Wednesday, August 12

CCM, Ukawa gumzo


Mikutano ya CCM (kushoto) na Chadema (kulia) 
iliyofanyika nchini hivi karibuni. 

Dar es Salaam. Mazungumzo kuhusu siasa na hasa Uchaguzi Mkuu, idadi ya watu waliojitokeza kujiandikisha kupiga kura na idadi kubwa ya watu wanaojitokeza kwenye mikutano ya hadhara ya wanasiasa ndiyo hali iliyoenea kila kona ya nchi kwa sasa, kitu ambacho wachambuzi waliohojiwa na gazeti hili wamekielezea kuwa ni kuongezeka kwa mwamko wa wananchi katika masuala ya siasa.
Wachambuzi hao, ambao waliohojiwa na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wameeleza kuwa mwamko huo pia unatokana wananchi kutaka mabadiliko, uamuzi wa kada wa CCM, Edward Lowassa kuhamia Chadema na umoja wa vyama vya upinzani ambavyo vimeamua kuunganisha nguvu kwenye uchaguzi, kitu ambacho kimewafanya wananchi waone kunaweza kuwa na ushindani wa kweli safari hii.
Tangu mchakato wa uchaguzi uanze ndani ya vyama, mazungumzo ya wananchi wa kawaida kwenye mikusanyiko mbalimbali kama sokoni, maskani, kwenye vyombo vya usafiri na mitandao ya jamii imekuwa ikitawaliwa na siasa na hasa baada ya CCM kuanza kutafuta mgombea wake wa urais.
Ufuatiliaji huo wa habari za siasa uliongezeka zaidi baada ya kumteua Dk John Pombe Magufuli kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho tawala na jina la Lowassa kutoingia tano bora, kitu kilichomfanya atangaze kujivua uanachama na kuhamia Chadema.
Wanasiasa hao wawili pia wamevuta maelfu ya watu kwenye mikutano yao ya kutambulishwa kwa wanachama, kutangaza kuhama chama na kuchukua fomu za kuwania urais, huku mbunge wa zamani wa Chadema, Zitto Kabwe akivuta mamia ya watu kwenye mikutano yake ya kukitangaza chama kipya cha ACT Wazalendo.
Idadi ya watu wanaotangaza kuhama chama kimoja na kwenda kingine imekuwa ikiibua mijadala mara kwa mara, huku bendera za vyama vikuu vya kisiasa—CCM, Chadema, CUF na NCCR Mageuzi—zikipepea maeneo mengi.
Wakati mwaka 2010 waliojiandikisha kupiga kura mwaka 2010 walikuwa milioni 11.5, mwaka huu idadi inaweza kuwa maradufu baada ya makisio ya watu waliotarajiwa kujitokeza kujiandikisha kuwa milioni 24 huku Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikieleza kuwa imefikia idadi iliyotarajiwa au kupita malengo kwenye baadhi ya mikoa.
Pamoja na ukweli kwamba kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25 kinatakiwa kitawaliwe na habari na mijadala ya kisiasa, wachambuzi wanazungumzia mwamko wa mwaka huu kuwa ni mkubwa zaidi kulinganisha na chaguzi zilizopita.
Kauli za wasomi
Akizungumza na Mwananchi kuhusu hali hiyo ya siasa kushika nafasi kubwa katika mijadala mbalimbali, Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha (Ruco) alisema wananchi sasa wameamka na kutambua haki yao ya kupigakura, na hivyo wanataka kuitumia kudai mabadiliko waliyoyakosa kwa muda mrefu.
“Kuongezeka kwa umasikini, vijana kukosa ajira, ufisadi na kuongezeka kwa rushwa kumewaamsha wananchi kwa kiasi kikubwa na kuamka kwao kunatokana na kukua wa utandawazi,” alisema Profesa Mpangala.
“Ukiongea na wananchi wengi, wanakwambia kuwa wanataka mabadiliko. Wana matatizo mengi na wanaamini kuwa wakichagua kiongozi mzuri anaweza kuondoa matatizo yanayowakabili.”
Hata hivyo, Profesa Mpangala alisema tatizo lililopo ni wananchi kuamini kuwa mtu mmoja ataweza kuwaletea mabadiliko na kusahau kuwa mabadiliko watayaleta wenyewe, akieleza kuwa ili mabadiliko yatokee ni lazima kubadilisha mfumo wa utawala.
“Wanatakiwa kutazama mfumo maana chama kitakachoingia Ikulu kitaweza kuleta mabadiliko kama mfumo wa utawala utakuwa mzuri. Chama kinaweza kuwa na mgombea mzuri, lakini akashindwa kuleta kipya kwa sababu ya mfumo,” alisema.
Kauli ya Profesa Mpangala juu ya Watanzania kutaka mabadiliko inaungwa mkono na Richard Mbunda ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambaye alisema mwamko huo pia unatokana na ugumu wa maisha kwa watu wengi.
“Ninatembea maeneo mbalimbali ya nchi yetu na kuzungumza na watu. Nilichokibaini ni wananchi kuchoshwa na maisha wanayoishi. Wanahoji wazi iweje maisha yao yawe duni na ya wengine yawe ya juu. Watanzania sasa si watu wa kufuata upepo tu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,” alisema Mbunda.
