Friday, October 13

Mpango wa nyuklia wa Iran: Trump atarajiwa kujiondoa

Waandamanaji nje ya Ikulu ya Whitehouse wamemtaka rais Trump kuunga mkono makubaliano hayo.Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionWaandamanaji nje ya Ikulu ya Whitehouse wamemtaka rais Trump kuunga mkono makubaliano hayo.
Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kutounga mkono makubaliano ya kinyuklia na Iran Ijumaa na kuweka chini mkakati wa kukabiliana na mpango huo.
Hatua hiyo hautaiondoa Marekani katika makubaliano hayo lakini utalipatia uwezo bunge la Congress siku 60 kuamua iwapo itafanya hivyo kwa kuiwekea Iran Vikwazo.
Waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani Rex Tillerson amekuwa akijadiliana na wenzake kutoka Ulaya na China kulingana na maafisa.
Bwana Trump amekuwaa akishinikizwa nyumbani na ughaibuni kutofutilia mbali mpango huo.
Chini ya makubaliano hayo ya 2015 , Iran ilikubali kusitisha mpango wake wa kinyuklia kwa lengo la kuondolewa kwa muda baadhi ya vikwazo ilivyowekewa.
Rais Trump amekuwa mkoasoaji mkubwa wa makubaliano hayo na akaahidi kuufutilia mbali wakati wa kampeni .
Rais Trump na mwenzake wa Iran Hassan Rouhani
Image captionRais Trump ameutaja mkataba huo kuwa mbaya zaidi na kuonya kuufutilia mbali.
Bunge la Congress litamtaka rais kuthibitisha kila siku 90 kwamba Iran inatekeleza makubaliano hayo.
Rais Trump tayari amethibitisha mara mbili .
Uvumi kwamba rais Trump huenda akakataa kuthibitisha kwamba Iran inatekeleza makubaliano hayo umezua hofu miongoni mwa washirika wa Marekani pamoja na maafisa wa utawala wake.
Waziri wa Ulinzi James Mattis aliambia kikao cha bunge la Seneti mapema mwezi huu kwamba sio lengo la taifa la Marekani kusita kuunga mkono mkataba huo.
Rais Trump ameutaja mkataba huo kuwa mbaya zaidi na kuonya kuufutilia mbali.

Marekani na Israel zajiondoa katika UNESCO

Unesco headquarters, Paris (file photo)Haki miliki ya pichaAFP
Image captionMarekani yajiondoa Unesco ikilalamikia ubaguzi dhidi ya Israel
Marekani inajiondoa kutoka shirika la elimu sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO ikililaumu kwa ubaguzi dhidi ya Israel.
Wizara ya mambo ya kigeni ilisema kuwa itabuni ujumbe wa waangalizi kwenye shirika hilo lenye makao yake nchini Ufaransa kuchukua mahala pa uwakilishi wake.
Mkuu wa Unesco Irina Bokova, alisema kujiondia kwa Marekani ni hatua ya kujutia.
"Kujiondoa kwa Marekani ni pigo kwa familia ya Umoja wa Mataifa," Bi Bokova alisema.
Mwaka 2011 Marekani ilifuta bajeti yake kwa Unesco kupinga hatua yake ya kuwapa wapalestina uanachama kamili.
Rais wa Marekani Donld Trump awali amekosoa kile alichotaja kuwa ni mchango mkubwa wa Marekani kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Marekani hutoa asilimia 22 ya bajeti ya kawaida ya Umoja wa Mataifa na asilimia 28 kwa shughuli za amani za Umoja wa Mataifa.
Unesco iko katika mikakati ya kumteua kiongozi mpya huku mawaziri wa zamani wa Qatari na Ufaransa, Hamad bin Abdulaziz al-Kawari na Audrey Azoulay wakiwa sako kwa bako kuchukua mahala pa Bokova.

