Sunday, September 10

Hasira ya Saudia baada ya mawasiliano ya simu na Qatar

Qatar AirwaysHaki miliki ya pichaAFP
Image captionNdege za Qatar zimepigwa marufuku kuruka katika anga ya mataifa jirani ya ghuba
Saudi Arabia imesitisha majadiliano ya aina yoyote na jirani yake Qatar.
Tangazo hilo la Saudia limejiri muda mfupi baada ya kinachoonekana kuwa ni mwanya katika kuafikiana kwenye jitihada za kutatua mzozo wa kati ya mataifa hayo mawili.
Zaidi ya miezi mitatu iliyopita Saudia na mataifa mengine ya ghuba yalikatiza uhusiano na Qatar --- wakiishutumu kwa kuunga mkono makundi ya wapiganaji jihadi na kuwa karibu mno na Iran.
Lakini usiku wa kuamkia Jumamosi kiongozi wa Qatar, Sheikh Tamim na mwanamfalme wa Saudia, Mohammad bin Salman waliwasiliana kwa simu ambapo walielezea hamu yao ya kufanya mazungumzo.
Hatahivyo, muda mfupi baadaye Saudia imesitisha mazungumzo ya aina yoyote ya ziada.
Walikasirishwa na namna Qatar ilivyoripoti mawasiliano hayo ya simu --- inavyoonekana ni kwasababu vyombo vya habari havikueleza kuwa upande wa Qatar ndio ulioidhinisha mawasiliano hayo.

Nato: Dunia yote inastahili kuichukulia hatua Korea Kaskazini

North Korean leader Kim Jong-un, centre, waves during a celebration, surrounded by high-ranking military officials and nuclear scientists. In the background, an orchestra and row of standing women can be seen on stageHaki miliki ya pichaKCNA
Image captionKim Jong-un alihudhuria sherehe za wanasayansi wa nyukila wa nchi hiyo baada ya jaribio la hivi majuzi
Katibu mkuu wa shirika la kujihami la nchi za magharibi Nato Jens Stoltenberg, amesema kuwa mpango wa nyuklia wa korea Kaskazini na tisho kwa dunia nzima.
Lakini hata hivyo alikaa kusema ikiwa shambulizi kwenye himaya ya Marekani ya Guam linaeza kusababisha hatua za pamoja za kijeshi.
Kipengee cha tano cha makubaliano ya Nato kinasema kuwa shambulizi dhidi ya mwanachama mmoja ni shambulizi dhidi ya wanachama wote.
Guam ambacho ni kisiwa himaya ya Marekani kilicho bahari ya Pacific ni kituo muhimu cha kijeshi na kimetishiwa mara kwa mara na Korea Kaskazini.
"Siwezi kusema ikiwa kipengee cha tano kitatumiwa wakati wa hali kama hiyo," Bw Stoltenberg alisema.
Alitoa wito wa Korea Kaskazini kuacha kuunda zana za nyuklia akisema kuwa huo ni ukiukaji mkubwa wa maazimio ya Umoja wa Mataifa,na tisho kwa amani ya dunia.
Matamshi ya Bw Stoletnberg yanakuja wakati wanachama wa baraza la ulinzi la Umoja wa Mataifa wanatofautiana kuhusu njia za kuukabili mzozo wa Korea Kaskazini kufuatia hatua yake ya hivi punde ya kufanyia jaribio kombora kupitia anga ya Japan.