“Wanaona tatizo kubwa tulilonalo ni la kimfumo na wanaamini kuwa wakichagua kiongozi wa aina fulani hali yao ya maisha itabadilika.”
Alisema kitendo cha Ukawa kumsimamisha Lowassa kimeibua changamoto mpya kwa sababu ni mgombea anayekubalika na watu wengi na wengi wanaamini kuwa akiwa rais ataweza kuwavusha.
“Hata Magufuli amefanya mengi ikiwa ni pamoja na kujenga barabara nyingi na wananchi wanamfahamu. Wagombea hawa wanaufanya uchaguzi wa mwaka huu kuwa wa kihistoria,” alisema.
Dk Benson Bana ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) naye alimtaja Lowassa kama chachu inayowafanya Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi.
“Mabadiliko ni hali ya kutoka katika hali uliyokuwa nayo kwenda katika hali nzuri zaidi. Watu hawajaanza kuyataka mabadiliko leo, wamekuwa wakiyataka kila uchaguzi. Wapo wanaomuonea huruma Lowassa na kuona kuwa dhamira yake ya kuhama CCM kwenda Chadema ni ya kweli na kuna jambo anataka kulifanya,” alisema.
Alisema CCM imekaa madarakani kwa muda mrefu na kufikia hatua ya kujisahau, jambo ambalo linawafanya wananchi kutaka mabadiliko.
“Binadamu siku zote hupenda mabadiliko. Hili suala la watoto wa viongozi nao kupewa uongozi, wananchi wanaliona na linawaudhi na wanaona CCM kama uwanja fulani hivi wa kubebana. Hawasemi tu ila wanayaona haya na wanayatafakari,” alisema.
“Mfumo wa CCM kujiendesha unatakiwa kutazamwa upya maana chama kineonekana kama cha (katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman) Kinana na (katibu wa itikadi na uenezi wa CCM), Nape (Nnauye),” alisema na kusisitiza kuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula amebaki kushughulikia masuala ya nidhamu. Hivi utapata kura kwa kushughulikia nidhamu?”
Alisema wanachotakiwa kukifanya Watanzania ni kuzichambua sera za CCM na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kama zinaweza kutatua matatizo yanayowakabili, si kutazama sifa za mgombea mmoja mmoja.
“Wagombea wote wanakuja na lugha za kuwasaidia machinga, waendesha bodaboda, mamantilie na tatizo la ajira. Hizo ni lugha za kutafuta kura tu. Wanachotakiwa kutueleza wagombea wote ni mkakati watakaoutumia kumaliza matatozo hayo,” alisema.
Hoja za kuwapo mwamko pia zilitolewa na mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala na mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Hamad Salim.
“Watanzania wanataka mabadiliko na wapo wanaodhani watayapata kupitia CCM na wanaodhani watayapata nje ya CCM kutokana na kuyasubiri ndani ya chama hicho tawala kwa muda mrefu,” alisema Salim.
Alisema kitendo Lowassa kuhamia Ukawa kumeibua mihemko na ushindani mpya wa kisiasa nchini, na kwamba hilo limekuwa moja ya sababu ya wananchi wengi kujiandikisha.
“Ila si wote wanaojiandikisha kupigakura watapiga kura kuchagua viongozi, wapo watakaotumia shahada zao katika masuala yao binafsi,” alisema.
Profesa Damiani Gabagambi wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine(Sua) anaouona mwamko huo kwa vijana waliozaliwa mwishoni mwa miaka ya tisini na mwanzoni mwa miaka ya tisini, akisema wengi wanataka mabadiliko lakini hawajui yataletwaje.
“Miaka ya nyuma wananchi walikuwa hawapigi kura wakiamini kuwa nguvu ya upinzani ni ndogo, ila kitendo cha vyama vinne kuungana na kusimamisha mgombea mmoja kimewazindua  na sasa wanauona ushindani wa kweli. Ila wapo waliojiandikisha ili wapate shahada tu kwa matumizi mbalimbali,” alisema.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, watu saba wamejitokeza kuwania urais kumrithi Rais Jakaya Kikwete ambaye amemaliza vipindi vyake viwili vya miaka mitano kila kimoja.
Wakati CCM imemsimamisha Dk Magufuli, vyama vinne vinavyounda Ukawa vimekubaliana kumsimamisha Lowassa, hali inayofanya uchaguzi wa mwaka huu uonekane kuwa ni vita vya kihistoria baina ya wawili hao.
Pia mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila amechukua fomu za kugombea urais sambamba na Chifu Lutayosa Yemba (ADC), Macmillan Lyimo (TLP), Hashimu Rungwe (Chauma) na Fahami Dovutwa (UPDP).
Mgombea wa nane anatarajiwa kutoka chama kipya cha ACT Wazalendo.

