Saturday, August 31

Serikali yasalimu amri kwa wabunge


Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Mohamed Keissy
akichangia bungeni mjadala wa kupitisha muswada wa
sheria ya taifa ya umwagiliaji wa mwaka 2013,
ambapo alikuwa akipinga wawekezaji wa kilimo kwenda kuwekeza mkoani Rukwa, 

Dodoma. Muswada wa Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji wa mwaka 2013, jana ulipita kwa mbinde bungeni mjini Dodoma, huku Serikali ikisalimu amri kwa wabunge na kukubali kurekebisha baadhi ya vifungu vyake.

Bila kujali tofauti zao za kisiasa, wabunge jana walisimama kidete na kuonyesha uzalendo wa hali ya juu, wakitaka sheria hiyo imlinde mzawa badala ya mwekezaji.

Moto huo wa wabunge uliwalazimisha Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chizza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema kusalimu amri na kukubali mapendekezo ya wabunge.

Msimamo wa wabunge hao katika kuibana Serikali, pia ulililazimisha Bunge kutengua kanuni zake na kuendelea na shughuli za kupitia muswada huo hadi saa 7:35 mchana, badala ya kusitishwa saa 7:00 kwa ratiba ya kawaida.

Serikali ilikubali mapendekezo ya wabunge hao na kurekebisha vifungu ambavyo sasa vinampa mmiliki wa ardhi itakayotangazwa eneo la umwagiliaji kuwa mwanahisa na kulipwa fidia.

Awali, wabunge waliowasha moto huo ni pamoja na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina na Suleiman Jaffo wa Kisarawe, wote kutoka Chama Cha Mapinduzi(CCM), ambapo walisema baadhi ya vifungu vya muswada huo wa sheria vilikuwa na ajenda ya siri.

Wakichangia mjadala huo wabunge hao walitaka vifungu vinavyotamka kuwa eneo litakalotangazwa kuwa la umwagiliaji litatwaliwa na Tume itakayoundwa na kupewa fidia viboreshwe, ama kama haifai, vifutwe.

Mpina alishikilia msimamo kuwa badala ya kumlipa fidia mwananchi, vifungu hivyo vitamke kuwa atalipwa fidia ama kuwa mwanahisa wa mradi ama alipwe fidia na papo hapo kuwa mwanahisa.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), aliitaka Serikali itunge sheria zinazolinda wazawa na kwamba hatua ya kuacha mianya, ndiyo mwanzo wa wawekezaji kuwanyang’anya ardhi wazalendo.

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), alisema kuwa haihitaji kuipitia sheria yote ili kubaini maudhui yenye dhamira ovu dhidi ya Watanzania ndani yake akisisitiza kuwa baadhi ya vifungu vina ajenda ya siri.

“Vifungu hivi vina ajenda ya siri ya kuwapeleka Watanzania kwenye utumwa…Kama msipobadilisha vifungu hivi, mwondoe huu muswada maana hii ni dhambi ya mauti,” alisisitiza Ole Sendeka.

Ole Sendeka alisisitiza sheria itamke kuwa kama ni kutwaa ardhi yoyote, hata kama ni Rais anataka kufanya hivyo ni lazima hilo lifanyike kwa ushirikiano na mmiliki wake, ama na wanakijiji wote kupitia mkutano mkuu.

Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM), alisema Watanzania wameshindwa kunufaika na rasilimali nyingine na waliyobakia nayo ni ardhi hivyo hawako tayari kurudisha ukoloni mamboleo.

Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama (CCM), alisema ni lazima sheria hiyo iweke sharti la lazima kwa mwekezaji kuingia ubia na mmiliki wa ardhi na kama hataafiki, ndipo apewe fidia.

IGP aibiwa upanga wa dhahabu - mwananchi newspaper




Jeshi la Polisi limeingia katika kashfa nzito baada ya mkuu wake, Inspekta Jenerali Said Mwema, kuibiwa upanga wa dhahabu ambao ni mali ya Shirikisho la Wakuu wa Majeshi ya Polisi wa nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO).

Upanga huo wenye uzito wa takriban kilo tatu na wenye thamani ya zaidi ya fedha za Tanzania Sh600 milioni, ni kielelezo kwa nchi inayokabidhiwa uongozi wa SARPCCO.

Mwaka jana Tanzania ilikuwa mwenyekiti wa SARPCCO, ambapo upanga huo ulikabidhiwa kwa IGP Mwema na Jenerali Magwashi Victoria ‘Riah’ Phiyega, ambaye ni Kamishna wa Taifa wa Polisi wa Afrika Kusini aliyekuwa amemaliza muda wake kwa wakati huo.

Hilo ni tukio la pili la wizi la mali zinazohusu ofisi ya IGP, ambapo mwaka jana ndani ya ofisi hiyo kuliibwa kompyuta ndogo (laptop), ikiwa na taarifa muhimu za kipolisi. Hadi sasa hakuna taarifa za kupatikana kwa kompyuta hiyo.

IGP Mwema alikabidhiwa upanga huo Septemba 5, 2012, katika mkutano saba wa SARPCCO uliofanyika Zanzibar na kuhudhuriwa na wakuu wa majeshi ya Polisi kutoka nchi 13, pamoja na mashirika ya kimataifa.

Upanga huo ambao unakwenda sambamba na bendera ya SARPCCO, ni moja ya vielelezo vya nchi iliyochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa shirikisho hilo, ambaye moja kwa moja anakuwa ni Mkuu wa Jeshi la Polisi katika nchi husika.