Waziri mkuu wa Australia aunga mkono ndoa ya jinsia moja

Protestors gathering in central Sydney, thousands are seen with signs and rainbow flagsHaki miliki ya pichaEPA
Image captionZaidi ya watu 20,000 walikusanyika mjini Sydney kwenye kampeni kabla ya kura ya maoni isiyo rasmi ya kubadilishwa sheria za ndoa nchini Australia.
Viongozi wa siasa nchini Australia akiwemo waziri mkuu Malcolm Turnbull, wameunga mkono kampeni inayopigia debe ndoa ya jinsia moja.
Zaidi ya watu 20,000 walikusanyika mjini Sydney kwenye kampeni kabla ya kura ya maoni isiyo rasmi ya kubadilishwa sheria za ndoa nchini Australia.
Bwana Turnbull alijitokeza kwa ghafla na kutoa hotuba wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo huko New South Wales.
Kiongozi wa upinzani Bill Shorten kisha akahutubia umati kwenye mkutano mkuu.
Kura hiyo ya kubadilisha sheria ya ndoa inapigwa kwa njia ya posta kuanzia Septemba 12 na matokeo yakitarajiwa mwezi Novemba.
Image caption
Kura hiyo haitakuwa na uwezo wa kuhalalisha ndoa ya jinsia moja, lakini itachangia kura kupigwa bungeni ikiwa asilimia kubwa na watu nchini Australia wataunga mkono mabadiliko hayo.
Awali waziri mkuu alisema kuwa yeye binafsi atapiga kura kuunga mkono ndoa ya jinsia moja lakini hajafanya kampeni hadharani kabla ya hotuba ya kungashaza leo Jumapili.
Bwana Turnbull alisema kuwa nchi zingine 23 tayari zimehalalisha ndoo ya jinsia moja.

Kimbunga Irma chalipiga kwa nguvu jimbo la Florida

Kimbunga Irma chaingia jimbo la FloridaHaki miliki ya pichaAFP
Image captionKimbunga Irma chaingia jimbo la Florida
Kimbunga Irma kimepiga visiwa vilivyo kusini mwa jimbo la Florida nchini Marekani kikiwa katika kiwango cha nne, kwa mujibu wa watabiri wa hali ya hewa.
Kimbuga hicho kumepiga visiwa vilivyo nyanda za chini na upepo wa kasi ya hadi kilomita 209 kwa saa kabla ya kuelekea kaskazini magharibi kwa ghuba ya Florida.
Zaidi ya watu milioni 6.3 waliambiwa waondoke Florida, huko onyo likitolewa kuwa kubunga hicho kinaweza kuwa tisho kwa maisha.
Irma tayari kimeharibu eneo ya Caribbean ambapo takribana watu 25 wameuawa.
Viwango vya maji tayari vimeanza kuogezeka katika maeneo ya pwani ya Florida, eneo ambalo linatarajia kimbunga kikubwa kuwasili.
Taharuki na hatma ya baadaye ya mji wa Tampa, ambao unakabiliana ana kwa ana na njia inakopitia kimbunga hicho, haijulikani.
Image caption
Tampa inasemekana kuwa ni mji ulioko katika mazingira magumu zaidi nchini Marekani, hasa kuhusiana na hatari ya kugongwa mara kwa mara na vimbunga.
Pia wakuu jimbo la Florida wametangaza hali ya tahadhari ya kutotoka nje, katika baadhi ya maeneo ya jimbo hilo, ukiwemo mji wa Miami.

Wachimbaji dhahabu wahofiwa kufa mgodini




Wachimbaji wawili wa dhahabu katika mgodi wa Sekenke One kitalu namba moja wilayani Iramba wanahofiwa kufa baada ya kufukiwa na udongo.
Mgodi huo katika Kijiji cha Konkilangi kata ya Nwike tarafa Shelui mkoani  Singida.
Ajali hiyo imetokea jana Jumamosi saa 7:47 usiku mgodini humo na pia imesababisha majeruhi watano.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Isaya Mbughi amesema wachimbaji wanaohofiwa kufa ni Simon Odochi (26) maarufu kwa jina la Wamwanza mkazi wa Jiji la Mwanza.
Mwingine ni Kashinde Nkula (27), mkazi wa Kijiji cha Mangusu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Amesema juhudi za kuwaokoa zimeanza tangu usiku wa manane na kwamba hadi leo Jumapili saa 3:30 asubuhi wachimbaji hao walikuwa bado hawajapatikana.
Kaimu Kamanda Mbughi amesema ajali hiyo pia imesababisha majeruhi ambao ni Ayubu Msengi (34), mkazi wa Ntwike; Mwita Salumu (42) wa Gumanga; Lazaro Edward (28) wa Kiomboi Soweto; Jeremi Idd (41) wa Kijiji cha Gumanga na Jumanne Said (24) wa Kijiji cha Mgongo.
Majeruhi hao watano amesema waliokolewa na wenzao na chanzo cha ajali hiyo ni kutitia kwa udongo.