Mwanasoka wa zamani George Weah anaongoza kwa kura

Mwanasoka maarufu George Weah anaongozaHaki miliki ya pichaAFP
Image captionMwanasoka maarufu George Weah anaongoza
Mwanasoka wa zamani George Opong Weah anaongoza, katika matokeo ya awali ya uchaguzi mkuu wa Liberia.
Takwimu kutoka tume ya uchaguzio NEC zinaonyesha Weah yupo mbele kwa majimbo 11 katia ya majimbo 15 japo kura zote hazijahesabiwa.
Mgombea anayefuatia ni makamu wa rais Joseph Boakai,ambaye anaongoza katika jimbo moja na mengine yanayosalia ameshika nafasi ya pili.
Mshindi katika kinyang'anyiro hicho analazimika kujipatia asilimi 50 ya kura zote ili aweze kutangazwa mshindi,na kama hakuna mgombea atakayefikisha kiwango hicho,uchaguzi wa marudio unapaswa kuwa mwezi Novemba.
Atakayetangazwa mshindi anachukua nafasi ya mwanamke wa kwanza Afrika kuwa rais Bi.Ellen Johnson Sirleaf anayemaliza muda wake kwa mjibu wa katiba ya taifa hilo na ambaye pia ni mshindi Nobel.

Majeshi ya Uturuki yaendelea na operesheni Syria

Majeshi ya UturukHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionMajeshi ya Uturuk
Vikosi vya majeshi ya Uturuki vimepiga hatua katika operesheni ya kijeshi nchini Syria kutokomeza wapiganaji wa jimbo la Idlib.
Operesheni hiyo imeanza siku ya jumamosi ambapo majeshi ya Uturuk yakisaidiana na yale ya Syrian walifanikiwa kuvuka mpaka.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema hatavumilia vitendo vyovyote vya kigaid katika eneo lake.
Mgari ya Uturuki yameonekana yakisindikizwa na makundi ya wapiganaji wanaoungwa mkono na Al Qaeda katika jimbo la Idlib,huku kundi la Tahrir al-Sham likimili maeneo karibu na kambi ya majeshi ya Kikrud ambayo yanapigana dhidi ya IS.

Trump atia saini agizo la kudhoofisha Obamacare

Rais Donald Trump akisaini agizo la urais dhidi ya bima ya afya ya ObamacareHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionRais Donald Trump akisaini agizo la urais dhidi ya bima ya afya ya Obamacare
Rais wa Marekani Donald Trump ametoa agizo la urais akiruhusu mauzo ya bima za afya ambazo zinakinzana na sheria za bima ya afya ya Obamacare.
Agizo hilo linawapatia fursa wafanyibiashara wadogo wadogo pamoja na watu binafsi kununua bima za rahisi zilizo na manufaa machache.
Raia pia wanaweza kununua bima za muda mfupi ambazo zitawalinda iwapo wataugua.
Agizo hilo linajiri baada ya bunge la Congress kushindwa kuifutilia mbali sheria hiyo ya Obamacare
Rais Trump amesema kuwa ikulu ya Whitehouse imeanza mpango wa kuifutilia mbali sheria hiyo ilio na bima ya afya ya nafuu.
Alisema kuwa agizo hilo ni awamu ya kwanza ya kuwapatia mamilioni ya raia wa Marekani nafuu ya Obamacare.
Agizo hilo litawaruhusu wafanyibiashara wadogo na watu binafsi kuungana na kuanzisha miungano na kufadhili usimamizi wa bima mbadala kulingana na sheria ya majimbo yote ya Marekani.
Mpango huo mpya pia utaondoa sheria ya viwango vya kuwepo kwa bima za muda mfupi na kutafuta njia mbadala ya bima ya afya ya Obamacare.
Agizo hilo hatahivyo haliondoi sheria inayowashiikiza raia wote wa Marekani kuwa na bima ya afya la sivyo wapigwe faini ya kodi.