Kwa mujibu wa taratibu za SARPCCO, vielelezo hivyo hutakiwa kuwekwa ofisini kwa kiongozi husika, ikiwa ni alama ya kila mgeni atakayeingia ofisini hapo kutambua uwepo wa wadhifa huo wa kimataifa.

Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa IGP aligundua kutoweka kwa upanga huo wiki iliyopita, wakati akijiandaa kwenda kuukabidhi kwa mwenyekiti mpya wa SARPCCO, ambaye ni IGP wa Namibia.

Taarifa za ndani ya jeshi hilo zilibaini kuwa, IGP alilazimika kuondoka bila upanga huo alipokwenda Namibia wiki iliyopita kuhudhuria mkutano wa nane wa SARPCCO, uliofanyika Jumapili iliyopita mjini Windhoek.

Kwa mujibu wa uchunguzi, IGP Mwema alikabidhi upanga unaofanana na huo ambao siyo wa dhahabu, alioazimwa kutoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi la Namibia, Inspekta Jenerali, Luteni Jenerali Sebastian Ndeitunga, na kukabidhiwa kama ishara ya kukabidhiwa uenyekiti wa SARPCCO kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Uchunguzi ulibaini kuwa IGP Mwema alitoa ahadi ya kurejesha upanga halisi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, au Serikali ya Tanzania italazimika kutengeneza mwingine kulipa uliopotea.

Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa kashfa hiyo ametupiwa Mkuu wa Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa pamoja na dereva wake, ikidaiwa kuwa upanga huo baada ya kupokewa na IGP Mwema, Septemba mwaka jana uliwekwa kwenye gari la kamishna huyo.

Kamishna Mussa ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano wa Saba, na pia ofisa mwenyeji kwa wajumbe wa mkutano huo uliofanyika Zanzibar.

Hata hivyo, taarifa zingine zilidai kuwa IGP Mwema naye analaumiwa kwa kutofuatilia kwa karibu zana za kazi, kwani baada ya kuupokea alitakiwa kuhakikisha unakuwepo ofisini kwake kama alama ya uenyekiti wake.

Gazeti hili lilipowasiliana kwa njia ya simu na Mkuu wa Polisi Zanzibar, Kamishna Mussa Ali Mussa kuhusu madai hayo alisema, kitara (upanga) hicho ni kweli kimepotea, lakini yeye hahusiki kwa kuwa kila kitu kina utaratibu wake.

“Ni kweli kitara kilikabidhiwa kwa afande IGP na mimi nilishuhudia kikikabidhiwa, na ni kweli kitara hakijulikani kiliko, lakini mimi sihusiki na kupotea kwake. Ni kweli mimi nilikuwa ofisa mwenyeji wa mkutano huo, lakini siku hiyo zilitolewa zawadi nyingi, watu walipewa mikoba, kwa hiyo mtu akipoteza mkoba wake niulizwe mimi?” alihoji Kamishna Mussa.

Alisema kila kitu kina utaratibu wake na kwamba taarifa kwamba yeye amehojiwa kutokana na upotevu wa kitara hicho au kuna kamati imeundwa, hazina ukweli.

“Sijawahi kuona kamati hiyo. Kamati hiyo kwanza imeundwa na nani na inatoka wapi? Hayo maneno yanatengenezwa na watu wa nje,” alisema Kamishna Mussa.

Alisema kinachofanyika hivi sasa ni kukitafuta ili kiweze kurejeshwa kunakohusika.

Taarifa zingine zilidai hata bendera ya mezani ya mwenyekiti wa SARPCCO, aliyokabidhiwa sambamba na upanga huo nayo kuna hatihati ilipotea.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema aulizwe kamishina wa polisi Zanzibar.

“Suala hilo muulize Kamishina wa Zanzibar ndiye anayejua,” alisema Senso.

Uchunguzi unaonyesha kuwa maofisa katika ofisi ya IGP na ile ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, wamehojiwa akiwamo Kamishna Mussa, na kwamba upelelezi mkubwa umekuwa ukiendelea ndani ya jeshi hilo.

Hata hivyo, juhudi za gazeti hili za kutaka kufahamu uamuzi wa SARPCCO katika ofisi yake ya uratibu iliyopo kwenye ofisi za Makao Makuu ya Kanda ya Polisi wa Kimataifa (INTERPOL), Harare, Zimbabwe, hazikuzaa matunda baada ya baruapepe iliyotumwa kwa ofisa mratibu wa SARPCCO ambaye pia ni mkuu wa ofisi ya Kanda ya INTERPOL, C. Simfukwe kutopata majibu.

SARPCCO ilianzishwa mwaka 1995, Victoria Falls, Zimbabwe, lakini kisheria ilitambulika rasmi mwaka 2006 na lengo lake kuu ni kupambana na uhalifu wa kuvuka mipaka.

Uenyekiti wake ni mwaka mmoja, ambapo kwa sasa mwenyekiti ni Mkuu wa Jeshi la Polisi la Namibia Inspekta Jenerali, Luteni Jenerali Sebastian Ndeitunga, aliyepokea wadhifa huo kutoka kwa IGP Mwema.

Friday, August 30

IGP asafisha vigogo Uwanja wa Ndege


Siku chache baada ya kuibuliwa kwa kashfa ya kupitishwa kiholela kwa dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Jeshi la Polisi limemwondoa Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege Kamishna Msaidizi (ACP), Deusdedit Kato pamoja na Mkuu wake wa Upelelezi, David Mwafwimbo.

Mbali ya maofisa hao, pia jeshi hilo limemwondoa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Linus Sinzumwa, naye ikiwa ni miezi michache baada ya kutokea kwa ghasia wakati baadhi ya wakazi wa huko walipokuwa wakipinga mpango wa Serikali wa ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam.

