Tuesday, January 31

JK abariki posho mpya za wabunge

KILA MMOJA KULIPWA 330,000 KWA SIKU, ZITTO, MAKAMBA, KIGWANGALA WASULUBISHWA KWA KUZIPINGA

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema tayari Rais Jakaya Kikwete amesaini kuidhinisha ongezeko la posho za vikao (sitting allowance) kwa wabunge kutoka Sh70,000 hadi Sh200,000 kwa siku. Kupitishwa kwa posho hizo ambazo ziliandikwa kwa mara ya kwanza na gazeti hili, kunafanya sasa mbunge kupokea Sh330,000 kwa siku; Sh200,000 zikiwa ni posho ya kikao, Sh80,000 posho ya kujikimu na Sh50,000 nauli.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao cha utanguzi cha wabunge jana, zilidai kuwa baada ya Pinda kutoa taarifa hiyo, wabunge walishangilia huku Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, akisimama na kudai kuwa taarifa alizonazo ni kwamba Rais Kikwete alikuwa hajasaini kuidhinisha posho hizo.

Hatua hiyo ilisababisha Mbunge wa Kondoa Kaskazini, Juma Nkamia (CCM), kusimama na kuhoji iwapo Zitto ni miongoni mwa wasemaji wa Rais kabla ya Pinda kusimama na kuthibitisha kusainiwa kwa posho hizo akisema siyo ajabu kwani hata watumishi wa Serikali wanalipwa kati ya Sh150,000 na Sh200,000. Hata hivyo, Zitto alitetea msimamo wake kwamba alitarajia baada ya kusainiwa kwa posho hizo na Rais, angepewa masharti mapya ya kazi za ubunge.

Katika kikao hicho baadhi ya wabunge wanadaiwa kuwashambulia Zitto, Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba na Mbunge wa Nzega (CCM), Dk Khamis Kigwangwala kwamba wamekuwa mstari wa mbele kupinga posho hizo hadharani. Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye anadaiwa kwamba aliungana na Pinda kuthibitisha kwamba Rais Kikwete ameidhinisha posho hizo mpya, pia aliwashambulia wabunge wanaozipinga akisema kwamba wanafuta umaarufu wa kisiasa.

“Wanachotafuta ni umaarufu wa kisiasa tu, mimi ninavyojua umaarufu wa kisiasa unakuja kwa kufanya kazi za kibunge za wananchi lakini siyo kupinga posho,” chanzo chetu cha habari kilimnukuu Makinda.

Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa anadaiwa kwamba alitumia mafumbo kuwashambulia wabunge hao ambao wamejitokeza kupinga nyongeza hiyo ya posho. Kauli hiyo inadaiwa kuungwa mkono na Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Nkumba ambaye alidai kuwa hawezi kumsemea Zitto kwa sababu ni kawaida yake kupinga, lakini akaelekeza shutuma zake kwa Makamba kwamba ameanza kupinga baada ya kugharamiwa na CCM. “Januari anapinga posho hizo kutokana na CCM kumpa gari, nyumba na analipwa na chama,” kilisema chanzo chetu kikimkariri Nkumba.

Pia, Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM), anadaiwa kumshambulia Zitto kuwa lazima apinge posho hizo kwa sababu, anapewa fedha na wafadhili kutoka nchi za nje. “Shelukindo anasema amefanya ziara nje na kuhakikisha kuna wahisani wanamfadhili Zitto kwa hiyo ana haki ya kupinga posho hizo,” chanzo chetu hicho kilimkariri Shelukindo.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa baada ya mashambulizi hayo, Dk Kigwangwala alisimama kutetea msimamo wake kwamba ongezeko hilo halina ‘mashiko’ na haliwezi kuelezwa mbele ya umma likaeleweka, lakini alizomewa na wabunge wengi huku wakimtaka kukaa chini.

Hatua hiyo ilisababisha Zitto kusimama na kueleza kuwa tatizo la wabunge kwamba wana fikra finyu, kauli ambayo alitakiwa na wenzake kuwaomba radhi kuwa amewatukana. “Zitto ametumia Kiingereza kuwa tatizo la wabunge ‘we think small’, Shelukindo na (John) Komba wakaja juu wakitaka kuwaomba radhi kwa kuwatukana,” chanzo chetu kilieleza. Zitto anadaiwa kusema wabunge walitakiwa kujenga hoja ya kuongeza fedha za mafuta ya gari wanayolipwa hivi sasa Sh2.5 milioni kwa mwezi, kutokana na kupanda kwa nishati hiyo, lakini siyo posho.

Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alinukuliwa akisema matatizo ya posho yamefikia hapo baada ya kuonekana ni ya watu binafsi siyo mfumo hivyo, wanaopinga wanaonekana kama wanatafuta umaarufu na wana vipato vya fedha, akaitaka kamati ya uongozi ijadili na kupata mwafaka badala ya wajumbe kutofautiana mbele ya umma. Wabunge wengine wanaodaiwa kutetea posho hizo ni Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini na Jenister Mhagama (Peramiho CCM).

Msimamo wa January
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Makamba alijibu: “Si sahihi kwangu kutoa taarifa za kikao cha ndani. Lakini msimamo wangu kwenye suala hilo unajulikana na haujabadilika. Msimamo wa CCM ulishawekwa wazi na sote tunaujua. Nitalizungumzia suala hili kwa kirefu katika siku zijazo.”

Kuhusu taarifa kwamba anagharamiwa na CCM, alisema hawezi kuzungumzia suala hilo na badala yake kutaka kiulizwe chama hicho.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipoulizwa kuhusu taratibu za kuwagharamia viongozi wa chama chake ambao ni wabunge alisema: “Mbunge au kiongozi yeyote wa chama mwenye nafasi nyingine anagharamiwa na chama pale anapokwenda kufanya shughuli za chama tu na si vinginevyo.”

“Kwa hiyo kama ni mbunge suala la mafuta, dereva, mahali pa kulala na mahitaji mengine anagharamiwa na taasisi anayoifanyia kazi na siyo chama.”

“Kwa mfano, mimi kwenye sekretarieti hata posho za vikao huwa sichukui, nadhani na mwenzangu January naye sidhani kama huwa anachukua posho, kwa sababu tukifanya hivyo ni kama tunakiumiza chama, huo ndiyo msimamo wetu na uko wazi wala siyo kificho.”

Kwa upande wake, Zitto alisema jana kwamba hakuwa katika nafasi ya kuzungumzia suala hilo na badala yake kuahidi kwamba atalizungumza leo atakapokutana na waandishi wa habari.

Wabunge walia njaa
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zilisema wabunge hao walilalamikia kucheleweshwa kulipwa posho zao za wiki mbili walizokaa Dar es Salaam wakati wa vikao vya kamati.

Walidai hivi sasa wanaishi kwa shida huku wakihoji sababu za
kucheleweshewa.

Imeelezwa kwamba Spika Makinda alidai kuwa fedha hizo zipo na kwamba kilichochelewesha ni uhakiki wa wabunge waliohudhuria vikao.

Makinda alisema baadhi ya wabunge wamekuwa wakilipwa posho za vikao bila kuhudhuria, hatua ambayo imesababisha Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), kuhoji maswali mengi.

Wauguzi Muhimbili wawakataa wanajeshi


LICHA ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa amri kwa madaktari wote wenye mikataba na Serikali kurejea kazini, bado wanataaluma hao jana waliendeleza mgomo baada ya kutia saini vitabu vya mahudhurio na kutoweka kusikojulikana huku wauguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wakitoa msimamo mpya kwamba hawako tayari kufanya kazi na madaktari kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ).

Juzi, Waziri Mkuu Pinda alitoa onyo kwa madaktari hao akiwataka kurejea kazini kufikia jana kinyume chake ambaye angeshindwa angekuwa amejifukuzisha kazi na kwamba madaktari wa JWTZ wangechukua nafasi zao.
Agizo hilo la kwamba wangewatumia madaktari kutoka JWTZ jana liliamsha hasira za wauguzi Muhimbili ambao walitangaza msimamo wao wa kutofanya kazi nao.

Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi Tanzania, Tawi la MHN, Paul Magesa alisema madaktari hao hawana uwezo wa kufanya kazi katika hospitali hiyo ya taifa ambayo ndiyo kubwa nchini kwa kuwa inahudumia wagonjwa walioshindikana katika hospitali wanazotoka.

“Ifahamike kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ni ya rufaa na inapotokea wagonjwa walioshindikana katika hospitali nyingine inakuwaje leo wakaletwa madaktari kutoka katika hospitali hizo kuja kutibu?” alihoji Magesa na kuongeza:
“Sisi tulishafanya kazi nao mwaka 2005 na tunawafahamu wengi hawajui mambo mengi, watakuja kutuuliza na kutuongezea kazi za kufanya... tunaomba katika hili Serikali isikwepe tatizo, ilishughulikie kwa maslahi ya taifa,” alisema.

Hali mbaya
Hali katika hospitali hiyo kuu ya nchini imezidi kuwa mbaya, kutokana na kuendelea kwa mgomo wa madaktari hao huku kukiwa na dalili nyingine za mgomo wa wauguzi kupinga kufanya kazi na madaktari kutoka jeshini.
Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na uongozi wa hospitali hiyo, zilisema kwamba madaktari wengi walifika na kusaini katika kitabu cha mahudhurio na kuondoka.

Mmoja wa madaktari katika hospitali hiyo, Dk Azizi Keto aliyekuwa katika wodi ya Mwaisela alisema kauli ya Pinda dhidi ya madaktari imewakatisha tamaa na kuwavunja moyo wa kufanya kazi. Alisema hali ni mbaya ndiyo sababu hata waliofika asubuhi hawakujisikia kufanya kazi.

Katika hospitali hiyo madaktari walioendelea na kazi ni wale washauri, wanaotarajia kustaafu na walioingia mkataba na Serikali mwaka 2005, walipoitwa wakati madaktari walipogoma.
Vilio vilitawala jana katika eneo la nje ya Wodi ya Mwaisela huku waombolezaji wakidai kuwa kama si mgomo huo wa madaktari, ndugu zao wasingepoteza maisha.

