Tuesday, June 13

Nani alifanya nini mikataba ya madini

Wakazi wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro wakiwa kwenye bar iliyopo katika eneo la Plaza wakitazama matangazo ya moja kwa moja kwenye luninga kuhusu tukio la Rais John Magufuli kupokea ripoti ya kamati ya pili ya uchunguzi wa madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga unaosafirishwa nje ya nchi lililofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana. 
Ripoti ya kamati ya pili ya makinikia iliyowasilishwa jana imeibuka na majina ya vigogo ikieleza jinsi walivyohusika kuingia mikataba mikubwa ya migodi ya madini na kulitia hasara Taifa.
Kamati hiyo iliyoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na mchanga wenye madini unaosafirishwa nje ya nchi yakiwamo makontena 277 imependekeza vigogo hao wachukuliwe hatua za kisheria.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Nehemiah Osoro akiwasilisha ripoti kwa Rais Magufuli mbele ya viongozi wengine wakuu wa Serikali, Ikulu jijini Dar es Salaam jana, aliwataja Dk Abdallah Kigoda (marehemu), Daniel Yona, Nazir Karamagi, William Ngeleja na Profesa Sospeter Muhongo kuhusika
Hao wote wamewahi kushika nafasi ya Waziri wa Nishati na Madini kwa vipindi tofauti.
Wengine ni wanasheria wakuu wa zamani na manaibu; Andrew Chenge, Johnson Mwanyika, Felix Mrema na Sazi Salula.
Mbali na hao pia wamo makamishina wa madini na wakuu wa idara ya mikataba wa zamani; Paulo Masanja, Ally Samaje Dk Dalaly Kafumu, Maria Ndossi na Julius Malaba.
Kamati ya Profesa Osoro imeitaka Serikali ifanye uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waliokuwa mawaziri, wanasheria wakuu wa Serikali na manaibu wao, wakurugenzi wa idara za mikataba, makamishna wa madini na wanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini.
Pia imetaka hatua zichukuliwe kwa watumishi wengine wa Serikali na watu wote waliohusika katika kuingia mikataba ya uchimbaji madini, utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini na kuongeza muda wa leseni, watumishi na wamiliki wa kampuni za madini, kampuni zilizohusika kuandaa nyaraka za usafirishaji wa makinikia na kampuni za upimaji wa madini kwa kuvunja sheria za nchi na upotoshaji.
Ndani ya ripoti
Katika ripoti hiyo, Profesa Osoro ameeleza jinsi Dk Kigoda alipokuwa Waziri wa Nishati na Madini alivyoingia mkataba na mgodi wa Bulyanhulu Gold Mines Ltd (Kahama Mine Corporation Limited) ambapo kwa jitihada kubwa alifanikiwa kujadiliana na kampuni hiyo na kuiwezesha Serikali kupata asilimia 15 ya hisa katika kampuni za uchimbaji.
“Hata hivyo, mkataba huo ulifanyiwa marekebisho Juni, 1999 na kusainiwa na Waziri wa Nishati na Madini aliyefuata, Dk Abdallah Kigoda. Marekebisho hayo yaliondoa asilimia 10 ya hisa ambazo Serikali ilikuwa inamiliki na kubakiza asilimia tano tu,” alisema.
Alisema marekebisho mengine katika mkataba huohuo yalifanyika Oktoba, 1999 ikiwa ni miezi minne tangu yale ya awali yafanyike.
“Marekebisho haya ya pili pia yalitiwa saini na Dk Abdallah Kigoda, ambayo yaliondoa asilimia tano ya hisa za Serikali zilizokuwa zimebakia na hivyo Serikali kubaki bila hisa yoyote.”
Profesa Osoro alisema katika marekebisho hayo, Serikali ilikubali kulipwa Dola 5 milioni za Marekani ikiwa ni malipo ya mauzo ya hisa zake.
Vilvile, Serikali ilikubali kuendelea kulipwa kiasi cha Dola 200,000 za Marekani kila mwaka.
Hata hivyo, alisema kamati yake haikuweza kupata uthibitisho wa kufanyika kwa malipo ya jumla ya Dola 6,800,000 za Marekani.
“Kamati imeona kwamba marekebisho hayo ya mkataba yaliyofanywa na Mheshimiwa Dk Abdallah Kigoda hayakuwa na masilahi kwa Taifa kwani Serikali ilipoteza haki ya umiliki wa hisa na kuinyima mapato kutokana na gawio,” alisema Profesa Osoro.
Mlolongo wa hatua haukuishia kwa waziri huyo ambaye Rais Magufuli alisema marehemu tu ndio hawatachukuliwa hatua, pia ulienda kwa mawaziri wengine Yona na Karamagi katika kampuni ya Pangea Gold Mine.
Profesa Osoro alisema kampuni hyo ina mikataba miwili ya uchimbaji madini na wa kwanza ulisainiwa Desemba 2003 na Yona akiwa Waziri wa Nishati na Madini na wa pili ulisainiwa na Karamagi akiwa waziri wa wizara hiyo.