Nafasi ya Kamanda Sinzumwa imechukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Zelothe Stephen kutoka Makao Makuu ya Polisi.

Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso ilisema Mkuu wa jeshi hilo, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema amemteua, ACP Selemani Hamisi kuchukua nafasi ya Kato ambaye anahamishiwa makao makuu ya jeshi hilo. Kabla ya uteuzi huo, Kamanda Hamisi alikuwa Makao Makuu Idara ya Upelelezi.

IGP Mwema pia amemteua Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Hamad Hamad kuchukua nafasi ya Mwafwimbo aliyehamishiwa mkoani Lindi kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Lindi (OCD).

Taarifa hiyo ya Polisi ilisema uhamisho huo ni wa kawaida kwa mujibu wa kanuni, taratibu na miongozo yake. Hata hivyo, katika siku za karibuni, kumekuwa na malalamiko mengi kuwa vyombo vya usalama katika uwanja huo vimeshindwa kudhibiti biashara hiyo na matokeo yake Tanzania imechafuka katika medani ya kimataifa kutokana na idadi kubwa ya vijana wake kukamatwa sehemu mbalimbali duniani.

Matukio ya karibuni yanahusisha kukamatwa kwa wasanii Agnes Masongange na Melisa Edward waliokamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo, Johannesburg, Afrika Kusini.

Kutokana na kashfa hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe aliamua kulivalia njuga suala hilo na kuchukua hatua kadhaa na pia alifichua jinsi wasichana hao walivyosaidiwa kupitisha dawa hizo na mtandao uliohusisha polisi, maofisa usalama wa taifa na baadhi ya wafanyakazi wa JNIA.

RPC Mtwara

Sinzumwa anaondoka Mtwara baada ya ghasia kubwa zilizozuka Mei mwaka huu wakati baadhi ya wakazi wa Mtwara walipokuwa wakipinga gesi kutoka Msimbati kusafirishwa kwa bomba hadi Dar es Salaam.

Katika ghasia hizo, ambazo Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), liliingilia kati, polisi walishutumiwa na wakazi wa huko kwa kutumia nguvu kubwa na kuwasababishia madhara.

RAIS KIKWETE AMUOMBA RAIS WA UGANDA AONGEE NA KAGAME ILI KUMALIZA UGOMVI ULIPO

RAIS Jakaya Kikwete, amewasiliana na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ili azungumze na Rais wa Rwanda, Paul Kagame kwa nia ya kumaliza mvutano wa maneno kati yao kwa busara.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema hayo jana bungeni, alipokuwa akijibu swali la Kiongozi wa Upinzani bungeni, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema).

“Tunataka suala hili limalizike kwa njia ya busara, ili watu waendelee kuchapa kazi, ninaamini busara zitatumika kumaliza tatizo hilo,” alisema.

Akiuliza swali katika kipindi cha maswali ya Papo kwa Hapo kwa Waziri Mkuu jana, Mbowe alitaka kujua kauli ya Serikali na mikakati iliyopo kupata suluhu katika mvutano wa maneno uliojitokeza kati ya Rais Kikwete na Rais Kagame.

Pia Mbowe alitaka Serikali kuunda jopo la ushawishi wa kimataifa, kutokana na Rwanda kuonekana kushawishi nchi za Uganda na Kenya, jambo ambalo linaashiria kuitenga Tanzania katika shughuli mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Mbowe, kitendo cha marais wa Kenya, Uganda na Rwanda kukutana katika mikakati ya kuanza kutumia bandari ya Mombasa ambayo ingekuwa ya nchi za Afrika Mashariki, ni dalili kuwa Tanzania imeanza kutengwa.

Mbowe alisema pamoja na kuanza kutengwa kwa Tanzania katika shughuli za Afrika Mashariki pia kumekuwa na mgogoro uliozuka hivi karibuni wa Bunge la Afrika Mashariki, kutaka vikao vya Bunge hilo vifanyike kwa kupokezana katika nchi wanachama, tofauti na ilivyokuwa awali, ambapo vikao hivyo vilifanyika Arusha.

Hata hivyo, Pinda katika jibu lake, alisisitiza kuwa hakuna sababu ya Serikali kuunda jopo la kutafuta ushawishi wa suluhu na Rwanda kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwa kuwa hakuna sababu za kufanya hivyo.

Hakuna uhasama Akifafanua, Pinda alisema Serikali haina sababu ya kujenga uhasama na Rwanda, kwa kuwa nafasi ya Tanzania na mchango wake katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu na Afrika unajulikana.

Alisisitiza, kuwa ushauri aliotoa Rais Kikwete wa kutaka Rwanda kukaa meza moja na waasi, ulikuwa wa busara na haukuwa na tatizo lolote.

Kutokana na msingi huo, alifafanua kwamba ndiyo maana Tanzania haiangalii mvutano huo wa maneno kama tatizo, ingawa Serikali haitapuuza suala hilo linaloonesha kuwepo kwa dalili ya kutoelewana.

“Ukilitazama suala hili huwezi kuamini kama kweli kauli ya Rais Kikwete ingeleta haya, nadhani wenzetu wanalitazama kwa namna tofauti na sisi tunavyolitazama,” alisema.

Pinda alirejea kiini cha mtafaruku huo, kuwa ni ushauri wa Rais Kikwete kwa nchi ya Rwanda kukaa meza moja na waasi, ili kuacha mapigano kwa maslahi ya wananchi wa Rwanda.

