Monday, August 28

Kesi ya uchaguzi Kenya yaanza kusikilizwa




Mahakama Kuu nchini Kenya imeanza kusikiliza kesi ya kupinga ushindi wa Rais wa Kenya,Uhuru Kenyata, iliyotakiwa kuanza kusikilizwa jana.
Kesi hiyo ilitakiwa kuanza jana   jioni baada ya kumalizika kwa hatua ya kwanza iliyofanyika juzi kwa pande zote tatu yaani upande wa NASA, Jubilee na Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mipaka nchini humo(IEBC) kuwasilisha mahakamani hoja zao za maandishi.
 Msajili wa Mahakama hiyo, Esther Nyaiyaki akinukuliwa na  gazeti la Kiingereza la Standard nchini humo bila kueleza mabadiliko hayo alisema itasikilizwa leo.
Kesi hiyo inatokana na uamuzi wa Muungano wa vyama vya upinzani NASA chini ya mgombea wake Raila Odinga kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 8, wakidai kuwa haukuwa wa haki na huru.
Odinga amepinga  matokeo yaliyotangazwa Agosti 11, mwaka huu na Tume hiyo yakimtambua Rais Uhuru Kenyatta wa Muungano wa Jubilee kuwa mshindi wa kiti cha urais katika ungwe ya pili akipata kura 8, 203, 290 sawa na asilimia 54.27 huku mpinzani wake mkuu, mgombea wa Muungano wa upinzani wa NASA, Raila Odinga akIpata kura milioni 6,762,224 sawa na asilimia 44.74.
Odinga hakukubaliana na matokeo hayo hadharani na aliamua kuwasilisha stakabadhi zake mahakamani hapo ikiwa ni saa nane kabla ya tarehe ya mwisho. Baadaye, Agosti 24, mwaka huu, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kwa upande wao, pia waliwasilisha stakabadhi zao kuhusiana na kesi hiyo.
Odinga ambaye alikuwa ni miongoni mwa wagombea nane wa kiti hicho cha urais, alilalamika pia kuwapo hujuma za Rais Uhuru Kenyatta kutumia mamlaka yake vibaya katika kuingilia mfumo wa tume hiyo.

ACT waiunga mkono Chadema, waazimia kwenda mahakamani


Chama cha ACT Wazalendo kitafuata nyayo za Chadema baada ya kupitisha azimio la kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga amri ya Serikali kuzuia mikutano ya hadhara na shughuli halali za vyama vya upinzani.
Azimio la ACT limefikiwa juzi katika Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia wa pili wa chama hicho.
Wajumbe wa mkutano huo wameazimia pia kumuandikia barua Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakitaka atengue amri waliyoiita batili ya kuzuia mikutano ya hadhara na shughuli halali za vyama vya siasa.
Kupitishwa kwa azimio hilo ambalo ni sehemu ya maazimio manne ya chama hicho, ni sawa na kuunga mkono harakati zilizoanzishwa na Chadema iliyowahi kufungua kesi Mahakama Kuu.
“Maazimio haya yote yatapelekwa kwenye idara husika za chama kwa ajili ya utekelezaji mara moja. Pia, viongozi wa chama wa ngazi mbalimbali wataendelea kuipigania misingi ya haki na demokrasia,” alisema Ado Shaibu ambaye ni Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT, kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa jana.
Azimio lingine la mkutano huo ni kukemea vitendo vya baadhi ya wakuu wa wilaya, watendaji wengine wa Serikali na vyombo vya dola wanaowanyanyasa na kuwakandamiza watumishi wa umma na wananchi kwa jumla, bila sababu ya msingi ikiwamo kuwaweka hovyo mahabusu. “Wajumbe wametoa rai kwa wananchi kuwapinga watawala wanaokumbatia vitendo vya kibabe dhidi ya wananchi na kwa wale watakaopuuza wito wa kuzingatia matakwa ya kisheria na kiutu katika kutekeleza wajibu wao, watengwe na jamii na wanyimwe ushirikiano,” ilisema taarifa hiyo.
Pia, wajumbe walisema kuna viashiria vinavyoonyesha kuwa mwenendo wa kiuchumi na hali ya maisha ya watu inazidi kuwa mbaya. “Wakati Serikali inajinasibu kuhusu viwanda, mauzo ya bidhaa zitokanazo na viwanda kwenda nje ya nchi yameshuka. Mwaka unaoishia Mei, 2016, Tanzania iliuza nje bidhaa za viwanda za thamani ya Dola1.5 bilioni za Marekani (Sh3.3 bilioni) lakini mwaka unaoishia Mei, 2017 Tanzania imeuza nje bidhaa za viwanda za Dola 0.8 bilioni tu,” ilisema taarifa hiyo.
ACT imesema uagizaji wa bidhaa za chakula kutoka nje umeongezeka kwa asilimia 14 ndani ya mwaka mmoja wa Mei 2016 mpaka Mei 2017 kwa Tanzania kutumia Dola 480 milioni hali inayotafsiri utegemezi zaidi nje ya nchi katika manunuzi ya bidhaa

