Thursday, August 10

SEKTA BINAFSI KUWEZA KUNUNUA NYUMBA.

WHC WAFUNGUA DIRISHA JIPYA LITAKALOWEZESHA WATUMISHI WA SEKTA BINAFSI KUWEZA KUNUNUA NYUMBA.

 Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Company (WHC),  Dkt. Fred Msemwa (Katikati)akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo wakati wa kufungua dirisha jipya  litakalowezesha watumishi wa sekta binafsi  kuweza kununua nyumba zake kwa garama nafuu na kuwainua kiuchumi. Kushoto  ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mauzo wa Watumishi Housing Company (WHC), Raphael Mwabuponde na Kulia ni Afisa Uhusiano na mauzo wa Watumishi Housing Company (WHC),  Maryjene Makawia.





 

Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mauzo wa Watumishi Housing Company (WHC), Raphael Mwabuponde akifafanua jambo wakati wa kufungua dirisha jipya  litakalowezesha watumishi wa sekta binafsi  kuweza kununua nyumba zake kwa garama nafuu na kuwainua kiuchumi. katikati ni 
Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Company (WHC),  Dkt. Fred Msemwa na kulia ni Afisa Uhusiano na mauzo wa Watumishi Housing Company (WHC),  Maryjene Makawia.

kulia ni  Afisa Uhusiano na mauzo wa Watumishi Housing Company (WHC),  Maryjene Makawia akizungumza na waandishi wa ahabari jijini Dar es Salaam leo. kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Company (WHC),  Dkt. Fred Msemwa.


Kulia ni Afisa Mauzo wa Watumishi Housing Company (WHC), Irene Kasanda akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mauzo wa Watumishi Housing Company (WHC), Raphael Mwabuponde, Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing Company (WHC),  Dkt. Fred Msemw na Afisa Uhusiano na mauzo wa Watumishi Housing Company (WHC),  Maryjene Makawia.
Picha na Avila Kakingo, Blog ya Jamii.
Na Karama Kenyunko blogu ya jamii.
WATUMISHI Housing Company (WHC),  wamefungua dirisha jipya  litakalowezesha watumishi wa sekta binafsi  kuweza kununua nyumba zake kwa garama nafuu na kuwainua kiuchumi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa WHC,  Dkt. Fred Msemwa, amesema, dirisha hilo ambalo litajumuisha Watumishi wote wale wa umma na wa binafsi, litawawezesha wafanyakazi wote kuwa na makazi bora kupitia umiliki wa nyumba kwani nyumba hizo wanaweza kuzitumia kwa kukopa kuanzisha miradi mbali mbali ya uchumi.

Amesema Watumishi hao wa sekta binafsi ambao nao wanapata fursa ya kununua nyumba hizo ni wale ambao hawako katika utumishi wa umma lakini wanachangia katika mifuko ya pensheni.

Ameongeza kuwa, wigo huo mdogo unatokana na mahitaji ya wengi kwani watu wengi ukitoa Watumishi wa umma ambao hapo awali ndio walikuwa na sifa ya kununua nyumba hizo,wanashida ya makazi bora na ya kisasa

"Kufuatia uamuzi huu, WHC sasa itakuwa ikiwahudumia Watumishi wa umma pamoja na wafanyakazi wengine walioko katika sekta binafsi ikiwa ni muendelezo wa juhudi za Serikali na mifuko ya hifadhi ya jamii katika kuwawezesha wafanyakazi wote kuwa na makazi bora na kuwainua kiuchumi kupitia umiliki wa nyumba", amesema Dkt Msemwa.

Naye Mkuu wa Kitengo cha mauzo na masoko wa WHC, Raphael Mwabuponde amewaalika watanzania wote wenye uhitaji wa nyumba hizo, kutuma maombi kwa kuchukua fomu katika tovuti ya WWW.whctz.org.
Ameongeza mpaka sasa bado kuna nyumba za kuuza zilizopo Bunji B, Gezaulole Kigamboni, Mkundi Morogoro, Mwanza Kisesa na Njedengwa Dodoma.