Alisema kauli hiyo iliyotolewa na Rais Kikwete katika mkutano wa Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Ethiopia, ilikuwa na nia njema kwa maslahi ya Rwanda, lakini imechukuliwa tofauti nje ya mkutano huo.


Propaganda za biashara
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba, alisema kauli zinazotolewa kuwa mizigo ya Rwanda haitapitishwa kwenye bandari ya Dar es Salaam, ni propaganda za kibiashara kutoka nchi washindani.

Hata hivyo, Dk Tizeba hakuwa tayari kubainisha ni nchi ipi inahusika zaidi kutoa propaganda hizo ingawa aligusia kwamba ni nchi zenye bandari.

Alisema baada ya kukutana na wafanyabiashara wa Rwanda na viongozi wa Serikali ya nchi hiyo, wamebaini kuwa hakuna upande uliozuia mizigo kupita Tanzania.

“Huku wanasema kuna maelekezo kwamba wafanyabiashara wa Rwanda wasipitishe mizigo Tanzania, lakini kwa Rwanda wao wanasema Tanzania imezuia mizigo ya Rwanda kupita Tanzania … tumebaini kuwa kauli hizi hazikuwa na ukweli,” alisema.

Alisema wafanyabiashara wa Rwanda wamesema kama Tanzania wanataka Rwanda ipitishe mizigo mingi, ifanye marekebisho kadhaa, ikiwemo kukabiliana na matatizo kama lililowahi kutokea la kupotea kwa kontena mbili za dhahabu na mbolea, kuangalia tozo za kusafirisha magari yasiyosajiliwa Tanzania na kupunguza wingi wa mizani ambao wanadai unachelewesha usafirishaji.

Pia Tizeba alisema walilalamikia udokozi wa vitu vidogo kwenye magari bandarini, jambo ambalo limefanyiwa kazi na hali hiyo haipo tena, kwani baadhi ya magari vifaa vyao vilikuwa vikiibwa maeneo mengine kabla ya kufika Dar es Salaam.

“Kuna mambo mengi yanafanyiwa kazi ikiwamo kuwa na treni mbili za mizigo hadi Isaka, ambazo zitasafirisha mizigo ya Rwanda, Kongo na Burundi, na pia kuweka ofisa wa bandari Kigali, ambaye atakuwa akishughulikia matatizo na kuanzisha mizani ambayo itapima gari likiwa linatembea na kuwa na mizani maeneo matatu,” alisema.

Kuhusu hatua ya Rais Kagame kuzindua mpango wa nchi yake kutumia bandari ya Mombasa, Tizeba alisema nchi inaweza kuwa na njia nyingi za kupitishia mizigo, na kubainisha kuwa bado Tanzania ndilo eneo pekee zuri kwa kusafirisha mizigo kwa nchi zisizo na bandari.

Thursday, August 29

Dk Ndalichako: Siasa zisipewe nafasi kwenye mitihani yetu


Swali: Unazungumziaje alama za upimaji wa mwanafunzi (continuous assessment) zinazotoka shuleni na nafasi yake katika matokeo ya mwisho?

Jibu: Ni vigumu kujua uhalisia wa alama zinazoletwa kutoka shuleni, wengine wanasema Necta tufuatilie huko shuleni ili kujua uhalisia wake, tutafanya vipi hilo wakati wafanyakazi wote wa Necta ukijumlisha na walinzi tupo 297 na shule za sekondari pekee zipo 430?

Mwaka 2011 wale wanafunzi walioandika vitu visivyoeleweka kwenye mitihani ya mwisho, kwenye alama zao za maendeleo zilizoletwa walikuwa mpaka na 75. Wengine walishindwa kuandika chochote kwenye mtihani wa mwisho lakini kwenye alama zao za maendeleo walikuwa na alama nzuri tu.

Ukiwauliza walimu wengine wanasema hawakuwa na walimu, wanasema walikuwa wanatumia waliomaliza kidato cha sita na hawajui kujaza vizuri hizo alama.

Wengine walisema mitihani ya ndani watoto wanatazamiana majibu na sababu nyingi kama hizo.

Kwa sasa kuna kamati imepewa jukumu la kuangalia hizo alama za maendeleo, kwa hiyo hilo ni eneo ambalo lazima tuliangalie.

Pia nafikiri kwa sababu ya mazingira ya shule zetu, tufike mahali tuwe na uwazi zaidi.

Nafikiri tufike mahali kwenye cheti tuweke alama za mtihani wa Necta na zile zilizotoka shuleni.

Tuseme mathalan huyo mtoto amepata A, lakini kwenye mtihani wa Necta alipata alama hii na ile ya shuleni alipata hivi. Baada ya hapo tukifika kwenye soko la ajira mwajiri achague kama ataangalia alama za shule au za Necta.

Swali: Tangu uanze kuiongoza Necta mpaka sasa unajivunia nini?

Jibu: Nimekaa Necta tangu mwaka 2005, yapo mengi naweza kujivunia, kwanza wakati naingia kila kitu kilikuwa manual (hatukutumia mashine), lakini hivi sasa kila kitu kuhusu mtihani kuanzia usajili tunatumia kompyuta.

Hili limesaidia kupunguza makosa, hasa kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea kwa sababu zamani watu walikuwa wanafanya udanganyifu sana.

Sasa hivi haiwezekani kutumia namba ya mtu mwingine. Usahihishaji kwa darasa la saba sasa hivi pia tunatumia mfumo wa OMR, zamani tulikuwa tunatumia watu 480 kusahihisha mitihani kwa siku 30.

Baada ya kufanya tathimini ya mfumo huu kwa mwaka jana, tumebaini kuwa mashine haikufanya kosa hata moja, baadhi yaliyotokea yalisababishwa na watu na mashine iliwaumbua.