Jamii lawamani kwa changamoto za wasioona




Watu wenye ulemavu wa macho wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo, huku wakibainisha kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni jamii kutotambua haki za kundi hilo.
Wamesema jamii pia haiwatambui, wana ukosefu wa elimu na hudharauliwa.
Msemaji wa Chama cha Wasioona Wilaya ya Kilosa, Juventin Thomas amesema licha ya  chama hicho kuanzishwa mwaka 1964, bado jamii yawasioona inakabiliwa na changamoto nyingi.
Amesema baadhi ya watu katika jamii huwadharau nakuwaona watu wasioona kama wasiofaa na wasioweza kufanya kitu chochote, hivyo kusababisha wakose haki zao zamsingi ikiwamo elimu, kupandishwa vyeo kazini, kukosa semina na mafunzo kazini.
Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Kilosa, Tumaini Geugeu amesema Serikali ya Wilaya ya Kilosa inakitambua chama cha wasioona na inajua kuwa watu hao wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinawakwamisha katika kupata haki zao muhimu.
Amesema tatizo lingine lipo kwao wenyewe kwa kuwa baadhi hawajiamini katika kila jambo hivyo kuwepo hatari katika mustakabali wamaendeleo yao.
Mwisho.

Wapigwa marufuku kusafirisha mpunga Kilombero


Serikali wilayani Kilombero imepiga marufuku usafirishaji mpunga kwenda maeneo mengine,badala yake waukoboe na kusafirisha mchele ili kuongeza thamani ya zao hilo.
Marufuku hiyo imeelezwa inalenga kuwawezesha wakulima kunufaika na kilimo cha mpunga, kujikwamua na umasikini na kukuza uchumi.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunjo amesema hayo baada ya kuzungumza na wadau wa kilimo cha mpunga wakiwemo wakulima kutoka wilaya za Mvomero,Kilombero,Ulanga na Malinyi pamoja na mashirika na taasisi zinazojihusishana kusaidia wakulima wa zao hilo.
Ihunjo amesema wilayani mwake wameweka vizuizi viwili kudhibiti wafanyabiashara wanaokaidi agizo hilo.
“Mpunga unaouzwa lazima uchakatwe ili kuongeza thamani jambo linalomfanya mkulima aweze kufaidika,”amesema.

Wilaya yahamishia wanafunzi bwenini kuongeza ufaulu



Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samwel Jeremiah

Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samwel Jeremiah 
Wazazi na walezi wenye watoto wa kidato cha pili na cha nne katika Shule ya Sekondari Ifekenya wilayani Songwe, wametakiwa kuanzia leo Agosti 28 wahakikishe watoto wao wanahamia mabwenini ili kutoa muda mzuri kwao kujiandaa na mitihani ya kitaifa itakayofanyika Novemba.
Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samwel Jeremiah ametoa agizo hilo alipozungumza na wazazi, walezi na wanafunzi wa shule hiyo baada ya ofisi yake kupeleka vitanda 12, magodoro 22, magunia mawili ya mahindi na maharage kilo 100 ili kuwawezesha wanafunzi hao kufanya vizuri katika mitihani yao.
Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Songwe, Rowllens Kabuje amesema kwa miaka mingi wilaya hiyo imekuwa ikifanya vibaya katika ufaulu wa wanafunzi kutokana na asilimia kubwa ya wazazi ambao ni jamii ya wafugaji na wachimbaji madini kutotilia mkazo elimu.
Amesema muda mwingi wanafunzi wamekuwa wakijihusisha na masuala ya kuchunga mifugo na wengine kujiingiza kwenye uchimbaji wa madini ya dhahabu, huku wakipata msukumo huo kutoka kwa wazazi na walezi wao.
Kabuje amesema, “Tunashukuru tumepata kiongozi mwenye kuthamini elimu na hata sisi wakuu wa idara tumekuwa tukiunga mkono juhudi zake.”
Kabuje amesema Halmashauri ya Songwe imeanza kugawa vifaa vya maabara katika shule nne za sekondari ili kuhakikisha wanatekeleza kaulimbiu ya ‘Ondoa ziro Songwe’.

JPM afanya ziara ofisi za Takukuru


Ulinzi umeimarishwa katikaofisi za makao makuu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zilizoko Upanga, jijini Dar es Salaam huku ikielezwa kuwa Rais John Pombe Magufuli anatembelea ofisi hiyo.
Saa 3:17 asubuhi yaleo Agosti 28, msafara wenye magari yapatayo 10 uliingia katika ofisi hiyo.
Katika kuimarisha ulinzi,barabara zinazoingia kwenye ofisi hiyo nazo zimefungwa.

