Friday, April 25

Rais anakemea “wanasiasa wanaomtukana Nyerere na Karume” amekaa kimya matusi kwa Jaji Warioba na kauli za Lukuvi

NI dhahiri sasa kuwa mjadala wa Katiba mpya, hususan kipengele cha muundo wa Muungano, unaelekea kulipeleka taifa mahali pabaya. Japokuwa dalili za Bunge Maalumu la Katiba linaweza kuishia kuwa jukumu ghali kwa walipakodi masikini, hasa baada ya kusikika madai ya baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo kuwa posho ya shilingi 300,000 kwa siku haitoshi, lakini Watanzania wengi walikuwa na imani kwamba ‘upepo huo mbaya’ ungepita na hali ingekuwa shwari.

Hata hivyo, kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo hali inavyozidi kuwa mbaya. Kinacholeta wasiwasi zaidi 
kwa sasa ni kuibuka kwa dalili za ubaguzi wa waziwazi, sambamba na jitihada hatari za kumwaga petroli kwenye moto kwa kuingiza udini kwa nguvu kwenye siasa.

Lakini pasi ‘kuuma maneno’ naomba nielekeze lawama zangu kwa Rais Jakaya Kikwete na chama chake - CCM. Pamoja na wasiwasi uliokuwepo awali, kwamba huenda Rais Kikwete angeendeleza desturi iliyoota mizizi ndani ya CCM kwamba kila wazo lililoanzia vyama vya upinzani (kama hilo la umuhimu wa kuwa na Katiba mpya) ni baya, na hivyo angekwamisha uwezekano wa kupata Katiba mpya, alitushtua wengi alipoonyesha dalili za kuwa amepania kwa dhati kuweka historia kwa kufanikisha suala hilo muhimu.

Mambo yalionekana kwenda vizuri licha ya jitihada za hapa na pale ndani ya CCM kulifanya suala la Katiba mpya kuwa la kiitikadi zaidi kuliko la kitaifa. Wengi mtakumbuka vijembe walivyopigwa baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani walipotaka kukutana na Rais Kikwete. Badala ya kupongeza kile kilichoonekana kama mwanzo mpya wa siasa za maridhiano, baadhi ya wanasiasa huko CCM waliwakebehi wapinzani kuwa wanataka kwenda Ikulu kunywa chai tu!

Dalili za mwanzo kuwa hatma ya suala la Katiba mpya ipo shakani zilianza kujichomoza zaidi baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Jaji Joseph Warioba kuweka hadharani Rasimu ya Kwanza ya Katiba mpya, ambapo pendekezo la muundo wa Muungano wa Serikali tatu liliwekwa bayana. Taratibu, CCM, chini ya uongozi wa Kikwete, ilianza harakati za chini chini kujaribu kuingilia mchakato wa Katiba mpya, ikiwa ni pamoja na jitihada za kubinafsisha mchakato huo.

Lakini Mungu si Athumani au John, pamoja na vizingiti vya hapa na pale, hatimaye Rais Kikwete alitangaza majina ya wajumbe 201 kutoka makundi mbalimbali ya jamii, kuingia katika Bunge la Katiba. Lakini kabla ya hapo, tayari Rais Kikwete alishatangaza mkoani Mbeya wakati wa maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM kwamba msimamo wa chama hicho ni Serikali mbili. Japo alitangaza msimamo huo kama Mwenyekiti wa taifa wa CCM, katika mazingira ya kawaida tu, isingewezekana kuwapo kwa mitizamo tofauti kati ya Kikwete wa CCM na Kikwete Rais.

Kuanzia hapo ikawa kama ‘jini lililopo kwenye chupa’ (a genie in the bottle) limefunguliwa. Zikaanza harakati za waziwazi ‘kulazimisha’ matakwa ya chama tawala kwamba muundo wa Muungano lazima ubaki kuwa wa Serikali mbili. Mara zikapatikana taarifa kuwa CCM imetengeneza rasimu yake ya siri.
Mara tu baada ya kikao cha Bunge Maalum la Katiba kuanza, ishara kuwa hali huko mbele inaweza kuwa si shwari zikawa zinajitokeza kila kukicha. Baada ya mshikemshike wa madai ya posho, likaibuka suala la utaratibu wa kupiga kura (yaani kura zipigwe kwa usiri au uwazi.)

Lakini kwa vile tangu awali CCM walionyesha kuwekeza nguvu zao kubwa katika suala la muundo wa Muungano wakitaka Serikali mbili, suala hilo limeteka takriban kila kipengele cha Katiba mpya, na kwa bahati mbaya au makusudi, mjadala wa muundo wa Muungano unazidi kutishia umoja na mshikamano wa taifa letu.

