti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), yamepingwa katika wilaya nne kati ya saba za Mkoa wa Mwanza kutokana na madai ya kugubikwa na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi.
Kaimu Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Acheny Maulid alitaja wilaya ambazo matokeo yake yamewekewa pingamizi kuwa ni Magu, Nyamagana, Misungwi na Sengerema.
Aliwataja wenyeviti ambao ushindi wao unapingwa ni Zebedayo Athumani kutoka Nyamagana, Daudi Gambadu (Misungwi), Zabloni Makoye (Magu) na Agostine Makoye wa Sengerema.
“Vikao husika vitakutana kujadili na kuamua pingamizi hizo kwa mujibu wa katiba na kanuni za uchaguzi ndani ya chama,” alisema Maulid.
Uchaguzi wa wenyeviti wa wilaya wa CCM katika wilaya zote saba za Mkoa wa Mwanza ulifanyika Oktoba 5. Wenyeviti wengine waliochaguliwa ambao hawajawekewa pingamizi hadi juzi ni Peter Muyanga kutoka Kwimba, Ally Mambile (Ukerewe) na Nelson Mesha wa Ilemela.

Kizza Besigye akamatwa kwa kutishia kuua


Kabale, Uganda. Mpinzani mkuu wa Uganda na kiongozi wa Forum for Democratic Change (FDC) Dk Kizza Besigye amekamatwa.
Wengine waliokamatwa pamoja na Dk Besigye, ni mgombea urais wa FDC Patrick Amuriat na katibu wa uhamasishaji Ingrid Turinawe. Wote walikamatwa jana jioni walipokuwa katika kijiji cha Burambira, tarafa ya Bubaare, Rubanda walipokuwa njiani wakielekea wilaya ya Kabale wakitokea Rukungiri.
Kamanda wa polisi wa mkoa Denis Namuwoza amesema Besigye anasakwa Rukungiri ambako inadaiwa alitenda makossa kadhaa ya uhalifu Jumatano. “Anatafutwa Rukungiri kwa kutishia kumuua ofisa wa polisi na kuandaa mkutano haramu,” amesema Namuwoza.
Ameongeza kwamba Besigye aliamuru watu kuwarushia mawe maofisa wa polisi ambao walikwenda kutawanya wafuasi wa FDC waliokusanyika kumsikiliza Amuriat aliyekuwemo wilayani kuomba kura.
Walipoondoka kuelekea Kabale saa 11:00 jioni walikutana na kizuizi cha polisi barabarani katika eneo la Burambira, kilomita nne kutoka mjini Kabale. Amuriat aliposhuka kwenye gari ili kuzungumza na polisi alikamatwa na kuingizwa kwenye gari la polisi. Kadhalika polisi walizingira gari walilokuwa wakisafiria Besigye na Turinawe.
Wanasiasa hao bado walikuwa wanashikiliwa na polisi hadi saa 1:00 usiku wakati habari hii inaandikwa.
“Bado tunamshawishi ashuke kwenye gari ili tumpeleke Rukungiri,” amesema Namuwoza.

‘Unga’, tindikali vyawa tishio kwa vijana


Mbeya. Vijana 105 wa kuanzia miaka 15 mkoani hapa wamebainika kuathirika na matumizi ya dawa za kulevya na vinywaji vyenye viashIria vya tindikali, baada ya kupatiwa huduma ya upimaji vinasaba kwa binadamu (DNA).
Mganga mfawidhi wa hospitali ya Mbeya, Dk Gloria Mbwire alibainisha hilo jana wakati akielezea mafanikio yaliyopatikana baada ya Serikali kuendesha kampeni ya kupima afya bure kwa wananchi.
Upimaji huo ulioanza Oktoba 14 hadi 18 ulifanyika kwenye viwanja vya Ruanda Nzovwe.
“Kimsingi hali si nzuri kwa wananchi wetu, kwa siku tano tu idadi hiyo ni zaidi ya watu 100 sasa tunaomba wazazi na jamii kuweni karibu na familia zenu katika kufuatilia nyendo shuleni,” alisema Dk Mbwire.
Mganga mkuu wa Mbeya, Dk Seif Mhina alisema wakati wakiendeelea na matibabu Serikali itaangalia namna ya kuwasaidia ili waepukane na matumizi ya dawa hizo na tindikali.
Dk Mhina aliwataka wazazi kutojikita katika shughuli za kiuchumi pekee na kushindwa kusimamia malezi bora kwa familia. hali inayozalisha kizazi kisichofaa na kushindwa kufikia malengo ya uchumi wa viwanda, kwani idadi kubwa ya vijana ni kuanzia miaka 15 ambao ni tegemezi kwa taifa.