JK NA LOWASSA WAJUMUIKA NA MAMIA YA WANANCHI MAZISHI YA BILIONEA MREMA ARUSHA


 Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete akiweka shada la maua katika kaburi la Bilionea marehemu Maleu Mrema katika ibada ya mazishi yaliyofanyika jana katika hoteli yake ya Ngurudoto iliyopo nje kidogo ya jiji la Arusha(Habari Picha NA Pamela Mollel,Arusha)
Waziri Mkuu mstaafu,Edward  Lowassa akiweka shada la maua pamoja na mke wake  katika mazishi ya bilionea Maleu Mrema jana nje kidogo ya jiji la Arusha katika hoteli ya Ngurudoto
Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo akiweka shada la maua katika kaburi la marehemu Mrema katika ibada ya mazishi yaliyofanyika katika hoteli yake ya Ngurudoto iliyopo nje kidogo ya jiji la Arusha
 Baadhi ya wake za marehemu wakiweka udongo katika kaburi la mpendwa wao

 Waziri Mstaafu wa mambo ya nje Benard Membe akiweka shada la maua katika kaburi la Bilione Mrema

 Meneja mahusiano Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa)Pascal Shelutete akiweka shada la maua katika kaburi la Bilione Mrema.
 Watoto wa marehemu wakiwa wamebeba mashada ya maua

 Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete wakisalimiana na Waziri Mkuu mstaafu,Edward  Lowassa katika mazishi ya bilionea Maleu Mrema leo nje kidogo ya jiji la Arusha katika hoteli ya Ngurudoto
 Baadhi ya wanakamati wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa marehemu Mrema kuelekea katika eneo maalumu lililotengwa na familia kwaajili ya maziko
 Hapa watoto wakiwa wanaweka udongo katika kaburi la baba yao
 Wake wa marehemu wakiwa wanaingia katika eneo maalumu lililotengwa kwaajili ya maziko
 Kulia ni Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete,katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo pamoja na Abdulrahman Omari Kinana wakiteta jambo katika msiba wa Mrema
 Wake wa marehemu Mrema wakiwa katika huzuni kulia aliyevalia suti nyeusi ni baba mzazi wa Bilionea huyo
 Mh Abdulrahman Omari Kinana mara baada ya kuweka shada la maua
 Jeneza la marehe Bilionea Maleu Mrema likiwa linashushwa katika nyumba yake ya milele

Wanafamilia wakiwa katika picha ya pamoja na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete
Nyumba ya milele ya Bilionea Maleu Mrema 

Polisi watawanya watu wanaochoma matairi Kenya


Nairobi. Jeshi la Polisi katika Mji wa Kisumu, nchini Kenya limelazimika kuanza kutumia nguvu kuwatawanya kundi la vijana waliojitokeza mtaani kuanza kuchoma matairi ya magari, wakidai kuibiwa kura kwa mgombea wao wa urais anayeungwa mkono na Muungano wa Nasa, Raila Odinga.
Tukio hilo limetokea baada ya saa chache Odinga kujitokeza mbele ya vyombo vya habari akituhumu uchakachuaji wa kura zake uliofanywa na Tume ya Uchaguzi isiyokuwa na mipaka (IEBC) wakati wa tukio la kuhesabu kura.
Wananchi nchini Kenya walipiga kura katika Uchaguzi Mkuu siku ya jana ,kabla ya vituo hiyo kufungwa kuanzia saa 11:00 jioni.
Mwandishi wetu aliyeko nchini Kenya, Noor Shija ameshuhudia vurugu hizo zikiendelea katika maeneo ya mitaa ya Kisumu hatua iliyosababisha kufungwa kwa baadhi ya barabara ya Kasumu Kakamea. Polisi walilazimika kutumia nguvu huku wakirusha risasi hewani ili kuwatawanya.
Baadaye Polisi iliamua kuondoa mawe yaliyokuwa yametegwa na vijana hao barabarani.Katika hatua nyingine, kuna taarifa za kupigana kwa wafuasi wa wagombea ubunge katika kituo vha kujumlishia matokeo , kilichopo Mji wa Mokewe, uliopo Lamu kabla ya Polisi kuwasili eneo la tukio na kurejesha hali ya utulivu