“Katika mikataba hii yote Serikali haina hisa yoyote katika kampuni na pia mkataba huu unatoa nafuu kubwa sana za kodi kwa kampuni, jambo ambalo linaikosesha Serikali kodi nyingi na mapato,” alisema Profesa Osoro.
Yona aliingia tena kwenye mkataba wa kampuni ya North Mara Gold Mine ambao aliusaini Juni 1999 akiwa waziri wa wizara hiyo na baadaye marekebisho ya mkataba huo yalifanywa mwaka 2007 na Karamagi.
“Katika mkataba huo Serikali haina hisa yoyote katika kampuni. Aidha katika mkataba wa awali uliotiwa saini na Yona, Serikali ilitoa nafuu ya asilimia 15 ya nyongeza ya mtaji wa kampuni na kuifanya kampuni hiyo iwe inajilipa kwanza ili kurudisha mtaji wake na asilimia 15 iliyopewa na Serikali na hivyo kusababisha kampuni kutangaza hasara katika biashara kila mwaka. Jambo hilo limekuwa linaikosesha Serikali kodi ya mapato,” alisema.
Mwenyekiti huyo wa kamati aliongeza kuwa, wamebaini kwamba marekebisho yaliyofanyika mwaka 2007 kuondoa nafuu ya asilimia 15, bado malimbikizo ya hasara kutokana na nafuu ya kodi iliyokuwa imetolewa na Serikali iliendelea kudaiwa na kampuni hiyo. Haikuishia hapo katika mkataba wa kampuni ya Geita Gold Mine (AngloGold Ashanti) uliosainiwa na Dk Kigoda akiwa waziri, Serikali haikupata hisa yoyote na pia mkataba huo unatoa nafuu mbalimbali za kodi kwa kampuni, jambo ambalo linaikosesha Serikali kodi nyingi na mapato. “Mikataba ya uchimbaji madini inaeleza kuwa inaongeza na kurekebisha masharti yaliyomo katika leseni za uchimbaji madini,” alisema.
Alisema kuwa kamati inaona kuwa masharti ya aina hiyo ni batili kisheria kwa kuwa waziri hawezi kurekebisha masharti ya leseni yaliyotolewa kwa mujibu wa sheria na kanuni kupitia vifungu vya mkataba wa uchimbaji wa madini.
Profesa Osoro alisema kamati imebaini kuwa kumekuwapo na uongezaji wa muda wa leseni wa maeneo ya uchimbaji madini kinyume cha sheria na bila kuzingatia masilahi ya Taifa.
“Kwa mfano, kuongeza muda wa leseni na maeneo ya uchimbaji uliofanywa na Ngeleja na Profesa Muhongo, kwa kampuni za North Mara Gold Mines Limited na Pangea Minerals Limited. Pia leseni mbalimbali zilizotolewa na Kamishna Paulo Masanja, Kamishna Dalaly P. Kafumu na Kaimu Kamishna Ally B. Samaje,” alisema mwenyekiti huyo.
Alisema katika kipindi hicho washauri wakuu wa Serikali kwa masuala ya kisheria walikuwa ni pamoja na Chenge, Mwanyika na manaibu wanasheria wakuu ambao ni Mrema na Salula na wakuu wa idara ya mikataba, Maria Ndossi na Julius Malaba.
Dk Kafumu Ngeleja wazungumza
Dk Kafumu ambaye ni mbunge wa Igunga akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu alisema yuko tayari kuhojiwa na vyombo vitakavyomhitaji. “Nisingependa kuzungumza lolote kuhusu mapendekezo hayo, nitakuwa ninazungumza kabla ya kuhojiwa na Serikali, kwani ni mmoja kati ya waliotajwa, nitakuwa tayari kuhojiwa kwa sababu ni maagizo ya Rais,” alisema Dk Kafumu.
Kwa upande wake, Ngeleja alisema hawezi kuzungumzia agizo la Rais Magufuli la kuhojiwa na vyombo vya usalama kutokana na kuhusika kwake katika mikataba ya madini. Hata hivyo alitaja uzembe wa usimamizi wa sheria kuwa ndiyo uliolifikisha Taifa hapo kwa kuwa sheria zilizopo ni nzuri, lakini hazisimamiwi ipasavayo.
“Kuhusu kuhojiwa au kuwajibika sina neno la kusema lakini nampongeza sana kwa moyo wa dhati Mheshimiwa Rais maana amezungumza kwa hisia na uzalendo kabisa kuhusu tunachostahili kupata badala ya tunachopata,” alisema Ngeleja ambaye pia mbunge wa Sengerema.
Hata hivyo, alikiri kuwa mikataba mingi iliyopitishwa siyo mizuri kwa kuwa inawanyonya Watanzania ambao wameshindwa kupitia sheria mpya (ya madini ya mwaka 2010) kuifanyia kazi.
“Kifungu cha 11 pia kinachosema mikataba yote ipelekwe bungeni baada ya miaka mitano na kifungu cha 10 kinasema Serikali ishiriki kimkakati kwenye migodi, lakini usimamizi wake ndiyo shida,” alisema Ngeleja.
Kuhusu mchanga kusafirishwa nje ya nchi, alisema walishaliona jambo hilo mapema lakini wakabainisha kuwa mashine za kufanya kazi hiyo zina gharama kubwa zaidi hivyo kuhitaji ubia katika ujenzi baina ya Serikali na sekta binafsi.
Wakati Ngeleja akisema hayo, Chenge hakutaka kuzungumza na waandishi habari waliomfuata mara baada ya kuahirishwa kikao cha Bunge jana. “Siongei na watu,” ndiyo maneno pekee aliyoyasema mbunge huyo mkongwe wa Bariadi Magharibi.