Japo lugha za matusi na kashfa si jambo geni kwenye vikao vya Bunge la Jamhuri, hali imezidi kuwa mbaya kwenye kikao cha Bunge Maalumu la Katiba, tunasikia baadhi ya wajumbe wakiwatuhumu wenzao kuwa mashoga, huko wengine wakienda mbali na kuhoji Uafrika wa wenzao. Lakini kama nilivyobainisha hapo juu kuwa tumeshazoea matusi na lugha chafu bungeni, kuna waliokuwa na imani kuwa “wakimaliza kutukanana, watarejea kwenye suala lililowakutanisha huko Dodoma.”

Mara vikaanza kuibuka vitisho kuwa iwapo Katiba mpya itaridhia Serikali mbili, jeshi litatwaa madaraka. Na aliyeanzisha vitisho hivi si mwingine bali Rais Kikwete katika hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge hilo la Katiba, wiki chache zilizopita.

Lakini wakati Rais Kikwete aliliongelea suala hilo katika jukwaa la kisiasa (bungeni), mmoja wa wasaidizi wake akaamua kulitoa suala hilo katika anga za siasa na kulipeleka kwenye nyumba za ibada. Hapa ninamzungumzia William Lukuvi.

Inaniwia vigumu kupata maneno stahili ya kumwelezea mwanasiasa huyo ambaye ghafla ametokea kuwa mtu mwenye kauli chafu, hatari na za kiharamia.

Huyu mtu bila aibu wala uoga amediriki kwenda kanisani na kutangaza waziwazi kuwa jeshi litaasi pindi uamuzi wa kuwa na Serikali tatu utakapopitishwa. Naomba nitamke bayana kwamba nahisi Lukuvi ana matatizo kutokana na hatua yake ya kwenda kanisani kufanya mahubiri ya kushawishi jeshi kuasi.

Lakini anayempa jeuri Lukuvi ni Rais Kikwete, kwani naye aligusia suala hilo kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge la Katiba. Kwa hiyo anachofanya Lukuvi ni kusambaza tu ujumbe ulioanzishwa na Rais Kikwete.

Na wakati Rais Kikwete akiwakemea “wanasiasa wanaomtukana Nyerere na Karume” amekalia kimya matusi ya Lukuvi kwa Mwenyezi Mungu (naam, kutumia nyumba ya ibada kujenga chuki na kuhamasisha uasi wa jeshi ni matusi kwa Mungu.)

Ni watu wenye upeo mdogo tu watakaochukia kusikia kwamba Nyerere na Karume wana mchango katika matatizo tuliyonayo kuhusu Muungano, hasa kwa uamuzi wao wa kulifanya suala hilo kama lao binafsi bila kuangalia madhara yake miaka kadhaa ijayo.

Mara kadhaa Rais Kikwete amekuwa akiasa kuhusu athari za kuchanganya siasa na dini. Amewahi kudai kuwa kuna maadui wa nje wanaotumia suala la dini kwa minajili ya kututenganisha.

Lakini kipi cha kushangaza ilhali kwenye chaguzi kadhaa wamekuwa wakitumia nyumba za ibada kupandikiza chuki dhidi ya wapinzani wao?

Japo hainisumbui sana iwapo Katiba mpya haitopatikana, napata wasiwasi kuona uhuni wa kisiasa (political thuggery) ukihalalishwa kwa kisingizio cha ‘kuhubiri athari za Serikali tatu.’
Lakini nani wa ‘kuokoa jahazi’? Rais Kikwete anakemea wanaowatukana Nyerere na Karume, lakini anapuuza matusi ya wasaidizi wake kwa Jaji Warioba.

Nimalizie makala hii kwa kumkumbusha Rais Kikwete kwamba mwakani ataondoka madarakani na kurejea uraiani. Asipotengeneza mazingira mazuri kwake na kwa Watanzania, janga hili linalopikwa na akina Lukuvi litamwathiri naye pia.

Ni muhimu kwa Rais kuweka kando ushabiki wa kisiasa na kuchukua hatua za makusudi kuepusha nchi kutumbukia kwenye machafuko yanayochochewa na mahubiri ya ubaguzi na kuitumia dini kwa minajili ya kisiasa.