IEBC kuendelea kuonyesha matokeo hadharani


Nairobi. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini hapa, (IEBC), imepinga matakwa ya National Super Alliance (Nasa) ya kutaka tume hiyo iache kuonyesha matokeo ya kura za urais hadharani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo(Jumatano), Makamu Mwenyekiti wa IEBC, Consolata Maina amesema kuweka hadharani matokeo ya kura za urais ni sehemu ya kazi yao.
Maina ametoa kauli hiyo kufuatia hoja ya Nasa iliyoitaka IEBC isimamishe kuweka hadharani matokeo, wakati mgombea wa Jubilee Uhuru Kenyatta akiwa tayari anaongoza kwa kura milioni 1.2.
Maina amewaambia waandishi kwamba wao wana wajibu kwa wananchi wa Kenya na kufanya kazi kwa uwazi. Pia, amesema kwa uwazi huo unaviwezesha hata vyombo vya habari kupata taarifa za uhakika na kuwaeleza wananchi wanaosubiri matokeo hayo.
Amesema kuonyesha matokeo hayo pia kunakwenda sambamba na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kwamba kura zilizotamgazwa kwenye vituo vya kupigia kura zitakuwa ndio uamuzi wa mwisho.
Kabla ya tamko hilo, mgombea wa Nasa Raila Odinga amewaambia waandishi wa habari kwamba matokeo ya kura za urais yanayotangazwa na IEBC ni 'kazi iliyofanywa' na kompyuta.
Odinga amesema matokeo yanayoendelea kutangazwa na IEBC, hayaonyeshi matakwa ya wapiga kura ,akitaka tume hiyo ionyeshe fomu namba 34A na 34B ili kuthibitisha matokeo yanayotangazwa.
Madai hayo ya Odinga anayatoa ikiwa ni saa chache zimepita baada ya wakala wake mkuu Musalia Mudavadi na mwanasheria wa Nasa, James Orengo kutoa madai kama hayo walipozungumza na wanahabari eneo la Bomas. 