Watano Nida wafikishwa Takukuru


Dodoma/Dar. Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projest Rwegasira amewafikisha watendaji watano wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kwenye vyombo vya uchunguzi.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo alilopewa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyomtaka kuwafikisha watendaji hao kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Akizungumza na gazeti hili jana ikiwa ni siku ya mwisho ya agizo hilo, Jenerali Rwegasira alisema: “Nimepeleka huko kama nilivyotakiwa, kazi yangu ya kutekeleza maagizo hayo nimefanya.”
Wakati Rwegasira akiwafikisha katika vyombo hivyo vya uchunguzi, ameshauriwa kujiuzulu kufuatia ubadhirifu wa mabilioni ya fedha yaliyofanywa na taasisi anazozisimamia.
Taasisi hizo ambazo Jenerali Rwegasira ni ofisa masurufu ambazo ziliitwa na kamati hiyo kwa ajili ya mahojiano kufuatia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini madudu hayo ni; Polisi, Idara ya Uhamiaji na Nida.
Jenerali Rwegasira na maofisa wa idara hizo kwa siku tatu mfululizo wamekuwa katika kiti moto mbele ya PAC ambayo inapitia ripoti ya mwaka 2015/16 kwa taasisi hizo.
Ashauriwa kujiuzulu
Akichangia hoja katika kamati hiyo jana Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alimshauri Jenerali Rwegasira kuomba kuondolewa kwa kuwa uchafu huo utamharibia sifa aliyoijenga kwa miaka mingi.
Mbunge huyo alisema Jenerali Rwegasira amefanya kazi kubwa kwenye nchi tena ya kutukuka, ni vyema kukabidhi kazi yake kwa Rais kama watu wa taasisi hizo wasipojirekebisha. “Haya madudu matatu ya Nida, Polisi na Uhamiaji yanaweza kukuchafulia sifa yako kwa sababu vitu vinavyofanywa huko nje si rahisi kwa Katibu mkuu kujua.”
Naye Mbunge wa Iramba Mashariki, Allan Kiula alisema Katibu mkuu amefanya kazi iliyotukuka kuna mambo hayaendi vizuri na kwamba si yeye anayesababisha lakini baadhi ya watendaji wa chini yake ni tatizo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka alisema majibu yaliyotolewa kwenye hoja za ukaguzi wa fungu hilo ni hafifu.
“Fedha inayozungumziwa ni mabilioni yametumika vibaya na kwa uzembe, inaonyesha Polisi kumekuwa na uzembe wa hali ya juu kuna watu wamejiwekea wigo… hawa waliostaafu si ajabu wameacha mizizi ambayo ndiyo inayotufikisha hapa,” alisema.
Kwa upande wake Jenerali Rwegasira alisema wameona kuna upungufu mkubwa na katika kujibu hoja wameonekana hawakidhi kiu ya wajumbe.
“Tunakwenda kuyafanyia kazi haya na maelekezo yaliyotolewa hapa ukweli unaonekana, tutakwenda kuelezana ukweli na kutekeleza maagizo haya na tutachukua hatua kadri tulivyoona,” alisema.