Daktari: Mbowe yuko salama


“Ninachoweza kuwaambia Watanzania, 
niko salama na hali yangu inaendelea vizuri, 
tatizo  nililonalo limetokana na kufanya kazi usiku na mchana bila kupumzika.” 
Freeman Mbowe. 

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe kuugua ghafla akiwa kwenye maandaamano na kuwahishwa hospitali ya Taifa Muhimbili, imebainika kuwa hali hiyo imesababishwa na kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika.
Daktari bingwa wa Moyo Kitengo alicholazwa kiongozi huyo, Dk Tulizo Sanga alieleza kuwa baada ya jopo la madaktari wanane kumfanyia uchunguzi waligundua kwamba tatizo kubwa lililokuwa likimsumbua Mbowe ni uchovu ambalo kitaalam linaitwa ‘Fatigue’.
“Jopo la madaktari lilimfanyia vipimo na tumegundua kuwa tatizo kubwa linalomsumbua ni uchovu unaosababishwa na kusafiri na kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika.
“Uamuzi uliochukuliwa ni kumuweka mapumziko kwa ajili ya uangalizi zaidi ndani ya saa 48 lakini hali yake inaendelea vizuri anaweza kuruhusiwa muda wowote,” alisema Dk Sanga
Dk Sanga alieleza kuwa Mbowe alipokelewa hospitalini hapo kwenye kitengo cha magonjwa ya dharura akitokea katika hospitalia ya Doctors Plaza iliyopo Kinondoni.
Mwananchi lilishuhudia viongozi kadhaa wa upinzani wakiwasili katika Jengo la Moyo kumjulia hali kiongozi huyo.
Baadhi ya viongozi walioonekana ni Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Juma Duni Haji, Godbless Lema, Joshua Nassari na Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia.
Kwa upande wake, Mbowe aliwatoa hofu watanzania na kuwahakikishia kwamba yupo salama na waondokane na hofu ambayo imeonekana kuenea kwenye mitandao na vyombo vya habari.
“Hakuna hali yoyote ya hofu na wasiwasi kama ambavyo imeshaanza kujengeka kwenye mitandao ya kijamii nipo hospitali kwa sababu za kitabibu na si vinginevyo.
“Ninachoweza kuwaambia Watanzania niko salama na hali yangu inaendelea vizuri, tatizo nililonalo limetokana na kufanya kazi usiku na mchana bila kupumzika,” alisema Mbowe.
Akizungumza na wanahabari Mbatia aliwata watanzania kuendelea kumuombea kiongozi huyo na kuwaunga mkono Ukawa ili waendeleze harakati zao katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.
“Suala la kuugua ni kawaida kwa kila binadamu ninachoweza kusema tuondelee kumuombea ili arejee kwenye mapambano na wazidi kutuunga mkono kwenye harakati zetu”alisema Mbatia
Kuhusiana na uwezekano wa ugonjwa wa Mbowe kusitisha ziara za Ukawa mikoani Mbatia alisema ratiba inaendelea kama kawaida na afya ya kiongozi huyo ikitengemaa ataungana na wenzake kwenye harakati hizo.
Mbowe aliugua ghafla juzi akiwa katika maandamano ya kumsindikiza mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa baada ya kuchukua fomu za kugombea urais katika Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC).

CCM yatengua matokeo majimbo ya vigogo

Nape Nnauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM 

Dodoma/Dar. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetengua matokeo ya kura za maoni na kuamuru kurudiwa kwa uchaguzi katika majimbo matano, baada ya kubaini kulikuwa na ukiukwaji wa kanuni.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema jana kuwa Kamati ya Maadili iliyoketi juzi hadi usiku, iliamua majimbo ya Kilolo (Iringa), Makete (Njombe),  Rufiji (Pwani), Ukonga (Dar es Salaam) na Jimbo la Busega mkoani Simiyu yarudie uchaguzi.
“Siyo kwamba Kamati Kuu ilikuwa inapitia rufaa pekee bali tulikuwa tunaangalia mambo yote yaliyotokea na kuona namna bora ya kufanya, ndiyo maana tumekubaliana lazima uchaguzi huo urudiwe katika majimbo hayo Alhamisi (kesho) Agosti 13, mwaka huu,” alisema Nape.
Kilichotokea
Ingawa Nape alikataa kutaja kasoro zilizojitokeza katika majimbo hayo akisema hayo ni mambo ya ndani ya chama, kumekuwapo na  malalamiko ya vitendo vya rushwa katika majimbo mbalimbali nchini, hali iliyosababisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwakamata baadhi ya watuhumiwa.
Kilolo
Katika jimbo la Kilolo, kurudiwa kwa kura za maoni si jambo geni kwani hata mwaka 2010 uchaguzi huo ulirudiwa kati ya Profesa Peter Msolla na Venance Mwamoto aliyekuwa anamaliza kipindi chake wakati huo na Msolla kuibuka mshindi.