Craca Machel awataka vijana wajitume

Mke wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Afrika

Mke wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Afrika Kusini Nelson Mandela, Graca Machel 
Dar es salaam. Mke wa aliyekuwa Rais wa kwanza wa Afrika Kusini Nelson Mandela, Graca Machel amewataka vijana wa Afrika kuacha kulalamikia serikali zao katika masuala mbali mbali ya kiuchumi na badala yake waonyeshe mfano kwa kufanya kazi.
Machel amesema hayo leo wakati akizungumza na vijana kutoka nchi mbalimbali katika mjadala wa kujadili changamoto zinazowakabili vijana wa Afrika katika uchumi, Elimu ikiwa ni maandalizi ya kuelekea siku ya vijana duniani 12 Agosti mwaka huu.
"Nimewasikia vijana wengi mkilalamika serikali haijaweka mazingira mazuri kwa vijana, serikali haijafanya hiki na kile, naomba ni waambie vijana wangu acheni kulalamika, fanya! Onyesha unaweza nini "amesema.
Amesema kulalamika pekee hakuwezi kuwasaidia vijana wa Afrika kuwa na maisha mazuri hakuna serikali inayoweza kuwaletea ama kuwafanyia kila jambo mengine vijana wenyewe wanatakiwa kufanya na wanapokwama basi waifuate serikali.
" Zambia mnasema tumepiga kelele kwa serikali juu ya kuboresha mazingira ya uwekezaji wa uchumi kwa vijana lakini hakuna jitihada niwaambie vijana wangu tengenezeni mipango yenu kama vijana kisha wapelekeeni muwaambie tumefanya hivi lakini tumekwama hapa "amesema.
-" Kama wasipowasikiliza waambieni tutawanyima kura, nawaambia lazima serikali itawasikiliza kinachotakiwa nikujikusanya vijana wengi msiwe kikundi cha watu sita au kumi" amesema
Amewataka pia vijana kuacha visingizio na kuuliza maswali ya sasa tunafanyaje? Tutaanzaje? kwani majibu ya maswali hayo wanatakiwa kuwa nayo wao wenyewe.
"Acha kuuliza maswali ambayo majibu yake unayo wewe, fanya, jiwekeeni mipango kama mtalalamika tu mnataka nani afanye "amesema.
Hata hivyo baadhi ya vijana wanaharakati wamesema vijana wa Afrika wengi bado wa na changamoto nyingi ikiwamo ukosefu wa ajira na elimu ya uzazi hali inayosababisha vijana wengi hasa wasichana kukosa fursa ya elimu baada ya kubeba ujauzito wakiwa shuleni.
Akizungumza katika kongamano hilo kijana mwanaharakati kutoka Tanzania, Halima Lila amesema "Hatuna mwongozo sahihi wakulinda elimu ya mtoto wa kike,bado Kuna hitaji kubwa la kutoa elimu juu ya uzazi kwa vijana wakike na wa kiume" amesema.
Seif Ibrahim amesema Tanzania bado kuna tatizo la ajira kwa vijana na mimba kwa watoto wakike ambao wengi wanashindwa kumaliza elimu zao za sekondari lakini pia elimu zinazotolewa kwa vijana mashuleni haziwapi uwezo wa kujitegemea wamalizapo masomo "amesema.