IPTL, kaa la moto lililoteketeza vigogo kwa miaka 20


Sakata la mkataba wa kampuni ya kuzalisha umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) limezuka tena hivi karibuni baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) kutoa tangazo la kuongeza muda wa leseni ya kampuni hiyo hivi karibuni.
Kashfa ya mkataba wa IPTL uliosainiwa mwaka 1995 imekuwa ikigharimu madaraka ya baadhi ya viongozi kila inapoibuka na hivi karibuni imesababisha Mkurugenzi wa Ewura, Felix Ngamlagosi kusimamiswa kazi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Kashfa hii iliyozalisha kashfa nyingine ya Akaunti ya Tegeta Escrow pia ilisababisha kuvuliwa madaraka kwa mawaziri wa awamu ya nne ambao ni aliyekuwa Waziri Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, huku baadhi ya watendaji wa Serikali na wanasiasa wakiitwa kwenye Tume ya Kijaji kuhojiwa kwa mgawo walioupata.
Chimbuko la IPTL
Mwaka 1994 kulitokea tatizo kubwa la umeme, hivyo Serikali ilitafuta suluhisho la dharura na la kudumu. Mwaka huo, aliyekuwa Waziri wa Mipango marehemu Horace Kolimba alitembelea nchini Malaysia na kuzungumza na wawekezaji katika sekta ya umeme nchini humo na kuwaomba waje nchini kuangalia uwezekano wa kuwekeza ili kupunguza tatizo la umeme.
Agosti 19, 2014, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mechmar, inayomiliki asilimia 70 ya hisa za IPTL, Datuk Baharuden Majid, aliongoza ujumbe mzito kutoka Malaysia kuja kuzungumza na Serikali ya Tanzania.
Walioshiriki katika mazungumzo hayo kwa upande wa Tanzania walikuwa ni pamoja na Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa wakati huo Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Simon Mhaville, Kamishna wa Nishati Msaidizi, Ester Masunzu na Dk Juma Ngasongwa ambaye alikuwa msaidizi wa Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi wa mambo ya uchumi.
Septemba 1994, Mkataba wa Maelewano (MOU) ulifikiwa, licha ya tahadhari kutoka kwa washauri wa Tanesco ambao ni kampuni za Acres (Canada) na Hunton and Williams (Uingereza), kwamba uwekezaji huo ulikuwa ni janga kwa sekta ya umeme na kwa uchumi wa Taifa.
Kampuni hiyo ambayo wamiliki wake ni Mechmar ya Malaysia mwenye asilimia 70 na VIP ya Tanzania yenye asilimia 30 ilisaini mkataba wa miaka 20 (1995-2015) na Serikali ya Tanzania (Tanesco) ambapo kwa mujibu wa mkataba huo endapo kutatokea shauri lolote, uamuzi wa mwisho utatolewa na baraza la usuluhishi la migogoro ya kiuwekezaji (International Centre for Settlement of Investment Disputes-ICSID).
Chini ya mkataba huo, Tanesco ilitakiwa kuilipa IPTL Dola 3.6 milioni sawa na Sh7.92 bilioni kwa mwezi kama ada ya huduma za mtambo.
Juu ya malipo hayo, Tanesco pia inalipa senti 13 (dola) kwa kila uniti ya umeme (sawa na kilowati moja) kwa kuendesha mtambo kwa nusu ya uwezo wake kwa mwezi.
Mikosi yaanza
Kosa la kwanza la IPTL lilikuwa ni kutokamilisha mradi wake mwaka 1995 kwenye kipindi cha dharura na badala yake ikakamilisha mwaka 1998.
Hivyo mwaka 1998 Tanesco ilifungua shauri ICSID ikiilalamikia IPTL kwa kukuza gharama za uwekezaji na hivyo kukuza gharama za umeme.
Mwaka 2001 uamuzi wa ICSID ukatoka ikabainika ni kweli IPTL ilikuza gharama kwa kiasi cha Dola 27milioni.
Mwaka 2002 IPTL ikaanza kuiuzia umeme Tanesco lakini ilipofika mwaka 2004 ikabainika kuwa mwaka 2004 IPTL ilidanganya kuhusu mtaji.
Awali IPTL ilisema asilimia 30 ya mtaji ilikuwa nao kama ‘equity’ sawa na Dola 36 milioni na kwamba asilimia 70 ilikopa. Lakini baada ya ukaguzi ikabainika kuwa IPTL haikuweka dola 36 milioni kama equity bali iliweka dola 50 ambazo kwa wakati zilikuwa sawa na Sh50,000.
Kutokana na kasoro hiyo, Tanesco ikataka gharama ya umeme ishuke kwasababu bei ilizingatia ‘equity’ ya dola 36 milioni.
Mabishano yakaendelea mpaka mwaka 2006 ambapo Serikali ilishinikiza ifunguliwe akaunti maalumu (Tegeta Escrow) ili malipo yawekwe huko mpaka mgogoro utapokwisha kuhusu bei sahihi ndipo pesa hiyo igawanywe kwa kuzingatia bei sahihi kwa pande mbili.