Mapato finyu yaitesa halmashauri ya Siha


Siha. Mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro yameshuka kutokana na uongozi wa halmashauri hiyo kushindwa kuwalipa wenyeviti wa vijiji wanaosimamia ukusanyaji katika maeneo yao
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Frank Tarimo amesema hayo jana Ijumaa katika kikao cha baraza la madiwani.
Amesema miradi mingi katika halmashauri hiyo imekwama kutokana na ukusanyaji wa mapato ya ndani kuwa chini jambo ambalo lisipochukuliwa hatua za haraka litasababisha madhara makubwa.
Tarimo amesema  zaidi ya Sh11milioni zinadaiwa na vijiji kutokana na kufanya kazi ya kukusanya  ushuru wa aina mbalimbali  kwenye miradi  ambayo iko kwenye maeneo yao ikiwemo mageti, masoko pamoja na vituo vya mabasi.
''Wenyeviti wakishirikiana na watendaji tulikubaliana waisaidie halmashauri kukusanya ushuru katika maeneo yao na asilimia 15 watalipwa lakini halmashauri haijafanya hivyo toka Februari mwaka huu hadi sasa,'' amesema Tarimo.
Diwani wa Kata ya Karansi, Dancan Urassa amesema halmashauri kushindwa kulipa asilimia 15 ya makusanyo ya ushuru kwenye maeneo yao imesababisha halmashauri kushindwa kufikia malengo ya makusanyo kwa mwaka huu.
“Hadi sasa halmashauri imefikia asilimia  38 ya ukusanyaji wa mapato ya ndani angali tuna vyanzo vingi sana vya mapato ni vema fedha zinazodaiwa zikatolewa ili kuweza kurudisha ari ya ukusanyaji,” amesema.
Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Barnabas Mbwambo alikiri kuwepo kwa deni hilo ambapo alifafanua kuwa wameshindwa kutoa asilimia hizo kutokana na kushuka kwa mapato.
Hata hivyo  mkuu wa wilaya hiyo, Onesmo Buswelu amesema malalamiko ya madai ya asilimia 15 za vijiji alipokea na sasa yupo katika hatua za kutatua tatizo hilo ili wenyeviti hao waweze kuendelea na ukusanyaji wao  na kuimarisha hali ya mapato.

Messi aficha kidonge kwenye soksi


Barcelona, Hispania. Lionel Messi ameonekana kitia mdomoni kitu alichokificha katika soksi kabla ya kuweka rekodi mpya katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa.
Nyota huyo wa Barcelona alifunga bao lake la 100 katika mashindano yote ta Uefa akiiongoza klabu yake kushinda 3-1 dhidi ya Olympiakos kwenye Uwanja wa Nou Camp  na alionekana ameficha siri ya mafanikio yake katika soksi.
Katika dakika ya 10, kwenye Uwanja wa Nou Camp, kamera za uwanjani zilimuonyesha Messi akichukua kidoge chake kutoka katika soksi na kukitia mdomoni.
Nyota huyo wa Argentina alitafuta kabla ya kwenda kuandika rekodi yake mpya.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Hispania, Messi alikuwa akitafuta kidonge cha glukozi ili kujiongezea nguvu.
Messi alifunga bao moja na kutegeneze lingine la Lucas Digne huku mchezaji wa Olympiakos, Dimitris Nikolaou akijifunga mwenyewe na kufanya kadi nyekundu aliyopewa Gerard Pique kukosa maana usiku huo.
Kabla ya mapumziko Pique alikuwa ametolewa kwa kadi ya pili ya njano, wakati akijaribu kwenda kushambuliaji.