Maisha ya usiku kwa waliokumbwa na bomoabomoa

Waathirika wa bomoa bomoa ya nyumba zilizopo

Waathirika wa bomoa bomoa ya nyumba zilizopo eneo la Kimara Stopover jijini Dar es Salaam wakijadiliana jambo huku wakiota moto kwa ajili ya kujikinga baridi juzi usiku, baada nyumba za eneo hilo kuvunjwa kwa ajili ya kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro.  Picha na Salim Shao 
Inasikitisha! Neno hili linatosha kueleza hali halisi ya wakazi wa Kimara Stop Over hadi Kibamba CCM ambao wanalala nje baada ya nyumba zao kukumbwa na bomoabomoa.
Kazi hiyo inatekelezwa na Wakala wa Barabara (Tanroads) kuondoa majengo yaliyo katika hifadhi ya Barabara ya Morogoro, mita 121.5 kutoka katikati ya barabara kila upande kuanzia Kimara hadi Kiluvya.
Waandishi wetu walitembelea maeneo yaliyoathiriwa juzi usiku na kukuta baadhi ya wananchi wakiwa wamelala nje wengi wao wakiwamo watoto, wazee na kina mama.
Walikuwa wamelala kwenye magofu ya nyumba zao, gizani na hatari zaidi ni kwamba sehemu za kujisaidia pia zimebomolewa.
Kutokana na hali hiyo, wapo waliotenga maeneo na kuyafanya kuwa vyoo na kutumia moto kupata mwanga na joto kutokana na baridi.
Maisha ‘mpya’
Ziara ya usiku ya waandishi wetu ilianzia Kimara Stop Over ambako waliwakuta waathirika zaidi ya 20 wakiishi kwenye vifusi vya zilizokuwa nyumba zao na mmoja alikuwa ameweka hema.
Waandishi wetu walipofika katika hema hilo, saa mbili usiku juzi, waliwakuta watu wapatao 20 wakiwa wamekusanyika katika hema huku Salma Msisi (50) akisonga ugali pembeni kidogo.
Katika hema hilo, kina baba na kina mama aliokuwa wakiota moto uliowashwa kwa kutumia kuni ambazo ni masalia ya mbao zilizokuwa katika nyumba zao pia kulikuwa na watoto watano wanaokadiriwa kuwa na miaka kati ya mitano hadi minane waliokuwa wamesinzia kwenye mikeka na magodoro.
Kutokana na giza lililokuwapo, ujio wa waandishi uliwastua baadhi yao, “Hao ni kina nani?” alihoji mmoja wao. “Sisi ni watu wema, msiwe na wasiwasi,” alijibu mmoja wa waandishi kisha ‘mwenyeji’ kuendelea, “Haya ndiyo maisha yetu, msishangae, karibuni tuote moto.”
Wakati wote wa makaribisho hayo, Mzee Nicomed Leo (61), ambaye nyumba zake nne zilizokuwa eneo moja, mbili zikiwa za ghorofa moja na nyingine za kawaida zote zimebomolewa, alikuwa ‘bize’ akichochea kuni ziwake vizuri.
Baadaye mzee huyo ambaye aliwahi kuwaeleza waandishi wetu kuwa nyumba zake zilikuwa na thamani ya Sh900 milioni alisema, “hapa ndipo maskani kwetu, tunalala hapa hadi asubuhi.”
Baada ya kusema hayo alicheka kisha akaketi baada ya moto kukolea.
Awali, alipohojiwa na gazeti hili kabla ya nyumba zake kubomolewa alisema amejiandaa kisaikolojia na kwamba atajenga kibanda juu ya magofu na ataishi hapo hadi atakapokufa kwa kuwa aliwekeza ujana wake wote katika eneo hilo lakini siku nyumba zake zilipobomolewa alizimia.
Baada ya ugali kuiva, walijigawa makundi mawili na kula kwa pamoja. Uliliwa kwa dagaa.
“Waandishi karibuni tule, mmefika wakati muafaka. Jamani sogeeni huku tupate chakula wapendwa. Waamsheni hao watoto wale kwanza,” hizo ndizo kauli za wakazi hao ambao mazingira yamewalazimu kuishi pamoja.
Katika maisha yao mapya, wakazi hao huchangishana kati ya Sh1,000 na Sh500 kulingana na uwezo wa mtu ili kununua chakula.
Wengi wao walisema wameuza mbao, matofali na mabati ili wapate fedha za kujikimu kwa wakati huu.
“Nimeuza mbao na matofali kwa bei ya hasara walau nipate fedha za kunisukuma katika kipindi hiki,” alisema Hamis Juma.
Kuhusu sehemu za faragha, Aisha Abel, mama wa makamo ambaye alikuwa mwingi wa maneno alisema, “Hatuna vyoo, tunajisaidia kama mbwa wasio na kwao. Tunajisaidia kwenye vifusi... huko kwenye magofu. Usalama wetu kiafya si mzuri maana licha ya vyoo, hatuna hata maji na tunakaa gizani.”
Wahofia ndoa zao
Baadhi ya waathirika hao walisema wamelazimika kuzisafirisha familia zao kwenda vijijini na sasa wanahofia usalama wa ndoa zao.