Tanesco yaacha kilio kwa kaya 200 Dar

Baadhi ya majengo yakiwa yamekatiwa umeme baada

Baadhi ya majengo yakiwa yamekatiwa umeme baada ya kuwekewa alama ya ‘X’ yakitakiwa kubomolewa kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro katika eneo la Kimara Stop Over. Baadhi ya ofisi zilizomo kwenye majengo hayo zinatumia jenereta kupata huduma hiyo kabla ya kuhamisha ofisi zao. Picha na Emmanuel Herman 
Dar es Salaam. Kaya zaidi ya 200 zilizopo eneo la Kimara Stop Over na Mbezi Kibanda cha Mkaa jijini Dar es Saalam ziko gizani baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuzikatia umeme ikiwa ni agizo la Serikali.
Kaya hizo ni miongoni mwa zilizowekewa alama ya X na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kwa lengo la kubomolewa ili kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro-Dar es Salaam.
Mwananchi ilizunguka maeneo mbalimbali ambayo yamekatiwa umeme na kushuhudia wananchi wakitumia mishumaa, vibatari, taa za kandiri na simu nyakati za usiku huku maeneo ya nje yakionekana kuwa na giza totoro.
Miongoni mwa kaya ambazo kwa sasa zinakaa gizani ni pamoja na ya wajane Joyce Elias (70), Zainabu Mwinyimvua (78) na jengo la biashara lenye gorofa tatu linalomilikiwa na Revy Kapinga ambaye pia ni mjane.
Mbali na nyumba za wananchi, majengo mengine yatakayokumbwa na bomoabomoa hiyo ni nyumba za ibada, vituo vya mafuta, kituo cha watoto yatima, vituo vya afya zikiwamo hospitali na zahanati pamoja na ofisi moja ya kata.
Tanesco wakata umeme chini ya ulinzi
Tanesco imeendelea kukata umeme huku mafundi wake wakifanya kazi hiyo wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi ikiwa ni hatua ya awali ya wananchi hao kubomoa nyumba zao.  Wakizungumza na Mwananchi, wananchi hao walisema wanashangaa hatua ya kukatiwa umeme wakati kesi yao bado ipo mahakamani na hivyo kulazimika kuishi gizani.
Mkazi wa eneo hilo, Rehema Kalolo alisema ni vizuri Tanesco ingesubiri uamuzi wa mwisho utakapotolewa kwa sababu mpaka sasa hawajui hatima ya nyumba zao na kwamba, anatumia kibatari kwa ajili ya mwanga wakati wa usiku baada ya nyumba yake kukatwa umeme. Alisema tangu walipokatiwa umeme hali ya uchumi imebadilika kwa sababu nje ya nyumba alikuwa akiendesha biashara zinazotegemea nishati hiyo.
Rehema alidai kuwa hawezi tena kufanya biashara hizo na kwa sasa anasubiri siku watakayobomolewa kabisa nyumba wanayoshi jambo ambalo litawaongezea umaskini.
“Tupo gizani kwa wiki sasa, Tanesco walikuja hapa wakang’oa mita zao na kuondoka. Ni giza tu eneo lote hili, tunaishi kwa hofu kubwa. Kibaya zaidi hata kazi tulizokuwa tukitegemea kuendeshea maisha hatuwezi tena kuzifanya,” alisema.
Rose Robert, mkazi wa Mbezi Kibanda cha Mkaa alisema hofu imetawala kwenye familia yao kwa sababu wanajua wakati wowote watabomolewa kwa kuwa tayari wameshakatiwa umeme. “Sina amani na sijui nitaelekea wapi kwa sababu kukatiwa umeme ni dalili kwamba wakati wowote nyumba yangu itabomolewa. Ni maumivu makali ni sawa na mtu kukuchoma mkuki kwenye kidonda.” alisisitiza.
Kiongozi wa wananchi waliowekewa X kwenye eneo la Kimara Stop Over, Ephraim Kinyafu alisema kuwapo kwa giza kwenye nyumba nyingi za wananchi waliokatiwa umeme kumesababisha kuongezeka kwa wimbi la uharifu.
Alisema kwa sasa wanashindwa hata kukutana na kuzungumzia hatima yao kwa sababu hawajui kinachoendelea zaidi ya kuwaona wafanyakazi wa Tanesco wakiendelea kukata umeme.
“Hatupingani na ujio wa maendeleo lakini walau wananchi wangekuwa wanashirikishwa, wajue ni nini kinaendelea,” alisema Kinyafu.
Alisema kuwa awali mita zilizokuwa zinapaswa kuachwa kama hifadhi ya barabara zilikuwa 60 hivyo wananchi wengi walijenga nje ya umbali huo. Hata hivyo, baadhi ya maeneo bado hayajakatiwa umeme japokuwa wananchi wanaendelea kuishi kwa hofu wakisubiri hatima ya nyumba zao.
Mzee John Mlangi, mkazi wa Kimara Suka alisema tangu awekewe alama X hajui kinachoendelea japo ikitokea nyumba yake ikabomolewa atabaki hapo kwa sababu hana sehemu nyingine ya kwenda.
“Mimi sijakatiwa umeme bado, lakini huenda wakaja kukata kama walivyofanya kwa wengine, nimeshastaafu na kwa kweli sijui hatima ya maisha yangu ya uzeeni. Nilijenga nyumba hii miaka 35 imeshapita nadhani, Serikali inalo jambo la kutazama hapo,” alisema.
Kwa upande wake, Ahmad Kalolo alisema barabara hiyo ndiyo iliyovamia baadhi ya maeneo ya wananchi hasa wale waliojenga miaka mingi iliyopita wakati bado haijajengwa.
“Barabara hii imenikuta. Zamani ilipita kule upande wa pili, kwa hiyo nipo eneo sahihi ambalo sio mimi natakiwa kuvunja, Serikali inapaswa kunilipa fidia na kuvunja,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa barua ya Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, wanatarajia kufanya upanuzi wa barabara ya Morogoro umbali wa mita 121.5 kutoka katikati ya barabara.
Barua hiyo ilisema kwa kuwa nyumba, ukuta, shimo la majitaka, uzio na fremu za biashara viko ndani ya hifadhi ya barabara kinyume cha sheria, wamiliki wanaagizwa kubomoa. Pia, barua hiyo iliwataka wabomoe ndani ya siku 30 kuanzia siku ya barua hiyo na wasipofanya hivyo, watalazimika kulipa gharama zote zitakazojitokeza.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamelazimika kwenda mahakamani ili kuweka zuio la ubomoaji wa nyumba hizo.