Ilipofika mwaka 2008, IPTL ilishindwa kujiendesha hivyo ikawekwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA).
Hukumu ya Mahakama Kuu iliyotoka Septemba 2013 chini ya Jaji Utamwa iliamua IPTL iondolewe chini ya usimamizi wa Rita na mali zote za IPTL ipewe Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Ltd (PAP) ya Harbinder Singh Sethi.
Sethi aliyetajwa katika rekodi za ufisadi tangu Kenya kwenye kashfa ya Goldenberg mwaka 2002 na hakuwahi kuwa mwekezaji katika sekta ya umeme, akapewa haki na mahakama kuzalisha ikisema atazalisha 500MW na kwamba ataiuzia umeme Tanesco kwa bei nafuu ya dola senti 6 mpaka 8 kwa uniti.
Hukumu hiyo ilitoka huku mmiliki wa asilimia 70 ya IPTL (Mechmar) akiwa mufilisi nchini Malaysia na zaidi ICSID kukiwa na kesi inayohusu mgogoro wa IPTL na Serikali uliofunguliwa na Standard Chartered Bank ambayo ilinunua deni la IPTL mwaka 2005 na ikaruhusiwa kuishtaki Serikali ya Tanzania kwenye baraza hilo lenye mamlaka ya mwisho.
Februari 2014, ICSID ilifanya uamuzi wa awali kwamba ni kweli IPTL inaitoza zaidi Tanesco na kuelekeza pande mbili zikafanye hesabu upya ndani ya siku 90 zilizoisha Mei 2014 kwa lengo la kujua ni kwa kiasi gani IPTL imeipunja Tanesco tangu 2002 mpaka 2013 katika bei.
Hata hivyo, Tanesco na Serikali hawakutoa ushirikiano ndani ya siku hizo 90 kutekeleza uamuzi huo. Inaelezwa kuwa wakati huo aliyekuwa Waziri wa Fedha, marehemu Dk William Mgimwa alikuwa mgonjwa.
Hadi Novemba 2013 wakati mchakato wa kukokotoa malipo hayo, hali ya Dk Mgimwa ilikuwa mbaya hospitalini nchini Afrika Kusini.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu ukaguzi wa Akaunti ya Tegeta Escrow na umiliki wa Kampuni ya IPTL iliyowasilishwa bungeni Novemba 2014 ilionyesha kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Sh306 bilioni na zilitakiwa kurudishwa Tanesco.
Kutokuwepo kwa umakini kwa Serikali kulisababisha Kampuni ya PAP kujimilikisha fedha za IPTL kwa asilimia 70 bila kuwa na ushahidi wowote kwamba iliinunua IPTL ikiwemo malipo ya kodi kama ilivyofanya kwa VIP yenye asilimia 30 za hisa.
Mechmar yenyewe ilikanusha kuuza hisa zake za IPTL kwa kuwa ilikuwa chini ya ufilisi na kuitaka PAP kuonyesha cheti cha hisa.
Pamoja na maelezo hayo, Novemba 26, 2014 aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alilieleza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa fedha za Tegeta Escrow si za umma na kwamba bado Serikali ina mzigo wa madeni katika sakata hilo.
Msimamo huo pia ulitolewa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye aliwahi kunukuliwa akisema kwamba sakata la Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), ni upuuzi.
Kwa upande mwingine, mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira aligawa jumla ya Sh31 bilioni kwa watu binafsi wakiwemo wanasiasa na watendaji wa Serikali na makampuni.
Miongoni mwa waliokiri kupokea fedha hizo ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka aliyepewa Sh1.6 bilioni akisema fedha hizo zilikuwa ni za mchango wa kulipa mkopo wa shule anayoisimamia.
Wengine waliopata fedha hizo ni mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge na wengineo.
Katika vikao vya Bunge wakati wa sakata la Escrow, aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha wakati huo, Mwigulu Nchemba aliwataka wote waliopokea fedha hizo kuthibitisha mapato yao ili wakatwe kodi kutokana na fedha hizo ambazo pia zinapaswa kuhakikiwa na vyombo vya usalama kwamba ni mapato halali.
Hivi karibuni, Ewura imetoa tangazo la kutaka maoni ya wadau kwa ajili ya kuongeza muda wa leseni ya IPTL.
Tangazo hili limezua mjadala mzito miongoni mwa Watanzania wakiwemo wanasiasa na wanaharakati, wakihoji sababu ya IPTL kuongezewa muda.
Wakati mjadala ukiendelea, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kumsimamisa kazi Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, hatua iliyosababisha mamlaka hiyo kutoa tangazo lingine la kusitisha mchakato wa kuongeza leseni ya IPTL.