“Nimesafirisha familia yangu yote kwenda kijijini kwetu mkoani Mtwara, nimebaki mimi mwanaume nikitafuta namna ya kuanza maisha upya,” alisema Chande Mohamed.
“Naishi hapa sina amani, maana lolote linaweza kutokea. Mke wangu yuko kijijini na watoto, mimi nimebaki hapa peke yangu. Hivi unategemea nini hapo kama si mwanzo wa kusalitiana,” aliongeza John Patrick.
Alisema kitendo cha kukaa mbali na familia yake kinamtesa kifikra kwa kuwa alizoea kukaa nao pamoja na kulala sehemu nzuri, lakini sasa analala nje tena kwenye hema kama mkimbizi.
“Acha kabisa haya maisha... kupitia hili janga kiukweli nimejifunza mengi. Sikia kwa mwingine tu yasikukute,” alisema.
“Mimi leo wakulala nje hivi! Acha tu dada yangu, sitaki kuongea chochote inaumiza sana” aliongeza Faustine John ambaye alisema ameiombea hifadhi familia yake kwa majirani.
“Mke wangu na watoto wanalala huko mimi nikitafuta namna ya kuanza upya maisha” alisema.
Salma aliyekuwa akisonga ugali alisema, “Sina makazi. Nyumba iliyobomolewa aliniachia urithi mume wangu ambaye ametangulia mbele za haki, hapo ndipo nilikuwa nikiishi na watoto wangu.”
Alisema yeye na watoto wake ambao ni wakubwa wanalala nje na wajukuu wake wanane amewaombea hifadhi kwa majirani.
Maisha ya kaya
Baada ya mazungumzo na waathirika wanaoishi katika mahema, waandishi wetu walifika katika kaya ya Halima Ramadhani ambaye ana watoto watatu na wajukuu wanane.
Wakati huo ilikuwa saa nne usiku na walimkuta, Halima ambaye alipoteza nyumba zake mbili akiwa anaota moto huku watoto wajukuu wake wakiwa wamelala kwenye mkeka karibu na moto aliokuwa akiota wakiwa wamefunikwa vitenge na khanga.
“Siku walipokuja kubomoa mimi sikuwepo nilitoka kwenda sokoni, na hata watoto wangu ambao ni wakubwa hawakuwepo, walibaki wajukuu zangu, sasa nikiwa ninakaribia nyumbani niliona watu wamekusanyika. Nikauliza nini hicho? Mmoja wa watu waliokuwa jirani akanijibu ‘Tanroads wanabomoa....’ Mwanangu nilihisi kuishiwa nguvu nikashindwa hata nifanye nini,” alisema.
Wakati wanabomoa alisema, hakubahatika kuokoa hata kitu kimoja.
Yote tisa, kumi ni hii familia ya watu 14 ya Bernard Mbonde ambayo imepoteza makazi na eneo lao lote lenye ukubwa wa eka nne yakiwamo makaburi ya familia kuwa katika hifadhi.
Waandishi wetu walipofika katika familia hiyo iliyopo Kibamba CCM saa sita usiku, walikaribishwa na ulinzi mkali wa mbwa ambao walibweka muda wote hali iliyowalazimu wanafamilia hao kuhofia kuwa huenda wamevamiwa na wezi.
“Jamani usalama upo? Mnatafuta nini usiku huu? Alihoji mmoja wa wanafamilia hao ambaye baadaye alijitambulisha kuwa anaitwa Ibrahim Aboud aliyekuwa macho usiku huo.
Baada ya waandishi kujitambulisha, aliwakaribisha na kuwapeleka eneo ambalo wanafamilia wenzake walikuwa wakiota moto.
Huko walikuta nyumba ya familia hiyo ikiwa imetolewa mabati na milango na kubaki gofu. Vitu vyote vilikuwa nje, wanaume walilala nje ya kibaraza cha gofu hilo.
Walitandika godoro kubwa na kufunga neti. Wanawake na watoto walilala ndani ya kichumba kidogo ambacho kilikuwa hakina paa. Humo walilala watu 10 wakiwamo watoto na mama zao.
“Karibuni jamani, poleni na kazi hakika kazi yenu ni ngumu mnafanya kazi hadi usiku poleni sana,” alisema mmoja wa wanafamilia hao Moses Mbonde aliyekuwa akiota moto nje.
Baada ya makaribisho, moto ulichochewa upya hali iliyosababisha kuwapo kwa mwanga mkubwa. Wakati wote huo bado mbwa waliokuwa wamefungwa kila upande wa nyumba hiyo waliendelea kubweka.
“Msiogope hawa mbwa tumewaweka kama walinzi, vitu vyetu vyote viko nje,” alisema Aboud.
“Tuna vitu vya thamani kusema ukweli, lazima tuvilinde, tuna mabati ya aluminiamu, mbao za mninga na madirisha. Tunachofanya tunapokezana kulala,” alisema Moses.
Moses alisema wamekuwa wakiishi maisha ya hofu na hata kutokupata usingizi.
“Tulizoea kulala ndani ya kiyoyozi leo tunalala nje tunaumwa na mbu inaumiza sana. Hata usingizi tunaoupata ni wa kuungaunga tu” alisema.     