Mmoja wa waombolezaji alikaririwa akisema ndugu yake alipoteza maisha bila ya kupata huduma hospitalini hapo.
Baadhi ya wagongwa waliowasili katika hospitali hiyo wakitokea hospitali mbalimbali, walirudishwa bila ya huduma.

Muhimbili yakiri
Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa mgomo huo, uongozi wa MNH umekiri kwamba hali ya upatikanaji wa huduma katika hospitali hiyo imezidi kuzorota.

Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Hospitali hiyo, Aminael Aligaesha aliwaambia waandishi wa habari kuwa madaktari walio wengi wamefika na kujiorodhesha kwenye daftari la mahudhurio lakini wakagoma kufanya kazi.

Hospitali za Dar
Kwa upande wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, madaktari wamegawanyika wengine waliendelea na mgomo na wengine walionekana wakitoa huduma kwa wagonjwa.

“Pamoja na kwamba wagonjwa wanahudumiwa lakini, inachukua muda mrefu kuipata huduma jambo linaloonyesha kuwa mgomo upo,” alisema mmoja wa wagonjwa hospitalini hapo.
Taarifa hizo ziliongeza kwamba madaktari waliogoma, jana asubuhi walifika hospitalini hapo na kusaini majina yao kisha kuondoka.

Habari zilisema maofisa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, walifika hospitalini hapo kuhakiki majina ya madaktari hao lakini walipoondoka na wao wakaondoka.
Katika Hospitali ya Amana, Ilala nako baadhi ya madaktari walifika kazini wakasaini mahudhurio na kuondoka bila kufanya kazi yeyote.

Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Shimwela Meshack alisema hali ni mbaya katika hospitali hiyo kutokana na madaktari wote kufika kazini lakini wakagoma kutoa huduma.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mwananyamala, Dk Sophinias Ngonyani alisema mgomo huo ulifanywa na madaktari ambao hawajaajiriwa tu.

“Mgomo huu upo kwa wale wasioajiriwa ila tunachokifanya kwa sasa ni kuhakiki waliokuwepo na wasiokuwepo kujua idadi ilio sahihi,” alisema.

Ofisa Afya wa Manispaa ya Kinondoni, Dk Gunini Kamba alisema hospitali hiyo ina wataalamu wa afya 58, kati yao 42 ni madaktari, watano wako katika kitengo cha wafamasia, watano wengine maabara na sita katika kitengo meno.

Hospitali mikoani
Mkoani Morogoro, madaktari walifika kazini kama kawaida lakini hawakutoa huduma hali iliyofanya wagonjwa wasote kwa muda mrefu bila huduma.

Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Frida Mokiti alisema madaktari wote wameripoti kwenye maeneo yao ya kazi na kwamba taarifa zaidi angezitoa baada ya muda wa kazi.

Hali kama hiyo pia iliripotiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru ambako madaktari waliingia kazini lakini baada ya kusaini daftari la mahudhurio waliendelea na mgomo.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo jana asubuhi alifanya ziara ya ghafla katika hospitali hiyo na kuonana na uongozi. Hata hivyo, hakuna taarifa ambayo ilitolewa juu ya nini kilichozungumzwa.

Madaktari wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, waliendelea na mgomo huku baadhi yao wakisisitiza kuwa hawawezi kurejea kazini hadi Serikali itakapoamua kutekeleza madai yao.

“Sisi tunachokitaka ni kutekelezewa madai yetu, hiyo kauli ya Waziri Mkuu ya kututishia kutufukaza kazi kama hatutarejea kazi kuanzia leo (jana) wala hatuiogopi hata kidogo, tunachotaka ni haki yetu itendeke,” alisema mmoja wa madaktari kwa sharti la kutotajwa jina.

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk Eleuter Samky alisema hadi saa 7:00 mchana jana kulikuwa na madaktari watano tu kati ya 75 waliokuwa wamefika kazini.

Katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi, hali pia imekuwa ya kusuasua. Jana kulikuwa na msururu mkubwa wa wagonjwa wa nje waliokuwa mapokezi, wakisubiri huduma kwa zaidi ya saa nane huku wengi wakilalamikia uchache wa madaktari kwani aliyekuwapo zamu alikuwa mmoja tu.

Baadhi ya madaktari ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini walisema mgomo wa sasa ni mbaya kuliko ule wa awali kwani kwa sasa wanaandika majina yao kwenye daftari la mahudhurio lakini hawatoi huduma kwa wagonjwa.

Wanasiasa waingilia kati
Baadhi ya wanasiasa wameingilia kati mgomo huo wakiwataka madaktari hao kurejea kazini kama walivyoagizwa na Pinda ili kuokoa maisha ya Watanzania.

“Uhai wa mtu ni kitu kikubwa sana… Mimi naona ni vyema busara ikatumika ili kuokoa maisha ya Watanzania yanayopotea,” alisema Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Hata hivyo, alisema madaktari hao wanayo madai ya msingi lakini akawataka watekeleze wajibu wao huku wakifanya mazungumzo na Serikali.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema madaktari wanapaswa kufahamu kwamba kuendelea kugoma ni kuchezea maisha ya wananchi.

Alisema kitu cha muhimu ni madaktari hao kurudi kazini kama walivyoagizwa na Waziri Mkuu na wasifikiri kwamba, Serikali itaendelea kuwavumilia huku ikiona maisha ya Watanzania yanapotea.

Aliwataka wajifunze kwa kilichotokea mwaka 2004 wakati wa utawala wa Rais Benjamini Mkapa, ambako waligoma na Serikali ikaamua kutumia madaktari kutoka vikosi vya jeshi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alimtaka Pinda kuacha vitisho na matumizi makubwa ya vyombo vya dola kwa madaktari wanapotumia uhuru wao wa kikatiba wa kukusanyika huku akisema chama hicho kinaunga mkono madai ya msingi ya madaktari.

Tucta yawageuka
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limesema haliwaungi mkono madaktari hao kutokana na kushindwa kufuata utaratibu wa mgomo.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Nicholaus Mgaya alisema sababu ya kutounga mkono mgomo huo ni baada ya madaktari hao kukaidi wito wa kukutana na Serikali jambo ambalo alisema ni kinyume na taratibu za kazi.

“Kwa hali hii madaktari wamepotea maboya. Kitendo cha kuitwa na Waziri Mkuu ili kufanya mazungumzo na kukataa ni dhahiri kuwa mgomo huo si halali maana walitakiwa kusikiliza Serikali inasemaje baada ya hapo wangeweza kukataa kama wangeona bado madai yao hayajafanyiwa kazi lakini kitendo cha kugoma bila kufanya mazungumzo ni kosa,” alisema Mgaya.

Habari hii imeandaliwa na Geofrey Nyang'oro, Gedius Rwiza, Leon Bahati, , Raymond Kaminyoge na Joseph Zablon, Dar; Godfrey Kahango, Mbeya; Mussa Juma, Arusha na Rehema Matowo, Moshi.

Sunday, January 29

Madaktari wawagomea mawaziri mkutanoni


SAKATA la madaktari nchini linazidi kuchukua sura mpya baada ya wataalamu hao kukataa hoja za ujumbe wa Serikali ulioongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi, Hawa Ghasia huku wakigoma kusikiliza kauli yoyote kutoka kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk Hadji Mponda

Wakati mawaziri hao wakikumbwa ana tafrani hiyo tayari wauguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na ile ya Mkoa wa Dodoma wametishia kusitisha utoaji huduma ifikapo Jumatatu kama masuala yao hayajapatiwa ufumbuzi.

Vigogo wa Serikali waliofika kukutana na madaktari hao jana ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na naibu wake, Dk Lucy Nkya, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa.
Tukio hilo lilitokea jana kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Star Light, Jijini Dar es Salaam ambako madaktari hao walikusanyika na baadaye kupewa taarifa kuwa kuna ujumbe wa Serikali utafika kwa majadiliano. Madaktari hao waliwatimua ujumbe huo baada ya kuusikiliza juu ya wito wao wa kuwataka wasitishe mgomo ili wafungue ukurasa wa majadiliano, wakajibiwa kuwa kwa sasa ni wakati wa kutekeleza kwa vitendo na siyo ahadi.

Ujumbe huo wa Serikali uliwasili ukumbini hapo majira ya mchana na kukaribishwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka ambaye baada ya kuwawekea viti pembeni mwa jukwaa kuu, aliwatambulisha kwa washiriki. “Ugeni tuliokuwa tunasubiri umefika, si rahisi sisi wote kuwafahamu ni vema wangejitambulisha wao kwa majina kisha tuendelee na utaratibu tuliojiwekea,” alisema Dk Ulimboka.

Mara baada ya kauli hiyo, wageni hao walianza kujitambulisha. Wa kwanza alikuwa Waziri Ghasia aliyewasalimia madaktari hao na kujitambulisha kisha kueleza kuwa aliongoza ujumbe huo kuwasilisha taarifa ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Dalili mbaya kwa ujumbe huo, zilianza kujitokeza walipoitika kwa nguvu salamu ya Waziri Ghasia huku wakiwanyamazia Waziri wa Afya na maofisa waandamizi wa wizara hiyo.

Baada ya tukio hilo kumalizika, Dk Ulimboka alitoa taratibu za mkutano kuwa ni kusoma taarifa maalumu iliyoandaliwa kwa ajili ya kupelekwa kwa Waziri Mkuu. “Sisi hapa tutawakabidhi taarifa iliyoandaliwa na madaktari ambayo ni maalumu kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda na baada ya kuwasomea, tutawakabidhi kisha tusubiri majibu ya taarifa yetu tukiwa hapahapa,” alisema Dk Ulimboka.

Dk Ulimboka alisoma taarifa hiyo mbele ya wageni hao ambayo ilitaja madai yao kadhaa ikiwemo kumtaka Waziri Ghasia kumshauri Rais Jakaya Kikwete kuwaondoa katika wizara hiyo, Waziri Mponda na naibu wake Dk Nkya, Katibu Nyoni na Mganga Mkuu, Dk Mtasiwa.