Siku 67 za mipasho, matusi bungeni

Wajumbe wa Bunge Maalum la katiba wakipinga jambo ndani ya bunge juzi  wakati Kamati namba tatu  na nne za kijadili vifungu vya rasimu ya Katiba walipokuwa wakiwasilisha ripoti zao Bungeni Dodoma juzi. Picha na Salim Shao 


Dodoma. Bunge Maalumu la Katiba linaahirishwa leo baada ya kukutana kwa siku 67 bila kupitisha hata ibara moja kati ya 240 zilizomo katika Rasimu ya Katiba.
Badala yake Bunge hilo likiongozwa na Samuel Sitta “Mzee wa Kasi na Viwango” linaahirishwa hadi Agosti, mwaka huu likiendelea kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita zenye jumla ya Ibara 19, zinazohusu masuala yanayojenga msingi wa aina ya Muungano unaopendekezwa.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba katika rasimu iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba ilipendekeza muundo wa shirikisho lenye serikali tatu, pendekezo ambalo limeligawa Bunge hilo vipande viwili.
Kutokana na mgawanyiko huo, kauli zenye utata, kejeli, matusi, dhihaka na ubaguzi ni mambo yaliyoshika hatamu katika mjadala wa sura hizo mbili, huku viongozi wa Bunge; Sitta na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan wakilaumiwa kwa kushindwa kudhibiti hali hiyo.
Mwanzoni mwa wiki hii, Mjumbe wa Bunge hilo, Ezekiah Oluoch alimshutumu Sitta kwamba ameshindwa kudhibiti nidhamu katika Bunge na kwamba ndiye chanzo cha kuondoka kwa wajumbe wapatao 200 ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Mwenendo wa Bunge Maalumu ulikuwa na dalili zote za kuonyesha kungetokea matatizo ndani yake kutokana na mipasho ambayo ilikuwa ikitokea kwa wajumbe pamoja na lugha ambazo siyo za staha wakati wa kutengeneza kanuni,” alisema Oluoch na kuongeza:
“Kwanza matumizi ya lugha zisizo na staha, mwenyekiti anaruhusu wajumbe kuchangia hoja kwa kupeana mipasho bila kujali hoja iliyopo mezani kinyume na kanuni,” alisema Olouch.
Hata hivyo, Suluhu alisema amekuwa akiendesha Bunge hilo kwa umakini mkubwa na kwamba kila anaposikia lugha chafu amekuwa akiwabana wajumbe kwa kuwaamuru kufuta kauli au kuomba radhi kwa matamshi. “Sipendezwi na lugha chafu, kwa hiyo mojawapo ya mambo ambayo huwa najitahidi kusikiliza kwa makini kila michango inapotolewa na wajumbe bungeni ni kubaini kama wametumia lugha zisizostahili, kisha kuchukua hatua kwa mujibu wa kanuni zetu,” alisema Suluhu.
Alikiri kwamba wapo baadhi ya wajumbe ambao wamekuwa wakigoma au kukataa kuomba radhi na kwamba masuala yao hupelekwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo ina mamlaka ya kuchukua hatua zaidi kwa mujibu wa kanuni za Bunge hilo.
Matakwa ya Kanuni
Sehemu ya Tano ya Kanuni za Bunge Maalumu inatoa mwongozo wa mambo yanayokatazwa na yale yanayopaswa kufuatwa wakati wa mjadala.
Kanuni ya 46 imeorodhesha mambo yasiyoruhusiwa ambayo ni pamoja na kusema uongo, kutoa taarifa zisizokuwa za kweli, kuzungumza jambo lolote ambalo halipo kwenye mjadala na kutumia majina ya marais na waasisi wa Taifa kwa dhihaka.
Pia inazuia matumizi ya lugha ya kuudhi, kubagua, kunyanyapaa au inayodhalilisha watu wengine, kuzomea, kupiga kelele za aina yoyote zinazoweza kuvuruga mjadala au mwenendo bora wa shughuli za Bunge hilo.
Licha ya makatazo hayo, wajumbe wamekuwa wakikiuka kanuni bila kuchukuliwa hatua na hali hiyo imekuwa chanzo cha mivutano, zomeazomea, kelele na mambo mengine hadi kundi la Ukawa kususia kikao wakieleza kutokuridhishwa na mwenendo wa Bunge.
Kuufyata na kuufyatua