Bomoabomoa nyingine kutikisa Dar


Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), limesema wakati wowote litaendesha operesheni ya kubomoa nyumba zote zilizojengwa kando ya Bonde la Mto Msimbazi kinyume cha sheria.
Operesheni hiyo itawahusu pia wale wote waliojenga vibanda katika Bonde la Mkwajuni eneo la Magomeni wilayani Kinondoni.
Akizungumza na wanahabari leo Agosti 28 katika eneo la Mto Msimbazi, Mwanasheria Mwandamizi wa Nemc, Manchare Heche amesema watu wanaoishi katika maeneo hayo wanatakiwa kujiandaa kuondoka katika bonde hilo.
Amesema wanaoishi eneo hilo wanavunja utaratibu kwa kuwa ni sehemu hatarishi kwa maisha yao na kwamba, walishapigwa marufuku lakini baadhi wamerudi kinyemela.
"Mfano hawa wenye vibanda ambavyo vinachomoza kila kukicha katika Bonde la Mkwajuni, tulishawapiga marufuku na hapa palikuwa peupe lakini wamerudi.Sasa nawaambia wajiandae kuondoka hapa, operesheni hii itawahusu,"amesema.
Alipoulizwa bomoabomoa inaanza lini, Heche hakutaka kusema zaidi ya kusisitiza wananchi wajiandae kuondoka ili kupisha operesheni hiyo.

Sunday, August 27

HALI YA ESTER BULAYA INAENDELEA VIZURI BAADA YA KUPATIWA MATIBABU


Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Mh. Edward Lowassa amefika Hospitali ya Taifa Muhimbili Dar kumjulia hali Mbunge Ester Amos Bulaya.


Dar es Salaam
. Hali ya Mbunge wa Bunda Ester Bulaya aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH ) inaendelea vizuri baada ya kuanza kupatiwa matibabu jana.

Bulaya ambaye alipata tatizo la kupumua baada ya kuzidiwa akiwa mahabusu ya Kituo cha Kati cha Polisi mjini Tarime, alifikishwa hospitalini hapo juzi usiku na kulazwa katika wodi namba 18 Sewahaji.

Akizungumza Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, John Stephen alisema leo Bulaya amepata ahueni kiafya na anaendelea vizuri na matibabu.

"Sasa ameanza kujihudumia mwenyewe, anakula vizuri na bado anaendelea na matibabu," amesema Stephen huku akisisitiza kuwa mgonjwa bado anahitaji utulivu kwa kipindi hiki.

Bulaya amesota rumande tangu akamatwe Ijumaa ya Agosti 18 kwa madai ya kuingia jimbo la Tarime na kufanya shughuli za kisiasa kwa kutoa msaada wa mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika shule za msingi jimboni humo baada ya kualikwa na mbunge mwenzake Ester Matiko