Rais Magufuli ateua Jaji Mkuu


Rais John Magufuli amemteua Profesa Ibrahim Juma kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu imesema uteuzi huo unaanza leo Jumapili.
Kabla ya uteuzi huo, Profesa Juma alikuwa akikaimu nafasi hiyo tangu Januari alipostaafu Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman.
Ikulu imesema Jaji Mkuu ataapishwa kesho Jumatatu saa nne asubuhi, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Magufuli Januari 17 alimteua Profesa Juma kuwa Kaimu Jaji Mkuu.
Kabla ya kuteuliwa katika nafasi hiyo, Profesa Juma alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa.
Jaji Mkuu mstaafu Chande hadi kufikia Januari Mosi alikuwa ameshafikisha miaka 65 ambayo ni ya kustaafu majaji wa Mahakama ya Rufani kama ilivyobainishwa katika Ibara ya 120 ya Katiba ya mwaka 1977.
Jaji Chande aliteuliwa katika nafasi hiyo na Rais mstaafu Jakaya Kikwete mwaka 2010 akichukua nafasi ya Jaji mstaafu Augustino Ramadhani.


Maswali tata shambulio la Lissu




Wakati hali ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ikiwa bado haijatengemaa, yameibuka maswali kadhaa kuhusu shambulio dhidi yake lililotokea Alhamisi iliyopita mjini Dodoma.
Watu wasiojulikana walimshambulia rais huyo wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) kwa risasi zipatazo 32 akiwa ndani ya gari lake baada ya kuwasili katika makazi yake eneo la Area D, na ni risasi tano zilizompata na kumjeruhi vibaya.
Lissu, ambaye ameibukia kuwa mwanasiasa aasiyeogopa kusema analoamini, amelazwa Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi ambako amewekwa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu.
Taarifa zilizopatikana jana zinasema mbunge huyo, bado anaangaliwa kwa karibu na madaktari.
Habari za shambulio dhidi yake zilitapakaa kwa kasi Ijumaa mchana, na juzi watu walikuwa wakitoa salamu za pole na kumuombea arudi katika hali yake, lakini jana kukaibuka maswali.
Gazeti hili limeyachambua maswali machache kati ya mengi ambayo yamejitokeza katika mijadala mbalimbali.
Miongoni mwa maswali hayo ni kwa nini Jeshi la Polisi halikuchukua hatua baada ya Lissu kutangaza kuwa kuna watu wanamfuatilia kwa muda mrefu.
Agosti 18, Lissu aliwaambia waandishi wa habari kuwa anafuatiliwa na watu anaowashuku kuwa ni maofisa usalama kwa takriban wiki tatu mfululizo.
Lissu alikwenda mbali zaidi kwa kumtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro pamoja na mkurugenzi wa idara ya usalama wa Taifa (TISS) kuwaeleza wakubwa wao kuhusu watu hao kwamba wapambane na wahalifu badala ya kutumia rasilimali za nchi kufuatilia raia wasio na hatia.
Hata hivyo, juzi IGP Sirro aliwaambia waandishi wa habari mjini Dopdoma kuwa Lissu, ambaye amekuwa akikamatwa mara kwa mara na polisi kutokana na kauli anazotoa katika mikutano na waandishi wa habari, hakutoa taarifa hizo katika kituo chochote cha polisi.
“Hili ni swali ambalo lingefaa zaidi aulizwe yeye. Hivyo tunaomba apone halafu mumuulize kama alitoa taarifa kituo chochote cha polisi,” alisema Sirro.
Swali hapo ni, kama iliwezekana kumkamata kutokana na anachokisema kwenye vyombo vya habari, ilishindikana vipi kufuatilia madai anayoyatoa katika mikutano hiyo?