Kilo 6.2 za dhahabu zakutwa ndani ya Noah bandarini


Dar es Salaam. Mamlaka zinaendelea kubaini mbinu mbalimbali za utoroshaji rasilimali za nchi baada ya watu wawili walioficha kilo 6.244 za dhahabu ndani ya gari aina ya Toyota Noah, kugutukiwa bandarini jijini Dar es Salaam.
Noah hiyo ilikuwa imewapeleka watu hao wawili bandarini na walipotaka kushuka, walishtukiwa na askari, lakini dereva alikimbia huku akiliacha gari eneo la tukio.
Watu hao walikuwa wakipeleka mzigo huo unaokisiwa kuwa na thamani ya Sh500.3 milioni visiwani Zanzibar.
Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko alisema dhahabu hiyo iliyokamatwa katika eneo ambalo hutumiwa na wasafiri wanaokwenda Zanzibar ilikuwa katika miche mitano ambayo ilihifadhiwa kwenye begi.
Aliwataja watu hao kuwa ni Akifa Mohamed na Jaffer Hussein.
Kakoko alisema walipohojiwa, mmoja wao alidai kuwa nyaraka za dhahabu hiyo ziko Zanzibar, lakini uchunguzi wao umebaini hakuna nyaraka zozote.
Alisema mtuhumiwa mwingine alidai kuwa alikabidhiwa dhahabu hiyo ili aipeleke Zanzibar.
Kakoko alisema watuhumiwa wote wawili wako kituo cha Polisi cha Bandari ya Dar es Salaam na watafunguliwa shtaka la kupatikana na madini isivyo halali.
Akizungumzia walivyokamatwa, Kakoko alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 10, saa 5:20 usiku eneo la Azam Sea Link/DMI, wakati askari wa TPA na wa vyombo vya ulinzi na usalama, walipokuwa katika ukaguzi wa abiria, mizigo na magari yaliyokuwa yakiingia katika meli ya MV Azam Sea Link – I.
Alisema watu hao wawili walikuwa wa mwisho kufika eneo hilo wakiwa na gari hiyo aina ya Toyota Noah.
Alisema begi lililokuwa na dhahabu hiyo lilifichwa kwenye viti vya nyuma vya gari.
Alisema mwanzoni watuhumiwa hao walikataa kukaguliwa, lakini walipobanwa walikubali na ndipo walipoufuma mzigo huo.
Alisema gari hilo linashikiliwa na dereva anaendelea kusakwa.
“Tunaendelea kuimarisha ulinzi na usalama ili kudhibiti uhalifu kwa kufanya ukaguzi wa mizigo yote kabla ya kupakiwa melini,” alisema Kakoko.
Katika siku za karibuni Serikali katika vita yake ya kiuchumi imekuwa ikikamata watu tofauti wanaokutwa na madini na rasilimali nyingine za nchi.

Makinikia yaendelea kuitesa Acacia


Dar es Salaam. Ikitarajia kuchapisha hesabu zake za fedha kwa robo ya tatu ya mwaka, kampuni ya Acacia inaendelea kuugulia maumivu ya zuio la kutosafirisha mchanga wa madini.
Kwenye taarifa yake ya awali iliyotolewa jana kwa wadau wake na jamii kwa ujumla, kampuni hiyo imeeleza kuimarika kwa uzalishaji lakini ikabainisha kupungua kwa mapato kutokana na zuio hilo lililoanza mapema Machi.
“Mauzo yalikuwa madogo kutokana na zuio la kusafirisha makinikia yanayozalishwa kwenye migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi nchini Tanzania,” inasema taarifa hiyo fupi.
Machi, Serikali ilizuia usafirishaji wa mchanga wa madini na Rais John Magufuli akaunda kamati mbili za kuchunguza uchimbaji, usafirishaji na biashara nzima ya dhahabu ambazo zilibaini udanganyifu unaofanywa hivyo kulinyima Taifa mapato linayostahili.
Licha ya zuio hilo, Serikali ilifanya mabadiliko kwenye sheria za madini ili kuongeza usimamizi wa uzalishaji, udhibiti wa mapato na ushiriki wa Watanzania katika umiliki wa kampuni zenye vibali vya uchimbaji nchini.
Kwa robo nzima ya mwaka, kampuni hiyo inayomilikiwa na Barrick Gold Corporation kwa asilimia 63.9 imezalisha wakia 191,203 na kuuza wakia 132,787. Pamoja na takwimu hizo, changamoto za upatikanaji wa vibali na kupunguzwa kwa uzalishaji kwenye baadhi ya migodi yake kumeathiri kiasi cha dhahabu iliyopatikana.
Vibali viliathiri uzalishaji wa Mgodi wa North Mara ambao umetoa wakia 72,011 ndani ya miezi mitatu ya Julai, Agosti na Septemba wakati Mgodi wa Bulyanhulu ukizalisha wakia 50,094 kutokana na kupunguza operesheni zake.
“Uzalishaji umezidi matarajio katika Mgodi wa Buzwagi uliochangiwa na ubora dhahabu iliyopatikana. Tulizalisha wakia 69,097,” inasomeka taarifa hiyo.
Kuanzia Julai 31, mazungumzo baina ya Serikali na Barrick yanaendelea kutafuta muafaka wa zuio hilo pamoja na kuongeza faida kwa kila upande. Miongoni mwa yanayojadiliwa kwenye mazungumzo hayo ni faini ya Dola 190 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh424 trilioni) ambayo Acacia imeandikiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) ikiwa ni kodi iliyokwepwa pamoja na riba yake.
Tangu kuanza kutekelezwa kwa zuio hilo, bei ya hisa za kampuni hiyo iliyoorodheshwa Soko la Hisa London (LSE) na Dar es Salaam (DSE) imeshuka kutoka Sh12,000 mpaka Sh5,000 kila moja.