Mara baada ya kusoma taarifa hiyo alikabidhi barua hiyo kwa Waziri Ghasia huku akisisitiza kuwa wataendelea na mgomo hadi watakapopatiwa majibu ya hoja zao.

“Tunaomba taarifa hiyo imfikie haraka Waziri Mkuu, ijadiliwe kwa haraka na kutoa majibu yatakayotupatia ufumbuzi ili nasi turudi kazini tukaokoe maisha ya Watanzania,” alisema Dk Ulimboka ambaye kwa kauli yake iliashiria kufunga mjadala.

Baada ya kauli hiyo, Waziri Ghasia alisimama na kueleza kuwa wao walifika wakiwa na ujumbe toka kwa Waziri Mkuu hivyo ni vema wangekubaliwa wauwasilishe ambapo alimtaja Waziri wa Afya Dk Mponda kuwa angeusoma.
Dk Ulimboka alijibu hoja hiyo akisema “Madaktari hatuna tatizo na ujumbe toka kwa waziri Mkuu Mizengo Pinda ila ujumbe kutolewa na Waziri wa Afya Dk Hadji Mponda hatukubali kwasababu hatuna imani naye labda kama kweli ni taarifa, ungesoma wewe,” alisema Dk Ulimboka na kukaa chini.

Waziri Ghasia alikubaliana na hoja hiyo na katika kuwasilisha taarifa hiyo, alisema alisononeshwa kusoma majibu yanayohusu madai ya madaktari hao kwa niaba ya waziri mwenye dhamana ya Wizara ya Afya wakati yeye (Dk Mponda) akiwepo.

Ghasia alisema wizara imetafakari kwa kina suala la madaktari waliokuwa kwenye mafunzo katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili na kuwarudisha kwenye kituo hicho cha kazi huku ikiahadi kuwalipa stahili zao.
“Wazira imetafakari kwa kina na imeamua kuwarejesha madaktari wote waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili na wanatakiwa kuripoti katika vituo hivyo vya kazi kuanzia Jumatatu,” alisema Ghasia.

Kuhusu madai mengine, alisema Serikali itaendelea na majadiliano ya pamoja huku akiwaomba warejee kazini.
“Sisi tuwaombe tu kwamba madai yenu yote Serikali inayafanyia kazi. Suala la nyumba tayari tumeshapata fedha kutoka Global Fund kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za madaktari ili waweze kukaa karibu na vituo vyao vya kazi,” alisema Ghasia. Akijibu ombi la kuwataka warejee kazini, Dk Ulimboka alisema hilo litategemea majibu ya taarifa walioiwasilisha kwa Waziri Mkuu, ambapo alisisitiza kuwa wao wataendelea na mikutano katika ukumbi huo.

“Sisi tutaendelea na mikutano kujadili taarifa yenu na pia tungeshauri taarifa hii mtuletee kwa maandishi, lakini pia tunasubiri majibu ya taarifa yetu tuliyoiwasilisha kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambayo tumeitoa kwa maandishi,” alisema Dk Ulimboka. Dk Uliomboa aliwataka wawakilishi hao wa Serikali kutambua kuwa ujumbe haukuwa wa kushawishiana kurudi kazini bali ni wa kupeana taarifa.

Kauli hiyo iliashiria kwamba hoja ya ujumbe huo haina uzito wa kuwashawishi kuacha mgomo huku wakikataa hoja zao sasa kujadiliwa na wizara badala yake walisisitiza Waziri Mkuu kushughulikia suala hilo. Walimtaka Waziri Mkuu, kutoa majibu ya madai yao kwa wakati ili asiwafanye kufikia hatua ya kusitisha huduma katika vitengo vya dhararu.

“Mgomo huu unaendelea nchi nzima hadi majibu ya madai yetu tuliyowasilisha kwa Waziri Mkuu yamepatiwa majibu.
Tunashauri kazi hiyo ifanywe haraka vinginevyo tusije tukashawishika kusitisha huduma kwenye vitengo vya dharura,” alisema Ulimboka.

Tishio la mgomo zaidi
Wakati huo huo, Chama cha Wauguzi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kimesema kuwa wauguzi wataendelea kutoa huduma kwa kusuasua hadi Jumatatu na kama suala hilo litakuwa halijapatiwa ufumbuzi, watasitisha huduma na kufunga hospitali.

“Sisi tutaendelea kutoa huduma katika mazingira ya shida hivi mpaka Jumatatu tu,” alisema Mwenyekiti wa chama hicho, Paul Magesa.

Habari kutoka katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma zilieleza pia kuwa, kwa sasa hakuna wagonjwa wapya wanaopokelewa na kuwa waliopo wodini wakitoka, hospitali hiyo nayo itasitisha kutoa huduma.

Urais CCM 2015 balaa

KIGOGO AMWAGA MAMILIONI, ATUMA MAKADA MIKOANI KUMNYOSHEA NJIA
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikionya wanachama wake kuacha ndoto za urais wa mwaka 2015, kauli hiyo sasa imeonekana kupuuzwa na kugeuka kichocheo cha kuongeza kasi ya kujipanga kwa baadhi ya makada wenye nia ya kusaka nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa taifa.Hivi karibuni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye, alionya kwamba chama hicho hakiko tayari kuendelea kuwakumbatia wanachama wake wanaunda makundi ndani ya chama, kwa lengo la kusaka umaarufu wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2015.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, Nape alisisitiza kuwa endapo mwanachama yeyote atabainika kuvuruga mshikamano ndani ya chama kutokana na kigezo hicho, CCM haitasita kuchukua hatua kali dhidi yake.

Pamoja na CCM kutoa onyo hilo kali, mbio za urais wa mwaka 2015 ndani ya chama hicho, zimeelezwa kuingia katika sura mpya baada ya mmoja wa makada anayetajwa kuwania nafasi hiyo, kufanya kikao kizito jijini Arusha, kwa lengo la kuweka mikakati ya kujipanga na kuimarisha kambi yake.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na baadhi ya wana CCM mjini Arusha, zinaeleza kuwa, kigogo huyo alifanya kikao chake wiki chache zilizopita katika moja ya majengo ya mfanyabiashara mmoja kutoka Kanda ya Ziwa, yaliyopo nje kidogo ya jiji.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na baadhi ya viongozi wa CCM kutoka mikoa mbalimbali nchini, wakiwamo baadhi ya wenyeviti wa mikoa wa chama hicho na baadhi ya viongozi wa Serikali, pamoja na mambo mengine, kilifanya tathmini ya kina kujua maeneo ambayo mgombea huyo hakubaliki.

Chanzo chetu kilidokeza kwamba tathmini hiyo ilionyesha kuwa kada huyo hakubaliki sana katika mikoa ya Lindi , Mtwara pamoja na maeneo ya mikoa ya Kanda ya Ziwa, ukiwemo Mkoa wa Mara.

Kutokana na hali hiyo, ilikubaliwa kuwa fedha nyingi zitumike na watu mahiri wenye ushawishi, watumwe katika maeneo haya ili kuwalainisha baadhi ya viongozi wa CCM ambao wanaonekana kuwa mbali na mgombea huyo, na jambo hilo lifanyike haraka kabla ya kuanza kwa chaguzi mbalimbali ndani ya CCM mwaka huu.

Kauli ya Nape
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alipoliuzwa kuhusiana na kikao hicho, alisema hana taarifa zozote lakini alionya kuwa endapo itathibitika kuwa kuna makada wa chama hicho wanafanya ‘rafu’ hizo, watachukuliwa hatua za kisheria za chama kwani huu si muda wa kufanya kampeni za urais.

Aliwataka wanachama wa CCM kuipa nafasi Serikali yao kutekeleza majukumu yake na ilani kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.Awali, pia Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi, aliwahi kukaririwa akisema kuwa wanaotarajia kutumia fedha kupata urais kupitia chama hicho wanajidaganya, ni bora watafute kazi nyingine za kufanya.


Kikao cha mkakati
Habari zaidi kutoka ndani ya kikao hicho, zililidokeza Mwananchi Jumapili kuwa makada watakaotumwa kuzunguka mikoani, baada kukamilisha kazi yao, watatakiwa kurejesha ripoti itakayofanyiwa kazi, ili kundi hilo liweke mikakati zaidi ya kufanikisha lengo lake.

Inaelezwa kuwa hofu kuu ya kundi hilo, ni kutoka kwa baadhi ya makada wengine wa CCM, wanaotajwa kuonyesha nia ya kuwania nafasi ya urais, kukubalika zaidi ndani ya chama katika mikoa hiyo, ambapo baadhi yao wanatoka huko.
Chanzo chetu kilidokeza pia kuwa mbali ya kuweka mikakati hiyo kabambe ya kuwania urais, pia wajumbe wa kikao hicho ‘kizito’, walifanyiwa sherehe kubwa ambapo nyama na vinywaji mbalimbali vilimwagwa kwa wingi, ndani ya majengo ya mfanyabiashara huyo, ambayo yamezungushiwa ukuta mrefu.

“Aisee! kikao kilikuwa kizito mno mikakati mizito imewekwa , jamaa yuko serious (makini) kuutaka urais, “alidokeza kada mmoja aliyekuwa ndani ya kikao hicho kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.
Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa tayari, makada waliotumwa kwenda mikoani ‘kumnyoshea njia’ mgombea huyo wa urais, hivi sasa wanavinjari kwenye maeneo hayo, wakiwa na fedha za kutosha na vitendea kazi vingine, yakiwemo magari ya uhakika.

Waliotumwa kufanya kazi hiyo, ni wenyeviti wa baadhi ya mikoa ambao imeelezwa kuwa watatumia nafasi zao kufanya ushawishi huo kwa urahisi.