Hata hivyo, mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Patrobas Katambi amesema jana kuwa walishamuandikia IGP Sirro kuhusu tishio dhidi ya Lissu na hajawajibu.
Jibu hilo la IGP Sirro limeibua swali jingine; kwa nini Lissu hakutoa taarifa hizo polisi?
Swali jingine ni kitendo cha polisi kutochukua hatua za haraka kuhoji wahusika wa karibu na tukio. Jana, polisi ilitangaza kuwa inamsaka dereva wa Lissu ambaye tangu wakati wa tukio alikuwa akionekana na viongozi wa Chadema na alikuwepo Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.
Ilikuwaje, polisi walishindwa kumchukulia kama ni mtu muhimu kumuhoji mara baada ya tukio badala ya kusubiri hadi siku tatu baadaye?
Swali jingine ni mazingira ya tukio hilo. Dereva wa Lissu alieleza kwamba kuna gari jeupe lilikuwa linawafuatilia kutoka bungeni mpaka nyumbani kwa Lissu, eneo ambalo wanakaa wabunge na mawaziri.
Kwa maelezo yake ni kwamba yeye ndiye aliyemzuia Lissu asishuke ndani ya gari na kumtaka alaze kiti wakati risasi zikipigwa kwenye gari lao.
Watu hao walikuwa wakimfuata kila siku hadi nyumbani? Na kama siku hiyo pekee walimfuata hadi anaanza kuelekea nyumbani, dereva hakuona hali ni tofauti na kuamua kupeleka gari sehemu salama au kutumia mbinu ambayo ingemthibitishia kuwepo kwa nia ovu?
Kingine kinachozua utata ni kufuatiliwa kwa gari la Lissu tangu bungeni. Hii ina maana kuwa watu hao wenye nia mbaya walikuwepo kwa muda mrefu kwenye viunga au eneo la jirani na Bunge wakimsubiri waliyemtaka.
Je, askari wanaolinda hapo na madereva wengine wa wabunge hawakuliona na kulitilia shaka gari hilo kwa siku zote kama Spika Job Ndugai alivyolieleza Bunge kuwa maeneo ya chombo hicho yako salama?
Swali jingine ni kuhusu hali ya usalama katika eneo la makazi ya wabunge na mawaziri. Je, viongozi hao wako salama? Kama washambuliaji walimudu kufyatua risasi takriban 32 na kufanikiwa kuondoka, bado wabunge na mawaziri wako salama?
Eneo wanalokaa vigogo hao lina ulinzi na wafanyakazi wa ndani. Wote hao hawakuona tukio hilo.
Kama kuna ulinzi au walinzi, walifanya juhudi gani kusaidia kudhibiti washambuliaji au kutoa taarifa ambazo zingewezesha polisi kuwabana mapema?
Hata hivyo, Jeshi la Polisi jana lilisema linawahoji baadhi ya majirani kuhusu tukio hilo.
Spika Ndugai alisema watu hao walifyatua risasi kati ya 28 na 32, kwa nini walitumia idadi hiyo kubwa kumshambulia mtu asiye na silaha?
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema shambulio hilo ni la kisiasa kwa kuwa Lissu hana adui nje ya siasa.
Hao maadui ndani ya siasa ni nani? Ni wanasiasa wa chama kingine au walio ndani ya Chadema? Ni maadui katika ngazi gani ya kisiasa ambayo inaweza kufikia kiwango cha kutaka kumuua mpinzani?
Katika hatua nyingine, taarifa zilizopatikana jana jioni kabla ya kwenda mitamboni zilisema Lissu alikuwa bado kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu wa madaktari katika hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi.
Hakuna kiongozi wa Chadema wala ndugu aliyekuwa tayari au kupatikana kuzungumzia maendeleo ya hali yake.
Lissu, mwanasheria wa kujitegemea na mwanaharakati wa haki za binadamu na mazingira, amejipatia umaarufu zaidi katika miaka ya karibuni, hasa kutokana na misimamo yake mikali na matukio ya kukamatwa kila mara na polisi na wakati mwingine kufunguiliwa mashtaka, hasa ya uchochezi.