Majaliwa amaliza sintofahamu ya tumbaku Tabora


Tabora. Serikali imefanikiwa kumaliza sintofahamu iliyokuwepo baina ya wakulima na wanunuzi wa tumbaku mkoani Tabora juu ya uwepo wa tani 3,700 zilizokosa soko.
Tani 3,700 zilikuwa zimekosa wanunuzi kwa sababu hazikuwa na mkataba kati ya wakulima na wanunuzi na hivyo kuhitaji utatuzi wa haraka wa Serikali ili kuinusuru tumbaku hiyo.
“Tumefanikiwa kuongea nao na tutauza zile tani 3,700 kwa wanunuzi,” alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kuamsha shangwe ukumbi mzima.
Majaliwa alitoa ahadi hiyo jana jioni Agosti 9 wakati akizungumza na wadau wa zao la tumbaku zaidi ya 600 wakiwemo wabunge, viongozi wa dini, chama na Serikali kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Isike-Mwanakiyungi, mjini Tabora.
Aliwashukuru wanunuzi kwa kukubali kumaliza tatizo hilo kwani litaleta ari mpya kwa wakulima na kuwafanya wajipange vizuri kwa msimu ujao. “Makampuni ya ununuzi yatapita kwenye maeneo yenu, WETCU watafuatilia na tumekubaliana nao kuwa tutafanya kazi pamoja,” alisema..
Kufuatia sintofahamu hiyo, wiki iliyopita, wakazi wa mkoa huo waliomuomba Rais, John Magufuli aingile kati ili kuwanusuru na adha ya zao hilo kukosa soko naye akawaahidi wananchi hao kwamba suala hilo atalikamilisha Waziri Mkuu.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakati akiwasilisha muhtasari wa taarifa ya mkoa huo alisema katika masoko ya tumbaku yanayoendelea, kuna tatizo la kukosa  wanunuzi kwani hapakuwa na mkataba kati ya wakulima na wanunuzi.
“Tumbaku inayofikia kilo milioni 3.7 kwa sehemu kubwa ililimwa kwa ufadhili wa WETCU Ltd, kwa fedha ambazo zilikuwa ziende APEX. WETCU walinunua pembejeo na kuwapa wakulima waliokuwa chini ya vyama sinzia, na sasa haina wanunuzi. Tunaomba ulisemee hilo ili tupate ufumbuzi wa suala hili,” alisema.