Ingawa hadi sasa hakuna kada ndani ya CCM ambaye ametangaza hadharani kutaka kuwania urais, inadaiwa kwamba kuna kundi kubwa la watu ambao tayari wanapigana vikumbo chini chini kutaka nafasi hiyo, kutokana na Rais wa sasa Jakaya Kikwete, kufikia ukomo wake kikatiba mwaka 2015.

Hatua hiyo imedaiwa kuibua makundi yanayosabisha nyufa zinazoweza kuleta mgawanyiko mkubwa ndani ya chama hicho.
Tayari CCM kimekiri kupitia Katibu Mkuu wake, Wilson Mukama kuwa harakati za kuwania urais ndani ya chama hicho, zinakivuruga.

Taarifa ya Kamati Kuu ya CCM iliyosomwa ndani ya Kikao cha Halmashuari Kuu (NEC) ya CCM mjini Dodoma Novemba mwaka jana ,pamoja na mambo mengine, ilikiri kuwa mbio za kuwania urais mwaka 2015 ndani ya chama hicho, ndicho kiini kikuu cha mgawanyiko.

Kamati Kuu ilionya kuwa wanaotaka kuwania nafasi ya urais kupitia chama hicho, wanapaswa kudhibitiwa na kwamba matumizi ya fedha katika kampeni hayatakubalika.

Ushauri wa Kinana
Alhamisi wiki hii, Mjumbe wa Kamati Kuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alikaririwa na gazeti la Mwananchi akieleza kuwa vigogo wa chama hicho walioanza kampeni za urais, sasa wanavuruga utendaji wa Serikali ya Rais Kikwete.
Akiwa kwenye ziara ya kutembelea matawi ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kinana alisema vigogo hao ni wabinafsi, wanaivuruga nchi na hawana lolote wanalolifanya kwa maslahi ya chama hicho tawala.

Kinana ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Kampeni za Rais Jakaya Kikwete wakati akigombea urais kwa CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, alionesha kukerwa na watu hao na kueleza kuwa si sahihi kuanza kuzungumza masuala ya urais sasa wakati Rais Kikwete bado ana miaka minne ya kutekeleza Ilani ya chama hicho.

“Sasa hivi Rais Kikwete ana miaka mingine minne mbele kabla ya kumaliza uongozi wake na CCM ina kero nyingi za kushughulikia ili kutekeleza ilani yake, halafu wengine wanazungumzia urais sasa,” alikaririwa akisema Kinana.
Alisema anasikitishwa na hali hiyo hasa ikizingatiwa kuwa wanaoanza kupiga kampeni za urais ni watu wazito ndani ya nchi na ni wajumbe wa vikao vikuu ndani ya CCM.

Tishio lingine
Mbali ya chama hicho kukabiliwa na tishio la mgawanyiko kutokana na urais wa 2015, pia kinakabiliwa na kazi ngumu ya utekelezaji wa mkakati wake, kuwavua gamba baadhi ya makada wake wanaohusishwa na kashfa za ufisadi.

Kikao kilichopita cha NEC ambacho kilitarajiwa kuchukua maamuzi magumu ya kuwavua gamba wanachama hao, kilishindwa kufanya hivyo, badala yake kikatoa muda kwa wanachama hao kujitathmini wenyewe na kuchukua uamuzi kabla ya CCM kuwachukulia hatua.

Monday, January 16

Kikwete, Pinda waongoza waombolezaji kwa Mtema


RAIS Jakaya Kikwete jana alikuwa miongoni mwa mamia ya watu wa kada mbalimbali waliokwenda Tabata, Chang’ombe, Dar es Salaam kuifariji familia ya marehemu Regia Mtema aliyefariki juzi katika ajali ya gari eneo la Ruvu, Pwani. Mbali na Rais Kikwete, wengine waliofika msibani hapo kutoa pole ni Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na mkewe Tunu na Mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.

Marehemu Mtema ambaye alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), alifariki juzi wakati akitokea Dar es Salaam kuelekea mkoani Morogoro. Jana katika msiba huo, msemaji wa familia, Canutte Mtema alisema ibada ya kuuaga mwili wa marehemu itafanyika leo katika Kanisa Katoliki Parokia ya Segerea kuanzia saa 9:00 alasiri.

Alisema kesho, mwili wa marehemu Mtema utaagwa katika Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kisha kusafirishwa kuelekea Ifakara, ambako atazikwa Jumatano. Mbali ya viongozi, viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa wakiwemo wabunge walifika msibani hapo kuwapa mkono wa pole kwa wafiwa wakiwemo Baba wa marehemu, Estelatus Mtema na mama yake, Catherine Kilaule.

Rais Kikwete atoa neno Akitoa pole kwa wafiwa, Rais Kikwete alisema Marehemu Mtema amefariki akiwa bado kijana mdogo na aliitaka familia kuwa na uvumilivu kwani kila mtu ana siku na mkataba wake na Mungu. Marehemu Mtema amefariki akiwa na umri wa miaka 32. “Poleni sana, tupo pamoja katika msiba. Nasi tutaangalia eneo gani tutaweza kuwa pamoja,” alisema Rais Kikwete.

Spika na wabunge Kwa upande wake, Spika Makinda alisema Bunge limepoteza mbunge kijana ambaye alikuwa na hulka kipekee. Alisema marehemu alikuwa na uwezo mkubwa wa kujenga hoja licha ya ugeni wa kazi bungeni. Kutokana na msiba huo, Spika Makinda alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge itakaa na kupanga taratibu za jinsi ya kushiriki msiba huo ikiwa ni pamoja na kuchagua wawakilishi wa Bunge watakaokwenda katika mazishi.

“Tunasikitika kuondokewa na mbunge kijana Regia, alikuwa mchapakazi hodari na alikuwa na marafiki wengi bila kujali itikadi za vyama na kikubwa zaidi, alikuwa anakubali kukosolewa,” alisema Spika.

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema chama na Bunge kwa ujumla vimepata pigo kubwa kwa kuondokewa na marehemu Mtema. Alisema kutokana na uzito wa msiba huo, wabunge wote wa Chadema watashiriki mazishi yake huko Ifakara. Mnyika alisema wabunge wa chama hicho wameshaanza kuwasili kwa ajili ya msiba huo.

Aliyejeruhiwa asimulia
Mmoja wa majeruhi saba, Rogers Abdallah alisema ingawa ameruhusiwa, bado ana maumivu makali kifuani na kitu kibaya zaidi hakupata kipimo cha X-Ray... “Nimeruhusiwa lakini sikufanyiwa X-Ray, nina maumivu kifuani na ninashukuru nimetoka mzima nafikiri mkanda niliokuwa nimefunga umenisaidia,” alisema. Kati ya majeruhi hao, sita wameruhusiwa kutoka hospitalini isipokuwa mama mdogo wa marehemu, Bernadeta Mtema ambaye bado yupo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Kilombero kwazizima
Wakazi wa Wilaya ya Kilombero humo wamezipokea kwa masikitiko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha mbunge huyo. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Francis Miti, Mbunge wa Jimbo la Kilombero Abdu Mteketa, Mwenyekiti wa Halmashauri Ramadhani Kiombile, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilombero, Abdallah Kambangwa na viongozi mbalimbali walifika nyumbani kwa marehemu kwa maandalizi ya mazishi.

Wakati hali ikiwa hivyo nyumbani kwake, ofisini kwa mbunge huyo nako kulikuwa na shughuli mbalimbali za maandalizi ya mazishi na viongozi wa Chadema na wanachama wa chama hicho, walikusanyika ili kuunda kamati maalumu itakayoshughulikia mazishi hayo.

Akizungumzia msiba huo, Dk Mponda alisema: “Namfahamu vizuri marehemu ukizingatia sisi wabunge wa wilaya hizi mbili za Kilombero na Ulanga tupo karibu sana katika ushirikiano bila kujali itikadi zetu na marehemu alikuwa makini katika kutetea wananchi punde anaposikia matatizo,” alisema Dk Mponda.

Kwa upande wake, Mteketa alisema: “Unajua nilikuwa nashirikiana naye vizuri sana tofauti na baadhi ya wananchi walivyokuwa wanadhani kutokana na sisi kuwa vyama viwili tofauti na ndiye aliyekuwa akinipa changamoto zaidi ili niweze kutekeleza ahadi zangu kwa wakati kwa wananchi walionichagua.”

Naye Kiombile alisema msiba wa Regia ni pengo kubwa ndani ya wilaya ya Kilombero hasa ikizingatiwa kwamba alikuwa mbunge kijana kama alivyo yeye na mara kwa mara alikuwa akimpigia simu ili kumpa ushauri naye kupokea ushauri kutoka kwake. Kambangwa alisema mbunge huyo alikuwa mwanasiasa kijana aliyekuwa akijali zaidi maslahi ya wananchi aliokuwa akiwaongoza na hakufuata itikadi za chama chake pekee.

Rafiki wa karibu wa marehemu Regia, Amina Simbamkuti alisema amempoteza mtu wa karibu aliyeshirikiana naye katika kutatua kero mbalimbali za wananchi. Mbunge huyo alifariki dunia baada ya gari alilokuwa akiendesha kupinduka saa 5:30 asubuhi karibu na Shule ya Sekondari Ruvu.

Habari hii imeandikwa na Joseph Zablon na Shakila Nyerere Dar na Venance George, Morogo

Ahadi ya Rais Kikwete kuhusu umeme utata mtupu


AHADI iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete ya kupatikana kwa megawati 3,000 za umeme huenda isitekelezwe katika muda uliopangwa kutokana na kutofanyika kwa maandalizi ya kutosha.Akilihutubia Taifa kuukaribisha mwaka 2012, Rais Kikwete alisema tatizo la umeme nchini litakuwa historia katika muda wa miezi 18 ijayo kutokana na mpango wa Serikali wa kusafirisha gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.