Nusu ya wabunge CCM kupigwa panga

Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey
Katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole 
Dar es Salaam. Wanachama wanaotaka kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM, sasa watalazimika kuwa wakazi wa eneo wanalotaka kuliwakilisha, sharti ambalo linaweza kuwaondoa takriban nusu ya wabunge wa sasa.
Kutokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuruhusu mtu kwenda sehemu yoyote apendayo, imekuwa rahisi kwa mtu kuishi mji kama Dar es Salaam na kugombea ubunge wa jimbo lililoko katika mkoa mwingine.
Na uhuru huo umewawezesha watu kama Augustine Mrema, ambaye ni mwenyekiti wa chama cha TLP, kuwa mbunge wa Moshi Vijijini kwa tiketi ya CCM, Temeke (NCCR-Mageuzi) na Vunjo (TLP).
Na ni kutokana na uhuru huo, wabunge wengi wa vyama tofauti, wanaishi Dar es Salaam na kuwakilisha majimbo ya maeneo ya asili yao.
Hata wafanyakazi kutoka serikalini, hasa wakuu wa mikoa na wilaya na sehemu nyingine, huchukua likizo wakati wa uteuzi wa wagombea na kwenda maeneo yao asilia au waliyokulia kuomba wapitishwe na wasipopitishwa hurejea makazini.
Lakini masharti mapya ya CCM yanazuia mwanachama kugombea ubunge, udiwani au nafasi nyingine yoyote bila ya kuwa mkazi wa eneo hilo.
“Shika maneno yangu, mwaka 2020 wagombea ubunge watakuwa ni wale ambao wanatoka kwenye maeneo husika, wanaojua na kushughulika na shida za wananchi,” alisema katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole katika mahojiano na kituo cha redio cha Times FM jana.
Alisema hatua hiyo imetokana na chama hicho kujitathmini na kujisahihisha baada ya kugundua watu wanataka viongozi wanaotoka miongoni mwao ambao wanajua kero zao na hivyo wataweza kuzishughulikia.
Polepole, ambaye alipata umaarufu wakati wa Bunge la Katiba akitaka litumie rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi, alisema wanachama watakaokuwa wakazi wa maeneo tofauti na wanayotaka kuyaongoza, hawataruhusiwa.
Akihojiwa katika kipindi cha Maisha Mseto, Polepole alisema ili mwanaCCM awe na sifa za kugombea, ni lazima awe mkazi wa eneo husika.
Polepole, ambaye alikuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, alisema suala hilo lilikuwa sehemu ya maoni ya wananchi wakati wa mchakato wa Katiba Mpya.
Alisema msisitizo mkubwa uliopo ni cheo kimoja kwa mtu mmoja jambo linalofundisha kuwa watu wenye kiasi.
“Haya mambo ndiyo watu wanayoyataka. Rais (John) Magufuli alienda mbele zaidi kwamba utagombea nafasi ya uongozi kwenye eneo ambalo wewe ni mkazi vinginevyo, marufuku kugombea,” alisema Polepole.
“Mwaka 2020 unakuja, si mtu upo zako Times FM unapiga kazi, halafu ikifika mwishoni unaenda Ileje eti unaenda kuchukua jimbo.”
Akizungumzia uamuzi huo, katibu wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza alisema sharti hilo litakomesha tabia iliyojengeka kwa baadhi ya wanachama wa chama hicho kwenda kugombea ubunge maeneo ambayo hawajui yana matatizo gani.
“Unakuta wananchi wana shida ya maji, umeme na barabara anakuja mgombea kipindi cha uchaguzi na ahadi kemkem, kumbe yote ni kuwavutia wampigie kura na akishajihakikishia ushindi humumuoni tena,” alisema Rweikiza.
Rweikiza alisema hatua hiyo itasababisha watu wathamini kwao na kuelewa matatizo ya maeneo waliyotoka na uchaguzi utakuwa huru bila ya rushwa.
Suala la rushwa pia lilizungumzwa na Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), BensonBana ambaye aliusifia uamuzi huo.
“Huwezi kuwa mwakilishi ambaye muda wote uko Dar es Salaam unafanya biashara zako,” alisema gwiji huyo wa sayansi ya siasa.
“Kwa kuangalia dhana ya uwakilishi, ni lazima uwe ni mtu unayeishi kwenye eneo hilo, unajua matatizo yao, unajenga nao barabara na kushiriki shughuli nyingine.
“Hawa watu wanaishi Dar es Salaam na tena wana fedha hivyo wanapokwenda vijijini wanakuwa na uwezo wa kutumia fedha zao kufanya kampeni na mambo mengine tofauti na wale wanaotoka maeneo hayo.”