Acacia kikaangoni, yajibu mapigo


Dar es Salaam. Kamati ya pili iliyoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi katika mchanga wenye madini unaosafirishwa nje imetoa mapendekezo 21 kwa Serikali, ikiwamo kuichukulia hatua za kisheria kampuni ya Acacia ambayo imekuwa ikiendesha shughuli zake nchini kinyume na matakwa ya sheria.
Mapendekezo hayo yote yamekubaliwa na Rais Magufuli na ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuanza mara moja kuwachunguza wote waliohusika katika kulitia Taifa kwenye hasara kubwa kutokana na upotevu wa rasilimali ya madini na kuwachukulia hatua za kisheria.
Hata hivyo, Acacia imeeleza kusikitishwa na matokeo ya ripoti ya pili ya kuchunguza makinikia iliyowasilishwa kwa Rais Magufuli.
Katika maelezo yaliyotolewa jana na kampuni hiyo, ilieleza kusikitishwa na matokeo yaliyotolewa na kamati ya pili na kudai ilijikita katika yaliyobainika kwenye ripoti ya kwanza iliyowasilishwa Mei 24 ambayo waliyakanusha.
“Kamati ilijikita katika kuchunguza sampuli kutoka makontena 44. Katika miaka 20 na takwimu tulizonazo ni vigumu kubainisha uchunguzi huo na iko wazi wameongeza thamani ya makinikia kwa zaidi ya mara 10,” ilieleza taarifa ya Acacia.
Kamati ya pili imeonyesha jinsi Acacia imekuwa haiweki bayana malipo ya kodi na mapato kwa miaka kadhaa ambayo ni mabilioni ya dola za Marekani.
Hata hivyo, kampuni hiyo imekanusha kwa kile ilichoeleza ni tuhuma mpya zilizotolewa.
“Tumekuwa tukifanya biashara zetu kwa kiwango cha juu na kuendesha shughuli zetu kwa kufuata sheria za Tanzania,” ilieleza taarifa yao.
Kamati hiyo iliyoundwa Aprili 10 ilitoa mapendekezo hayo ikiwa ni wiki tatu tangu kamati ya kwanza ilipowasilisha taarifa yake kwa Rais Magufuli, naye akaamua kutengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wake, Profesa Nehemiah Osoro alibainisha mapendekezo mengine kuwa ni Serikali kudai kodi na mrabaha kutoka kwa kampuni zote za madini ambayo yamekwepwa kulipwa na mrabaha stahiki kwa mujibu wa sheria.
Profesa Osoro alisema kampuni nyingi za madini zimekuwa zikiliibia Taifa kutokana na mikataba mibovu wanayoingia na pia kuendesha shughuli zao kwa kukwepa kodi na kutofuata sheria na taratibu nyingine za madini.
“Kuna tatizo kubwa katika mikataba yetu, lakini pia watendaji wetu wamekuwa hawasimamii masilahi ya Taifa. Naweza kusema wanaangalia masilahi binafsi katika kusimamia madini yanayozalishwa nchini,” alifafanua Profesa Osoro.
Mwenyekiti huyo aliishauri Serikali kuendelea kuzuia usafirishaji wa mchanga wenye madini kwenda nje ya nchi mpaka pale kampuni zinazodaiwa zitakapolipa kodi, mrabaha na tozo stahiki kwa mujibu wa sheria.
Mapendekezo mengine yaliyotolewa na kamati ni Serikali kuanzisha utaratibu utakaowezesha ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji wa makinikia (smelter) ili kuondoa upotevu wa mapato na kutengeneza ajira kwa Watanzania.
Kamati hiyo imependekeza Serikali ifanye uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waliokuwa mawaziri, wanasheria wakuu wa Serikali na manaibu wao, wakurugenzi wa idara za mikataba na makamishna wa madini pamoja na wanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini.
Pia, kamati imependekeza kuwa watumishi wengine wa Serikali na watu wote waliohusika katika kuingia mikataba ya uchimbaji madini, utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini na kuongeza muda wa leseni, watumishi na wamiliki wa kampuni za madini, kampuni zilizohusika kuandaa nyaraka za usafirishaji wa makinikia na kampuni za upimaji wa madini kwa kuvunja sheria za nchi na upotoshaji.
Profesa Osoro alitaja mapendekezo mengine ya kamati kuwa ni Serikali kufanya uchunguzi kuhusu mwenendo wa watumishi wa idara ya walipakodi wakubwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwenye kushughulikia madai ya kodi ambayo mabaraza ya rufani ya kodi na mahakama zimekwishayatolea uamuzi.
Mapendekezo mengine ni Serikali kufuta utaratibu wa kupokea malipo ya mrahaba ya asilimia 90 na kusubiri malipo ya asilimia 10 kulipwa baadaye wakati kampuni za madini zinauza madini na kupewa fedha taslimu kwa mkupuo.
Kamati hiyo imependekeza pia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ifuatilie malipo ya fedha za kigeni yanayotokana na mrahaba kwa mauzo ya madini, jambo ambalo lilikuwa halifanyiki kwenye sekta ya madini kwa muda mrefu.
Profesa Osoro aliongeza kuwa Serikali ianzishe utaratibu wa kulinda maeneo ya migodi na viwanja ndege vilivyopo migodini ili kudhibiti vitendo vya hujuma vinavyoweza kufanywa na kampuni za migodi ikiwamo utoroshaji wa madini.
Kamati hiyo iliyotumia miezi miwili kukamilisha ripoti yake, imependekeza Serikali kupitia wataalamu wabobezi katika majadiliano na mikataba wapitie mikataba yote mikubwa ya uchimbaji madini na kufanya majadiliano na kampuni za madini ili kuondoa misamaha yote ya kodi isiyokuwa na tija kwa Taifa na badala yake kuweka masharti yenye tija kwa pande zote mbili kwa kuzingatia masilahi ya nchi.
Mapendekezo mengine yaliyotolewa na kamati yalitaka mabadiliko ya sheria ya madini ikiwa ni pamoja na kuongeza kiwango cha adhabu kwa makosa ya ukiukwaji wa sheria ya madini na sheria ya kodi.
Mabadiliko mengine ni sheria kuweka kiwango cha asilimia za hisa ambazo zitamilikiwa na Serikali; kutamka bayana kuwa madini ni mali asili ya Watanzania na iwekwe chini ya udhamini wa Rais na mikataba yote ya uchimbaji wa madini isiwe ya siri na iridhiwe na Bunge.
Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema sheria pia iondoe mamlaka ya waziri wa Nishati na Madini, kamishna wa madini na maofisa wa madini na iweke masharti kwa waombaji leseni ya uchimbaji kuonyesha mchanganuo wa mafunzo kwa wazawa.
Mabadiliko mengine yaliyopendekezwa na kamati ni sheria ielekeze kampuni za madini kuweka fedha zinazotokana na mauzo ya madini katika benki zilizopo nchini.
“Serikali iunde chombo cha kusimamia biashara ya usafirishaji bidhaa nje ya nchi kupitia bandari kama lilivyokuwa shirika la Nasaco ili kudhibiti biashara haramu na kuondoa mianya ya ukwepaji kodi,” alibainisha Profesa Osoro.
Pia, kamati imependekeza kuwa Serikali ipitie na kufanya marekebisho au kufuta na kubadili kabisa sheria ya madini na sheria za kodi ili kuondoa pamoja mambo mengine masharti yote yasikuwa na manufaa kwa Taifa ikiwa ni pamoja na yaliyomo kwenye kifungu thabiti.
Vilevile kamati hiyo imemtaka kamishna wa madini kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa kampuni za madini ili kuhakikisha uzingatiaji wa ukiukwaji wa sheria na kuchukua hatua.