“Maombi yetu kwa Serikali ya China ya kupata mkopo wa kujenga bomba la kusafirisha gesi kutoka Mtwara na mtambo wa kuchakata gesi inayotoka Songosongo yamekubaliwa,” alisema Kikwete katika hotuba yake ya Desemba 31, mwaka jana na kuongeza:“Utekelezaji wake unatarajiwa kuchukua miezi 18 na gesi itakayoletwa inaweza kuzalisha mpaka Megawati 3,000 za umeme. Baada ya hapo kasi ya kuongeza umeme itakuwa kubwa zaidi na tatizo la upungufu wa umeme linaweza kuwa historia.

”Hata hivyo, imebainika kuwa hadi sasa Serikali ya Tanzania na China hazijasaini mkataba wa kifedha ili kupata mkopo wa Dola bilioni moja za Marekani (karibu Sh1.6 trilioni) ambazo zitatumika kugharamia ujenzi wa bomba hilo, hivyo kuzua wasiwasi iwapo ujenzi wa bomba hilo utakamilika katika muda uliopangwa.Makubaliano ya awali ya ujenzi wa bomba hilo yalisainiwa China Septemba 26, 2011 na Tanzania ikiwakilishwa na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.

Baadaye ilisainiwa mikataba mingine midogomidogo lakini, kikwazo hadi sasa ni mkataba wa fedha.Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alisema hadi mwishoni mwa wiki jana, mkataba wa kifedha ulikuwa bado haujasainiwa lakini akasema taarifa alizonazo ni kwamba utasainiwa hivi karibuni.“Kweli bado hatujasaini mkataba huo ila niko informed (nina taarifa) kwamba majadiliano yako kwenye hatua nzuri na yakikamilika tutasaini,” alisema Mkulo.

Mkulo alisema majadiliano yanayoendelea yanawahusisha Makatibu Wakuu wa Wizara za Fedha na Uchumi, Nishati na Madini, maofisa wa Serikali ya China na wakala wa utekelezaji wa mradi huo kutoka nchi hizo mbili.“Ninachoweza kusema ni kwamba bado tuko kwenye ratiba, tunafahamu umuhimu wa kukamilika kwa hatua hii, lakini lazima tujiridhishe.”Mapema wiki iliyopita, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile alisema bado kuna maeneo machache ya majadiliano baina ya wataalamu wa Tanzania na China na kwamba yakikamilika mkataba huo wa kifedha utasainiwa.

“Ahadi ya Rais itatekelezwa kama alivyosema, kuna sehemu chache tu bado wataalamu wetu wanajadiliana na wenzetu wa China, wakikamilisha basi nadhani tutaweza kusaini ili kuwezesha mradi huo kuanza,” alisema Dk Likwelile.Kwa upande wake, Ngeleja alisema wizara yake imejipanga kusimamia kikamilifu ujenzi wa bomba hilo, baada ya mkataba wa fedha kusainiwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba katika maoni yake alisema kuchelewa kusainiwa kwa mkataba wa kifedha kunaweza kuathiri kasi ya utekelezaji wa mradi wa bomba la gesi kutoka Mtwara.“Ni vigumu sana kuwa na uhakika wa kutekelezwa kwa mradi kabla ya kuwa na uhakika wa fedha, sina uhakika kama hilo limefanyika lakini kwa kuwa tunaanza vikao vya kazi zetu karibuni, nadhani tutapata taarifa,” alisema January.Vikwazo vingineWakati Serikali ikihaha kukamilisha mchakato wa kusainiwa kwa mkataba wa fedha, habari kutoka ndani ya Serikali na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) zinasema kinahitajika kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kujenga vituo vya kusambaza umeme na njia mpya za kusambaza umeme huyo.

Mmoja wa wahandisi ndani ya Tanesco ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema ikiwa kiasi hicho cha megawati 3,000 za umeme kitafikishwa Dar es Salaam basi vinahitajika vituo 30 kwa ajili ya kusambaza umeme.“Ujenzi wa kituo kimoja (sub-station) gharama zake si chini ya Dola za Marekani milioni 15 (zaidi ya Sh23 bilioni) kwa hiyo piga hesabu kama tunahitaji vituo 30 basi zidisha utapata majibu ni kiasi gani cha fedha kinachohitajika,” alisema mhandisi huyo wa umeme.

Kwa kuzingatia hesabu hizo, Serikali inalazimika kutafuta zaidi ya Sh700 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vituo hivyo ambavyo hata hivyo, hadi sasa bado mpango wake haujawekwa wazi. Pia italazimika kutafuta kiasi kama hicho kwa ajili ya ujenzi wa njia mpya ya kusafirishia umeme huo.

Habari zaidi zilisema ili kupatikana kwa megawati 3,000 za umeme, kunahitaji pia njia mpya za kusafirishia nishati hiyo ya msongo wa kilovolt 400, tofauti na njia za sasa ambazo uwezo wake ni msongo wa kilovolt 220.“Kama tunataka kuongeza kiasi cha umeme katika njia zetu za sasa, lazima tuongeze uwezo maana njia zetu zinazidiwa ndiyo maana wakati mwingine umeme unakatika ovyo,” alisema mhandisi huyo.Hivi sasa Serikali inajenga njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovolt 400 kutoka Iringa kupitia Dodoma, Singida hadi Shinyanga, ujenzi ambao utaigharimu kiasi cha Dola za Marekani milioni 500 (karibu Sh800 bilioni) hadi utakapokamilika.

Hata hivyo, njia hiyo ni maandalizi ya umeme unaotarajiwa kuzalishwa kutoka miradi ya makaa ya mawe ya Ngaka mkoani Ruvuma na Mchuchuma Wilaya ya Ludewa mkoani Iringa na siyo kwa ajili ya usafirishaji wa umeme utakaozalishwa kutokana na gesi ya Mnazi Bay kutoka Mtwara.Gharama za UmemeIkiwa ahadi ya Rais Kikwete itashindwa kutekelezwa katika muda wa miezi 18 kama alivyoahidi, inaamanisha kwamba taifa litaendelea kutumia umeme wa gharama kubwa unaozalishwa kwa mafuta.

Tayari gharama hizo zimeanza kuwaelemea watumiaji baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura), kuiruhusu Tanesco kupandisha gharama za umeme kuanzia leo kwa asilimia 40.29.Upandishaji huo umezua kilio nchi nzima ambako watu wa kada tofauti wamesema utaongeza gharama za maisha na kuwaathiri wananchi wa kipato cha chini.

Kutumika kwa umeme wa mafuta kunatokana na kutokuwepo kwa maji ya kutosha katika mabwawa ya kuzalisha umeme. Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, uzalishaji ulikuwa ni asilimia 62.9 ya uwezo wa mabwawa hayo.Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud alisema hadi sasa umeme unaotokana na maji ni megawati 353 kati ya 561 zinazotakiwa na kwamba hali hiyo inatokana na uhaba wa maji.

Mwisho……

Wednesday, January 11

Fundi sudi maarufu kama Mzee Kipara amefariki

Fundi sudi maarufu kama Mzee Kipara amefariki muda si mrefu huko Kigogo kwenye nyumba ambayo alikuwa amepangishiwa na kundi la sanaa ambalo alikuwa anafanyia kazi la Kaole.

Kwa taarifa ambazo tumezipata sasa hivi kutoka kwa Swebe ambaye yupo nyumbani kwa mzee Kipara, kwa sasa wanauandaa mwili wake kwenda kuupeleka Hospitali ya mwananyamala kuuhifadhi.
Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika kesho, kwa taarifa zaidi tutawaletea hapo baadae.

Kigamboni bridge a dream which is about to happen

A Sh 214.639 billion project was signed yesterday to build a bridge across the Kigamboni Creek.
Under the deal signed by the National Social Security Fund (NSSF), the China Railways Construction Engineering Group and the China Major Bridge Engineering Company, it will take 36 months to complete the construction.

Works minister John Magufuli and his Labor and Employment counterpart Gaudencia Kabaka witnessed the signing of the contract by NSSF managing director Ramadhan Dau, China Railways Construction Engineering Group CEO Shi Yuan and Major Bridge Engineering representative Zhou Yiqiao.

NSSF will bear 60 per cent of the construction cost while the rest will come from the government.Before signing the pact, Dr Dau said the idea of constructing the bridge was mooted in 1977.
According to him, the project involves the construction of a one-kilometre tarred road of six lanes from Kurasini, a 680-metre cable stayed bridge and another 1.5km tarmac road that will also have six lanes. 

The construction will start immediately after a site for placement of equipment is found. Dr Magufuli challenged the two companies to finish the work at an agreed time to win the hearts and minds of the public.
“I visited China recently and I found a 27km super bridge that was constructed in 18 months…I wonder why it should take 36 months to construct a bridge of less than 2km in Dar es Salaam,” he said. “Do whatever you can to complete the bridge before President Kikwete’s term ends. Kikwete is the one who is supposed to inaugurate it.”

Tanzania National Roads Agency chief executive Patrick Mfugale said the bridge would have an international standard.Arab Consulting Engineers from Egypt would supervise its construction.


Lowassa aponda nguvu ya umma

Anthony Kayanda, Kigoma
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, ameibuka na kukemea matumizi ya nguvu ya umma, yanayoendeshwa na baadhi ya vyama vya siasa nchini kushinikiza mambo mbalimbali, akisema hayalifikishi taifa popote.

Akizungumza katika harambee ya kuchangia ujenzi wa Sekondari ya Kanisa la FPCT Bigabiro, mkoani Kigoma, Lowassa alisema nguvu wanazotumia wanasiasa kuhamasisha nguvu ya umma, ingefaa kutumika kushiriki kazi za maendeleo ili kuliletea taifa maendeleo endelevu.

Ingawa Lowassa hakutaja chama cha siasa kwa jina, lakini Chadema ndicho ambacho kimekuwa kikitumia kauli mbiu ya Nguvu ya Umma (Peoples Power) kushinikiza mambo mbalimbali.

"Badala ya kuonekana wakihamasika kufanya maandamano ya kupambana na Serikali, jambo ambalo halitasaidia taifa kuondokana na umasikini, nguvu hiyo ingetumika kushiriki kazi za maendeleo," alisema Lowassa.