Jambo hilo limejirudia mwaka huu baina ya wagombea hao, baada ya Profesa Msolla anayemaliza muda wake kugomea kusaini matokeo ya uchaguzi, akidai kuwapo udanganyifu baada ya kuangushwa na Mwamoto.
Katika uchaguzi huo uliohusisha wagombea 15, Mwamoto alipata kura 11,200 wakati Profesa Msolla akipata kura 10,014. Kama ilivyokuwa katika majimbo mengine, tuhuma za rushwa na uvunjaji taratibu ziliripotiwa wakati wa mchakato huo.
Hata baada ya Profesa Msolla kugomea matokeo, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga alisisitiza kuwa kitendo hicho hakizuii vikao vya kamati ya CCM ngazi ya mkoa na wilaya kufanyika na kwamba matokeo hayawezi kubadilishwa wala uchaguzi kurudiwa.
Ukonga
Moja ya majimbo yaliyotawaliwa na madai ya rushwa na ukiukwaji wa taratibu lilikuwa Ukonga ambalo Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa alipata ushindi wa kura 10,000 dhidi ya mpinzani wake Ramesh Patel aliyepata kura 7,356 wakati Robert Masegesi aliambulia 548.
Hata baada ya ushindi huo wa Silaa, kuliibuka utata wa matokeo baada ya wagombea kutuhumiana kuchakachukua. Slaa alipoulizwa jana kuhusu uamuzi huo, alisema yeye si msemaji wa CCM, aulizwe Nape.
Makete
Licha ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Binillith Mahenge kutangazwa mshindi wa kura za maoni jimbo la Makete, uliibuka utata juu ya matokeo hayo huku kukiwa na madai ya upande wa mshindani wake, kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Norman Sigala ndiye mshindi.
Katika uchaguzi huo, Dk Mahenge alipata kura 8,534, Dk Sigala (8,211), Bonic Muhami (500), Fabianus Mkingwa (466) na Lufunyo Rafael aliyepata 226.
Busega
Kura za maoni za Jimbo la Busega nazo ziligubikwa na utata baada ya wagombea wawili, mbunge anayemaliza muda wake, Dk Titus Kamani na Dk Raphael Chegeni kujitangaza kwa nyakati tofauti kuwa washindi kabla ya matokeo rasmi.
Katika matokeo yaliyotangazwa baadaye, Dk Chegeni aliibuka mshindi kwa kupata kura 13,048 dhidi ya 11,829 za Dk Kamani.
Utata huo ulifanya hata kikao cha Kamati ya Siasa cha Wilaya ya Busega kilichokuwa kimehudhuriwa na watia nia sita kati ya saba, kuvunjika mbele ya Mkuu wa Wilaya hiyo, Paul Mzindakaya na Katibu wa CCM mkoa huo, Hilda Kapaya.
Vurugu ziliibuka katika eneo hilo na kusababisha baadhi ya wajumbe kurushiana makonde na karatasi za matokeo kuibwa mbele ya polisi na viongozi wa chama hicho.
Dk Kamani aliiambia gazeti hili hivi karibuni kuwa, amekata rufani kupinga matokeo hayo.
Rufiji
Katika Jimbo la Rufiji hali ilikuwa tofauti baada ya CCM wilayani humo kutoyatambua matokeo yaliyokuwa yametangazwa kuwa mbunge anayemaliza muda wake na Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid alikuwa ameangushwa kwa kupata kura zaidi ya 3,000 dhidi ya mpinzani wake Mohammed Mchengelwa aliyepata kura zaidi ya 4,000.
Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya hiyo, Musa Mng’eresa alisema kuwa kulikuwa na uvunjwaji wa kanuni ukiwamo ubadhirifu katika uchaguzi huo uliohusisha wagombea wanane, hivyo matokeo ya jimbo la Rufiji na Kibiti yalisitishwa.
Wizi wa kura
Alipotakiwa kujibu tuhuma kwamba CCM ni hodari wa kuiba kura nyakati za uchaguzi, zilitolewa juzi na mgombea urais wa Chadema na Ukawa, Edward Lowassa, Nape alisema, “tuzungumze haya (kurudia uchaguzi) kwanza tuachane na oil chafu, hayo siwezi kuyasemea nimeshawapa story, inatosha.”
Alisema baada ya kikao cha Kamati Kuu jana, leo inaweza kukutana Halmashauri Kuu ya Taifa kuidhinisha majina ya wagombea ili kuwaruhusu kuanza mchakato mwingine.
Kamati Kuu
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akifungua kikao cha Kamati Kuu kilichohudhuriwa na wajumbe 25 badala ya 32, alisema, “Habari za toka tulipoachana, haya tufanye kazi iliyotuleta hapa, leo na kesho watu wanasubiri kwa hamu kubwa nani ni nani ili waweze kuimba iyena iyena, kikao kimefunguliwa waandishi mtupishe.”
Wakati waandishi wakitoka, Rais Kikwete alisikika akisema, “tunaanza kupitia majina na kila mmoja anatakiwa kuwa makini.