Ripoti ya makinikia yaibua uozo wa mikataba ya madini


Kamati ya pili iliyoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza masuala ya kiuchumi na kisheria kwenye makinikia iliyotolewa jana imeibua uozo uliopo kwenye mikataba ya madini, huku ikifichua kutosajiliwa kwa kampuni ya Acacia Mining inayojinasibisha kuwa mmiliki wa kampuni za Bulyanhulu Gold Mines, North Mara Gold Mine na Pangea Minerals.
Ripoti hiyo ilitanguliwa na ripoti ya kwanza iliyokabidhiwa Mei 21 kwa Rais Magufuli ikieleza upungufu katika mapato ya madini.
Akiwasilisha ripoti hiyo jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Nehemiah Osoro alisema kampuni hiyo haikuwahi kuandikishwa Tanzania.
“Kamati imebaini na kuthibitisha kwa mujibu wa nyaraka na maelezo kutoka ofisi ya msajili wa makampuni (Brela) kuwa kampuni ya Acacia Mining Plc haikusajiliwa nchini Tanzania na wala haina hati ya utambuzi kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni, Sura ya 212,” alisema Profesa Osoro.
Alisema kamati yake pia imebaini kampuni hiyo haikuwahi kuwasilisha nyaraka wala taarifa yoyote kuonyesha kuwa ni mmiliki wa kampuni zinazomiliki wala kuwa na hisa katika kampuni hizo.
“Kwa kuwa Acacia Mining Plc haina usajili wala utambuzi wa kisheria nchini Tanzania, haina sifa ya kupata leseni, kuchimba wala kufanya biashara ya madini nchini Tanzania. Hivyo basi, kamati imebaini kuwa Acacia Mining Plc, inafanya biashara ya madini hapa nchini kinyume cha sheria za nchi,” alisema.
Kuhusu biashara ya uuzaji na usafirisaji wa makinikia nje ya nchi, Profesa Osoro alisema uuzwaji wake umekuwa ukifanyika kwa udanyanyifu Bulyanhulu Gold Mines Ltd na Pangea Minerals Ltd.
“Jumla ya thamani ya madini katika makontena 44,077 yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 1998 hadi 2017 kwa kutumia kiwango cha wastani cha Sh132.56 trilioni au Sh229.9 trilioni kwa kiwango cha juu,” alisema Profesa Osoro.
Kuhusu thamani ya madini yaliyomo kwenye makinikia katika makontena 61,320 yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi cha kati ya 1998 na 2017 kwa kutumia kiwango cha wastani ni Sh183.597 trilioni.
“Jumla ya thamani ya madini katika makontena 61,320 yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi kati ya 1998 na 2017, kwa kutumia kiwango cha juu ni Sh380.499 trilioni,” alisema.
Aliongeza kuwa jumla ya mapato ya Serikali ambayo ilipoteza ni Sh68.59 trilioni ambazo ni sawa na bajeti ya miaka miwili ya Serikali kwa kigezo cha makadirio ya mwaka 2017/2018. “Robo ya fedha hizo zingetosha kujenga reli ya standard gauge kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza,” alisema Profesa Osoro.
Kiasi cha mapato ambacho Tanzania imepoteza (kiwango cha juu) ni Sh108.46 trilioni ambazo ni sawa na bajeti inayokaribia miaka mitatu ya Serikali kwa kigezo cha makadirio ya matumizi ya mwaka 2017/2018 na gharama ya kujenga reli ya standard gauge kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Kuhusu uchenjuaji wa makinikia nje ya nchi, Profesa Osoro alisema kamati hiyo ilisoma mikataba ya mauzo kati ya kampuni za uchimbaji na wachenjuaji na kugundua kuwa Serikali siyo sehemu ya mikataba hiyo, licha ya kuwapo na salio la kodi katika makinikia hayo. “Kwa msingi huo, taarifa ambazo zimekuwa zikiwasilishwa kwa TMAA (Wakala wa Ukaguzi wa Madini) baada ya kuomba taarifa hizo kutoka makampuni ya madini hazina ukweli na hazibebi takwimu sahihi kuhusu aina, kiasi na thamani ya madini yaliyochenjuliwa ambazo zingewezesha TRA kutoza kodi stahiki,” alisema Profesa Osoro.

Monday, June 12

TAARIFA YA KAMATI YA PILI YA KUCHUNGUZA MAKINIKIA ILIYOTOLEWA KWA RAIS MAGUFULI 12 JUNI, 2017

RAIS DKT MAGUFULI APATA PICHA ZA PAMOJA NA VIONGOZI BAADA YA KUPOKEA RIPOTI TA MAKANIKIA IKULU DAR ES SALAAM LEO


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Spika Job Ndugai,  Kaimu Jaji Mkuu Profesa Ibrahim wakiwa katika picha na kamati ya Rais ya pili ya kuchunguza makinikia na mustakabali wa sekta ya madini nchini baada ya kupokea ripoti yao Ikulu Dar es salaam leo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Spika Job Ndugai,  Kaimu Jaji Mkuu Profesa Ibrahim wakiwa katika picha na kamati ya Rais ya pili ya kuchunguza makinikia na mustakabali wa sekta ya madini nchini na vingozi wa vikosi vya Ulinzi na Usalama baada ya kupokea ripoti yao Ikulu Dar es salaam leo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Spika Job Ndugai,  Kaimu Jaji Mkuu Profesa Ibrahim wakiwa katika picha na kamati ya Rais ya pili ya kuchunguza makinikia na mustakabali wa sekta ya madini nchini na vingozi wa vikosi vya Ulinzi na Usalama na baadhi ya wanahabari baada ya kupokea ripoti yao Ikulu Dar es salaam leo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Spika Job Ndugai,  Kaimu Jaji Mkuu Profesa Ibrahim wakiwa katika picha na kamati ya Rais ya pili ya kuchunguza makinikia na mustakabali wa sekta ya madini nchini na viongozi wa dini baada ya kupokea ripoti yao Ikulu Dar es salaam leo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Spika Job Ndugai,  Kaimu Jaji Mkuu Profesa Ibrahim wakiwa katika picha na kamati ya Rais ya pili ya kuchunguza makinikia na mustakabali wa sekta ya madini nchini na wakuu wa Mikoa baada ya kupokea ripoti yao Ikulu Dar es salaam leo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Spika Job Ndugai,  Kaimu Jaji Mkuu Profesa Ibrahim wakiwa katika picha na kamati ya Rais ya pili ya kuchunguza makinikia na mustakabali wa sekta ya madini nchini na viongozi wa vyama vya siasa baada ya kupokea ripoti yao Ikulu Dar es salaam leo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Spika Job Ndugai,  Kaimu Jaji Mkuu Profesa Ibrahim wakiwa katika picha na kamati ya Rais ya pili ya kuchunguza makinikia na mustakabali wa sekta ya madini nchini na wabunge baada ya kupokea ripoti yao Ikulu Dar es salaam leo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Spika Job Ndugai,  Kaimu Jaji Mkuu Profesa Ibrahim wakiwa katika picha na kamati ya Rais ya pili ya kuchunguza makinikia na mustakabali wa sekta ya madini nchini na wazee wa jiji baada ya kupokea ripoti yao Ikulu Dar es salaam leo.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Spika Job Ndugai,  Kaimu Jaji Mkuu Profesa Ibrahim wakiwa katika picha na kamati ya Rais ya pili ya kuchunguza makinikia na mustakabali wa sekta ya madini nchini na wawakilishi wa Sekta binafsi baada ya kupokea ripoti yao Ikulu Dar es salaam leo.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Spika Job Ndugai,  Kaimu Jaji Mkuu Profesa Ibrahim wakiwa katika picha na kamati ya Rais ya pili ya kuchunguza makinikia na mustakabali wa sekta ya madini nchini kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Dar es salaam baada ya kupokea ripoti yao Ikulu leo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan, Spika Job Ndugai,  Kaimu Jaji Mkuu Profesa Ibrahim wakiwa katika picha na kamati ya Rais ya pili ya kuchunguza makinikia na mustakabali wa sekta ya madini nchini na wasanii wa Tanzania All stars baada ya kupokea ripoti yao Ikulu Dar es salaam leo.