Alisema miradi mingi ya maendeleo imekuwa ikikwama kutokana na wananchi kukataa kushiriki kujitolea nguvu zao kwa kufanya kazi, badala yake, wanataka kulipwa fedha kutekeleza miradi maeneo yao.

“Nguvu ya umma tunayoshuhudia kwenye maandamano ya baadhi ya vyama vyetu, ingekuwa inatumika kwa kiwango kilekile kufanya kazi za kujitolea kwenye miradi ya maendeleo kama ujenzi wa sekondari zetu, hakika taifa lingepiga hatua kubwa ya maendeleo, lakini linapokuja suala la kufanya kazi nguvu ya umma hutoweka,” alisisitiza Lowassa.


Harambee
Katika harambee hiyo, Lowassa na rafiki zake walichangia Sh60.5milioni taslim na kufanya michango yote kufikia Sh125 zikiwamo ahadi.

Lowassa alisema elimu ikitiliwa umuhimu ni wazi taifa litajikomboa kutoka kwenye hali duni kwa kuwa litakuwa na watu wenye uelewa wa kutosha juu ya mabadiliko na mifumo mbalimbali ya dunia, kiasi kwamba itakuwa rahisi kufundishwa na kuelekezwa mambo muhimu.

“Baada ya kubaini hakuna usawa katika taifa, tulilazimika kutembea nchi nzima kuhamasisha ujenzi wa sekondari za kata ili kila eneo watoto wasome. Watoto wa Kigoma wawe kama wenzao wa Kilimanjaro au mikoa mingine iliyopata mwanga wa elimu mapema, ndiyo maana angalau watoto wengi wanafika kidato cha nne sasa ikilinganishwa na miaka ya nyuma,” alisema Lowassa.

Ajira
Lowassa alitumia harambee hiyo kurejea kauli yake kuhusu tatizo kubwa la ukosefu wa ajira kwa vijana nchini, ambao wamehitimu masomo yao ngazi mbalimbali lakini wanaishia mitaani bila kupata kazi zinazoeleweka.

Alisema tatizo la ajira kwa vijana ni bomu linaloweza kulipuka wakati wowote na kuleta shida kwa taifa, kwa vile ndiyo nguvu kazi inayohitajika zaidi kujenga uchumi imara wa nchi, hivyo kusaidia kuondokana na umaskini, mfumko wa bei na hata kudorora kwa uchumi.

“Nimekuwa nikilisemea sana suala hili la ukosefu wa ajira kwa vijana, kiasi kwamba kuna watu walinibatiza jina la Yohana Mbatizaji, lakini bado natoa mwito kama jamii tutafakari kwa makini jambo hili,” Lowassa alirejea kauli hiyo na kuongeza:

“Kila tunapokutana kwenye semina na makongamano tulijadili kwa kina, vinginevyo tutakuja kujilaumu siku moja kwa sababu hata wanaohitimu vyuo vikuu, wanaopata ajira ni asilimia tano tu kwa mwaka.”

Alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali mstaafu Issa Machibya, kusaidiana na kanisa hilo kuwashawishi watu wanaomiliki eneo inapojengwa sekondari hiyo, wapunguze gharama za fidia ya ardhi na mazao yao ya kudumu, inayofikia Sh75milioni kwa madai kwamba ni nyingi ikilinganishwa na thamani ya mradi unaotekelezwa.

Mchungaji
Awali, katika risala yao iliyosomwa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo la FPCT Bigabiro, David Nkone, alisema wameamua kujenga sekondari ya kidato cha kwanza hadi sita kutokana na uhaba mkubwa wa sekondari za ngazi hiyo mkoani Kigoma, hususan zenye michepuo ya sayansi.

Mchungaji Nkone aisema Chuo cha Theolojia cha FPCT Bigabiro kinachotoa mafunzo ngazi ya stashahada pia kinakusudiwa kupanuliwa na kufikia kutoa Shahada, hivyo kuongeza fursa za elimu na ajira kwa baadhi ya Watanzania.

Kanisa hilo lilimteua Lowassa kuwa mlezi wa sekondari hiyo aliyowekea jiwe la msingi ambayo kwa sasa ina madarasa matatu yaliyofikia hatua ya rinta, lengo likiwa ni kujenga madarasa ya kidato cha kwanza hadi sita.

Katika hatua nyingine, mjumbe wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM Mkoa wa Kigoma, Muhsin Abdallah Sheni, aliahidi kuchangia Sh10 milioni na kompyuta mbili, huku Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba akiahidi Sh3 milioni, Mbunge wa Viti Maalumu, Josephine Ngenzabuke aliahidi kutoa Sh2 milioni na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Machibya akiahidi Sh2.5 milioni.

Tuesday, January 10

MPANGO WA SERIKALI KUPUNGUZA MATUMIZI - ZITTO KABWE MB.

Punguza Matumizi ya Posho SIYO Matumizi ya Reli, Barabara, Elimu na Afya

Mwezi Disemba mwaka 2011 Waziri wa Fedha na Uchumi alimwandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) kumwahidi mambo yepi Serikali ya Tanzania itafanya ili kurekebisha Bajeti yake. Utaratibu huu hufanyika kila mwaka kupitia mpango unaoitwa ‘Policy Support Instrument (PSI). Katika barua hiyo Waziri wa Fedha wa Tanzania ameahidi kwamba Serikali itafanya juhudi kupunguza matumizi ili kuweza kupunguza uwiano wa nakisi ya Bajeti na Pato la Taifa (fiscal deficit to GDP ratio) kutoka asilimia 7.2 mpaka asilimia 6.6 ya Pato la Taifa.

Waziri wa Fedha na Uchumi ameiambia IMF kwamba ifikapo mwisho wa Mwezi Disemba mwaka 2011 (wiki mbili zilizopita) Baraza la Mawaziri la Tanzania limefikia maamuzi ya kupunguza nakisi ya Bajeti kwa kiwango kilichotajwa. Maeneo yanayotajwa ni Pamoja na Miradi ya Maendeleo ambapo jumla ya miradi yenye thamani ya Tshs 157bn itakatwa. Waziri
wa Fedha ametaja miradi hiyo katika Ukarabati na Ujenzi wa Miundombinu.

Kambi ya Upinzani Bungeni inapinga kuondolewa kwa miradi ya maendeleo ili kupunguza matumizi ya Serikali. Kimsingi wakati kama huu ambapo hali ya uchumi ni mbaya na vijana wengi vijijini na mijini hawana ajira tunasisitiza umuhimu wa kutumia zaidi kwenye miradi ya maendeleo.

Punguza matumizi ya kawaida

Kambi ya Upinzani Bungeni inarejea wito wake kwa Serikali kupunguza matumizi ya kawaida ili kupata fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo. Haiwezekani kamwe tukawa Taifa huru iwapo miradi yetu yote ya maendeleo inafadhiliwa na wahisani. Kiwango kidogo tulichokiweka katika Bajeti ya mwaka huu ndicho hicho sasa kinakatwa na hivyo miradi yote ya maendeleo kubakia kwa wahisani ama kwa mikopo au misaada. Kiwango cha Tshs 203bn sawa na 0.5% ya Pato la Taifa ambacho Serikali imeahidi kupunguza ni kidogo mno na kinalenga kuumiza watumishi wa kada ya chini ya Serikali na sio viongozi wakubwa. Bajeti ya Mafunzo inayoenda kukatwa itaumiza Manesi na Walimu au watumishi wanaoongeza ujuzi ili kuboresha kazi zao. Serikali ikate matumizi yote yasiyo ya lazima na hasa posho (360bn), ipunguze matumizi ya magari na yale yasiyo na uhitaji yapigwe mnada na viongozi wote isipokuwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika na Jaji Mkuu washushwe madaraja ya kusafiria kwenye ndege. Safari zote ambazo hazina mahusiano na miradi ya maendeleo zipigwe marufuku kwa muda wote wa miezi sita ya Bajeti iliyobakia.

Serikali ihakikishe matumizi katika Sekta ya Elimu na Afya hayakatwi kabisa ili kuhakikisha tunalinda mafanikio kiduchu ya upanuzi wa sekta hizi na kuongeza uwezo wa Serikali kutoa huduma bora kwa wananchi hasa wa vijijini.

Matumizi ya Maendeleo yasiguswe, yaongezwe

Tayari imeonekana kwamba katika kipindi chote cha nusu ya Bajeti Halmashauri za Wilaya hazijapata fedha za maendeleo. Mfano Halmashauri ya Wilaya Kigoma imepata asilimia 0.3 tu ya Bajeti ya Maendeleo ilhali Halmashauri ya Mji wa Mpanda imepata asilimia 4 tu. Ni dhahiri miradi ya maendeleo kwa maeneo mengi ya vijijini itakwama kwani ni wazi kabisa kwamba Halmashauri hazipati fedha zote za Bajeti ya Maendeleo. Serikali itambue kwamba miradi ya maendeleo sio anasa bali ndio vyanzo vya baadaye vya mapato ya serikali. Miradi ya maendeleo hutoa ajira kwa wananchi na hivyo kuwapunguzia umasikini wa kipato. Jumla ya Tshs 157bn zinazotakiwa kukatwa zisikatwe bali ziongezwe ili kupata fedha za kurekebisha miundombinu kama Reli ya Kati.Kwa mfano Reli ya Kati inahitaji Tshs 200bn katika kipindi cha miaka 3 ili iweze kusafirisha mizigo tani 1.5m kwa mwaka kila siku na kuzalisha faida.

Ongeza Mapato ya Ndani

Inashangaza kwamba katika mpango wa Serikali kupunguza nakisi ya Bajeti mkazo umewekwa kwenye kuondoa miradi ya maendeleo badala ya kuongeza mapato. Nakisi hupunguzwa ama kwa kupunguza matumizi au kwa kuongeza Mapato. Serikali katika Taarifa yake kwa IMF imeibua njia moja tu ya kuongeza mapato, kodi ya mapato kutoka Kampuni ya Geita Goldmine. Huu ni uvivu wa kufikiri.