Dk Slaa aikana twitter inayomzushia mazito


Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willibrod Slaa 


Dar es Salaam. Wakati kukiwa na taarifa zinazosambaa mtandaoni zikimuhusisha Dk Willibrod Slaa na akaunti ambayo imekuwa ikitoa msimamo wake wa kujitenga na shughuli za siasa pamoja na Ukawa, katibu huyo mkuu wa Chadema amekanusha taarifa hizo akisema hajawahi kuwa na akaunti ya twitter.
Hii ni mara ya pili kwa Dk Slaa kuzungumza na gazeti hili, lakini akikatakaa kufafanua mambo mbalimbali yanayohusu sakata lake na Chadema, akiahidi kuwa kufanya hivyo baadaye, huku akiweka bayana kuwa hajawahi kuwa na akaunti ya twitter.
Dk Slaa, aliyekuwa anatajwa kuwa mgombea urais wa Chadema, hajaonekana hadharani katika matukio makubwa ya kichama tangu Chadema na Ukawa walipomkaribisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kumteua kuwa mgombea urais anayeungwa mkono na vyama vinne vinavyounda umoja huo.
Mara ya mwisho kuonekana kwenye shughuli za chama hicho ni katika kikao cha Kamati Kuu wakati Lowassa alikaribishwa kufanya majadiliano na kujibu hoja za wajumbe.
Lakini baada ya hapo Dk Slaa hakuonekana wakati wa kutambulishwa kwa Lowassa kwa waandishi wa habari, tukio la kuchukua na kurudisha fomu za urais ndani ya chama na tukio la juzi la kuchukua fomu za urais kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Wakati hayo yakiendelea, kuna akaunti ya twitter yenye jina la “Dr Willibrord Slaa” ambayo imekuwa ikitoa kauli mfululizo zikiwa na ujumbe mbalimbali unaoendana na mazingira aliyomo sasa mwanasiasa huyo.
 Agosti 10, kulitumwa ujumbe zaidi mara 10, mmojawapo ukijaribu kuwaaminisha watu kuwa hiyo ni akaunti halisi ya Dk Slaa.
“Ndugu zangu Watanzania, hii ni akaunti yangu rasmi, bila shaka yoyote na naomba ninachoandika hapa kifikishwe kwa Watanzania popote walipo,” unasema ujumbe huo.
Taarifa nyingine zilizotumwa kwenye akaunti hiyo ya twitter ni pamoja na ile iliyoeleza kuwa   Dk Slaa ameomba ulinzi kutoka nchi na mashirika ya kimataifa na atazungumza kupitia runinga na redio pindi atakapopata ulinzi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Slaa alisema hajawahi kutuma taarifa yoyote kwenye mitandao ya kijamii.
“Sijawahi ku-operate (kuendesha) kitu chochote kwenye akaunti ya twitter, sina akaunti kama hiyo,” alisema Dk Slaa.
Mbali na kukanusha kumiliki na kuendesha akaunti hiyo, Dk Slaa alirudia kauli yake ya wiki iliyopita kuwa atatoa msimamo wake muda muafaka utakapofika, baada ya kuulizwa swali kuhusu hatma yake ndani ya Chadema na kisiasa kwa ujumla.
“Subira yavuta heri, sasa ili uipate hiyo heri unatakiwa kuvumilia. Kwa hiyo wakati ukifika nitazungumza tu na Watanzania,” alisema.
Alipoulizwa ni wapi alipo kwa sasa, alisema yupo Dar es Salaam anapumzika, lakini akasisitiza kuwa ipo siku ataweka wazi mustakabali wake kisiasa.
Dk Slaa alisema yeye na mke wake Josephine Mushumbusi wanatarajia kusafiri kwenda nje ya nchi katika siku chache zijazo, ingawa hakuweka wazi nchi anayotarajia kuitembelea, lakini akasema atarejea baada ya wiki moja.