TRA yafungia vituo vya mafuta 241, vingine 840 hatarini


Dar es Salaam. Unaweza kusema  kwamba moto ambao Rais John Magufuli aliuwasha dhidi ya wafanyabiashara ya mafuta waliokuwa wakilalamikia matumizi ya mashine za kielektroniki za kutoa risiti (EFD), haukuwa wa kifuu.
Kuthibitisha hilo, tayari vituo 241 vya mafuta katika maeneo mbalimbali nchini vimefungiwa kuendelea na biashara hiyo hadi pale vitakapotekeleza agizo hilo huku vingine 840 vikipewa wiki tatu kuanzia leo kuhakikisha kuwa vinafunga na kuanza kutumia mashine hizo.
Hatua ya kufungwa kwa vituo hivyo iliyochukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekuja siku ya 12, tangu Rais Magufuli alipotoa siku 14 kwa vituo hivyo kuwa na mashine hizo la sivyo vifungiwe.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo Julai 20, wakati wa uzinduzi wa Barabara ya Kigoma - Biharamulo - Lusahunga na kuwataka wafanyabiashara hao kutekeleza hitaji hilo la kisheria, la sivyo watafute shughuli nyingine ya kufanya kwa sababu leseni zao zitafutwa. Aliiagiza Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia TRA, kusimamia utekelezaji wa agizo hilo kwa kufuta leseni zote za vituo vitakavyokuwa havijafunga mashine hizo.
Hata hivyo, siku chache baada ya agizo hilo la Rais Magufuli, katibu wa uhusiano na mawasiliano wa Chama cha Wamiliki na Wauza Mafuta Rejareja (Tapsoa), Kanda ya Ziwa, Ahmed Msanga alikaririwa akisema bei kubwa ya mashine hizo ni moja ya changamoto zinazozorotesha utekelezaji wa agizo la Serikali na kuiomba kuingilia kati kwa kuwadhibiti wafanyabiashara wa kati wanaoagiza na kuziuza.
Alisema moja inanunuliwa kati ya Dola 2,500 na 3,500 za Marekani; hivyo mfanyabiashara mwenye pampu nne hadi tano kulazimika kutumia kati ya Sh40 milioni hadi Sh50 milioni.
Lakini jana, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo alisema baada ya kukagua vituo hivyo, 241 vilikutwa havijafunga wala kununua mashine hizo.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015 na kanuni zake za mwaka 2016, mfanyabiashara anayethibitika kukwepa kutumia au kutoa risiti za kielektroniki anaweza kukabiliwa na adhabu ya faini ya Sh3 milioni hadi Sh4.5 milioni, huku mnunuzi anayekutwa na kosa la kutodai risiti, adhabu yake ikiwa faini ya kati ya Sh30,000 hadi Sh150,000 au kifungo au adhabu zote kwa pamoja.
“Vituo hivyo viko maeneo mbalimbali mikoani, tumevifungia kabisa kutokufanya biashara yoyote ya mafuta hadi pale watakaponunua na kufunga mashine hizo, ni sawa na unapofunga duka lisifanye biashara yoyote,” alisema.
Kayombo alisema kufungiwa kwa vituo hivyo kumetokana na wamiliki wake kushindwa na kutoonyesha nia ya kufunga mashine hizo. “Tumeagiza mameneja mikoa wote kufunga vituo hivyo na bado kuna vingine ambavyo vinaendelea kufungwa moja kwa moja,” alisema.
Kuhusu vituo 840, Kayombo alisema wamiliki wamepewa wiki tatu kuanza sasa na watasainishwa mikataba ya kufunga mashine hizo vinginevyo vitafungiwa pia. Alisema wapo ambao walishalipia mashine hizo na kazi inayoendelea ni usambazaji na ufungaji.
“Hawa wamesaini makubaliano, ikifika Agosti 31, wanatakiwa wawe wamemaliza kufunga na kuanza kutumia mashine hizo. Tumetoa muda huo kwa sababu wengi wao wapo mikoani kama Mbeya, Bukoba na maeneo mengine hivyo wana kazi ya kusafirisha...” alisema.
Kayombo alisema hadi kufikia jana, vituo 519 vilikuwa vimeshafungwa mashine za EFD.
Majengo yaingiza Sh31 bilioni
Mbali ya kuzungumzia vituo vya mafuta, Kayombo pia aligusia mafanikio yaliyopatikana katika operesheni kubwa ya kodi ya majengo akisema TRA imekusanya kiasi cha Sh31 bilioni kwa mwaka wa fedha ulioisha Juni 31.
“Tunaendelea kusisitiza ukusanyaji wa kodi pamoja na kwamba muda uliongezwa kwa sababu ya wingi wa watu kuja mwishoni. Waendelee kulipa kodi kwa mwaka wa fedha 2017/2018,” alisema.
Alisema mamlaka inaendelea kupokea kodi ya majengo, na wale ambao walichelewa kulipa ya mwaka 2016/2017, bado wataendelea kulipa ila watalipa na adhabu kwa kuwa ulitolewa muda wa nyongeza na walishindwa kutekeleza.
Alisema kwa ambao hawajalipa kodi ya majengo hadi kufikia jana, wanatakiwa wafanye hivyo.
Mkurugenzi huyo wa elimu kwa mlipakodi TRA, alisisitiza ulipaji kodi  kwa mujibu wa sheria, “Wananchi watoe ushirikiano. Nia sio kuadhibu wafanyabiashara kwa kutoa risiti au kudai risiti, ni kujenga utamaduni na mazoea ya kulipa kodi.”
Alisema mfanyabiashara mwenye mauzo yanayozidi Sh14 milioni kwa mwaka, anatakiwa kutumia mashine za EFD.
Profesa wa uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Haji Semboja alisema pamoja na juhudi hizo, Rais Magufuli anakabiliwa na changamoto ya wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga baada ya kuwaruhusu kufanya biashara maeneo yoyote.
“Hawa ni bomu la kisiasa, kiuchumi na kijamii, ni wengi na baadhi yao wanauza bidhaa zisizokuwa na ubora, hazina uhalali, hazina utambulisho (nembo) kwenye soko.
Alisema kisiasa, kundi hilo linaweza kukwamisha hata ndoto za uchumi wa viwanda kwa sababu vingine itabidi vianze kujiendesha kiujanjaujanja ili kuleta ushindani wa masoko katikati ya changamoto hiyo.