TAMKO LA BAVICHA KUHUSU HALI INAYOENDELEA NCHINI YA KUTOFUATA UTAWALA UNAOZINGATIA SHERIA ZA NCHI


Jeshi la Polisi Arusha lazuia mikutano ya Lema


Arusha. Jeshi la polisi mkoani Arusha, limepiga marufuku mikutano ya mbunge wa jimbo la Arusha mjini (Chadema), Godbless Lema iliyokuwa inaendelea katika jiji la Arusha ili kupisha maandalizi ya mtihani wa darasa la saba na mbio za Mwenge.
Katika barua ya Mkuu wa polisi wilaya ya Arusha, Mrakibu mwandamizi wa polisi (SSP),E.Tille ambayo imethibitisha na Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha,(SACP) Charles Mkumbo imeeleza kuwa, Lema amezuiwa kufanya mkutano kuanzia kesho Agosti 27 hadi Septembaa mosi.
"Ofisi ya Mkuu wa polisi wilaya ya Arusha, inakutaarifu kuwa imezuia mikutano yako yeye ratiba kuanzia Agosti27 hadi Septema mosi kwa ajili ya kupisha maandalizi ya kuhitimisha mtihani wa darasa la saba na mwenge wa uhuru" ilisomeka barua hiyo na kushauri Lema kupanga mikutano kuanzia Septemba 8 mwaka huu.
Kamanda Mkumbo amesema, sababu kubwa ya kuzuiwa mikutano hiyo ni kwa kuwa wanahitajika polisi wa ulinzi na hivyo haiwezekani kupata polisi wa kulinda mikutano na pia kushiriki katika masuala ya mitihani na mwenge.
"Haya ni mambo ya kitaifa hivyo ndio sababu OCD amesitisha mikutano ya mbunge na mambo haya yakimalizika ataendelea na mikutano yake"alisema.
Akizungumza na mwananchi jana, Lema alisema anapinga polisi kuzuia mikutano yake, kwani ni ukiukwaji wa sheria na haki za mbunge.
Lema amesema sheria ya bunge kifungu cha  nne fasihi ya  kwanza, kinazungumzia uhuru wa mbunge kufanya mikutano jimboni kwake na kifungu cha 4(1) na (2) vinaelezea uhuru huo wa mbunge kufanya mikutano na pia ni ukiukwaji wa sheria kuzuia mikutano ya mbunge kwenye jimbo lake.
Lema amesema anaamini, kuzuiwa mikutano yake ni njama baada ya kubainika katika mikutano zaidi ya  10 ambayo amefanya katika jimbo la Arusha imekuwa na mafanikio makubwa na wananchi wa Arusha wamepata fursa ya kujua ukweli wa mambo mbali mbali.
"Hizi ni njama najua walipanga kuvuruga mikutano na kuharibu vyombo vyangu wakashindwa, wakanitakama kwa kuzidisha dakika 7 kwenye mkutano wangu mmoja nikawashinda kwa hoja sasa wameona wazuie kabisa na ikiwezekana watumie nguvu"alisema
Amesema sasa anashauriana na wanasheria wake kuona kama akubali barua ya polisi ama aendelee na mikutano kwani kimsingi, maeneo ambayo mikutano imepangwa kufanyika sio ya shule .
"Sasa kesho Jumapili nipo nje ya mji eneo la Olmoti kuna maandalizi yapi ya mwenge na darasa la saba , ntakuwa na mkutano eneo la soko la Shuma kuna mkusanyiko kila siku wa watu, nitaathiri nini huo mwenge ambao utafika kuanzia Septemba 6"amesema
Hata hivyo amesema, baada ya barua hiyo na  kushauriana na mawaziri kadhaa na viongozi wa serikali, atalifikisha pia bungeni, kwani ni jambo la ajabu mbunge kuzuiwa kufanya mikutano kwasababu za mwenge na mitihani ya darasa la saba.
Amesema muda ambao umetakiwa na polisi afanye mikutano, anapaswa kuwa katika shughuli za kibunge jambo ambalo anaamini litaathiri ratiba za utendaji wa kazi zake.

''Je, Dembele anaweza kufikia kiwango cha Neymar?''

Dembele akifiungia France bao la ushindi dhidi ya UingerezaHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionDembele akifiungia France bao la ushindi dhidi ya Uingereza
Ousmane Dembele ana uwezo wa kuwa kama Neymar na huenda akawa mshindi wa taji la mchezaji bora dunia Ballon d'Or, kulingana na mchezaji wa zamani wa Uingereza na Bayern Munich Owen Hagreaves.
Dembele anatarajiwa kujiunga na Barcelona kwa kitita cha pauni milioni 135.5 kutoka klabu ya Ujerumani ya Borussia Dortmund.
Kiticha hicho cha uhamisho ni cha pili kwa thamani baada ya kile cha pauni milioni 200 ambazo Barca walipokea walipomuuuza Neymar kwa PSG.
Akizungumza kuhusu Dembele, Hagreaves aliambia BBC ni mchezaji bora mwenye umri wa miaka 20 duniani.
Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United aliongezea: Amekuwa akisakwa lakini mtu yeyote ambaye amemuona akicheza nchini Ufaransa na katika ligi ya Bundesliga msimu uliopita atajua kwamba ni mchezaji mzuri sana.
''Atakuwa ndoto dhidi ya mabeki wengi''.
''Kimaumbile ana nguvu na anaweza kucheza kwa kutumia miguu yote miwili.Anaweza kupiga mipira ya adhabu kwa kutumia miguu yote miwili''.