Mwakyembe ataka ubingwa kuogelea Afrika


Dar es Salaam. Waziri wa Habari Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe ameitaka timu ya Taifa ya kuogelea kupambana na kubakisha kombe la ubingwa wa Afrika linabaki nchini.
Waziri Mwakyembe ameyasema hayo leo Alhamisi Oktoba 19 wakati akifungua mashindano ya Afrika ya Cana ya kanda ya tatu yanayoendelea kwenye bwawa la kuogelea la Hopac jijini Dar es Salaam na kushirikisha nchi za Kenya, Uganda, Zambia, Afrika Kusini, Sudan na wenyeji Tanzania.
"Nimeambiwa nyinyi (Timu ya Tanzania) ndio mabingwa watetezi wa mashindano hayo, naamini rekodi yenu itabaki pale pale msimu huu," alisema Mwakyembe ambaye pia aliahidi kusimamia mchakato wa ujenzi wa mabwawa ya kuogelea hapa nchini.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha kuogelea Tanzania (TSA), Phillip Saliboko alisema Tanzania inawakilishwa na timu mbili, Tanzanite ambayo itakuwa na jumla ya wachezaji 30 na ya pili inajulikana kwa jina la Platinum itakuwa  na wachezaji 21.
“Maandalizi yote yamekamilika na wachezaji wamepata maandalizi Timu hizo zipo kambini hotel ya Giraffe chini ya makocha, Alexander Mwaipasi na Michel Livingstone, tuna matumaini makubwa ya kufanya vyema,” alisema Saliboko.
Mmoja wa makocha wa timu hiyo, Alexander Mwaipasi alisema kuwa wamemaliza mafunzo yao yote kwa waogeleaji hao na wanatarajia kupata ushindi mkubwa.
“Kazi ya kufundisha tumemaliza, iliyobaki sasa ni waogeleaji kufanya mambo yao kwenye bwawa, lengo ni kutetea ubingwa, tupo tayari kwa mashindano,” alisema Mwaipasi.
Alisema kuwa timu yao inaundwa na wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu na wanaamini wataonyesha uwezo wao na thamani yao ya kuwa katika timu ya Taifa.
“Nawapongeza sana wadhamini, Giraffe Hotel,  Vodacom Tanzania, Swissair, JCDecaux,  Coca Cola, Label Promotions , Print Galore na Slipway Hotel. Wametuwezesha kufanya maandalizi makubwa katika mashindano haya, hatuta waaangusha,” alisema.
Mbali ya Tanzania, mashindano hayo pia yatashirikisha waogeleaji kutoka nchi za Uganda, Zambia, Afrika Kusini,  Sudan, Kenya na wenyeji Tanzania ambayo itawakilishwa na timu mbili.
Wachezaji wanaoumda timu ya Tanzanite ni Rania Karume , Chichi Zengeni, Maia Tumiotto, Smriti Gokarn, Sonia Tumiotto, Anjani Taylor ambao wote wanatoka klabu ya DSC, huku wengine ni Natalie Abwooli Sanford (MIS), Anna Guild, Emma Imhoff (MSC), Sanne Kleinveld ( ISM Moshi),  Angelica Spence, Tara Behnsen, Tami Triller,Kayla Gouws na Amani Doggart ambao wanatoka klabu ya Taliss.
  Wachezaji wanaume ni Judah Miller, Elia Imhoff, Delvin Barick, Caleb O'Sullivan, Khaleed Ladha na Matthew Guild wanatoka klabu ya Mwanza, Chris Fitzpatrick (ISM Moshi), Marin DE Villard (DSC), Adil Bharmal, Hilal Hilal, Harry McIntosh, Dhashrrad Magesvaran (Taliss) na wanaotoka klabu ya shule ya kimataifa ya Morogoro ni   Joseph Sumari, Collins Saliboko na Dennis Mhini.
Wachezaji wanaounda klabu ya Platinum kwa upande wa wanawake ni  Shivan Bhatt, Natalia (Taliss), Charlotte Sanford,  Vanessa Dickson (MIS), Rebecca Guild, Meredith Boo (MSC), Maria Bachmann ( ISM Moshi), Kayla Temba na Maya Somaiya  ambao wote wanatoka klabu ya DSC.
Wanaounda timu ya wanaume ni Aravind Raghavendran, Mohameduwais Abdullatif (Bluefins), Abraham Kayugwa( ISM Moshi), Terry Tarimo,  Aliasgar Chakera(Taliss), Zeke Boos (MSC), Yuki Omari, Augustino Lucas (Champion Rise), Fallih Ahmed (Taliss), Carter Helsby (MSC), Ian Lukaza(ISM) na Emmanuel Stenson wa shule ya kimataifa ya Morogoro.

Zitto asema ACT si jukwaa la kuisifia Serikali


Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema chama chake siyo jukwaa sahihi la kuisifia Serikali kama wanachama wengine wanavyodhani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi, Zitto amesema wanachama wanaodhani kama chama hicho ni jukwaa la kuisifia Serikali wajitathimini au kuchukua hatua kama wenzao walivyofanya.
Zitto amesema hayo ikiwa ni siku chache tangu aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba na wenzake kumi kuhamia CCM.
“Tulimwita Mwigamba katika kikao cha chama aje kutueleza kama tunakikuka misingi ya chama lakini hakufika. Chama kinaheshimu mchango wa kila Mwana-ACT, lakini tunawashauri wanaondoka wasiwashawishi wanachama wengine kuondoka,”
“Chama kimejiridhisha kwamba bado tunaendelea kusimamia misingi ikiwamo uzalendo sanjari na kupigania haki za demokrasia,”amesema Zitto
Amesema wanafanya yote hayo wakiongozwa na utu na uadilifu.
“Chama chetu kina ahadi tano ambazo ni kupambana na rushwa na ufisadi na kamati ya uongozi imebaini kama haijatoka katika misingi yake kama wengine wanaoondoka wanavyodai,”amesema Zitto.
Amesema bado wanaendelea kupambana na umasikini na hali ya maisha kwa Watanzania wote.
“Hatujawahi hata siku moja kwenda kinyume  na misingi ya chama hiki kama watu wanavyodai.”