Maagizo ya Magufuli wilayani Handeni yaanza kufanyiwa kazi


Handeni. Maagizo aliyoyatoa Rais John Pombe Magufuli alipokuwa kwenye ziara yake wilayani Handeni kwa mkandarasi aliyejenga mabwawa ya Maji ya Manga na Mkata kurudia ujenzi huo kutokana na kuyajenga chini ya kiwango yameanza kuchukuliwa hatua.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alisema wakandarasi ambao wametakiwa kufika eneo la ujenzi kwa siku 14 tayari ameshawaandikia barua kwa kutakiwa kufika eneo la kazi kwa siku tano kuanzia tarehe iliyopangwa.
Gondwe alisema agizo hilo linafanyiwa kazi kwa ushirikiano na viongozi wote na kuhakikisha kila agizo lililotolewa linafanyika kwa wakati uliopangwa na endapo itatokea kinyume na hapo kamanda wa polisi atafanya kama aliyoagizwa na Rais Magufuli.
“Wakandarasi hawa, wale ambao wanatakiwa kufika site (eneo la kazi) kwa siku 14 kamanda wa polisi wa mkoa analifahamu hilo na tayari nimeshamuelekeza mkurugenzi na amesha waandikia barua ya kufika kuja kufanyakazi kama mheshimiwa Rais alivyosema na fedha zao bado tumezishikilia hadi pale watakapokuja kufanya kazi na sisi turudishe taarifa kama tulivyoagizwa,”alisema Gondwe
Mkurugenzi mtendaji wa Halmshauri ya Handeni, William Makufwe alisema tayari wameshawandikia barua wakandarasi hao na kuwataka kuwasilisha mpango kazi wao  na gharama watakazotumia pia kwa kufuata ule wa awali wa mwezi wa tatu wa jinsi ya kurekebisha miradi hiyo.

Mwanafunzi apeta ubunge Kenya


Dar es Salaam. Aliyekuwa mgombea wa Ubunge Igembe Kusini nchini Kenya, John Mwirigi (24) ameshinda nafasi hiyo baada ya matokeo kutangazwa na Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Mwirigi ambaye anatajwa kuwa Mbunge mwenye umri mdogo kuwahi kutokea aliwashangaza wengi katika kampeni zake ambapo alikuwa akitumia baiskeli na bodaboda.
Mwirigi ambaye ni mwanafunzi wa Shahada ya elimu katika chuo cha Mount Kenya alikuwa mgombea binafsi hakuwahi kuwa na matangazo kwa kile kilichodaiwa kukosa pesa za kufanya kazi hiyo.
Katika matokeo hayo, Mwirigi alipata kura 18,867 huku mgombea wa Jubilee, Rufus Miriti akipata kura 15,411.