Kwa kidato cha nne na kuendelea, hatujaanza kutumia kompyuta lakini kuna mengi tumefanya, sasa hivi tumeweka mfumo kuweka alama, zikishaingizwa kwenye mfumo kutoka kwenye kituo cha usahihishaji hakuna mtu anayeweza kuzigusa na akigusa anaonekana.

Hata msahihishaji akishaziweka mara moja hawezi kuzigusa tena na akigusa anaonekana. Kwa hiyo kwa mfumo huu, huwezi kumwongezea mwanafunzi alama. Kwa hiyo alama za wanafunzi zinakuwa katika mazingira salama sana.

Databank (benki ya mitihani) tumeiimarisha, maswali ni mengi tofauti na zamani ulikuwa unakuta kwa somo husika kuna mitihani miwili tu.

Kwa sasa maswali ni mengi, ndiyo maana hata kuvuja kwa mitihani hakuna. Kwa mfano, somo kama hisabati kuna maswali kama milioni moja, hata ukimpa mwanafunzi hawezi kuyafanya yote na ajue kwenye mtihani ni lipi litatoka.

Sasa hivi kweli mitihani ni salama sana, lengo letu ni kupunguza mikono kwenye mitihani. Naamini zaidi mifumo kuliko mtu na kwenye mitihani tukileta kuaminiana tunaweza kuwa pabaya.

Swali: Nini ambacho bado unatamani kukifanya ndani ya Necta?

Jibu: Ninachotamani kwa sasa ni kufika mahali tuwe na mashine zinazochapisha mitihani, kuhesabu na kuweka zenyewe kwenye bahasha.

Kwa sasa tunatumia kama siku 40 kuweka mitihani ya shule za msingi kwenye bahasha tu, hii ni kwa sababu lazima watu wanaofanya hii kazi wawe ni wachache na wenye weledi mkubwa. Hawa watu wangetumia hizi siku kufikiri namna ya kuwa na mitihani bora zaidi ingesaidia.

Suala jingine ni kuwajengea uwezo wa wafanyakazi wetu, haswa wa kuandaa maswali. Nina bahati nimesoma nje ya nchi nikasoma kwa undani juu ya mitihani.

Nataka tuwe tunawepeleka watu nje kusomea zaidi juu ya kazi zao, utunzi wa mitihani na masuala mengine, wawe na taaluma nzuri mtu awe na shahada au shahada ya uzamili kwenye eneo la utungaji wa mitihani tu.

Natamani pia jamii ijue majukumu yetu sisi kama baraza, baraza ni kama daktari tu, ukija unapimwa na kuambiwa una vijidudu 10 vya malaria. Daktari akishakupa hayo majibu ni jukumu lako kuangalia kama unatumia neti au mazingira yako vipi na ufanye nini ili usipate tena malaria. Kwa sasa watu wanakuwa na mtizamo hasi sana.

Nimekaa miaka minane baraza, wakati naingia watoto walikuwa hawaandiki madudu lakini sasa hali ni ngumu, wanachora vitu vya ajabu wanaandika matusi, wengine wanaonyesha kabisa hawajui kitu walichokuwa wanafanya.Baada ya hali hiyo, watu wengine wanasema kwa nini mnapeleka mitihani shuleni na hakuna vifaa, wengine wanasema kwa nini mtihani mmoja wakati shule hazifanani, mimi nauliza kwa nini shule isiwe na vitabu.

Wanasema mitihani ilingane na mazingira, Watanzania wote tuko sawa, kama hakuna vifaa shuleni hiyi siyo kazi ya baraza, umma unabidi uelewe hilo. Kwa sasa kitu ambacho naona ni tishio kwa baraza na mitihani ni mitizamo watu. Wengi wanaukataa ukweli, muda wote anatumia nguvu nyingi kuukataa ukweli.

Suala ni la kweli kabisa lakini mtu anakataa mimi naona hiyo ni hatari sana, huwezi kutibu tatizo bila kujua na kuukubali ukweli, ili tuweze kuboresha elimu lazima tukubali ukweli na kukubali kurekebisha, hali ikiendelea ilivyo sasa huko mbele tutakuwa kwenye hali mbaya sana


Ponda asimamisha shughuli Morogoro

Sheikhe Ponda Issa Ponda akiwa chini ya ulinzi wa
askari magereza wakati akielekea katika mahakama ya
hakimu mkazi Morogoro kusikiliza kesi yake inayomkabili. 

Morogoro. Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda jana alisababisha kusimama kwa shughuli za Serikali wilayani Morogoro baada ya ofisi kadhaa ikiwamo ya Mkuu wa Wilaya na baadhi ya mitaa kufungwa ili kupisha kusikilizwa kwa kesi inayomkabili katika Mahakama ya Mkoa wa Morogoro.

Tofauti na Agosti 19, mwaka huu wakati aliposafirishwa kwa helikopta, jana Sheikh Ponda alisafirishwa kwa barabara kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro akiwa chini ya ulinzi.

Mbali ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Morogoro kufungwa, nyingine ni Hazina Ndogo, Madini, Posta, Vipimo, Ukaguzi na Maktaba ya Mkoa.

Sababu za kufungwa kwa ofisi hizo pamoja na Mtaa wa Stesheni na maeneo ya Posta ni kuwa jirani na Mahakama hiyo. Magari yalizuiwa kutembea katika njia na maeneo ya karibu na ofisi pamoja na Mahakama hiyo huku kukiwa na idadi kubwa ya askari polisi na magereza kwa muda wote wa takriban saa mbili.