Kibano kingine vyama vya siasa


Dar es Salaam. Rasimu ya Sheria ya Vyama vya Siasa inayotarajiwa kufanyiwa marekebisho kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao, inapendekeza kufutwa kwa mikutano ya hadhara hadi wakati wa uchaguzi pekee.
Rasimu hiyo, ambayo imetumwa kwa vyama vya siasa kwa ajili ya kutoa maoni yao, pia inapendekeza ruzuku ilipwe mara moja na kwa vyama vyote kulingana na idadi ya kura za urais katika Uchaguzi Mkuu.
Iwapo mabadiliko hayo yatapelekwa bungeni, uwezekano wa kupitishwa kuwa sheria ni mkubwa kutokana na idadi kubwa ya wabunge kutoka chama tawala (CCM) kinachoongoza Serikali ambayo itawasilisha muswada wa mabadiliko hayo.
Rasimu hiyo imekuja wakati vyama vya upinzani vikipigia kelele kutoheshimiwa kwa Katiba na sheria na kuminywa kwa demokrasia iliyofanya vishindwe kupiga siasa kwa uhuru, hasa baada ya Serikali kupiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano.
Serikali imeruhusu mikutano ya ndani ambayo pia imesababisha viongozi kadhaa kukamatwa au kuhojiwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kupanga mikakati ya uchochezi.
Na tayari vyama vya upinzani vimeshaingiwa na hofu dhidi ya mapendekezo hayo, vikisema yanalenga kufuta sheria ya mwaka 1992, kwa mujibu wa viongozi waliozungumza na Mwananchi jana na juzi.
Katika Rasimu ya Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ambayo Mwananchi imeiona, Kifungu cha 45(2) kinaeleza kuwa mikutano ya vyama haitaruhusiwa katika kipindi ambacho hakuna uchaguzi, isipokuwa itakayoitishwa na wabunge, wawakilishi na madiwani katika maeneo yao.
Kuhusu ruzuku, rasimu ya muswada huo katika Kifungu cha 59 (1) inaeleza itatolewa mara moja katika mwaka wa fedha na waziri atazingatia hali ya kiuchumi na kifedha katika wakati husika.
“Sheria inayotungwa kwa kuangalia mtu au kundi la watu ni sheria mbaya,” alisema mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alipoulizwa maoni yake kuhusu mapendekezo hayo.
“Kinachofanyika sasa kinaturudisha miaka 25 nyuma. Uhuru alioupigania Mwalimu (Julius)Nyerere upo wapi? Uhuru wa kukusanyika, uhuru wa mawazo?”
Mbatia, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) alisema nchi inaendeshwa kwa matukio na kushauri kuwa maendeleo ya nchi ni lazima yawe shirikishi.
“Ajenda ya Malengo ya Milenia ya amani, haki na uimara wa taasisi unatoweka nchini,” alisema Mbatia, ambaye ni mbunge wa Vunjo.
“Zamani, mataifa ya nje yalikuwa yanakuja kujifunza siasa hapa kwetu, lakini kwa hali inavyoendelea sasa, watakuja kujifunza kitu gani? Tunapaswa kurejea katika mchakato wa Katiba ya Jaji Warioba, Katiba imara itatuondoa hapa tulipo na kwenda mbele zaidi.”
Serikali ilitangaza kupiga marufuku mikutano ya hadhara mwaka 2016, ikisema inataka watu wajikite kufanya kazi za maendeleo na kwamba yataruhusiwa mwaka 2020 wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Tamko hilo kwanza lilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, lakini alipoulizwa bungeni alisema ilihusu jimbo lake na baadaye likatolewa na Jeshi la Polisi wakati Chadema ilipotangaza mikutano ya hadhara ya kuishtaki Serikali, kabla ya Rais John Magufuli kuweka bayana wakati wa hafla ya uzinduzi wa huduma za polisi Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Kwa wakati wote, vyama vya upinzani vimekuwa vikipinga marufuku hiyo kwa maelezo kuwa inapingana na Ibara ya 20 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano inayotoa uhuru kwa watu kukusanyika na kuitishana kwa lengo la kujadili, kufanya mkutano au kupeleka ujumbe kwa jamii au Serikali kuhusu jambo lolote ilimradi wanafanya hivyo kwa amani.