Majaliwa aishukuru Cuba kutambua mchango wa Nyerere


Cuba.Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameishukuru Serikali ya Cuba kwa kutambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na mashujaa wa ukombozi wa Bara la Afrika, akiwemo Baba wa Taifa Mwalimi  Julius Nyerere kwa kuwajengea mnara wa kumbukumbu.
Mnara huo umejengwa katika Manispaa ya Playa jijini Havana kwenye eneo maalumu la makumbusho ya mashujaa hao walioshiriki katika ukombozi wa Afrika, ambapo  zimewekwa sanamu zao pamoja na maelezo mafupi ya historia zao na nchi wanazotoka.
Waziri Mkuu amefanya ziara katika eneo hilo Ijumaa, Agosti 25, 2017 na kuweka shada la maua katika mnara huo uliozungukwa na sanamu za mashajuaa wa Bara la Afrika na kuonyeshwa sehemu itakayowekwa sanamu ya  Nyerere.
Akiwa katika eneo hilo, Waziri Mkuu aliishukuru Serikali ya Cuba kwa kujenga makumbusho ya mashujaa hao na kwamba Serikali ya Tanzania itashirikiana na Cuba kuhakikisha kuwa sanamu ya Mwl. Nyerere inawekwa katika sehemu iliyotengwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Instuto Cubano De Amistad Con El Pueblo (Taasisi ya Ushirikiano wa Cuba na Nchi Marafiki),  Jose’ Prieto Cintado amesema mnara huo umejengwa kwa lengo la kutambua thamani na umuhimu wa viongozi hao.
Mkurugenzi huyo amesema Serikali ya Cuba inathamini mchango mkubwa uliotolewa na mashujaa hao katika vita ya ukombozi wa Bara la Afrika, ambapo iliamua kujenga mnara wa kumbukumbu katika nchi yao.
 Amesema wananchi wa Cuba pamoja na watu kutoka mataifa mbalimbali ndani na nje ya Bara la Afrika wanakwenda katika eneo hilo la makumbusho na kujifunza historia za viongozi hao. Pia eneo hilo linatumiwa na watafiti wa masuala ya kihistoria.
Mashujaa ambao tayari sanamu zao zimekwishawekwa kwenye eneo la kuzunguka mnara huo ni pamoja na Jomo Kenyatta (Rais wa kwanza wa Kenya), Modibo Keita (Rais wa Mali), Amilcar Cabral (Rais wa kwanza wa Guinea Bissau).
Wengine ni  Dk Kwame Nkrumah (Rais wa kwanza Ghana), Oliver Thambo (Kiongozi Mwandamizi wa Chama cha Ukombozi cha ANC cha Afrika Kusini), Eduardo Chivambo Mondlane (Kiongozi wa ukombozi nchini Msumbuji).
Wengine ni Samora Moises Machel (Rais wa kwanza wa Msumbuji), Sekou Toure (Rais wa kwanza wa Senegal), Seretse Khama (Rais wa kwanza wa Botswana), Alhaji Aboubakar Tafawa Balewa na Obafemi Jeremiah Awolowo (Mawaziri Wakuu wa zamani wa Nigeria) na Chifu Jeremia Azikiwe (Rais wa zamani wa Nigeria)  .