Gwajima alaani Lissu kupigwa risasi




Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema hatasita kukemea uhalifu nchini likiwemo tukio la kupigwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Gwajima amesema hayo leo Jumapili wakati wa ibada maalumu ya kumuombea Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi Alhamisi wiki hii nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na watu ambao hawajajulikana.
Lissu hivi sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan iliyopo mjini Nairobi, Kenya.
"Naomba tusimame kidogo nizungumze jambo, nimesema leo nitakuwa na ibada maalumu ya kumuombea Lissu. Somo langu la leo linasema damu isiyo na hatia," amesema akizungumza na waumini.
Gwajima amesema kama kiongozi wa dini hatasita kukemea tukio lililomfika Lissu na kwamba, anashangaa viongozi wenzake wa dini kukaa kimya.
Amesema neno la Mungu linasema atakayemwaga damu ya mwanadamu mwenzake naye damu yake itamwagika vivyo hivyo.
“Damu inayomwagika chini ya ardhi ina sauti, inamlilia Mungu," amesema.
Awali, wanakwaya wa kanisa hilo waliimba wimbo maalumu wa kumuombea Lissu wakihamasisha Taifa lote kufanya hivyo.
"Amani ya Tanzania inapotea, wasione tuko kimya... kwa nini haya yanatokea na watu wasiyojulikana... Watanzania wote tumuombee Lissu," haya ni baadhi ya maneno katika wimbo huo.

Askofu mkuu KKKT atoa tamko Lissu kupigwa risasi




Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT), Askofu Dk Fredrick Shoo amewataka watu waovu watambue kumuondoa Tundu Lissu mmoja kutazalisha Lissu wengine maelfu.
Kauli ya Askofu Shoo inatokana na kuchukizwa na jaribio lililoshindwa la kumuua Lissu Alhamisi iliyopita mjini Dodoma, ambapo watu waliokuwa na silaha walishambulia gari lake kwa risasi 32.
Katika shambulizi hilo, kati ya risasi hizo 32 zilizofyatuliwa, risasi tano zilimpata Lissu maeneo mbalimbali ya mwili wake, na sasa anatibiwa katika hospitali ya Aghakhan ya Jijini Nairobi,Kenya.

Akizungumza  kutoka Bonn Ujerumani leo , Askofu Shoo ametoa  wito maalum kwa Serikali ya Rais John Magufuli, kuhakikisha wote waliohusika na unyama huo wanakamatwa.
“Nimeshtushwa na kusikitishwa sana na taarifa za kupigwa risasi Mheshimiwa Tundu Lisu. Watanzania tunapaswa kukataa na kulaani kwa nguvu zote vitendo kama hivi,”amesema na kuongeza;-
“Mimi ninaamini kuwa nguvu zile zile za uovu zilizokuwepo tangu awamu zilizotangulia ndizo zinazoendeleza unyama kama huu. Ninamwomba Mungu ampe (Lissu) uponyaji wa haraka”.
“Tundu Lissu amekuwa mstari wa mbele kufunua ufisadi unaoendeshwa na wababe wachache. Hawa wanaona sasa wameanza kutikiswa, na kwa kuwa kwao wingi wa mali na pesa ndio mungu wao”
“Hatushangai wakitumia kila njia kuzuia  ufisadi wao usianikwe hadharani. Watajaribu kila njia kuzuia ukweli  lakini wanasahau kuwa ukweli hauzuiliki milele kuna siku utajitokeza tu”.
“Kumwondoa Lissu mmoja kutazalisha Lissu maelfu. Wito wangu kwa serikali ya Dr Magufuli ni huu,  kwamba watu wote waliohusika wasakwe na wafikishwe mbele ya sheria,”.
Dk Shoo ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya KKKT amesema Serikali yoyote makini inajua namna ya kuulinda upinzani kwani ukitumika vizuri unakuwa kioo cha serikali cha kujitazama.
Mara kadhaa, kiongozi huyo amekuwa akitoa hotuba zenye hisia kali akitaka Serikali na vyombo vyake vya usalama kuchukua hatua, kutokana na kuongezeka kwa matukio ya ajabu ya kihalifu.