Alifikishwa mahakamani hapo saa 4:10 asubuhi akiwa katika basi la Magereza ambalo lilisindikizwa na jingine dogo, huku magari mengine yakisimamishwa kupisha msafara huo. Mahakama hiyo ilifurika umati wa wafuasi wa kiongozi kiasi cha kuwalazimu polisi na wana usalama wengine kuweka utepe kuwazuia wengi wao kufika katika jengo lililokuwa likitumika kuendesha kesi hiyo.

Shughuli katika eneo hilo zilirejea katika hali yake ya kawaida saa 6:25 mchana baada kesi yake kuahirishwa na msafara wa Sheikh Ponda kurejea katika Gereza la Segerea, Dar es Salaam ambako yuko rumande.

Muda wote tangu kuwasili mpaka kusikilizwa kwa kesi hiyo, wafuasi hao walikuwa kimya hadi pale ilipoahirishwa na hasa baada ya Sheikh Ponda kuwapungia mkono alipokuwa akielekea kwenye basi ambako walisikika wakisema: “Takbriir na kuitikia Allahu Akbar – (Mungu Mkubwa).”

Kesi yenyewe

Katika kesi hiyo, Wakili wa Serikali, Benard Kongola alisema mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, Richard Kabate kuwa Sheikh Ponda alitenda makosa ya uchochezi Agosti 10, mwaka huu saa 11.45 jioni kwenye maeneo ya Kiwanja cha Ndege, Morogoro.

Alisema siku hiyo, Sheikh Ponda alialikwa kutoa maelezo machache kwenye Kongamano la Eid lililoandaliwa na Umoja wa Wahadhiri Mkoa wa Morogoro (Uwamo) na kwamba akiwa hapo alitamka maneno: “Ndugu Waislamu, msikubali uundwaji wa kamati za ulinzi na usalama za misikiti kwani kamati hizo zimeundwa na Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), ambao ni vibaraka wa CCM na Serikali na kama watajitokeza kwenu watu hao na kujitambulisha kwamba wao ni kamati za ulinzi na usalama za misikiti, fungeni milango na madirisha ya misikiti yenu na muwapige sana,” huku akijua kutoa maneno hayo ni kosa kisheria.

Alisema kwa kufanya hivyo, Sheikh Ponda anayetetewa na mawakili watatu wanaoongozwa na Juma Nassoro, alivunja masharti ya Mahakama ya kifungo cha nje iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya Mei 9, mwaka huu iliyokuwa imetamka kuhubiri amani.

Katika shtaka la pili, Sheikh Ponda anadaiwa kuwashawishi wafuasi wake kutenda kosa la jinai kwa kuwaambia: Serikali ilipeleka jeshi Mtwara kushughulikia suala la vurugu iliyotokana na gesi kwa kuwaua, kuwabaka na kuwatesa wananchi kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Waislamu, lakini haikufanya hivyo kwa wananchi wa Loliondo waliokataa Mwarabu asipatiwe kipande cha ardhi ya uwindaji baada ya kudai ni mali yao kwa sababu asilimia 90 ya wakazi wake ni Wakristo.” Shtaka la tatu ni kudaiwa kutamka maneno yaliyoumiza imani ya watu wengine kama yalivyo katika shtaka la pili.

Baada ya kusoma mashtaka hayo, Kongola alisema walikuwa na mashahidi 15 na vielelezo vitatu ambavyo ni DVD mbili na kibali kilichotolewa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Morogoro(OCD), Agosti Mosi, 2013 cha kongamano husika na hati ya hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu, Mei 9, 2013.

Baada ya kusomewa, Sheikh Ponda alikana mashtaka yote matatu huku akikubali kuwemo kwenye kongamano hilo. Alikiri kukamatwa na polisi Agosti 11, Dar es Salaam.

Wakili wa utetezi, Nassor aliwasilisha ombi la dhamana kwa mteja akisema mashtaka hayo yote kisheria yana dhamana. Pia aliwasilisha ombi la kupatiwa hati yenye maelezo ya mlalamikaji ambaye ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani alisema kuwa kutokana na upelelezi upande wa mashtaka kukamilika, wanahitaji maelezo hayo kwa ajili ya kuandaa utetezi.

Hata hivyo, Wakili Kongola aliiomba Mahakama kutompa dhamana mshtakiwa kutokana na cheti kilichotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kupinga dhamana ya mshtakiwa huyo kwa masilahi ya usalama wa nchi.

Akitoa mwongozo wa maombi yaliyowasilishwa na pande zote mbili, Hakimu Kabate aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 11, mwaka huu itakapotajwa tena na kwamba Septemba 17, mwaka huu Mahakama itatoa uamuzi endapo mshtakiwa atapewa dhamana au la wakati itakapoanza kusikilizwa.

MWIGULU NCHEMBA ATAKA MBOWE NA DR. SLAA WAKAMATWE KWA MAUAJI YA RAIA

MBUNGE wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), amechafua hali ya hewa bungeni kwa kuitaka Serikali kuwachukuliwa hatua viongozi wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Mbunge huyo alisema mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe pamoja na Katibu Mkuu wake, Dk. Wilbroad Slaa, wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa madai ya kusababisha mauaji ya raia.

Mwigulu, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bara, alisema katika kipindi cha miaka miwili tangu nchi ilipotoka kwenye uchaguzi, viongozi hao wamekuwa wakihamasisha maandamano na kusababisha umwagaji wa damu za Watanzania.

“Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka miwili tangu nchi yetu ilipomaliza Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Mbowe na Dk. Slaa wamekuwa wakitoa kauli za wazi na hata kusababisha mauaji ya watu bila hatia.