“(Muswada huu) Umehalalisha makatazo ambayo hayakuwa kwa mujibu wa sheria na hasa tamko la kuzuia mikutano ya vyama vya siasa sasa yanawekwa kwenye sheria,” alisema mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema.
“Kama chama tutakaa kupitia kifungu kwa kifungu na kutoa msimamo kuhusu rasimu ya muswada huu.
“Muswada huu umeweka vifungu vingi ambavyo siasa sasa imefanywa kuwa kosa la jinai.”
Pamoja na vyama vya siasa, hasa vya upinzani kupinga mapendekezo hayo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ameyatetea kuwa yametoka kwa wadau.
Akizungumza na Mwananchi juzi, Jaji Mutungi alisema mapendekezo yaliyomo kwenye rasimu hiyo yametoka kwa wadau, akisema ndio waliowezesha kupatikana kwa rasimu hiyo.
“Yeyote mwenye hoja afike ofisini kwangu,” alisema Jaji Mutungi.
Katika Kifungu cha 47 cha mapendekezo hayo, vyama vya siasa vinazuiwa kuajiri, kusambaza, kuunda vikundi vya ulinzi au kuwa na muundo sawa na wa Jeshi la Polisi au chombo chochote cha ulinzi na usalama cha Serikali.
Pia, vyama vinazuiwa kuratibu au kutoa mafunzo ya kijeshi na kutumia silaha.
Mapendekezo hayo pia yanalenga kuondoa utaratibu uliopo sasa wa vyama vya siasa kuwa na wanachama wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kutokana na kifungu cha 32 kuzuia vyama kufanya shughuli za kisiasa kwenye maeneo ya kazi, shule au vyuo na majengo ya Serikali.
Mapendekezo hayo yanapendekeza adhabu ya Sh3 milioni au kifungo cha miezi sita jela au adhabu zote kwa pamoja kwa yeyote atakayekiuka kifungu hicho.
Mapendekezo hayo pia yanabadilisha utaratibu wa kuwasilisha ilani za uchaguzi. Kifungu cha 31(1)(c) kinapendekeza vyama kupeleka ilani hizo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa badala ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Mrema, ambaye aliratibu kampeni za urais cha Chadema mwaka 2015, alisema mapendekezo hayo yanampa mamlaka makubwa Msajili kama ya kimahakama kwa kuwa anaweza kuagiza kupelekewa taarifa yoyote ya chama cha siasa, jambo alilosema ni la hatari.
Alikuwa akirejea Kifungu cha 36 cha rasimu hiyo kinachopendekeza kuwa kama chama cha siasa kitaitwa au kualikwa katika mafunzo ndani au nje ya nchi, ni lazima kitoe taarifa kwa Msajili siku saba kabla na kikikiuka kitakumbana na faini ya kati ya Sh1 milioni hadi Sh10 milioni au kifungo cha miezi sita gerezani au vyote kwa pamoja.
Sheria wanazotaka wao
Wakizungumza kuhusu rasimu hiyo, viongozi wa kisiasa walilaumu kuwa inalenga kuwabana.
“Tangu nchi hii ilipopata uhuru Desemba 9, 1961, sheria zinazotungwa ni zile wanazotaka wao na ndiyo maana zimekuwa na matatizo,” alisema mwenyekiti wa chama cha United Peoples’ Democratic (UPDP), Fahmi Dovutwa.
“Wao wamepanga na wanataka wanachotaka wao. Mimi nimepeleka mapendekezo, lakini sidhani kama yatafanyiwa kazi. Wanachokifanya si sawa. Huwezi kuweka sheria ngumu, huwezi kutubana tusifanye siasa.
“Sawa tutawasikiliza kwa kuwa wametaka wao. CCM wanaogopa kivuli chao na itakuja kuwagharimu siku moja. CCM isifikirie itapata kila siku na upinzani utakosa kila siku. Ipo siku CCM watang’oka na itawagharimu.”
Maoni kama hayo alikuwa nayo mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), Costantine Akitanda ambaye alisema mapendekezo hayo yana lengo la kumaliza siasa na watu kama yeye wanaweza kujiondoa kutoka katika siasa.
“Sitaki kuamini kama kuna wabunge wanaojitambua hata wa CCM ambao watakubali kupitisha mapendekezo hayo,” alisema Akitanda. “Kwa nini tunashughulika na kuweka sheria kandamizi zinazokinzana na Katiba? Tunapaswa kutengeneza sheria zinazotekelezeka. Mimi nitakuwa miongoni mwa watakaoachana na siasa kwa sheria hizi na itafika wakati mzazi akimsikia mwanae anataka kuwa mwanasiasa atamzuia kwa sheria za aina hii.
“Ngoja tusubiri tukiitwa kuijadili na hata ikienda tutaitwa Kamati ya Bunge na tutaipinga.”