UVCCM: Lissu si wa kwanza kupigwa risasi




Uongozi wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umesema mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu si kiongozi wa kwanza kupigwa risasi, hivyo vyombo vya dola viachwe vifanye upelelezi.
Lissu alishambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi tano Alhamisi wiki hii nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na sasa anaendelea na matibabu jijini Nairobi, Kenya.
Kaimu Katibu Mkuu wa umoja huo, Shaka Hamdu Shaka amesema hayo leo Jumapili, akilitaka Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) lisione kwamba wao ndio wameguswa na tukio la Lissu kupigwa risasi kuliko Watanzania wengine.
“Ukweli ni kwamba sote tumeguswa na tukio hilo, jambo la msingi ni kuviachia vyombo vya Dola vifanye upelelezi,” amesema.
Shaka amesema kuna viongozi wengine walikufa kwa kupigwa risasi na uchunguzi ukafanyika kupitia vyombo vya ulinzi na usalama.
Kauli ya UVCCM imetolewa baada ya Bavicha kukaririwa ikiitaka Serikali kuunda tume huru itakayochunguza matukio ya uvunjifu wa amani likiwemo la kupigwa risasi Lissu.
Bavicha imesema tume hiyo inapaswa kuihusisha Chadema kwa kuwa viongozi wake wengi wamekumbwa na vitendo hivyo. Shaka amesema Bavicha iache kuingilia utaratibu wa upelelezi.
Amesema Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume aliuawa kwa kupigwa risasi.
Kiongozi mwingine aliyeuawa kwa risasi amesema ni naibu waziri katika Serikali ya Awamu ya Pili, Nicas Mahinda.
Katika duru za kimataifa, Shaka alitoa mfano wa aliyekuwa Rais wa Marekani, John F. Kennedy na Rais wa Misri, Anuar Saadat  ambao waliuawa kwa kupigwa risasi.
“Matukio ya ujambazi yanayofanywa na watu wasiojulikana hutokea hata katika mataifa makubwa na mara nyingi upelelezi wake huchukua muda mrefu kwa wahusika kukamatwa,” amesema.
Amesema Bavicha waache kuyahusisha matukio makubwa yanayochukua uhai wa watu na masuala ya kisiasa.
Shaka amesema UVCCM inamuunga mkono Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliposema huu si wakati wa kunyoosheana vidole vya lawama bali viachiwe vyombo vya usalama vitimize wajibu wake.
“Mbowe ametamka matamshi yaliyopevuka kifikra, kiupeo na kisiasa,” amesema Shaka.
Amsema Bavicha wasitumie tukio la Lissu kupigwa risasi kama jukwaa lao la kufanya siasa.
Shaka amesema umoja huo unashauri wananchi wakaongozwa kwa busara kuliko ushabiki ambao unaweza kuliingiza Taifa katika machafuko.