Magufuli ataka kampeni za kisayansi kupata ushindi wa tsunami


Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli 
akiwahutubia wananchi wa Mkoa wa Mtwara 
nje ya ofisi ya CCM 

Mtwara. Waziri wa Ujenzi na mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema kuwa wana-CCM mwaka huu wanapaswa kufanya kampeni za kisayansi zaidi kuhakikisha wanapata ushindi wa tsunami utakaowezesha kuundwa kwa Serikali imara itakayowaletea maendeleo Watanzania wote.
Alisema kwa kufanya hivyo kutawasaidia kupata viti vingi na kusimamia shughuli zote za maendeleo na kwa manufaa ya wanaCCM na Watanzania wote kwani mahitaji yao na matarajio yao ni kupata maendeleo makubwa.
“Niwaombe wana CCM wenzangu, tushikamane tuwe wamoja. Kampeni za mwaka huu ni lazima tufanye kampeni za kisayansi zaidi, ni lazima kampeni zianze katika ngazi ya nyumba kumi, vitongoji kwa vitongoji, vijiji, mitaa, kata majimbo , wilaya, mikoa na baadaye urais kwa ujumla. Katika umoja huu nataka niwahakikishie ushindi wa mwaka huu wala si wa kimbunga, ni wa tsunami,” alisema Dk Magufuli.
Dk Magufuli aliyekuwa katika ziara ya mikoa ya kusini ya kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotelekezwa katika kipindi cha awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, alisema hayo hapo jana wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho nje ya ofisi za CCM mkoa wa Mtwara, ikiwa ni siku moja baada ya rais kukamilisha ziara yake na kuwaaga wananchi wa mkoa huo.
Mgombea huyo na mbunge wa Chato alibainisha kuwa amekuwa kiongozi katika maeneo mbalimbali nchini kwa kipindi kirefu, hivyo anakifahamu vema chama, shida za wanaCCM na matarajio yao yanayojumuisha matarajio ya Watanzania wote na shida zao.
Alisema kuwa endapo atachaguliwa kuwa rais, hatawasahau wanaCCM na Wanamtwara kwa ujumla, lakini wote hao wanapaswa kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa kuwa maendeleo hayana chama na akichaguliwa atakuwa rais wa Watanzania wote.
Alisema katika kipindi cha miaka 20 ya uongozi, amekuwa akifika Mtwara na hivyo ana uhakika endapo Wanamtwara wataamua kumpatia nafasi ataujua zaidi mkoa huo kuuendeleza katika kipindi cha miaka mingine zaidi.
“Wanamtwara nafahamu matarajio yenu, nataka niahidi kwenu na nimwombe Mungu nitapenda sana niwe mtumishi wa watu, nisiwe na majivuno wala kujiona, niwe mtumishi hasa wa wanyonge niweze kuwasikiliza na kusikiliza matarajio yao.
“Matarajio ya Watanzania na Wanamtwara ni makubwa, wanahitaji maendeleo makubwa na tunahitaji kuyasukuma. Nchi yetu imelelewa katika misingi ya umoja pasipo kubaguana kutokana na maeneo tunayotoka, dini, makabila hivyo tunahitaji umoja na palipo na umoja pana amani na palipo na amani pana maendeleo,” alisema Dk Magufuli.
Makundi ndani ya vyama
Akizungumzia makundi katika chama hicho, alisema  yalikuwapo zaidi ya 40 na baada ya uchaguzi makundi yote yalimuunga mkono yeye aliyepitishwa na vikao vya chama, hivyo wanaoondoka ndani ya chama hicho kwa chama kikubwa kama CCM ni jambo la kawaida kwa kuwa hata enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wapo walioondoka na waliofukuzwa.
“Mti ambao unataka upate mbao zake nzuri, matawi kudondoka ni neema, lakini kwa watu kuondoka ndani ya CCM ni kawaida na kwa chama kikubwa kama CCM ni jambo la kawaida sana,” alisema Dk Magufuli.
Mtwara wajipanga
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Homamed Sinani alisema watahakikisha CCM Mtwara inaendelea kupata ushindi wa kishindo kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais.
“Chama kipo imara, mimi kama mwenyekiti wa chama mkoa nasema chama kimejipanga kikamilifu na nina imani kama mshikamano ukidumishwa tunatarajia ushindi wa vishindo kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais,” alisema Sinani.
JK akemea siasa chafu
Katika hatua nyingine, wakati akihitimisha ziara yake juzi, Rais Kikwete aliwataka wanasiasa mkoani Mtwara kuacha siasa chafu za kupotosha wananchi badala yake wawaambie ukweli juu ya miradi na mikakati ya maendeleo inayoendelea mkoani humo.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi wakati akiweka jiwe la msingi katika tawi la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Mtwara ambalo ni la saba nchini na baadaye kuirudia wakati akihutubia mkutano wa kuwaaga wananchi.
Rais Kikwete aliwataka wananchi kutosikiliza maneno ya watu wapotoshaji wanaotafuta umaarufu wa kisiasa kwa bei nafuu.
Alisema kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kuzuia maendeleo ya Mtwara kwa sababu kuna fursa nyingi zinazovutia uwekezaji.
“Msisikilize maneno ya wapotoshaji wanaotafuta umaarufu wa kisiasa kwa bei nafuu, Mtwara na Lindi kulichelewa lakini kutakuwa kwa kwanza na kule kulipokuwa kumetangulia kutafuata,” alisema Rais Kikwete.
Ingawa hakufafanua, kauli hiyo ya Rais Kikwete ilikuwa inalenga vurugu za wananchi wa Mkoa wa Mtwara zilizotokea mwaka jana zikipinga usafirishaji wa gesi kwa njia ya bomba kwenda Dar es Salaam ambazo zilihusishwa na ushawishi wa kisiasa.
Hata hivyo alisema kuwa Mtwara ndio muhimili mpya wa uchumi wa Tanzania kutokana na kuwa na rasilimali nyingi zinazotoa fursa za uwekezaji hivyo kunahitajika uwepo wa huduma za kibenki kwa karibu.
“Wanasiasa wa Mtwara msiwachanganye  wananchi badala ya kuwaeleza msimamo sahihi wenye mwelekeo mnakwenda kuwapeleka kwenye mambo ambayo yanawaongezea  sifa ya muda mfupi na kuwavuruga wananchi hawa na kukosa utulivu wa kufanya mambo ya maana,”alisema Rais Kikwete.
Gavana: Tumepiga hatua
Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alisema Tanzania imepiga hatua katika matumizi ya teknolojia ya huduma za simu za mkononi za kibenki zenye gharama nafuu na kuingia katika nafasi ya kumi duniani na namba moja kwa Afrika.
Profesa Ndulu alisema BoT wamekuwa wakitumia vituo maalumu vya kusambazia fedha na inapobainika kuongezeka kwa mahitaji ya sarafu kwa kuzingatia ongezeko la shughuli za kiuchumi katika eneo fulani hufungua tawi kama ilivyofanyika Mtwara.
Alisema kulingana na tathimini mbalimbali za matumizi ya huduma za kifedha nchini, hadi kufikia mwaka 2006 asilimia tisa ya Watanzania walifikiwa na huduma rasmi za kifedha za benki na zile zisizokuwa za kibenki.
Alisema hadi Machi 2015, idadi ya akaunti za huduma za kifedha kupitia simu za mikononi ilifikia 40.7 milioni huku Watanzania milioni 26.8 sawa na asilimia 95 wakiwa na akaunti za matumizi ya fedha kwenye simu zao.