“Kutokana na hali hii, sijui Serikali inafanya nini katika kuwachukulia hatua, kwani viongozi hawa wamekuwa wakitafuta umaarufu wa kisiasa kwa kuchochea chuki na mauaji dhidi ya raia.

“Kwa hali hiyo, tangu kipindi hicho hadi leo hii wanasubiri nini badala ya kwenda kuwaweka jela, kwani huko ndiko wanatakiwa kuwa,” alisema.

Mwigulu, alisema kukosekana kwa maadili kwa baadhi ya viongozi wa siasa, ambao wamekuwa wakitumia majukwaa na kuhubiri umwagaji damu ni hatari kwa taifa.

Alisema viongozi hao wamekuwa wakitumia majukwaa hayo na kusababisha vifo vya wananchi, huku akitaja vurugu zilizotokea katika mikoa ya Morogoro, Iringa, Arusha na Singida.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, alisema Serikali inafanya kazi kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kukusanya ushahidi na kwamba mahakama ndicho chombo chenye uamuzi wa mwisho dhidi ya adhabu kwa raia au kiongozi yeyote wa kisiasa.

Kauli hiyo ya Mwigulu ilionekana kuchafua hali ya hewa ndani ya Bunge, ambapo Mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (Chadema), alisimama na kuomba mwongozo wa Spika, huku akimtaka Mwigulu kuthibitisha kauli yake, vinginevyo aombe radhi.

Wenje alisema hoja ya Mwigulu imekosa mashiko na ina lengo la kuwadhalilisha viongozi wa Chadema, huku akisahau kuwa baada ya uchaguzi wa Arumeru Mashariki, aliyekuwa Mwenyetiki wa Chadema tawi la Usa River, Omari Mbwambo, aliuawa na watu anaodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM.

Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango (CCM), alitaka kujua Serikali inachukua hatua gani kwa wanasiasa wanaokiuka maadili na kusababisha uvunjifu wa amani.

“Wanataaluma kama vile madaktari, wahandisi, wahasibu na hata wakandarasi pindi wanapokiuka maadili ya kazi zao huchukuliwa hatua kwa kufutiwa leseni zao.

“Vile vile viongozi wa kisiasa wanayo maadili yanayowaongoza, kwanini pale wanapokiuka maadili ya kazi zao hawachukuliwi hatua kama ilivyo katika makundi hayo? (taaluma),” alisema Kilango.

LUKUVI: WABUNGE WENGI WAMO ORODHA YA DAWA ZA KULEVYA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi amesema baadhi ya majina ya wabunge yametajwa miongoni mwa watu wanaoshukiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya lakini Serikali haiwezi kuwataja hadharani kwa haraka.

Majibu hayo ya Waziri Lukuvi yamekuja baada ya wabunge kumbana na wengine wakizomea baada ya kueleza ugumu wa kutaja majina ya washukiwa pasi na ushahidi wa kutosha.

“Serikali haiwezi kutaja majina haraka kiasi hicho kwani inaogopa kukurupuka na kushindwa mahakamani, hivyo lazima tuwe makini sana na jambo hilo. Hatuwezi kukurupuka tu eti ni fulani wakati hatuna vithibitisho.

“Kumbukeni wengine mpo humu ndani ya Bunge na tukianza wengi mtakwisha maana katika orodha hiyo kubwa na ninyi mmo na orodha ni kubwa kweli ambayo wakati mwingine inatakiwa umakini wa hali ya juu,” alisema Lukuvi alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Karatu (Chadema), Mchungaji Israel Natse.

Katika swali lake ambalo lilisababisha kelele za kuzomea, Natse alitaka majina hayo yatajwe hadharani. Hata hivyo, hali ilitulia baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuingilia kati na kusema: “Hii tabia ya zomeazomea siitaki humu ndani, acheni tabia hiyo lazima mumsikilize mtu kwa kile anachokisema kwanza lakini mtindo huu si mzuri...”

Patashika hiyo ilitokana na swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Catherine Magige aliyetaka kujua iwapo Serikali inaweza kuwaambia Watanzania ukubwa wa biashara hiyo nchini na kama haioni kama kuna tatizo katika ukaguzi wa abiria na mizigo katika viwanja vya ndege na juhudi za Serikali kumaliza tatizo hilo.

Akijibu swali hilo, Lukuvi alisema ukubwa wa biashara hiyo hapa nchini unadhihirishwa na idadi ya Watanzania 274 waliokamatwa kati ya mwaka 2008 hadi Julai mwaka huu kwa kosa la kujihusisha na dawa za kulevya katika nchi mbalimbali za nje.

Alisema Serikali inafahamu ukubwa wa tatizo la matumizi ya biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya nchini na alitaja takwimu za ukamataji wa dawa hizo katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 hadi Machi, 2012.

Alisema pamoja na kukamatwa kwa Watanzania hao nje ya nchi, wageni 31 wanashikiliwa mahabusu katika Magereza ya Keko na Ukonga, Dar es Salaam ambao ni raia wa Iran, Pakistan, Senegal na Afrika Kusini.

Hata hivyo, katika swali lake la nyongeza, Magige alisema uteketezaji wa dawa zinazotajwa kukamatwa umekuwa wa siri kiasi cha kutiliwa shaka kuwa huenda zinachukuliwa na maofisa waliozikamata ndiyo maana hakuna uwazi.

Kuhusu hilo, Waziri Lukuvi alisema suala la uteketezaji wa dawa hizo hauko wazi kutokana na sheria zilizopo kutotoa nafasi ya kuteketezwa mapema kwa kuwa zinatumika kwa ajili ya ushahidi akisema wakati mwingine hukaa zaidi ya miaka 10.