Samia ataka wanawake wamrithi


Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema anatamani atakapomaliza muda wake wa uongozi nafasi yake ichukuliwe na mwanamke na watokee wanawake wengi waliofikia mafanikio yake .
Ili kufikia mafanikio hayo Samia amesema ni muhimu kwa wanawake kuwa na umoja na mshikamano na kushirikishana fursa za kujikwamua katika nyanja mbalimbali.
“Mimi siamini kwenye msemo wa adui wa mwanamke ni mwanamke kwani mpaka kufikia hapa kuna mchango mkubwa wa wanawake wenzangu walionilea na kuniamini naweza,”.
Mama Samia amesema hayo leo wakati akizindua jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi mkoa wa Dar es Salaam hafla iliyoambatana na uzinduzi wa huduma ya Sim Account ya benki ya CRDB.
Amesema hata sheria zote zikibadilishwa na kuwapendelea wanawake haitaleta tija kama wanawake wenyewe hawatajituma na kuamua kujikwamua.
Amesema muda umefika sasa kwa wanawake kujipanga ni namna gani wataweza kujikomboa kiuchumi na kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kuijenga Tanzania mpya.
“Niwasihi wanawake hebu tuache mambo ya umbea, majungu na fitina, tushirikishane fursa, tusaidiane kujikwamua kiuchumi ili kutimiza malengo yetu. Nguvu tunazotumia kwenye kurushana rojo na kupigana majungu tuzitumie kuinuana,”
“Ule wakati wa kutambulika kama mwanamke ‘jiko’ pekee umeisha sasa ni mwanamke ‘viwanda’. Hapa  namaanisha kuwa ni mwanamke mwenye maamuzi yake kiuchumi, kielimu, kibiashara, kisiasa na mwenye uwezo wa kushika nyadhifa za juu katika sekta binafsi na umma na kuwa wawekezaji katika viwanda,”.
Mama Samia amesema ni anategemea kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni chachu ya wanawake waliofanikiwa kuwainua wenzao ili kuhakikisha kila mwanamke ananufaika na keki ya watanzania.
Alisema, “Nafahamu miongoni mwetu kuna wabobezi wa masuala mengi tusinyimane ujuzi, tufundishane, tushirikishane fursa.
Aidha alizitaka taasisi za fedha kubuni huduma zitakazowavuta wanawake ikiwa pamoja na kuwawekea riba ndogo kwenye mikopo hasa wanaojihusisha na shughuli za ujasiriamali.
“Kupitia jukwaa la wanawake sasa tunategemea taasisi za fedha zitashindana kututafuta ili zifanye biashara, tutumie fursa hiyo kwa lengo la kuleta maendeleo,” alisema Mama Samia
Akizungumzia huduma ya Sim Account Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB, Dk Charles Kimei alisema inalenga kuwarahisishia wanawake kufungua akaunti kupitia simu ya mkononi.
Amesema  benki hiyo imeona  fursa kubwa ya utekelezaji wa mkakati  kwa kuwakutanisha wanawake katika nyanja ya kiuchumi hivyo ikawaletea huduma hiyo.
"Ni asilimia 17 ya watanzania kati ya 50 milioni ndiyo wanatumia huduma rasmi za kibenki.Katika takwimu hizo wanawake ni milioni 25 pekee. Hii inaashiria kuwa upatikanaji wa huduma hizi bado ni changamoto”.
Kupitia Simu Account mtumiaji anaweza kuhamisha na kupokea fedha kwenda kwenye mitandao ya simu, kulipa ada, kulipia huduma, kuweka fedha kwenye kaunti ya CRDB, kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma nyingine nyingi.

CUF watoa salamu za pole


Dar es Salaam. Chama Cha Wananchi (Cuf) kimetoa pole baada ya ofisi  Mawakili wa Kampuni ya Ishengoma Karume Masha and Magai (IMMMA ADVOCATES) yenye makao makuu yake kando ya barabara ya Umoja wa Mataifa, Upanga, Dar es Salaam kuteketea kwa moto.
Chama hicho  kimedai kupokea kwa  masikitiko ya taarifa ya kutokea kwa moto ulioteketeza ofisi hizo leo asubuhi.
Pole hiyo imetolewa kupitia  taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Habari uenezi na Mahusiano ya Umma Mbarala Maharagande kwa madi kwamba  kwamba kinatambua mchango wao katika kupigania haki.
“Tunatoa pole na kuungana na Mawakili na wafanyakazi wote katika kipindi hiki kigumu cha uharibfu wa mali na vitendea kazi mbalimbali vyenye thamani kubwa. Tunatambua mchango mkubwa wa Kampuni ya IMMMA na mawakili wake katika kutetea na kupigania haki, usawa, demokrasia na utawala bora katika nchi yetu,” amesema Maharagande.
Chama hicho kililitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka katika kufanyia uchunguzi tukio hilo na kutoa taarifa kwa umma ili ujue nini chanzo cha moto huo.
“Nchi yetu hivi sasa  imekumbwa na matukio makubwa ya ukiukwaji wa haki za binaadamu na vitendo vya uhalifu vinavyoonekana wazi kuwa vinaratibiwa makhsusi na kikundi cha watu wenye nia ovu dhidi ya watetezi wa haki, uhuru na demokrasia kwa lengo la kuogofya,” anasema.
Amesema ni wajibu na jukumu la kila Mtanzania kupinga na kulaani vitendo na mwenendo mbaya wa muelekeo wa Taifa letu katika hali hii.

Saturday, August 26

Wake wa wanajeshi walalamika kuhusu hali ya waume zao Ufaransa

Wake wa wanajeshi walalamika kuhusu hali ya waume zao UfaransaHaki miliki ya pichaAFP/GETTY IMAGES
Image captionWake wa wanajeshi walalamika kuhusu hali ya waume zao Ufaransa
Mamia ya wake wa wanajeshi wa Ufaransa, wanafanya maandamano mjini Paris, kupinga hali ya maisha wanamoishi waume zao, wakaiwa katika zamu za kupambana na ugaidi.
Mercedes Crepin, ambaye alisaidia kuunda kundi la "wake wa jeshi wenye hamaki"; amesema , baadhi ya wanajeshi wamewekwa katika mabanda ya maji na yaliyojaa mende na kunguni.
Baada ya wapiganaji wa Kiislamu kushambulia ofisi ya gazeti la Charlie Hebdo, Januari mwaka wa 2015, serikali ya Ufaransa iliweka wanajeshi zaidi ya elfu saba kulinda mahala na matukio muhimu.