HOTUBA YA RAIS DKT MAGUFULI BAADA YA KUPOKEA RIPOTI YA KAMATI YA PILI YA MADINI JUNE 12, 2017


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Taarifa ya Kamati ya pili ya Uchunguzi wa Madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga unaosafirishwa nje ya nchi kutoka kwenye machimbo ya madini sehemu mbalimbali hapa nchini kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Profesa Nehemiah Osoro Ikulu jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akionesha Ripoti hiyo ya Kamati ya pili ya Uchunguzi wa Madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga unaosafirishwa nje ya nchi kutoka kwenye machimbo ya madini sehemu mbalimbali hapa nchini mara baada ya kukabidhiwa Ikulu jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na kulia ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakishuhudia.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Ripoti hiyo ya Kamati ya Pili ya Uchunguzi wa Madini Ikulu jijini Dar es Salaam.

SERENGETI, NGORONGORO NA KILIMANJARO SI VIVUTIO PEKEE VINAVYOPATIKANA TANZANIA

kwa mujibu wa issa michuzi blog

Watalii wanaokuja Tanzania na kuelekea moja kwa moja kwenye hifadhi za taifa za Serengeti, Kilimanjaro au Ngorongoro inamaanisha nini? Ni kwamba wanakuwa wamekwishaambiwa kuwa ukifika Tanzania sehemu pekee za kutembelea ni hizo tu? Je tunawezaje kukabiliana na hali hii ambayo kwa namna moja ama nyingine inaweza kufifisha vivutio vilivyopo maeneo mengine nchini kutotembelewa?
Hakuna anayeweza kubisha kwamba sehemu ya Kaskazini mwa Tanzania imebarikiwa kwa kiasi kikubwa kuwa na vivutio visivyopatikana duniani kote. Vivutio kama hifadhi za kitaifa za Serengeti, bonge la Ngorongoro, Mlima Kilimanjaro na hivi karibuni mti mrefu zaidi barani Afrika uligunduliwa.

Tunapenda kukufahamisha kwamba tangu mwaka huu wa 2017 uanze nchi yetu imeshuhudia watu mbalimbali maarufu duniani wakifurika nyanda za Kaskazini wakiwemo Waziri Mkuu mstaafu wa Israel, Bw. Ehud Barak, muigizaji wa filamu kutokea Hollywood nchini Marekani, Will Smith na familia yake.

Kama hiyo haitoshi hazijapita hata wiki mbili tangu aliyekuwa nguli wa kusakata kabumbu nchini Uigereza, David Beckham ambaye aliwahi kuvichezea vilabu vya Manchester United, Real Madrid, LA Galaxy na PSG naye kutembelea hifadhi ya mbuga ya Serengeti akiwa na familia yake.

Huyo hakuwa mchezeji pekee kutokea bara la Ulaya kufanya hivyo kwani nyota anayechezea kwa mkopo katika klabu ya Crystal Palace inayoshiriki ligi kuu ya Uingereza akitokea Liverpool, Mamadou Sakho naye pamoja na mkewe na watoto wake wa kike wawili wameonekana wakifurahi mapumziko yao katika hifadhi ya mbuga ya wanyama ya Serengeti.
Jambo la msingi la kujiuliza hapa ni kwanini watu hao wote mashuhuri pindi tu watuapo uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwl. Nyerere hubadilisha ndege na kuelekea moja kwa moja uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro ambapo kutokea pale ni rahisi kwenda hifadhi za kitaifa za Serengeti, Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro?

Tunafahamu kwamba suala la watalii kutembelea sehemu wanazozitaka wanapofika nchini Tanzania ni maamuzi yao na pia huchangiwa na sababu kadhaa kama vile vivutio miundombinu kama vile usafiri, hoteli zenye hadhi na kuvutia lakini pia na hali ya hewa kinaweza kuwa kigezo kingine.

Kwa kuzingatia sababu za miundombinu na huduma bora za malazi na zenye viwango vya kimataifa, hakuna ubishi kwamba nyanda za Kaskazini zimejitahidi kwa kiasi kikubwa kukidhi mahitaji ya watalii. Lakini linapokuja suala la vivutio vya kitalii na hali ya hewa bado Tanzania tumejaaliwa vivutio vya kila aina na hali ya hewa nzuri karibuni kila mikoa ya nchi hii.

Kwa mfano, ukitembelea mikoa ya Magharibi utakutana hifadhi za Gombe, Katavi, Mahale, Rubondo na Saanane. Kwa ukanda wa Mashariki kuna fukwe safi za bahari ya Hindi, visiwa vya Zanzibara, hifadhi ya Saadani, kisiwa cha Kilwa, mapango ya Amboni (Tanga) na Mikindani (Mtwara). Wakati ukienda Kusini mwa Tanzania yapo mengi ya kufurahi na kuyaona katika hifadhi za Kitulo, Mikumi, Ruaha na Udzungwa.
Utajiri wa maliasili unaopatikana katika hifadhi hizo hapo juu ni Dhahiri kwamba nchi ya Tanzania haijabarikiwa sehemu chache pekee. Bali tu ni namna tunavyovitangaza, kuvitolea elimu ya kutosha na kuvipa kipaumbele kwa wageni na watalii kuvitembelea.