Wednesday, August 28

TAARIFA YA RASMI YA KUREJESHWA URUSHAJI MATANGAZO RADIO IMAAN FM NA KWA NEEMA FM


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KUREJESHWA KWA URUSHAJI MATANGAZO RADIO IMAAN FM NA KWA NEEMA FM RADIO

1.0 Utangulizi:

Mnamo tarehe 26/02/2013 Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ilitoa uamuzi wa kuvifungia vituo vya utangazaji vya Radio Imaan ya mjini Morogoro na Kwa Neema FM Radio ya jijini Mwanza baada ya kukiuka Sheria na Kanuni za Utangazaji.

Kamati ya Maudhui iliuita uongozi wa vituo hivyo tarehe 11/02/2013 na tarehe 14/02/2013 ili kujitetea na vyote vilikiri kosa. Baada ya kutafakari utetezi wa Radio Imaan na Radio ya Kwa Neema FM na kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Utangazaji, Kamati iliamua kutoa adhabu kwa vituo vyote viliwi kama ifuatavyo:-

a) Vituo vyote vilipewa onyo pamoja na kufungiwa kurusha matangazo kwa kipindi cha miezi sita kuanzia
tarehe 26/02/2013;

b) Vituo vyote vilitakiwa kuithibitishia Mamlaka ya Mawasiliano na Kamati ya Maudhui kwa maandishi kuwa hawatarejea kutenda kosa la aina hiyo au linalofanana na hilo. Ikiwa vitarudia Kamati ya Maudhui haitasita kuvifutia leseni zao za utangazaji.

2.0 Kutekeleza adhabu na hatua zilizochukuliwa na vituo hivyo na Mamlaka ya Mawasiliano:

Baada ya Uamuzi huo kusomwa, vituo vyote viwili vilianza kutekeleza adhabu mara moja kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utangazaji. Mamlaka ya Mawasiliano ilipokea barua ya udhibitisho wa kutofanya kosa tena yaani “Commitment letter” pamoja na sera ya uhariri (Editorial Policy) na ratiba ya vipindi kutoka kwa vituo vyote viwili.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ilifanya ukaguzi kwa vituo vyote viwili ili kujiridhisha na kuzipitia sera za uhariri pamoja na mwongozo wa vipindi kabla ya kuvifungulia.

3.0 Kurejeshwa kwa Matangazo

Kamati ya Maudhui iliandika barua tarehe 27/08/2013 kuhusu kuvifungulia vituo hivyo vya utangazaji vya Radio Imaan ya mjini Morogoro na Kwa Neema FM Radio ya jijini Mwanza baada ya kutumikia adhabu kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utangazaji. Vituo hivi vimeanza kurusha matangazo yake kuanzia leo tarehe 28/08/2013 baada ya muda wa adhabu kuisha.

Kamati ya Maudhui inapenda kutumia fursa hii kuvionya vyombo vya habari vya utangazaji vya redio na televisheni kuwa makini katika kutekeleza masharti ya leseni pamoja na kufuata Sheria na Kanuni za Utangazaji. Kamati ya Maudhui haitasita kutoa adhabu kali au kuvifungia vituo vitakavyokiuka Masharti ya leseni, Sheria pamoja na Kanuni za Utangazaji au hata kuvifutia leseni zao.

Kamati ya Maudhui inatoa wito kwa vyombo vya habari vya utangazaji kuzingatia Sheria, Kanuni na Masharti ya leseni ilikuboresha Sekta ya Utangazaji na kudumisha amani nchini.

Eng. Margaret Munyagi
Mwenyekiti,
Kamati ya Maudhui Ya TCRA,
S.L.P. 474,
DAR ES SALAAM.
28/08/2013

----

KUHUSU KAMATI YA MAUDHUI:

1.1. Kamati ya Maudhui ni kamati iliyoundwa kwa mujibu wa sehemu ya IV kifungu cha 26 (1) cha Sheria Namba 12 ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ya mwaka 2003, na marekebisho yake katika kifungu 173 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) Mwaka 2010

Kwa mujibu wa sheria, majukumu na kazi za Kamati ya Maudhui ni pamoja na:-

(a) Kumshauri Waziri wa Sekta kuhusiana na Sera ya Utangazaji nchini;
(b) Kushughulikia malalamiko kutoka kwa watangazaji na watumiaji wa huduma za utangazaji nchini;
(c) Kusimamia na kuhakikisha kuwa kanuni za utangazaji zinafuatwa.
(d) Kusimamia na kufuatilia maudhui ya vituo vya utangazaji.

1.2. Kamati hii ilianza kazi zake Oktoba 2012 baada ya kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (MB) tarehe 4 Desemba, 2012.

1.3. Kamati ya Maudhui inaundwa na wajumbe watano. Wanne ni wateuliwa wa Waziri mwenye dhamana ya Sekta ya Utangazaji na Mwenyekiti ambaye huchaguliwa miongoni mwa wajumbe wa Bodi ya TCRA. Muundo huo umetolewa na sehemu ya 26 (2) ya Sheria ya TCRA ya Mwaka 2003.

Majina ya wajumbe ni kama ifuatavyo:-

i. Mhandisi Margareth Munyagi -Mwenyekiti
ii. Bwana Walter Bgoya -Makamu Mwenyekiti
iii. Bwana Abdul Ngarawa -Mjumbe
iv. Bwana Joseph Mapunda -Mjumbe
v. Bwana Yusuf Nzowa -Mjumbe