Lowassa: Wameisoma namba


Watu wakiwa wamekusanyika katika makutano ya Barabara ya Uhuru na Msimbazi 
wakati msafara wa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, 
Edward  Lowassa  ulipokuwa ukielekea Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) 
kuchukuwa fomu za urais, Dar es Salaam

Dar es Salaam. Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema anayewakilisha vyama vinavyounda Ukawa, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsindikiza wakati akienda Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu ni salamu kwa CCM na ‘wameisoma namba’ kwamba Watanzania wanataka mabadiliko.
Akiwahutubia mamia ya wafuasi wa vyama vinavyounga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika Ofisi za Makao Makuu ya Chadema jana, Lowassa aliyeonekana kuwa na furaha muda wote, alisema maandamano waliyoyafanya hayajawahi kutokea katika historia ya Tanzania.
“Haijatokea katika historia ya nchi yetu maandamano makubwa ya aina ile, nimefurahishwa na vijana wametembea kutoka Buguruni hadi Kinondoni na hamjachoka nawapongeza sana, asante sana,” alisema Lowassa.
Alisema ana mambo mawili ya kusema; kwanza kuwashukuru wafuasi na wapenzi wa Ukawa kwamba kwa kujitokeza kwa wingi wamepeleka meseji moja kwa wasiowatakia mema, wanaosema CUF na Chadema ni watu wenye fujo, wamethibitisha kwamba si kweli.
 “Tumewahakikishia kuwa sisi ni watu wenye nidhamu na uwezo, Mwenyezi Mungu akipenda Oktoba tunachukua nchi asubuhi peupeee, kwa hiyo watu wasitafute visingizio, watafute vingine, watoto wa mjini wanasema wameisoma namba,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na umati wa watu.
Akizungumzia jambo la pili, mbunge huyo wa Monduli aliyejiondoa CCM siku 15 zilizopita, alisema anauchukia umaskini kiasi kwamba anauona kama ukoma.
Lowassa ambaye mara nyingi husema hajakutana barabarani na Rais Jakaya Kikwete, alisema rafiki yake huyo ndiye aliyeharibu uchumi wa nchi, lakini akasema asingetaka kutoa mashtaki bali kutoa takwimu za hali ilivyobadilika.
“Wakati Rais Benjamini Mkapa anaondoka madarakani, bei ya sukari ilikuwa Sh650, leo ni Sh2,300, kutoka 650 hadi 2,300 ameharibu uchumi, hajaharibu?” aliuliza na kujibiwa, “ameharibuuu.”
“Bei ya mchele ilikuwa Sh550 leo Sh2,200, ameharibu uchumi, hakuharibu? Sembe kilo ilikuwa Sh250 leo ni Sh1,200, ameharibu hakuharibu?” alihoji Lowassa na watu wakamjibu ‘ameharibuuu” na kisha akaongeza kuwa kwa sababu hizo, CCM haistahili kuendelea kutawala.
Lowassa alitumia fursa hiyo kuwaalika wanachama wa CCM wasioridhika na hali ilivyo kujiunga na Ukawa kwa kuwa inawezekana kutafuta mabadiliko nje ya chama hicho na kwamba wasione haya bali waangalie idadi kubwa ya vijana waliojitokeza jana.
Mgombea huyo, alisema Tanzania imeshuhudia uporaji mkubwa wa mali za Taifa, ambapo tembo wameuawa kuliko wakati mwingine wowote, hivyo kutokana na vitendo hivyo, CCM haistahili kuendelea kutawala.
Kuhusu kutunza shahada za kupigia kura, Lowassa alisema Wanaukawa hawapaswi kufanya mchezo kwa kuwa CCM imekuwapo madarakani muda mrefu watatumia kila kitu ndani ya uwezo wao kubaki madarakani.
“Na sisi tutumie kila kitu kilicho ndani ya uwezo wetu kuingia madarakani. Kitakachotuingiza madarakani ni kura, hifadhi shahada yako, shawishi na wengine, tarehe 25 Oktoba tunawatoa madarakani,” alisema.
Alisema amesikia maneno kuwa kuna mchezo wa watu wanapita mitaani wanachukua shahada za kupigia kura za wanajeshi, askari magereza wanachukua namba.
Alimuhoji mmoja wa wanasheria wa Chadema, Mabere Marando iwapo kama amesikia taarifa hizo, naye akajibu: “Kwa niaba ya wanasheria wote wa Chadema tunaahidi kitu kimoja, njama zote walizonazo kujaribu kuhujumu kura za Lowassa tutazidhibiti, njama zote walizonazo kuhujumu ushindi wa wabunge wetu tutazidhibiti, njama zote walizonazo kujaribu kudhibiti ushindi wa madiwani tutazidhibiti.”
Marando alisema mawakala wote wa vyama hivyo wanapaswa kupeleka matokeo ya vituo vyote baada ya kubandikwa saa 12 jioni na kwamba yeye hatasubiri atatangaza badala ya kusubiri saa saba usiku.
Mbatia
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi na mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema maandamano yaliyofanyika jana ni historia mpya ambayo ni elimu kwa Watanzania. Ari iliyoonyeshwa tangu asubuhi inasadifu hamu ya Watanzania.
Pia, alisema Rais Kikwete ametangaza kuwa wapinzani ni maadui na kumtaka kuangalia lugha anayoitumia, kwa kuwa Ukawa watajibu kwa hoja na si matusi.
“Ninamhusia sana Rais Jakaya Kikwete amebaki na siku 75 tu za kuwa Amiri Jeshi Mkuu, ni ushauri wangu wa bure kabisa yeye na wenzake wachunge sana ndimi zao, maslahi ya taifa kwanza vyama baadaye, tunampa nishani iwapo atamaliza siku 75 kwa amani na kumkabidhi Amri Jeshi Mkuu, Edward Lowassa,” alisema Mbatia. “Rafiki yangu (Ibrahimu)Lipumba amekimbia akidhani Ukawa utaparaganyika lakini sasa umeimarika zaidi,” alisema Mbatia huku akishangaliwa na umati wa watu na kumaliza kuwa “Hakuna mwanadamu ambaye yupo juu kuliko wengine au taasisi yoyote.”
Makaidi
Mwenyekiti wa NLD Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi alisema kuwa katika umri wake mkubwa alionao hajawahi kuona maandamano ya watu wengi kama waliojitokeza kumsindikiza Lowassa jana.