Thursday, October 12

Saratani ya matiti na vifo vya wanawake duniani

Dkt Riaz Kasman
Saratani ya matiti inaelezwa kuwa ni moja ya saratani zinazoongoza kwa vifo vingi vya wanawake duniani.
Saratani ya matiti inaelezwa kuwa ni moja ya saratani zinazoongoza kwa vifo vingi vya wanawake duniani. Daktari Riaz Kasman kutoka Kenya anasema wanawake wengi hawafanyi uchunguzi wa mara kwa mara kujua kama wako salama dhidi ya saratani ya matiti.
Saratani ya matiti inaelezwa kuwa ni moja ya saratani zinazoongoza kwa vifo vingi vya wanawake duniani. Daktari kutoka Kenya anasema wanawake wengi hawafanyi uchunguzi wa mara kwa mara kujua kama wako salama dhidi ya saratani ya matiti.

Wizara ya Madini kufanya mnada wa Tanzanite Mirerani


Dar es Salaam. Wizara ya Madini kwa mara ya kwanza itafanya mnada wa madini ya Tanzanite kutoka kampuni nne za uchimbaji na biashara ya madini eneo la Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.
Kaimu Kamishna Msaidizi (Uchumi na Biashara ya Madini), Godleader Shoo amesema mnada huo utafanyika Oktoba 15.
Shoo amesema utaratibu wa kufanya mnada huo ni jitihada za Serikali za kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo nje ya nchi na pia kuwasaidia wachimbaji kuuza madini yao kwa bei ya ushindani inayoendana na soko la dunia.
Taarifa ya Wizara ya Nishati na Madini imemkariri Shoo akisema mnada huo utashirikisha wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema atakayenunua madini hayo katika mnada ni atakayeshinda bei iliyowekwa.
Amezitaja kampuni zitakazouza madini katika mnada huo kuwa ni TanzaniteOne, Franone, Glitter Germs na Classic Gems. Amesema zitauza madini ghafi na yaliyokatwa.
Shoo amesema mnada utafanyika kwa uwazi kwa kushirikisha wachimbaji, wanunuzi, Shirika la Madini la Taifa (Stamico), vikosi vya ulinzi na usalama, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro na Wizara ya Madini.
“Mnada huu utaendeshwa kwa usalama mkubwa kwa kuwa madini ya Tanzanite yana thamani kubwa. Serikali imeimarisha ulinzi ili kujihadhari na watu wasio waaminifu,” amesema Shoo.
Amesema mnada utaiwezesha Serikali kupata mrabaha stahiki na kodi kwa uwazi ili kuchangia pato la Taifa na kuimarisha ulinzi na usalama kwa wauzaji, wanunuzi na mali zao.
Shoo amesema minada kama hiyo pia hufanyika kwa nchi za Afrika zenye madini ya vito kama vile Zambia (emerald), Zimbabwe (almasi) na Afrika Kusini (almasi).