Serikali imeambiwa mara kadhaa suala la kuanza kutumika kwa sheria mpya ya madini kwa Kampuni za Madini zilizokuwapo. Makusanyo ya Mrahaba peke yake kwa sheria mpya, kiwango kipya na kanuni mpya ya kukokotoa ingeongeza mrahaba mpaka Tshs 203bn kutoka Tshs 99bn za sasa. Kwanini Serikali ianvuta miguu katika kutekeleza hili? Waziri wa Nishati na Madini aliahidi Bungeni kwamba mazungumzo na Kampuni za Madini yanaisha Mwezi Septemba. Mbona Serikali imekuwa BUBU katika hili?

Serikali iliahidi kuangalia suala la mauzo ya mali za makampuni zilizoko Tanzania na kodi ambayo tunapaswa kukusanya, Serikali imekuwa kimya kabisa katika suala hili. Marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kuondoa msamaha kwenye ‘deemed capital goods yangeongeza mapato ya Serikali kwa kiwango kikubwa na kupunguza mzigo wa
misamaha ya Kodi.

Uwajibikaji kwa Bunge

Inashangaza zaidi kwamba sasa imekuwa ni mtindo kwa Serikali kutoa ‘commitments’ muhimu za kibajeti kwa Shirika la IMF badala ya wananchi kupitia Bunge. Bunge limepitisha Bajeti, mapitio yeyote ya Bajeti yanapaswa kuidhinishwa na Bunge. Bila kufanya hivyo maana ya Bunge kupitisha Bajeti inakuwa haina mantiki na uhuru wa Taifa letu unakuwa haupo kwetu.

Umuhimu wa Bunge kutunga haraka Sheria ya Ofisi ya Bajeti ya Bunge (Parliamentary Budget Act) sasa unaonekana waziwazi. Muswada umewasilishwa Bungeni na Wabunge binafsi kutaka kuundwa kwa mfumo wa kuisimamia Serikali katika Bajeti. Ofisi ya Spika wa Bunge ihakikishe muswada huu unachapishwa katika Gazeti la Serikali mara moja ili usomwe kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Sita wa Bunge na kutungwa kuwa sheria katika mkutano wa Saba.

Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ilete mpango wa kupunguza matumizi Bungeni ili ujadiliwe na kuidhinishwa na Bunge kabla ya kuanza kutumika. Vinginevyo Mpango wa Serikali kwa IMF utakuwa ni kudharau wananchi na kuuza uhuru wetu kwa Shirika la Fedha la Kimataifa. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema mwishoni mwa miaka ya Sabini ‘toka lini Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limekuwa Wizara ya Fedha ya Kimataifa (International Ministry of Finance)?’

Kabwe Zuberi Zitto, Mb

Waziri Kivuli Fedha na Uchumi

Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni (NKUB)

Dar es Salaam, 10 Januari 2012.

Monday, January 9

Muziki wa Bongo 2011

HIVI wasanii wa kike walikuwa wapi 2011? Ndiyo swali ambalo mashabiki wengi wa muziki nchini wanajiuliza wanapofanya majumuisho ya mwaka 2011 katika siku ya leo Jumamosi tunapoufunga mwaka.
Ukiachilia wachache ambao waliibuka na kupotea, vidole wananyooshewa zaidi wakubwa wawili ambao ni Ray C na Lady Jaydee. Walikuwa kimya muda mrefu na walikuwa wakifanya mambo kimahesabu zaidi.
Ray C aliamua kujichimbia Nairobi, Kenya na kupiga dili zake huko kimya kimya na kudondosha Dar es Salaam baadhi ya singo zake ambazo hazikutamba kama enzi hizo.

Jaydee akakomaa na bendi yake ya Machozi ambayo ilipata shoo nyingi ndani na nje, lakini hakuwa mwepesi kuachia singo kwa fujo kama siku za nyuma, waliokuwa wakienda kwenye kumbi za starehe Bongo ndiyo walimfaidi, lakini upande wa pili alikuwa kibiashara zaidi alizindua miradi yake mingi na kila mara alikuwa bize kuiendesha.

Lakini kuna vichwa ambavyo viliburuza sana kwenye Bongofleva japokuwa wengi wao walikuwa wana nyimbo za kufurahisha na kujirusha zaidi, ambazo zilikuwa hazina ujumbe wowote.

Inawezekana wakati mwingine labda ulizisikia ukaamua kusogeza mbele DVD yako ili zisikuchefue. Lakini huko mitaani wenzio walizipenda na jamaa wakapata mwanya wa kutengeneza fedha ndani na nje ya nchi.

BONGOFLEVA
Wasanii wengine walikuwa wakiibuka na wimbo mmoja na kupotea baada ya wiki chache, wala shoo hawakuambulia. Ingawa baadhi walijitahidi kujitengenezea kashfa na kucheza dili na magazeti ya udaku kupandisha majina yao, lakini bado wakashindwa kuhimili vishindo kutokana na kutokuwa na kazi za maana.

Wasanii wafuatao angalao walijitahidi kuwa bize mwaka mzima wa 2011 na walitengeneza kiasi cha fedha kutokana shoo nyingi za ndani na nje ya nchi, hawakutoka masikioni mwa mashabiki.

20 Percent:
Hakuhitaji kubebwa na prodyuza, redio wala kujitengenezea kashfa ili aibuke. Muziki wake ulimbeba na kumpa tuzo tano kwa wakati mmoja, kitu ambacho hakuna msanii aliyempiku.
Alizurura sana mikoani kufanya shoo pengine kuliko msanii mwingine yeyote na nyimbo zake zilizotamba ni zile zile kama �Tamaa Mbaya�, �Ya Nini Malumbano� mpaka mwisho wa mwaka alipoachia �Pasu Kwa Pasu� ambayo ni jibu baada ya kuacha na prodyuza wake wa siku nyingi Man Walter kwa ugomvi.

Ally Kiba:
Huyu jamaa ameshanasa kwenye masikio ya mashabiki na aliishi kiujanjaujanja kwa kujitangaza zaidi nje ya nchi ambako alipiga shoo nyingi sana.
Alipiga shoo Afrika Mashariki na Ulaya na wimbo wa �Dushedede� ambao uko kwenye staili ya Bolingo ulimbeba kwa kiasi fulani kwa vile ulipendwa na wote.

AY:
Huyu jamaa ni mjanja sana, kama alivyofanya mwaka jana na mwaka huu alifanya hivyo hivyo tena alipiga hatua zaidi na kuwa msanii wa Bongo aliyefanya shoo na wasanii wengi zaidi wa nje achilia mbali Afrika Mashariki hakuna aliyeamini kama angeweza kuwanasa Lamya na Romeo wa Marekani.
Amejiimarisha pia Bongo kwa kufungua maduka mengi ya biashara za nguo na saluni na hata maisha anayoishi ni bora.

DULLY Sykes:
Alifuata nyayo za mastaa wa Uganda na Kenya kibiashara. Ndiye msanii wa Bongofleva aliyekuwa na dili ya kueleweka ya matangazo mengi ya kampuni ya simu za mikononi ya Tigo.
Kama kawaida yake hakuna na nyimbo za kuumiza kichwa, ujumbe wake ulikuwa ni mwepesi sana uliojaa masihara, lakini vijana walimpenda sana na kumsapoti kwa kucheza nyimbo zake na kuibuika kwenye shoo.

BANANA
Kwenye redio hakusikika sana lakini akiwa na B-Band yake alikuwa bize sana kwenye kumbi za Dar es Salaam karibu wiki nzima alikuwa bize kuliko msanii yoyote yule wa muziki wa kizazi kipya. Kilichombeba ni ubunifu wake na bendi yake ambayo imekuwa na vijana wanaovutia wengi.

LINAH na BARNABA
Ukiachilia mbali nyimbo walizofanya kwa kushirikiana hata kila mmoja kivyake walibamba sana mashabiki ndani na nje ya Bongo, ni kizazi kipya kilicholeta mageuzi masikio mwa wengi na hawakutaka makuu.

Shoo za Ulaya wamepiga sana, Linah aliosha jina zaidi baada ya kunasa tuzo mbili za Muziki za Kili, ile ya Mwimbaji Bora wa Kike na Msanii Bora anayeibukia. Usisahau 2011 ndiyo mwaka ambao Linah alinunua gari aina ya Vitz.

DIAMOND
Awali wapinzani wake walidai kwamba alikuwa akichonga dili na magazeti ya udaku ili kujipandisha chati pamoja na kupanua njia yake kibiashara, ingawa hakuna aliyeweza kuthibitisha hilo.

Msanii huyo kama alivyo Ally Kiba walitunisha sana akaunti zao 2011 na walicheza karata zao vizuri na kufunika hata wakongwe.

Skendo zake na wasanii mbalimbali wa kike zimechangia kumweka bize machoni na masikioni mwa mashabiki, lakini hata kazi alifanya nzuri na yenye ubunifu.

BOB JUNIOR
Aliibuka kama masihara, lakini mwisho wa siku akaingia kwenye chati ya wasanii wanaovuma Bongo, singo zake kama Oyoyo zimembeba na kumpa shoo nyingi ingawa zote ni ndani ya mipaka ya Tanzania ya Rais anayependa michezo na Burudani, Jakaya Mrisho Kikwette.

PROF JAY
Kama ipo ndiyo wimbo wake uliotamba miezi ya hivi karibuni, lakini huwezi kuamini ndiyo msanii wa Bongo aliyefanya shoo nyingi zaidi Afrika Mashariki na Ulaya.
Heshima yake kimuziki imeendelea kuwa palepale licha ya kwamba ni mwajiriwa kwenye kampuni moja kubwa ya jijini Dar es Salaam.

Ni msanii msomi na anayefanya kazi kwa hesabu sana na anayefaa kuigwa na chipukizi ambao wamekuwa wakikimbia shule na kung�ang�ania muziki.
Alipokanyaga Uganda, Kenya, Rwanda au Burundi mashabiki walichanganyikiwa.