Mdogo wake Lissu azungumza kanisani kwa Gwajima


Mdogo wake Tundu Lissu, Vicent Lissu akiwa na
Mdogo wake Tundu Lissu, Vicent Lissu akiwa na Mbunge wa Ubungo Saed Kubenea walipohudhuria Ibada katika kanisa la ufufuo na uzima. 
Vincent, mdogo wake Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amesema kabla ya kaka yake kushambuliwa kwa kupigwa risasi aliwaeleza kwamba kuna mtu anafuatilia gari lake.
Akizungumza wakati wa ibada ya kumwombea Lissu iliyofanyika katika Kanisa la Ufufuo na Uzima leo Jumapili, amesema alimwona kaka yake akiwa amelala kitandani hospitalini mwili ukiwa na damu.
Amesema alipoamka leo asubuhi alielezwa na mtu kuwa kuna ibada maalumu ya kumwombea Lissu, hivyo akaamua kuhudhuria katika kanisa hilo la Mchungaji Josephat Gwajima.
Vincent amesema baada ya kaka yake kushambuliwa Alhamisi wiki hii, alienda Dodoma na kwamba anawashukuru madaktari waliofanya kila waliloweza kuokoa maisha ya ndugu yake.
Amesema kaka yake ni mpenda haki tangu akiwa mdogo na ameomba wananchi wazidi kumuombea.
Lissu hivi sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Aga Khan jijini Nairobi nchini Kenya.
Katika shambulio lililofanywa na watu wasiofahamika nyumbani kwa Lissu Area D mjini Dodoma, mbunge huyo alipigwa risasi tano.


Friday, September 8

Kimbunga Irma chasababisha uharibifu mkubwa Caribbean

Police patrol the area as Hurricane Irma slams across islands in the northern Caribbean on Wednesday, in San Juan, Puerto Rico, 6 SeptemberHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionKimbunga Irma kimesababisha uharibifu mkubwa huko Caribbean
Kimbunga kikali kwa jina Irma kimesababisha uharibifu mkubwa katika eneo la Caribbean ambapo takriban watu saba wameuawa.
Kisiwa kidogo cha Barbuda kilisemekana kukumbwa na uharibifu mkubwa hadi kutajwa kuwa kisichoweza kukalika huku maafisa wakionya kuwa maeneo ya kisiwa cha St Martin yanayomilikiwa na Uingereza yameharibiwa kabisa.
Jitihada za uokoaji zinatatizwa kutokana na kuwepo ugumu wa kuyafikia maeneo mengine.
Image captionKimbunga Irma kimesababisha uharibifu mkubwa huko Caribbean
Wakati huo huo upepo umetajwa kupata nguvu na kuwa vimbunga viwili.
Kimbunga Irma cha kiwango cha tano, ambacho ni kiwango cha juu zaidi kwa sasa kinapita kaskazini mwa Puerto Rico.
Zaidi ya nusu ya wakaazi wote milioni tatu wa Puerto Rico hawana umeme baaada ya kimbunga Irma kusababisha mvua kubwa na upepo mkali. Maafiasa wanasema huenda umeme ukakosa kwa siku kadhaa.
Image captionKimbunga Irma kimesababisha uharibifu mkubwa huko Caribbean
Kimbunga hicho chenye nguvu nyingi kuwai kushuhudiwa kwa miongo kadha kilikuwa na upepo wa kasi ya kilomita 295 kwa saa na kilitarajiwa kupita karibu na kwenye pwani cha Jamhuri wa Dominica leo Alhamisi
Kimbunga Irma kwanza kilikumba kisiwa cha Antigua na Barbuda. Takriban mtu mmoja aliripotiwa kuuliwa ambapo waziri mkuu Gaston Brown alisema kuwa karibu asilimia 95 ya majengo yaliharibiwa.
Image captionKimbunga Irma kimesababisha uharibifu mkubwa huko Caribbean
Hata hivyo alisema kuwa watu wote 80,000 nchini Antigua na Barbuda walinusurika maafa.
Maafisa wamethibisha vifo vya takriban watu 6 na uharibifu kwenye himaya za Ufaransa za St Martin na Saint Barthélemy.
Umeme umekatwa katika visiwa vyote na makundi ya kutoa huduma za dharura yanajaribu kufika maeneo yaliyoathirika zaidi.