“Nina miaka 74 lakini sijaona kitu kama cha leo nakaanza kujiuliza hii maana yake nini? Nikachukua mfano kama mimi ni chama tawala na wapinzani ni wengi namna hii ningeanza kufanya nini, ningejiuzulu mara moja,” alisema Makaidi.
Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Twaha Tasilima alisema kuwa walioleta siasa mbaya nchini wanatakiwa kuwajibika kwa kuwa wamesababisha kuwapo kwa uchumi mbaya pia.
“Lowassa akiingia Ikulu ataenda kuondoa uchumi na siasa mbaya,” alisema Tasilima.
Maalimu Seif
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad alisema umati mkubwa wa vijana waliojitokeza kumsindikiza Lowassa umedhihirisha kuwa watu walikuwa wamekata tamaa sasa wanataka matumaini mapya.
Hata hivyo, alisema haitoshi kumsindikiza Lowassa kwa idadi kubwa namna hiyo kama hawataenda kupiga kura kwa kuwa maandamano hayawezi kuiondoa CCM madarakani.
“Hatutaishinda CCM kwa maandamano bali kwa kupiga kura, tunza kadi yako zimebaki siku chache,” alisema Hamad.
Onesmo Ole Nangolo
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole, alipokewa rasmi na kusema alijiunga CCM mwaka 1977, lakini alichokishuhudia Dodoma kwenye uchaguzi wa mgombea wa Rais kwa tiketi ya chama hicho kimemlazimisha kuhamia Chadema.
“Ile CCM niliyokuwa naifahamu si tuliyokwenda juzi Dodoma, misingi na haki imegeuka, kimekuwa chama cha viongozi wachache kwa maslahi yao binafsi, unyanyasaji umetawala ndani ya CCM, sina moyo wa chuma,  sikuridhika na mchakato wa Dodoma,” alisema Nangolo.
Ilivyokuwa
Jiji la Dar es Salaam lilisimama kwa wastani wa saa nane kutokana na msafara wa Lowassa kwenda kuchukua fomu.
Makundi ya watu wa kada mbalimbali wakiwamo madereva wa bodaboda, bajaji, magari na watembea kwa miguu walionekana kufunga barabara ya Uhuru kuanzia Buguruni eneo la Rozana zilipo ofisi za CUF na Posta zilipo ofisi za NEC.
Maandamano hayo yalisababisha msongamano wa magari na kusababisha magari ya abiria maarufu kama daladala na magari binafsi kutafuta njia mbadala kufanikisha safari zao.
Idadi ya watu waliojitokeza katika msafara inaweza kufananishwa na ile iliyojitokeza wakati wa ziara ya Rais wa Marekani, Barack Obama Julai 2013.
Watu wengi walionekana wakitumia simu kupiga picha na kurekodi video za matukio mbalimbali pembeni mwa barabara huku wengine wakiwa juu ya maghorofa wakitazama.
Wapo waliokuwa wakitoka maofisini na kukaa pembezoni mwa barabara kushuhudia tukio hilo huku maelfu wakitembea umbali wa kilometa sita kuufuata msafara huo.
Msafara huo ulitumia saa mbili na nusu kutoka Buguruni hadi ofisi za NEC.
Kabla ya msafara
Wafuasi wa vyama vinavyounda Ukawa; CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD walianza kukusanyika tangu saa moja asubuhi katika makao makuu ya CUF yaliyopo Buguruni na viongozi mbalimbali walianza kuingia saa 3:56 asubuhi na kumkuta mwenyeji wao Maalimu Seif.
Wengine
Makundi ya mashabiki waliokuwa wakizunguka wakiimba nyimbo mbalimbali, ukiwamo; ‘kama siyo juhudi zako Kikwete, Lowassa tungempata wapi? Na wengine wakikejeli, “Magufuli toroka uje, Tanzania mpya bila CCM inawezekana, tumechoka kuokota makopo na funguo za Magufuli zipo Ukawa.
Safari ya Biafra
Baada ya kukabidhiwa fomu na Ofisa Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Deogratius Nsanzugwanko, Lowassa, mgombea mwenza, Juma Duni Haji na viongozi waandamizi wa Ukawa waliendeleza msafara wa kwenda Makao Makuu ya Chadema mtaa wa Ufipa, Kinondoni.
Licha ya umati uliomsindikiza kutembea kilomita nane ukitoka Buguruni, idadi ya watu ilizidi kuongezeka na kuendeleza maandamano yaliyoanzia makutano ya mtaa wa Ghana na Ohio ilipo NEC kupitia Barabara ya Barack Obama na kuunga hadi Ali Hassan Mwinyi.
Kama ilivyokuwa awali, wafuasi hao waliendelea kuimba bila kuchoka nyimbo mbalimbali za hamasa ili wasichoke na kila eneo walilokuwa wakipita umati mkubwa wa watu waliojipanga katika barabara hizo ulishangilia na hata kuwafanya baadhi ya waliokuwamo kwenye magari kuonyesha alama ya “V” inayoyotumika na Chadema.
Msafara ulizidi kuongezeka urefu baada ya wale waliochelewa kuungana nao na baadaye uliiacha barabara ya Ali Hassan Mwinyi na kuingia barabara ya Kinondoni ambayo kutokana na wembamba wake iliwalazimu wenye magari waliokuwa safarini kuegesha pembeni kupisha watu waliokuwa wakiandamana.
Katika safari yote hiyo, polisi walikuwa wameegesha magari yao katika kila umbali wa kilomita moja na nusu au zaidi na kufanya umati huo uwashangilie kila unapowapita.
Licha ya kuwa taarifa za awali zilibainisha kuwa maandamano hayo yangeishia Makao Makuu ya Chadema, ilibidi uongozi wa chama hicho ubadilishe utaratibu na kuwapeleka watu wote katika Viwanja vya Biafra, Kinondoni kwa kuwa eneo la mtaa wa Ufipa lisingetosha.
Walipofika Biafra baada ya kumaliza takribani kilomita saba kutoka NEC, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu aliwasalimia wafuasi hao na kumkaribisha Lowassa awashukuru ambaye alizungumza kwa ufupi akitamka maneno, “hii haijawahi kutokea.”
Lowassa aliwapongeza polisi kwa kufanya kazi kwa weledi na kueleza kuwa busara na amani vilivyotumika katika maandamano hayo vinadhihirisha kuwa Chadema na Ukawa ni vyama vya kushika dola.
Baada ya watu kutawanyika, msafara wa viongozi ulirudi mtaa wa Ufipa kuendeleza hotuba ambako baadhi ya wafuasi walioshtukia kuwa walidanganywa walirudi kwenda kuwasilikiliza viongozi.