Yapo mambo kadhaa ya kujifunza kutokana na ugeni wa watu hao mashuhuri kupendelea kuzuru baadhi ya sehemu tu nchini.

Kwanza kabisa, kuwa na vivutio pekee haitoshi kuwashawishi watalii kuja nchini kuvitembelea bila ya kuvitangaza. Dunia kwa sasa ina takribani zaidi ya nchi 190 na zote hizo zikiwa na vivutio vya kila namna. Watalii hawawezi kutembelea sehemu kama hawajafahamishwa ina mambo gani yatakayowavutia na kushawishika kutoka huko walipo. Hivyo basi badala ya kutegemea watalii na watu mbalimbali kusikia sifa za vivutio tulivyonavyo Tanzania kutoka kwa watu wao wa karibu, serikali na wananchi tunaowajibu wa kuvitangaza vivutio vyetu.
Lakini pia, sekta ya utalii kwa kiasi kikubwa huendena na uwepo wa miundombinu ya kisasa na ya kuvutia itakayowawezesha watalii kuvifikia vivutio na kufarahia muda wao pindi wanapokuwepo huko. Hapa tunazungumzia miundombinu kama vile usafiri na huduma za malazi kitu ambacho mikoa ya Kaskazini imejitahidi kuwekeza kwa kiasi kikubwa. Uwepo wa uwanja wa ndege kimataifa wa Kilimanjaro, barabara na hoteli kadhaa zenye hadhi na viwango vya kimataifa ni vichocheo vikubwa kwa watalii kupenda kutembelea vivutio vya huko.

Hivyo basi kwa kumalizia, bado serikali na wananchi kwa ujumla tunalo jukumu la kuvitangaza na kuvilinda vivutio tulivyonavyo. Kwa kuvitangaza tunaweza kulifanikisha hilo kwa kuvitembelea na kuwajulisha watu wetu wa karibu juu ya mambo yanayopatikana huko. Pongezi kwa serikali kwani siku chache zilizopita katika kuadhimisha siku ya mazingira duniani ilitoa ofa kwa watanzania wote kutembelea hifadhi za mbuga za wanyama bila ya kiingilio chochote kwa siku tatu mfululizo ili kujionea mazingira na maliasili tulizojaaliwa.

JPM: Tumepoteza zaidi ya Sh68 trilioni za kodi


Thamani ya kodi ambayo haikulipwa na kampuni za uchimbaji madini ni kati ya Sh trilioni 68 hadi 108.5.
Hayo yameelezwa na Rais John Magufuli, leo Jumatatu baada ya kukabidhiwa ripoti ya pili ya mchanga wa madini.
Pia Rais amesema anashangazwa na jinsi mawaziri wa sekta za madini na wadau wengine wa sekta hiyo ambavyo hawajawahi kufikiria kuitembelea mashine ya uchenjuaji (smelter) inayotajwa na kampuni za madini.
“Kila siku wanaomba vibali vya kusafiria lakini hawakosei wakaenda kuiangalia mashine hiyo inayochenjua mamchanga yetu,” amesema.
 Tutaendelea kuwajuza yanayojiri Ikulu leo

JPM amtaja Dalaly Kafumu sakata la mchanga wa madini

Rais John Pombe Magufuli (JPM) amesema aliyekuwa Kamishna wa Madini, Dk Dalaly Kafumu alikwenda kujaribu kufanya ujanja ili ripoti ya pili ya mchanga wa madini ibadilishwe lakini hakuweza.
Kafumu kwa sasa ni Mbunge wa Igunga(CCM) ambaye alijiuzulu kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini mapema mwaka huu.
Rais Magufuli, ameyasema hayo leo Jumatatu wakati akipokea ripoti ya pili ya mchanga wa madini Ikulu na kueleza kuwa ameyasoma na kuyakubali mapendekezo yote yaliyotolewa na kamati hiyo.
“Ninawashukuru viongozi wa vyama mbalimbali ambao mmetoa ushirikiano katika hili, hizi fedha ni nyingi sana na zikienda hospitali zinawatibu wote,” amesema.
“ Haya madini hayana vyama.” Aliongeza.

Magufuli aitaka Acacia itubu na kuanza upya


Rais John Magufuli amesema iwapo kampuni ya uchimbaji wa madini ya Acacia ikitubu na kukubali makosa yake, serikali ipo tayari kwa majadiliano lakini kwa sasa hakuna mchanga  wa madini utakaotoka nje ya nchi.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo (Jumatatu) Ikulu baada ya kukabidhiwa ripoti ya pili ya mchanga wa madini.
Amewataka Acacia kuomba leseni upya lakini kwa makosa yaliyoonekana hawana budi kuilipa Serikali.
Pia amewataka wanasheria wa nchi hii wasimame pamoja kwani suala hili ni kwa ajili ya maslahi mapana ya taifa hili.
Amemtaka Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi, aunde timu ya wanasheria waaminifu, wasiokubali kuhongwa na kisha sheria hizo zipelekwe bungeni na zijadiliwe  
“Hata kama kipindi cha bunge kitaongezwa, lakini wanasheria wapitie sheria hizo kifungu kwa kifungu ili mradi lipatikane suluhisho,” amesema.
Ameongeza: “Tukiendelea kukaa kimya tutaliangamiza taifa, tutakuja kujibu mbele za Mungu ‘its so painful, really painful.”
Amesema ukienda maeneo mengi hapa Dar es Salaam, mikoani utaona jinsi Watanzania wanavyoishi katika mateso na hata wakati alipokuwa akipita mikoani kuomba kura za urais aliona mateso ya Watanzania. “Nilifikia wakati nikajiuliza naomba hii kazi ya nini.”