ROMA MKATOLIKI
Aliibuka kimasihara, lakini amefanya shoo nyingi pengine kuliko alivyotarajia, katika kila shoo kubwa 2011 lazima ungemkuta. Pengine hata yeye hakutarajia kama mashabiki wangeikubali staili yake kiasi hicho.

MWANA FA
Ni Msanii msomi ambaye ukikutana naye ana kwa ana mtaani ukilinganisha na makali yake kwenye kipaza sauti ni vitu tofauti kabisa.
Yuko simpo sana. Alikanyaga Afrika Kusini mara kadhaa na humu ndani ya Bongo aliendelea kujitunzia heshima yake hususani kwa vijana.

BELLE 9
Singo yake ya Sumu ya Penzi imembeba sana na ni mbishi kwelikweli kwenye fani, hachuji. Ameshirikishwa kwenye singo za mastaa kadhaa Bongo na wimbo wake wa Nilipe Nisepe hauna maneno halisi ya kuelezea kwa jinsi ulivyopokelewa mitaani.

JOH MAKINI
Kwa wanaoijua Hip Hop ya Tanzania, wanamjua na hata ambao hawafuatilii aina hiyo ya muziki wanamkubali. Ameonyesha ukomavu sana bila kutetereka au kupotea kama walivyofanya wasanii wengine wa aina hiyo ya muziki.

Wapinzani wake kama Chid Benz, Fid Q, Afande Sele walikuwa wakiibuka na kupotea kipindi kirefu zaidi na walionekana kujishughulisha na dili zingine binafsi zaidi.

DOGO JANJA
Ni msanii mdogo aliyetamba sana mwaka huu wa 2011 ingawa hakua na muda mwingi wa kufanya shoo kutokana na kubanwa na shule, lakini ameonyesha kwamba Bongofleva si jina bali kipaji na ubunifu binafsi.

CPWAA
Yupo kama hayupo, lakini ametengeneza sana na kwenye orodha ya wasanii wa Tanzania waliopiga hela kwa shoo za ndani na nje yumo, hakuna shoo ya maana itapigwa sehemu umkose. Wimbo wake wa Action umembeba.

CHEGE NA TEMBA
Hawa jamaa nuksi na pengine bila wao sasa TMK Wanaume Family itapotea kwenye ramani ya muziki, wao wako juu kuliko kundi na hakuna anayezungumzia tena kundi.

Ukiacha wimbo wao wa Mikono Juu, wametoa nyimbo ambazo zimekubalika ndani na nje na wameshirikishwa na wasanii tofauti na hata ndege wamekwea sana kwenda kufanya shoo zisizo na idadi Ulaya. Je nini hatma ya wengine waliobaki kundini?

TIPTOP CONNECTIONS
Madee na Tundaman waliwaongoza wenzao wa Tip Top kufanya shoo nyingi za ndani tofauti na makundi mengine ambayo ambayo yalionekana kupooza na hayakuwa na jipya 2011 labda tusubirie 2012.


BENDI ZA DANSI
Upepo wa bendi za dansi bado ulibaki kwa Twanga Pepeta, FM Academia, Akudo Impact na Extra Bongo ambazo zilikuwa zikipokonyana mashabiki na kuacha bendi nyingine zikitumbuiza viti katika shoo zao nyingi za Dar es Salaam.


Lakini 2012 huenda ukawa mwaka wa Twanga na Extra endapo FM na Akudo wasipojipanga kwani katika siku za hivi karibuni wameonekana kuyumba na kutokuwa na jipya jukwaani.

MUZIKI WA TAARAB
Taarab ilizoa mashabiki kadhaa wa dansi mwaka 2011, jambo ambalo liliwalazimu watu wa bendi kuwa wanafanya shoo za pamoja na bendi za Taarab ili kujaza mashabiki.

Bendi za Taarab zilizotamba sana ni Jahazi, Five Stars na Mashauzi Classic.

Filamu Bongo 2011

WASANII wa filamu Bongo mwaka 2011 walifanya mambo makubwa na kupiga hatua katika tasnia ya filamu, huku wasanii wengine wakiibuka na kuwa gumzo.

RAY
Ray yeye kama ilivyo kawaida ndiye kioo cha tasnia ya filamu kwa mwaka huo. Aliweza kufanya mambo makubwa ikiwa ni pamoja na kusafiri kwenda kununua vifaa vyake vya kazi Ulaya.
Pia kwa kutumia kampuni yake aliibua wasanii wapya kama Otilia Joseph.

MONALISA
Yvonne Cherryl �Monalisa� alishiriki tuzo za Pan African zilizofanyika nchini Marekani kupitia filamu yake ya Binti Nusa iliyotengenezwa na kampuni yake.

Mwaka jana pia alipata nafasi ya kwenda kushiriki filamu nchini Ghana ikiwa ni sehemu mojawapo ya kutafuta soko la kimataifa. Jambo jingine kubwa kwa mwanadada huyo ni kuwa alisambaza filamu ya Binti Nusa yeye mwenyewe.

KANUMBA
Kanumba naye hakuwa nyuma kwani alitoa filamu nyingi zilizofanya vizuri, si hayo tu bali pia alitumia uwezo wake katika kumleta msanii nyota wa kimataifa kutoka nchini Nigeria, Ramsey Nouah, kushiriki katika filamu yake ya Devil Kingdom.

Filamu ilitikisa katika tasnia ya filamu Bongo. Pia ndiye msanii ambaye amekuwa balozi wa makampuni mbalimbali kwa mwaka jana. Alisafiri kwenda nchini Marekani katika shughuli za sanaa, pia alikwenda Ghana kwa ajili ya kurekodi filamu akishirikiana na nyota wa filamu Afrika kutoka nchi kama Nigeria, Ghana na Afrika Kusini.

WOLPER
Jacqueline Wolper ni moja kati ya wasanii ambao kwa mwaka uliopita alifanya vizuri katika mauzo hata kuweza kuwafunika baadhi ya wasanii wa kike katika tasnia ya filamu.
Wolper pia alitengeneza filamu zake akiwa kama mtayarishaji, amefanya vema katika tasnia hii ya filamu Bongo anastahili Pongezi.

JB
Jacob Stephen �JB� ndiye msanii anayeshikilia nafasi ya kwanza kwa mauzo Bongo kupitia filamu anazoshiriki na kutengeneza mwenyewe.
Filamu yake ya Senior Bachelor ilionyesha uwezo wake wa hali ya juu na kumfanya ashikilie nambari moja.
Filamu zake nyingine ni pamoja na Nipende Monalisa, DJ Ben na Regina.

PATCHO
Patcho Mwamba ni mwanamuziki, lakini tangu alipoingia katika tasnia ya filamu akiwa sambamba na swahiba yake Kanumba. Moja ya sifa ya Patcho pamoja na kuigiza vizuri ni bingwa wa viwalo Bongo, kwa hiyo kama unampatia nafasi ya kuigiza suala la pamba unasahau.

DOTNATA
Dotnata alifungua kampuni ya Tanganyika Entertainment kwa ajili ya kusambaza kazi zake. Alitengeneza filamu iliyojulikana kwa jina la Chupa Nyeusi akiwashirikisha wasanii kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Burundi.

MR. MTUNIS
Amefanya vizuri sokoni baada ya filamu yake ya Mrembo Kikojozi kuwa gumzo. Hata filamu zake nyingine za Clinic Love na Kisasi zilitamba.

NDAUKA
Rose Ndauka ni moja kati ya akina dada waliofanya vizuri katika tasnia ya filamu Bongo, ikiwa ni pamoja na kufungua kampuni yake ya Rose Ndauka Entertainment kwa ajili ya kazi zake na kufanikiwa kutengeneza filamu kama Bad Girl, The Diary, Reuben na Angel.
Alienda Rwanda kwa ajili ya kurekodi filamu ya Maisha Baada ya Vita Rwanda.
Alitangaza ndoa na meneja wake Mariki iikiwa sambamba na kubadili dini, sasa anaitwa Aisha.


RICHIE
Single Mtambalike �Richie� ni moja kati ya wasanii waliofanya vizuri katika mauzo ya filamu Bongo na aliwaingiza wanaye katika uigizaji kwenye filamu ya Uswahilini Kwetu.

TINO
Hisani Muya �Tino� msanii huyu anarudi kwa nguvu zote, baada ya filamu yake ya Cut Off kufanya vizuri na kufuatiwa na Zowa, sasa ameingiza sokoni filamu ya Loreen inayofanya vizuri sokoni.

Kumbuka kuwa filamu yake ya Shoga ilikuwa gumzo baada ya Bodi ya filamu kuizuia na hatimaye kuibadili jina na kuwa ni Shoga Yangu badala ya Shoga.


DR CHENI
Naye alifanya vema kupitia filamu yake ya One By One na kuwa gumzo akiendelea kuuza sokoni.

Funga mwaka kubwa kuliko zote ni lile wazo la magwiji wa tasnia hiyo, Vincent Kigosi �Ray The Greatest� na Steven Kanumba �Kanumba The Great� walipoamua kutengeneza filamu kwa pamoja na kuipa jina la Off Side,

Walipoenda kuizindua nchini Kongo, ilisababisha baadhi ya watu kupoteza maisha wakipigania kuwaona nyota hao ambao waliandamana na Irene Uwoya, Jenifer na Johari.

Ukija katika fani ya uchekeshaji kwa vichekesho vya filamu, waliofanya vizuri ni King Majuto, Kingwendu, Sharo Milinea, Pembe bin Kichwa na Erick.
Katika upande wa wachekeshaji wa televisheni, kijana Lucas Mhuvile �Joti�' hakuwa na mpinzani. Kila siku amekuwa akibuni na kuibuka na kitu kipya ambacho ni burudani kwa mtazamaji.

Joti ameufunga mwaka kwa kuwa na pointi nyingi pengine kuliko msanii mwingine yeyote.