Baadhi ya kauli tata zilizojitokeza ni pamoja na ile iliyotolewa na Asha Bakari Makame kwa mjumbe mwenzake, Ismail Jussa kuwa anafanana na watu wenye mabusha nyuma ambao ndiyo huufyata.
Makame ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), alikwenda mbali zaidi na kumwambia Jussa kuwa ana matatizo ya kiafya na si mwanamume kamili, kwani ameshindwa kuoa na hana watoto wakati ana umri mkubwa.
“Huyu Jussa anasema kwamba tumeufyata, hapa tuwekane sawa, maana ya kuufyata ni mtu kuwa na mabusha pale yanapokuwa nyuma ndiyo kuufyata kwa hiyo yeye ndiyo ameufyata, ana busha huyu,” alisema Bakari.
Naye Profesa Ibrahim Lipumba alichafua hali ya hewa pale alipowafananisha wajumbe wa Bunge Maalumu na kundi la mauaji nchini Rwanda, Intarahamwe.
“Tumechoka kusikiliza matusi. “Tumechoka kudharau mawazo ya wananchi, tumechoka ubaguzi hatuwezi kuwa sehemu ya kundi la Intarahamwe linalohamasisha ubaguzi ndani ya Tanzania hili hatulikubali. Tunawaachia, watu wote tunaotaka Katiba ya wananchi tunawaachia Intarahamwe mwendelee na Bunge lenu.”
Mjumbe mwingine ni Mwanakhamis Kassim Said aliyesema: “Mimi nilikuwa namwomba baba yangu mdogo Seif (Maalim Seif Sharif Hamad) awarejeshe watu wake humu (bungeni) kwa sababu mpira unachezwa huku ndani. Hatutakii mema humu, tena ana choyo na husuda. Namwomba baba mdogo atuache, alichokitaka amekipata, king’ora anazunguka saa 24 Dar es Salaam, Unguja. Mheshimiwa Mwenyekiti Baba mdogo kila mara yuko kwenye pipa (ndege) mara Uingereza, mara Canada mara wapi? Hicho ndicho anachokitaka amekipata.”
Mjumbe mwingine, Mohamed Seif Khatibu alisema: “Nimejifunza kuwa baadhi ya wanasiasa wa upinzani ni vinyonga. Lakini Maalim Seif ni kinyonga, wakipita kwenye mvua wanakuwa na rangi ya mvua, kwenye jua wanakuwa na rangi ya jua, baharini wanakuwa na rangi ya bahari.”
Tuhuma za rushwa
Mjumbe Ezekiah Wenje alisema baadhi ya mawaziri wamewahonga wajumbe wa kundi la 201 ili waunge mkono msimamo wao, lakini alipotakiwa kufuta kauli hiyo alikataa na suala lake kufikishwa kwenye kamati ya kanuni.
“Kuna wajumbe wengine walikwenda hadi kwa waziri mkuu ambako walikula, walikunywa hadi saa 7:00 usiku, wengine walikwenda kwa Gaudensia Kabaka (Waziri wa Kazi na Ajira) na walikula na kunywa na kupewa bahasha.”
Kuingia msituni
Kapteni John Komba alitangaza kuingia msituni iwapo Bunge Maalumu la Katiba litapitisha muundo wa serikali tatu, huku akimshutumu Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na timu yake ni waasi kama Adamu na Eva waliomuasi Mungu kutokana na kile walichokifanya cha kupendekeza serikali tatu. Mwingine katika orodha ni Bernard Membe aliyesema, Tume ya Mzee Warioba itakuja kukumbukwa kwa kuratibu mauaji ya Muungano na Bunge nalo litakuja kulaaniwa kwa kubariki mauaji hayo.
Watoto wa shetani
Mjumbe Paul Makonda alisema: “Shetani alikuja duniani kuiharibu dunia, kuiangamiza na kuteketeza kila kilichostahili kuungana… watoto wake ni Mheshimiwa Jussa, watoto wake ni Mheshimiwa Mbowe, watoto wake ni Mheshimiwa Lipumba… Hawa ni watoto wa shetani”.
Mwingine: Waride Bakari Jabu alisema: “Chiku Abwao mimi namshangaa sana anayesema bora Muungano uvunjike lakini Tanganyika iwepo. Tunafahamu asili yake mwenyewe ni Mkongo mumewe ndiye Mtanganyika, namwambia Muungano huu utakuwepo na utaendelea kuwapo.”
Mjumbe Tundu Lissu alisema: “Tanganyika haikuuawa na makubaliano ya Muungano, bali iliuawa kwa amri za Nyerere…. Mwalimu Nyerere hakuwa na mamlaka yoyote ya kikatiba ya kutunga amri na kuua Tanganyika.”

Imeandikwa na Neville Meena, Daniel Mjema, Sharon Sauwa na Beatrice Moses.